View attachment 3681892
KIGOMA: Tukio la wizi limetokea usiku wa kuamkia leo katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Kigoma, ambapo mikeka 100 imeibwa ikiwa na thamani inayokadiriwa kufikia shilingi milioni 1.5.
Mikeka hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mhe. Babalevo, kwa ajili ya matumizi ya waumini katika shughuli mbalimbali za kijamii na kidini, ikiwemo misiba na harusi katika Jimbo la Kigoma Mjini.
Baada ya tukio hilo kugundulika, mlinzi wa eneo hilo amechukuliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira ya tukio hilo.
Kinachowashangaza viongozi wa BAKWATA Mkoa wa Kigoma pamoja na Jeshi la Polisi ni kwamba, kwa mujibu wa taarifa za awali, milango ya ofisi haikuonekana kuvunjwa, huku mikeka hiyo ikiwa ndiyo mali iliyobainika kupotea.
Katika hatua za awali za uchunguzi, imeelezwa kuwa wakati wa makabidhiano ya ofisi hiyo, kuna mtu ambaye hakukabidhi funguo za mlango wa ofisi ya Mwenyekiti wa BAKWATA Mkoa wa Kigoma, ambako mikeka hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwa muda.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, funguo hizo bado hazijakabidhiwa hadi sasa, jambo ambalo linatarajiwa kuchunguzwa na vyombo vya dola ili kubaini iwapo lina uhusiano wowote na tukio la kupotea kwa mikeka hiyo.
Hata hivyo, suala hilo bado ni sehemu ya uchunguzi na halijathibitisha kuwa mtu huyo anahusika na wizi huo.
Viongozi wa BAKWATA Mkoa wa Kigoma wameeleza kuwa watafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, na kwamba endapo atabainika mtu yeyote kuhusika na tukio hilo, hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa.
Viongozi hao wameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mali za Baraza, pamoja na kuhakikisha kuwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika na upotevu au uharibifu wa mali hizo anachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.