Papaa Mobimba
JF-Expert Member
- Jan 27, 2018
- 882
- 3,337
Wakati zoezi la upigaji wa kura za kuchagua viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa likiwa limeanza tangu saa 02:00 asubuhi nchini, hali ni tofauti kwa jimbo la Mikumi, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro ambapo inadaiwa kuwa kata nane (8) kati ya 15 za jimbo hilo zoezi la upigaji wa kura halijaanza mpaka sasa
Akizungumza na Jambo TV leo, Jumatano Novemba 27.2024, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Mikumi Ally Rashidi amesema zoezi hilo limechelewa kuanza kutokana na kile kinachoelezwa kuwa baadhi ya karatasi za kupigia kura za wajumbe wa serikali za vijiji mchanganyiko na karatasi wa kupigia kura za wajumbe wa serikali za vijiji maalum kundi la wanawake hazijafika hadi kufikia wakati huu, jambo ambalo linatengeneza sintofahamu miongoni mwa wadau wa uchaguzi
Amezitaja kata zinazodaiwa kuchelewa kuanza kwa zoezi hilo kuwa ni Ruaha, Ruhembe, Mabwelebwele, Masanze, Zombo, Tindiga, Mhenda, Kidodi huku baadhi ya maeneo ikiwemo kata ya Ulaya zoezi lilianza mapema kama ilivyopangwa lakini sasa limesimama kutokana na uwepo wa karatasi chache za kupigia kura
Ally ameielesha Jambo TV kuwa kwa muda mrefu tangu mchakato wa uchaguzi huo uanze Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilosa hapokei simu zake wala za viongozi wengine wa CHADEMA wa eneo hilo, hivyo kupelekea mara kadhaa viongozi hao kuwasiliana na Mkuu wa Polisi wilaya ya Kilosa ambaye mara kadhaa walivyompigia leo simu yake imekuwa ikitumika
Sambamba na hilo, amedai kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi za kata na vijiji walipoulizwa kuhusu suala hilo wamesema mwenye mamlaka ya kutolea majawabu yake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa ambaye ndio huyo anayelalamikiwa kutopokea simu
Jambo TV imemtafuta Msimamizi msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo la Mikumi ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Michael John Gwimile simu yake haikupokelewa, huku wakati mwingine ilikuwa ikitumika, na hata tulipojaribu kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kwa ajili ya kujitambulisha bado sms hizo hazikujibiwa
Hata hivyo, Jambo TV inaendelea kufuatilia jambo hilo kwa undani zaidi ili kujuwa kiini chake.