UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Uchunguzi huu umebaini kuwa, changamoto za kijigrafia, umaskini, na upungufu wa miundombinu ya shule hasa madarasa na walimu ni miongoni mwa sababu zinazofanya wanafunzi washindwe kuendelea na elimu ya sekondari.
Sehemu ya kwanza ~ Watoto maelfu wanaofaulu la saba hawafiki Sekondari
Wakati nchi ikipiga hatua katika kuimarisha mifumo ya elimu na kusisitiza umuhimu wa nguvu kazi ya vijana kwa maendeleo ya taifa, wilayani Uvinza mkoani Kigoma kuna mlima mkubwa wa changamoto unaozima ndoto za maelfu ya watoto.
Kwa wanafunzi wengi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza, mwezi Januari unatajwa kama kipindi cha kuanza kwa safari mpya ya elimu ya sekondari kwa wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi, kwa watoto wa Uvinza kipindi hiki kimekuwa ni kiashiria cha kuanza kwa mkanganyiko mzito kwakuwa baadhi yao huanza elimu ya sekondari kuanzia mwezi Machi.
Mkazi wa Kata ya Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Yahaya Swalehe, akizungumza na gazeti hili, kuhusu mwenendo wa elimu katika kata hiyo.
PICHA: ADELA MADYANE
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 waliofaulu mitihani yao walishindwa kuripoti shuleni kuanza kidato cha kwanza kati ya mwaka 2021 na 2025. Hali hii inatoa picha halisi ya swali la msingi, nini kinasababisha watoto hawa kuachwa nyuma, na nani hasa anayewajibika?
Uchunguzi wa kina wa makala hii unabainisha kuwa tatizo hili halisababishwi na sababu moja tu, bali ni mtandao mgumu wa changamoto za kimuundo, kiuchumi na kijamii.
Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Uvinza, Julius Kakyama, anasema, “Changamoto ya wanafunzi kushindwa kuripoti inajirudia kila mwaka kutokana na miundombinu duni na jiografia ngumu ya wilaya hii."
Anasema wilaya ina jumla ya shule za sekondari 29 pekee, ambapo mbili ni za watu binafsi na 27 za serikali, na kwamba jiografia ya wilaya hiyo haipo rafiki kwani umbali kutoka kwenye makazi ya wananchi hadi shuleni unafikia hadi kilomita 40.
“Watoto hawa wengi wao wana umri mdogo wa takriban miaka 12, wanashindwa kuhimili kutembea umbali huo mrefu kila siku, huku wazazi wengi wakikosa uwezo wa kuwapangishia nyumba au hosteli karibu na shule,” anasema Kakyama na kusisitiza kuwa wilaya inahitaji shule zaidi ya 24 za sekondari ili kukabiliana na uhitaji uliopo.
Hali hii inakwenda kinyume na miongozo ya kisheria na sera za kitaifa na kimataifa zinazolinda haki ya mtoto kupata elimu na kukua katika mazingira salama. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2024 (toleo la 2023), kupitia ibara yake ya 3.1.1.5, inaweka wazi kuwa elimu ya lazima inajumuisha elimu ya msingi na sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne na itatolewa kwa jumla ya miaka 10.
Aidha, Lengo namba nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linaelekeza mataifa kuhakikisha watoto wote wanakamilisha elimu ya msingi na sekondari iliyo bure, yenye usawa na bora ifikapo mwaka 2030.
Hali kadhalika, Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) na ibara ya 3.1 na 3.2 ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 zinasisitiza wajibu wa serikali, wazazi, na jamii katika kuhakikisha mtoto anapata ulinzi, malezi na haki ya kupata elimu bila kikwazo
Suala la umbali na ugumu wa usafiri linathibitishwa na wanafunzi wenyewe. Mwanafunzi Elias Kavano wa shule ya sekondari Ruchugi ambaye anaeleza kuwa, “Inakuwa ngumu zaidi kwetu tunapotakiwa kurudi shuleni, tunatoka saa tisa, kufika nyumbani saa 11 jioni, na tukishindwa kurudi tunapata adhabu, hali hii inawafanya wengi kuacha shule na walioko nyuma yetu kuogopa shule.
Hali hii inaungwa mkono na Rehema Jummane, mwanafunzi wa shule ya msingi Ruchugi\, anayeeleza kuwa huwakuta ndugu zake wakirejea kutoka shuleni wakiwa wamechoka na njaa kupita kiasi, hali inayowakatisha tamaa watoto wengine wanaotakiwa kuanza safari hiyo ya elimu.
Hata hivyo, mzigo huu haubebwi na jiografia pekee, bali unachochewa na hali ngumu ya kiuchumi ndani ya jamii. Wananchi wa Kata ya Kazuramimba wanabainisha kuwa umaskini wa kipato na misimu ya kilimo inayoambatana na gharama kubwa za pembejeo zinawafanya wazazi kushindwa kumudu mahitaji ya kuanza shule kwa wakati.
Nusra Hamis mkazi wa Kazuramimba anaeleza, "Ni kweli kuna ruzuku, lakini kuna kipindi mbolea mfuko mmoja tunanunua mpaka Sh. 120,000, mbegu mfuko mmoja tunanunua Sh. 12,000 gharama ni kubwa, kupata fedha za pembejeo, na maandalizi ya mtoto kwenda shuleni kwa wakati mmoja inakuwa ngumu, ndio maana watoto wengi huchelewa na kushindwa kusoma."
Mtazamo huo unaungwa mkono na Yahaya Said, mkazi wa Kazuramimba, ambaye anasema, "Matokeo ya wanafunzi kuingia kidato cha kwanza yanatoka mwezi wa 12, yanatukuta bado tunakabiliwa na kununua mbolea, na gharama nyingine za kilimo, na inakuwa bado ni masika, inabidi mtoto aripoti shuleni kuanzia mwezi wa tatu tunapokuwa tumeuza mavuno ya awali."
Hali hii ya kiuchumi inawasukuma watoto kuingia katika mfumo wa kujitafutia riziki au kusaidia familia tangu wakiwa wadogo. Thomas Roman,aliyekuwa mwenyekiti wa kijiwe cha bodaboda ambaye pia ni mwathirika aliyeacha shule ili kusaidia wazazi wake, anaeleza, "Mimi niliacha shule ili kuwasaidia wazazi wangu, kwanza nilikuwa najinunulia sare na daftari, nililazimika kila mwisho wa wiki nitafute vibarua ili nipate hivyo vifaa, niliacha shule, pesa ninayopata ndio tunakula pale nyumbani."
Mtazamo kama huo unasisitizwa na Amisa George mkulima, anayekiri kuwatumia watoto shambani ili kusaidia shughuli za uzalishaji kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za ziada za masomo.
Mchungaji Elias Joshua wa Kanisa la FPCT naye anabainisha kuwa wazazi wengi wanakata tamaa ya kuwekeza kwenye elimu kutokana na wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana waliomaliza masomo.
Upande wa usimamizi na malezi nao unatajwa kuwa na mchango mkubwa katika mmomonyoko huu wa elimu. Ofisa Elimu Divisheni ya Msingi na Awali, Hilary Bitwaye, anaeleza, tabia ya kuhamahama kwa wafugaji wilayani humo pia inachangia wanafunzi kushindwa kuripoti kuanza kidato cha kwanza.
"Uvinza ni wilaya yenye wafugaji wengi ambao mara nyingi hulazimika kuhama mara kwa mara kutafuta malisho ya mifugo yao, hali hii inawafanya watoto wao kukosa utulivu wa kielimu na kushindwa kuendelea na masomo kwa wakati," alisema Bitwaye.
Aidha, Ofisa wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma, Msafiri Nzunuri, anataja migogoro ya kifamilia, akieleza, "Mabadiliko kama hayo yakitokea yanaweza kupelekea watoto wakashindwa kuendelea na masomo, kwakuwa wanakosa uangalizi, wazazi lazima washirikiane kwa pamoja kuwalea watoto wao.
Ripoti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ya Machi 2025 inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watoto mkoani humo wanakosa malezi sahihi hali inayowafanya watoto wengi kushindwa kusoma vizuri.
Kwa upande wa uongozi wa vijiji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kazuramimba, Moshi Kamlonga, analalamikia ukosefu wa mrejesho kutoka kwa mamlaka za halmashauri na idara husika.
Anasema, "Tunafanya jitihada nyingi, lakini bila mrejesho tunabaki gizani, halmashauri inapaswa kutupa mrejesho ili tujue nini kinaendelea na tuweze kubuni mbinu mpya za kukabiliana na tatizo hili."
Kuhusu uwajibikaji upande wa kuboresha miundombinu, katibu tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa anasema serikali imekuwa ikiweka jitihada za kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la shule ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya wanafunzi.
Anasema mnamo mwaka 2020 mkoa wa Kigoma ulikuwa na shule za msingi 442 lakini hadi kufikia sasa zipo 758 ikiwa ni ongezeko la shule 316 katika kipindi cha miaka mitano, vilevile lipo ongezeko la shule za sekondari 147kutoka 119 mwaka 2020 hadi 266 hali inayoonyesha jitihada za serikali katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya mwaka 2014 (toleo la 2023)
“Mkakati wa serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anamaliza elimu ya msingi ya lazima ya miaka 10, maana yake ni kwamba vijana wanaomaliza shule ya msingi lazima waende sekondari, kama tunazo shule za msingi 758 maana yake tunahitaji kuwa na shule za sekondari 758 ili kuendana na uwezo wake kama ilivyoruhusiwa na serikali” anafafanua Rugwa
Anasema kwa mkoa wa Kigoma linahitajika ongezeko la zaidi ya shule 500 ili wanafunzi wote wanaomaliza shule ya msingi wanendelea na sekondari, akieleza kuwa serikali imeshaweka mipango yake ya kuhakikisha kuwa mpaka mwaka 2028 kunakuwa na miundombinu inayokidhi mahitaji ya watoto wote.
Katika taarifa iliyotolewa na Waziri mkuu, Mwigulu Nchemba, mnamo Aprili 01, 2026, akiwa bungeni jijini Dodoma alibainisha kuwa jumla ya trilioni 1.77 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, maabara, ajira mpya za walimu, ruzuku ya vitabu na uendeshaji na ruzuku ya mitihani katika mwaka wa fedha 2027/2028 akitaja kuwa chanzo cha upatikanaji wa mapato hayo ni kupitia serikali kuu, mapato ya ndani ya halmashuri na wadau mbalimbali.
Katika sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala hii, tutaangalia nini suluhisho la tatizo la wanafunzi waliofaulu kushindwa kuripoti shuleni kuanza kidato cha kwanza.
ANDIKO LA: Adela Madyane – Kigoma
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.