MIAKA mitatu sasa imetimia tangu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, mtoto wa mkulima na kwa sasa mfugaji wa nyuki, kutangaza mali anazomiliki.Ilikuwa Januari, mwaka 2010 ndipo alipofanya uamuzi huo wa kipekee, akiwa Waziri Mkuu wa kwanza nchini kutangaza mali anazomiliki. Kwa maana nyingine, ni Waziri Mkuu pekee aliyeamua (kwa wakati huo) kuwa muwazi kwa wananchi kuhusu mali zake bila kushurutishwa kisheria.
Ni katika mazingira hayo ya kipekee na kwa kuzingatia miaka mitatu imekwishapita bila kumsikia tena Waziri Mkuu Pinda akiendelea na utaratibu wake huo, si vibaya kutafakari tena uamuzi wake huo katika kipindi hiki cha miaka mitatu.Ni kwa nini alisita kuendelea kutangaza mali zake kwa kadiri anavyojaza fomu za maadili kila mwisho wa mwaka katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma?Je, uamuzi ule wa kutangaza mali ulikuwa ni sawa na ajali (kukurupuka)? Je, hakuwa amejiandaa kisaikolojia kuendeleza utaratibu huo kila mwaka? Au atakuwa tayari kutangaza mali alizochuma pindi atakapoondoka madarakani?
Na kama akiamua hivyo, kutakuwa na tija yoyote kwa nchi? Na je, ni jambo gani la busara zaidi; kumtathimini kiongozi (kwa jambo mahsusi) wakati akiwa madarakani au baada ya kustaafu?Pengine kabla ya kuendelea na mjadala zaidi, tukumbushane, kwa wakati ule, Waziri Mkuu Pinda alisema nini kuhusu mali zake.Katika kutaja mali zake hizo, alisema anamiliki nyumba mbili pamoja na akaunti za benki zenye fedha zisizozidi milioni 25 (fedha ambazo - kwa sasa - kama angekuwa kijana na akaamua kugombea uongozi wa kitaifa katika Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi –UVCCM- zisingetosha kumpatia ushindi wa kishindo).Lakini kwa maneno yake siku hiyo, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam Pinda alisema; ''Kama shilingi milioni 25 ni utajiri basi nami nimo.''
Akasema anamiliki nyumba moja mjini Dodoma na nyingine kwao Mpanda mkoani Rukwa eneo la Makanyagio, na ana kibanda shambani kwake Pugu, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.Pinda aliwaambia wahariri; ''Mimi kila mwaka nataja mali zangu kwa Tume, sijaulizwa, sijagombana na Tume.'' Ukiniuliza ni masikini kiasi gani, nitakwambia nina nyumba Dodoma nimejenga kwa utaratibu wa serikali wa kuomba mkopo, ninayo nyingine kwetu Mpanda pale Makanyagio,"Dar es Salaam sina nyumba, pale Pugu nina nyumba kidogo inahitaji kazi ya ziada, kijijini nilikuwa nafikia kwa Babu, Babu ana kanyumba kake ka ovyo ovyo kile ambacho mlikiona, ana vyumba viwili nilikuwa nalala pale, lakini baada ya uwaziri mkuu, jamaa wakaniambia aah...haiwezekani pale, nilijua nitaweza kulala pale na hawa jamaa (wasaidizi wake) watalala mjini hotelini, nikaambiwa hapafai.Alisema hana gari lolote zaidi ya gari alilopewa kwa kuwa mbunge, na kubwa zaidi alisema kwa jinsi serikali inavyowajali watu wanaoshika wadhifa kama wake (Waziri Mkuu), haoni ni kwa nini awe na tamaa ya fedha na mali, kwa sababu serikali inamjali kwa kumtunza kwa kila kitu.
"Kwa utaratibu wa serikali unapewa nyumba, magari, unalishwa na serikali... kwa mshahara wangu unaweka akiba ya kutosha, unataka utajiri wa nini? Maisha yako ni mazuri, unataka nini zaidi ya hapo? Ukitoka nje ya utumishi wa serikali akiba yako inakusaidia kusomesha watoto wako,'' alisema.Kwa mujibu wa maelezo yake kwa wakati huo, jukumu lake kubwa aliloomba kwa Mwenyezi Mungu ni kumpa uwezo wa kuwatumikia Watanzania vizuri zaidi.Alisema; "Sina hisa popote, labda huko mbele ya safari nitafikiria. Yaani ukiwa Waziri Mkuu ndio mwanya wa kujinufaisha, kwa nini? Labda mimi watu wanaweza kusema Waziri Mkuu wa sasa ni mjinga, nipo kwa ajili ya watu, kuwatumikia si kujinufaisha mwenyewe."
Hayo maneno ya Waziri Mkuu Pinda ambayo kwa namna fulani yanamweka katika mazingira ya kuhitajika kuendeleza utaratibu huo. Kwa mfano, katika maneno yake hayo ameweka bayana kwamba hana hisa katika kampuni yoyote lakini akasema; "labda huko mbele ya safari nitafikiria." Je, Waziri Mkuu amekwishafikiria? Je, amekwishafika "huko mbele ya safari?"Katika kipindi hiki cha miaka mitatu tangu atangaze mali anazomiliki, akaunti zake zina kiwango gani cha fedha? Je, ni kweli ameweza kuhimili shinikizo kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji wengine wakubwa wenye lengo la kutaka akaunti zake benki zijae fedha, ili, ikibidi baadaye naye aweze kuchangia kwa kiasi cha kutosha ujenzi wa makanisa na misikiti nchi nzima (ngazi ya mkoa hadi wilaya)?Ni kweli bado dhamiri yake haijatetereka kiasi cha kutothamini tena ukweli kwamba taifa linamgharimia kwa karibu kila kitu kama Waziri Mkuu na ataendelea kugharimiwa hata baada ya kustaafu.
Ni kweli dhamiri yake bado inashawishika kwa maneno yake "haoni kwa nini awe na tamaa ya fedha na mali?"Lakini kwa nini nimeandika haya, miaka mitatu tangu Waziri Mkuu Pinda atangaze mali zake hadharani? Kwanza ni kutaka kumkumbusha kwamba hata Rais Benjamin Mkapa aliwahi kutangaza mali zake alipoingia madarakani, lakini hadi anaondoka na hata katika maisha yake ya kustaafu anayoendelea nayo leo, hajawahi kurudia kutaja mali hizo. Ni dhahiri, Pinda anaweza kufuata mfano huo wa Mkapa au la.Lakini jambo la pili ni ukweli kwamba, uamuzi huo wa Pinda unatukumbusha ya kuwa katika mchakato wa sasa wa kukusanya maoni ya Katiba mpya, tuweke mfumo wa wazi kisheria kuhusu taarifa za viongozi. Si taarifa zote, lakini angalau taarifa kwa mfano za mali zake.