Date::8/28/2008
Mambo ya Richmond: Karamagi, Msabaha wachunguzwa
Na Ramadhan Semtawa
Mwananchi
SERIKALI imesema imeanza kuwachunguza mawaziri wa zamani wa wizara ya Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, kama walihusika na rushwa wakati wa mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura uliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond Development Limted.
Mbali ya uchunguzi huo, serikali imetangaza pia kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Athur Mwakapugi, wametakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kuwajibika katika mchakato huo hadi kulitia taifa hasara.
Akitoa tamko hilo la utekelezaji wa maagizo ya Bunge kwa watuhumiwa wa mkataba wa Richmond bungeni jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema uchunguzi dhidi ya mawaziri hao wa zamani ambao kwa nyakati tofauti waliongoza Wizara ya Nishati na Madini, unalenga kuona kama walihusika na rushwa wakati wa utoaji zabuni.
Azimio namba nane la Bunge lilitaka Waziri wa Nishati na Madini (wakati wa mkataba, Karamagi) awajibishwe, azimio namba tano lilitaka AG awajibishwe namba tisa lilitaka Hosea awajibishwe, wote wawajibishwe na mamlaka ya juu (Rais) huku maafisa wengine nane wa Takukuru wawajibishwe na mamlaka husika kutokana na kuisafisha Richmond.
Katika azimio lake namba 14, lilimtaja Dk Msabaha (aliyekuwa Waziri wa Nishati, kabla ya Karamagi), Katibu Mkuu Mwakapugi na Kamishna wa Nishati Bashir Mrindoko, ambao nao walipaswa kuwajibishwa hata hivyo, tayari mawaziri hao wawili (Dk Msabaha na Karamagi), walishajiuzulu kabla ya kuwajibishwa katika Mkutano wa 10 wa Bunge uliofanyika Februari, mwaka huu.
Azimio la saba la Bunge lilitaka wajumbe wote wa Timu ya Wataalamu wa Kuishauri Serikali katika mazungumzo kuhusu Mikataba (GNT), ambao walitoka Benki Kuu (BoT), Shirika la Umeme (Tanesco), Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, wawajibishwe kutokana na kushindwa kuishauri serikali hadi taifa likaingia hasara kwa kuingia mkataba mbovu na Kampuni ya Richmond.
Akizungumzia utekelezaji wa azimio moja hadi jingine, Waziri Mkuu alifafanua kwamba, katika azimio namba 8 na 14, licha ya mawaziri hao kujiuzulu, serikali imeamua kujiridhisha ndiyo maana imeagiza vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina kuona kama walihusika na jinai ya rushwa kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yao.
Pinda alifafanua kwamba, tayari pia serikali imeanza utekelezaji wa azimio namba 14 ambalo pia linamtaja Katibu Mkuu Mwakapugi, Mrindoko na namba tano linalomtaja Mwanasheria Mkuu na kuongeza kwamba wameandikiwa barua za kutakiwa kujieleza kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kumchukulia hatua kwa kuwa ndiye mamlaka ya kikatiba kufanya hivyo.
Alifafanua kwamba, Hosea na Mwakapugi wametakiwa kujieleza kwa Katibu Mkuu Kiongozi (Philemon Luhanjo) ambaye atatoa maelekezo kwa serikali namna ya kutekeleza zaidi maazimio hayo.
Aliongeza kwamba, Takukuru inatakiwa kueleza kwanini ilishindwa kubainisha kasoro kama ilivyofanya Kamati ya Bunge katika mkataba wa Richmond na pia vipi haikubaini kupuuzwa ushauri wa Mamlaka ya Zabuni (PPRA).
Kuhusu utetezi wa Mwakapugi, Pinda alisema Katibu Mkuu huyo alitakiwa kujieleza kwanini alikiuka maelekezo ya Baraza la Mawaziri, PPRA na kushindwa kuishauri serikali kufanya uchunguzi zaidi kwa RDC kabla ya mkataba.
Pinda alifafanua kwamba Mrindoko, alitakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kumshauri Katibu Mkuu wake ambaye alikuwa ni mgeni wizarani hapo wakati alijua kampuni hiyo ya Richmond haikuwa na uwezo, kwani Juni 30, 2004 alisitisha mradi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, baada ya kubaini udhaifu huo.
Kuhusu azimio namba 10 ambalo linahusu malipo ya dola za Marekani 4.8 milioni kwa Dowans, alisema uchunguzi wa kina BoT ulibaini kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni halali kwani kililipwa kwa ajili ya kuingiza mitambo kwa ndege.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba, baada ya serikali kufanyia kazi mapendekezo hayo ya Bunge imebaini kulikuwa na mapungufu ya usimamizi na uwajibikaji wakati wa mchakato wa mkataba huo hadi ulipotiwa saini Juni 23 mwaka 2006.
Alisema kutokana na uthibitisho huo serikali, licha ya kuchukua hatua kwa mawaziri na watendaji hao wa ngazi za juu, pia imetaka maafisa nane wa Takukuru na wajumbe wengine wote wa GNT, wajieleze kwanini walishindwa kutumia utaalamu wao kuliepusha taifa na hasara.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba, uamuzi huo wa kuwapa nafasi ya kujieleza, unalenga kutoa haki ya msingi ya kumsikiliza mtu kabla ya hatua nyingine zaidi za kinidhamu kwa mujibu wa sheria hazijachukuliwa.
Huku akionekana kupitia njia ile aliyopita Rais Kikwete wakati akizungumzia watuhumiwa wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya BoT, Pinda alisema utekelezaji huo umechukua miezi sita badala ya mitatu kutokana na kuwa jambo hilo linahitaji umakini na utekelezaji kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia azimio namba 17 ambalo lilitaka RDC ifutwe katika orodha ya Ofisi ya Msajili wa Makampuni na Majina ya Biashara (Brela), alisema uchunguzi umebaini kwamba katika ofisi hiyo kuna Kampuni ya Richmond Tanzania (LTD).
Pinda alifafanua kwamba, RDC haikusajiliwa Brela na kuongeza kwamba, hadi sasa haijathibitika uhusiano kama Richmond hiyo ya nje ilikabidhi majukumu yake kwa Richmond ya nchini.
Hata hivyo, alisema maelekezo ya serikali ni kwamba Brela ifute Richmond Tanzania (LTD), na kufafanua kwamba tayari kampuni hiyo ilipewa barua ili ijitetee lakini hadi sasa haijafanya hivyo.
Kuhusu kama RDC ilighushi nyaraka na kupata zabuni hiyo, alisema jinai huchunguzwa na polisi na kwamba tayari jeshi hilo linachunguza kuona kama wamiliki walifanya kosa hilo la jinai kupata zabuni.
Sakata la Richmond lilitikisa nchi kuanzia Juni mwaka 2006, miezi michache baada ya serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani na nchi kukabiliwa na ukame na uhaba wa nishati, hivyo kulazimu serikali kutafuta mitambo ya dharura ya kukodi kwa ajili ya kufua umeme.
Hata hivyo, mpango huo uliingiza serikali ya awamu hiyo ya nne katika kashfa nzito ambayo ilifanya Bunge kuunda Tume yake chini ya Mbunge wa Kyela Dk Harrison Mwakyembe, ambayo katika mkutano wa 10 wa Bunge la Februari ilitoa matokeo yake ambayo yalisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Dk Msabaha na Karamagi, kujiuzulu.