TAARIFA
Jana tarehe 18 Septemba 2017, Mbunge wa Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile (Mb) akiambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt Medard Kalemani (Mb) walifanya ziara ya kukagua miradi ya umeme inayolisha Dar Es Salaam na hususan Kigamboni.
Ziara hii ilijumuisha Kamishna wa Nishati toka Wizara ya Nishati na madini, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, wakurugenzi wa Tanesco, Mameneja wa Tanesco wa Kanda, Mkoa, Wilaya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Hashim Mgandilwa.
Dkt Ndugulile akiongozana na Dkt Kalemani walitembelea vituo vya kupoozea umeme vinavyojengwa kwenye maeneo ya Mbagala, Kurasini na Tungi, Kigamboni.
Vile walitembelea eneo linalilokusudiwa kujengwa kituo kikubwa cha umeme eneo la Dege, Somangila.
Dkt Ndugulile alimjulisha naibu Waziri kuhusu changamoto za umeme katika Jimbo la Kigamboni ikiwa ni pamoja na kukatika mara kwa mara kwa umeme, umeme mdogo (low voltage) na kusuasua kwa miradi kwa miradi mipya kutokana na uhaba wa vifaa.
Dkt Kalemani aliahidi kusimamia miradi hii kwa karibu na pia aliwahakikishia wananchi wa Kigamboni kupata umeme wa uhakika ifikapo Disemba, 2017.
Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza Tanesco kuipatia Tanesco Kigamboni vifaa vinavyohitajika kwa miradi mipya kama vile waya, nguzo na transfoma.
Vile vile, Dkt Kalemani aliwataka Tanesco kuharakakisha mchakato wa ujenzi wa substation utakaogharimu Tsh 5 Bilioni ili ukamilike katika muda uliopangwa ifikapo Machi, 2018.
Aidha, Dkt Kalemani alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya kufunga umeme kwenye vitongoji vilivyorukwa kwenye mradi wa REA II na vile vile maeneo mapya kwenye REA III unatarajia kuanza Januari, 2018.
Dkt Ndugulile alimshukuru Dkt Kalemani kwa kutembelea Kigamboni na kumtaka kusimamia kwa karibu ahadi zake ili wananchi wa Kigamboni waondokane na adha ya umeme inayowakabili kwa sasa.
IMETOLEWA NA OFISI YA MBUNGE WA KIGAMBONI
19.09.2017