Mjasiriamali kijana wa Tanzania abadilisha nywele kuwa mbolea

Mjasiriamali kijana wa Tanzania abadilisha nywele kuwa mbolea

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG41N1316832848.jpg


Wakati David Dennis alipoona kwa mara ya kwanza nywele zimetawanyika katika duka lake la kinyozi la shule ya sekondari, hakujua kabisa kwamba nywele hizo zilizotupwa siku moja zitamweka mbele kabisa katika harakati za uvumbuzi wa kijani zinazochipukia.

Leo, Mtanzania huyo mwenye umri wa miaka 27 ndiye mwanzilishi na afisa mkuu mtendaji wa Cut-Off Recycle Limited, kampuni ya usimamizi wa taka na usaidizi wa kilimo ambayo hubadilisha nywele za binadamu kuwa mbolea za kikaboni.

Kile kilichoanza kama uchunguzi wa kawaida tu kimebadilika na kuwa uvumbuzi ulio na hati miliki, mfumo wa uchumi wa mzunguko unaoleta nafasi za ajira, na biashara ambayo sasa imeunganishwa na masoko ya kimataifa, haswa China.

Wazo la Cut-Off Recycle lilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, wakati ambao Dennis alikuwa bado katika shule ya sekondari. "Nilifuata kila mahali nywele zilipopelekwa. Zilichomwa katika eneo la wazi la shule," alikumbuka.

Uchomaji huo ulitoa moshi mzito na gesi zenye madhara, na kusababisha uzalishaji wa kaboni, uchafuzi wa hewa, na uharibifu wa mazingira, jambo ambalo ni upotevu na hatari, Dennis alibainisha.

Akiwa pamoja na mwanafunzi mwenzake ambaye sasa ni mwanzilishi mwenza, Ojung'u Jackson, Dennis alianza kutafiti sifa za nywele za binadamu.

Waligundua kwamba nywele kimsingi zimeumbwa na keratin, protini yenye nitrojeni nyingi. Zinapokatika, keratin hutoa amino asidi, ambazo ni virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mimea.Wawili hao walivumbua uwezekano wa aina tatu wakati wa majaribio yao ya awali. Baada ya kumaliza shule ya sekondari, Dennis alichukua mapumziko kwa mwaka mzima kusoma ukubwa wa tatizo na fursa hiyo.

Kote Tanzania na sehemu kubwa ya Afrika, taka za nywele mara nyingi hutupwa kwenye majalala, ambapo huwa zinachomwa au kuachwa tu. Katika baadhi ya jamii, watu huzika nywele kutokana na imani za jadi za muda mrefu kwamba zinaweza kutumika kwa uchawi. Kukusanya nywele za binadamu kwa kiwango kikubwa hakuhitaji teknolojia tu, bali uaminifu pia.

Wakati huo huo, Dennis aligundua suala jingine kubwa yaani utegemezi wa mbolea. Karibu asilimia 90 ya mbolea zinazotumika Tanzania huagizwa kutoka nje, hasa bidhaa za kemikali zisizo za kikaboni zinazotengenezwa na makampuni ya kimataifa. Dennis aliona fursa ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

Mwaka 2020, kampuni ya Cut-Off Recycle Limited ilianzishwa rasmi katika mkoa wa Arusha, ikilenga ukusanyaji wa taka za nywele za binadamu na uzalishaji wa pembejeo za kilimo cha kikaboni.

Kampuni hiyo haikupata tu hati miliki ya njia ya kusindika nywele za binadamu kuwa mbolea za majimaji zenye amino asidi, bali pia ilipanuka na kutoa njia ya kukuza nywele zilizotengenezwa kutokana na nywele zenyewe na vifaa vingine vya kikaboni.

Dennis pia alisafiri zaidi ya kilomita 600 kutoka mji wake wa asili, Arusha, hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kusomea shahada ya kwanza ya sayansi ya mazingira na usimamizi. Safari yake ya kitaaluma ilifikia kileleni kwa kufanya tasnifu kuhusu kuoza kwa nywele za binadamu, na kumpatia daraja la kipekee

Ili kushughulikia miiko ya kitamaduni kuhusu ukusanyaji wa nywele, kampuni ya Cut-Off Recycle ilitekeleza mfumo unaotegemea motisha, kulipa maduka ya nywele, wakusanyaji taka, na watu binafsi kwa nywele wanazokusanya na kuzipeleka kwenye vituo vya kampuni.

Zaidi ya watu 350 tayari wamepata mapato kupitia mpango wa ukusanyaji wa nywele jijini Arusha pekee. Kwa kuanzisha kituo kipya cha ukusanyaji jijini Dar es Salaam, kampuni hiyo inataka kutoa fursa kwa wakusanyaji zaidi ya 500.

"Badala ya kuomba pesa nyumbani, vijana wanaweza kukusanya taka za nywele kutoka kwa vinyozi walio karibu na kupata mapato," alisema Dennis.

Katika Afrika, ambapo mifumo ya usimamizi wa taka bado haijaendelezwa vizuri, taka za nywele mara nyingi huwa hazipewi kipaumbele. Hata hivyo, athari yake inaonekana mitaani na katika mifereji ya maji, Dennis alisema.

Mwaka 2024, Dennis alisafiri kuja China mara mbili. Safari yake ya kwanza ilitokana na programu iliyoungwa mkono na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) chini ya Umoja wa Mataifa, ambacho kilichagua biashara 100 za Afrika kushiriki katika mpango wa biashara ya kidijitali.

Wakati wa programu hiyo, Dennis aliweza hata kujifunza namna viwanda vya jadi vinavyoweza kufikia masoko ya kimataifa kupitia majukwaa ya kidijitali. Kampuni ya Cut-Off Recycle ikawa ya kwanza nchini Tanzania kuuza pembejeo za kilimo nchini China, na kufungua milango kwa washirika na wateja wa kimataifa.

Dennis pia alihudhuria Maonesho ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yaliyofanyika Changsha, mji mkuu wa Mkoa wa Hunan, ambapo alifahamiana na wazalishaji wa China, akiwemo mzalishaji wa pembejeo za kilimo aliyeko Shenzhen.

Kampuni ya Cut-Off Recycle sasa inapata vifaa vya vifungashio na vya usindikaji kutoka China kwa gharama ya chini sana, huku pia ikishiriki katika ubadilishanaji wa teknolojia. Dennis alishangazwa na thamani ambayo wajasiriamali wa China wanaitoa kwenye uhusiano wa muda mrefu.

"Urafiki ni muhimu nchini China," alisema. "Niliporudi kwa ziara yangu ya pili, mshirika huyo huyo alikuja kunipokea uwanja wa ndege. Uaminifu umefanya ushirikiano uwe rahisi sana."

Wakati wa safari yake ya pili, Dennis alitembelea miji ya Guangzhou, Shenzhen, na Beijing, pamoja na makampuni ya teknolojia, likiwemo la Baidu. "Kama kampuni ya teknolojia inaweza kuwa ya uhamaji, basi kampuni ya kilimo inaweza kupanuka katika kutoa suluhisho nyingi za usaidizi kwa wakulima," alisema.

Licha ya mafanikio yake, kampuni ya Cut-Off Recycle inakabiliwa na changamoto kubwa, hasa katika teknolojia ya kuongeza ukubwa. Dennis na timu yake sasa wanafanya kazi na watengenezaji wa vifaa vya asili, hasa wale walio nchini China, kubuni mashine maalum za kuchambua, kukata, na kutengeneza mbolea ya taka za nywele.

Tawi jipya la Cut-Off Recycle lilifunguliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kwa ushirikiano na Watende Investment Company Limited, kampuni ya wenyeji inayoshughulikia huduma za ukusanyaji na usimamizi wa taka. Akitupia macho mbele, Dennis anafikiria mtandao wa vituo vya ukusanyaji nywele katika miji mikubwa ya Afrika na matawi ya vituo vya utengenezaji wa mbolea vinavyofanya kazi ndani ya nchi. Anatumai kubadilisha mtazamo wa watu kuhusu taka. "Ndoto yangu ni kwamba kila mtu aone nywele sio taka, bali ni fursa," aliongeza.
 
Back
Top Bottom