Salute Mkuu..
Kwakua umemgusia Constantine na Ukatoriki, Basi nami ngoja nimgusie Mfalme
NERO na ukatoriki. Twende pamoja...
Wakuu Mfalme Nero alikuwa mtawala wa dola ya kirumi, kwani alikuwa mtawala wa dola hiyo kuanzia mwaka 54 baada ya Kristo hadi mwaka 68 baada ya Kristo akiwa mtawala wa mwisho wa ukoo wa Julius. Watawala wa dola hiyo waliomtangulia Nero walikuwa Augustus aliyetawala kuanzia mwaka 27 kabla ya Kristo hadi mwaka 14 baada ya Kristo na huyu ndiye mwanzilishi wa dola hiyo na ndiye anayetajwa na mwenjili Luka sura ile ya pili aya ya kwanza kuwa ndiye aliyeitisha sensa ya watu. Baada yake alifuatia Tiberius ambaye anatajwa na mwenjili Luka katika sura ile ya tatu aya ya kwanza, yeye alitawala kuanzia mwaka 14 baada ya Kristo hadi mwaka 37 baada ya kristo na ndiye aliyeshuhudia kazi za Yesu hadi kufa kwake. Baada ya Tiberius alifuata Kaligula aliyetawala kuanzia mwaka 37 baada ya kristo hadi mwaka 41 baada ya Kristo. Kisha akafuata Kladius aliyetawala kuanzia mwaka 41 baada ya Kristo hadi mwaka 54 baada ya Kristo. Huyu Klaudius ndiye anayetajwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume sura ile ya kumi na nane aya ya pili, kuwa aliamuru wayahudi wote waondoke Roma. Baada ya Klaudius ndipo akafuata huyo Nero ambapo kwa kufuata mlolongo huo yeye alikuwa mtawala wa tano baada ya hao niliokutajia.
Ni kweli pia kwamba huyu Nero ni mmoja kati ya watu ambao historia inawatambua kuwa ni watu wabaya-kama anavyojulikana. Na hiyo ndiyo sababu ambayo wewe umetoa kuwa unataka kufahamu historia yake. Labda kabla ya kukupa historia ya huyu mtawala yaani Nero ni bora kama nikikueleza kwanza sababu zilizomfanya mtawala huyu abebe sifa hiyo ya ubaya.
Pengine umewahi kusikia juu ya madhulumu ya Kanisa! Kama umewahi kusikia basi kifupi madhulumu hayo yaliasisiwa na mtawala huyu Nero hapo mwaka 64 baada ya Kristo. Pamoja na kuongoza madhulumu ya wakristo, kama mtawala, inasemekana alikuwa katili sana na ushahidi wa ukatili huo ni kwamba alipanga na ufanikiwa mauaji ya mama yake mzazi hapo mwaka 59 baada ya Kristo yaani miaka mitano tu baada ya kuanza kutawala dola hiyo ya kirumi.
Zaidi ya hayo, Nero hakuona haya kumnyang’anya mke rafiki yake na kumuoa yeye mwenyewe kwa kutumia tiketi ya mamlaka aliyokuwa nayo. Kama haitoshi, Nero anafahamika zaidi kwa ubaya wake kwa sababu ndiye anayetajwa katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane kwa namba 666 kama mnyama hatari sana. Hilo rejea kitabu cha Ufunuo 13:11-18.
Katika kipindi cha utawala wake ndipo mitume Petro na Paulo walipouawa katika mfululizo wa madhulumu.
Ingawa NERO hakuwa kiongozi pekee wa dola ya kirumi aliyeongoza madhulumu, kwani kuna wenzake tisa waliomfuata tena walikuwa wauaji hata kuliko Nero. Huyu tumemfahamu pia kwa sababu ametajwa pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume 25:10. Yeye ndiye aliyepokea rufaa ya Paulo aliposhtakiwa na wayahudi baada ya kesi kuanza kusikilizwa na Festus.
Baada ya kupata maelezo juu ya mazingira yaliyomfanya Nero asikike au kufahamika na hasa kwa ubaya wake, basi sasa nikupe historia yake kama ulivyoniomba.
Nero alizaliwa mwaka 38 baada ya kristo katika sehemu iliyoitwa Antium kwa wakati ule siku hizi sehemu hiyo inaitwa Anzio, karibu na mji wa Roma huko Italia. Baba yake aliitwa Domitius na mama yake aliitwa Agrippina ambaye alikuwa dada wa mtawala wa dola hiyo hiyo aliyeitwa Kaligula-kama nilivyokuambia pale awali kuwa Kaligula alikuwa mtawala wa tatu. Huyu mama aliolewa kwa mara ya pili na kaisali Kladius- naye nilimtaja pale awali kuwa alimtangulia Nero. Aliolewa kwake mnamo mwaka 49 baada ya kristo. Hivyo Nero alilelewa na huyo baba yake wa kambo yaani mume wa mama yake.
Akiwa na miaka 17 tu ya kuzaliwa, NERO alikabidhiwa dola ya kirumi kama mtawala. Hii ilikuwa mwaka 54 baada ya Kristo-kama nilivyokuambia hapo awali. Miaka mitano ya mwanzo ya utawala wake ilielezewa kuwa na mafanikio makubwa. Wakati wake mradi mkubwa kabisa wa maji na uzalishaji nafaka ulimalizika baada ya kuanzwa na Klaudius mtawala aliyemtangulia. Kwa kweli katika kipindi hiki Nero alionekana kama mtawala bora kabisa na mwenye hekima, ndiyo maana Mtume Paulo aliposhtakiwa na wayahudi alikata rufaa ili kesi yake ikasikilizwe na mtawala huyu akijua kuwa alikuwa mtu mwenye busara na hivyo angetenda haki. Rejea. Matendo ya Mitume 24-25. Pamoja na kuwa na busara, huyu bwana alikuwa anapenda sana michezo. Bila shaka kwa wakati wetu huu angekuwa kipenzi cha vijana na wanapenda michezo.
Nilisema hapo awali kuwa Nero alimnyang’anya rafiki yake mke na kumuoa yeye mwenyewe. Huyu mke wa rafiki yake ndiye aliyeanza kuififisha nyota ya mafanikio ya Nero. Huyo alikuwa mshauri wake mkuu kiasi kwamba Nero alikuwa hamsikilizi yeyote isipokuwa huyo mke wa rafiki yake aliyekuwa anaitwa Salvius Otho na huyo mke wake aliitwa Poppaea.
Mwaka 59 baada ya Kristo, Nero kama nilivyokuambia hapo awali kuwa alipanga mauaji ya mama yake na mwaka huo huo alimtaliki mke wake aliyeitwa Octavia (huyu ndiye binti ya Claudius) na kumuoa Poppea –yaani mke wa rafiki yake. Baada ya kumuoa akampa jina Augusta.
Kutokana na kutotulia kwake, Nero alianza kuonja mporomoko mkubwa wa kiuchumi katika dola yake hata washirika wake walichukizwa naye. Katika harakati za kurekebisha uchumi katika dola yake, mwaka 62 baada ya Kristo Nero alifanya marejereo ya sheria iitwayo Maiestas, sheria ambayo ilisababisha marajiri wengi kuuawa kwa tuhuma tu jambo ambalo lilizidi kuchochea chuki na uhasama dhidi yake.
Kanisa halitausahau mwaka 64 baada ya Kristo mwaka huo ndipo yalipoanza madhulumu ya wakristo. Ilikuwaje. Nero katika harakati za kurekebisha uchumi na kujaribu kurudisha uhusiano wake na watu, alipanga kuurekebisha na kuujenga upya mji wa Roma ambao wakati huo ndiyo ulikuwa makao makuu ya dola ya kirumi. Alichokifanya yeye ni kusababisha moto mkubwa kuunguza mji huo kusudi baada ya kuuungua aujenge upya. Jambo hilo alilifanya kwa siri, kumbe siri hiyo ilifichuka watu walianza kumsakama tena ndipo Nero alipozihamishia tuhuma hizo kwa wakristo ambao wakati huo walionekana kuwa watu wa pekee. Wakristo wengi waliuawa kikatili hasa mjini Roma.
Kabla ya kuanza mauaji hayo ya wakristo, matukio niliyoyataja hapo awali, yaani ya kushuka kwa uchumi, kuchoma moto mji wa Roma na mauaji ya matajiri, yalimpunguzia Nero umaarufu na kukaanza vulugu sehemu nyingi za dola yake. Kulikuwa na migomo na maandamano mengi hasa Afrika, Hispania-sehemu ambazo wakati huo zilikuwa chini ya dola ya kirumi. Hata baada ya kuanza madhulumu hayo, NERO hakuweza kurudisha heshima yake na machafuko yalizidi na misukosuko iliongezeka. Mnamo tarehe 9/6/68 baada ya Kristo Nero aliamua kujiua na huo ndiyo ukawa mwisho wa historia ya maisha yake hapa duniani. Alikufa akiwa kijana tu wa miaka 31 ya kuzaliwa. Baada ya kifo chake dola hiyo iliongozwa na mtawala aliyeitwa Galba aliyefanya kazi kwa mwaka mmoja tu akafuatiwa na wengine hadi mwaka 476 ikiwa chini ya Romulus Agustus kama mtawala wa mwisho kabla ya kuangushwa kwa dola hiyo ya kirumi na wabaribaria.
Kwa hii ndiyo historia ya Nero aliyekuwa mtawala wa Dola ya kirumi. Anakumbukwa sana katika historia ya kanisa letu kwa sababu hasa ya uovu alioufanya kama nilivyokueleza hapo awali kuwa aliwaua mitume Petro na Paulo, aliwaua matajiri wengi wa nchi yake, aliuchoma moto mji wa Roma na kisha kuwatesa na kuwaua kikatili wakristo wengi sana. Kwa kweli sehemu kubwa ya kipindi cha utawala wake kiligubikwa na madhulumu.
Lakini nilikuambia pia kwambwa, huyu Nero hakuwa mbaya tangu kuzaliwa. Mwanzoni alikuwa mtu mwema tu na kipenzi cha watu. Alikuwa mwanamichezo na mpenda maendeleo lakini mke aliyemtwaa kutoka kwa rafiki yake ndiye aliyempotosha hata akapewa rekodi mbaya ya maisha yake hapa duniani. Kwetu sisi hilo liwe fundisho. Watu tunaweza kuwa wema lakini wema huo unageuka na kuwa ubaya kwa kupotoshwa na watu. Mwishoni mema yote husahauliwa na mabaya ndiyo hurekodiwa. Kama illivyompata bwana Nero.
Cc.
Palantir