Baraza la Mitihani la Taifa linafanya kazi kwa umakini sana.
Inapotokea kuna suala lolote la udanganyifu katika mitihani ambao unaweza kupelekea kufutiwa matokeo au kufungiwa kituo, huwa hawakurupuki.
1. Wanafungua faili, na wanalipeleka kwa wataalamu wa upelelezi wa makosa ya kughushi na udanganyigu. (Polisi Makao makuu)
2. Kitengo hiki kinafanya uchunguzi na kikikamilisha uchunguzi wake kinashauri Baraza kama kuna udanganyifu au la.
3. Baraza linachukua hatua.
4. Baraza linatunza mafaili ya upelelezi kama ushahidi kwa watakaodhani haki haikutendeka.
Vielelezo hivyo na mafaili vipo, na endapo Shule yoyote au kikundi chochote kinadhani kina sababu za kutosha za kupinga hatua za baraza, kuna utaratibu unaoweza kufanyika wa hata wao kwenda pale na kuoneshwa ushahidi huo.
Tume nyingi tu zimeshaundwa kushughulikia malalamiko kadhaa yaliyokwisha tolewa kuhusu utendaji wa baraza, lakini zote zimetoka zimeridhika na utendaji huo.
Hivi karibuni, Wanasiasa na wanaharakati wa Zanzibar walikaribishwa na Baraza kujionea udanganyifu uliofanywa na watoto wa Sekondari za Zanzibar ambao ulipelekea kufutwa kwa matokeo ya wanafunzi 1200. Wanasiasa hao na wanaharakati walitoka wameridhika, kama inavyoonesha kauli hii ambayo Waziri wa Elimu wa Zanzibar aliitoa kwenye Baraza la Wawakilishi:
Kumbuka Waziri wa Elimu wa Zanzibar ni Muislamu na anawakilisha maslahi ya Wazanzibar ambao walikuwa na jazba sana baada ya matokeo hayo kufutwa.
SMZ yakubali wanafunzi 1,200 wafutiwe matokeo
Imeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar; Tarehe: 4th April 2012
HabariLeo | SMZ yakubali wanafunzi 1,200 wafutiwe matokeo
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imekubaliana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), kwa hatua yake ya kuwafutia matokeo ya mitihani ya kidato cha nne wanafunzi 1,200 kutoka Zanzibar baada ya kubainika kufanya udanganyifu kwa kushirikiana na wasimamizi wa mitihani.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema hayo wakati akijibu hoja za wajumbe waliopitisha Muswada wa Kuanzishwa kwa Bodi ya kufanya tathimini ya vipimo vya elimu Zanzibar.
Shaaban alisema SMZ iliwasiliana na NECTA kuhusu kuwepo kwa taarifa za kuvuja kwa mitihani pamoja na wanafunzi wengi wa Zanzibar kufutiwa mitihani yao ya kidato cha nne waliofanya mwaka jana.
"Tulifanya mawasiliano na kupeleka mjumbe wetu huko, lakini baada ya utafiti ilibainika kwamba wanafunzi wamefanya udanganyifu mkubwa wa mitihani yao baada ya kupata vielelezo mbalimbali," alisema Shaaban.
Alisema hata hivyo SMZ imeunda chombo kuchunguza suala hilo la kufutiwa kwa wanafunzi wa Zanzibar mitihani ya kidato cha nne, lakini taarifa za awali pamoja na uthibitisho wake unaonesha kwamba wanafunzi wamefanya udanganyifu ambao ni kinyume cha maadili ya mitihani.
Alisema hivi sasa wanafunzi wengi wanakabiliwa na dhana potofu ya kusubiri kununua mitihani ya taifa ya kidato cha nne na sita na kuacha kusoma kwa bidii.
Aidha, Shaaban aliwataka wazazi nao kuacha kabisa tabia ya kushawishiwa na watoto wao kununua mitihani ya taifa, kwani kufanya hivyo madhara yake ni makubwa ikiwemo kufutiwa mitihani ya taifa.
Akijibu hoja za wajumbe, Shaaban alisema SMZ haina mpango wa kujiondoa katika Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kwani chombo hicho kipo kwa mujibu wa sheria kikiwa ni taasisi ya Muungano.
"Hatuna mpango wa kujiondoa katika chombo cha NECTA......tumeunda Bodi ya kuangalia tathimini ya vipimo vya elimu, lakini haina maana kwamba tunajiondoa katika Baraza la Mitihani la Taifa," alisema.
Wajumbe wengi wa Baraza la Wawakilishi waliochangia muswada huo waliitaka Zanzibar kujiondoa NECTA baada ya kuwepo tuhuma za kufutiwa mitihani yao taifa kidato cha nne wanafunzi wengi kutoka Zanzibar.
Mimi ningekushauri ndugu yangu kama unadhani una malalamiko ya msingi, uende pale na mbunge wako au Mwakilishi wa Taasisi inayokutetea, utaoneshwa vielelezo vyote ujiridhishe kuwa haki imetendeka. Maneno matupu kama haya ni kupandikiza chuki za kidini ambazo hazitakusaidia wewe wala yeyote yule Tanzania hii.