Sunday, 12 July 2009 16:53
Na Benjamin Masese
WAUZAJI wa vocha za simu wamesitisha utoaji huduma hiyo siku chache baada ya tamko la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwataka wateja kununua vocha kwa mujibu wa bei zilizoandikwa juu ya kadi hizo.
Hatua hiyo imetokana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi TCRA, Bw.John Nkoma aliyeagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mawakala na wauzaji wa rejareja waliopandisha bei kinyume cha utaratibu.
Wakizungumza na Majira Dar es Salaam jana wafanyabiashara hao, walisema wameamua kusitisha huduma hiyo kutokana na bei wanayonunulia wao kuwa juu huku wao wakizuiwa kupandisha bei.
"Vocha zimepanda kutoka sh.450 hadi sh. 490 katika maduka ya jumla (mawakala) tofauti na ilivyokuwa awali hivyo haiwezekani tukafanya biashara kwa faida ya sh. 10, kinachotakiwa bei irekebishwe kuanzia kwa mawakala,"alisema muuzaji wa reja reja, Bw. Sadiki Ndege.
Alisema kuwa wao kama wauzaji wadogo wanashindwa kuelewa nani mkweli kuhusu bei halisi ya vocha hizo hivyo kuzitaka kampuni husika kubainisha bei halisi za vocha zake.
Alisema bei za jumla wanazouziwa na mawakala ni; Vodacom sh. 490, Tigo sh. 485, Zantel sh.480 na Zain sh.483 ambapo faida ni kati ya Sh.10 hadi 20.
Naye mteja mwingine, Bw. Godfrey Emanuel alisema wamelazimika kuachana na biashara hiyo kutokana na kulazimishwa kuuza bei isiyokuwa na faida kwao.
"Sisi tunazilaumu kampuni za simu kwani zinatambua kabisa kiwango kilichopanda na hata risiti za mawakala zinaonesha lakini wao wameshindwa kututetea badala yake wanatugandamiza," alisema Bw. Emanuel.