Mkanganyiko wa Mauzo ya Vocha za Simu kwa Bei ya Rejareja
Serikali inastahili lawama
Na Mwana wa Haki
NILIPOKUWA masomoni nchini Marekani, kwa masomo ya Stashahada (ya kwanza) ya Uchumi, huku nikiwa nimeongeza nondo ndogo (wenyewe wanaita Minors) za Uandishi wa Habari na Sayansi ya Tarakinishi, sikuwahi hata siku moja kufikiria kwamba ningeweza kunufaika na taaluma hii ya uchumi, haswa katika uchambuzi wa mkanganyiko ambao umejitokeza kwenye Bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2009-2010.
Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango, imepitisha bajeti ambayo inaathiri mwenendo mzima wa kiutendaji wa biashara ya mawasiliano kwa simu za mkononi, yaani, Mobile Cellular Telephony, kama ifuatavyo:
Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2009-2010 imeainisha kwamba, mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya Ongezeko la Thamani, hususan kwenye sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi, ni kama ifuatavyo:
72. (x) Kutoza kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye muda wa maongezi kwenye simu kwa kutumia bei halisi inayoonyeshwa kwenye vocha badala ya bei nafuu anayotozwa muuzaji wa jumla. Lengo ni kuhuisha mapato yatokanayo na chanzo hiki cha kodi na kuziba mwanya wa ukwepaji kodi;
Kidonda hiki kinaleta maumivu makubwa kwa wauzaji wa jumla wa vocha za matumizi ya simu za mkononi, lakini, kana kwamba kidonda hiki hakikutosha, Serikali yetu tukufu ikaongeza kingine, kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa:
74. (i) Kutoza Ushuru wa Bidhaa katika huduma za simu za mkononi pale vocha au muda wa maongezi unapouzwa badala ya kusubiri hadi muda wa maongezi utumike; na
(ii) Kurekebisha kwa sailimia 7.5 viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu, isipokuwa zile za mafuta ya petroli.
Sipendi, narudia, sipendi kuonekana kwamba mimi ni mtoto mtukutu, lakini nauliza: Aliyefanya marekebisho haya yasiyo na kichwa wala miguu, alikuwa anatumia dawa aina gani za matatizo ya akili?
Hii haingii akilini hata kidogo. Hata kidogo!
Tuanzie kwenye suala la kodi ya Ongezeko la Thamani, au Value Added Tax (VAT). Hapo awali, ina maana kwamba VAT ilikuwa inatozwa KABLA au BAADA ya gharama inayooneshwa kwenye vocha? Kwa mfano, hapo awali kabla ya mkanganyiko huu wa kiwendawazimu vocha ya thamani (iliyochapishwa) ya Shilingi Elfu Moja (TZS 1,000/=) ilijumuisha yafuatayo:
Gharama halisi ya muda wa maongezi, bei ya jumla TShs. 750/=
(ikijumuisha kodi nyinginezo)
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT 20%) TShs. 150/=
(hii imejumuishwa kutoka kwenye thamani
halisi ya vocha)
Jumla ya Thamani (pamoja na VAT, bei ya jumla) TShs. 800/=
Kwa wale wataalam wa masuala ya kodi, naomba mnikosoe, lakini hivi ndivyo mimi nilikuwa nimeelewa, kwamba, VAT ilikuwa inatozwa kwa kuzingatia gharama halisi ya vocha, kwa bei ya jumla.
Kwa kuwa tayari mwuzaji wa jumla amelipa VAT, mwuzaji wa rejareja anauza vocha hiyo kwa thamani ya TShs. 1,000/=, na kujipatia faida ya TShs. 200/=.
Kilichobadilika hapa ni VAT kutozwa kwa gharama halisi ya vocha, yaani, TShs. 1,000/=! Hapo, ukifanya hesabu, kwa kiwango kipya cha asilimia 18, unapata TShs. 180/=, na kuifanya bei mpya ya hiyo vocha kuwa TShs. 1,180/=!
Ninauliza, toka lini thamani ya Shilingi Elfu Moja ikawa Shilingi Elfu Moja na Mia Moja na Themanini? Huu wi wizi wa mchana huu?
Hiyo tofauti, ya nyongeza ya TShs. 180/=, nani anatozwa? Ni mteja, mtumiaji wa mwisho. Bei ya jumla iko pale pale, na mwuzaji wa rejareja bado ananunua (labda?) kwa bei ile ile, ila anakuuzia wewe na mimi kwa bei mpya, ambayo bado ina utata
bei mpya isiyo rasmi ikaja kuwa TShs. 1,100/= (kwa vocha ya TShs. 1,000/=), TShs. 2,200/= (kwa vocha ya TShs. 2,000/=), TShs. 5,500/= (kwa vocha ya TShs. 5,000/= na TShs. 11,000/= (kwa vocha ya TShs. 10,000/=)!
Astghafirullah!
Wizi mtupu!
Suala la pili la Ushuru wa Bidhaa wala sitaligusia, maana hili la kwanza bado halijakaa vizuri. Bado sana! Pamoja na usomi wangu wote, tena wa nondo ya nguvu ya Marekani, hii haijaniingia akilini. Nawaomba wanazuoni wenzangu wanisaidie hapa, maana imekaa vibaya mno hapa!
Nikiangalia kwa upande wa sheria, hususan kwa kuwalinda watumiaji wa mwisho, walaji, mimi na wewe, Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), iliunda Kamati ya Mashauriano ya Walaji ya TCRA, yaani, TCRA-Consumer Consultative Council, ambayo jukumu lake kuu ni kuhakisha kwamba haki za walaji zinalindwa KILA WAKATI!
Cha ajabu ni kwamba, mitaani tunauziwa vocha kwa bei ya kuruka na TCRA-CCC wamekaa kimya! Kimya kabisa! Tuli, kama vile mtu anayenyolewa kichwa kwa maji na wembe, asijiguse wembe ukamkata kichwani! Lahaula! Mambo gani tena haya? Ina maana huko TCRA-CCC hawakuliona hili? Mbona hawajatoa tamko haraka na kuitisha Mkutano wa Dharura na watoa huduma (au ni hujuma) wa mawasiliano ya simu za mkononi, ili ufumbuzi upatikane? Kwa nini mlaji anapuuzwa kihuni huni wakati ni yeye ndiye anayetoa fedha mkononi mwake, kuwalipa wenye mitandao hii ambayo sasa inaonekana kuwa dili la aina yake? Nadhani mnanielewa nikisema dili sihitaji kuongezea.
Mimi napenda kutoa ushauri wangu, kama ifuatavyo, katika hitimisho la makala tete hii:
1. Ili kuonesha hasira zetu, sisi, kama walaji, tuendeshe mgomo baridi wa saa 24, wa kutopiga simu au kutuma ujumbe mfupi, kuwapa somo watu hawa kwamba kimya chetu kisitambulike kama unyonge wetu, sisi si wanyonge katu!
2. Baada ya mgomo huu, tuanzishe Chama Cha Watumiaji wa Mitandao ya Simu za Mkononi (Tanzania Cellular Subscribers Association), ili kuhakikisha kwamba Chama hiki kinakuwa mstari wa mbele daima kuwalinda watumiaji wa teknolojia hii, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kila tukio la, (a) mtumiaji kutopata thamani halisi ya fedha zake anazotumia kwenye mtandao, (b) mtumiaji kukatwa fedha kwa makosa na kutorejeshewa fedha hizo, (c) mtumiaji kupoteza fedha wakati wa kuhamisha salio kutoka namba moja hadi nyingine, na kadhalika.
Watanzania tunaaminika kwamba ni watu wapole na hivyo, kutokana na upole wetu huu tunaweza kufanyiwa hujuma au ubabe wa aina yoyote ile pasi na sisi kujibu mapigo.
Ndugu zangu, nawaombeni mtafakari haya yafuatayo:
1. Leo tumepandishiwa bei ya vocha za simu za mkononi kiholela, kinyume cha sheria, tumeibiwa. Hatujatoa tamko.
2. Mimi sijui wewe mwenzangu ninavipata vijisenti vyangu kwa shida; kama wanavyosema wenzangu kule Eldoret, Ninahenya sana! Huoni uchungu kuibiwa mchana kweupe fedha zako, kwa madai kwamba bei imepanda?
3. Kama wameweza kutupandishia bei kiholela, leo, kutubia mchana kweupe, kesho watafanya nini cha ziada ili tuamke usingizini, na kuanza kudai haki zetu? Tutalala usingizini MPAKA LINI?
Natumai tutalifanyia kazi suala hili, hususan lile la mgomo
ni suala la kuamua tu, kwamba TUMECHUKIA na TUTAWANYIMA MAPATO hawa wenye mitandao ya simu pamoja na maswahiba zao, kwa muda wa saa 24! Nadhani ni adhabu tosha.
Lini mkakati huu ufanyike? Napendekeza siku ya Ijumaa, Julai 31, 2009, ili wote tupate fursa nzuri ya kujiandaa kuwa kimya kwa siku hiyo, kuanzia saa 6 za usiku wa kuamkia Ijumaa, Julai 31, 2009, hadi saa 6 usiku, wa kuamkia Agosti 1, 2009! Jina rasmi la siku hiyo litakuwa Siku ya Ukimya Mkuu, kwani, hata kwenye UKIMYA kuna SAUTI KUBWA!
Tuongee kwa SAUTI KUBWA kwa KUKAA KIMYA na kutozungumza kwa simu wala kutuma ujumbe mfupi, tutoe fundisho kwamba, HATUTACHEZEWA TENA, SASA BASI, IMETOSHA!
Watanzania, mpo? Mna uchungu na nchi yenu? Haitatokea fursa nyingine tena ya kuwaambia hawa wafanyabiashara waliokuja kuchuma kwenye migongo yetu, kwamba, ENOUGH IS ENOUGH! Kazi kwenu!