Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
MKATABA WA SHILINGI BILIONI 4.7 KUWAFIKISHIA WANANCHI MAJI SAFI NA SALAMA KATA YA MUGANGO NA TEGERUKA WASAINIWA
WIZARA ya Maji imemtaka mkandarasi kampuni ya Kiure Engineering L.T.D. kukamilisha kazi ya mradi wa Maji Kata ya Mugango na Tegeruka kwa kuzingatia muda wa mkataba.
Kauli hiyo ya Wizara kwa niaba ya Serikali imekuja mara baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kiasi cha shilingi bilioni 4.7 kati ya mkandarasi huyo na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MUWASA) ambao ndio wasimamizi wa mradi ili kuvifikia vijiji 6 vya Kata hizo.
Akizungumza kwenye tukio hilo la kusainiwa mkataba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, amesema hakuna sababu za kuongeza muda nje ya mkataba katika utekelezaji wa mradi. Mkataba ni miezi 6 mradi ukamilike na sio vinginevyo ili dhamira ya Rais Samia ya kumtua Mama ndoo kichwani iweze kukamilika.
Katibu Mkuu huyo amesema fedha zipo ndio sababu mkataba umesainiwa hivyo hakuna sababu za kucheleweshwa kwa mradi. Wizara imejipanga vizuri kuwawezesha wataalamu wake ili kuwa na uwezo mkubwa wa usimamizi mzuri wa miradi.
"MUWASA mmeona wamesaini mkataba leo na Wizara inawaamini katika usimamizi wa miradi na hata huu watamsimamia vizuri mkandarasi ili aweze kutekeleza kwa wakati. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Musoma vijijini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo kwa ufuatiliaji wa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji" - Mhandisi Nadhifa Kemikimba
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo ameishukuru Serikali ya awamu ya 6 kwa kutoa fedha kwaajili ya miradi ya Maji na kusema kwa sasa katika Vijiji vyote 68 ndani ya Jimbo ipo miradi ya Maji ambayo inaendelea na mingine imekamilika na wananchi wanapata maji.