Na Eckland Mwaffisi
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Bw. Zitto Kabwe amesema kusuasua kwa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kumechangiwa na idadi ndogo ya wawekezaji waliojitokeza kuomba zabuni kuendesha reli hiyo, hivyo kuifanya Serikali kukosa mbadala na kumua kuipa Kampuni ya RITES kutoka India kwa mtindo wa 'hakuna namna.'
Bw. Zitto aliyasema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na kipindi cha Mambo Leo, kinachorushwa na Kituo cha Times 100.5 fm
Alisema migogoro mbalimbali ya wafanyakazi inayoendelea TRL, inachangiwa na mwekezaji, Kampuni ya RITES kushindwa kuboresha huduma wanazotoa katika kiwango kilichoratajiwa na kuongeza kuwa kampuni imeshindwa hata kuboresha usafiri wa mizigo na abiria hadi sasa.
Alifafanua kuwa, pamoja na Serikali kumiliki asilimia 49 na RITES asilimia 51, Serikali imeendelea kubeba mzigo mzito zaidi kuliko kampuni hiyo ambayo wananchi waliamini ingeleta mabadiliko makubwa kwa kuboresha huduma hizo.
Alieleza kuwa katika mchakato wa kutangaza zabuni ya uuzaji Shirika la Reli Tanzania (TRC), kampuni mbili tu ndizo zilijitokeza ambazo ni RATES ya India na mwekezaji mwingine kutoka Afrika Kusini ambaye hata hivyo alijitoa hatua za mwisho hivyo kuifanya Serikali kukosa namna na kuingia mkataba na mwekezaji aliyebaki(RITES) .
Sababu kubwa ya mlundikano makontena bandarini ni huduma mbovu zinazotolewa na TRL, nchi mbalimbali duniani, hutumia usafiri wa treni kusafirisha mizigo yao tofauti na Tanzania hivi sasa ambayo haina huduma hiyo pamoja na kuwepo mwekezaji aliyepewa shirika hilo, alisema.
Alidai kuwa mwaka 1996, Serikali ilifanya maamuzi mabovu kubinafsisha mashirika ya umma na kwamba yalikuwepo mashirika ambayo hayakupaswa hata kufikiriwa kuingizwa katika mchakato wa kubinafsishwa.
Alitoa mfano wa Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwamba haikupaswa kuingizwa katika mpango huo zaidi ya kufanyika mabadiliko ya uwekezaji kutoka serikalini.
Alisema Tanzania imebahatika kwa kuwa na nishati nyingi ya gesi na mafuta ambayo kama TANESCO itaongezewa nguvu na uwezo wa kuzitumia nishati hizo, Tanzania itakuwa nchi ya kwanza Afrika kutoa huduma ya umeme na kulifanya shirika hilo kujiendesha kwa faida.
"Mwaka 2006 TANESCO ilipata hasara ya sh. bilioni 167 ikiwa chini ya usimamizi wa Net Group Solution, ambayo baada ya kumaliza mkataba wake, uongozi mpya chini ya Serikali uliweza kupunguza hasara hiyo kutoka sh. bilioni 167 hadi sh. bilioni 62. Kufikia Desemba 2008, hasara hiyo imepungua kutoka sh. bilioni 62 mpaka bilioni 30," alisema.
Alisema Serikali haipaswi kuuza shirika hilo zaidi ya kuliboresha kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati yake ikiwa ni pamoja na kuuza hisa zake katika soko la hisa.
Bw. Zitto alisema, Kamati yake ilipendekeza kusitishwa zoezi la ubinafsishaji ili kufanya tathimini na kurekebisha makosa yaliyojitokeza, kwani alidai ubinafshaji uliofanywa nchini kuanzia mwaka 1996, umesababisha mali nyingi za umma kupotea na kunufaisha wachache.
Alitoa mfano mwingine kuwa, Shirika la Ndege Tanzania (ATC),lipo mahututi kiasi cha kuzidiwa na kampuni binafsi ya Precision Air,inayotoa huduma zenye ushindani kibiashara katika soko.
Kamati yangu imetoa pendekezo kwa Serikali, kuipa mtaji wa kutosha ATC ili iweze kutoa huduma zake kwa ubora zaidi na kujiendesha kwa faida ikiwa ni pamoja na kuimarisha viwanja vya ndege katika miji mikubwa na midogo na kuingia katika ushindani wa soko la kibiashara, alisema.
Aliongeza kuwa asilimia kubwa ya marubani wa ndege za Serikali wamezeeka hivyo ni jukumu la Serikali kuwawezesha kielimu marubani wapya ili kuongeza ufanisi wa shirika hilo.
Alisema, pamoja na mapendekezo mengi yanayotolewa na kamati yake, historia inaonesha kuwa, kwa nchi nyingi duniani Serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na Kamati za Bunge.
Alisema, mfano mzuri wa mapendekezo hayo ni yale yaliyotolewa na Kamati ya Bunge kuhusu Richmond iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe lakini hadi sasa Serikali imeshindwa kuyafanyia kazi.
Source: Majira
Hili shirika letu la reli silielewi. Nadhani kuna elements nyingi za ufisadi ndani yake na sasa shirika linaelekea kufa kutokana na utendaji mbovu. Sijui sana kuhusu uendeshaji wa hili shirika letu la reli labda kuna wadau humu wanajua zaidi.