MKENYA ALIYESHINDA TUZO YA MWALIMU BORA DUNIANI AKUTANA NA TRUMP: walimu Peter Tabichi kutoka nchini Kenya aliyetunukiwa Tuzo ya Mwalimu Bora Duniani Machi mwaka huu, amekutana na Rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya nchi hiyo huku akitarajiwa baadaye kuhutubia mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mwalimu huyo ambaye ni mwalimu wa somo la Sayansi, akiwa ni mtawa wa Shirika la Kikatoliki la Mtakatifu Fransisco wa Kapuchini ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwashinda washiriki 10,000 waliochaguliwa kutoka nchi 179.
Akizungumzia umuhimu wa tuzo hizo mwalimu Tabichi amesema, anatamani kila mtoto afikie ndoto yake na ndiyo maana inasemekana kuwa katika kipato chake (mshahara) mwalimu huyo hutoa takribani asilimia 80 ya fedha yake kusaidia familia masikini.
Akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mseto ya Keriko iliyopo katika Kaunti ya Nakuru,Kaskazini magharibi mwa jijini la Nairobi, mwalimu Tabichi amesema, kazi hiyo inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za ukosefu wa vifaa kama vitabu na upungufu ya walimu shuleni kwake.
Aidha ameongeza kuwa, kazi ya ufundishaji pia huwawia ngumu kutokana na darasa moja linalopaswa kuwa la wanafunzi 35 – 40 hulazimika kuwa na wanafunzi 70 -80 huku wengi wa wanafunzi hao wakilazimika kutembea umbali mrefu katika barabara mbovu.
Akizungumzia sababu ya kushinda Tuzo hizo, Stephanie Grisham mmoja wa watendaji wa Ikulu ya Marekani amesema, "Uwajibikaji wake na kazi yake ngumu na imani kwa talanta ya wanafunzi, imeifanya shule anayofundisha kuibuka kidedea baada ya kushindana na shule zilizo bora nchini katika mashindano ya kitaifa ya sayansi.”
#AZAMTWO #AzamUTV #Azamtvtz #AzamTVApp