SEHEMU YA 60
Nilipotoka pale hospitali, niliendesha gari kwa makini, nikichelea nisije kupatwa na ajali kama ilivyompata mume wangu, nahisi mume wangu aliendesha akiwa amechanganyikiwa, na sio kwasababu ya ulevi.
Nilitaka nifike nyumbani, maana kulikuwa na mambo nilihitajika kuyachunguza, lakini pia nilihitajika kwenda kuonana na rafiki yangu, ambaye nasikia karudi kutoka huko alipokwenda kusoma, nilishindwa kuelewa ni kwanini akaamua kurudi haraka hivyo..nahisi kuna sababu kubwa sio bure…
Nikaona nipitie kwake kwanza kabla sijafika nyumbani, nikakumbuka kuwa sehemu aliyokuwa akiishi awali, alikuwa amepakabidhi kwa mwenye nyumba, na alisema akirudi atakuwa akiishi kwa ndugu yake mmoja, japokuwa nilimuambia kwangu kuna nafasi akirudi anaweza kuja kuishi kwangu hadi hapo atakapomalizia nyumba yake anayojenga.
Nilipofika hapo kwa ndugu yake, nikaambiwa hayupo…
‘Hayupo katoka au hakufikia hapa kwako…?’ nikauliza
‘Amefikia hapa, ila aliondoka muda tu, aliniaga kuwa anakwenda hospitalini…’nikaambiwa
‘Anaumwa…?’ nikauliza
‘Hapana kasema anakwenda kumuona mgonjwa…’nikajibiwa na hapo nikahisi mwili ukinichemka, nikajua atakuwa kaenda kuonana na mume wangu, lakini mbona hatukukutana naye njiani, au kachukua usafiri gani
‘Na mtoto wake yupo wapi?’ nikauliza.
‘Mtoto wake…!! ’akasema kwa mshangao, na mimi nikasema
‘Ndio, si ana mtoto mdogo, au…?’ nikauliza.
‘Hayo mengine utamuuliza mwenyewe, ….’akasema na alionyesha kama hataki kumuongelea ndugu yake, nikaona hakuna haja ya kupoteza muda.
‘Basi sawa akirudi mwambie nilikuja kuonana naye…kama hatajali nataka nionane naye…’nikasema
‘Sawa nitamuambia….’akasema na wakati nataka kuondoka, huyo mwenyeji akaniuliza
‘Kwani kuna tatizo, gani maana kuna mtu mmoja alikuja,..hata sijui ni kwanini rafiki yako anaogopa kufuatilia …’akasema
‘Kufuatilia nini…?’ nikauliza
'Tuyaache hayo, hayanihusu sana...nisije kuharibu lawama ikarea kwangu...'akasema
'Lawama gani kwani kuna nini kimetokea...?' nikauliza
‘Kama nilivyoambiwa, maswala ya mtoto nisiseme lolote…’akasema
‘Na nani, kwani mtoto yupo…?’ nikauliza
‘Ndio nakuwambia, nimeambiwa nisiseme lolote kuhusu mtoto, na wala sijui lolote kuhusu mtoto…’akasema
‘Sikiliza mimi ni bosi wake, na rafiki yake,…na nina wasiwasi na hali ya mtoto, ndio maana nauliza hivyo…’nikasema
‘Basi akirudi nitamwambia hivyo, …samahani kwa hilo…’akasema
Basi na mimi, nikaamua kurejea nyumbani kwangu, nilipofika nyumbani kwangu kwa kujirizisha tu, nikataka kujua mambo fulani fulani, kwahiyo, nikawa nawahoji tena watu wangu wa nyumbani kuanzia mlinzi hadi wafanyakazi wa ndani, kama kuna mtu yoyote aliwahi kufika hapo, kabla…
Sikuweza kupata nilichokitaka, hapo nikaona nifanye jambo jingine kwa haraka kwa kujirizisha tu..., sikupendelea kufanya hivyo, lakini nikaona ndio muda pekee ninaoweza kufanya jambo kama hilo,…
Nikaanza kupekua vitu vya mume wangu, sehemu zote anapoweka vitu vyake…pia kwenye chumba cha akiba ambacho alikuwa akilala akiwa kalewa, sikupata kitu cha maana, mwishowe nikaona nirejee kwenye maktaba niangalie vyema.
Nikafungua tena lile kabati langu, safari hii kwa uangalifu kidogo, na cha ajabu niliona ile nakala ya mkataba wangu na mume wangu, ikiwa umewekwa pale pale nilipopendelea kuuweka,...!
‘Mhh, nani kairudisha tena,…?’ nikasema kwa sauti ndogo, kwanza sikuugusa, nikachuka kitu cha kuzuia alama za vidole mkononi, nikaanza sasa kuukagua huo mkataba, kwa haraka nikagundua kuwa sio ile nakala yangu, maana ile nakala yangu ilikuwa na alama zangu maalumu, ambazo mtu hawezi kuzigundua, na hiyo nakala haikuwa nayo, kwahiyo ni nakala nyingine!
‘Hii nakala imewekwa baadaye....sio ile nakala yangu.’nikasema ,
Nilichukua ile nakala na kuanza kuipitia kwa haraka haraka, sikuweza kugundua mabadiliko, sijui kwa vile muda huo sikuwa nimetuliza kichwa,...nikaona nipumzike kwanza…nikatuliza kichwa kwa kupata kinywaji cha matunda…
Baadaye nikaichukua ile nakala na kuanza kuipitia kwa makini kidogo nikagundua kitu, kwenye sehemu ya kipengele cha watoto naona kama kuna vitu vimebadilika, lakini bado sikuwa na uhakika , ....nikaanza kuisoma sehemu hiyo kwa makini, ilikuwa sio kazi rahisi, ila niligundua sehemu moja, inasema hivi;
‘Kama wazazi watakuwa wamefariki,..Watoto wote wana haki sawa, na mali ya urithi itagawiwa sawa,.’hili neno `wote’ sikumbuki kama ilikuwa hivyo mwanzoni, nakumbuka tulitumia neno `wetu’ na hili neno wetu kwenye ufafanuzi tuliandika, kuwa linasimama badala ya wanandoa mimi na mume wangu kwa kutaja majina. Nikafungua kwenye ufafanuzi, sehemu hiyo ya ufafanuzi, ilikuwa imeondolewa!
‘Kwanini wafanye hivyo, na ni nani huyu, ni mume wangu na wakili wake nini, na kwanini wafanye hivi, hii sasa imevuka mipaka....’nikasema.
Hapo nikaanza kuingiwa na ufahamu, kuwa kumbe mashaka na wasiwasi ya mume wangu ni kuhus huo mkataba, kumbe nia yao ilikuwa kubadili huo mkataba, nikaanza kusoma tena sehemu nyingine kuna sehemu zimeondolewa na kuongezwa maneno mengine ili kuleta maana fulani, sikuelewa ni kwanini walifanya hivyo.
Nikafungua sehemu nyingine lakini sikuweza kugundua mabadiliko mengine, japokuwa nilihisi kuwa kuna sehemu fulani fulani zimebadilika, lakini kiutalaamu zaidi, na hapo nikaona niwasiliane na wakili wangu, nikampigia simu.
Simu iliita kwa muda bila kupokelewa, na baadaye akaipokea, na kusema alikuwa akimsaidia mgonjwa, maana alikuwa kwao, akimuuguza mzazi wake, nikamwambia hayo yaliyotokea, na akasema;
‘Kuna mtu ana nia mbaya, maana mimi nilipoondoka tu, nilipata taarifa kuwa kuna watu waliingia ofisini kwangu wakaiba baadhi ya vitu, sasa sina uhakika kama ni pamoja na hiyo nakala ya huo mkataba, ni mpaka nikirudi huko ndio nitaweza kulifahamu hilo.....’akasema.
‘Mimi nahisi watu hao lengo lao ni kuhakikisha kuwa wameiba nakala zote, na kuziweka nakala wanazotaka wao,…je kwenye mtandao hukuhidhi chochote?’ nikamuuliza.
‘Katika vitu ambavyo nasikia wameiba, ni pamoja na komputa yangu ambayo nimehifadhia mambo yote, na sijahifadhi sehemu nyingine zaidi, maana sikuwa na mashaka kuwa hali kama hiyo inaweza kutokea, hii sasa ni changamoto kwangu, kazi zote sasa nitaziweka kwenye mtandao ya kudumu..’akasema
‘Ni bora uwe unafanya hivyo , maana kwa hali hii hatutakuwa na na kumbukumbu ya mkataba wetu ule wa awali…’nikasema.
‘Hili nitapambana nalo nikirudi, hata wajifanye wajanja vipi…kiukweli kwa hivi sasa siwezi kufanya lolote, maana namuuguza mama, kwahiyo mambo mengine sitaweza kusaidia…’akasema
‘Sasa kama nakala ya huo mkataba imechukuliwa huko kwako na komputa imeibiwa, tunawezaje kuipata nakala nyingine wapi, maana nahisi wamebadili huu mkataba kwa makusudi maalumu, na cha ajabu wameweza kutumia sahihi yangu kama ilivyo,..ina maana huyu mtu ni mtaalamu kweli wa kugushi hata sahihi za watu....’nikasema.
‘Kama wameamua kufanya hivyo, basi nina imani kuwa hata huko serikalini watakuwa wameshafanya hivyo hivyo,watakuwa wameshabadili huo mkataba na kuweka huo wanaoutaka wao, na kugushi sahihi, sio kazi ngumu sana, maana wanaweza kutumia mtandao..ni shida kidogo, lakini upo utaalamu wa kuligundua hilo....’akasema.
‘Lakini huko serikalini watawezaje kuipata hiyo nakala nyingine, sizani kama wamefanya hivyo hata huko…, ?’ nikauliza
‘Unafahamu hali ilivyo, kama una pesa lolote linaweza kufanyika, sina uhakika sana na hilo, na sijui kwanini wafanye hayo yote,…kwakweli ni mpaka nirudi ndio nitajua cha kufanya…’akasema
‘Mhh, inanitia mashaka hii hali, kwanin lakini…’nikasema
‘Sasa fanya hivi kama unaweza nitumie hiyo nakala, ipige picha sehemu unazohisi zimegishiwa, unitumie, ili na mimi niupitie upya,mimi nitagundua ni sehemu gani wamebadili, na kwanini...hata kama unaweza kunitumia yote itakuwa ni vyema zaidi…si inawezekana hiyo?’ akaniuliza.
‘Sawa nitakutumia, sasa hivi, hiyo ni kazi rahisi tu, ......’nikasema,
‘Itakuwa vizuri, kama hatujachelewa, tunaweza kufanya jambo, usijali, ujanja ujanja wao utakuja kujulikana, japokuwa inanipa mashaka..huyo mtu anajiamini vipi…lazima kuna kitu wanategemea, lakini tutalimaliza hilo, hakuna mjanja juu ys sheria....’akasema
‘Kama hatujachelewa una maana gani..?’ nikauliza na simu ikakatika, nikaona haina haja, nikaanza kazi ya kuipiga picha hiyo nalaka ya mkataba, hadi nikamaliza na kumtumia huyo wakili.
***********
Wakati nataka kuondoka nyumbani, nikakumbuka jambo, nikarudi kule kwenye maktaba yetu na kufungua kabati sehemu ninapohifadhia silaha yangu, niliikuta ipo pale pale, ililinijia wazo la kuichukua hiyo bastola niwe natembea
nayo, ni bastola ndogo
‘Kwanini nitembee na silaha…aah, haina haja…’nikasema kwa suti ndogo
Baadae nikaondoka hapo nyumbani hadi ofisini kwangu, na nilipofungua kabati langu, nikakuta nakala ya mkataba ipo, imerejeshwa na kuwekwa pale pale ilipokuwa, nikaichunguza na kugundua kuwa sio ile nakala yangu ya awali!
Nikaifungua na kuanza kuisoma, ni kama ile ile niliyoikuta nyumbani kwangu, na safari hii nilitulia kidogo, nikagundua sehemu kubwa ya vipengele vya umiliki wa mali, vimbebadilishwa pia.
‘Huyu mume wangu anataka nini, ina maana akili yake yote ipo kwenye mali, kama ni mali si angelisema tu…kwanini anafany ahaya yote..’nikawa naongea peke huku napitia sehemu hiyo kwa uangalifu zaidi, ndio nikaona sehemu ikiwa imebadilishwa kwa kirafu zaidi
‘Mume ndiye atakayekuwa muangalizi wa mali yote na mwenye mamlaka ya mali zote, na atakuwa na uhuru wa kumuingiza mtu yoyote katika umiliki wa mali kama atakavyoona yeye inafaa, hata bila ya idhini ya mke wake...’
‘Oh, hii mpya…’nikasema
‘Hii seehmu haikuwepo kwenye mkataba wa awali, ilitakiwa kila kitu kisifanyike bila ya makubaliano,…na awali mimi niliona iwe hivyo, kuwa mume ndiye anakuwa na mmalaka zaidi, lakini mume wangu mwenyewe ndiye alipinga hiyo hoja, akisema;
‘Baba yako hatatuelewa,..atahisi mimi nataka mali yake…’alisema hivyo
‘Sasa unataka tuweje..au tutamsikiliza wakili wetu, yeye akapendeleza kuwa kila kitu kisifanyike bila ya maridhiano ya pande mbili, na ikawekwa sawa kisheria, sasa hilo wamelifuta na kuweka maneno mengine.
Nikasoma maelezo mengine, lakini akili yangu ilikuwa imechafuka, hasira zilianza kunipanda, hapo hapo nikampigia simu wakili na kumuulizia hicho kipengele, mbona hakikuwepo, ndipo akaniambia kuwa hawo watu wamefanya hivyo makusudi, huenda kuna mtu wanataka kumuingiza kwenye umiliki wa mali...
‘Kumuingiza kwa vipi?’ nikamuuliza.
‘Kwenye maelezo ya mwanzo, ilikuwa imesema kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingizwa kwemue umiliki wa mali, au kwenye hisa za kampuni , zaidi ya wewe na mume wako na watoto wenu. Na watoto wenu ikiwa na maana mlizaa wewe na yeye.hilo wameliondoa na kuweka maneno yao…’akasema
‘Kwahiyo lengo lake ni nini hapo…?’ nikauliza
‘Lengo lake ni ili awe mwenye mamlaka zaidi yake na ataweza kufanya kila kitu bila ya kukushirikisha wewe, labda akiona kuna umuhimu huo…’akasema
‘Kwa mtizamo huu, moja kwa moja mume wangu ndiye yupo nyuma ya haya?’ nikamuuliza.
‘Kwa jinsi ilivyo inaonyesha hivyo.... nahisi anafanya hivyo kwa shinikizo fulani, ....’akasema wakili
‘Kwa ushauri wako nifanye nini, nitoe taarifa polisi....?’ nikamuuliza.
‘Bado huo sio muda muafaka, inabidi kwanza kuchunguza hili kwa ukamilifu wake maana hapo kuna kesi ya kugushi, je unawezake kulithibitisha hilo, wakat nakala zote zinasema hivyo…na ukitoa taarifa polisi kwa sasa moja kwa moja, atakayekamtwa ni mume wako, na kutokana na hali yake unaweza ukammaliza kabisa, ...’akasema.
‘Sasa nifanyeje wakili wangu…?’ nikamuuliza.
‘Ngoja kwanza niupitie huo mkataba wote, halafu nitakuwa na nafasi ya kusema lolote,...usijali hawo wamechukulia kienyeji sana, huwezi ukafanya hayo waliyoyafanya kirahisi hivyo, labda wawe na mtu fulani kwenye sehemu za uandikishaji wa mikataba hiyo…’akasema
‘Ok…kwahiyo bado tuna nafasi ya kulimaliza hili, nataka tulimaze na ule mkataba wa awali ufanye kazi yake, sitaki utani tena..’nikasema
‘Hii ni hatari, kama kuna watu wa namna hii kwenye taaluma yetu, wanatuharibia sana, ni lazima hili jambo likemewe, ngoja nirudi, nitahakikisha nalifanyia kazi..’akasema.
‘Nahisi anaweza kuwa huyo wakili wa mume wangu...’nikasema.
‘Wakili wa mume wako, ina maana mume wako keshatafuta wakili mwingine, kwanini...?’ akaniuliza
‘Ni yule wakili Makabrasha.....’nikasema.
‘Oh, balaa, huyo mtu tena…!!, nakumbuka nilishawaonya kuhusu huyo mtu, ...’akasema.
‘Mume wangu sijui kaingiwa na wazimu gani, nahisi kuna tatizo kubwa kwa mume wangu, sio yeye, sio mume wangu ninayemfahamu, sasa wewe, utarudi lini?’ nikamuuliza.
‘Kiukweli sijui, maana hali ya mzazi wangu sio nzuri, na siwezi kumuacha katika hali kama hii, kama hali yake itakuwa hivi, nitachelewa sana, na ikibidi nitakuja naye huko kwa ajili ya matibabu zaidi japokuwa yeye mwenyewe kakataa, ningelishamchukua, nije naye huko, lakini hakubali, kabisa, yeye anasema anataka afie nyumbani kwake, kwahiyo kwa hivi sasa siwezi kusema lolote, ....’akasema.
‘Sawa nimekuelewa,…’nikasema
*************
Nilimuita yule mfanyakazi wa ofisini ambaye ndiye anatunza ufunguo, nikamuhoji , Safari hii nikawa mkali, nikamuuliza anieleze ukweli, kama kweli hakuna mtu analiyewahi kuingia kwenye hiyo ofisi yangu;
‘Niambie ukweli ni nani ambaye aliingia ofisini kwangu, maana nina ushahidi kuwa kuna mtu aliingia wakati mimi sipo kazini, na kuchukua vitu vyangu muhimu kwenye kabati langu?’ nikamuuliza.
‘Bosi hakuna mtu aliyeingia,mimi nina uhakika, maana ufungua ninao mimi, na sijawahi kuuacha popote, kama ulivyoniagiza,....’akalalamika akionyesha wasiwasi.
‘Sasa sikiliza, kama nitakuja kugundua kuwa kuna mtu aliyeweza kuingia ofisini kwangu, na wewe unafahamu ujue ndio mwisho wa ajira yako, na nitahakikisha unakwenda jela...’nikasema kwa ukali na yeye akaniangalia kwa mashaka, lakini aliendelea kukataa kuwa hakuna mtu aliyewahi kuingia, au yeye kumruhusu mtu yoyote kuingia kama nilivyomuagizia.
‘Sawa nitaiarifu polisi, na watafanya uchunguzi , na ujue wewe ndie uliyekuwa na mamlaka ya ufunguo kwahiyo wewe ndiye utakayekuwa mshukukiwa mkuu, utalala jela hadi hapo huyo mtu aliyeinga kwenye ofisi yangu na kuchukua vitu atakapopatikana..,kama sio wewe uliyefanya hivyo’nikasema.
‘Bosi, mimi sijui lolote, na kama polisi watanikamata, watakuwa wakinionea bure, maana sijui, na sijawahi kumruhusu mtu kuingia ofisini kwako..nakuomba bosi, unisaidie, nasema ukweli sijawahi hata siku moja kufanya hayo .......’akasema kwa uchungu, huku akipiga magoti, kitu nisichokipenda mtu kunifanyia hivyo, mimi ikabidi nimwamini tu, ila nikamwambia kuwa nifanya uchunguzi kama nitagundua kuwa anafahamu sitakuwa na msamaha na yeye.
Akilini mwangu nilijiuliza maswali mengi ni nani huyo angeliweza kuingia ofisini kwangu na kujua wapi nimeweka vitu vyangu vya siri, na kuweka kila kitu, kama kilivyokuwa na aliingia muda gani maana kama aliingia kwa uficho, basi itakuwa ni usiku , na kama ni usiku, walinzi walikuwa wapi. Hapo nikaona niwahoji walinzi.
Niliwaendea walinzi na kuwahoji, na wote walikana kabisa kuwa hakuna mtu angeweza kuingia usiku bila ya wao kumuona,wakasema kama ni mtu kuingia huko ofisi, basi itakuwa imefanyika hivyo mchana sio usiku....nikajikuta nikikosa ushahidi wa kuwabana hawa walinzi, lakini nilihisi kwa vyovyote vile ni lazima kuna mtu wa ndani anayehusika,hakuna mtu angeliweza kuingia hadi ofisini kwangu, kama sio mtu anayenifahamu, na kufahamu taratibu zangu.
Sikutaka kuwahoji wale wote ninaowahisi, kama katibu muhutasi wangu, ambaye sizani kama angelifanya hivyo,...niliona hilo swala niende nalo kimiya kimiya, na ikibidi nitatafuta mpelelezi wa kujitegemea.
Nilimpigia jamaa yangu wa mambo ya komputa, nikamuomba aniwekee vifaa vya kunasa matukioa ili kama huyo mtu ataingia tena aweze kuonekana, japokuwa nilikuwa na uhakika kuwa huyo mtu hakuwa na sababu ya kuingia tena kwani walichokitaka wamekipaa, sasa ataingia ofisi kwangu kufanya nini....
Hapo ndio nikamkumbuka rafiki yangu , msomi, aliyerejea kutoka nje, huyu ndiye alikuwa akinisaidia sana kwenye mambo kama haya, alikuwa hodari wa kufuatilia jambo hadi kulitatua, kiukweli ni mtaalamu, lakini kwa hili, siwezi kumtumia yeye tena.
Basi hapo hapo nikaingiwa na hamasa ya kuongea naye, nikapiga simu, ikawa haipatikani, nikampigia docta, na docta akanipatia namba yake mpya, kumbe ile ya zamani haitumii tena
Nilipopiga hiyo namba mpya mara moja akapokea simu, na sikutaka kumuuliza maswali mengi kwenye simu, nikamwambia
‘Nilikuwa na maongezi na wewe, tunaweza kukutana wapi?’ nikamuuliza.
‘Hata mimi nimekuwa nikikutafuta sana, ...kuna mambo nilitaka kukuweka wazi, kuhusu ile kazi uliyonipa kabla sijaenda kusoma,...na nimejitahidi ili tuonane, lakini imekuwa vigumu kukupata, ....’akasema.
‘Kwanini ishindikane, kwangu hukufahamu ofisini kwangu au nyumbani kwangu…?’ nikamuuliza.
‘Nilifanya hivyo, lakini ni kama vile imepangwa tusionane, maana nilifika kwako kwa mara ya kwanza nikaambiwa haupo, mara ya pili nikaambiwa umekwenda hospitalini niliwafuata huko, na bahati mbaya nilipofika nikaambiwa umetoka muda huo huo,…’akasema
‘Ok, kwahiyo, tukutane wapi…?’ nikamuuliza.
‘Kwa hivi sasa nipo uwanja wa ndege kwa jamaa yangu, maana natarajia kuondoka leo usiku, nikaona nije kulala huku kwake, ili iwe rahisi kuwahi kuondoka , ninaondoka leo usiku, na ndege ya usiku kurudi masomoni...’akasema na kuniacha hoi.
‘Ina maana ulikuja mara moja tu, ,..?’ nikauliza.
‘Ndio nilikuja mara moja, kwa dharura,....’akasema.
‘Dharura gani?’ nikauliza.
‘Kuna mkataba nilihitajika kuja kuweka sahihi yangu, ni muhimu sana kwa ajili yangu na mtoto na mambo mengine yalikuja kujitokeza hata sikuwa nimepangilia hivyo, lakini tumeyamaliza salama..’akasema
‘Huo mkataba, ni mkataba gani huo, mpaka urudi kwanini usingelianiambia mimi nikaukamilisha, unajua mimi niye mdhamini wako kwenye masomo huko Ulaya?’ nikauliza nikihisi kichwa kikizunguka.
‘Ni mambo yangu binafsi, siwezi kukuambia..na kutokana na vikwazo mbali mbali nimeondoa udhamini wako, nimemuweka mtu mwingine, nimeona nisiendelee kukutia gharama wakati wewe upo kwenye matatizo, na awali nilipata vistisho vingi, nikajua ni wewe, kumbe sio wewe...’akasema.
‘Unasema nini, na kwanini hujaniambia hilo…?’ nikauliza kwa ukali.
‘Samahani, kiukweli nikiwa huko nilijaribu sana kuwasiliana na wewe lakini haikuwa rahis, na hata nilipofika, imekuwa ni hivyo, kila ninavyopanga tuonane, sikupati, nikifika nyumbani, umetoka..na nilikuwa na mambo mengi ya kufuatilia, kwahiyo nikashindwa kujigawa, si unajua tena….’akasema
‘Na mtoto wako yupo wapi?’ nikamuuliza.
‘Natarajia kuletewa leo......’akasema
‘Sijakuelewa, kwanini unasema unatarajia kuletewa leo, kwani alikuwa wapi?’ nikamuuliza.
‘Kuna mambo mengine siwezi kukuambia, ni ..aah, unajua kuna watu wananichezea akili yangu, na imebidi nifanye wanavyotaka wao, kwa ajili ya usalama wa mtoto wangu, sijui walijuaje kuwa nimerudi kwa dharura, na wakatumia mwanya huo kunifanyia waliyonifanyia,….’akasema
‘Walikufanyia nini…?’ nikauliza
‘Waliniibia mtoto,…’akasema
‘Walikuibia mtoto kwa vipi,na kwanini…?’ nikauliza
‘Ndio maana nasema, sitak kukuambia haya, yatakuchanganya bure, ngoja nimalizane nao, nione hatima yake ni nini, lakini bado sijakubali, muhimu kwa sasa ni usalama wa mtoto wangu…’akasema
‘Kwa hapo ni lazima unielezee, kwanini, …unajua nasita kwenda polisi kwasababu yako wewe na mume wangu..’nikasema
‘Polisi kwa kosa gani..?’ akauliza
‘Niambie kwanza ni nao hao walimuiba mtoto na kwa minajili gani, na kwanini hujaenda polisi..?’ nikauliza
‘Kiukweli mpaka sasa sijaelewa..ila leo ndio wananirejeshea mtoto wangu baada ya kufanya hayo waliyoyataka wao, na sikuweza kwenda polisi kwa usalama wa mtoto wangu ila baada ya hapa, nitajua la kufanya…’akasema
‘Wao walitaka nini kwako..?’ nikamuuliza
‘Siwezi kukuambia mpaka nimpate mtoto wangu, nielewe hivyo tu, kwani hata sasa wananifuatilia kuhakikisha sifanyi kitu kinyume na makubaliano yetu....’akasema
‘Hivi mbona siku hizi unanichanganya, na hata hilo la hatari hivyo hutaki kuniambia, kwahiyo mtoto wako yupo wapi…?’ nikamuuliza
‘Wanasema yupo salama watanikabidhi leo,…’akasema
‘Unajua wewe..ra-rafiki yangu, ..ooh, hata kukuita rafiki tena nasikia vibaya, maana hilo neno rafiki nahsi kwako halina ukweli tena,…hii sasa naona ni hadithi ya kutunga sikuamini tena, hebu niambie kuna nini kinachoendelea kati yako wewe na mume wangu..?’ nikamuuliza
‘Mimi na mume wako, ..una maana gani, …hapo mimi sijakuelewa…’akasema
‘Usinichezee akili yangu….upo uwanja wa ndege sehemu gani, ni kule kule kwa shangazi yako…?’ nikauliza
‘Ndio ni kule kule…ina maana unakuja huku..?’ akauliza
‘Sasa ulitaka nifanye nini….ila kuna foleni sana…nikiona vipi nitarudi zangu…’nikasema
‘Mhh..tafadhali usije kuniharibia, nikamkosa mtoto wangu…’akasema
‘Unajua ulipoamuakia wewe ndio mimi nilikuwa nalala siku nyingi…najua kila kitu kwa sasa, mchezo mliocheza wewe na mume wangu…’nikasema
‘Mchezo gani ?…tafadhali usinichanganye, mimi hapa nipo na mashaka na mtoto wangu, wewe ni mzazi hebu jiweke kwenye nafasi yangu uhisi ungelijisikiaje kama tukio kama hili lingekukuta wewe.., yaani hapa mpaka nimpate mtoto wangu ndio nitakuwa na amani…’akasema
‘Mtoto wako aliibiwa wapi..?’ nikauliza
‘Nilipofika tu pale nilipofikia, wakati nipo bafuni naoga, niliporudi chumbani kwangu nikakuta mtoto hayupo, nilichanganyikiwa, maana kwa muda huo nilikuwa peke yangu na mwenyeji wangu alikuwa hayupo…lakini kabla sijafanya kitu nikapigiwa simu, kuwa kama namtaka mtoto wangu hai basi nifanye wanavyotaka wao, nikawaulize nifanye nini......’akatulia.
‘Ehe…’nikasema
‘Kuna mambo mengi walitaka niwafanyie, sitaweza kukuambia yote kwa sasa, ila moja wapo ikawa kuweka sahihi kwenye karatsi walizoniletea ilikuwa mfano wa mikataba na sikutakiwa kusoma ndani ...’akasema.
‘Mkataba gani huo, na una nini ndani yake, utaweka sahihi tu bila kujua kilichoandikwa…?’ nikamuuliza.
‘Sikupewa nafsi ya kuusoma huo mkataba wote…, kwani ulikuwa na mambo mengi sana, alichoniambia, ni kuwa hayo yanafanyika kwa ajili ya maisha ya baadae ya huyo mtoto..’akasema
‘Kwa maana hiyo huyo, kama walifanya hivyo kwa ajili ya mtoto, ina maana huyo aliyefany ahivyo ni baba wa huyo mtoto au..?’nikauliza
‘Mimi sijui, mtoto wangu hana baba, ..’akasema
‘Hana baba ulizaa na mti..’nikasema kwa hasira.
‘Nikuambie kitu nikiwa huko collage…, kuna watu walikuwa wakinifuatilia, na nikaja kugundua kuwa huyo mtu anadai mimi nimezaa naye..anadai hivyo, na mimi najaribu kulificha hilo, keshagundua kuwa huyo ni mtoto wake, anavyosema yeye…’akasema
‘Lakini wewe siunafahamu umezaa na nani, au sio…au wewe hukui, kwani wewe ulitembea na wanaume wangapi..?’ nikamuuliza
‘Kuna mambo mengi ni siri yangu, lakini baada ya yale maongezi yangu ya mimi na wewe ..unakumbuka , ukanishauri kuwa nikaze na mwanaume yoyote, ilimradi nimpate mtoto, kiukweli,…sikutembea na mwanaume mmoja, hilo nilikuficha , nilitembea na zaidi ya mwanaume mmoja…’akasema
‘Malaya mkubwa wewe…’nikajikuta nimesema hivyo
‘Ahsante…’akasema hivyo
'Hivi ni wewe yule rafiki yangu ninayekufahamu kweli…’nikasema
‘Nisamehe tu, kiukweli…mambo ni mengi, mitihani ni mingi imenikuta,…sijui niliingiwa na nini… ila kwa hili nimejifunza sana, kuwa kuanzia sasa nisimame kwa miguu yangu mwenyewe maana kila kitu kina gharama yake…ipo siku nitakuhadithia kila kitu, ila kwa leo, niache tu, maana sina amani hapa nilipo…’akasema
‘Je huyo mtu aliyekufanyia hivyo sio mume wangu…?’ nikamuuliza
‘Kunifanyia nini?..kumchukua mtoto?, hapana, sio mume wako, ..mume wako si mgonjwa, ..si anaumwa jamani, siwezi kumsingizia, kwasababu hata mimi niliwazia hivyo awali kwa haraka.., ndio maana nilikwenda hadi huko hospitalini nikiwa namshuku mumeo, lakini sio yeye, …’akasema
‘Kwanini ulimshuku mume wangu si kwa vile ulitembea naye, au…?’ nikamuuliza
‘Mimi sijatembea naye….kwanini nitembee naye….hilo usimsingizie mume wako, mtakosana naye bura…’akasema
‘Ulipofika hospitalini, uliongea na mume wangu..?’ nikamuuliza
‘Ndio niliongea naye, lakini hakuwa vizuri,…naona kama ana matatizo, ..hana amani, sikutaka kumchanganya zaidi, nikamdanganya kuwa mtoto nimemuacha nyumbani…’akasema
‘Kwani alikuuliza kuhusu mtoto..?’ nikauliza
‘Ndio, ilikuwa cha kwanza, alifurahi sana kuniona, unajua shemeji ananijali sana…’akasema
‘Ni kwa vile mume zaa naye au sio..?’ nikauliza
‘Wewe…unasema nini bo-si, …ndio unanifikiria mimi hivyo rafiki yangu, ..hapo umevuka mipaka, na ulikirudia kauli kama hizi mimi nitakata simu samahani…’akasema
‘Nataka ukweli kutoka kwako,….je umewahi kutembea na mume wangu…?’ nikamuuliza kwa sauti ya kibosi, kuwa sitaki utani
‘Samahani, nasikia watu wanakuja…’akasema, lakin hakukata simu
Nikasikia watu wakiongea na huyo rafiki yangu alikuwa hajakata simu, labda ni ili nisikie wanachoongea na hao watu.. .
Nikasikia, wakiongea lakini maneno siyanakili vyema masikioni, baadae nikasikia kama mtu anasema
‘Mtoto wangu yupo wapi…’ilikuwa ni sauti ya rafiki yangu huyo.
‘Mtoto yupo tumekuja naye..’sauti ya kiume ikasema
‘Nipeni sasa mtoto wangu, nimefanya kila mlichotaka, …mnataka nini tena..’akalalamika rafiki
‘Kuna kitu bado, kuna hizi nyaraka tumeambiwa uweke sahihi yako…’wakasema
'Mimi sina ugumu wa kuweka sahihi, lakini kwanza nimuone mtoto wangu…’akasema rafiki yangu,
‘Mtoto wako huyu hapa…’sauti ikasema na mara mtoto akaanza kulia, na rafiki akawa anaomba amchukue lakini wao wakasema sahihi kwanza
‘Huwezu kumchukua mpaka uweke sahihihi hapa, unasikia…’akaambiwa
Baadaye kukawa na ukimia,
‘Haya nipeni mtoto wangu…nimeshaweka hiyo sahihi,…na, hapa pia sawa, mii sijui inahusu nini, ila…nawaonya hili mtakuja kulijutia..’akasema rafiki yangu, na mara kukawa na kilo cha mtoto, na baadae hao watu wakasema
‘Sasa ulikuwa unaleta ubishi wa nini, haya yote ni kwa masilahi ya mtoto wako, bosi wetu kafanya hivyo, kwa vile anataka mtoto atabulike ni wake kisheria, …maana ni damu yake..keshathibitisha hilo…na kafurahi kweli hasa kwa vile ni mtoto wa kiume ‘akasema.
‘Si akazae na mke wake…’sauti rafiki yake ikasema.
‘Hayo mengine.. muhimu tumemalizana…’sauti ikasema
‘Sawa tumemalizana, naomba muondoke hapa…’akasema rafiki yangu
‘Sawa tunakutakia safari njema ila ukumbuke kuwasiliana na baba wa mtoto wako,ila kakutahadharisha, ukianza mambo ya sijui polis, utajitaharibia kila kitu..na hii iwe ni siri yako umeelewa shauri lako,,…’sauti zikasema na rafiki yangu hakujibu kitu.
Baada ya muda simu ikakatika, na mimi nikaamua kumpigia simu huyo rafiki yangu, kwanza hakupokea, baadae yeye ndio akapiga simu.
‘Haya niambie kinachoendelea…?’ nikauliza
‘Wamemleta mtoto wangu, yupo salama…’akasema
‘Kuna nini kinachoendelea, naona kama ni mchezo wa kuigiza, unataka nini ..wewe na huyo mwenzako..?’ nikauliza
‘Mwenzangu yupi….jamani, naomba uniulize mambo yenye maana hapa akili yangu haipo sawa , na nipo kwenye maandalizi, kuna mambo yangu mengi yameshindikana kwa sababu ya hawa watu, kwahiyo angalau huu muda mchache niache niyamalizie, yatakayowezekana, tafadhali…’akasema
**********
Moyoni nilihisi huyu rafiki yangu ananidanganya kitu, huenda hayo yote aliyonieleza ni hadithi ya kutunga, lakini …yawezekana ikawa ni kweli pia, labda rafiki yangu yupo matatani, na mimi ndiye mtu ninayeweza kumsaidia, nikataka nipige simu kwa watu wangu ili waweze kulifuatilia hilo jambo, na wakati nawaza hilo mara simu yangu ikaita,...nilipoangalia ni nani anayenipigia nikagundua kuwa ni docta rafiki wa mume wangu;
'Upo wapi wewe, nakutafuta sana.....'akasema.
'Unanitafutia nini..mbona simu yangu ipo hewani wakati wote?' nikamuuliza kwa sauti ya kama mtu anayekerekwa, kiukweli sikuwa na amani na kila anayenipigia naona kama anazidi kunichanganya tu
'Kuna mambo muhimu sana, nataka kuongea na wewe....'akasema kwa sauti ya kikazi zaidi
‘Mambo gani?’ nikamuuliza kwa mkato, kwani kwa sauti hiyo inaonyesha kuna jambo.
‘Kuhusu huyo wakili wa mume wako.....’akasema
‘Wakili wa mume wangu, huyo tapeli, ana nini huyo wakili..hebu ongea moja kwa moja..kuna tatizo, au kuna jambo?’ nikauliza
‘Huyu mtu ni hatari sana, kama tusipofanya haraka, utakuja kujijutia..’akasema
‘Ulishaniambia hilo, au kuna jingine..’nikasema
‘Ndio kuna jingine mimi…, nimegundua mambo mengi sana juu yake, na sipendi niyaongelee hapa kwenye simu, tuonane sehemu tuongee tuone tutafanya nini, ni muhimu sana, kabla hujachelewa...’akasema na sauti yake ilinitia mashaka, inaonyesha msisitizo ...’nikasema;
‘Nitakuja nyumbani kwako....’nikasema.
‘Hapana, usije nyumbani kwangu, … njoo ofisini kwangu....’akasema
‘Sawa vyovyote utakavyo, nipo njiani, nakuja....’nikasema na kugeuza gari na kurudi nilipotoka, foleni ya kwenda uwanja wa ndege ilikua haiende kabisa, hapo sikujali tena mambo ya rafiki yangu.
NB: Sehemu hii iliishia hivyo
WAZO LA HEKIMA:Usalama wa majumbani kwetu, usalama wa watoto wetu, au usalama wa maofisini, ni muhimu sana, na ni vyema, vitu kama ufunguo, ulinzi, na usafi, vikapewa kwa watu wanaoaminika, kwa mkataba maalumu. Tatizo kubwa lililopo, ni kuwa watu hawo hawalipwi vizuri, na kutokana na hali ngumu za kimaisha, ni rahisi kwao kushawishiwa na kurubuniwa kwa pesa ndogo tu. Cha muhimu ni kuwajali sana hao watu, na kuwatimizia mahitaji yao muhimu, ili waione hiyo kazi kama yao.
'Kuna mambo muhimu sana, nataka kuongea na wewe....'
‘Kuhusu huyo wakili wa mume wako.....’
‘Huyu mtu ni hatari sana, kama tusipofanya haraka, utakuja kujijutia..’
‘Ndio kuna jingine mimi…, nimegundua mambo mengi sana juu yake, na sipendi niyaongelee hapa kwenye simu, tuonane sehemu tuongee tuone tutafanya nini, ni muhimu sana, kabla hujachelewa...’
Kisa kinaendelea....
************
Ilikuwa siku ya aina yake, maana foleni likuwa kila mahali, sikuweza kufika uwanja wa ndege, na sasa nimeamua kurudi ili nionane na huyo rafiki wa mume wangu, na foleni ikanifanya nichelewe hadi usiku ukaingia.
Lakini kwasababu ya kusikia ni kitu gani alichokigundua huyo docta, ikabidi nipitie kazini kwake, kwani bado alikuwa ofisini..nikafika kwenye hospitali yake, nikasimamisha gari langu kwenye eneo la maegesho ya mgari.
Hiyo ilikuwa hospitali yake ambayo anaifanyia kazi baada ya muda wa kazi, kuanzia saa kumi na mbili mpaka saa sita usiku…kwahiyo muda wote huo utakuwata wagonjwa wapo.
Niliingia ndani hadi mapokezi, niliangalia mlango wa kuingia kwenye ofisi ya huyo docta, nikawaona wapo wagonjwa wawili tu wanasubiria kuonana naye. Nikaona nisubiria waishe hao wagonjwa, lakini walipoisha hao wakaongezeka wengine…
Nilitaka nimpigie simu kumuelezea kuwa nimeshafika, lakini nikaona nimpe muda, maana nitawadhulumu hao watu wenye shida ya kutibiwa, wao ni waginjwa wamefika kutibiwa, na mimi siumwi, japokuwa nina mambo muhimu na huyo docta, ....
Na niwakati natafakari hayo, mara mlango wa ile ofisi yake ukafunguliwa, na yeye akatoka, na kuangalia sehemu mapokezi, ambapo, nilikuwa bado nimesimama, inaonyesha alikuwa keshajua kuwa nimeshafika. Akanionyeshea ishara ya tano, nikafahamu kuwa ananiambia nimpe dakika tano, na mimi nikatikisa kichwa kumkubalia,...
Nikasogea sehemu ya kupumzikia wageni, kuna masofa, nikachagua sehemu ya kukaa, ili niwe naone kule kwenye ofisi ya huyo mwenyeji wangu,nikawa naangalia runinga. Na baada ya dakika tano, nilimuona akitoka tena, na safari hii, alionekana akimuita mtu, nahisi alikuwa akimuita msaidizi wake, na huyo aliyeitwa alipofika,wakaongea naye kidogo.
Walipomaliza kuongea, nikamuona akija sehemu hiyo niliyokuwa nimekaa, na aliponikaribia, akanionyeshea ishara kwa mkono kuwa twende sehemu ambayo alihitajia tukaongee, ni kwenye chumba kingine.
‘Kwanini usingemalizana na mgonjwa wako kwanza...naona kuna watu wawili tu pale wamebakia, ila kila wakiisha wawili wanakuja wengine, pole na majukumu, hivi unapumzika saa ngapi..?’ nikamuuliza.
‘Wale sio wagonjwa, wale ni vijana wangu wamekuja kunipa taarifa mbalimbali, hawana haraka, wanaweza kunisubiria tu..’akasema,
‘Vijana wako, wewe unafanya kazi ngapi…?’ nikamuuliza
‘Hahaha, ushaanza kunichimba, ..unakumbuka nilikuambia wakati nasoma nilipendelea sana kuwa mpelelezi, lakini udakitari ukazidi nguvu ile ndoto yangu y utotoni, kwahiyo chini kwa chini nimekuwa nikijifunza mwenyewe mambo ya upelelezi kupitia mitandao kwa kujifurahisha tu…’akasema akitabasamu
‘Ili uwachunguze watu, na ndoa zao au…’nikasema
‘Ikibidi kwa watu ninaowajali kama nyie..kama wewe…’akasema akinipiga piga mgongoni, nikawa nauzuia mkono wake.
Tukafika kwenye hicho chumba, na tulipoingia, akasimama kidogo, kama vile ananipisha, lakini, nikamuona akinisogelea, kama anataka kunikumbatia, na mimi nikamsukuma;
‘Jiheshimu, kumbuka nafasi yako na yangu pia....’nikasema.
‘Samahani, unajua tena, kuna mda nashindwa kujizuia,…hahaha, nisamehe tu mwenzako, nisije kuongeza madhara, maana siku hizi tuwe makini sana…hata hivyo nilitaka kukusalimia, ....kwani kusalimia kwa kukumbatiana kuna nia mbaya,....usiwe mshamba bwana....’akasema.
‘Sawa acha niwe mshamba, lakini nafahami ni kitu gani ninachokifanya, naheshimu ndoa yangu na wewe fanya hivyo hivyo...’nikasema.
‘Ni kweli samahani….’akasema huku sasa akiwa mbali na mimi.
Tukaingia ndani, akanisogeza kiti, ili mimi nikae, na nilipokaa, yeye akatembea hadi kwenye kiti kikubwa, ilikuwa ofisi yake, maalumu, kulikuwa na kila kitu muhimu cha ofisi, alipokaa akaniangalia moja kwa moja usoni, hapo tulitengenishwa na meza. Mimi sikujali huku kuniangalia kwake, nikatulia kama vile mgonjwa anavyosubiria kuhudumiwa na dakitari.
Nilisubiri kidogo, kumuachia nafasi hiyo ya kuniangalia, maana sijui alikuwa na maana gani, au ndio hulka hizo za wanaume…kwani alivyokuwa akifanya ni kama mtu anayemwangalia mpenzi wake, na hali kama hiyo sikuipenda, lakini kwa vile nilishamfahamu tabia yake, sikujali, ...nikatulia kimiya, na aliponiona nipo kimiya sicheki nimeangalia mbele, akasema;
‘Nimekuita hapa sio kama mgonjwa, na sio kama nimekuitia hapa kwa maswala ya masihara, ya uchumba wetu wa zilipendwa, ila siwezi kuficha nakupenda sana, japokuwa siwezi kufanya lolote kwa sasa….hahaha, usijali,…hayo tuyaache mimi nimekuita hapa kwa jambo muhimu sana zaidi ya hilo..’akasema.
‘Mhh,...niambie, najua usingelipoteza muda wako kuniita..’ nikasema;
‘Kutokana na vyanzo vyangu vya habari, unafahamu ukiwa katika hali kama hii yetu ya kujiajiri, hasa ukawa na miradi yenye wateja wengi , na maadui wengi kibiashara, ni lazima pia uwe na vyanzo vyako vya kukupatia taarifa muhimu, naomba unielewe hivyo tu, mimi siwezi kukuficha kuwa nasubiria tu wateja, wakati mwingine inabidi uhangaike kama hivyo, kujua wenzako wanavyofanya..’akasema
‘Sawa nakuelewa, kila mtu anafanya hivyo, kwa masilahi ya biashara yake…’nikasema
‘Sawa kabisa, tuachane na mimi,..nataka kuongelea kuhusu wewe…’akasema
‘Nimefanya nini tena…’nikasema
‘Ni hivi, usione kama ni kwanini, kiukweli, sio siri nimekuwa nikifuatilia ndoa yenu hatua kwa hatua, sio kwa nia mbaya, bali kwa ajili ya kukulinda wewe, hujui tu..hili nimeshakuambia mara nyingi, …’akasema
‘Pole sana…’nikasema
‘Sasa… siku ile nilipoona mume wako yupo na huyo wakili, nikaingiwa na mashaka, sio kwa vile sikuamini wewe…lakini huyu mtu,…nimeshasikia tetesi zake na sikutarajia kuwa atakuja kuingia kwenye anga zangu….’akasema
‘Ndio hajaingilia biashara zangu au maisha yangu, lakini yule anayekugusa wewe kanigusa mimi..sisemi kinafiki, ila kutoka moyoni, na wazazi wako wanalifahamu hilo, kuwa mimi ndiye mlinzi wako,..tuliache hilo hivyo.
Mimi huyo mtu, nimesikia sifa zake nyingi,..mbaya na nzuri, mimi awali sikulichukulia hilo maanani, kwasababu sikuwa na sababu yoyote na mtu huyo...kabisa kabisa….’akasema.
‘Sawa ..naogopa kukatali, lakini naomba yasiwe ya kujirudia rudia endelea...’nikasema.
‘Nafahamu una kazi nyingi sana, nafahamu angelikuwepo yule rafiki yako yupo hili ungelimtumia yeye, na mimi nisngelikuwa na nafasi hii tena, kwa vile hayupo basi mimi nikaona nikusaidie kwa hili, na kwa vile rafiki sasa kakugeuka, hilo utakuja kuligundua mwenyewe baadae , sio sasa, sasa hivi nataka kukuweka wazi ni kwanini nimekuwa nikikufuatilia hivyo…’akasema na mimi hapo sikusema kitu.
‘Pole sana na foleni, ya kutoka uwanja wa ndege, natumai ulikwenda kuonana na rafiki yako, na nashukuru hukuweza kuonana naye , vinginevyo mtego uliotayarishwa, ungekunasa, na sijui ni nini kingelitokea baada ya hapo..’akasema.
‘Umefahamu vipi kuwa nilikwenda huko kumfuatilia huyo rafiki yangu, mbona unapenda kunifuatilia sana nyendo zangu, unanitafutia nini wewe ?’ nikamuuliza.
‘Nimeshakuamba kuwa mimi nina vyanzo vyangu vya kunipatia taarifa kama nina umuhimu na jambo fulani, na kufuatilia nyendo zako ni kwa ajili ya kuhakikishia usalama wako, na nitahakikisha nafanya hivyo,utake usitake, kwani niliahidi mbele ya wazazi wako, na kwako pia, kuwa nitafanya hivyo, ...’akasema
‘Yatakushinda, wewe niambie ulichoniitia masaa yamekwenda sana , unajua nimechelewa kufika nyumbani, kama mume wangu angelikuwepo nyumbani, ningekuwa na kesi ya kujibu…lakini hata kama hayupo nyumbani isiwe ndio ababu ya kuvunja miiko ya ndoa, sitakiwi nifanye mambo ya kunivunjia heshima yangu, unanielewa hapo…’nikasema huku nikiangalia saa yangu.
‘Ni kweli kabisa kwa hilo mimi nakuvulia kofia, …sina shaka na wewe.., hata mimi sijafanya hivi kwa nia mbaya, hili ni muhimu sana..’akasema na kukaa vyema, halafu akaniangalia tena machoni, na kusema;
‘Haya nitakayokuambia sasa hivi, ni muhimu kuliko hayo unayoyafuatulia wewe…nakuomba unielewe hivyo’akasema
‘Sawa , mima nakupa robo saa, nakusikiliza, baada y ahapo naondoka zangu…’nikasema
‘Kuna mambo bado hayajathibitishwa, ila ya kikamilika, nitakuambia ila kwasasa nataka kukuelezea jambo kubwa tuliloligundua....kwa kukutahadharisha, na kukuomba usifanye hayo uliyoyakusudia kuyafanya hadi hapo utakapoambiwa, kwa manufaa yako na ya watu wengine wanaokujali...’akasema, na mimi nikatulia kusikiliza.
Akaangalia saa yake halafu akasema
‘Robo saa sio, inatosha kabisa baada ya hapo utakuwa huru kuondoka, naahidi hivyo…’akasema akiandika kwenye karatasi yake.
‘Mhh..haya, yaseme…’nikasema nikiona kama ananipotezea muda, kiukweli pale nilipo bado nilikuwa namuwazia huyo rafiki yangu je kumeendelea nini huko, isije ikawa yupo matatani..sikufikiria ubaya wake zaidi..niliwazia ubinadamu, hasa mtoto wake.
‘Mpendwa, sio kwamba nakulaumu, na mimi kama walivyo wazazi wako, tulishakuambia kuhusu mume wako, kwani tabia za watu za asili, kizalia, huwa hazibadiliki sana, labda mtu mwenyewe aamue kiukweli kufanya hivyo, ila akipata mwanya, kurudia asili yake haichelewi, mtu habadili kwa hivyo kama mwenyewe hatataka kujibadili...’akasema.
Mimi nikakaa kimia, najua huyu ni mtu wa wazazi wangu, nilishamzoea,…
‘Na nafahamu hali uliyo nayo kwa sasa, kwani mume unampenda sana hata pamoja na hayo yaliyotokea...lakini huko kunapoelekea, itabidi ufikirie hilo mara mbili, sio kwamba nakushauri uachane naye, hapana,..hautakiwi kufanya hivyo, …hata wazazi wako hwataki ufanye hivyo…’akatulia kidogo
‘Ni kweli wazazi wako wamelifikiria sana hilo ya kuwa, mna watoto, nakadhalika… sio vyema mkaachana, lakini sasa mtaishije kwa hali kama hiyo, hilo ni lenu wawili,..muhimu uishi naye ukiwa na tahadhari tofauti na awali, sasa kwa hayo waliyopanga, itakuwaje, ni kazi ambayo inafanyiwa kazi,..
‘Kwangu mimi kwa hivi sasa nataka kukuelezea yale tuliyoyagundua ambayo, yatakushtua,..maana hata mimi sikuamini, lakini ukweli ni ukweli tu, na ukweli huo hatutaweza kuupata zaidi , ikiwa wewe utachukulia jazba, nafahamu itafikia sehemu utasema basi liwalo na liwe, hapana, kwa vita hivi, bado tunahitajia uvumiliv wako....’akasema.
‘Kwanini unazunguka, unanipotezea muda, na kuniweka roho juu, niambie ulichoniitia, nina mambo mengi ya kufanya…’ nikasema kwa hasira.
‘Huo ni utangulizi mpendwa, nilazima nikuambie hayo kama ilivyotakiwa nikuambie.....’akasema
‘Ulivyoambiwa na nani, na wazazi wangu au…?’ nikauliza
‘Kwanza ni kuhusu huyo wakili wa mume wako, anayejiita wakili wa kujitegemea, ni kweli kitaaluma ni wakili..na sio kwamba hana fani hiyo, anayo na kaisomea kweli, vyeti anavyo na kazi pia anaifahamu, akisimama mahakamani sio mchezo, ila yeye n ndumilakuwili,…na tabia isiyopendezahula na tabia yake ndivyo vinamkosoa...’akasema
Nilitaka kumuambia hayo nayafahamu lakini nikaa kimia ili nimsikilize zaidi, huenda kuna kitu cha zaidi sikifahamu
‘Sasa huyo anataka kuwatumia marafiki zako,…bila ya wao kujua, kuhakikisha anakamilisha lengo lake , akiwemo huyo mume wako…huyu jamaa ni mjanja kweli kweli ..na hutaamini keshafanikiwa…’akasema
‘Marafiki zangu..!!’nikasema kwa mshangao.
‘Ndio…marafiki zako wameshatekwa kimawazo, na kwa jinsi ilivyofanyika, hawana ujanja, na kiukweli huenda hata wao hawafahamu ni kwanini, wameingizwa huko, ni ujanja wa hali ya juu,….na usione mengine yanatokea ukaona ni bahati mbaya, ni mpango wenye masihali fulani ya kisiasa…’akasema
‘Mhh..sasa ni siasa, awali ilikuwa ni maswal ya kindoa, mimi simjali mume wangu, ikaja …mume huenda kasalitio ndoa, sasa imekuwa ni mambo ya kisiasa, kweli mnahangaika sana, nikuambie kitu, hili hebu niechieni mwenyewe, nafahamu sana, kuwa wazazi wangu wananijali, lakini nimeshakuwa mtu mnzima, najua kujitetea, kwanini niendelee kuwatesa wazazi wangu, waacheni wapumzike, nitapambana kivyangu…’nikasema
‘Mtoto hakuwi mbele ya wazazi wake, ilimradi wapo hai, hata kama ni vikongwe, unasikia, msidharau wazazi wenu hata siku moja…pamoja na yote unayofanya, usifikirie kuwa utakuja kuwazidi wazazi wako, ….kumbuka wao wamepitia mengi, na utu uzima wao ni dawa..wao wana hekima ambayo hujaipata…mungu huwapa watu wazima maono ambayo wewe huwezi kuyafahamu…’akasema
‘Sikatai, hilo siwezi kupinga lakini pia wanahitajika kumpumzika, niwasaidie na mimi, nitawasaidia lini, eeh…’nikasema.
‘Haya ninayokuambia sio kwamba naongea tu,… ni kitu kilichofanyiwa uchunguzi na nina ushahidi wa kikao hicho kilichofanywa na maadui zenu…, ukitaka nitakupatia…ni hujuma zimepangwa kisayansi ya kisiasa…, na ni kweli zilianzia ndani ya familia yako, na sasa zimekwenda zaidi ya hapo, siasa imeshaingizwa..’akasema
‘Mimi sio mwanasiasa na sitarajii kuingia huko, sipendi siasa kabisa…’nikasema
‘Lakini baba yako ni mwanasiasa, kajiingiza huko pamoja na shughuli zake, je humjali…?’akasema kuniuliza
‘Hayo ni maisha yake, mimi sipo huko ndio maana nikajitenga naye, na nimekuwa mbali naye, na nilishamuambia, sitaki tuingiliane, ili nisije kumuharibia mambo yake…’nikamwambia docta
‘Sikiliza, kwenye uwanja wa siasa, kila kitu ni silaha kwa adui yako, …na wengi wanakimbilia kuangalia familia zinavyoishi hilo kwa upande mmoja japokuwa huku kwetu Afrika sio sana, lakini zaidi ni vitega uchumi, mali nak, je havina mkono wa pesa chafu, je hakuna ukikuwaji wa maadili, kwenye zabuni nk, rushwa na vitu kama hivyo…’akasema
‘Najitahidi sana kukwepa hayo…nikasema
‘Baba yako alijitahidi sana kuwasaidia, na alijitahidi sana kuona kuwa nyie mnaendesha biashara kimaadili, sasa huo msaada unafuatiliwa, ulitokaje, na je huko unapokwenda, umefanyia nini,…unaona mtego uliopo hapo, msaada unageuka kuwa mtihani…’akasema
‘Ni kweli , mimi sijavunja miiko ya biashara, nafuata sheria, kwahiyo baba hastahiki kuogopa kwa hilo, sijafanyia vibaya mtaji alionipa kwenye biashara zangu, kama kuna ubaya, niambieni…’nikasema
‘Je mume wako anafanya hivyo..anafuta sheria, analipa kodi, anafanya biashara halali kwenye zabuni na serikali, je, matumizi yake, je..hajafanya mambo yasiyo mema kwenye jamii, kimaadili..nyie wote mnamulikwa kihivyo..?’ akaniuliza
‘Mimi sijui…’nikasema
‘Wewe hujui lakini maadui wa siasa wanilijua hilo, hebu nikuulize kwa hivi sasa mume wako ikatokea tatizo kwake, wewe utaziba masikio yako kuwa hayakuhusu, angalia huo ugonjwa wake, umefanya nini, ulilala kitandani…chukulia kafanya madhambi, unafikiri jamii itasemaje, hasa maadui wa kimaisha, hasa katika Nyanja za kisiasa maana mabo yako ni ya kisiasa, kuongea, kutoa propaganda potofu, watasemaje hapo, je wanataja jina la baba yako au jina la baba wa mume wako…kisiasa…?’akauliza
‘Ndio maana nilimuambia baba, mimi anichie maisha yangu, sikutaka kabisa yeye ajiingize kwangu, mtaji wake uwe ni mkopo kwangu nikiurejesha ajitoa kabisa na mimi, wala asitambulikane, ..lakini hajataka kunisikia..’nikasema
‘Je uliwahi kurejesha huo mkopo, ..?’ akaniuliza
‘Nitaurejesha, mambo hayajakaa sawa..’nikasema
‘Mpaka muda huo, unafikiri mangapi yamefanyika …nakuambia haya kwa mawazo mapana,…, huyo jamaa , wakili wa mume wako, ndio jembe la mpinzani wa baba yako, unielewe hapo, yeye alipikwa akasomeshwa na mpinzani mkubwa wa baba yako kisiasa,..sasa natakiwa kulipa fadhila, ndio hayo anayafanya je anayafanya bure bure tu, kuwa anataka masilahi ya pesa tu, jiulize kwa makini, ..’akatulia
‘Mimi sijui…’nikasema
‘Kitu kikubwa watu walikuwa wakijiuliza bila kupata jibu ni kwanini huyu jamaa anajiamini hivyo, ni kwanini hakamatwi, na akifunguliwa mashitaka hapatikani na hatia, ni kwanini…n hebu sikia alivyokuwa akikujibu pale hospitalini ni kwanini alijiamini hivyo, jiulize hapo…’akasema
‘Na wewe ni jembe la baba yangu, au…?’ nikauliza
‘Usifanye utani, hili ni jambo nyeti sana, sivyo kama unavyofikiria wewe, achana na hulika yako kuwa labda nafanya haya kwa vile, …hapana hili ni jambo nyeti na ukicheza, utajiharibu wewe na familia yako yote, kuanzia kwa wazazi wako, na utakuja kujuta wakati umeshachelewa…’akasema
‘Kwa mume wangu ulisema hivyo hivyo, na huyo ni rafiki yako, sasa umemgeuka, sasa ni kwa wazazi wangu, ni nini, siasa au sio, lakini mimi zipo huko, na baba akipatwa na matatizo, wasinisingizie mimi, ..niakuambie kitu…’nikasema
‘Tunamuongelea huyo jamaa, tusipoteze muda, najua umenipa dakika ngapi, au umeziongeza ….sikiliza sasa…’akasema
‘Natumai huyu jamaa unamfahamu kwa juu juu tu, nitakuelezea sifa za huyu mtu, ambaye kitaaluma ni wakili wa kujitegemea, na polisi wamekuwa wakitafuta kila njia kumnasa, kutokana malalamiko ya watu wengi, waliowahi kufanyiwa utapeli na huyu mtu, akitumia mgongo wa taaluma yake hiyo, lakini kutokana na ujanja wake hajawahi kukamatwa.....’akasema.
‘Unaposema huyo jamaa una maana wakili Makabrasha...?’ nikauliza.
‘Nisingelipendelea kumtaja jina lake kihivyo, lakini ndio huyo,...mtu huyu ni rafiki wa mume wako toka utotoni, na tabia zao zinafanana, japokuwa mume wako alikuja kubadilika baada ya wewe kuolewa na yeye, huo ndio ukweli,....’akatulia kidogo.
‘Mume wako, alikuwa akishirikiana na huyu jamaa kabla, jamaa akitoka ulaya, rafiki yake mkubwa alikuwa mume wako…wakawa wanashikirikiana kwenye mambo mbalimbali, ya kutafuta maisha… kipindi hicho mume wako alikuwa akihangaika tu kazi yoyote anafanya, maisha yalikuwa magumu sana kwake, kwa hiyo tunaweza tusimlaumu moja kwa moja, japo sio sababu ya kufanya mabaya kwenye jamii..’akasema....
‘Mkaja kupendana,…na hatimaye kuvuruga uchumba wetu,…sio nakulaumu, ila nakuelezea hali ilivyoweza kubadilika, ni kweli ulimsaidia sana, na kweli kipindi hicho aliamua kubadilika kiukweli, lakini kunguru hafugiki.
‘Watu wanasema huenda, rafiki yake huyo wakili, ndiye aliyemshauri rafiki yake afanye kila awezavyo mpaka akuoe, ili baadae iwe ni chambo, au mlango wa kuingilia, lakini sio kweli…huyu jamaa alikupenda kiukweli, ila tamaa ndio iliyomuharibu,sio tamaa tu, bali hulka ya kuzaliwa, ilikuw na nguvu zaidi…’akasema
‘Una ushahidi gani..?’ nikamuuliza
‘Kila kitu kipo, mpaka nimeamua kukuita hapa nimeshahakikisha kila kitu kipo kiushahidi, maana mimi nakufahamu wewe ulivyo, lakini kwa leo nitakuelezea tu, ili kwanza nitimize wajibu wangu kama mimi na pili, niwakilishe ujumbe kutoka kwa wazazi wako, japokuwa hawajanituma nikuambie hivyo…’akasema
‘Endelea…’nikasema
‘Ulipoolewa na huyo jamaa, rafiki yake akawa anakusoma, anawasoma kufahamu madhaifi yenu,…kwanza alitaka kumweka sawa mume wako ili apitie kwake, kwa kujifanya anamjenga ili lolote likitokea asija kuadhirika..akajaribu akashindwa, …kwasababu ulishamweka sawa mume wako…;lakini jamaa alishajua kuwa kuna muda muafaka utafika, kunguru hafugiki, unanielewa hapo …’akatulia
Jamaa akaja kwa mgongo wa taaluma yake, akitaka awe wakili wenu, mume wako alimkubalia, lakini wewe ukaja kuvuruga, lakini hakukata tamaa, akawa anatafuta njia ya kuwaingilia,….. lakini kwanini afanye hivyo, jiulize ni kwanini, ni mali tu..,..au kuna nini cha kumfanya ahangaike hivyo…’akatulia
‘Mali ni nyenzo mojawapo, lakini sio sababu kubwa sana, hili hata polisi walikuwa hawajaligundua wao macho na masikio yao ni kwenye mali,..rejea niliyokuambia kuwa wakili huyu alipikwa na mwanasiasa adui, mpinzani wa baba yako…ukirejea huko ndio utanielewa vyema…’akasema
‘Je atawezaje kuingilia ngome iliyojengwa imara, kimaadili, kisomi, na mnajitahidi kila namna kuhakikisha kuwa hamna kashfa, …sasa nikuambie kitu baada ya kuona bado ni shida kuingilia ngoma ya baba yako zikapikwa kashfa…
‘Zikapikwa kashfa kwa vipi…?’ akauliza
‘Haya mambo ya dunia hii, yaone tu, usione nchi zinapigana ukafikiri ni wao tu propoganda potofu, kashfa, hujuma, jamii kuchonganishwa, bila wao kujua, wanakuja kukosana,…kashfa nyingine hutengezwa, na kwa ushahidi…, kashfa imeshaingia kwenye familia yenu, sasa ni ya kutengenezwa au ni kweli ilifanyika kiuzembe, ndio nilichokuitia hapa, ili ulifahamu hilo, kuwa sio jambo dogo kihivyo, limeshakwenda zaidi ya kifamilia, sasa chagua kuwasaidia wazazi wako, au ..…’akatulia hivyo hakumalizia, akaangalia saa
‘Kashfa gani unayozungumzia hapa, ni huyo mtoto wa rafiki yangu, si ndio hiyo, lakini nimegundua kitu...na nilikuwa nakifuatilia, huko uwanja wa ndege, ndio ukaniwahi, nina uhakika ningelilimaliza hilo, na utata wote ungeliisha…?’ nikauliza na kusema
'Hahaha, hujua kuwa unajipeleka kwenye mdomo wa ..kenge,..huo ni mtego ulitayarishwa, inajualikana ulitakiwa uende huko, ukajinase...najua nia yako ni kupata damu ya huyo mtoto ukapime DNA,lakini usingeliweza kumpata...kuna mchezo ulitakiwa ufanyike, lakini sasa...'akaangalia saa yake
‘Ahadi ni deni, dakika ulizonipa zimekwisha, unasemaje, tuendelee…’
WAZO LA LEO: Ukisikia taarifa yoyote ifanyie kazi kwanza, hata kama unaona kuwa ni taarifa yenye masilahi kwako, usiwe na papara nayo, inaweza ikawa nzuri kumbe ndani yake kuna ubaya, kuna mitego, walimwengu sio wema…, inaweza ikawa kama asali yenye sumu ndani yake, kumbuka kuwa sio kila taarifa ina lengo jema kwako... Ipokee taarifa, ichunguze ukweli wake, na angalia athari zake, je inaweza kupokeleka, vinginevyo, ipuuze, weka subira, mola yupo pamoja nawe, na muda utasema