Mkuki Kwa Nguruwe (Kisa Cha Kweli)

Mkuki Kwa Nguruwe (Kisa Cha Kweli)

SEHEMU YA 86



‘Bado mmoja ..’

Kiukweli ushahidi niliokuwa nao ulikuwa unatosha kabisa, kufanya lolote, lakini kuna baadhi ya mambo nilihitajika kuyafuatilia, ili kuhakiki, na sikutaka kutumia nguvu, sana, ni hekima ndogo tu....

Tuendelee na kisa chetu.

*********

Docta alisafiri kwenda kijijini kuonana na mke wake!

Wakati nipo nyumbani nikijiandaa kwenda kumtembelea mume wangu hospitalini, mara nikasikia kuwa nina mgeni, nilipouliza ni nani wakasema ni Inspekta wa polisi, nikajua kuwa sasa mambo yameanza kuvuja, sikutaka mambo haya yaharakishe sana kabla sijamalizana na uchunguzi wangu.

Ukisikia polisi kaja kwako hata kama huna kosa utakuwa na wasiwasi tu…

Nikatoka nje kwa kupitia mlango wa nyuma, hadi bustanini, nikaagiza huyo mgeni aletwe huko , kwani likuwa kakaribishwa chumba cha maongezi, sikutaka niongee naye ndani, nilitaka sehemu huru ambayo kila mtu anaweza kuona.

Mkuu huyo akaja huko bustanini, akiwa kashikilia mkoba wake, kuonyesha yupo kazini. Alikuwa mtu wa makamo, na hali yake kiafya ilionyesha sio haba, kitambi kidogo, japokuwa ukakamavu wa kiaskari bado ulikuwa kwenye damu, akasogea hadi pale nilipokuwa nimesimama, na mimi nikamsogelea na kunyosha mkono kusalimiana.

‘Samahani kwa ujio huu wa ghafla, unafahamu kazi zetu tena, pale unapopata taarifa unatakiwa uifuatilie kwa haraka , maana tuna kazi nyingi sana za kufanya,…kwa hili sikupenda kuwatuma vijana wangu, namuheshimu sana baba yako,...’akaaza kujieleza.

‘Nashukuru kwa hilo pia nashkuru kwa kunitembelea japokuwa nilikuwa na ratiba zangu nyingine kiukweli,..,kwani sasa hivi natakiwa kwenda kumuona mgonjwa...huko alipolazwa..’nikasema

‘Oh, kwani mume wako anaendeleaje?’ akauliza

‘Hajambo kidogo, unajua matatizo yake sio yale ya kusema kapona, anahitajia muda wa kuchunguzwa, itokee hiyo hali ndio unaweza kufanya jambo, lakini hajambo, sasa hivi yupo kwenye mazoezi tu ya kawaida...’nikasema

‘Kwahiyo kumbe tunaweza kumtembelea na kuongea naye?’ akauliza

‘Mhh, hayo anayeweza kuyajibu ni dakitari wake,…kwani kuna jambo mnahitaji kuongea naye,?’ nikamuuliza

‘Ni maswali ya kawaida tu....lakini kama bado hali yake haijawa sawa hakuna haraka sana, ....’akasema

‘Haya niambie ujio wako kwangu una makusudio gani na mimi, maana nyie watu hamji kwa mtu bila lengo maalumu, na mkionekana kwa mtu ujue kuna jambo...’nikasema.

‘Ni kweli, nimekuja kwa lengo maalum, lakini sio kwa ubaya,....’akasema na kutoa makabrasha yake, halafu akasema;

‘Katika uchunguzi wetu, tumegundua kuwa yule kijana mdogo wa mume wako alikuwepo siku ile Makabrasha alipouwawa, na alionekana akiranda randa eneo la lile jengo, na baadaye akaondoka na mtu siyefahamika, ..’akatulia

‘Sasa tulitaka kuongea naye, lakini hayupo, na watu wangu wamejaribu kumtafuta bila mafanikio, hata kazini kwake hawajui huyo mdogo wake mume wako kaenda wapi, je unafahamu huyu kijana wenu kaenda wapi, maana ni muhimu sana..?’ akaniuliza

‘Kwakweli hata mimi sijui kaenda wapi, na nilishamwambia kuwa asiondoke bila ya kuwasiliana na mimi…’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka.

‘Haiwezekani, ina maana hata nyie, hata …mke wake naye hayupo…sasa inatupa mashaka kidogo, ....Je hata mume wako hafahamu wapi kijana wenu alipokwenda...? ‘ akauliza

‘Hafahamu kabisa, maana jana nilipofika kumuona mgonjwa, yeye mwenyewe ndiye aliniulizia kama nimewahi kuonana na mdogo wake, kwani anaona ajabu siku mbili kupita bila mdogo wake kufika kumuona,.... sio kawaida yake..’akasema

‘Ina maana katoroka basi…, au kuna kitu kimemtokea, maana msije mkakaa kimiya kumbe yupo kwenye matatizo?’ akaniuliza

‘Kwanini atoroke, hilo la kutoroka halipo…na sizani kama yupo kwenye matatizo, huenda ni katika kuhangaika na mishe mishe za kutafuta riziki…huenda kuna jambo alilifuatilia, akakwama mahali, na hataki kusema wapi alipo, unafahamu tena vijana...lakini kauli yako hiyo ya kusema katoroka, ina nitia mashaka, kwanini unasema hivyo?’ nikamuuliza

‘Sisi katokana na uchunguzi wetu, tuna mambo tulitaka kumuuliza, tunahisi kuna mambo anayafahamu, unajua bado tunafuatilia ile kesi ya mauaji ya Makabrasha.....’akasema

‘Kwahiyo mnamshuku kwa msingi gani, kuwa anafahamu muuaji, au yeye kashiriki, au ni kutaka kufahamu mambo ambayo huenda yatawasaidia kumpata huyo muuaji?’ nikamuuliza.

‘Tunahisi yeye anaweza kutusaidia, ....kumpata huyo muuaji, ‘akasema.

‘Mhh, kama angelikuwa anafahamu hilo, angelisema, maana ukumbuke Makabrasha alikuwa ndiye wakili wao, na alikuwa hajafanikisha malengo yao, wasingeliweza kukaa kimiya kama wanamfahamu huyo muuaji...’ nikasema

‘Kiukweli Mkabrasha alikuwa haaminiki, inawezekana, huyo kijana anamfahamu huyo muaaji, lakini hana uhakika kuwa kweli huyo jamaa kafanya hivyo, akiogopa kujiingiza kwenye matatizi ya ushahidi.., au pia inawezekana alishirikiana na huyo muaaji, ,....’akasema.

‘Hilo la kushirikiana na huyo muuaji, nalipinga, kama nilivyokuambia, Makabrasha alikuwa ni kama ndugu yao, pili alikuwa ni wakili wao .....’nikasema.

‘Yote yawezekana, ndio maana nilitaka niongee naye mimi mwenyewe uso kwa uso, na sisi ni wataalamu wa mambo hayo, nikiongea naye tu, ninaweza kuhakiki hayo ninayotaka kuyafahamu, kama hahusiki hatutamlazimisha,...’akasema

‘Nakumbuka mara ya kwanza ulisema aliyefanya hivyo, atakuwa mtu wa ndani, anaweza akawa mfanyakazi wa mule mule,..akishirikiana na watu wa nje, ina maana mnahisi kuwa huyo aliyekuwa nje ni huyo kijana?’ nikamuuliza.

‘Ni moja ya mambo ambayo tunayafuatilia, kuhakiki, ndio maana tunataka kumuhoji yeye binafsi,…kuna ushahidi huo kuwa huenda ni yeye aliyekuwa nje,...lakini kama ulivyosema , ni kwanini wamuue mtu kama huyo,..hata sisi tunashindwa kuunganisha huo ukweli, mpaka tumuone, ila tunahisi huyo kijana atakuwa anahusika, kwa namna moja au nyingine,...sasa kinachotufanya tuzidi kumweka kwenye kundi la wahusika, ni huko kutoweke kwake kwa ghafla...’akasema

‘Mimi sijui kama kweli katoweka , hiyo kauli bado sijakubaliana nayo, kwani sio mara ya kwanza kufanya hivyo, nilishawahi kumkanya kuhusu hiyo tabia yake ya kuondoka bila kuaga, na kukaa kimiya,....’nikasema.

‘Kwahiyo hiyo sio mara ya kwanza kuondoka ghafla hivyo…?’ akauliza

‘Sio mara ya kwanza, ..ni tabia yake, na mwenyewe hujitetea akisema kazi zake zinamfanya awe hivyo, anaweza kuitwa mahali, akajikuta hana mawasiliano, au hataki kufahamika yupo wapi, kwasababu ya ushindani wa kibiashara..ndivyo anavyojietetea....’nikasema.

‘Hiyo sio kawaida kabisa, kama ni hivyo kwanini kazini kwake wasifahamu wapi alipo…ina maana kuondoka huko ni kwa kibinafsi, au sio…?’akauliza

‘Ndivyo anavyofanya hivyo, ....sio jambo geni kwetu...akirudi nitamfahamisha kuwa nyie mnamtafuta....’nikasema

‘Ni bora ufanye hivyo, kwasababu wanafamilia wa Makabrasha wanataka hiyo kesi ikamilike haraka iwezekanavyo…, na wanadai kuwa kuna njama za kuficha ukweli, na wameshapeleka malalamiko yao ngazi za juu...’akasema

‘Ni nani kafanya hivyo?’ nikauliza

‘Ni mwafamilia wao mmoja ambaye ni mwanasheria, ni mmoja wa watoto wake, acha yule mkubwa, yule mkubwa tuliongea naye tukamalizana, lakini kuna huyo mwanasheria, ni mkorofi kidogo…,anajifanya anafahamu sana sheria,....’akasema

‘Kazi ipo…kam ni huyo eeh,…haya hilo ni jukumu lenu,..na , kwahiyo mkaamua kuanza tena upelelezi au sio kutokana na shinikizo hilo.....?’nikamuuliza

‘Sio kuanza upelelezi, mbona upelelezi ulikuwa unaendelea, japokuwa sio ule wa haraka haraka, maana tulifika mahali tukasema muuaji ni mmoja wa maadui za marehemu, lakini sio kwamba tulishafunga jalada lake,..hapana,bado tunachunguza....’akasema.

‘Mimi niwatakie kila-laheri, maana mauaji hayo, yalinitia doa, kwahiyo akipatikana huyo muuaji, hata mimi nitakuwa katika wakati mzuri hata ikibidi kuwashitaki nyie polisi kwa kunisingizia mambo nisiyohusika nayo...’nikasema.

‘Huwezi kutushitaki, sisi ni moja ya kazi zetu...’akasema akijiandaa kuondoka.

‘Haya nashukuru kwa hilo, nitafanya kama ulivyoniomba, na inaonekana huyo muaaji ni mjanja sana, kafanya mauaji na imeshindikana kumfahamu ni nani, isije ikawa ni mmoja wa watu wenu...’nikasema

‘Hiyo haipo, sio watu wangu...ni tetesi za mitaani tu, hilo nakuhakikishia, ni mmoja wa maadui za marehemu, na tutampata tu....ni swala la muda...’akasema.

‘Lakini nahisi sasa hivi mnafanya hivyo kwa shinikizo la wanafamilia, nyie mlishakata tamaa..’nikasema.

‘Hapana hatukuwa tumekata tamaa, ila ushirikiana wa wananchi umekuwa mdogo, ni kama vile watu walitaka mtu huyo afe tu. Sisi bado tupo kazini, tutapambana na hawo watu,na kama kuna watu wanafahamu muuaji watuambie, sisi hatuwezi kuwashika watu kama hakuna ushahidi…’akasema

‘Nakuelewa afande..’nikasema

‘Tuliwaambia hao wanafamilia, kama kuna watu wanaowahisi watufahamishe,...maana mzazi wao, alikuwa kajijengea maisha ya kuwa na maadui wengi, hata ndani ya familia yake mwenyewe, hata marafiki zake, sasa ni nani unaweza kumhisi, hiyo sio kazi rahisi....’akasema

‘Lakini ni moja ya kazi zenu, msikwepe majukumu...’nikasema

‘Hilo silikatai, lakini ili tufanikiwe, tunahitajia ushirikiane wenu,...na nilikuwa nataka kukuuliza swali…kuna tetesi kuwa kuna vitu viliibiwa kwako, na sasa umevipata ni kweli au si kweli?’ akaniuliza

‘Vitu gani hivyo…?’ nikamuuliza.

‘Nimesikia kuwa kuna mikataba yako ilipotea, ..na umeshaipata, je ni nani aliichukua?’ akaniuliza

‘Mimi sijafika kwenu kulalamika kuhusu kuibiwa,..ila nilisema kuna vitu vyangu havionekani, … je ulishawahi kuniona kuja kwako kulalamika kuhusu kuibiwa?’ nikamuuliza

‘Hujashitakia hilo...lakini unaweza ukaacha kutokana na shinikizo, na tunahisi uliogopa, kufanya hivyo kwa sababu ya ujanja wa Makabrasha,..na ndio maana kipindi kile tulikushikilia, tukijua huenda uliamua kumuondoa kwa tabia yake hiyo..’akasema

‘Hapana sio hivyo…’nikasema

‘Kuna tetesi hizo…,hebu niambie ukweli, maana huenda ikatusaidia katika uchunguzi wetu..’akasema

‘Mkuu mimi sina cha kukuambia,...kama ningelikuwa na tatizo hilo ningelishawaambia, na kwanini niogope kuwaambia kwa shinikio la mtu kama Makabrasha, mimi simuogopi yoyote inapohusu sheria, na nikiwa nimesimamia kweli ukweli na haki, mimi nina wanasheria wangu, wangelifanyia hilo kazi...’nikasema.

‘Sawa, lakini kama kuna lolote unalifahamu, tueleze, na ukimuona huyo kijana mwambie aje kituoni, asije akasubiri tukatumia nguvu, kwani hata kama atajificha wapi sisi tutampata tu....na kama kuna lolote wewe unahisi litatusaidia kuimaliza hiyo kesi kama raia mwema, tunakuhitajia ushirikiane wako,...’akasema akiondoka.

‘Nikimuona nitamshauri hivyo afande....’nikasema

************

Nilipomaliza kuongea na mkuu wa upelelezi, niliondoka hadi hospitalini , na nilimkuta mume wangu akiwa kwenye mapumziko baada ya mazoezi, alionekana kuchoka kidogo, sikutaka kuongea naye sana, kwani alitakiwa kupumzika, ila yeye akaanza kuongea;

‘Mdogo wangu yupo wapi, ,mbona haji kuniona....?’ akauliza

‘Nafikiri kazi zimekuwa nyingi, nitamwambia nikimuona’nikasema

‘Nasikia kuwa polisi wanamtafuta, kwani ana kosa gani?’ akaniuliza

‘Kwakweli mimi sijui,...na inaonekana una vyanzo vingi vya habari, kwanini unajihanganisha na wewe hustahili kufanya hivyo, unatakiwa kujali afya yako kwanza’nikasema

‘Mimi nazungumza kuhusu mdogo wangu...’akasema kwa ukali, na mimi nikakaa kimiya nikimsikiliza.

‘Mke wangu nilishakuambia kuwa mdogo wangu ni mtu muhimu sana kwangu,sitafurahia kama ananyanyaswa, au kusingiziwa mambo ambayo hajafanya,nilikuambia kuwa umlinde , sasa wewe unasema hujui lolote..mbona mimi nimefahamu kuwa polisi wanamtafuta’akasema

‘Yule sio mtoto mdogo anafahamu ni nini anachokifanya, ...na kutafutwa na polisi ni jambo la kawaida, kama hana hatia unafikiri watamfanya nini, au unafahamu lolote kuhusu yeye, kuwa huenda ana jambo kalifanya?’ nikamuuliza.

‘Hajafanya kitu bwana....kama kuna tatizo lolote waje waniulize mimi..’akasema kwa kujiamini

‘Wakuulize wewe kuhusu nini?’ nikamuuliza

‘Kama wanahisi kafanya kosa, waje waniulize mimi, kwasababu yule ni mdogo wangu...’akasema

‘Ina maana akifanya kosa lolote huko alipo, waje wakuulize wewe kwani yule ni mtoto mdogo, yeye umri wake, uanastahili kushitakiwa, na hata kuhukumiwa, kama kafanya kosa, ...’nikasema.

‘Mke wangu mimi nimeshakuhisi kuwa una jambo dhidi ya mdogo wangu, nimeshakushitukia unamtafuta nimi mdogo wangu, kama kuna lolote dhidi yangu pambana na mimi, usimshinikize mdogo wangu kwenye mambo yanayonihusu mimi, nikuambia ukweli, kama kuna lolote unalifahamu ambalo linamfanya mdogo wangu ashindwe kuja kuniona, naomba unifahamishe, ...maana kama nikifahamu kuna jambo baya dhidi yake, ambalo wewe unalifahamu, ukanificha, mke wanguhatutaelewana...’akasema akiniangalia na kwa kujiamini sana.

‘Mimi sijui lolote, kama ningelifahamu hilo, ningelishakuambia, ukumbuke yeye alikuwa kama mtoto wangu, mdogo wangu wa damu, nimemuhangaikia hadi hapo alipofika, sasa kwanini nishindwe kumfuatilia hilo....labda kama kafanya makosa, na kaamua kuyakimbia, mimi siwezi kujua...’nikasema.

‘Huwezi kujua..hahaha huwezi kujua lakini mengine unafuatilia na kujua…hilo kwa vile sio damu yako, unalipuuza, kama kweli angelikuwa ni mdogo wako ungelifanya hivyo, upuuzie hivyo.....!?’ akaniuliza kwa mshangao.

‘Nikuulize kitu ili tusaidiane kwa hilo, je yeye kwa mara ya mwisho kuonana naye, ilikuwa lini, alifika lini kukuona kwa mara ya mwisho..na mliongea nini, au ulimuagiza nini..?’ nikamuuliza na yeye akatulia kidogo, na baadaye akasema;

‘Kuna vitu nilimtuma, akasema kabati halifunguki, na akasema huenda wewe umebadili kitasa, na akaniambia mambo yamekuwa mabaya, hawezi tena kuendelea na mimi, ...sikumuelewa, na hatukupata muda wa kuongea naye kwa undani maana nilikuwa kwenye ratiba maalumu, ambayo haikutakiwa kusubiria...’akasema

‘Ulimtuma nini, kwanini hukuniambia mimi, au kumtuma kwangu ili niweze kukupatia hivyo vitu ..kuna siri gani kati yako na mdogo wako?’ nikamuuliza

‘Hicho nilichomtuma ni mambo yangu mimi na yeye, kuna mambo mengine yanahusu maswala yangu, mimi na yeye, sikutaka kukusumbua, kama ningelikuhitajia wewe, ningelikuambia tu, kwanini niogope kukuambia eeh…’akasema

‘Bado hujanirizisha kwa jibu lako…’nikasema

‘Sikiliza mke wangu, unajua mimi mume wako nimebadilika, wewe hulioni hilo,…matatizo haya yamenibadili, mimi sio yule mume wako wa wa…ok, ngoja nikirudi nyumbani tutaongea hapa sio mahali salama kwa mazungumzo hayo, unanielewa mke wangu…’akasema

‘Nona kweli umebadilika, …na kubadilika huko ujiandae vyema, maana kunaweza kukubadili kweli…’nikasema

‘Mke wangu niamini…nataka tuwe mke na mume kweli…na mimi niwajibike kama mume, hivi hutaki kunisaidia kwa hilo,..na na… kuna mambo mengi nahitajia kuyaweka sawa, ili nitimize dhamira yangu hiyo...na kwa hilo ni lazima tuwe na makubaliano,ya kimsingi, bila hivyo mambo hayatakwenda vyema, na sioni kwanini, ufunge kabati langu, ...’akasema kama analalamika.

‘Nilifunga hilo kabati,kwasababu kuna vitu vilipotea, na hatujajua ni nani alivichukua, wewe ulisema hujavichukua, kwahiyo nikaona ili kulinda usalama wa vitu vyetu, ni muhimu kubadili kila kitu. Nitakupa ufungua wa kabati lako, ukitoka,kwa hivi sasa ninao, hili ni kwa usalama wa vitu vyote mle ndani...’nikasema

‘Kuna vitu nahitajika kuvichukua mara kwa mara, hata nikiwemo humu.., na mara nyingi ndio namtuma mdogo wangu, huoni itakuwa vigumu kuvipata, na utafanya nifanye majukumu yangu kwa shida,…nielewe hapo, ni kwa masilahi ta familia, unanielewa mke wangu?’ akaniuliza

‘Ukihitajia vitu vyako, niambie mimi, au mtume mdogo wako kwangu mimi, na kwa vile mimi nipo nitampatia, au mimi sio mke wako, huniamini, unamuamini mdogo wako zaidi yangu, huoni hilo ni kosa...’nikasema.

‘Mhh, haya,....nikitoka hapa tutayaweka sawa,....mimi ni mume wako, nahitajia kujua kila kitu, na ilitakiwa mimi ndiye nifanya hivyo, lakini naona wewe umejiamulia wewe mwenyewe tu, ...nikitoka hapa ni lazima niweke haya mambo sawa, itakuwa sio vyema kila mtu anafanya anavyotaka...’akasema

‘Hamna shida ukitoka tutayamaliza, na usiseme ‘sio kila mtu..’, aliyefanya hivyo ni mke wako, na nimefanya hivyo kwa nia njema, na nitashukuru sana ukirudi nyumbani...maana sasa hivi kila kitu kipo sawa, usijali ...’nikasema na yeye akaniangalia, na kusema;

‘Mke wangu, nikuulize tena hili swali, ni nini mliongea na mdogo wangu ambacho kimefanya awe hivyo, alipofika siku ile alikuwa hana amani,…namfahamu sana, kuna kitu kimemtokea, mpaka akakimbia…na ni wewe unayeweza kumfanya awe hivyo…?’ akaniuliza

‘Ina maana kakimbia?’ nikamuuliza kwa mshangao

‘Sio kawaida yake, nahisi kuna kitu,....kama unahusika na jambo baya, au ….kuna kitu anajishuku, au..hata sielewi,…..ni bora uniambie mapema, sitaweza kuvumilia, kama kweli unahusika na hilo..’akasema

‘Mimi sijakuelewa, ...mume wangu, hebu kwanza nikuulize, uniambie kwa uhakika wako, je umeshapona na kuweza kukumbuka yote yaliyotokea nyuma, maana docta kaniambia sasa hivi umeshaanza kujijua na kukumbuka mambo yaliyopita,..je ni kweli?’ nikamuuliza.

‘Usikwepe swali...nimekuuliza kuhusu mdogo wangu...’akasema

‘Ndio maana nataka niwe na uhakika na hilo kabla sijakujibu swali lako..na kabla sijakuambia lolote, maana kuna mengi ya kuongea,…lakini siwezi kukiuka mkataba wetu,..sasa niambie ukweli je umeshapona, kiukweli, isije ikatokea jambo ukaja kunilaumu….’nikasema

‘Nimeshapona….unataka kuniuliza swali gani…’akasema

‘Una uhakika umeshapona, docta kaniambia umepona, lakini nataka uhakika wako, usije kujifany aumepona ukaharibikiwa tena, ukafanya mambo ya ajabu tena…una uhakika umepona…?’ nikauliza.

‘Swali gani unataka kuniuliza, nikujibu?’ akauliza, kwanza akajibaragua kama anatabasamu, ile ya kuonyesha ananijali.

‘Unakumbuka siku alipouwawa Makabrasha..?’ nikamuuliza hapo akashtuka, na akageuka kuangalia nje, halafu akasema

‘Mhh…kwanini unaiuliza hivyo…?’ akaniuliza bila kuniangalia

‘Nakuuliza hivyo ili kupima kama kweli umepona au la…’nikasema

‘Ehee…yah, nakumbuka, ..ilikuwa tarehe eeh…mmh, sina uhakika na tarehe, ila nakumbuka tu hivyo…’akasema

‘Je siku ile uliwahi kufika kwake, ukaongea naye, na ukiwa humo ndio akapigwa risasi..?’ nikamuuliza

‘Wewe…ni-ni-ni nani kakuambia hayo....?’ akauliza akionyesha mshituko fulani, nikamkagua kuhakikisha kama yupo sawa.

‘Nimekuuliza swali nikiwa na maana, je ulikuwepo au hukuwepo, ndio au hapana, sitaki maelezo, nisije nikakuchosha?’ nikamuuliza

‘Hapana, sikuwepo mimi nilikuwa naumwa, .’akasema sasa akijituliza.

‘Hapo sasa inaonyesha umepona, unakumbuka, kama unafahamu kuwa siku hiyo ulikuwa unaumwa, ndio maana hukuweza kwenda huko, basi inaonyesha unakumbuka vyema, ...’ nikasema na hapo akainua uso kuniangalia.

‘Kuna nini mke wangu kimetokea…?’ akaniuliza

‘Ni bora ukumbuke vyema, maana watu wanaweza kukudhania kuwa ulikuwa unajifanya unaumwa, kutokana na kuonekana sehemu mbali mbali, wakati ulitakiwa uwe hospitalini, ..’nikasema na yeye akabakia kimiya, na baadaye akasema;

‘Mke wangu sikiliza nikuambia kitu,..na hili ni muhimu sana kwako, hayo maswala ya mauaji ya Makabrasha yaache kama yalivyo, mimi nimeshaongea na wakili, anayashughulikia, usijitumbukize kwenye maswala yasiyokuhusu, utajitakia matatizo ambayo sipendi wewe uyapate, wewe ni mke wangu, ninajali sana usalama wako, hayo mambo mengine uwaachie wanaume...’akasema kwa kujiamini

‘Una uhakika na hilo, kuwa hukumbuki kilichotokea, ....maana kama ulionekana huko, ujue polisi wanasubiri upone wakuulize hilo swali, ni bora ukaniambia ukweli ili nijue jinsi gani ya kuwasaidia,...’nikasema.

‘Mimi sikumbuki bwana, hayo sijui umeyapata wapi, ina mana ndilo lililomfanya mdogo wangu akimbie, kama ni hilo, umemshinikiza mdogo wangu mpaka akakuambia mambo ambayo hutakiwi kuyafahamu, utaniweka mahali ambapo sitakuelewa, ....’akasema kwa hasira.

‘Utanielewa tu , siku ikifika, maana sio mimi tu ninayehitajia huo ukweli, hata mkuu wa upelelezi anahitajia huo ukweli, hata watoto wa Makabrasha wanahitajia huo ukweli, na hata huyo docta anayekuhudumia hapa atapenda kujua ukweli, kuwa kweli muda wote huo ulikuwa unaumwa au ulikuwa na mambo yako, isije ikawa ulipona, ukawa unasingizia, ili kufanikisha mambo yako...’nikasema

‘Unasema nini,.! yaani wewe umdiriki kusema hivyo mke wangu kuwa mimi siumwi, hivi wewe mwanamke una ubinadamu kweli, siwezi kuamini haya...’akasema kwa sauti ya unyonge.

‘Kuumwa ulikuwa unaumwa kweli, lakini matendo yako yananitia mashaka, nahisi kuna muda ulikuwa umepona, ukaamua kutumia kama ulivyoshawishika…, ili kuweza kukamilisha mambo yako, sasa mimi sijui, ...’nikasema

‘Siamini masikio yangu…’akasema

‘Naongelea uhalisia….kama ulipona lini mimi sijui…, je ulipona baada ya Makabrasha kuuwawa, au kabla ya hapo, ....hilo litakuwa juu yako na docta anayekuhudumia, cha muhimu ni ukweli...nausubiria sana huo ukweli, siku utapoona umepona kweli, uwe tayari kuelezea hayo na kila kitu....na wote wanaohusika, na tukimalizana, huenda Inspekta naye atakuwa akikusubiria ......’nikasema

‘Inspecta!!!...wa nini…huyo mzee atulie ..ndiye kaanza tena, hajakoma ubishi eeh, wewe ubiria, kasema nini huyo mzee…?’ akauliza

‘Anatimiza wajibu wake…’nikasema

‘Wewe mwanamke, usijifanye upo juu...nakuonya kwa hilo, usijiingize kwenye matatizo, unakumbuka mkataba wetu unasema nini, mume ndiye nani...’akataka kuongea na mimi nikasema.

‘Huo ulikuwa mkataba wako sio na marehemu sio.., ...ongea kuhusu mkataba wetu, je mkataba wetu unasema nini, hilo ndilo la muhimu, ama kuhusu maswala ya mkataba usiwe na shaka nayo, mimi ninachokihitajia ni afya yako, ...ukipona mambo ya mkataba yatajielezea yenyewe, utahukumu haki kwa haki, au sio, si ndio unautegemea huo..’nikasema

‘Sio mimi, ni wewe uliyeutengeneza au sio…’akasema

‘Halafu nimesahau jambo....’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka sasa, ...nikamsogelea kama kumnong’oneza;

‘Eksi, wako, mpenzi wako yule wa kujifunzia, si unamkumbuka…enzi kabla hatujaona…na yeye kakimbilia kwao...nahisi kafahamu kuwa mliyoyafanya yameshagundulikana...sasa sijui, huenda wapo na mdogo wako huko, au ndio mumepanga iwe hivyo, mimi sijui, na docta....’nikakatiza maana mlango ulifunguliwa

*************

Mlango ulipofunguliwa…mume wangu bado alikuwa kashikwa na butwaa, mdomo unamcheza cheza akitaka kuongea jambo…uso ukajenga chuki…lakini alipomuona docta akatabasamu kidogo, akakunjua uso, uliokwisha kuanza kuharibika kwa chuki fulani,...halafu akasema;

‘Mke wangu hayo hatujamaliza, ngoja nirudi nyumbani tutapambana huko huko, ....siogopi lolote, ...nafikiri ulikuwa hujanitambua,mimi sio yule mume wako wa zamani , mume bwege, nimeshajitambua, nikuambie ukweli, mimi siogopi polisi au yoyote yule, hilo nimeshajipanga vyema tu....’akasema na docta akawa keshaingia,

Docta akawa anamuangalia mume wangu kwa uso wa kujiuliza aliona jinsi mume wangu alivyobadilika usoni...

‘Karibu sana docta, nimeshapona unaonaeeh, naongea na mke wangu....’akasema akijibaragua kwangu;

‘Hajapona huyu anajifanyiza tu kupona…’nikasema na yeye akageuka kuniangalia, na mimi sikumjali, na docta akasema

‘Leo tutalithibitisha hilo..maana hata polisi wananisumbua, wanataka kuongea nay eye..’akasema docta

‘Polisi..!!’akasema hivyo docta

`Bado mmoja...’ nikasema kwa sauti iliyowafanya wote waniangalie.

Nb Je ni kweli kuwa mume wa huyo mdada alikuwa akisingizia kuumwa, je ni kweli anahusika na hayo yote, na swali kubwa hadi sasa, ni nani aliyemuua Makabrasha, ...?


WAZO LA LEO: Maisha ya ndoa sio kuonyeshana ubabe, kuwa ni nani zaidi, maisha ya ndoa ni makubaliano , yenye lengo jema, la kila mtu kufahamu nafasi yake na wajibu wake, kwani wanandoa ni kitu kimoja, ili mfanikiwe kwenye safari yenu ya upendo na furaha, ni vyema kila mmoja akajiona ni muhusika mkuu, kwa nafasi yake. Kila mmoja amjali mwenzake,amuonee huruma, na hekima, busara na upendo viwe ndivyo dira ya kila mmojawapo.
 
SEHEMU YA 87


‘Mke wangu hayo hatujamaliza, ngoja nirudi nyumbani tutapambana huko huko, ....siogopi lolote, ...' huyo alikuwa mume wangu

**************

‘Karibu sana docta, nimeshapona unaonaeeh, naongea na mke wangu....’akasema akijibaragua kwangu;

‘Hajapona huyu anajifanyiza tu kupona…’nikasema na yeye akageuka kuniangalia, na mimi sikumjali, na docta akasema

‘Leo tutalithibitisha hilo..maana hata polisi wananisumbua, wanataka kuongea nay eye..’akasema

'Polisi wanataka kuongea na mimi...?' akauliza mume wangu sasa akimuangalia docta kwa uso wenye wasiwasi.

'Ndio, lakini siwezi kuwaruhusu mpaka nihakikishe upo salama, ...nimewaambia leo nitakufanyia majaribio, nikiona bado, sitawaruhusu, au wewe unasemaje..?' akamuuliza mume wangu.

'Waambie wataongea na mimi kupitia kwa wakili wangu...'akasema

'Kwanini wakili!!?' docta akauliza kwa mashaka

'Hao watu wananihis vibaya,..yaani hata akili hawana..mimi siwaogopi maana ukweli upo wazi, eti docta mimi nawezaje kutoka humu eeh,..waache waje bwana...'akasema

'Docta unaona huyu mtu hajapona..'nikasema

'Nimepona bwana...waache waje, na wewe mke wangu haya yote ni sababu yako,...'akasema na akajitambua kuwa docta yupo akageuza maneno.

'Ni hivi docta, sitaki hawa watu wamsumbue mke wangu, sasa yeye namwambia aniachie haya mambo anadai mimi bado naumwa...'akasema

***********
Docta aliniangalia na baadaye akamwangalia mume wangu, akahisi kuna kutokuelewana kati yangu na mume wangu, akamgeukia mume wangu akamuangalia kwa makini, halafu akasema;

'Usiharibu masharti, kwanini unafanya hivyo...?' akamuuliza

'Docta nipo safi, usijali kabisa, sijaharibu kitu....'akasema, na alipoona docta kageuka upande mwingine akanitupia jicho, lenye chuki fulani, lakini mimi sikumjali, sasa moyo wangu ulishaingiwa na kutu.....

Kiukweli japokuwa nilijifanya sijali, lakini ndani ya nafsi bado nilikuwa na mashaka kuwa, huenda kweli bado, mume wangu anaumwa, lakini nikaona pia ni moja ya njia ya kumpima kama kweli kapona au la, ja anaumwa au anaigiza kuumwa, alishapona!

Docta akageuka na kutuona tunaangaliana, ....

‘Kuna tatizo lolote...?’ akauliza docta, akiniangalia mimi na baadae mume wangu

‘Muuulize mgonjwa wako, mimi sina tatizo ...’nikasema na kugeuka kama nataka kuondoka

‘Hakuna tatizo docta, ni mambo ya kifamilia, na majukumu ya nyumbani..na pia docta, unajua tena, siku nyingi sijaonana na mke wangu, na kwahiyo kila mmoja ana hamu na mwenzake...’akasema mume wangu huku akicheka kicheko cha kujilazimisha.

‘Lakini tulishakuambia kuwa mambo ya kifamilia uyaweke pembeni, hapa ni afya yako tu, je ukifa ni nani ataangalia hayo ya kifamilia...?’ akauliza

‘Nimekuelewa docta, hakuna tatizo...’akasema mume wangu na mimi nikageuka mara moja kumwangalia mume wangu ambaye na yeye aliniangalia, na uso wake ulionyesha chuki fulani kwangu, mimi sikujali, nikageuka kumwangalia docta;

‘Docta mgonjwa anaendeleaje maana nimeongea naye , anadi keshapona, je ni kweli?’ nikauliza

‘Kwa ujumla anaendelea vyema, na wiki hii tutaangalia, kama hali ni hii hii, ni bora tu arudi nyumbani, na cha muhimu ni yeye mwenyewe kutimiza yale tuliyomuagiza, apunguze hasira, asiwe na mawazo, yaani ajiepusha nayale yote yanayoleta mashinikizo ya damu,....yeye mwenyewe keshaelewa, na wewe pia kama mtu wake wa karibu ujaribu kumsaidia kwa hilo...’akasema docta.

‘Lakini kumbukumbu na kila kitu sasa kipo kama kawaida?’ nikauliza

‘Kipo kama kawaida, hatujaona tatizo ya hilo..na pia haijatokea tatizo kuhusu matendo yale ya kufanya vitu kama ndoto, haijatokea tena..lakini bado hatujajitosheleza kwa hilo, ndio maana tunahitajia tena wiki hii moja, tuone, ‘akasema

‘Sawa nitakuja ofisini kwako tuongee kidogo...’nikasema, na mume wangu hapo akanitupia jicho la kujiuliza, na sikujali hilo.

‘Karibu sana,...’akasema huku akimwangalia mgonjwa wake, ili kuhakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, na alipomaliza, akageuka kuondoka, akisema

'Haya mkimaliza kuongea mim nipo ofisini kwangu, usichelewe...'akasema

'Sawa nakuja docta...'nikasema huku nikimsogelea mume wangu, na nilipohakikisha docta kaondoka, nikasema;

‘Sasa mimi nataka kuondoka, kuna zaidi labda au.. , kuna kitu unahitaji, mdogo wako hayupo, kama kun akitu muhimu niambie tu?’ nikamuuliza

‘Hakuna zaidi, ....nitafurahi kama utampata mdogo wangu, na ukimuona mwambia aje tuonane , ni muhimu sana hilo, ikibidi leo leo...’akasema

‘Nitafanmya hivyo,...na nasikia rafiki yangu, anarudi karibuni’nikasema.

‘Rafiki yako!! Ohhh..yule msomi wa Ulaya, ina maana keshamaliza kusoma, mbona mapema hivyo...?’akasema akionyesha furaha usoni.

‘Mapema, kwa masomo yake, sio ya kuchukua muda mrefu, labda akitaka kuongezea kozi yake, lakini kiratiba keshamaliza, natumai umemkosa sana,..’nikasema, na kuongea hivyo kiutani.

‘Kwahiyo anarudi lini?’ akauliza bila kujali utani wangu

‘Natumai wiki ijayo..’nikasema

‘Muda huo nitakuwa nyumbani,...hakuna shida...’akasema

‘Na mtoto wake atakuwa mkubwa sasa, watoto hawachelewagi kukua...’nikaanza kuchokoza

‘Ni kweli watoto hawakawii kukua,..unaweza kushangaa anatambaa, lakini bado kutambaa au sio...?'akasema huku akionyesha kuwaza jambo.

‘Yawezekana..sina uhakika na hilo...mmh, mimi najiuliza mpaka sasa hivi baba yake atakuwa ni nani maana rafiki yangu kanificha kabisa, hutaamini kama ni rafiki yangu kweli....’nikasema.

‘Mzazi hafichwi,baba yake yupo na atajulikana tu, ...’akasema.

‘Yeye kasema mtoto wake hana baba, hata jina kaandika la kwake, yaani jina la mtoto na kwa baba yake, kaandika jina la babu yake’akasema.

‘Thubutu, huyo anajidanganya, baba yake yupo, hata akificha vipi, ...we utaona tu...’akasema akionyesha kukerwa.

‘Wewe unamfahamu baba yake?’ nikamuuliza

‘Kama wewe humfahamu, mimi nitamfahamu vipi, hiyo ni siri yake, lakini nafahamu kuwa kila mtoto ana baba yake...hata wewe unalifahamu hilo...’akasema.

‘Lakini yeye kasema mtoto wake hana baba, kwani hakutaka baba yake ajulikane, na alifanya hivyo makusudi, nia yake ulikuwa kupata mtoto, na sio kuwa na mtu mwingine anayeitwa baba, ni maamuzi yake, huwezi kumuingilia’nikasema.

‘Hilo anasema tu kwa watu wengine, lakini yule mtoto ana baba yake..., na hilo yeye analifahamu fika, ni kuwahadaa watu wengine tu, labda kutokana na mipangilio yake, lakini ipo siku baba yake utamuona...’akasema

‘Mbona unasema kwa uhakika hivyo, kama vile unamfahamu huyo baba yake?’ nikamuuliza

‘Uhakika ndio, kwasababu mtoto hawezi kuzaliwa bila baba, mimi napinga hiyo kauli yako ya kusema huyo mtoto hana baba..’akasema.

‘Mimi nimeongea naye, na amesema hakuna mtu wa kudai kuwa yule mtoto ni wake, na kila kitu keshakiweka sawa, hataki mwanaume yoyote kuja na kudai kuwa yule mtoto ni wake...’nikasema.

‘Mliongea naye lini?’ akaniuliza

‘Jana usiku nilipata bahati ya kuongea naye, na sijana tu , siku zote nikifikia hapo kumuuliza baba wa huyo mtoto ni nani, yeye anasema hilo keshaliweka kisheria, huyo mtoto hana baba ...’nikasema.

‘Hana akili, anajidanganya tu..., kama kasema hivyo, basi ujue anakuficha tu,..lakini nina uhakika anafahamu fika ni nani baba wa mtoto wake, na huenda wameshakubaliana, jinsi gani mtoto huyo ataishi, na haki zote keshazijua, sizani atakuwa mjinga kukataa haki za mtoto wake..’akasema na kushituka kidogo, kwani alishaanza kujieleza.

‘Haki gani, kama yeye keshasema mtoto hana baba, hajafunga ndoa na mume yoyote, haki hizo zitatoka wapi...?' nikauliza na yeye hapo akakaa kimia.

'Kasema hata kama, kuna maandishi ya kukubaliana, kayakubali tu, kuepusha shari, lakini haki za mtoto wake zipo kwa mama yake, kwa mujibu wa imani yake..na hata kisheria, keshaandikisha hivyo...'nikasema

'Mhh, tatizo wewe unaongea kwa vile...lakini sizani kama kweli anamjali mtoto wake atakaa haki za mtoto wake...'akasema

'Haki zipi...kama yeye mwenyewe ana uwezo wa kumlea, yeye keshaweka wazi, ndio maana hataki watu wajipendekeze kwake, kuwa ni wao, kuwa eti huyo mtu ni baba yake,...akirudi kila kitu kitakuwa wazi,...’nikasema kuzidi kumchokoza.

'Sawa ngoja tumsubirie...yeye si rafiki yako, tutamsikia...'akasema

'Ni kwanini wanaume wanahangaika, huenda hata huyo mwanaume ana mkewe, anakwenda kutembea nje ya ndoa, hivi mnatafuta nini huko...?' nikajifanya kumuuliza.

‘Mke wangu usicheze na wanaume, ..mmh, unafahamu pamoja na kuwa mke na mume wanaishi pamoja, lakini kuna mambo mengine yanaweza kutendeka nje, kwa masilahi fulani au kwasababu fulani..ndio nakubali ni makosa, lakini wakati mwingine inatokea tu...au tuseme..., inakuwa ni bahati mbaya, au aah, mke wangu tuachane na hayo....’akasema

'Inatokea tu kwa vipi, bahati mbaya kwa vipi, mtu ana akaili zake anajua masharti ya ndoa, anajua imani ya dini inasemaje...aende kuzini nje useme ni bahati mbaya,,,,,?’ nikamuuliza

‘Kwa kuongea tu mke wangu, zipo sababu tu, kuna watu wanataka mtoto, labda wa kike, au wa kiume, na mkewe hajajaliwa, au...vyovyote vile, sasa inatokea mwanaume anashindwa kuvumilia, na akatekwa na tamaa, ikatokea bahati mbaya, wakakutana na mwanamke mwingine..eeh, wakajikuta kwenye mapenzi ya wizi,...inawezekana bila kupanga hivyo, lakini tii...mimba, sasa wakipata mtoto, unafikiri hapo itakuwaje...’akawa anajiuma uma.

‘Kwa mfano kama wewe hivi, ulivyokuwa unataka mtoto wa kiume, tuchukulie hivyo, na ikawa umetekwa na ulevi, bila kujijua, ukakutana na mwanamke, mkazaa naye, si ndio hivyo...hiyo ni bahati mbaya?’ nikamchokoza na yeye akatoa tabasamu la mwaka, sikujua kwanini anatabasamu hivyo.

‘Mke wangu bwana,...hahaha, unanichokoza eeh..mimi naona tuyaache hayo, ila mimi nina uhakika kuwa huyo rafiki yako anafahamu ni nini anachokifanya, mtoto wake ana baba, na huenda wameshakubaliana jambo hapo, ila hataki kusema ni nani..’akasema.

‘Na huenda baba yake akawa ni wewe?’ nikamuuliza, na akaniangalia, na mimi nikawa nimemkazia macho

‘Mke wangu bwana, kwanini unasema hivyo...mimi, hahaha, umenichoka kweli?’ akaniuliza huku akiniangalia pembeni, huku akijifanya kucheka.

‘Kwasababu mtoto huyo anafanana na wewe...’nikasema

‘Hahaha..mke wangu leo umeamua kunichekesha, ulimuona kabisa kuwa anafanana na mimi,... hahaha, hata yeye, aliwahi kusema hivyo...mmmh, lakini mimi sijapata muda wa kumwangalia vyema, kuwa anafanana na mimim unafahamu rafiki yako amemficha sana huyo mtoto wake,....kama anafanana na mimi duuh, hiyo itakuwa...hapana sio kweli...’akasema huku akiendelea kutabasamu, na mimi moyoni nikasema `nimekunasa, .....’.

‘Kama anafanana na wewe hapo ina maana gani..huwezi kulikwepa hilo, huo ni ushahidi tosha, na ukumbuke...au?’ nikamuuliza

‘Ina maana gani,...itakuwa na maana gani, mbona watu wanafanana tu,...inatokea tu, mimi sina uhakika na hilo,na tuliache kama lilivyo, kama anarudi, tutamuona, na mimi kama mume wako, kama mkataba unavyosema, nitaona ni nini cha kufanya kwa masillahi ya familia....’akasema

‘Yah,...kama mume, na masilahi ya familia yanahusikanaje na yeye...sema ukweli wako mume wangu...'nikasema

'Nasema kuhusu mkatba wetu, ..sio kuhusu yeye...'akasema

'Mkataba mkataba...sawa, huo utamaliza kla kitu au sio, na nina uhakika hutaupinga, mimi nipo tayari kwa hilo...'nikasema na hapo akanitupia jicho..na kusema

'Tutaongea huko nyumbani au unasemaje...'akasema

'Ndio tutaongea, ...tutaongea yote, na kama una mtoto nje pia, ni lazima hilo liwekwe bayana... wewe kama mume, unaweza kufanya unavyooona ni vyema kwa masilahi ya familia, unaweza kuzini nje, ukapata mtoto,na kwa vile wewe ni mwanaume, utafanya lile uonavyo ni jema, au sio?’ nikamuuliza

‘Tuyaache kama yalivyo, naona huko unakwenda mbali...nenda docta anakusubiria, wewe si umesema unataka kuongea na yeye...’akasema

‘Aaah, hilo nimuhimu sana, kabla sijaondoka hapa, nikushauri jambo, kama huyo mtoto wa rafiki yangu ni wa kwako nakushauri ufuata taratibu za kisheria, umchukue kabisa, mshauri mwenzako, ili awe ni wako kisheria, vinginevyo, utamkosa mtoto wako, kwani mwenzako keshakataa kuwa mtoto yule hana baba...’nikasema

‘Thubutu..anajidanganya tu...wewe utaona...’akasema halafu akajibaragua na kusema;

'Utaonaeeh, ushakubali...'nikasema na yeye akageukia upande mwingine na kusema;

‘Mke wangu tuyaache hayo,....niache nipumzike...’akasema.

‘Mume wangu hayo yote ilikuwa ni mazunguzmo tu, ila nataka kukuelezea kuwa ndoa ni makubaliano kati ya mke na mume, kuna masharti ya ndoa, na moja ya masharti hayo ni kutokuzini kweli si kweli....?' nikamuuliza

'Nani kazini..mimi ...?' akaniuliza

'Sijui..kwani ukizaa nje ya ndoa, umefanya nini..huyo mtoto kapatikanaje, au mlifunga ndoa ya siri...?' nikamuuliza na yeye hapo akakaa kimia.

'Kwahiyo,..., ukitembea nje ya ndoa ni kosa kubwa sana, ndio maana hata vitabu vya dini vimetoa adhabu kubwa kwa tendo hilo, kwa mwanandoa aliyekiuka hilo...nilishawahi kukuomba useme ukweli, hukutaka kufanya hivyo, na huenda kama binadamu unakose,a basi kama muungwana ngelianiambia ukweli, lakin je uliwahi kufany ahivyo...?' nikamuuliza

‘Mke wangu nimeshakuambia kuwa hilo tuliache kama lilivyo, na sijakuambia kuwa huyo ni mtoto wangu, hayo unayasema wewe....na ni kweli, inaweza ikatokea hivyo, mume ukateleza, kwa bahati mbaya, na hata pia inawezekana kosa likatokana na wanandoa wenyewe...hilo hatulioni, tunasubiri matokea ya makosa ya wanandoa ndio tuje tulalamike, ....mke wangu haya...haya, maana umeyachokoza wewe mwenyewe, tutakuja kuyaongea, na tutayamaliza, mimi kama mume, nina hekima ya kuyamaliza hoyo, wal usijali....’akasema

‘Hakuna utetezi hapo,...mimi sitaki kukuweka kwenye mawazo mengi, ila ninachotaka kusema ni kuwa tukumbuke misingi ya ndoa, na pia ukumbuke ule mkataba wetu unasema nini, nafahamu unaukumbuka vyema huo mkataba wetu, haujabadilika, upo pale pale...’nikasema

‘Nakumbuka sana, wewe mwenyewe ulikataa kuusoma, lakini kila kitu kipo wazi, mimi naukubali huo mkataba, na nikitoka hapa nataka tuupitie tena, kama kuna mapungufu tuyaangalie, kwani kama binadamu kuna kuteleza, au sio...kwahiyo nahisi kuwa kuna haja ya kuufanyia mabadiliko ya hapa na pale, hayo yote ni muhimu tuyaangalia, nilimtegemea sana, Marehemu, lakini...mmmh,.’hapoa katulia.

‘Lakini mhh, vipi, .....mume-muua kabla ya wakati wake au sio..’nikasema

‘Tume-muua, unasema nini mke wangu, nani kamuua, ...!?’ akauliza

‘Siku anapigwa risasi ulikuwepo, ...unabisha?’ nikamuuliza na yeye akanitolea macho, na baadaye akasema;

‘Mke wangu achana na mambo hayo ya kusikia...,umeyapatia wapi hayo,....nishakuambia hilo ni swala la wanaume, liache kama lilivyo, utaona mwisho wake, utakuwaje, hilo lisikuumize kichwa ...wewe huoni hata polisi wenyewe wanajiuma-uma, kuna mambo yamejificha hapo,...tuyaache kama yalivyo...’akasema.

‘Vyovyote iwavyo, nakuomba ujitahidi upone haraka, ili tuweze kuyamaliza hayo mambo, na ili kama kuna lolote la kisheria, ujue jinsi gani ya kulitatua, kama ulivyosema kuwa hayo ni mambo ya wanaume, sawa, tutaona jinsi gani wanaume mtakavyolitatua hilo..'nikasema

'Yah...hilo halitushindi...wanaume...'akasema

'Haya.., maana nijuavyo mimi polisi wapo mbioni kukutana na wewe, sasa hivi wanamtafuta huyo muuaji kwa nguvu zote,.....na sijui kwanini mdogo wako akaamua kukimbia, nashangaa, na yeye si-ni mwanaume kwanini anakimbia, au,... kwanini asisubiri kupambana kiume?’ nikamuuliza.

‘Mdogo wangu hajakimbia,... sizani kama kakimbia kwasabbu ya hilo, ukimuona mwambie aje, na nilishakukanya,inaonekana kuna jambo mumemfanya huyo mdogo wangu, akaingiwa na wasiwasi, kama kuna lolote umemfanya na ndio ikawa sababu ya yeye kukimbia ,ohoooh, mke wangu sijui kama utanielewa, ....yule ni mdogo wangu, na lolote baya dhidi yake, ni kama umenifanyia mimi, sitavumilia,...kamwe, vyovyote iwavyo, nitapambana na huyo mtu kwa hali yoyote ile...’akasema.

‘Unanitisha au unaniambia, ukumbuke unayeongea naye ni nani,...mimi ni nani kwako, mimi ni mke wako...au sio, au unafikiri unaongea na nani?’nikasema huku nikimwangalia na tabasamu mdomoni.

‘Kama unalielewa hivyo, basi fuata masharti ya mke ....kwani mke anayefahamu taratibu za ndoa hawezi kumchezea mume wake, na mume wake akae kimiya, na mimi kama mume wako siwezi kukubali hilo,siwezi kamwe kuchezewa na mwanamke, niliyemuoa, hilo ujue, ...’akasema huku akiniangalia kwa hasira.

‘Sawa nimekuelewa mume -wangu, ugua pole, na pona haraka ili upate nguvu, unahitajika sana, mume wangu uliyeniona, kwa mahari niliyokuchangia, au sio.....na hayo unayoyasema yanahitaji nguvu , na sio nguvu tu, bali akili, busara na hekima ni muhimu sana...'nikasema na hapo akakaa kimia.

'Mume wangu usione naongea haya tu....kwanza nataka kukupima kama kweli umepona..lakini pia..kukuweka tayari na mapambano yaliyopo mbele yako,...sio lele mama..kuna mauaji, kuna maswala ya mikataba...na kiukweli kuhusu mkataba mimi sirudi nyuma tena, nimeamua, na unanifahamu nikiamua jambo sirudi nyuma, ugua pole...’nikasema na kugeuka kuondoka.

‘Hahahaha, mke wangu bwana, nakuamiania sana mke wangu, nashukuru kama umeukubali huo mkataba, natamani nipone haraka..hahaha kweli wewe ni kiboko, tutapambana tu... , usijali kabisa mke wangu, mimi ni mume wako, hakitaharibika kitu,....unachezea wanaume wewe....hahaha..’akasema akicheka na mimi sikugeuka nyumba, nikaelekea ofisi kwa docta.

***********

‘Hivi bado mume wangu anaumwa kweli,....sio kuwa alipona muda akawa anajiigiza kuwa bado anaumwa?’ nikamuuliza docta moja kwa moja nikiwa bado ma mawingu ya hasira kichwani.

‘Kwanini unaniuliza hivyo, ?!’ docta naye akauliza kwa mshangao

‘Sio kwamba nasema haumwi, ila nahisi alishapona muda mrefu,... kwasababu wakati mwingine anaonekana kufanya mambo kama haumwi vile...alishafanya mambo ambayo hayawezi kufanywa an mtu anayeumwa kihivyo’nikasema

‘Ni kawaida maana matatizo yake ni ya kuja na kuondoka sio ugonjwa ambao unakuwa nao wakati wote, anaweza akawa yupo na hali nzuri kwa wakati fulani lakini baadaye hali ikabadilika, kutokana na matukio,..’akasema

‘Na anaweza akafanya mambo bila kujua kuwa alifanya?’ nikamuuliza

‘Ndio, ....nilishakuambia kuwa hata usiku anaweza akaamuka akafanya kazi, na asiweze kujitambua kuwa alifanya hivyo,...nikuulize kwanini umefikia kuniuliza hivyo?’ akauliza

‘Nahisi kuwa mume wangu alishapona muda mrefu, lakni anaigiza kuumwa..mimi nimeshaingiwa na mashaka hayo....’nikasema na yeye akaniangalia kwa mashaka na kusema;

‘Kwhiyo hata sisi wataalamu hutuamini, maana ukisema hivyo, unatufanya hata sisi tuonekane hatujui kazi zetu...’akasema akiniangalia kwa mshangao

‘Samahani docta, sina nia mbaya, ila ninataka kuhakiki mambo fulani fulani, nikuulize kwahiyo hayo matatizo aliyo nayo mume wangu, kama kwa mfano mtu akaamua kuigiza tu, mnaweza kumtambua kuwa anaigiza, huenda kwasababu zake akajifanya bado anaumwa, je mtaweza kumtambua kuwa anaumwa kweli, au anaigiza?’ nikamuuliza

‘Kwa hilo tatizo, huwezi kutudanganya sisi, tuna vipimo vya kuligundua hilo...ila sio muda wote mtu anaweza akawa anaumwa, kuna muda anaweza akawa na akili zake vizuri tu,...sasa labda muda huo ndiyo aigize, lakini kwanini afanye hivyo...'akasema docta

'Kwasababu za kibinafsi anaweza ..au sio..?' nikamuuliza

'Lakini sio kwa mume wako...maana keshapitia vipimo akaonekana aana tatizo hilo, sasa huko kuigiza kunatokea wapi...mimi naomba usichanganye mambo yenu ya kifamilia na taaluma yetu, acha tufanye kazi yetu, mume wako apone, mengine mtajuana nyumbani au sio....’akasema

‘Sawa, docta, samahanai kwa kusema hivyo, maana kuna mambo mume wangu aliyafanya, na kwa akili za kawaida asingeliweza kuyafanya, ....nilikuwa nimeshamshuku kuwa anaigiza kuumwa, na nina imani hiyo shuku sio kwangu tu...’nikasema

‘Ni kawaida kwa matatizo kama hayo, wengi wanaweza wasioone mtu kuwa anaumwa,matatizo aliyo nayo ni ya akili, ni kukosekana kati ya uwiano wa akili na mwili, hilo kwasasa limeshaimarika, ...'akasema

'Sawa...'nikasema

'Na...bado, ana walakini, hatuwezi kusema limekwisha kabisa, usiwe na papara, na tunakuomba baada ya hapa,usimpe mume wako wakati mgumu,..bado atahitajia hali ya utulivu,atahitajia kujiweka sawa, japokuwa kwa kiasi kikubwa anaweza kuendelea na mambo yake kama kawaida..’akasema

‘Naomba akipona, kitaaluma yenu,..basi mniambie…’nikasema

‘Bila shaka hilo ni wajibu wetu..’akasema

‘Samahani docta…naomba nikuulize jambo jingine kidogo….’nikasema

‘Uliza tu…’akasema sasa akiniangalia moja kwa moja usoni

‘Je docta, …samahani lakini, .. je wakati yupo hapa, aliwahi kutoka nje ya eneo lenu, nilisikia kitu kama hicho nikiwa jela?’ nikamuuliza

‘Mhh, hata mimi nilisikia hivyo, lakini sikuamini, maana kipindi kile, alikuwa hana uwezi huo, wa kwenda mbali sana…hata sikuamini, lakini, mmh..ni jambo la ajabu kidogo,niliwauliza wasaidizi wangu, wakasema hawana uhakika, wakalifuatilia, lakini sisi hatukulichukia maanani sana..’akasema

‘Docta hukulichukulia maanani, mtu atoweke hospitalin kwenu..!’nikasema

‘Unajua..kama ilitokea basi ni kosa, kwa mgonjwa na uzembe wa watu wangu, lakini huwezi kuwalaumu sana watu wangu, maana hakuna ushahidi huo kuwa kweli alitoweka…na cha ajabu mgonjwa nilipoongea naye hakukubaliana na hilo..ndio tukaona umuhimu wa kumuita docta huyu wa akili..’akasema.

‘Kwa jibu lako hilo docta, unanipa mashaka docta, je kama ni kweli alitoroka akarudi bila ufahamu wenu..’nikasema

‘Kwanini nikupe mashaka na jibu hilo, ni jibu lililowazi, au sio..na ni mashaka gani, sawa labda alitoroka, lakini alirudi salama au sio, au kuna kitu kilitokea, …sema tu usiogope…?’ akauliza docta

‘Mhh,.., je polisi waliwahi kuja kukuulizia swali kama hilo?’ nikamuuliza

‘Polisi,...!! mhh, hapana,…na nikuulize tu, kwanini unitilie mashaka na majibu yangu, na kwanini polisi,...labda nimekosea kuelezea, niambie tu, kuna tatizo lolote limetokea, kuhusu mgonjwa, kun akitu kibaya kakifanya labda..?’ akasema na kuniuliza

‘Docta kuna uhakika kuwa kweli mume wangu alitoka hapa na kwenda nje...kwa muda wa saa moja kasoro-soro hivi, ni kipindi kirefu hicho na akaenda huko alipokwenda, yakafanyika yaliyofanyika, akarudi, na hakuna aliyemuona,..'nikasema

'Akafanya nini labda...?' akauliza

'Siwezi kusema hilo kwa sasa...wanajua wenyewe wahusika...'nikasema na hapo akatikisa kichwa kama kutokukubaliana na mimi.

'Mimi sina uhakika na hilo..kama nilivyokuambia...'akasema

'Kama huna uhakika na hilo, na ikaonekana ni kweli, huoni kuwa hilo ni tatizo kwa watendaji wako, na pia wewe huoni kuwa kitendo hicho cha mtu kutoka kwa siri, na akurudi kwa siri, ni kitendo cha mtu aliye mzima,...na je nyie mtaeleweka vipi kwa kitendo hicho, je hakuna mtu kweli aliyeshirikiana naye humu ndani?’ nikamuuliza

‘Mimi kama docta wake, inanipa mashaka kwa hilo, maana..hali ya mume wako kipindi hicho haikuwa nzuri, ukumbuke, matatizo aliyo nayo ni ya uti wa mgongo, hilo sio tatizo dogo kama mnavyofikiria nyie...ndio kuna muda alikuwa na hali nzuri, akawa anachukua mazoezi ya kutembea, ikatia moyo…lakini ikatokea tena matatizo hayo ya kuchanganyikiwa, na tukawa makini sana naye..’akasema

‘Docta, hayo ya kuchanganyikiwa je yanaweza yeye kutoroka akaenda akafanya mambo yenye akili, maana ni mambo yenye kupangiliwa, na akarudi salama, ni kweli hayo ni ya kuchanganyikiwa, si yanatendwa na mtu mwenye akili zake…’nikasema.

‘Mimi siwezi kukukataliam kwasababu ya tetesi tu..kama ushahidi upo basi tutaliangalia kwa nyanja hiyo, ikibidi, … anaweza kufanya ya ajabu kabisa, ambayo huwezi kufikiria,... lakini ile hali aliyokuwa nayo...kutoka humu, ni lazima kuna msaada wa mtu, sasa ni nani, kwa vile hatukuliona hilo kama ni tatizo kubwa, basi tukaliacha hivyo, ila kisisi madocta, tulilichukulia kama sababu ya ugonjwa wake, na kwa watendaji wangu tuliwapatia onyo, sasa kama kuna tatizo zaidi ya hilo, labda mtuambie ....’akasema

‘Docta je akija polisi akakuuliza hivyo wewe utamjibu nini?’ nikamuuliza

‘Akaniuliza hivyo nini, sijakuelewa?’ akauliza

‘Kwa mfano polisi akaja akakuuliza je mume wangu aliwahi kutoka hapa hospitalini siku fulani, kwa muda kadhaa, na kurudi bila ya watu kufahamu?’ nikamuuliza

‘Jibu lipo wazi, nitawajibu kama nilivyokujibu wewe, siwezi kujibu kinyume na ukweli, ndio hivyo, au....’akasema

‘Ni muhimu sana, ukajiandaa kwa hilo docta...swali kama hilo linakuja,...’nikasema na kuinuka kutaka kuondoka, na docta akasema;

‘Hebu subiri kidogo kwanza.....’

NB:Mambo ndio hivyo, tunajitahidi kihivyo, je tunafikisha ujumbe, je kisa kinafundisha, kinaeleweka, kinapendeza...sijui, hilo nawaachia nyie,


WAZO LA LEO: Matatizo mengine yanayotokea kwenye ndoa, ni kutokana na elimu, au ufahamu mdogo wa watu wanaoingia kwenye ndoa, kuwa huenda watu wanaoana bila kujua ni nini maana ya ndoa, wanaingia kwenye ndoa kama fasheni tu, kwa vile inatakiwa iwe hivyo. Landa kwa suhauri wangu, hili kwetu sisi wazazi, na walezi, lakini pia kwa viongozi wa dini kuliangalia hili kwa mapana, maana kiukweli hapa ndio chimbuko la kizazi, na kizazi bora hujenga jamii bora, yenye amani na upendo. Tukiwa makini kwa hili, huenda tutakwepesha madhara mengi ndani ya jamii..ni wazo tu.
 
SEHEMU YA 88


Nilipokuwa nyumbani, nilijikuta nikiwazia mazungumzo yangu na docta, na nilishindwa kuhakiki mawazo yangu ambayo yalinituma kuwa huenda mume wangu anaigiza kuumwa,

‘Lakini mwenye uhakika wa kuwa kweli mume wangu anaumwa au kapona ni docta….Hata nikisimama mahakamani kauli ya docta inaaminika zaidi ya kauli yangu…’nikawaza hivyo.

'Hapa nipo na matatizo mawili yote yaanmgusa mume wangu, kuna tatizo la mauaji ya Makabrasha, bado linaiandama nyumba yangu...je ni kweli mume wangu kahusika,...ushahid unaelekeza huko..na hadi sasa sijafanikiwa kuwa na ushahid kamili, diary ya shemeji yangu haijalifichua hilo,....ngoja nizidi kuisoma...sijaimaliza bado...

'Lakini kuna hili tatizo langu na mume wangu...je ni kweli kanisaliti...ushahid unaonyesha hivyo, kuwa kweli ana mtoto nje ya ndoa,..na inavyoonekana mtoto huyo ni huyo wa rafiki yangu...je ushahidi nilio nao unajitosheleza..bado,...na mdada anaweza akafika hivi karibuni...

‘Nifanye nini, kuyathibitisha haya yote, …’nikakuna kichwa, na haraka nikachukua laptop a kuanza kuendelea kusoma diary ya shemeji yangu..

Tuendelee na kisa chetu

**********
Nikiwa nasubiria mgeni wangu kutoka ulaya, mawazo yangu yalikumbuka kuhusu ‘diary ya shemeji….’

Kabla sijaamua kuja huku uwanja wa ndege, nilikuwa nikiiptia hiyo diary,..na ghafla ndio nikapata hii safari ya kuja kumpokea mgeni wangu kutoka ulaya, wala sikuwa na utaratibu nao, haikuwa kwenye ratiba zangu kabisa...

Siku hiyo nilikuwa naapitia diary ya shemeji, nilifika sehemu inayoelezea tukio la usiku wa ajabu, yeye alindika hivyo, tukio la usiku wa maajabu, anasema siku hiyo hataweza kuisahau maana ni siku ambayo aliweza kuonja asali....sikuelewa hapo ana maana gani kuonja asali, hakuelezea zaidi,...

-Nikawa nawaza hapo kwa muda kwanza….,

'Kuonja asali, ..ni asali gani hii..., na usiku huo ni usiku gani mpaka uitwe wa maajabu,, hapo nikawekea alama ya kuuliza..ili ikibidi nifuatilie hilo, halafu nikaendelea kusoma, niliangalia tarehe ya huo usiku wa ,maajabu, nikaona ni siku nyingi kidogo, sikutilia maanani sehemu hiyo,kwani huyo ni kijana ana mambo mengi, kuna mengi kaandika ya ajabu ajabu

Nikawa naendelea kusoma diary yangu,..nikafika sehemu nyingine anasema;

‘Hivi kijana kama mimi ninaweza kumpenda mwanamke aliyenizidi umri, ...mbona nimetokea kuwapenda wanawake wakubwa, na..wengine wake za watu...’aliandika akaachia hivyo, sikuelewa ana maana gani, inavyoonyesha ni kuwa alikuwa akiandika kwa kifupi-kifupi kwa lugha anayoelewa yeye mwenyewe....

Nikafika sehemu nyingine kaandika hivi,; mpendwa alinipigia simu, akaniambia kuwa ana mazungumzo muhimu na mimi,...sikupenda mambo yake, nahisi yatanipeleka kubaya, japokuwa namuonea huruma sana...mambo aliyofanyiwa na kaka mkubwa sio mazuri, ...kaka mkubwa hatari…’akaandika hivyo

-Kaka mkubwa ni nani, na mpendwa ni nani…hapo napo nikaweka alama ya kuuliza

‘Mpendwa hana raha, anasema kuna siri zimegundulikana zinamuweka pabaya, zikivuja yupo matatani, na kaka mkubwa anazifahamu, na kamtishia kuziweka hadharani, anaogopa, ananiomba ushauri...’akamalizia hivyo, na mimi hapo nikaanza kuvuta hisia za dhana, huenda ni….

‘Mpendwa kasema hawezi kuvumilia, inabidi afanye anavyotaka kaka mkubwa, lakini inamuuma sana, hana jinsi anakuwa kama mtumwa wa kuzalilika, na anaogopa kuwa itakuja kujulikana, na huenda ikaathiri na watu wengine ambao hakuataka kuwafanyia ubaya wowote....’akamaliza hivyo

‘Huyu mpendwa....’nikasema kimoyomoyo huku nikisoma maelezo mengine, ambayo aliendelea kuandika kifupi kifupi, nikafika sehemu anaelezea, alivyokutana na mpendwa, aliandika hivi;

‘Mpendwa anataka kuniingiza majaribuni,....anataka kufanya jambo ambalo mimi siliwezi, na anachotaka kutoka kwangu ni kikubwa sana, naogopa na sijui kama nitaweza kumtimizia malengo yake, sijui ana kusudia kufanya nini...mimi siwezi,...lakini sipendi kumkatalia...nampenda sana japo ni mkubwa kwangu...’akaweka alama za kuuliza

‘Mpendwa kanituma...sijui kama nitaweza, na kama nikiweza sijui kama nitashirikiana naye, na je ni nini lengo lake, na kwanini anapenda kunitumia mimi, na wakati huo huo mbele za watu anaonyesha kuwa ananichukia, ni kwanini....’akaachia hivyo

‘Mpendwa kanitosa, ...sijui kafanya nini, sijui anashirikiana na nani,...je anahusika, na kwanini hataki kuniambia ukweli...nitajitahidi nifahamu kulikoni...hata hivyo namuonea huruma sana,’akaachia hivyo.

Kuna mengi niliyasoma hapo, lakini hayakuwa na maana sasa, mimi nilikuwa nafuatilia, hayo ya mpendwa, kaka mkubwa, kaka…mengine ni ya kikazi,..na mihangaiko yake mingine….nikawa naruka hadi nikafika sehemu hii…

‘Kaka kaniita na kunitaka nimpeleke mahali,...mimi naogopa, maana hali yake bado ni tete, je anataka nini, ..nitafanya hivyo ili kutokumsababishia mambo mengine.’akaacha hivyo na hapo nikaangalia tarehe, ni siku ile ile aliyouwawa !!

Hapo nikatulia,… kumbe ni kweli, mume wangu alitoka na mdogo wake…!!

‘Ushahidi huu…lakini hauna mshiko…’nikasema na kuyakoza hayo maelezo.

‘Nikiwa njiani kaniambia anafuatilia maswala ya mkataba, na anasema mkataba ni mzuri wenye malengo mazuri, lakini mimi niliona ni dhuluma, hata hivyo kasema ni shinikizo la mkubwa,

-Huyu kaka mkubwa…atakuwa ni….nimeshampata. bado uhakika wa huyu mpendwa, hapa kuna watu wawili, nawashuku, rafiki yangu na mke wa docta

‘Kasema atatusaidia, na kwa vile anajua sheria, tumtegemee yeye...ila gharama zake ni kubwa sana, ..mimi sikubaliani na hilo,lakini kaka anasema hana jinsi ni lazima tukubaliane naye kwani kashika kaka mkubwa kashikilia mpini, swali la kujiuliza ni kwanini kaka anakubali kirahisi hivyo, mimi ninahisi kuna jambo jingine, ni lazima nilijue, ni jambo gani...’akachia hapo.

‘Wakati tunafika, nilimuona mpendwa akitoka kwa haraka yaonekana ana wasiwasi, nikajaribu kumfuatilia kwa macho, nikaona anaelekea uwanja wa ndege

-Anaelekea uwanja wa ndege…huyu atakuwa ni rafiki yangu!!

Mpendwa alikuwa akisafiri, sikuwa na haja naye,mawazo yalikuwa kwa kaka, kwanini kataka nimlete hapo,..na nilikumbuka maagizo ya mpendwa, na mzigo wake nilikuwa nao, alisema atasaidia kuzuia hayo kaka anayotaka kuyafanya....

‘Kaka yupo kwenye hali ngumu, anaonekana kabanwa na kaka mkubwa, inabidi akubali kusaini mkataba wenye mamlaka makubwa kwa kaka mkubwa...ina maana mwisho wa siku kila kitu kitachukuliwa na kaka mkubwa, sasa ina maana gani, na kwanini kaka anakubali kirahisi hivyo, mimi sikubali, ni lazima nimsaidie kaka...’

-Hapahapa….kumbe ndio maana dogo kakimbia..je alimsaidiaje kaka yake ngoja tuendelee…

‘Yote sasa yanategemea juhudi za mpendwa,..’nikawa najiuliza mbona nyuma kaandika kuwa mpendwa anasafiri, kamuona akitoka na mizigo, ...sasa vipi tena, hapo sikuelewa, huenda nitapata hayo majibu huko mbele, na wakati nataka kusoma zaidi mara simu yangu ikaita...

‘Aaa, ni nani huyu tena…’nikasema nikitizama namba ya huyo aliyepiga simu..

**********

Mpigaji kapiga kama mtu asiyejulikana, hakuna namba wala jina, ..hapo nikazima lap-top yangu haraka nikiwa na lengo la kuendelea kusoma baadaye, nikaweka mitambo yangu ya kurekodi sauti,

‘Nitasoma baadae…’nikasema ni kuiweka laptop pembeni,...

Nikaiweka simu hewani na kutulia kidogo ili mpigaji aanze yeye kuongea, na yeye akakaa kimiya, nikauliza;

‘Wewe ni nani?’ nikauliza

‘Mwambie kaka mimi nipo salama, nitakuja mambo yakiwa shwari,nafahamu umeshafahamu kuwa nipo kwenye matatizo, na kuhusu mengi uliyoniuliza, nafahamu hadi sasa umeshapata majibu yake, japokuwa nilivyoandika naelewa mimi mwenyewe, sina zaidi ya hayo, ninachokuomba ni kumlinda kaka yangu....hana hatia, ...’akasema

‘Upo wapi?’ nikauliza

‘Usitake kujua nipo wapi nipo popote pale, nafahamu huenda simu zangu zikawa zinafuatiliwa, lakini nakuhakikishia kuwa nipo salama, hawo watu hawawezi kufahamu mahali nilipo, na nikitoka hapa, sitapatikana tena, ..’akasema.

‘Usijidanganye, kwanini unakimbia, una kosa gani, rudi mimi nitakusaidia...’nikasema

‘Umeshindwa kumsaidia kaka, ndio utaweza kunisaidia mimi, ...ninachokuomba ni wewe umsaidie kaka yangu, yeye hajui lolote kuhusu hayo yaliyotokea zaidi ya kufuatilia mkataba wake na makabrasha na hata huo mkataba hana ufahamu mwingi wa kile kilichofanyika,..hata mimi sina uhakika ni nani aliyefanya hivyo, ..’ akasema

‘Huna uhakika wakati umeandika ni lazima umsaidie kaka yako kuhus mkataba ambao marehemu alishinikiza…ulimsaidiaje kaka yako, kama sio kumuua makabrasha..’nikasema

‘Mimi sijamuua Makabrasha na nisingelifanya hivyo, kwanini nimue, kumsaidia kaka nilichosema hapo ni kitu kingine kabisa…’akasema

‘Wewe si ndiye uliyeiba silaha, ukaipeleka wapi, kama sio kwenda kumuua Makabrasha..?’ nikamuuliza

‘Ni kweli silaha iliyotumika niliichukua mimi,..lakini sio mimi niliyeitumia hiyo silaha kumuua kaka mkubwa, .. mengine utayaona, humo humo, sijui kama yatakusaidia lolote,...tafadhali nakuomba ten asana, usije ukawapa hao watu hayo mambo yangu kwani kuna mambo yangu binafsi, ...’akakata simu.

*******

Niliangalia saa yangu huku nikiangalia ratiba ya wageni, wanaofika kwa ndege, na mimi nilikuwa nimekuja rasimi kumpokea mgeni wangu, japokuwa mgeni mwenyewe hakuwahi kuniambia nije kumpokea, na wala hafahamu kuwa mimi ndiye nimekuja kumpokea, lakini nina uhakika anafika leo.

Kufahamu siku ya kufika huyo mgeni ilitokea kama nadra tu, maana siku hiyo nilikwenda nyumbani anapoishi rafiki yangu, nikiwa na malengo ya kuhakiki uchunguzi wangu, kutokana na maelezo niliyoyasoma kwenye diary ya shemeji yangu.

Nilifika hapo alipokuwa akiishi rafiki yangu kabla hajaondoka, kusoma, yeye kabla ya kuondoka alikuwa akiishi na mwanadada mmoja, ambaye wana udugu fulani naye, japokuwa hawakuzaliwa tumbo moja, nilimkuta kwenye duka lake..nikaanza kumuongelesha,.

Mazungumzo yetu yalikuwa yakikatishwa mara kwa mara akitokea mteja..kuna muda alielekea uwani akaniacha hapo dukani, na simu yake ikaonyesha kuwa kuna ujumbe umeingia,,...nilikuwa karibu nayo, macho hayana pazia, sehemu ile ya ujumbe ilikuwa imefunguliwa, na ilikuwa rahisi kuona

Nilipotizama nikaona jina la rafiki yangu, na ujumbe huo unatoka kwake,…sio kawaida yangu, lakini hamasa ikanijia kuona ni ujumbe gani kautuma huyo rafiki yangu, ni kitu tu kilivuta kufanya hivyo, nikachukua simu hiyo na kuufungua huo ujumbe...

‘Ndugu yangu ninakuja kesho, nipokee uwanja wa ndege, nitafika huko usiku saa mbili, usimwambie mtu yoyote...’mwisho wa ujumbe

Nilipohakikisha kuwa ni huyo rafiki yangu, kwa kuangalia namba yake, nikaufuta ule ujumbe, nikahakikisha haupo kwenye sehemu yoyote kwenye ile simu, halafu nikairudisha ile simu pale pale, na mara akaingia huyo mwenyeji wangu.

‘Nilisikia kama mlio wa ujumbe wa simu…sijui ni nani huyo tena, mimi sasa hivii nataka pesa, sio madeni...’ akasema huku akiangalia simu yake, na alipoona hakuna ujumbe akaniangalia na kuniuliza.

‘Au ni simu yako nini, …, maana nina uhakika kuna mlio wa ujumbe wa maneno, wa simu nimeusikia, na hapa kwangu hakuna ujumbe ulioingia?’ akauliza huku akiiweka simu yake pale alipoiweka awali.

‘Ndio kuna ujumbe umeingia kwenye simu yangu, huenda ndio uliousikia, naona una kazi nyingi, ngoja mimi niondoke, nitakuja wakati mwingine,...’nikasema

‘Hapana usiondoke kwanza…, mimi siku zote nipo hivi hivi, siunajua shughuli zenyewe zilivyo hapa, hata akija mgeni tunaongea hivi hivi,hebu niambie ni kitu gani ulikuja kuniuliza umesema unataka kuniuliza kitu...’akasema

‘Nilitaka kufahamu ni lini rafiki yangu anakuja, shoga yako...’nikasema

‘Alisema atanifahamisha leo, ndio nasubiria simu yake au ujumbe wa maneno kutoka kwake,, kwahiyo kifupi..sina uhakika ni lini hasa, unamfahamu zake, yule ni shushu wa kimataifa umemjenga wewe mwenyewe, au umesahau…’akasema

‘Sijasahau..ila nashangaa alikuambiaje hayo…’nikasema

‘Aliniambiaje..wakati unafahamu mimi na yeye nikitu kimoja, kazi zake nyingi alikuwa akitumia mimi..mimi ni mtoto wa mujini.....’akasema.

‘Hamna shida,...kama ningelifahamu ni lini anakuja ningeenda mwenyewe kumpokea, ..’nikasema

‘Mhh, mara nyingi hapendi mtu mwingine kumpokea, ni mimi tu...sijui kwanini, nashangaa hata wewe hakuambii, wakati wewe ni rafiki yake mkubwa..’akasema

‘Kila mtu ana hulka zake....labda ana maana yake, lakini ni safari hii tu, wala usijali hilo...’nikasema

‘Nina hamu sana ya kumuona mtoto wake, maana alivyo mzuri,...na hakutaka kabisa watu wamuone, mimi nilibahatika tu kwa vile alikuwa yupo hapa kwangu, tena nilimuona kwa kujiiba, hakutaka hata mimi nimuone...’akaanza kujileta mwenyewe, maana lengo la kuja kwangu hapo likuwa ni hilo.

‘Kwanini alikuwa akifanya hivyo, hata wewe hakutaka umuone, naona ajabu sana...?’ nikauliza.

‘Ni kujihami tu, maana ananifahamu nilivyo,..na atamficha nani bwana, mtoto yupo hapa, analala hapa, …hahaha, mjinga kweli yule..lakini siwezi kumlaumu ....’akasema

‘Mhh, kwani ulivyomuona mtoto wake anafanana na nani?’ nikajikuta nikimuuliza hivyo

‘Mhh, tatizo ni kuwa watoto wadogo wote hufanana, mimi nilimuona kama anafanana na watoto wako...yaani kabisa, utafikiri baba yao ni mmoja, ...’akasema

‘Labda baba yao ni mmoja, huwezi jua...’nikasema

‘Hapana, hawezi kufanya hivyo, japokuwa mmmh,....mume wako naye, mambo yake ya chini kwa chini, samba mwenda kimia, utafikiri muaminifu fulani, kumbe..watu wapole waogope....’akabenua mdomo nikajua kuna umbea hapo unataka kutembea, nikauliza

‘Kwanini unasema hivyo?’ nikauliza

‘Hata mimi ipo siku alinijia, akaanza zake, sikuamini, nikamtolea nje, hahaha, usije kumuambia , mdomo wangu huu…lakini ndio hivyo wanaume wengi wapo hivyo..’akasema

‘Kwahiyo alikutongoza?’ nikamuuliza

‘Hahaha, acha wivu bwana,mbona ni kawaida tu, ya wanaume au sio, na mwanamke usipokuwa mjanga unaingia kingi,…lakini sio mimi,..huwa nakuheshimu sana wewe, na kumuheshimu rafiki yako, vinginevyo, ....utajiri wake tungegawana, hahaha, mjini hapa....’akasema.

‘Ungefanya nini, kwani kutembea na mtu ni lazima magawane utajiri? Nikaanza kumdadisi

‘Sisi ambao hatuna waume, tunafahamu sana mambo mengi, kuliko nyie mliopo kwenye ndoa, hasa mimi ambaye nilionja ndoa nikaachika, nafahamu jinsi gani ya kumchuna mwanaume,...hasa akiwa ana pesa, na mimi nilivyo, hawezi mume wa mtu aje kwangu nimkaribishe bure bure tu…, hasa akiwa tajiri, nitahakikisha anakung’uta mfuko wake..wengi wananifahamu,....’akasema.

‘Kwahiyo wewe na shoga yako ndio tabia zenu hizo, ndio maana kaamua kuniingilia na mimi kwa mume wangu?’ nikamuuliza

‘Nini..! Hapana bwana, hilo sio kweli, japokuwa sina uhakika, maana wewe nay eye ni kama mtu na ndugu yeake, ungelisema mimi bora, mimi na wewe wapi na wapi.. kama kafanya hivyo, nitamshangaa sana…’akasema

‘Ndio kafanya ushahidi si unajionyesha , hata na wewe unafahamu ila unataka kumlinda rafiki yako…’nikasema

‘Kiukweli hilo mimi sijui.., maana yule ni sawa na mdogo wako,...lakini dunia hii ina mengi, huenda walipokuwa huko wakilewa, yaliwashinda, na kwa vile mume wako anaonekana ana njaa-njaa hivi .....hahaha, nisikuumize bure’akaanza kucheka, na mimi nikamuuliza.

‘Ulijuaje kuwa mume wangu ana njaa?’ nikamuuliza

‘Mwanaume mwenye njaa, utamfahamu tu, sisi tunafahamu ...mimi niliachana na mume wangu kwa mambo hayo hayo...na sitaki kuolewa tena, maana kuna wanaume hawashibi,...hata uwafanyie nini....sasa niliona nimpe nafasi hiyo, atembee kila nyumba ale weeeh, akishiba ndio atatulia, ataoa, lakini sio aje kunioa mimi tena, maana hata mimi sasa sishibi, bado nadai...’akasema.

‘Je mume wangu aliwahi kukuambia hivyo, kuwa hashibi?’ nikamuuliza

‘Sijawahi kumpa nafsi ya kuongea namimi kihivyo, maana simuhitaji, nakuheshimu, nawaheshimu watu wake...sikutaka tu, lakini kama ningelitaka ningempata tu na kama angeliingia anga zangu, nina uhakika angening’ang’ania kama ruba hahaha nakutania tu wewe bwana, mimi naongea sana…’akasema lakini hakujua mimi nimeshaumia tayari.

‘Mhh..’nikasema hivyo

‘Kiukweli ndio hivyo, ....nakuheshimu wewe tu....siwezi kukuvunjia heshima yako, unafahamu mimi nakujali sana, umenisaidia mambo mengi, na siwezi hata siku moja kukuvunjia heshima yako...’akasema.

‘Nashukuru kusikia hivyo, angalau wewe umeniambia ukweli...na je ulishawahi kumuona shemeji yangu hivi karibuni?’ nikamuuliza

‘Shemeji yako!!? Una maana huyo mdogo wa mume wako, huyu kikaragosi wa humu humu mjini, kuacha yule mwingine ambaya hakai sana hapa Dar, au sio..kama ni huyo kuwadi, mbona yupo tu, kwani kaenda wapi…?’ akauliza

‘Ndio...mimi sijui kama anasifa hizo zote.’nikasema

‘Jana tu nilikuwa naye hapa nyumbani...’akasema

‘Jana!!!?…sio kweli…ina maana bado yupo hapa Dar,...?’ nikauliza kwa mshangao.

‘Angeenda wapi yule, yule ni mtoto wa mjini bwana,...ni mjanja hutaamini, namtumia sana kwenye biashara zangu, ananitafutia wateja wa hapa na pale, ninachomsifia kijana huyo, yeye ni mwaminifu sana, haongezi cha juu kikibwa…, akipata pesa zangu ananiletea, sina wasiwasi naye...’akasema

‘Lini anatarajia kuja hapa kwako tena?’ nikamuuliza

‘Hilo sina uhakika, .....huwa kama kuna mteja wangu anamfahamu, na nikamtuma kuniletea pesa zangu, ndio anafika, na wakati mwingine alikuwa akifika kama katumwa na kaka yake kukutana na mwenzake hapa.....’akasema.

‘Mwenzake ndio nani huyo?’ nikamuuliza

‘Wewe sasa wataka kunichimba, usije kunichonganisha, mengine naonega tu, ukiyachukulia yote kuwa ni sahihi, utavunja ndoa yako shauri lako,…na kiukweli maisha ndivyo yalivyo, tatizo nyie mlioolewa mnataka kushiba wenyewe tu, sasa sisi tutakula wapi, hamtuonei huruma jamani…, mjini hapa , tutabanana kiaina ....heheheeee’akasema huku akicheka kile kicheko cha akina dada

‘Ina maana , kumbe hapo kwako ndio makutano yao...’nikasema

‘Hayo sijakuambia mimi, usije ukaniletea kesi, aaah, mimi hayo siyajui,....ngoja nisije kuitwa mbeya,akija mwenywe umuulize…, hivi nikuulize, toka lini, fisi na mbuzi watakuwa wakitembea na kukaa pamoja muda wote, wasitafunane, nani kakudanganya, shemeji shemeji..hahaha, tutaona mengi mwaka huu....,’akasema

‘Sawa nimekuelewa,…lakini nataka ukweli, hili swali nataka ukweli wako , je ni kweli mume wangu na rafiki yangu walikuwa wakikutania hapa kwako..?’ nikauliza

‘Rafiki yangu rafiki yangu…siwezi kukata kuwa alikuwa ni rafiki yako..lakini kwa haya mambo hakuna rafiki wa kweli au sio, basi kama ni rafiki wako wa kweli kweli, basi ukubali na kile kizuri chako mgawane kuba ubaya gani hapo…hahaha, hapana bwana kukutana kwako ilikuwa kikazi zaidi…usinielewe vibaya..’akasema sasa akiongea kidhamira

‘Niambie ukweli, maana wewe ni mtu wangu, je ni kweli ndugu yako alikuwa na mafungamano ya ukaribu na mume wangu,..na walikuwa wakikutana hapa kwako..naomba unitonye, unajua jinsi gani nitakulipa kwa ukweli huo..?’ nikamuuliza nikionyesha hasira

‘Hahahaha...acha wivu bwana, nikuambie ukweli shoga yangu, usihangaike na wanaume, wanaume ni kama kuku wa kienyeji, kila anayekutana naye, ni wake...ukiwachunguza sana, utakufa kabla muda sio wako...akiwa kwako ni wako, akitoka nje ni wakila mtu,….jibu la swali lako, sio kweli, na mimi sijui, mengi hapa nilikuwa naongea tu, akili kicwani mwako...’akasema

‘Ushahidi si upo..nakupima tu kama kweli unanijali, kama ulivyosema awali, na kama utanificha nikagundua, unajua hatutaelewana tena…’nikasema

‘Nikuambie shoga, ...hiyo iweke moyoni, mume hana mke akiwa nje, ...na wewe ukiweza fanya hivyo hivyo, usiumize kichwa chako, kwanza wewe unashida gani, pesa unazo, tajiri, kwanini uumize kichwa chako….’akasema sasa akiniangalia kwa makini usoni.

‘Tatizo wewe haupo kwenye ndoa, huwezi kufahamu machungu ya tabia hizo,…’nikasema

‘Nafahamu sana..niliolewa nikaachika, baada ya tukio, hilo, hata kama nitaolewa tena, mimi sijali..yeye afanye atakavyo na mimi nitafanya nitakavyo, tusiulizane, na akitaka tuwe waaminifu kwenye ndoa, nitafanya hivyo, lakini asinidanganye…huo ndio msimamo wangu…’akasema

‘Haya bwana endelea na biashara zako nashukuru…’nikasema na kuachana na huyo mdada, anayeongea kama redio iliyowashwa.

Kiukweli nilitoka hapo nikiwa nimeumia sana, japokuwa maneno mengi ya huyo mdada sio ya kuaminika, lakini hadi hapo nilishakuwa na uhakika kuwa mume wangu na rafiki yangu, walikuwa wakinisaliti.

*******

‘Ndege inayotoka Ulaya inaingia.....’sauti ya mtu aliyekuwa karibu na nilipokuwa nimekaa akasema na kunikatiza kwenye dimbwi la mawazo, na mimi kwa haraka nikasimama na kuelekea sehemu ya kupokelea wageni, nikiwa na hamu sana ya kumpokea mgeni wangu, ..

Nilikumbuka nilipoongea na wale mabaunsa ambao nilishapanga nao, nia ni kukomesha watu wenye tabia mbaya, wanawake wanaotembea na waume za watu, hao ndio kazi yao, ukiwalipa tu watakufanyia jambo unalolitaka.

‘Hii kazi nataka muifanye iwe ni fundisho, lakini sitaki iwe ni mauaji, sitaki kumuua mtu, mumenielewa....’ niliwaambia.

‘Sisi tunakusikiliza wewe, utakavyo, kama unataka vipi na vipi, na kama unataka turekodi na kanda kabisa ya video tutafanya hivyo, ili uhakikishe mwenyewe tulichokifanya, muhimu ni pesa tu..,....’ wakasema.

‘Pesa sio tatizo, muhimu hiyo kazi ifanyike kwanza..’nikasema

‘Dada wewe mwenyewe utasikia kwenye bomba, sisi hiyo kazi sio mara ya kwanza kuifanya, watu kama hawo ni lazima tuwafundishe adabu, ...tuna jinsi zetu za kuwawezea, hata awe mjanja vipi, ...tukimalizana naye, atakimbia huu mji kama ataweza kuhimili mambo yetu na wengi tuliowafanyia hivyo, walikimbilia kunywa sumu...’akasema huyo kiongozi wao

‘Mimi sitaki mumuue, mumesikia, nataka atie adabu, akione cha moto,..’nikasema.

‘Hatumui mtu sisi…, kama ni kujiua atajiua yeye mwenyewe,…na mambo ya polisi usiwe na shaka nayo, hao ni jamaa zetu, kwani wanafahamu tunalolifanya, ni kuwatia adabu watu kama hao,..si ndio wanachokitaka kwa waume za watu, au sio..ngoja uone kazi yetu ndio utatuambia.....’wakasema.

‘Mkimaliza kazi, pesa yenu mtapata, huyu mtu anatarajia kufika leo toka Ulaya, nitawaelekeza wapi pa kukutana naye, mengine mnajua nyie wenyewe,....’nikasema.

‘Sawa tunasubiri taarifa kutoka kwako....usituvunge tena kama kipindi kile, ulituambia tukasubiria lakini hukutuambia ni nani…utatulipa waiting charges..’akasema huyo kiongozi wao.

‘Msijali safari hii mtapata kazi, kaeni mkao wa kula…’nikaachana nao hivyo

***********

Mara abiria kutoka ulaya wakaanza kuingia, na mmoja mmoja akawa anapita sehemu ya kukaguliwa mzigo wake, na kutoka nje, na mgeni wangu akawa haonekani, nikahisi huenda kaahirisha safari ya kuja huku, lakini mwishoni nikamuona mgeni wangu akitokea na mtoto wake..

Kwa jinsi nilivyomuona yaonekana mtoto wake alikuwa akimsumbua, akafika sehemu ya kukaguliwa mizigo, akachukua mabegi yake, yalikuwa mawili makubwa, na wakawa wanazozana na mkaguzi , huyo mkaguzi alikuwa akidai pesa, yaonekana yale mabegi yalizidi uzito...

Mimi nikasogea karibu kiasi cha kuweza kuongea na yule mkaguzi…, japokuwa tulikuwa kwa nje na wao wako kwa ndani, isingeliruhusiwa mimi kama mpokeaji kuingia sehemu ile ya ndani, nikauliza;

‘Kiasi gani unadai kwa huo uzito ulizidi?’ nikauliza na yule mkaguzi akataja, nikampa pesa yake, na rafiki yangu akaruhusiwa kutoka, na mizigo yake, alionekana kushangaa sana kuniona , na hakusema kitu kwa wakati ule hadi mizigo yake ilipotolewa nje, na mimi nikamwambia.

‘Karibu bongo..’nikasema na yeye akatabasamu kidogo, halafu akauliza

‘Umekuja kumpokea nani?’ akauliza

‘Nimekuja kukupokea wewe, au huoni....’nikasema

‘Ulijuaje kuwa nafika leo?’ akauliza kwa mshangao

‘Wewe ni mfanyakazi wangu au umesahau, umeenda kusoma kwa kibali changu, hata kaam ulikuja kubadili baadae, isitoshe wewe ni rafiki yangu, nimeishi na wewe na kujitolea kukusaidia kama mdogo wangu, na zaidi ya hayo nasikia kuwa wewe ni mke mwenza,..au nyumba ndogo, kwanini nisihindwe kufahamu lini unafika,....’nikasema na yeye akaguna na kusema;

‘Mhh, imekuwa hayo, mbona unanitisha, hata hivyo nashukuru kwa kuja kunipokea, lakini kuna ndugu yangu anakuja kunipokea, nilimtumia ujumbe tatizo nay eye ana mambo mengi sana, huenda kasahau, naomba simu yako mara moja...’akasema

‘Ndugu yako hatafika, nimefika mimi badili yake, yeye ana kazi zake za kumalizia, hakuna shida, nipo hapa kwa ajili yako, na nitahakikisha unafika kunapohusika, unakumbuka ahadi yangu?’ nikamuuliza

‘Ahadi gani?’ akauliza na mimi nikatabasamu, huku nikiwaonyesha wabeba mizigo wapi gari langu lipo, nikasema;

‘Gari langu lipo tayari, mimi nimeona ni muhimu nikuwahi mapema, maana ahadi ni deni, au sio..., ....’nikasema

‘Ahadi gani mbona sikuelewi, ...’akasema huku akiwa kasimama,

‘Twende bwana,...unaifahamu sana hiyo ahadi, unaijua sana,’nikasema na yeye akawa hasogei pale aliposimama, halafu akasema ;

‘Mimi siondoki na wewe, nitaondoka kwa taksi, naona una lako jambo,...kauli yako inanitisha’akasema

‘Usipoondoka na mimi , utaondoka na polisi, ukumbuke siku Makabrasha anauwawa, ulikuwepo, umesahau eeh,..’nikasema na aliposikia hivyo akashituka, na kuniangalia kwa mshangao, akasema

‘Mhh, hayo sasa makubwa, ni nani kanivumishia huo uwongo,mimi niliondoka akiwa hai, taarifa za kifo chake nimezipata wakati nimeshafika Ulaya...’akasema

‘Tutaongea ndani ya gari, twende zetu...’akaanza kutembea kuelekea kwenye gari langu, na mizigo yake ikawekwa nyuma kwenye buti la gari yangu, na yeye akaingia kwenye gari moyoni nikasema;

‘Bado mmoja....wewe sasa umeshaingia kwenye mitego yangu, ...’nikasema kimoyo moyo. Kabla sijaingia kwenye gari nikainua simu na kuwapigia watu;

‘Muwe tayari, ....keshafika, nitawaambia ni nani, tukifika kwao, fuatilieni gari langu, nitapitia ile njia niliyowaelekeza, mengine mtajua nyie....’nikasema.

‘Sisi tupo tayari bosi....’wakasema

Nikaingia kwenye gari na kuanza kuondoka

NB: Je hayo yatafanyika, itakuwaje, tuzidi kuwemo,



WAZO LA LEO: Tuweni makini sana, kwenye maswala ya kulipizana visasi, tunapofanyiwa mabaya, na kutamani kulipiza kisasi, japokuwa mengine yanauma sana. Kabla ya kuingia kwenye hasira hizo,.. kwanza tuwe na subira, tuhakiki huo ubaya,tukimtegemea mungu, kwani huenda ubaya huo ulikuwa kwa masilahi yako, au wewe ndiye chanzo cha ubaya huo, unaweza ukalipiza kisasi ikawa ni matatizo kwako, na kile kisasi kikawa ni kidogo, kuliko mabaya utakayokuja kukumbana nayo mebeleni, na majuto ikawa ni mjukuu.
 
SEHEMU YA 89

Nilimfikisha rafiki yangu nyumbani kwao, na akapokelewa na shoga yake, na sikutaka kuongea nao zaidi nikaondoka, kwani ilikuwa ni usiku, na nilikuwa na hasira kweli kweli...na wakati natoka hapo, mara, akakatiza mtu mbele ya gari, nikafunga breki

'Wewe vipi...?' nikafoka

Na mara huyo mtu akasogea kwenye kiyoo cha gari, akaashiria nishushe kiyoo, kwanza nilihofia, sikusha,..akasogea karibu kiasi cha suti kusikika;

‘Usije ukatutosa tena bosi, kesho tunakuja kuchukua pesa zetu....tutakuwa tumeshamaliza kazi...tunasubiria muda muafaka, kama umebadili nia utuambie haraka, maana muda ukifika hakuna kurudi nyuma...na ukighairi bado kuna gharama zetu ni lazima utulipe..’akasema

Mimi pale sikusema kitu!

Tuendelee na kisa chetu

**************

Wakati naendesha gari, kurudi nyumbani kwangu, nilianza kuwaza hicho niichokusudia kifanyike, hapo hapo huruma ikaanza kunijia, nikikumbuka jinsi gani nilivyohadithiwa na mmoja wa watu waliowahi kushuhudia ndugu yao aliyewahi kufanyiwa hivyo, ni ukatili wa hali ya juu, alisema ndugu yao alishindwa kuvumilia, haikupita muda ndugu yao huyo akajiua.

‘Ina maana mimi nimekuwa na roho mbaya kiasi hicho, japokuwa rafiki yangu amenifanyia huo ubaya, lakini sio vyema, kumtendea hayo, huo utakuwa ni ukatili wa hali ya juu, mbona nimechukua mambo kihasira zaidi, ina maana ubaya nalipiza kwa ubaya wa kiasi hicho, ..kwanza huyo ni mama mtoto , analea, je hicho kitoto kitalelewa nani...’nikajiuliza

‘Ndio labda, nitamchukua mimi, na kumlea kama mtoto wangu,....lakini kila nitakapomuona huyo mtoto nitakumbuka huo ukatili...mmh, hapana...lazima nifikiriz zaidi hili...’nikawa nawaza kichwani huku naelekea kwangu na muda unazidi kwenda.

Kabla sijafika nyumbani ndio nikakumbuka mazungumzo yangu na rafiki yangu huyo tukiwa ndani ya gari;

'Vipi khali ya mtoto, mbona amekuwa mzungu, umemfanya nini mtoto...?' nikamuuliza nilipotupia jicho kwa mtoto, na haraka akamfunika

'Ni fasheni tu, na kuogopa vijicho cya watu...'akasema

'Siku hizi umekuwa mshirikina..?' nikauliza

'Sio wa kikwetu, huo ni wa kitaalamu, ...sitaki watu wamfahamu mtoto wangu alivyo, najua fitina ni nyingi sana, ambazo hazina ukweli...'akasema

'Zina ukweli, ila unauogopa huo ukweli, au sio, kwa vile umevuka mpaka..'nikasema

'Sawa...nitasema nini tena..ila kwa vile nimerudi tutamalizana na wote wanye kutaka ukweli, na sina shaka juu ya hilo...'akasema

'Haya, ila jiandae pia kuachana na huyo mtoto..'nikasema

'Kwanini...?' akauliza

'Unajua ni kwanini, ahadi ni deni, nilishawahi kukuambia kabla, kuwa dhamira yangu ni ile ile..'nikasema

'Sijakuelewa...'akasema

'Utaelewa tu muda ukifika, sizani kama wewe ni jasiri kiasi hicho, wapo mjasiri lakini walishindwa, ogopa sana macho ya watu, ogopa sana watu wakikunyoshea vidole kwa kashafa ya udalilishwaji..'nikasema

‘Huyu mtoto ndiye jicho langu, sitakubali kuachana naye hata siku moja, na hao watakaotaka kufanya hilo, wajiandae pia, maana mimi sio yule wa jana...’alisema kwa kujiamini

'Hahaha, ina maana unajiamini kiasi hicho,..hata baada ya hayo madhambi, badala ya kutubu, ..'nikasema

'Sawa nilitenda madhambi, lakini kwa misingi ya kukubaliana, sikujipeleka mwenyewe, sikulazimisha, na huenda yaliyotokea yalikuwa sio lengo langu, ..lakini ufanyeje na imeshatokea, muhimu ni huyu kiumbe asiye na hatia, nitampigania hadi tone la mwisho..'akasema

‘Hivi hata kama baba yake akimtaka, akaishi naye, kwani labda utakwua kwenye hali mbaya, utamkatalia?’ nikamuuliza.

‘Kwa misingi ipi, kwani mimi nimekufa, au sina uwezi wa kumlea..na hali mbaya gani hiyo ya kunifanya nishindwe kumlea mtoto wangu...hapana hilo halipo..’akasema.

‘Baba yake ana haki na mtoto wake pia au sio...’nikasema.

‘Hata mimi nina haki na mtoto wangu, hilo sikubaliani nalo hata siku moja, kwasabbu mimi mwenyewe nina uwezo wa kumlea, kwanini huyo anayejiita baba aje kumdai mtoto wangu, kwani tuliahidiana hivyo, sikuahidiana na mtu kuwa tuzae halafu mtoto awe wetu sote, hali halipo...’akasema.

‘Lakini wakija na hoja kuwa wanamtaka huyo mtoto, wamlee, ikizingatiwa kuwa huyo baba mtoto ana mke wake, na mke wake yupo tayari kuishi na huyo mtoto, utakataa?’ nikamuuliza.

‘Kwanini lakini...sijasema siwezi kumlea mtoto wangu,...aah, hebu kwanza maana nina mengi ya kufikiria, nimesharudi nahitajia muda wa kutafakari mengi kabla sijaanza kupambana na uhalisia, najua hata wewe unanihitajia sana ...lakini naomba muda kidogo...'akasema

'Muda utaupata tu...na huenda ukiwa umelala kitandani, hujiwezi,...'nikasema

'Mhh...maneno yako yananitisha sana...'akasema

'Dada yangu, bosi wangu...mimi sina cha kuongea kwa leo, sikujiandaa kwa hilo,.ila kwa hilo la mtoto na huyo anayejiita baba yake, kauli yangu ipo wazi, kuwa huyu mtoto sitaachana naye kamwe,labda mimi niwe maiti...’akasema.

‘Hujaniambia kwa kauli yako ni nani baba wa huyo mtoto ni nani,...?' nikamuuliza

'Kifupi hana baba...'akasema

'Au unaogopa kwa vile ni mume wangu kama inavyojulikana na wengi, maana nimeshayafahamu yoye hayo, na wapi mlipokuwa mkikitania?’ nikamuuliza

‘Waache watu waseme wapendavyo, lakini anayefahamu ukweli wa yote ni mimi mwenyewe, na ukweli huo hautabadilika kwa maneno ya watu..kwa vile hata mimi nina ushahidi wa kitaaamu, nina kila namna ya kujilinda..'akasema

'Ushahidi gani zaidi ya DNA, au umegushi hata hiyo, hata ukigushi tutapima tena na tena..'nikasema

'Kwanini tufanye hivyo, nikitaka nini sasa....?' akauliza

'Mume wangu anamuhitajia mtoto wake, ..hapo alipo hana amani, na ikizingatiwa ni mtoto wa kiume, anamuota na kuchanganyikiwa kwa ajili hiyo, hujui jinsi ani mume wangu aliposikia una mtoto wake wa kiume alivyofurahia...'nikasema

'Huyo shemeji, akiwa hivyo basi hana akili...'akasema

'Kwanini...?' nikauliza

'Wewe hujui jinsi gani niivyotaabika na huyo mume wako, hujui tu, vinginevyo angeliishia kutembea na changudoa, lakini nilimsitiri, na kumlinda ili aendelee kuitunza ndoa yake, lakini hayo hutanielewa kwa sasa nitakuja kukusimulia yote, nipe muda nipumzish kichwa, na kukusanya ushahidi wote..’akasema

‘Hahaha, yaani unajisifia kuwa uliweza kuhangaika naye, kuzini na mume wa mtu huoni ni kosa kubwa, au ulimsitirije...?' nikauliza

'Nitakuja kukuelezea...'akasema

'Vyovyote iwavyo, zinaa, na kutembea na mume wa mtu ni dhambi kweli si kweli..?' nikauliza

'Uliyajua hayo sio..sasa hivi unayajua hayo, umesahau eeh...kuwa wewe ndiye uliyenishauri nikazini, nitembee na hata mume wa mtu...'akasema kwa hasira.

'Hahaha...kwahiyo ukataka kunikomoa, au sio...na hata wakati nakushauri hivyo mlishakuwa na mahusioano wewe ulitaka upate mwanya tu wa kuyafanikisha hayo, mimi sikujua lengo lako ni nini,..na ushahidi upo...'nikasema

'Mhh..kichwa kimechoka jamani..'akasema

'Utapumzika tu..japo sijui., sasa kwa kumbukumbu maana huenda huko tunapokwenda tunaweza tusipate muda wa kuongea hivi tena, hebu niambie huo mkataba wa bandia mlioutengeneza, na Marehemu, lengo lenu ilikuwa ni nini, kulinda haki za mtoto, au kutaka mali, angalia mwenzko alikuwa na tamaa hiyo sasa yupo wapi..?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui lolote kuhusu huo mkataba, hayo ni ya kwao, mimi nina maisha yangu ya kujitegemea mimi mwenyewe sijawa kilema,..ni wao tu walinilazimsha kuweka sahihi, na wakati kaam ule sikuwa na jinsi,na sijakaa na kuliwazia hio...'akasema

'Sasa unavyosema kuwa una kila namna ya kujilinda una maana gani..?' nikauliza

'Mimi nazungumza maswala ya kitaalamu, kuhusu mtoto wangu,...kuwa hana baba,kama wanavyodai watu, na nitalithibistiha hilo hata mbele ya mahakama, huyu ni mtoto wangu mwenyewe....’akasema

‘Kwa vipi,...huwezi kuzaa mwenyewe, hukupandikizwa mbegu, wewe ulizini na waume za watu, ndio ukazaa, na huyo mwanaume ni mume wangu, hata kama ulizini na wengine, lakini aliyewezesha wewe kupata mimba ni mume wangu, kwei si kweli...?’ nikamuuiza.

‘Kuzini ni kitu kingine, wangapi wanazini na hawapati mimba,...sitaki kuyaongelea hayo zaidi maana hutanielewa, maana kwa hivi sasa huwezi hata kukumbuka kuwa wewe ndiye uliyekuwa mshauri wangu mkuu, mimi sikuwa na wazo hilo kabla, sikuwa na tabia ya kutembea na waume za watu kabla,..'akasema

'Hahaha, hiyo ni kauli ya kujitetea, wakati mlikuwa mkikutana kwa rafiki yako, ndio ilikuwa makao makuu yenu, mkisingizia mnaongea mambo ya kikazi, au umesahau,...'nikasema

'Haina ukweli kabisa hiyo,..mimi nilianza kutembea na waume za watu baada ya wewe kunishauri, nafahamu hutanielewa, na sina njia nyingine ya kukuelewesha, kwasasa,...sina zaidi, naomba tusiongee, tutakuja kuyaongea siku nyingine....’akasema

‘Hamna shida...lakini kiukwei, sitakuja kukuelewa kamwe, mimi siwezi nikawa mjinga kiasi hicho, eti nikushauri ukazini na mume wangu halafu, halafu kitendo hicho hujafanya mara moja, ungelisingizia kuwa ni bahati mbaye, mlikuwa mumelewa, kumbe kila siku ndio ilikuwa kazi yenu...’nikasema.

‘Wewe hujui tu, ...usilolijua ni sawa na usiku wa giza, ...’akasema.

‘Ndio siwezi kukuelewa, hakuna sababu ya msingi ya kuzini na mume wa mtu, tena mume wa rafiki yako, rafiki yako unayemtambua kama dada yako, anayekuamini..mpaka sasa akili yangu inashindwa kuamini kama kweli wewe ulifanya hivyo,huna sababu ya kusamehewa, ..’nikasema na kumwangalia, alikuwa kakunja uso na kushika kichwa kuonyesha kukerwa na hayo ninayoongea.

‘Naomba tuyaache hayo mazungumzo dada maana hayana ukweli..yananitesa sana moyo wangu, na kwa vile, nimesharudi ngoja nipate muda, nitakuambia ukweli ulivyokuwa,..lakini kwa sasa naomba uniache, sina cha kuongea zaidi...’akasema

‘Haya mimi naisubiri hiyo siku kwa hamu, maana umeshaniahidi mara nyingi kuwa utaniambia, sasa umerudi, sasa utausema hata ukiwa hao kitandani,...nataka kusikia huo utumbo wako, wa kujiidhinishia madhambi yenu, mimi nilichotaka ni kauli yako tu, kuwa kweli ulizini na mume wangu, ungeisema hapa, ningeshamalizana na wewe,...'unasikia

'Sawa nimesikia, na siwezi kusema uwongo..'akasema

'Ilimradi umekubali kuwa ulizini na mume wangu, hiyo inatosha... inatosha kabisa...asante sana.’nikasema

'Sijakubaliana na hilo..lakini subiria...'akasema na mimi nikaka kimiya,kwani hata mimi niikuwa na mawazo yangu kichwani, na hasira nilizokuwa nazo zilikuwa kubwa sana, kwahiyo tukawa tupo kimiya hadi tunafika.



*******

‘Je ni haki kumufanyia huyo mama wa mtoto hayo ninayotaka kuyafanya, akili yangu hakukubaliana na huo uamuzi, niliingiwa na wasiwasi, nikawa na mawazo mengine kuwa niwazuie wasiendelee na hilo zoezi, kwani kama walivyosema, vitendo watakavyomfanyia vinaweza kumuua, na hata kama hatakufa hapo, lakini anaweza kuja kujiua mwenyewe

Nikaamua kuwapigia simu ili wasitishe hilo zoezi, lakini simu zao zikawa hazipatikani, nikaamua kumpigia simu huyo rafiki yangu, ambaye alipokea simu yangu halafu aliposikia sauti yangu, akakata simu.

Muda ukawa unakwenda na na sikujua kabisa nifanye nini, maana muda huo ni usiku, na nisingeliweza kurudi kule kwa rafiki yangu, mara simu ikalia, nilipoangalia mpigaji nikaona ni baba yangu;

‘Baba mbona simu usiku-usiku..?’ nikauliza baada ya kusalimia

‘Je kikao cha kesho kipo , kama ulivyotaka?’ akaniuliza

‘Ndio baba nimeamua iwe hivyo, ..’nikasema, maana nilipanga kuwa , tuwe na kikao cha pamoja, kikiwahusisha wazazi wangu. Niitaka kikao hicho kiwe cha hitimisho ya hayo yote, ili hukumu itolewe na kila aliyehusika awajibike.

‘Basi itakuwa vizuri, na uwe na ushaidi wote, kwani sisi hatutaweza kuvumilia hayo yanayotokea kwenye familia yako, nilishakuambia kuwa mimi sitaki kashifa, sasa hicho kinachoendelea hapo kwenu kinaniharibia jina langu...unalifahamu hilo, na mpinzani wangu wa kisiasa anazidi kuwa juu yangu,..nikikosa kuchaguliwa safari hii, sitawasamehe..je una kila kitu?’akaniuliza

‘Kwanini unasema hivyo baba, kwani kuna nini kimetokea huko kwako…kwasabau hayo yote hayana ukweli, zaidi ya kashfa za kupandikiziwa?’ nikamuuliza

‘Jana Askari walifika hapa kwangu na kunihoji, ...wanahisi kuna uwezekano mkubwa kuwa mume wako kahusika kwenye mauaji ya Makabrasha, na wanayo ushahid wa kutosha, na kwanini waje kwangu badala ya kumkabili mume wako, unaona jinsi wanavyopanga mambo..’akasema

‘Na hapo najiuliza kwanini waje kwako, ungewauliza na kuwaambia utalichukulia kisheria zaidi ili waogope..?’ nikauliza

‘Kwasababu wanatumiwa na mpinzani wangu, sio kwa kuwatuma lakini mpinzani wangu anapandikiza fitina na askari kadi yao ni kuhakika ukweli,..na zaidi wameniuliza mahusiano ya kampuni zangu za zako, na kwanini kulionekana mikataba miwili..’akasema

‘Mikataba gani baba, hayo yanakuhusu vipi..?’ nikauliza

‘Yananihusu kwa vile nina hisa kwenye kampuni zenu, na kuna mikataba kama hiyo ya kuuza hisa kwa watu wengine mimi nina maoni gani kama mmoja wa wenye hisa..ni aswali ya mitego…’akasema

‘Kwahiyo umewarizisha kwa majibu..?’ nikauliza

‘Kuwarizisha kisiasa sio tatizo kwangu, tatizo ni huo mtego wa mpinzani wangu alikuwa na malengo gani,..na muhimu kwetu ni kuhakiksha tupo safi, familia ipo na mashirikiano manzuri, na isitokee kashafa nyingine tena…umenielewa..’akasema

Baba aliposema hivyo nikakumbuka hilo nililopanga litokee kwa rafiki yangu, linaweza kuleta kashfa mbaya kwenye familia na inaweza ikawa ni chanzo cha waandidhi kudadisi…oh, sasa nimefanya nini, nilitamani nikate simu, nianende kufuatilia hilo.

‘Swali jingine ambalo linawatia shaka, ni kwanini mume wako akamchuku amakabrasha kama wakili wake na ilihali tunatambua tabia ya huyo wakili, na kwanini kuna mikataba miwili ya familia yenu, je huo mkataba mpya ulitayarishwa lini na kwanini mkampa hiyo kazi Makabrasha, wakati mnamfahamu tabia yake?’ akauliza

‘Baba hilo ni moja ya jambo tutakaloliongea kesho, kuna mengi yamefanyika, nakubali hilo, na nimeamua kesho niyaweka yote wazi,, ili kijulikane kimoja, mume wangu hajambo, na anaweza kujieleza, na lolote linaweza kutokea, sijaamua ni nini cha kufanya baada ya hapo, ukizingatia kuwa mume wangu hajawa na afya ya kutosha, inabidi nitimize wajibu wangu kama mke wake..’nikasema

‘Hujaamua la kufanya hadi sasa, wakati unaishi na mtu anayeweza ku-kuua, kwa ajili ya mali zako, wewe hulioni hilo, kama wamefikia hatua ya kubadili mikataba ya halali...na katika harakati zao, inaonekana walishindwana, wakauana. Huoni kuwa mkono ukionja damu, inakuwa kama muonja asali, hajali tena kufanya maasi,....hilo sisi hatutalikubali, kama wazazi tutachukua hatua ...’akasema.

‘Baba nafahamu, mnavyojisikia ...lakini...’nikataka kujitetea lakini baba hakukubai kunipa nafasi , akasema;

‘Sitaki kusikia jambo jingine la kupinga maamuzi yangu, kama unanikubali mimi kuwa ni baba yako, kama unamkubali mama yako, basi itabidi ukubaliane na sisi, ....wewe huoni, wameamua kumuua,mtu wao wanayemuamini, na kumtambua kama sehemu ya famiia yao, kwa ajili ya kuficha ukweli, unafikiri watakuwa na huruma na wewe, binti yangu nilishakuambia huyo mume hakufai, mbona unatuweka roho juu...’akasema

‘Baba nilishawaambia mambo yangu nitajua jinsi gani ya kuyatatua, mwenyewe...niachieni,kwanza, nifanye nijuavyo mimi, ...msikimbilie kuchukua maamuzi yenu kwanza,kesho nimewaomba ili muweze kusikia maamuzi yangu, ambayo yatakuwa ni maamuzi yenye muafaka wa kudumu, nimesema sijafikia uamuazi bado, lakini mpaka kesho nitakuwa nimeshaamua ni nini cha kufanya, kwani kuna mambo ambayo nilikuwa nayamalizia...’nikasema.

‘Ulikuwa unamsubiria mpelelezi wako, ambaye keshakusaliti,...usimwamini huyo binti, kesharubuniwa, na kwasababu ya mali ..kwasababu ya tamaa, na kwa vile ana mahusiano na mume wako hatajali lolote itakao tokea kwako....anakufahamu udhaifu wako, anafahamu siri za kwako za nje na ndani, kwahiyo hatasita kukufanyia lolote baya....’akasema.

‘Baba huyo nimeshamweka sawa, hana lolote kwangu, nimeshamfahamu,...’nikasema

‘Sisi kama wazazi, tumeshafikia uamuzi, sisi kama wazazi, kesho tutatoa maamuzi yetu,kwa masilahi ya familia kuu, hili siwezi kulivumilia tena, na tuijaribu kuongea na mume wako, tuone lipi jema kwa hayo yote, asing’ang’anie ndoa tu wakati haiwezi, hivi karibu nikiongea naye ananijibu kama sio yule mkwe ninayemfahamu tena, kwanini kabadilika hivyo, wameshajua kuwa wamekuweka mkononi mwao, ....’akasema.

‘Baba kwanini mnaongea na huyo mtu wakati yupo kwenye matibabu,...hamuoni kuwa mtakiuka makubaiano yangu na yeye.....’nikasema.

‘Mume wako alishapona, na hayo yaliyotokea baada ya yeye kupona, ni moja ya mbinu zao, sisi hilo tulishaiona, na tumeshaongea na dakitari wake, na ingawaje dakitari wake anamtetea, lakini tuna uhakika kuwa mume wako anafanya hivyo makusudi, ili kufanikisha maengo yake na sio malengo yake, yeye anatumiwana mpinzani wangu bila hata ya yeye kulifahamu hilo...’akasema

‘Baba naombeni mniachie nifanye jinsi nionavyo mimi,...nisingelipenda nyie muingilie kati kwenye maamuzi, kwani mimi sijashindwa bado..’nikasema nikiangalia saa yangu

‘Ushindwe mara ngapi, kama umekubali, mume wako awe na nyumba ndogo, umekubai mume wako, azae nje, hujashindwa hapo. Hilo lilikuwa ni jukumu lako kubwa sana kuhakikisha kuwa mume wako anakuwa na utulivu wa ndani, ....hukuweza kulifanya hilo, na huo unaonyesha udhaifu, niambie kuhusu watoto wa mume wako ....au unafikiri sisi hatufahamu hilo?’ akaniuliza

‘Watoto!! Watoto….?? watoto gani wa mume wangu,?!’ nikauliza kwa mshangao

‘Unaniuliza, wakati sasa hivi umesema kuwa mambo yako utayaongoza mwenyewe, ..hufahamu kuwa mume wako ana watoto nje..huoni athari zake, wewe unalichukulia kawaida tu, hiyo ndio adabu tuliyokufundisha, huoni hiyo ni aibu kwenye familia yetu,…’akasema

‘Baba mimi nimesikia tetesi za mtoto lakini sio watoto..’nikasema

‘Mhh,. Halafu unajifanya kuwa unaweza kujimudu mwenyewe, hivi unatuweka wapi sisi,..hebu angalia maisha ya mbele, hao watoto, watakuja kujitokeza na madai yasiyoeleweka, watakuja kugombana na wenzao, ...maana kwa hivi sasa hamuwatambui, mpaka mmoja wenu afariki,..ndivyo ilivyo, ni heri wangejitokeza muda huu, mkiwa hai, ili mjue ni nini cha kufanya, haya tulikukanya, tunaifahamu sana hiyo familia...’akasema

‘Baba hili nimeligundua, lakini nijuavyo mimi , mtoto wa nje ni mmoja tu, huyo wa pili sio kweli’ nikasema.

‘Huyo wa pili sio kweli, ni yupi wa kweli na yupi sio wa kweli?’ akaniuliza na mimi hapo sikuwa na uhakika wa kumuelezea nikasema.

‘Baba yupo mtoto namfahamu,...japokuwa mume wangu hajanikubalia, na hata huyo mzazi mwenzake hajakubali lakini ushahidi wake kwa hivi sasa upo wazi, hawezi kuliping ahilo tena...’nikasema

‘Mimi nina ushahidi, ana watoto wawili,...unamkumbuka yule mfanyakazi wenu wa ndani aliyeondoka hapo bila kuaga,ulifuatilia ukajua ni kwanini aliondoka bila kuaga,...hujui kuwa aliondoka kwa shinikizo la mume wako…?’ akauliza

‘Mhh…mbona sina habari hizo..’nikasema

‘Ndio sasa tunakuambia..mume wako anaweza hata kutembea na mdogo wako kama mtaishi naye hapo nyumbani,…, ilikuwa siri yao wawili, huyo binti aliondoka akiwa mja mzito, na mume wako anafahamu, akawa anamtumia pesa za matumizi huko huko kwa siri, alijifungua, mtoto wa kiume, wanafanana na mume wako kama mapacha...’akasema

‘Mhh, hilo kwangu ni jipya, sikuwahi kulisikia, nitamuuliza mume wangu na ikibidi nitamtafuta huyo binti ii niweze kuhakikisha ...na kesho hayo yote yatajulikana, na ingekuwa vyema huyo msichana awepo kwenye hicho kikao, ..nyie mlipata wapi hiyo taarifa?’ nikamuuliza

‘Sio kwamba tumesikia, huyo msichana yupo hapa kwangu, alikuja kulalamika, kwasababu tangu mume wako aanze kuumwa hajatumiwa pesa za matumizi, na ilikuwa bahati tu kumpata, na sisi ikabidi tumchukue aje hapa kwetu, alikuwa mbioni kuja hapo kwako, tumelifanya hilo ili kuepusha kashifa zaidi…, sasa hili halina siri tena, unafikiri wewe utachukua hatua gani, ili hii hali isifike kwa hawa wadaku...’akasema

‘Oh,..baba naona unipe muda niweze kulfikiria hilo,,imekuwa ni mshtuko kwangu,…kiukweli siwezi kuvumilia tena....’nikasema nikiwa nimeingiwa na wasiwasi, kumbe namuhukumu mtu mmoja, na huyo je atahukumiwa na nani, na je ni hawo wawii peke yao....

‘Huna haja ya kuumiza kichwa, nashukuru kusikia kuwa umeshaupata huo mkataba wenu wa hiari, kati yako na mume wako,...nimeupenda, na ni vyema sasa ukachukua hatua kama mivyokubaliana, na kama utashindwa kuchukua hatua, ujue wewe huwezi kujiendesha wewe mwenyewe...huo ndio mtihani wako, sisi tumeshachukua maamuzi yetu,....’akasema

‘Baba naomba nipumzike, maana akili yangu haipo sawa...’nikasema

‘Haya usiku mwema,..lakini uwe makini, usije ukachukulia hasira, ukatenda mambo kama mtu asiyesoma, ujue kuna sheria,..ujue ni kitu gani unachotakiwa ukifanye kama msomi, unasikia, usije ukatenda mambo kama watu wengine, ...ukiharibu , sisi hatutakubali...’akasema

‘Sawa baba....’nikasema

Nikachukua simu yangu na kumpigia rafiki yangu, akawa hapatikani, nikajaribu kuwapigia hawo watu niliowapa hiyo kazi, na wao wakawa hawapatikani...sikukubali, nikatoka nje, na kuingia kwenye gari, sikuwa na muda wa kuongea na mlinzi, nikalitoa gari, na wakati nataka kutoka mlinzi akaja kunisalimia

‘Bosi unatoka?’ akaniuliza

‘Ndio kuna kazi nafuatilia, je mambo yapo sawa?’ nikamuuliza

‘Yapo sawa...’akasema lakini nilimuona kama alitoka kulala..

Wakati nimeshafika barabarani, nikahisi kuna mtu nyuma yangu, ndani ya gari, na kabla sijaweka gari sawa, sauti ikasema;

‘Fuata maelekezo yetu, la sivyo, tutakufanya kitu kibaya..’sauti nzito ya kiume ikasema na nikahisi kitu kikali kikigusa ngozi yangu, nikahisi kuwa ni kisu....

NB; Kulikoni...

WAZO LA LEO:Ushauri wa wazazi ni muhimu sana, tunaposhauriwa na wazazi wetu tujaribu kuwasikiliza, hata kama tunajiona tuna uwezo zaidi yao wa kihali na mali, tujue kuwa wao wameona mengi zaidi yako, na wamepitia maisha ambayo wewe hujawahi kuyapitia, hekima zao zinaona mbali zaidi, tuwasikilize, tukae pamoja nao, tuone je mawazo yao na mawazo yetu yanaweza kufikia muafaka wenye manufaa, tusichukulie ubabe kwa vie tunazo, tumesoma sana, nk.
 
SEHEMU YA 90

Hata hivyo, na wazazi nao wanahitajika kuwasikiliza watoto wao, wasikie mawazo yao, kwani huenda kwa elimu yao mpya, na upeo wao wa kuchanganyika na watu wanaweza wakaja na njia mbadala,...hii ni kwa nia njema, kwani maafa yakitokea ni athari za pande zote.


Niifuata maelekezo kama walivyotaka wao, walichokuwa wakifanya ni kuniamuru, kwa kunielekeza kuwa nielekee wapi, nikate kushoto au kulia, hadi tukafika maeneo yasiyokuwa na umeme, eneo hilo ilikuwa na majengo mapya mapya, na nikaambiwa nisimamisha gari.

‘Simamisha gari..’nikaamriwa

Nikafanya kama walivyoniamurisha na nilipotaka kugeuka kuwaangalia ni akina nani, maana nilishahisi kuwa wapo wawili, kiyoo cha kuangalia nyuma walikuwa wameshakigeuza kwa juu ili nisiweze kuwaona kwa nyuma.

Wakati nataka kugeuza kichwa, mkono wenye kitambaa ukapitishwa puani kwangu na aliyefanya hivyo, akanishika shingoni kama mtu anayenikaba, na mwenzake akasema;

‘Mbona unamkaba, hukusikia bosi alivyosema, bosi alisema tusimdhuru sehemu yoyote, atajua mwenyewe ni nini cha kufanya tukimfikisha..’akasema mwenzake

Niliposikia hivyo mawazo yakanipeleka mbali kuwa huenda ni yale yale niliyotaka kumfanyia rafiki yangu, ndio yamenigeukia mimi, sikuweza kujitetea maana kile kitambaa walichoniwekea puani, kilinivunja nguvu zote, viungo vyote vikalegea, japokuwa kwa mbali niliweza kusikia wanachokiongea.

‘Sasa ningewezeje kumweka hii dawa...kwanza haijaingia vyema huoni bado yupo macho...’akasema na wakanishikisha kile kitambaa puani, na nilipoivuta pumzi, nikahisi nikizama kwenye giza, sikujitambua tena.

Sijui ilipita muda gani, lakini nahisi ni karibu ya saa moja au nyuma kidogo, ..nilihisi kitu kikipita puani, na hapo nikapiga chafya mfulululizo, hadi nikashikwa na kikohozi, na hapo hapo nikawa kama mtu aliyekuwa kwenye ndoto ya majinamizi, napaigana kushindana na hiyo hali, lakini viungo havina nguvu, nikawa kwenye hiyo na hali na baadae nikaanza kurejewa na fahamu.

Ikapita muda, na taratibu akili yangu ikaanza kunirejea kama mtu anayetoka usingizini, bado wakati huo mwili mzima ulikuwa umelegea, nikajaribu kuinua mkono, mkono ulikuwa kama haupo kwenye mwili wangu mara nikasikia sauti kwa mbali;

‘Bosi anasema kila kipo tayari,..ngoja azindukane tu…’sauti ikasema

Nikajitikisa kidogo, kujaribu mkono kama unaweza kuinuka…

‘Naona kama keshaanza kuzindukana....mnaweza kumrejesha kwenye gari lake, lakini hakikisheni, anazindukana kabisa ndio muondoke, mlindeni asije akaumizwa na watu wengine, tukaja kupata lawama, kazi tuliyomuhitajia imekamilika, kila kitu chake kirudisheni kama kilivyokuwa....’sauti ikasema

‘Bosi ina maana tumuache hivi hivi tu....’nikasikia sauti ikisema

‘Wewe ulitaka kumfanya nini, acha na tama mbaya, hapa ni kazi tu, kama tulivyoagizwa, kazi yetu ni kufuata maagizo, tunachohitajia sisi ni pesa si vinginevyo, hatutafuti mengine, hayo unayoyataka wewe sio utaratibu wetu, na ole wenu mumuguse, huyo ni hatari kuliko ,mnavyofikiria, ...’sauti ikasema

‘Kama ni hatari huko mbele akizindukana itakuwaje...?’ akauliza mmojawapo

‘Ndio maana nawataka mumurudishe kwenye gari lake, na hakikisha mnamkalisha kwenye kiti chake aonekane kalala kwenye gari lake, akizindukana, atajijua mwenyewe, sisi kazi tumeshamaliza, tunakwenda kuchukua mshiko wetu, ...’ sauti ikasema

‘Sawa bosi…’sauti nyingine ikasema

‘Na muhimu hakikisheni kuwa yupo salama, na mkiona kuwa kazindukana, poteeni mbali kabisa, ukibakia hapo yatakayokupata sisi hatupo, na hakuna kutajana hapa, kila mtu afe kivyake,…nawaambia tena, ukishikwa ukafunua mdomo wako, utakuwa mgeni wa mchwa..’sauti ikasema

‘Sawa bosi tumekuelewa...’nikahisi mmoja akisema wakanibeba, na mmoja akawa anasema kichichini.

‘Huu mwili, laini, laini hivi, tutaishia kuubeba tu...hawa watu hawana akili kweli, ...’akasema

‘Unajua wewe utakufa kwa ukimwi, wewe unapenda mambo hayo sana, kama umelaaniwa nayo, mwili tu unakusumbua,..tunachokitafuta hapa ni pesa, tufanye kazi yetu tulipwe, ..ukishapata pesa, watu kama hawa utawapata wengi, ....’sauti nyingine ikasema.

‘Sawa bwana,...pesa yenyewe , shilingi ngapi kwanza, ...aheri ile ya wenzetu, wabakaji, wanaopewa kazi ya kudhalilisha wanawake,..wanaifanya hivyo na bado wanalipwa...’akasema.

‘Kubaka nako kazi, ..ile sio kazi ya kufanya, ni hatari tupu, na umewasikia wenzako, kilichowatokea,...sasa hivi wanatafutwa na polisi, safari hii wameshindwa, nasikia wamepewa kazi, kabla hawajaifanya wakafumwa, ngoja wafukuzwe na polisi,karibu wakamatwe..nilikutana na yule jirani yako, akikimbia utafikiri yupo kwenye mbio za dunia, na akaniomba nauli, anataka kupotea hapa jijini.’mmoja akasema

‘Kwani na nani na kwanani?’ mmoja akauliza

‘Nasikia ni kwa binti mmoja , aliyetoka ulaya hivi karibuni…’akasema

‘Sasa huyo ana kosa gani , maana nasikiwa wakijiita kundi la kurekebisha tabia..’akasema

‘Anajua huyo aliyewatuma kuwa ana kosa gani…’akasema

‘Ikawaje sasa
‘Basi bwana,..walifanya kama kawaida yao, na hizi dawa za kupoteza fahamu, kwanza walipambana, maana huyo binti sio mchezo, kilichowasaidia ni hiyo dawa ya nusu kaputi, walifanikiwa kumnusisha, hapo ndio wakamuweza, wakambeba, sasa walisahau kuwa nyumba hiyo kuna mtu mwingine,alikuwa chumba cha pili, huyo ndiye aliyewaharibia, akawapigia simu polisi..

‘Ehe, ikawaje..?’ akauliza na wakati huo, wameshanifikisha kwenye gari langu , wakawa kwenye harakati za kuniweka kwenye kiti, nilikuwa bado nimelegea lakini akili ilishaanza kufanya kazi,sikutaka kuwashitua ili nisikie ni nini wanakiongea, nikaendelea kufumba macho.

‘Basi bwana kama kawaida yao, maana wanapofanya hiyo shughuli, huku wakirekodi tukio nzima, kwahiyo walipomfikisha huyo binti kwenye kichochoro, walichoona kina usalama, wakaanza kuweka vyombo vyao vya kuchukua hilo tukio, ili wakamuonyeshe tajiri wao, wakati wanajiandaa, wapo tayari, kufanya mambo yao, mara king’ora cha polisi kikasikika, na hawo polisi walifanya hivyo makusudi, maana hawakujua hawa jamaa wamejificha wapi...’akasema

‘Oh, kwahiyo kazi ikavurugika...wakakamatwa...?’ akauliza mwenzake

‘Wakamatwe wapi, ...tatizo lao waliposikia king’ora cha polisi hakuna aliyemwangalia mwenzake kila mmoja akajua njia yake, wakaacha kila kitu hapo, polisi wakafika na kumuokoa huyo mwanadada...na vitu vyote vikachukuliwa kama ushahidi, na mijamaa hiyo inatafutwa kama alimasi...kwasababu wanajulikana, na huyo dada anawafahamu, ...’akasema

‘Mhh, hapo kazi ipo....’akasema

‘Nafahamu kukamatwa sio rahisi, watakuwa wameshavuka milima na mabonde, hawataonekana hapa hadi mwaka upite, tatizo, hawana pesa, maana kazi hawakufanya, watalipwaje sasa...je wataweza kuvumilia kuishi bila pesa, ...huko walipokwenda labda wakavunje nyumba za watu na kuiba, na hiyo sio fani yao....’sauti ikasema.

‘Mhh, imenitisha, kwahiyo polisi wamecharuka kwa hivi sasa, mmh, hapo sasa mimi naanza kuogopa, tuondoke zetu, kama ni hivyo polisi watakuwa kwenye patroo zao, hebu mwangalie, nimemuona kama anajitingisha, keshaamuka yule, funga mlango wa gari tuondoke zetu bwana...’sauti ikasema

‘Una uhakika..?.’akauliza mwenzake.

‘Nenda wewe ukahakikishe, unasikia ulivyo ambiwa, huyo dada sio mchezo, kwa vyote, ana pesa na pia anazijua ngumi,,...mimi sitaki jela, naondoka zangu...’sauti ikasema na mara baadae kukawa kimiya

Hapo nilipo nikahisi wameshaondoka, na mimi nikajaribu kuinua mkono, na huku nikijikagua, sikuhisi maumivu sehemu yoyote, nikajinyosha na kukaa vyema, nikafungua viyoo kupata hewa, nikataka kutoka nje ya gari, mara nikaona gari likija mbele yangu.

Mimi nikawasha gari langu, lakini kabla sijaanza kuendesha, gari hilo likiwa limeshafika, walikuwa ni polisi, wakasimamisha gari lao karibu na gari langu, na silaha zao mikononi, mmoja akasogea kwenye gari langu na kugonga kwenye kiyoo, mimi nikashusha kiyoo, akaniangalia kwa makini akaniomba kitambulisho, nikamuonyesha leseni yangu, akaikagua halafu akasema;

‘Madamu huku umefuata nini, kuna tatizo lolote..?’ akauliza

‘Nahisi hakuna tatizo, gari lilinizimikia , lakini naona lipo sawa...’nikasema, na sauti kavu ya kulazimisha ikanitoka, ilikuwa kama sio ya kwangu, nilihitajika kupata kitu cha kulainisha koo, na yule askari aliposikia hiyo sauti akaniangalia na kusema;

‘Unahis ulikuwa kwenye tatizo,…nyie zunguka kila mahali…’akatoa amri.

‘Madam tuambie ukweli maana hizi sehemu hizi sio nzuri, kuna watu wabaya huku, kuna kesi nyingi za wahuni, wavuta bangi na wabakaji, kama kuna tatizo lolote, tuambie, vinginevyo, ni bora uondoke kabisa eneo hili..’akasema na mimi sikutaka kumsikiliza tena zaidi, nikaondoa gari langu na sasa nikawa na kazi ya kutafuta njia ya kurudi nyumbani.

*************

Ilikuwa ni kama saa sita na nusu hivi za usiku nilipofika nyumbani, na mlinzi wangu alikuwa keshaanza kuingiwa na wasiwasi, aliponiona akanijia na kuanza kuongea kwa haraka haraka;

‘Bosi, nilishaingiwa na wasiwasi, hapa tu nilitaka kuwapigia simu polisi, lakini kwanza nilitaka kuwasiliana na wakubwa zangu wa kazi, sio kawaida yako kutoka usiku, na kuchelewa kurudi kama leo, kuna tatizo lolote bosi?’ akaniuliza

‘Hakuna tatizo..’nikasema na sikutaka kuongea na mtu nikakimbilia ndani, na cha kwanza ni kunywa dawa , ni dawa maalumu za kuvunja nguvu za madawa kama hayo waliyonunusisha puani.

Ninafahamu jinsi gani ya kuyavunja nguvu, na nafahamu ni aina gani ya dawa hizo, nilifanya juhudi ya kuyaondoa hayo madawa kabla sijala kitu, ilikuwa usiku sana kwakweli, na baadaye nikaoga, huku nikijikagua kuhakikisha kuwa nipo salama, na kilichofuata hapo ni kutafuta usingizi, nililala hadi saa tatu, asubuhi.

Niliamushwa na kelele za mlangoni, nikatoka na kukutana na msaidizi wangu wa kazini amfika nyumbani, akasema kapiga simu yangu haipatikani ndio maana akaamua kuja nyumbani…, nikamwambia sijisikii vyema, na akanikumbusha kuwa leo nina kikao cha kukutana na familia yangu, saa nne, nikamwambia kitafanyika kama kilivyopangwa.....

‘Na pia kutoka msajili wa mikataba, alikuwa anataka kuongea na wewe..’akasema

‘Kwanini aongee na mimi , anatakiwa kuongea na wakili wangu au sio…’nikasema

‘Hata mimi nimemwambia hivyo hivyo, lakini akasema ni muhimu angeongea na wewe …kasema atakupigia tena…’akasema

‘Ok akipiga niunganishie kwenye namba yangu nitakayokuwa hewani, kuna jingine …?’ nikauliza
‘Hakuna bosi mengine ni ya kawaida,…matumizi ya ofisi…kanipatia muhasibu, na hundi ya kuweka sahihi..’akasema

‘Ok, nipatie….’akanipa nikapitia kwa haraka, nikaweka sahihi, na mambo ya kiofisi yakaishia hivyo.

*********

Nilijiandaa kutoka, na nilipokuwa tayari nikaenda kuchukua laptop yangu, sehemu nilipoiweka, nikaumbuka sikuirudisha kabatini, ikawa ni kosa, haikuwepo...sikuamini, maana hapo nilipokuwa nimeiweka sio rahisi mtu kuigundua, lakini imeshachukuliwa

‘Ni nani huyu…?’ nikajiuliza na kwa haraka ,...nikajua huenda waliochukua ni hawo watu walionikamata jana...nikatoka na kwenda maktaba,huko niliona kila kitu kipo kama kilivyokuwa japokuwa kuna dalili za kutaka kuvunjwa...

Hawa watakuwa hawo watu wa jana, na kwanini wachukue laptop yangu tu...?’ nikajiuliza, na mara nikakumbuka,.

‘Ina wezekana ni shemeji yangu, huenda alitaka kuhakikisha kuwa sina zile kumbukumbu zake za diary yake, amejidanganya...’nikasema kimoyomoyo

Wakati nataka kuondoka, nilipotoka nje, niliona boksi limewekwa mlangoni, sikulishika kwanza, nikamuita mlinzi, kwani msaidizi wangu wa mambo ya ndani, alikuwa kaelekea sokoni kununua mahitaji ya nyumbani, Mume wangu alishatoka hospitalini, lakini tulikuwa hatukai naye hapo nyumbani, alikuwa akikaa kwenye nyumba yetu nyingine, tulikubaliana iwe hivyo.

‘Hili boksi kaweka nani hapa?’ nikamuuliza mlinzi, akasema yeye hafahamu

‘Hufahamu ina maana huu mzigo umeingia wenyewe humu, kuna mtu kaingiza, wewe hukuwepo getini?’ nikauliza kwa ukali, kiukweli hata mlinzi akiliniangalia kwa mashaka, sina kawaida ya kuongea na wafanyakazi wangu kwa ukali hivyo.

‘Bosi nilikimbia kidogo kujisaidia, nilipokuja , sikuangalia huko , hata hivyo, ...mmh, ndio, niliona mtu akitoka wakati wakati natoka chooni, nikajua ni wafanyakazi wako, ....kwani sio boksi lako bosi,..?’akasema

‘Haya lifungue mwenyewe, kama ni bomu utajua mwenyewe jinsi gani ya kulitegua...’nikasema na huyo mlinzi akiwa na wasiwasi akalifungua, ...

‘Oh, ni laptop yangu...’nikasema huku nikiitoa, nikaikagua, ilikuwa haina tatizo lolote, nikaingia nayo ndani cha kwanza ilikuwa kuangalia ni ile diary ya shemeji,...kila nilipojaribu kuiifungua inasema haifunguki, haifanyi kazi, na mwisho ikasema haipo kabisa...nikajua kuwa ni huyo shemeji yangu

Kabla sijaifunga hiyo laptop yangu, nikaona ujumbe kwenye komputa ulikuwa umeandikwa kama barua pepe, nikaufungua na kuusoma

Ujumbe;

‘Samahani sana shemeji imenibidi nitumie njia hii, ili kuzipata kumbukumbu zangu, ambazo nyingi ni mambo yangu binafsi, na si vyema watu wengine wakayafahamu, natumai ulifika salama, hakuna lolote lililotokea dhidi yako, na kila kitu chako kipo salama, japokuwa kuna vitu nilishindwa kuvichukua kwenye kabati la kaka, kaka aliniagiza, lakini hakijaharibika kitu, mtamalizana na yeye, ninachokuomba ni kumsaidia kaka, na mimi unisamehe sana kwa kutokukukutimizia yale uliyoyataka....’

‘Huna adabu kabisa,unafikiri hilo ulilolifanya litasaidia kitu, tatizo huyu kijana hanielewi mimi, yeye hujui kuwa mimi ni mjanja zaidi yako...’nikasema, nikachukua kidude cha mtandao (moderm), nikaweka mawasiliano, nikaingia kwenye mtandao, nikatafuta kumbukumbu zangu, nikaona ninachokitafuta, nikafungua, nikaiona kumbukumbu iliyoandikiwa diary ya shemeji, ipo kama ilivyokuwa...nikatabasamu, nikainakili tena kwenye laptop yangu.

Nilipohakikisha kuwa kila kitu kipo sawa, nikampigia simu, rafiki ya mume wangu, ili kuhakikisha kuwa na yeye atakuwepo kwenye kikao, kwani bado alikuwa akihangaika na mke wake,...

‘Vipi upo, maana siku hizi wewe hukai nyumbani kwako, sijui bado unatafuta mtoto wa kiume au..?’nikamuuliza

‘Ni kawaida tu, ...nipo kwenye kikao, na ikao cha familia nitafika pia, na mke wangu keshafika, alifika jana usiku, na amekubali kuwepo kwenye hicho kikao, anasema ana yake ya kuongea, baada ya hapo anarudi huko kijijini alipokuwa, sijamuelewa huyu mwanamke mpaka sasa, nimechoka...’akasema.

‘Vyema kabisa, nimefurahi kusikia hivyo, je uliwahi kuongea naye lolote na akaweza kukuambia chochote.... ?’ nikamuuliza

‘Hataki kuongea lolote, anasema yote atayaweka wazi hapo kwenye kikao, alikuwa anatafuta nafasi kama hiyo, ...nahisi kuna jambo kubwa linamkera, maana hata wazazi wake, wanasema kawa kama mtu aliyepagawa, hana raha,...sijui ana tatizo gani...’akasema

‘Pole zake, ndivyo ilivyo, majuto mara nyingi huja baada ya kitendo, tunapofanya mambo bila kuangalia mbele,mwisho wake unakuwa mgumu, ...natumai atakuwa mkweli, na ukweli wake ndio utakaoweza kumsaidia, sio vinginevyo...’nikasema.

‘Mhh,..kwanini unasema hivyo nahisi wewe kuna jambo unalifahamu kumuhusu yeye, na ameamua kuwa msiri sana, na hilo ndilo litakalomuangamiza, ni jambo gani hilo jamani..?’akasema na kuuliza

‘Kila jambo lina mwisho wake, nina uhakika yote yatajulikana kwenye kikao, ujiandae kwa lolote lile, na mimi siwezi kukuambia chochote, yote yataanikwa kwenye hicho kikao...’nikasema.

‘Kwanini lakini, hamjui mnavyonitesa?’ akaniuliza

‘Wewe ulijifanya unafahamu yangu mengi tiu…, mbona hukuniambia, hukujua jinsi gani nilivyokuwa nateseka,..sasa ni zamu yako, lakini usijali, yote yatajulikana kikaoni, natumai wote watafika, wasiwasi wangu ni kuwa shemeji yangu anaweza asifike, na yeye ni mtu muhimu sana....’nikasema

‘Kwani kaenda wapi, maana hata mimi namtafuta kwenye simu hapatikani..?’akaniuliza

‘Unamtafuta wa nini..au ndio kupanga njama za kuharibu ushahidi, safari hakiharibiki kitu,…’nikasema

‘Kijana amekuwa mtoto wa mjini, anayoyafanya anayafahamu yeye mwenyewe, na hata mke wake analalamika sana,..na zaidi hata kaka yake ananipigia simu mimi kuniuliza wapi alipo mdogo wake…’akasema

‘Waongo hao…jana tu walikuwa pamoja, walichokifanya mungu mwenyewe anajua, lakini ama zao, ama zangu…’nikasema

‘Mhh, haya bwana, lakini namlaumu sana mume wako, yeye ndio anamuharibu mdogo wake, ...nasikitika sana, kwani juhudi zangu zote zimekuwa hazina manufaa, kwa huyo mdogo wetu...’akasema.

‘Je mie niliyemgharamia masomo na kila kitu, hadi kuoa, nitasemaje…ni kweli shutuma zote ni kwa kaka yake, mimi sizani kama nitakuja kumsamehe…’nikasema.

‘Unajua sema ni kwa vile mambo yangu yamekuwa mengi nimeshindwa kuyafuatilia maisha yao, na yenu kwa ujumla,mnisamehe sana, hata wazazi wako nimewaambia hivyo, mambo yemeniwia mengi sana, ila kwenye kikao nitajitahidi niwepo tu, japokuwa …sijui..nitakuwepo, ngoja niweke mambo yangu sawa....’akasema.

‘Ni muhimu sana uwepo, kama mkeo yupo, basi hatima ya yote haya itajulikana kwenye hicho kikao, na wasiwasi wangu ni kuwa baada ya hicho kikao huenda kusiwe na urafiki tena, lakini sio kitu, bora nusu shari kuliko shari kamili ....’nikasema

‘Kwanini kusiwepo na urafiki, mimi nilijua ni kikao cha usuluhishi?’ akauliza

‘Kwasababu ukweli ni mzuri sana, lakini unauma, na utahukumu yanayostahiki kuhukumiwa, ili haki itendeke,...’nikasema.

‘Sawa hamna shida, mimi sina tatizo,...kama kuna ukweli ninaoufahamu nitausema, kama utasaidia, ...’akasema.

‘Na hasa uwe wa kumsaidia mke wako, ...’nikasema.

‘Yah, mke wangu na wewe pia,....nikuambe ukweli, hapa nilipo nakuwaza wewe, namuomba sana mungu, itokee miujuza, ile hali ya zamani irejee,sina raha kabisa, najuta kwanini haya yametokea, inafikia hatua natamani ndoa yangu ifike mwisho tu, ili nijue moja...’akasema.

‘Nini…ndivyo unavyoombea ili iweje sasa, muhimu ni wewe na mwenzako, ...kila mtu ana shida zake, hilo nilowahi kukuambia kuwa usione mimi napata taabu na mume wangu, wapo watu wanapata shida sana na ndoa zao, sio mchezo, lakini mwisho wa yote ni nyie wenyewe, kila mmoja anatakiwa kuwa na maamuzi yake, unasikia, kila mtu aubebe mzigo wake yeye mwenyewe..’nikasema.

‘Haya nakuja , ngoja nimpitie mke wangu, ,....’akasema

‘Sawa na mimi ndio naondoka nyumbani hivyo, uwe makini na mkeo..’nikasema

‘Na wewe pia…’akasema

Nikaanza safari ya kuelekea kikaoni na wakati nipo njiani nikahisi kuna pikipiki, ilionekana ikinifuata kwa karibu sana, sikusimamisha gari hadi ninafika, na yule mtu mwenye pikipiki, akanipita, na kunipungia mkono, sikujua ni nani, kwani alikuwa kavaa helimeti ...mimi nikafika kwenye eneo tulilopangia kufanya kikao.

Wazazi wangu na mawakili walikuwa wameshafika…,



WAZO LA LEO: Migogoro mingi huishia pabaya, wengine husihia hata kupigana, au kukosana kabisa, ni kwanini tukimbilie vita, kukosana, na hata kutalikiana, kwanini kwanza tusikae tukaongea tukatafuta chanzo cha tatizo ni nini, huenda ni shetani, tu, huenda ni wenzenu wanataka muharibikiwe tu…mzungumzo ya heri, ya kujadili tatizo yana tija zaidi ya uhasama wenyewe.
 
SEHEMU YA 91


Nilifika sehemu ambayo huwa tunafanyia vikao vyetu, ni kazini kwangu , lakini kuna sehemu maalumu imejengwa kwa ajili ya vikao, na siku hiyo sehemu hiyo ilipangwa mahsusi, kwa ajili ya hicho kikao cha familia yangu.

Nilipofika kwenye chumba cha mkutano nilimkuta baba keshafika, yeye alifika mapema tu baadae akafika mama, baba ni mtu anayejali sana muda.

Nilipofika tu nilimkuta akipitia makabrasha yake, na lapotop yake ikiwa pembeni, akionyesha kuwa anakwenda na wakati, na mar simu yake ikawa inaita, hapo akawa na wakati huo alikuwa anataka kuongea na mimi.

‘Tafadhali bint, karibu, ngoja niongee na hii simu…’akasema na mimi nikawa nimekaa kwenye kiti nikisubiria amalize kuongea na simu,…alipomaliza tu, akaanza kunilaumu akisema;

‘Nilitarajia watu watafika kwa muda, lakini naona dakika tano zimepita, siwaoni watu, ..’akaanza kulalamika

‘Foleni na hulka zetu baba, lakini nina uhakika wote watafika, ambao ni muhimu kwa kikao hiki,....’nikasema

‘Sawa hebu kaa kwenye kiti tuanze kuongea yetu, ya baba na binti yake, wewe mama unaweza kukaa kimia kwanza, usiingilie….’akasema

‘Sawa mimi siunaniona sina maana kwako…’akalalamika mama

‘Hapana unakaribishwa nilikuwa natania tu…’akasema baba

‘Umafanikiwa ulichokwenda kununua…?’ baba akamuuliza mama kwanza

‘Ndio…japokuwa sio vyote,…’akasema mama

Mama alisema alipitia kumfanyia manunuzi binti yake, nguo na vifaa, vya safari ya huyo bint.

‘Ni binti gani huyo?’ nikamuuliza.

‘Utamuona tu , na yeye atakuwepo kwenye kikao, ....’akasema na sikutaka kumuuliza zaidi, kuhusu huyo bint.

Nilipotulia kwenye kiti, baba akaniangalia kwa makini kama ananisoma kwenye ubongo wangu, halafu akasema;

‘Nilitaka kufahamu maamuzi yako, nataka nijue ni nini msimamo wako baada ya haya yote, nataka nikushauri kama baba yako, kama mzazi wako, japokuwa mimi na mama yako tumeshaongea na kufikia uamuzi wetu, ambao sio tofauti na ule wa awali, kwa nia njema tu lakini yote inategemea nyie wenyewe,....’akasema

‘Baba maamuzi yangu yatatolewa mbele ya wahusika, ninawahitajia wenyewe waje wathibitishe waliyoyafanya, ninataka kusikia kauli zao kwanza, je wamesimamia wapi, kwenye ukweli au kuficha ukweli..’nikasema

‘Sio rahisi mtu kukubali kosa kwanza, hasa akijua madhara yake..’akasema baba

‘Sasa kwa vile watakuwepo, ngoja tuwasikie kwanza , yote yaliyotokea tutayamaliza kwa amani na salama, kutegemeana na wao wenyewe, vinginevyo, kama ndivyo walivyo, na watang’ang’ania kuwa waongo, basi baba mimi nitanawa mikono..’nikasema

‘Hebu niambie wewe ulishafikia wapi, maana uliniambia kuwa unafanya uchunguzi, na utakuja kutoa maamuzi yako mbele ya kikao, ..nataka kuona mtoto wangu anaongea kama mimi, au zaidi ya mimi, unanielewa, nataka niione kazi yangu kwako, kama huwezi uniambie, nitajua ni nini cha kufanya...’akasema

‘Hivi baba hujaniamini, baada ya yote hayo niliyoyafanya, baba mimi sio mtoto tena, ni mtu mzima nafahamu ni nini ninachokifanya, nimeweza kuisimamia kampuni yangu bia kutetereka, na ikawa kubwa, kama unavvyoiona, nimetulia kidogo baada ya matatizo na mume wangu, lakini kuna msaidizi wangu ambaye anaifanya hiyo kazi vizuri tu, japokuwa sasa naona mume wangu kaamua kuingilia kati, lakini ni kwa muda tu, baada ya hiki kikao nitarejea tena kwenye ulingo wangu..’nikasema

‘Binti yangu, sio kwamba nakushusha chini katika utendaji wako wa kazi, hapana, kiukweli unajitahidi sana, hata mimi najisifia mbele ya wenzangu, lakini hili lililotokea, ....mmh, limekushusa, haya yaliyotokea kati yako na mumeo wako, imeharibu kila kitu. Unafahamu kupanda juu, kunachukua muda, akini kushuka, ni mara moja tu...’akarudisha kichwa na kuegemea kiti, haafu akasema;


‘Baba mimi sijashindwa kabisa kuiongoza familia yangu, na unapozungumza hivyo, unasahahu kuwa mimi ni mke wa mtu, ambaye nina mipaka yangu, ...lakini hata hivyo, sio kwamba nimeshindwa kuiongoza familia yangu kama mke...nimejitahidi kufanya yale ya mpaka wangu, kwa kadri ya uwezo wangu, yaliyotokea yamekuwa changamoto kwangu..na sizani kwamba nitafanya hayo makosa tena,..kamwe, baba niamini, ....’nikasema

‘Binti yangu, Usije ukaharibu, .mimi hilo sitakubali, kwasababu tabia ya kizalia haina dawa, hayo waliyokufanyia ni mwanzo tu, ujue chini kwa chini kuna dhambi za damu ya mtu, unafikiri hiyo damu itafukiwa kwa mchanga tu hivi hivi, hata kama tutayamaliza kienyeji, lakini sio sahihi, kuna mtu kauwawa, hakuna haki iliyotendeka, hata kama alikuwa na madhambi yake, watu wanasema aheri kafa, lakini ni wapi sheria ilisema auliwe hivyo,hilo uliangalie kwa makini..’akasema

‘Baba mimi naomba unipe nafasi hiyo, kama nitakuwa nimekosea mtanisahihisha, lakini nina imani kila mmoja atajihukumu mwenyewe muda ukifika, uwongo na hadaa una mwisho wake, ...wewe subiria, tu, tusichukue maamuzi kabla wenyewe hawajajitetea tukaona ukweli upo wapi..’nikasema.

‘Na muda mfupi uliopita nilikuwa nawasiliana na mkuu wa upelelezi wa kituo chenu, na yule aliyefuatilia kesi ya mauaji ya Makabrasha, wameniambia mengi ambayo wameyagundua wao kama wao,…’akasema na kabla hajaendelea watu wakaanza kuingie, ikabidi tukatize mazungumzo;




**********

‘Hivi mama huyo bint yupo wapi…?’ nikamuuliza mama

‘Ataingia tu usiwe na wasiwasi, hatutaki watu wamuone sana, na iwe ni maswali mengi, ataingia kwa muda muafaka akihitajika, baba yako kasema kuna muda atamuita, lakini sio kwasasa ..’akasema mama

‘Ni muhimu kulifahamu hilo, maana hayupo kwenye orodha ya wajumbe wanaohitajika kuwepo, kikao hiki kipo kisheria…’nikasema

‘Usijali, mimi nimemuita kama mwenyekiti…nitamlinda, na kumdhamini,…’akasema baba.

Muda wote tuliokuwa tukiongea mawakili walikuwa upande mwingine wakiongea yao , hawakutaka kuingia mambo ya kifamilia hasa pale tulipokuwa tunaongea na baba, lakini kwa hivi sasa wakasogea karibu, kwenye meza kubwa

‘Nyie mawakili wetu mtakaa kimia, ila mkihitajika kuongea au kuelezea jambo, tutawafahamisha, au sio, haya ni mazungumzo ya kifamilia zaidi, lakini kuna muda mtahitajika…’akasema baba, na mimi nikakubaliana na hilo.


Tulitaka kuanza kikao, lakini kuna wajumbe muhimu walikuwa bado hawajafika na wao ni muhimu sana, kikao kisingeliweza kuendeshwa bila kuwepo kwao, nikataka kupiga simu , lakin kabla sijafanya hivyo mara wakaanza kuingia wajumbe wengine.

Aliyefika sasa hivi alikuwa rafiki wa mume wangu akiwa na mkewe, na baadaye akaingia mume wangu, alipofika kwanza akajibaragua kidogo, kama ujuavyo, waliokuwepo hapo ni wazazi wangu tu, ni wakwe zake, kwahiyo alionyesha ile adabu ya ukwe, akawasalimia na baadaye akaja kukaa karibu yangu,

‘Samahani sana nimechelewa najua mimi ndiye mwenyeji, lakini kuna mambo yalinitinga,…’akasema

‘Hamna shida…’akasema mzee

‘Ni lazime niwajibike, hata mkataba wetu unasema hivyo…’akasema akijitutumua, na mimi nikamuelewa anaelekea wapi.

‘Mkataba upi unaouzungumzia hayo, wa zamani au mpya?’ nikamuuliza kumchokoza huku nikitabasamu, hapo akasita na baadaye akasema;

‘Hakuna mkataba mpya na wa zamani, hiyo kauli yako tu mke wangu usiwachanganye wajumbe...’akasema na hapo nikajua hajafahamu kuwa nimeshaupata ule mkataba wetu wa asili.

‘Tutaona..muda ukifika hilo litasahihishwa, ...fungua kikao, au nifungue mimi maana ndiye niliyekiitisha,…?’nikasema na kuuliza

‘Hapana, tunafuata mkataba wetu, nataka kikao hiki kitambue kuwa kuna mkataba wetu wa kifamilia…’akasema

Mume wangu kwanza akamuangalia baba, akainama kiheshima na kufungua kikao kwa kumkaribisha mwenyekiti wa kikao, ambaye ni baba, kikawaida kwenye familia yetu, kukiwepo kikao kama hicho mwenyekiti ni baba.

Baba kwanza alianza kufungua makabrasha yake, na kabla hajasema neno, mlango ukagongwa, na kwa vile wote tulijua kuwa tumekamilika, hatukutarajia mtu mwingine mpya, kujitokeza tena, kwahiyo hiyo hali ikatufanya, sote tugeuke na kuangalia mlangoni, kuona ni nani huyo anayetaka kuingia

***********,

Mara akatokea mtu akiwa kavaa kofia la waendesha pikipiki, akasimama pale mlangoni akisita kuingia…

Huyu mtu, alikuwa kavalia jaketi la kuzuia upepo mwilini, na kumfanya aonekane bonge, alisimama pale mlangoni kofia likiwa bado kichwani, inaonekana hakutaka kulivua huko nje, labda kwa vile aliona keshachelewa, kama ni mjumbe wa kikao hiki, ambaye mimi sikuwa na habari na yeye,au alifanya hivyo kwasababu zake nyingine.

Kila mmoja ndani ya kikao alimwangalia yeye, na yeye alipoona watu wote wanamtizama, akafanya mambo mawili kwa haraka, kwanza akainama, kama vile anasalimia au kutoa heshima na pili, akageuka kuangalia mlangoni, kuhakikisha kuwa amefunga mlango, akalivua lile kofia lake na kuvua koti , halafu taratibu akageukia watu, na kusema;

‘Samahani sana wakubwa zangu, na baba na mama pale..mimi nimechelewa, nilikuwa naweka mambo yangu sawa, maana kiukweli...jamaa wananifuatilia kila kona...’ akasema huku akiangalia pale alipokaa mwenyekiti, lakini alikuwa hamuangalii moja kwa moja usoni, na mwenyekiti akasema;

‘Huyu mtu amefuata nini kwenye hiki kikao...?’ mwenyekiti akaniuliza mimi na kabla sijamjibu akamgeukia huyo mtu na kusema;

‘Kikao hiki hakikuhusu, hiki ni kikao cha watu maalumu, sizani kama wewe ni mmoja wa waalikwa…sina uhakika na hilo, ‘ akasema sasa akikagua majina ya wajumbe..,

‘Mhh, sioni jina lako hapa…kama unavyoona hawa ni wanafamilia, na watu maalumu...walioalikwa..’akasema mwenyekiti.

‘Lakini mimi nimealikwa pia....’akajitetea huyo mtu akigeuka kuniangalia mimi.

‘Ni nani aliyekualika, majina yote ninayo hapa, sijaona jina lako,..., kwanza wewe unatafutwa na polisi, kweli si kweli…?’ akauliza

‘Ni kweli…lakini…’akasema lakini kabla hajajitetea, mwenyekiti akaendelea kuongea

‘Na kwhiyo ukionakena hapa tutaambiwa kuwa tunamficha muhalifu, tafadhali, ondoka, usituharibie mipangilio yetu, sisi sio wavunja sheria, kumficha muhalifu ni kuvunja sheria za nchi, unalifahamu hilo...’akasema baba, na mimi nikaona niingilie kati nakusema;

‘Baba , oh mwenyekiti, mimi ndiye niliyemualika huyu mtu, nilimualika wakati nimeshakupa hayo majina ya wajumbe, kwani sikuwa na uhakika naye, kwa vile alikuwa haonekani, lakini ni mmoja wa watu muhimu kwenye hiki kikao..’nikasema

‘Binti, hilo haliwezekani, huyu ni mshukiwa wa uhalifu, anatafutwa na polis, mbona unafanya mambo yasikubalika…’akasema mwenyewekiti

‘Baba uwepo wake ni muhimu sana kwenye hiki kikao, ili aweze kutoa ushahidi, kutokana na mambo tutakayoyaongelea leo hii hapa, hatuwezi kumkosa mtu kama huyu, na nilikuwa naombea sana awepo...’nikasema na mume wangu akadakia na kusema;

‘Unasema anakuja kutoa ushahidi…!!’ akasema sasa akimuangalia mdogo wake kwa mashaka

‘Ndio…’nikasema

‘Ushahidi gani atautoa mdogo wangu, kwanza niulize kwa kauli yako hiyo , kwani hapa kuna kesi ya nani, sijaelewa hapo mke wangu, ninani kashitakiwa, eeh..anyway, vyovyote iwavyo, lakini kitu kinachomuhusu mdogo wangu nilitakiwa mimi nikifahamu kwanza..’akasema akikunja uso, kuonyesha kukerekwa.

‘Utayafahamu yote hayo baadaye, kikao hiki nimekiitisha mimi, kuna mambo mengi ambayo yatajitokeza ndani y afamilia, ambayo yanaweza kuvunja usalama na umoja wa kifamilia,.., na yeye anayafahamu zaidi yako, kwa vile wewe ulikuwa mgonjwa,....’nikasema

‘Sio kweli,… mdogo wangu hawezi kufahamu jambo, mimi nisiwe nalifahamu, mimi na yeye muda wote nikiwa mgonjwa tulikuwa tunawasiliana, je kuna kitu gani anakifahamu mimi nisikijue…?’ akauliza
‘Subiria sasa kikao kipo kwa ajili ya hili na mengine..’nikasema

‘Hapana…wewe una nia mbaya na mdogo wangu, mdogo wangu kwanini, wewe hujui umejileta kwenye mtego,…’akasema akimuangalia mdogo wake, halafu akaniangalia mimi na kusema

‘Hivi kwanini mke wangu unataka kumuingiza mdogo wangu kwenye matatizo, ni kwa vile sio damu yako, au sio.. huyu ni mdogo wangu, mimi ndiye mwenye dhamana naye, ...kama alivyosema mwenyekiti ni bora mdogo wangu uondoke hapa hahusiki kwenye hiki kikao..’akasema

‘Kwanini aondoke unaogopa nini wewe, una mashaka gani…?’ nikauliza

‘Sio swala la kuogopa, ni swala la usalama wake, mimi nafahamu, polis wakimuona hapa watakimbilia kumkamata, kabla hatujaweka mambo sawa, wao hawajafahamu ukweli ulivyo..’akasema ndugu mtu akionyesha wasiwasi.

‘Hilo nimelifanyia kazi, wewe subiria kwanza…’nikasema

‘Hakuna swala la kusubiria haoa,..nafahamu lengo lako, ni ili mdogo wangu ajitokeze polis wamkamate, ndio hivyo tu…mimi naomba aondoke tu, nitaongea naye baada ya kikao, kwanini kila mara unapenda kumuingiza mdogo wangu kwenye matatizo......’akasema mume wangu.

Muda wote huo mwenyekiti alikaa kimia, akiandika mambo yake ni kama vile hajali hayo yanayoendelea.

‘Asiondoke, hiki kikao nimekiitisha mimi, na huyu ni mmoja wapo wa shahid wyangu muhimu sana na ajenda zote za kikao ninazo hapa kama katibu, na kwa bahati mbaya sikuwawagaia ajenda za kikao hiki mapema, kwasababu maalumu..’nikasema

‘Najua wewe hujali hilo…’akasema

‘Sio kweli …, mimi sijawahi kumuingiza mdogo wako kwenye matatizo, ni wewe ndiye uliyemuingiza ndugu yako kwenye matatizo, kama tutakavyokuja kuona huko mbele… hayo yote tutayabainisha kwenye hiki kikao, na ndipo itajulikana wazi ni nani anayemjali mdogo wako..mimi au wewe…’nikasema

‘Unasema nini, mimi ndiye niliyemuingiza mdogo wangu kwenye matatizo gani, usilete hoja za kuharibu hiki kikao, kama hakinifai mimi nitaondoka zangu…’akasema sasa akiniangali a kwa mashaka

‘Huyu ni mmoja wa wajumbe muhimu kwenye hiki kikao, na kuwepo kwake hapa ni kwa ajili ya kusema ukweli, ulitokana na wewe, yeye hawezi kuondoka mpaka huo ukweli uthibitishe, na ukweli ukiwa bayana, kama ni mtu wa kwenda polisi atakwenda tu...’nikasema

‘Hapana hawezi kwenda polisi, labda mimi niende huko kama lengo lako ndio hilo, hilo halitaweza kutokea nikiwemo hapa, na kwa hili nitachukua jukumu la kumuondoa, kwani mimi ndiye mwenye mamlaka ya familia na ndugu zangu, hata mkataba wetu,wa kifamilia, unaliongelea hilo ....’akasema na kuushika mkataba mkononi, utafikiri ndio mtetezi wake.

Hapo sasa mwenyekiti akaingilia kati na kusema; ‘Hebu tusikilizane kwanza… mimi ndiye mwenye mamlaka ya hiki kikao, au sio..kwahiyo mimi ndiye nitasikilizwa…’akasema na sisi tukatulia,

‘Kwanza , mimi kama mwenyekiti sijakubaliana na kuwepo kwa huyu mtu hapa, kwani anatafutwa na polisi, mnafahamu kuwepo kwake hapa ni kuvunja sheria za nchi, na mimi ni mmojawapo wa watu wanaosimamia hilo bungeni…,na mimi sio mvunjaji wa sheria, kama mwenyekiti ninaamuru huyu mtu atoke kwenye hiki kikao...’akasema mwenyekiti.

‘Hata mimi nakuunga mkono mwenyekiti, sawa kabisa...’akasema mume wangu.

‘Mwenyekiti, naomba huyu mtu awepo, na kama ni swala la uvunjifu wa sheria, hilo tutakuja kuliona hapa, kuwepo kwake, hapa kutasaidia kuyaweka haya mambo yote sawa, na huenda tukaisaidia hata hiyo polisi kwa hayo wanayoyatafuta..’nikasema na baba akaniangalia kwa makini, na akageuka kumwangalia huyo mtu,

‘Mimi bado sijaafiki kwasababu muda uliopita niliongea na mkuu wa upelelezi wa eneo lenu nikamkatalia kabisa kuwa huyu mtu sijawahi kumuona, na nikimuona moja kwa moja nitamfikisha kwao, au nitawaita waje wamchukue, na sasa hivi napiga simu waje wamchukue...’akasema

‘Usifanye hivyo baba tafadhali, huyu ni mdogo wangu, na mimi ndiye nabeba dhamana naye, kama polisi wanamuhitaji kwanza waje kuonana na mimi,...mdogo wangu hana hatia, kama wanavyodai wao, wanamuhisi tu..mimi ndiye niliyesababisha aonekane hivyo...’akasema.

‘Umekumbuka hayo eeh…’nikasema na hapo akatikisa kichwa kama kuchanganyikiwa halafu akasema, akiniangalia mimi kwa hasira

‘Wewe ndiye uliyesababisha yote haya hdi mdogo wangu kushukiwa uhalafu ambao hajawahi kuufanya,..basi polisi wakija utawaambai hivyo, lakini kuwepo kwake hapa ni ukiukwaji wa sheria....’akasema baba.

‘Baba usijali tuendelee na kikao, mwenyewe utakuja kuona umuhimu wake, kama nilivyokuambia, niamini, nisingemuita hapa kama asingelikuwa ni mtu muhimu sana kwenye hiki kikao, je hutaki kujua jinsi gani vitu vyangu vilipotea, hutaki huo ushahidi uwe bayana ...’nikasema na baba akasema;

‘Sawa mimi naendelea na kikao, lakini msimamo wangu ni huo huo, huyu mtu atoke nje, mimi kama mwenyekiti wa kikao sikumruhusu awemo kwenye hiki kikao...na kwa vile nimemuona, nitawapigia polisi waje wamchukue..siwezi kwenda kinyume na sheria...’akasema

Mdogo mtu akawa bado kasimama akishindwa kuondoka, na mwenyekiti akasema;

‘Kwanza mume wako kasema kuwa nyie katika familia yenu mna katiba, na Katiba hiyo ndiyo inayowaongoza,..naona katika ajenda zako katibu, hilo swala la katiba umeliweka kuwa la kwanza, na mume wako keshalianza, naona tuanze na hicho kipengele, tusipoteze muda…’akasema sasa akindika kitu kwenye simu yake.

‘Sawa lakini….’akasema mume wangu na kabla hajamaliza mwenyekiti akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Hebu niambieni kwanini mliamua kuanzisha katiba kama hiyo, hata mimi mwenyewe sina kitu kama hicho, labda itatusaidia na sisi …? Akauliza mwenyekiti, na mume wangu akasema;

‘Nafahamu kuwa swali hilo limemlenga mke wangu,kwa vile ndiye mwenye hiki kikao, na ndiye alitakiwa ataje ajenda zake, na bahati mbaya , kikao kimeanza juu kwa juu, kutokana na hili lilitokea, ...ni kweli ndugu mwenyekiti, katika familia yangu, nikiwa na maana mimi na mke wangu na watoto, tuna katiba yetu inayotuongoza....’akatulia kidogo akiishika ile katiba.

‘Kwanini tuliamau kuwa na katiba, ….kiukweli ni wazo la mke wangu , hata mimi nikalipenda sana….kwanza tulitaka familia yetu iongozwe kitaalamu zaidi, ...’ akageuka kuniangalia mimi

‘Lakini sababu kubwa ya kimsingi ni kuwa tulijiona kuwa tuna mambo mengi, mimi nikiwa nashughulika kwenye kampuni yangu, na mke wangu kwenye kampuni yake,lakini vyote hivyo ni vyetu, japokuwa kitaalamu kutokana na hisa kila mmoja alikuwa na mamlaka na kampuni yake...’akatulia

‘Kwa vyovyote iwavyo, mnapo-oana, hata kama mke alikuwa na vitu vyake, kampuni yake, mali yake, lakini akishakuwa mke wa mtu, basi kila kitu chake kinakuwa kwenye mikono ya mume kama kiongozi wa familia au sio....na hili tumelibainisha kwenye katiba yetu, ili kuondoa migongano, tukaona jambo nzuri ni kuwa na katiba....’akasema akitaka kufungua hiyo katiba.

Mwenyekiti akasema;

‘Mhh, usifungue hiyo katiba kwanza, nilichotaka mimi ni kufahamu ni kwanini mliamua kuanzisha hiyo katiba, na kwa ufupi tumeelewa hilo...swali langu la pili, je katiba hiyo imesajiliwa kisheria au ni katiba yenu tu kwa ajili ya mambo yenu ya ndani?’ akauliza

‘Sisi baba, eeh, ndugu mwenyekiti, kila kitu tumekipeleka kitaalamu, katiba yetu hii imesajiliwa, na aliyeiandika ni mwanasheria, kwahiyo katiba yetu ni kisheria, imetimiza matwakwa yote ya kisheria, ..hatuna matatizo na hilo....’akasema

‘Kwahiyo unataka kusema kila kitu chenu, taratibu zenu za kila siku mlidhamiria ikiwezekana, kifuate taratibu kama mlivyoanisha kwenye katiba yenu hiyo…, na likitokea tatizo, mnahukumiana kutokana na katiba yenu hiyo au sio?’ akaulizwa

‘Ndio mwenyekiti, ndio maana nashangaa kikao hiki, kuitishwa na mke wangu, nilitakiwa mimi ndiye nikiitishe, lakini kuna dharura kama hizo, siwezi kuktaa, au sio mke wangu…’akasema akinigeukia na mimi nikabakia kimia tu

‘Kama ikitokea dharura,basi mmojawapo anaweza kuitisha kikao, lakini ilitakiwa mimi niambiwe kila kitu kwanza…, kwanini kikao kiwepo, lakini mmh, kwa bahati mbaya kwa hili, silaumu, lakini halikufuata utaratibu...nimeshitukiziwa tu, kuwa kuna kikao, cha nini na kwanini, sijaambiwa, huo ni ukiukwaji wa katiba, ila tuliache tu hivyo, tupo pamoja...’akasema

‘Sawa kama imeshtukizwa tu ni makosa, na katibu wako atawajibika kuelezea ni kwanini…’akasema akiniangalia mimi, na mimi nikatikisa kichwa kukubaliana na hilo,…Na mume wangu akadakia kwa kusema;

‘Ndugu mwenyekiti naomba niongee kidogo kuhusu hii katiba, samahani sana, kwani mimi ndio mwenye mamlaka, na kiongozi wa familia yangu, na kwahiyo nina mamlaka ya kuona kila kitu kinaenda sawa...na hilo lipo kwenye katiba…’akasema na mwenyekiti akageuka kuniangalia, mimi nikamuashiria amuache mume wangu aendelee

‘Watu wanapofunga ndoa, wanakuwa na taratibu zao, kama mke na mume, na wanakuwa wameshajitoa kwenye mamlaka ya baba na mama zao, hawalindwi au kuchungwa tena na familia za baba na mama zao, kikeni au kiumeni, wao ni watu huru, na wanakuwa na utaratibu wao kama familia inayojitegemea, au sio …’akasema kama anauliza

‘Na ndivyo tulivyofanya sisi, na kwa ajili ya kurahisisha mambo yetu tukaona tuwe na katiba, ni wachache sana wanakuwa na utaratibu kama huo, ni tendo la ajabu lakini sis imetusaidia sana, ningeshauri kila familia iwe nayo....’akasema mume wangu.

‘Hii katiba imesajiliwa kisheria, kwasababu imeandikwa na mwanasheri a wa familia, yetu, na sote tukaweka sahihi zetu, mimi na mke wangu, na wakili wetu. Sio katiba ya mitaani , ni Katiba iliyokubalika kisheria, ukiangalia hapa ina kila sifa zote za kisheria, ...mimi kama kiongozi wa familia kwa kupitia hii katiba ninaweza kumshitaki yoyote atakayeingilia au kuingilia mambo yetu ya ndani....’akasema.

Aliposema hivyo akamuangalia mwenyekiti na mwenyekiti akawa naye kamkazia macho, halafu akageuka kuniangalia mimi….

‘Kwahiyo itakuwa ni ajabu kama mtu atakuja na kuingilia familia yangu,wakati yeye ana familia yake, ni ajabu kabisa, labda kuwe na jambo, na jambo hilo liwe wazi kwa kiongozi wa familia ambaye ni mume wa familia, au sio, huo ndio utaratibu, na ndivyo ilivyo kwenye hii katiba .....’akasema na mwenyekiti kwanza akatabasamu, maana aliona hizo shutuma zinaelekezwa kwake, akauliza

‘Hiyo Katiba yenu iliandikwa lini?’ akauliza mwenyekiti

‘Muda mrefu sana, kipindi wakati watoto wetu ni wachanga tu…, imeshafanya kazi zaidi ya miaka tisa, au sio mke wangu, kwahiyo sio kitu kigeni ndani ya familia yangu...’akasema

‘Naomba niione hiyo katiba..’akasema mwenyekiti, na mume wangu akasimama huku akiwa kashika ile katiba na kwa madaha, akaelekea pale alipokaa mwenyekiti kumkabidhi hiyo katiba, na wakati huo shemeji yangu alikuwa bado kasimama, alikuwa hajafahamu kuwa akae au aondoke, na mimi nikamuonyeshea ishara kuwa akae kwenye kiti. Na mwenyekiti akamuona , na haraka mwenyekiti akasema;

‘Mimi sijakuruhusu ukae, mimi bado sijakukubalia na uwepo wako kwenye hiki kikao, kama mwenyekiti siwezi kukaa kwenye kikao kinachovunja sheria, nimeshasema huyu mtu anatafutwa na polisi, kuwepo kwake hapa ni uvunjifu wa sheria....’akasema mwenyekiti sasa akiangalia kitu kwenye simu yake, na mimi nikasema;

‘Mwenyekiti nakuomba uniamini, huyu mtu ni mtu muhimu sana kwenye hiki kikao nakuomba umruhusu awepo, na kama ni uvunjifu wa sheria mimi nitalijibu hilo, ...’nikasema.

‘Mimi nakubaliana na mwenyekiti, ndugu yangu huyu atoke nje, kwanini mke wangu unamkaidi mwenyekiti, unaona ilivyo vigumu kwenye familia yangu, silaumu lakini hili halikubaliki, kiongozi ni kiongozi lazima aheshimiwe bila kujali ni nani, sasa na mimi ni kaka yake nipo hapa, nitawakilisha mawazo yake, kwanini ung’an’ganie awepo apa, au unataka polisi waje wamkamate...’akasema na kuongeza kusema;

‘Nina maana muhimu sana, …na ni muhimu sana kuwepo hapa, najua ni kwanini hutaki awepo hapa…’nikasema

‘Mke wangu umekuwa ukimuandama sana mdogo wangu, sijui kwanini,kama kuna lolote dhidi yangu niambie mimi mwenyewe…, na sio kumtumia mdogo wangu kinyemela,mimi sipendi, kama kaka yake ninaamuru atoke kwenye hiki kikao, mimi nitawakilisha mawazo yake kama kuna umuhimu huo, ni kwa usalama wake kwa sasa, mengine aniachie mimi ...’akasema mume wangu.

‘Hata mimi sioni umuhimu wake hapa, maana anatafutwa na polisi akionekana hapa itaonekana kuwa tunamficha sisi, au ngoja tulimalize hili, ngoja ofiswa wa upelelezi aje amchukue,...’baba akasema huku akinua simu yake kumpigia huyo mtu wa usalama

‘Baba tafadhali utaharibu kila kitu, nilishakuomba kuwa unipe nafasi nifanye nionavyo mimi ni sawa… , kama utamuita huyo ofisa wa polisi utaharibu kila kitu, naomba tafadhali endelea na kikao chako, muda utafika , utaona ni kwanini nimeamua awepo hapa kwenye kikao hiki...’nikasema,

‘Wewe unataka tufanye kikao kisicho fuata taratibu, unanielewa sheria za nchi zilivyo, unaelewa mamlaka niliyo nayo..unataka wapinzani wangu wapate cha kuongea..’mwenyekiti akasema;

Mdogo wa mume wangu, alipoona malumbano dhidi yake yanapamba moto, akaona aingilie kati mwenyewe, akasema;

‘Tafadhali mzee wetu, na wajumbe wote wa kikao hiki,mimi naomba mnipe muda, niongee kilichonileta hapa, na baadaye kama unaona nimevunja sheria, basi utampigia huyo mtu wa usalama, aje anichukue, mimi siogopi kukamatwa kwa hivi sasa, ..kwa vile nimeshathibitisha kile nilichokuwa nikikichunguza, na kumgundua muuaji wa Makabrasha,...

‘Nini…wewe unasema nini, acha kuongea haya hapa,…utaharibu!!’ ayetamka hivyo na hata kusimama alikuwa mume wangu.

‘Mimi kuja kwangu hapa,ni kusema ukweli…’akasema na kiukweli hapo kila mtu akabakia kimia, kumsikiliza yeye hasa hapo aliposema keshampata muuaji wa Makabrasha.

‘Pamoja na mengine, nafahamu kuwa askari polis wananitafuta mimi kuthibitisha kuwa kweli kaka ndiye muuaji,..’akasema

‘Hapana sio kweli…kaka yangu sio muuaji..’akasema

‘Mimi sijaua…ni uwongo wao tu..’akasema mume wangu

‘Ndio hivyo kaka,..ndio maana mimi nataka nilithibitishe hilo mbele ya hiki kikao, kuwa wewe hujamuua Makabrasha…’aliposema hivyo, kaka mtu akakaa kwenye kiti sasa akipumua kidogo.

‘Lengo langu hadi kufika hii leo hapa, ni kumtetea kaka yangu, kwani kuna mipango ilipangwa dhidi yake, yeye hafahamu tu…, kuwa kuna watu walioshirikiana kumuua Makabrasha, na kwa vile wanataka wasikamatwe, wameona kosa hilo wambambikie yeye, kaka yangu, bila ya hata yeye kufahamu, ...’akasema na kaka yake akabakia kuduwaa,

‘Mimi nina ushaidi kuwa kaka hajamuua Makabrasha, na wala hajui ni kitu gani kilitokea siku ile, yeye kwanza alikuwa mgonjwa, na pili, aliyemuua, alikuja bila ya kaka kufahamu kinachoendelea, alitokea kwa nyuma wakati yeye kaka akiongea na marehemu na huyo mtu alikimbia..kwahiyo kaka hafahamu lolote kuhus huyo mtu, na kwanini ilitokea hivyo..’akasema na kaka mtu akataka kumzuia mdogo wake asiendelee kuongea.

‘Inatosha, usiseme kilakitu,…’akasema kaka mtu

‘Kaka nakuomba utulie , nataka kuongea haya kwa masilahi yako, na masilahi ya wote waliohusika, kwasababu nimeona huk o tunapokwenda ni kubaya kuliko mnavyofikiria nyie…, na hayo yaliyopangwa dhidi yako, au yenu, yatakutia matatani kaka, yataharibu familia yako, na kashfa itasambazwa kila mahali..’akasema na kaka yake akamsogelea na kumshika mkono na kusema;

‘Mdogo wangu hayo sio ya kuongea hapa, tutakuja kuyaongea tukiwa wawili, wewe toka nje ya kikao,...’akasema huku akimshika mdogo wake mkono, ili watoke naye nje...mwenyekiti alipooa hivyo akasema;

‘Naomba mtulie mimi ndiye mwenyekiti wa kikao, nimeshamfahamisha mkuu wa upelelezi, amesema tuendelee na kikao, lakini kikao kikisha, huyu mtu tunatakiwa tumkabidhi kwake, kwahiyo kuanzia sasa upo mikononi mwa polisi mimi siwezi kuvunja sheria kwa ajili ya kumfurahisha mtu yoyote, hata akiwa mwanangu,mimi nafuata sheria na taratibu zilikubalika ....’akasema

‘Kwahiyo mimi sihitajiki tena kusema ukweli ambao nilitarajia kuusema?’ akauliza shemeji yangu.

‘Ukitaka kuusema sawa, sasa hivi upo huru kusema, maana wenyewe wameshatambua kuwa upo hapa, na ukweli gani ulio nao ambao ni tofauti na ukweli ninaoufahamu mimi, hayo unayotaka kuyasema , na jinsi ulivyoelezea hapo, ni mbinu tu ya kuficha ukweli halisi…ni jinsi nyingine ya kumtetea kaka yako kiujanja unjana, na mimi sikubaliani na hilo....maana ushahidi wote ninao hapa...’akasema baba.

‘Baba labda tufuate utaratibu wa kikao chetu, wewe endelea na kikao, ukifika muda wake wa kuongea ataongea, na ukweli utajionyesha, labda tuanze na ajenda zetu kama zilivyojipanga, kama tulivyoanza awali, tulikuwa tukiongelea kuhusu katiba,,...au sio mwenyekiti…’nikasema.

‘Utaratibu kama huu siutaki, mnasikia, … sawa tuendelee na kikao, na kijana upo chini ya ulinzi, kuanzia sasa, ...’akasema mwenyekiti kwa hasira.

Kikao kikaendelea kwa namna hiyo…Karibuni kikaoni..

WAZO LA LEO: Taratibu na sheria zilizowekwa zina umuhimu wake kwenye jamii husika, na jamii hiyo inatakiwa kuzifuata hizi sheria na taratibu zilikubalika, ili kuzuia uvunjufu wa amani. Watu wakianza kutafuta uchochoro wa kuzikweka sheria hizo kwa visingizio mbali mbali, malengo na dhamira ya kweli hupotea, na matokea yake ni fujo … Sheria au taratibu zinatakiwe ziwe kwa masilahi ya jamii, na sio kwa ajili ya kuwakandamiza wanyonge.
 
SEHEMU YA 92


Kikao kiliendelea, na mwenyekiti akawa mkali kidogo, kabla ya kusoma dondoo nyingine za kikao, akasema;

‘Ninataka hili niliweke hili wazi, siku nyingine mkiniita kwenye vikao vyenu, sitaki kuona kitu kama hiki, kwanza mumechelewa kufika, mimi kama mwenyekiti natoa onyo, sipendi tabia hiyo itokee tena, mkiniita kwenye kikao chenu mjipange vyema, muda ni mali, sina muda wa kupoteza…’akasema baba

‘Samahani kwa hilo mwenyekiti…’nikasema

‘Sijatoa nafasi ya mtu kuongea…’akasema na mimi nikabakia kimia

‘Pili sitaki mambo kama haya ya watu kujitokeza katikati ya kikao bila mipangilio, na tatu kikao kama hiki mkinichagua mimi kama mwenyekiti wenu, sitaki mtu kujiona yeye yupo juu yangu, mimi ndiye mwenye mamlaka ya kikao hiki, mambo ya familia zenu mnayaweka pembeni...mnanielewa …’akasema.

‘Sawa, lakini mzee, naweza kujitetea kwa hilo…’akasema mume wangu

‘Sijataka mtu kujitetea…’akasema na mume wangu akabakia kimia

‘Naona wewe mjumbe unataka kuongea sana, au nikupishe wewe uje hapa,..siolazima mimi niwe mwenyekiti..na kujitetea, unajitetea nini, kwani mimi nimesema nataka kutoa adhabu leo, ninachotaka kukiweka wazi ndio hicho, unasikia mkwe…na hapa sio mkwe, wewe ni mjumbe wa hiki kikao, au sio…’akasema mwenyekiti

‘Ndio nimekuelewa baba mkwe…, nilitaka tu, nikuelekeze kitu kwenye hiyo katiba…’akasema na mwenyekiti akaiangalia ile katiba halafu akaisogeza pembeni na kusema;

‘Hapa hatuongozwi na hii katiba yako,…maana sisi hatuijui, au nimekosea wajumbe, au niwaulize wajumbe je mnaifahamu hii katiba..?’ akauliza na wajumbe wakakaa kimia, na ndipo akaanza kuuliza mtu mmoja mmoja…

‘Docta na mkewe, mnaiafahamu hii katiba…?’ akauliza mwenyekiti

‘Hatuifahamu ndugu mwenyekiti…’akasema docta, na mkewe akabakia kimia.

‘Na…nimuulize na nani, haya wewe uliyetuingilia kwenye hiki kikao, nikuulize wewe unaifahamu hii katiba…?’ akaulizwa shemeji mtu

‘Mhh..naifahamu kwa mantiki…’akatulia

‘Ongea, usiwe na wasiwasi, nimekuuliza … kwa hivi sasa unaweza kuongea tu…haya kwa mantiki gani..?’akaambiwa na kuulizwa.

‘Naifahamu kwa vile nimemuona kaka akiwa nayo…’akasema

‘Ukajua kuwa ni katiba , au kwa vile imendikwa hapa juu, …Je yaliyoandikwa ndani unayafahamu, yanakuhusu wewe..umeshawahi kuyasoma..?’ akaulizwa

‘Hayanihusu, siku-ya-yasoma kwa sababu hayanihusu…’akasema

‘Kabla ya kaka yako kuionyesha hii katiba hapa, uliwahi kuiona wapi kabla…?’ akaulizwa

‘Mhh…niliwahi kutumwa na kaka, …kuichukua nyumbani na kumpelekea hospitalini…’akasema

‘Kwanini alikutuma wewe…?’ akaulizwa na kukaa kimia

‘Nduguzanguni, ninachotaka kukielezea hapa, ni jinsi gani katiba hii isivyowahusu watu wengine, zaidi ya familia husika,… haya ya kwanini…kukuhusu wewe bwana mdogo yatakuja baadae maana mpaka hapo nimegundua jambo….wewe ndiye unayetumwa kila kitu na kaka yako, au sio…?’ akaulizwa

‘Sio kila kitu mwenyekiti,..ila mara nyingi ananituma…’akasema

‘Kwahiyo wewe umeifahamu hii katiba kwa kutumwa, na sio kuwa inakuhusu au sio..?’ akaulizwa

‘Ndio mzee, …hainihusu…’akasema

‘Je kwenye kikao hiki inastahiki kutumiwa..kuongoza hiki kikao, ..?’ akaulizwa

‘Hapana mzee, nionavyo mimi, hiyo ni katiba ya wanafamilia, na sisi wengine haituhusu, natumai hilo ni jibu la wote, au sio …’akasema na wajumbe wakatikisa kichwa kukubaliana na hilo

‘Sawa kabisa, kumbe kweli unaifahamu kuwa ni ya wanafamilia, na huenda unaifahamu zaidi ya hilo…mmh, mawakili, nyie kwanza siwaulizi hili, hata mke wangu hapa simuulize maana yeye yupo na mimi, au nikuulize mke wangu,…’akasema akimgeukia mama

‘Hapana endelea tu mwenyekiti, tujali muda…’akasema mama, na baba hapo akanigeukia mimi akitaka kuniuliza lakini akaghairi na kugeukia kikao, akasema;

‘Tujali muda, msaidizi wangu wa nyumbani kaniasa hilo, haya tuliache hilo kwanza, ..nilitaka ndugu mjumbe, mume wa familia kuliweka hili sawa, kuwa kuna mambo ya kurejea katiba yako ni sawa…, na kuna mambo ambayo hayastahiki, na hili la kuongoza hiki kikao, halihitaji katiba yenu, katiba ya hapa ni dondoo za kikao na mimi mwenyekiti ndiye ninayeziongoza hizo, au sio…’akasema mwenyekiti

‘Sawa mwenyekiti nimekuelewa…’akasema mume wangu na alitaka kuongeza neno, lakini mwenyekiti hakumpatia nafasi,…

‘Kingine kuna mambo nataka kuyaweka wazi, ndio mna katiba mna utaratibu wenu wa kimaisha kama familia ni sawa pia…, mimi sikatai, na nimefurahi kama mlifikia hatua hiyo,lakini ninataka niwarejeshe nyuma kidogo, niwakumbushe, nyie wanandoa….’akasema na kumgeukia mume wangu

‘Nilishasema kwenye familia yetu hatutaki mambo ya kashifa, ikiwemo kuvunja sheria za ndoa na za nchi, na kuvunja sheria ni swala pana zaidi, ni pamoja na uwongo, kusalitiana, na kugushi, na mambo kama hayo, ..mambo ambayo yanatuharibia jina letu,achilia mbali kuua, ambalo ni kosa la jinai ....hilo niliwakanya tangu mapema, na nilisema hata kama ni mtoto wangu kafanya hayo, sitasita kumfikisha kunakostahili..

Nilifanya hilo kwa binti yangu, niliposika kakamatwa, sikukimbilia kumtoa, nilifanya uachunguzi wangu ili niupate ukweli, sijamlea binti yangu awe mvunjifu wa sheria,..hilo najisifu…sasa kama akitaka kunisaliti na mimi nitawajibika kwa hilo..hakuua, na ndioa maana nilimsaidia…’akatulia,

‘Sasa kwako wewe mume wa familia,…’akasema

‘Ndio mwenyekiti, nakusikia….’akasema mume wangu

‘Ni kwanini hayo, ni kwanini niliwaasa mapema hilo jambo…’akasema halafu akatoa gezeti, na kulikabidhi kwa mume wangu

‘Hebu soma hicho kichwa cha habari hapo juu…’ akaambiwa mume wangu na akawa anasita kulipokea, halafu akalipokea, na kusoma

‘Mkwe wa familia ya mzeemkongwe wa siasa,(akataja jina) anashukiwa kwa mauaji ya wakili wake…’akaliachia lile gazeti kama kashika kitu kichafu

‘Sio kweli mzee, waongo hawa, watu wa udaku hawa…’akasema

‘Hebu soma na hili…’kampa gezeti jingine

‘Mkwe wa…’akasoma hivyo tu na kuliweka pembeni, akasema

‘Ina maana mzee unaamini haya magazeti, haya hayakufai mzee…;akasema

‘Hebu nikuulize mimi ni baba yako…?’ akauliza mwenyekiti

‘Ni baba mkwe, mwenyekiti..’akasema

‘Kwanini hao watu wa magazeti hawajaandika, jina lako na baba yako, wakaandika mkwe wa…unaelewa mantiki yake..?’ akauliza

‘Ni magazeti ya udaku hayo tu mzee…’akasema

‘Hujanijibu, hata kama ni ya udaku lakini yanasoma na watu wengi kuliko hayo magazeti mengine,…nimekupati hayo magazeti kama mfano…kukuonyesha ni kwanini, ..nilikuasa mapema kabla hujaoa kwangu..’akatulia

‘Ni kwasababu mimi nipo kwenye ulingo wa kisiasa…silifichi hili, kuwa katika siasa kuna upinzani, na kila mmoja anajaribu kutafuta kashfa za mwenzake..ili afanikiwe kwenye ulingo wa siasa, hilo linakubalika, kisiasa, ndio maana najihami, na wenye lengo jema na mimi watanisaidia kwa hilo, mumenielewa jamani, mimi naongea sana …’akatulia

‘Lakini baba hayo ni maswala yako, na sisi hatuwezi kuyaingilia…au sio jamani..’akasema mume wangu.

‘Ndio maana ulipokuja kuoa kwangu nilikuambia hilo mapema tu, kuwa mimi nipo hivyo, na maisha yenu yawe vipi..na hayo maisha yenu, kuwa vipi sio kwamba nawataka muwe kama mimi, hapana, niliwatahdaharisha kuwa ningelipenda maisha yenu yawe mfani wa mume na mke bora…kweli si kweli…?’ akaulizwa

‘Ni kweli mzee…’akasema

‘Sasa tatizo lipo wapi, nimekosea nini hapo, kuyakemea hayo yanayokwenda kinyume na maadili ya mke na mume bora, nimekosea nin kuyakemea maovu, ..sitaki kashfa, na nilisema kama mtu hataliweza hilo, asioe kwangu, hata binti yangu nilimuwambia kama mume wako ..hana maadili mema, usikubali akuoe, akasema , atahakikisha mume wake yupo kwenye njia sahihi, kweli si kweli…’akasema na kuniuliza mimi, na kabla sijajibu mimi, mume wangu akasema;

‘Ni kweli mzee, mke wangu kanisaidia sana, na tunaishi vyema tu…mengine ni udhaifu tu wa kibinadamu…’akasema.

‘Sasa mimi nisingelikaa kimia tu, mfanye mtakavyo, na baadae mje kunisema kwanini mimi sikuwahi kuwaambia hilo, je sikukuambia hilo mapema, wakati unakuja kuoa kwangu…?’ akauliza mwenyekiti kumuuliza mume wangu

‘Uliniambia mzee…lakini..’akasema mume wangu

‘Sitaki lakini, huko kujitetea kuwa ni udhaifu wa kibinadamu, sio utetezi, ufanye makusudi halafu usingizie ubinadamu, hakuna hilo..unasikia

‘Sasa…kama kuna kujitetea utakuja kujitetea sana…au kama unataka kujitetea, basi nikuuliza ni kwanini umeyapinga hayo maagizo yangu, Ulidharau sio …kwa vile sasa una mamlaka kama ulivyoanza kunialati ..kuwa mna katiba inayokulinda…?’ akauliza

‘Hatujayapinga maagizo yako mzee, labda ni katika kuwekana sawa tu, au kuwajibika kama limetokea hilo ni kwa bahati mbaya tu mzee, na kashafa gani kubwa tumefanya sisi, kwangu mimi sijaiona, ni mambo ya uzushi tu..’akasema

‘Kufikia hadi kuua, sio kashfa…?’ akaulizwa

‘Mzee nani kaua, hakuna mtu aliyeua hapa,..huo ni uzushi, na polisi wanafanya hivyo kikamata watu katika kuhangaika kumpata muhalifu, lakini sio kweli…’akasema

‘Kutoka nje ya ndoa na kuzaa ovyo sio kashfa…?’ akauliza mzee

‘Aaah, huko mzee umeenda mbali, ..hapana mzee, ni maneno ya watu tu, waongo hao…’akasema

‘Una uhakika na hilo jibu lako..?’ akauliza mzee

‘Kwanini mzee unauliza hivyo, mke wangu hajafanya hilo, walimfunga kimakosa, wakimshuku kuwa ameua, na sio kweli, hata wewe mwenyewe umelithibitisha hilo…’akasema

‘Sijamuulize mke wako, nimekuuliza wewe, uliyekuja kuoa kwangu, umesema hujafanya kashafa kubwa, au sio,…na unavyoonekana kuzaa nje kwako sio kashfa, anyway…mimi najaribu kukuweka sawa hapo, au wewe kashafa kwako ni ipi, ya wizi, ya kuhujumu au nini kashafa kwako…?’ akauliza

‘Mzee mimi sijafanya kashafa kubwa kihivyo, ya kukuharibia mambo yako kisiasa ndio utetezi wangu huo…’akasema

‘Haya mume wa familia, ngoja tutakuja kuliona hilo…,’akasema mwenyekiti

‘Sawa mzee nitajitetea kwa shutuma zote, nina imani utakuja kunielewa…’akasema

‘Ngoja tusipoteze muda, twende kwa mujibu wa utaratibu wa kikao, dondoo zinasema sasa ni wakati wa kumkaribisha mwenyeji wa kikao, mtu aliyetuita hapa kwenye kikao, kuelezea duku duku lake, lakini kabla sijamkaribisha, nataka yeye anipe maelezo sahihi, maana yeye amekuwa muda wote akitetea ndoa yake, mume wake nk..sasa nataka haya uyaweke wazi, pamoja na hayo uliyotuitia…’akatulia kwanza akiniangalia mimi, halafu mume wangu

‘Ni kwanini sisi wazazi wenu tusiingilie familia yenu, wakati mumeshaingilia familia kuu, kwa matendo yenu yenye kashfa, ushahidi mmojawapo ni hayo magazeti, ina maana mumefanya mambo ambayo yamekiuka yale makubaliano yetu ya awali…ni kwanini sisi kama wanafamilia kuu tusichukue maamuzi, tuliyoona ni sahihi, kwa masilahi ya familia na vizazi vijavyo,…hili ni muhimu.’akasema mwenyekiti na mume wangu akawa anataka kuongea

‘Tulia…’mwenyekiti akasema na mume wangu akatulia.

‘Ni kwanini nyie watoto mnatengeneza katiba ya kutuzuia sisi wazazi wenu tusiwaingilie hata kama mumeshindwa kutimiza wajibu wenu ndani ya familia zenu, sitaki kusema yapi ni yapi mumeyakiuka, lakini kwa ujumla wake, mumetia doa familia yetu, haijawahi kutokea hivyo kabla, je ni kwanini, na kuna nini...’akasema na kuniangalia mimi, kabla sijasema kitu, mume wangu akanyosha mkono na hata kabla hajaruhusiwa akasema;

‘Mimi kama mume wa familia inayoshutumiwa kwa kukiuka hayo aliyosema baba, nataka kuelezea ni kwanini hayo yalitokea, naomba niongee mimi kwanza kabla hajaanza kuongea mke wangu japokuwa ni yeye aliyeitisha hiki kikao,....’akasema na baba, akataka kumkatiza lakini mimi nikasema;

‘Mwenyekiti, hebu muache kwanza aongee amalize yote…na akimaliza mimi nitaongea tu...’nikasema

‘Kikao ni lazima kiwe na mpangilio, sio kwamba mimi sifahamu hilo, kuwa wewe ni mume wako familia, hata mimi ni mume wa familia, tena ni baba mkwe wako, au wewe ni familia special,..mmh, …’akasema mwenyekiti kwa ukali

‘Hapana mzee…nilitaka kujibu shutuma zako mzee…’akasema

‘Hiki kikao sio wewe uliyekiitisha, tumeitwa na mke wako, na hii ipo kwenye ajenda ...na kama nilitaka wewe uongee, ningelikupa hiyo nafasi, sipendi kabisa huo utaratibu wako…’akasema mwenyekiti

‘Na nikuambie kitu,.., heshima ni muhimu sana,..sawa kwa vile mke wako kakuruhusu uongee, sijui labda ni heshima au ni kwa mujibu wa katiba yenu kuwa hawezi kuongea mke mpaka wewe umnyoshee njia, …haya ongea kama ulivyotaka wewe, maana kila hatua mnazidi kunionyesha jinsi gani mlivyo....’akasema baba na mume wangu bila kujali akasema;

‘Nakubali kuwa kuna udhaifu ulitokea, na hilo linaweza kutokea kwa yoyote yule, hasa mnapokuwa katika harakati za kutafuta maisha, kuna changamoto za hapa na pale,..huenda katika kuyafanikisha hayo tulijaribu njia ambayo sio stahiki, ...ni katika kujaribu, ndio tukajikuta tumeteleza,..naomba tusamehewe kwa hilo...’akasema.

‘Lakini, pamoja na hayo, mimi nimeshaitoa katiba yetu, ambayo inanilinda mimi jamani, sifanyi haya kwa vile..hapana ni kwa mujibu , ndio maana nikaitoa hiyo katiba hataka kama haiwahusu wote, lakini kikao hiki kinahusu familia husika …samahani kwa hilo mwenyekiti maana mimi nitakuwa narejea mara kwa mara hiyo katiba, kwa mantiki ya kulinda familia yangu…’akasema

‘Endelea…’akasema mwenyekiti

‘Kama kuna kitu kinaitwa makosa,au kashfa imefanyika, ..kama nilifanya mimi, basi ujue nilifanya kwa nia njema tu, na kama nilitenda jambo fulani, kama mume, nina haki zangu, kisheria...na nilifanya mengine kwa minajili ya msilahi ya familia, hatujui kama linakizana na wewe kisiasa, sijui mimi kama hayo ni kashfa..’akatulia

‘Endelea…’mwenyekiti akasema alipoona mjumbe yupo kimia kidogo

‘Na ningelipenda kuliweka hili wazi kwa nia njema tu kuwa, sisi kama familia tuna sheria na taratibu zetu, kwa vile ni familia inayojitegemea, kama mtaona tumekwenda kombo, ni swala la kutushauri tu, na sio kutuingilia kiasi cha kutoa hata adhabu,...’akasema

‘Endelea…’akasema mwenyekiti

‘Mwenyekiti, katiba yetu ipo wazi, inatulinda, inanilinda mimi kama mume wa familia, naomba hilo liwekwe bayana, hakuna familia nyingine yenye mamlaka ya kutuingilia, au kutuadhibu sisi kinyume na hiyo katiba, hakuna…sheria hiyo, hivi mimi kweli naweza kuja kuingilia familia yako mzee, hakuna kitu kama hicho..nachukulia mfano huo sio kwa kukosa adabu naomba nieleweke hivyo...’akasema na kukaa kimia

‘Umemaliza...?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, nilitaka kuliweka hilo wazi tu, maana nimeona ukitoa vitisho kwenye utangulizi wako..’akasema

‘Sio vitisho mjumbe…, hayo niliyoongea ni kweli na yatafanyika hivyo…’akasema mwenyekiti

‘Itabidi nimuite wakili wangu kwa hilo…’akasema mume wangu

‘Wa nini..?’ akauliza mwenyekit

‘Unavunja katiba yangu na familia yangu…’akasema

‘Wapi nimevunja katiba yako..?’ akaulizwa

‘Unatoa lugha za vitisho, kuwa nyie kama familia kuu mnaweza kutuwajibisha, ..na vitu kama hivyo, hilo halikubaliki…’akasema

‘Usitupotezee muda, na katiba yako, hii ambayo bado sijaimini, …’akasema

‘Ukisema hivyo mzee utakuwa unatuingilia, na kuvunja kanuni na sheria za nchi, katiba hiyo, inatambulikana maana tumeisajili …au unaniona mimi sifai kuwa mume wa familia…?’ akauliza

‘Sikiliza mume wa familia, ni matendo yako.. , kama ulikubali kuoa kwangu, ujue una wajibu wa kutunza heshima yangu, sio kwamba nakuingilia, ...na sina haja ya kukuingilia, ila kama umevuka mipaka sitasita kukuwajibisha, kama umefanya mambo yenye kuleta kashfa kwenye familia hilo sitalivumilia kamwe, umenisikia, ilibidi mliweke hilo kwenye katiba yenu, maana ndio katiba ya awali wakati unaoa kwangu..’akasema mwenyekiti.

‘Katiba ya familia yangu inanilinda ndugu mwenyekiti samahani sana kwa hilo, mtaniona napoteza muda kwa hilo, lakini ni lazima hilo lieleweke maana nafahamu ni nini kinachofuatia,..mimi sitakubali jambo lolote liende kinyume na katiba yetu ya familia, lije livuruge ndoa yangu, sitakubaliana na hilo..’akasema mume wangu, na mwenyekiti akaichukau ile katiba na kuinua juu na kuuliza

‘Hii ndio Katiba unayosema inakulinda?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, hebu gauze huku, ehee, ndio hiyo hiyo...’akasema mume wangu.

‘Katika katiba yenu halali,…sijui kama ni hii, mlikubaliana kuwa kila kilichoandikwa kitasimamiwa, kitatekelezwa, na sheria itafuata mkondo wake, si ndio hivyo, kama mmoja akikosea, kutokana na mlivyokubalia atawajibishwa kisheria, hata kama ni kuvunjika kwa ndoa..., au sio?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio…hahaha, kumbe uliwahi kuisoma, …ndio hivyo mwenyekiti…’akasema

‘Sijaisoma hii, maana mimi bado sijaihakiki, kisheria,…nakuuliza tu kama kipengele hicho kipo…’akaambiwa

‘Ndio tumekubaliana hivyo, na kila mmoja analifahamu hilo, ndio maana tukaisajili hiyo katiba, na mimi nipo tayari kuwajibka kwayo, hiyo hapo isome,utaona kila kitu kipo wazi, hakuna nilichokosea hapo,..’akasema ni kunigeukia mimi. Sikusema kitu

‘Lakini unaposema kuvunjika kwa ndoa una maana gani mzee?’ akauliza alipohisi kuna kitu kategwa.

‘Unaniuliza tena mimi, si kipengele hicho kipo kwenye katiba yenu halali au sio, si umakubali kuwa kipengele hicho kipo, au..…’akasema mwenyekiti

‘Nahisi hukusoma sehemu yote kwa ukamilifu wake, ukisoma vyema hiyo katiba utaona kuwa mimi ndiye mwenye usemi wa mwisho kuhusu ndoa, na ndivyo ilivyo hata kwenye dini…au sio,..na mimi kama mume, siwezi kukubali ndoa yangu ivunjike, nitailinda kidini na kikatiba yetu hii ya familia,tuliyokubaliana nayo..’akasema

‘Nauliza tena, upo tayari kuwajibika kutokana na katiba yenu halali,ambayo inatambulikana na msajili wa katiba,… ?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio nimeshakuambia hilo, yote yapo wazi kwenye hiyo katiba, sioni kwanini uniulize swali hilo, wakati katiba unayo hapo, isome tu mzee, ili kila mjumbe asikie hilo,.. na mimi nimekubali na sahihi yangu ipo na ya mke wangu ipo na ya wakili wa familia pia…wakili ambaye anayetambulikana na mke wangu, au sio mke wangu..?’ akauliza mume wangu.

‘Unajua kuongea sana siku hizi..’akasema mwenyekiti

‘Hapana ni lazima nionyeshe uhalisia, mimi kama mume wa familia, uliniozesha mimi, niwe mume wa binti yako, kwanini nisiongee kutetea ndoa yangu, hata wee utanishangaa nikikaa kimia, au sio..’akasema

‘Huyo wakili aliyesimamia huo mkataba wenu ni nani..?’ akauliza mzee, kabla mimi sijasema neno, na mume wangu kwa haraka akasema;

‘Ni wakili wa familia, yule pale,….akatae kama sio yeye aliyetayarisha hiyo katiba, sahihi yake ipo, hawezi kuikana, au…muulizeni yeye mwenyewe…’akasema

‘Nakumbuka awali ulilalamika kuwa mbona wakili wako hayupo, ina maana wewe una wakili mwingine zaidi ya huyo…?’ akaulizwa

‘Ndio yupo..’akasema

‘Ni kwanini sasa ukatafuta wakili mwingine kama huyu ndiye aliyewawekea sawa hiyo katiba yenu halali, inayosimamia kila kitu kwenye familia yenu mpaka hapa unatulizimisha na sisi tuifuate,…?’ akaulizwa kabla hajajibu mzee akaendelea hapo hapo kwa kusema;

‘Huyo si ndiye wakili wa familia sio, na katiba hiyo halali, ameiweka yeye sawa kisheria, maana nyie ndio mlitayarisha mawazo yenu, mkajadiliana kila mmoja akatoa mawazo yake kipengele kwa kipengele, wakili yeye, alichofanya nikuweka sawa hivyo vipengele kimoja baada ya kingine ili vikae sawa kisheria, kweli si kweli...?’ akaulizwa

‘Ndio mzee,… ni wakili wa familia, lakini kiutendaji, mimi kama mume wa familia niliona kuna haja ya kuwa na wakili mwingine,, ukiangalia kwenye hiyo katiba inanipa mamlaka hayo ya kufanya mambo nikiona ni sahihi kwa masilahi ya familia,…mimi niliona kuna umuhimu wa kuwa na wakili mwingie, sio mbaya wangapi wana wakili zaidi ya mmoja..’akasema

Mwenyekiti akaangalia saa, halafu akaangalia pale walipokaa mawakili, halafu akasema;

‘Kabla sijamuuliza wakili kulithibitisha hilo, nakuuliza maswali haya muhimu napenda uyajibu ukiwa na uhakika nayo …’akasema mwenyekiti

‘Uliza tu mzee, sina wasiwasi kabisa, mimi nipo hapa kwa ajili ya familia yangu ,na ndoa yangu…’akataka kuendelea na mzee akauliza

‘Kwahiyo kwa jinsi ilivyo, nyie maisha yenu , majukumu yenu, na kila kitu, siwezi kusema kila kitu, ila mambo yote muhimu yanategemea huo mkataba halali…?’ akaulizwa

‘Ndio mzee, unatusaidia sana…’akasema

‘Na je mtu akikosea, kuna vipengele vya hukumu,..?’ akaulizwa

‘Ndio vipi, hatukubakiza kitu…’akasema

‘Kwahiyo wewe kama umekosea,au mke wako kakosea, haihitajii kwenda mahakmani, hukumu zipo wazi, na hukumu hizo zinaweza kusimama kama ushahidi unajiotosheleza..?’ akaulizwa

‘Ndio kabisa…’akasema

‘Na wewe hapo ulipo, upo tayari kuhukumiwa kwa mujibu wa katiba yenu halali…?’ akaulizwa na hapo kidogo akasita

‘Kwa mujibu wa katiba yetu ndio…kama inavyosema ..ndio…kila kitu kipo wazi, na nashangaa kwanini mke wangu akaamua kuitisha kikao kama hiki, labda kama anaona yaliyopo kwenye hio katiba, hayafai, tubadilishe, labda, iwe hivyo, vinginevyo, sisi hatukuwa na haja ya vikao kama hivi..’akasema

‘Sasa nakuuliza swali, hili swali ni muhimu sana, nataka ujibu ukiwa na uhakika, maana baada ya hapa, sisi kama kikao, mimi kama mwenyekiti sitarudi nyuma tena, maana sikutaka iwe hivi, ila wewe mwenyewe umenilazimisha nifanye hili, kila mara katiba katiba, haya …ngoja tufuate katiba yenu, pamoja na mengine ambayo ni muhimu kwenye hiki kikao…

Sasa hili nahitajia jibu lako kutoka moyoni, uwe na uhakika nalo..’akasema na mume wangu akasubiria,…

‘Je una uhakika kuwa hii ndio katiba halali mliyokubaliana wewe na mke wako,...?’

Alipoulizwa swali hili akatulia kwanza akionyesha uso wa kushangaa…, halafu akageuka na kuniangalia mimi, mimi nikawa natoa tabasamu tu, lakini sikusema neno, yeye akasema;

‘Kwanini unaniuliza swali kama hilo mzee, kwani wewe ulikuwepo wakati tunaitengeneza hiyo katiba mpaka utoe kauli hiyo ya shaka,…, kuwa labda unaifahamu katiba nyingine zaidi ya hii…’akasema

Mwenyekiti akamuangalia tu, na yeye akaendelea kuongea kwa kusema

‘Ndugu mwenyekiti, wewe usisikilize maneno aliyonitania mke wangu awali, hakuna katiba mbili, na mimi ndiye ninayeifahamu hiyo katiba kwa vile mimi ndiye mume wa familia yangu, katiba ndio hiyo hakuna katiba nyingine…’akasema

‘Sikutaka maelezo mengi kihivyo, …nataka jibu la uhakika, …nakupa dakika moja ya kulifikiria hilo jibu lako vyema, ni muhimu sana kwangu na kikao hiki kilisikie hilo jibu kama ushahidi…, ‘ akasema

‘Kama ushahidi…!!’ akauliza mume wangu

‘Ndio…nataka kupima uadilifu wako wa ndoa…nataka katiba yako yenyewe ifanye kazi, si wewe umelisisitiza hilo, au unaanza kuogopa…?’ akaulizwa

‘Hapana..siogopi, maana naifahamu vyema katiba yangu, wewe uliza swali lako tu..’akasema

‘Wewe unatamba kuwa wewe ni mume mwema wa familia,,kama kweli wewe ni kiongozi muadilifu wa familia, nirudia swali langu, kumbuka uwongo, kugushi, wizi..kuua, ni moja ya mambo yanayokiuka sheria, sijui kwenye katiba yenu mumeyawekaje hayo, na kuna mambo ukiyafanya, unavunja ndoa,.., sasa nataka uwe muwazi kwa hilo, kama huna uhakika useme...’akasema mwenyekiti

Mume wangu hapo akakaa kimia kidogo, na mwenyekiti akauliza tena….;

‘Je kweli wewe una uhakika kuwa hii ndio katiba halali, mliyoitengeneza wewe na mke wako, ikasainiwa na wakili wa familia yenu..nasisitiz hapo, tena, je una uhakika nataka unijibu, na nataka uchukue muda kuliwazia hilo jibu lako…’akasema mwenyekiti akiangalia saa yake.

Nilimuona mdogo wake aliyekuwa pembeni, akiinamisha kichwa chini, kama anaomba, halafu akainua mikono na kujishika kichwani, akainua kichwa na kumuangali kaka yake,…

Rafiki wa mume wangu docta, alikuwa makini kweli akifuatilia hatua kwa hatua, na alipoona mdogo mtu anahangaika, kutaka kuongea, akamuangalia na nahisi alikuwa anataka kumuashiria huyo mdogo mtu atulie…

Sasa nikamuona mdogo mtu kama anataka kunyosha mkono aongee, lakini akarudisha, alipokutanisha macho yake nay a docta, kiukweli hata mimi pale nilipokaa, ..nilitamani huyu shemeji mtu aongee huenda ana jambo muhimu la kumsaida kaka yake, lakini sikuwa na jinsi ya kuingilia hilo

Nikageuka sasa kumuangalia mume wangu, alikuwa akitabasamu tu hana wasiwasi, akasema;

‘Naweza kujibu mwenyekiti, mimi sina wasiwasi…’akasema na mwenyekiti, kabla hajamjibu akaangalia saa yake

NB: Mambo yamenza, ushaidi wa kwanza wa kupima ‘uaminifu kwenye ndoa’.


WAZO LA LEO: Uongozi ni wito, uongozi ni kubeba dhamana za watu, na ukiwa kiongozi mwadilifu, watu wako ni kwanza, na wewe unakuja baadaye, kwahiyo kimasilahi, utahakikisha kuwa watu wako wametosheka kwanza, kabla ya kujali tumbo lako, huo ndio uongozi bora.

 
SEHEMU YA 93



Je kiongozi kama huyo yupo katika hii dunia ya sasa,...


‘Je kweli wewe una uhakika kuwa hii ndio katiba halali, mliyoitengeneza wewe na mke wako, ikasainiwa na wakili wa familia yenu…

‘Je ninaweza kujibu mwenyekiti swali lako…maana, mimi sina wasiwasi na hilo..’akasema mume wangu

Tuendelee na kisa chetu…

**************

‘Ndugu mwenyekiti mimi hapa ni mkweo, ni mume wa binti yako, ndiye ninayefahamu ukweli wa mambo ndani ya familia yangu, na kwahiyo hicho ninachokuambia ndio ukweli wenyewe,....’akasema

‘Hujajibu swali langu, je hii ndio katiba halali mliyokubaliana wewe na mkeo,?’ akauliza tena mwenyekiti, na mume wangu akasema

‘Ndio, hiyo ndio katiba halali tuliyokubaliana mimi na mke wangu, na ukiangalia humo utaona sahihi zetu wote ikiwemo ya wakili wetu,...’akasema.

‘Sawa nilitaka kusikia kauli yako tena ili wajumbe wote waisikie, na sasa nataka kuthibitisha ukweli wa kauli yako…’akasema mwenyekiti

‘Kuthibitisha…kuthibitisha nini…?’ akauliza mume wangu kwa uso wa kushangaa

‘Kuna malalamiko kuwa katiba iliyokuwa halali imebadilishwa , imegushiwa kiujanja ujanja na kutengenezwa katiba nyingine kwa minajili ya kujitwalia mali, na kuhalalisha mambo kwa manufaa ya mtu, au watu wake, bila ya mmoja wa wahusika kwenye mkataba huo kuhusishwa, na bila wakili wa familia hiyo kuhusishwa pia, .....’akasema mwenyekiti

‘Hiyo sio kweli mwenyekiti, muulize mke wangu, kama kweli hii sio katiba halali, na wakili yupo hapa, apinge kuwa hiyo sio sahihi yake, na sahihi ndio ushahidi muhimu kwenye vitu kama hivi....’akasema mume wangu kwa kujiamini.

‘Hiyo sio kazi yako, mimi kama mwenyekiti nafahamu jinsi gani ya kuhakiki uhalali wa hilo,… na kama kweli ndiyo katiba yenu, ambayo mlikubaliana, tutathibitisha hilo, bila shaka, na kama kuna ubabaishaji wa hilo ni kosa kubwa, na ni kosa linalostahiki kufikishwa mbele ya sheria..’akasema mwenyekiti.

‘Ni…hi, sio kweli mwenyekiti…’akasema mume

‘Unajua ..mimi sikutaka sana kuingilia kwenye mambo yenu ya katiba , kwasababu kikao chetu kilikuwa na utaratibu wake, huenda hilo ni moja ya mambo ambayo alitaka kuyaongelea mwenyeji wa hiki kikao, mimi sijui..’akasema mwenyekiti.

‘Lakini imenibidi niingilie hili kati,kwa vile wewe mwenyewe umekuwa ukisisitizia kuhusu hiyo katiba, na ya kuwa katiba kwenu ni kila kitu… na hata kikao hiki ni ukiukwaji wa katiba,…na zaidi ya hilo, nyie hamtaki watu wengine wawaingilie , kwasababu mna muongoz wenu, sio ndio hivyo mume wa familia?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio hivyo mwenyekiti, kila kitu kipo kwenye hiyo katiba..naona ajabu watu kutuingilia kwenye mambo yetu ya ndani,…hiyo ni kweli mwenyekiti, samahani kwa hilo…’akasema huku akitabasamu.

‘Kuna malalamiko,kuwa hii katiba uliyonipa , hii hapa...itakuwa ni hii au sio…maana sijajua kuwa kuna katiba nyingine nyie ndio mtanithibitishia, hilo…’akaiinua juu mwenyekiti,..

Mume wangu akataka kuongea lakini mwenyekiti hakumpatia nafasi hiyo

‘Mimi sijui, maana hii hayo mliyatengeneza nyie wawili, na kilichomo humu, mnakifahamu nyie wawili, lakini katiba hiyo imesajiliwa kisheria, kwahiyo yaliyomo humo ni sheria yenu wawili,na yupo shahidi wenu mkuu kisheria, wakili wenu, ..’akatulia akimuangalia wakili

‘Sasa kwa minajili hiyo kila mmoja wenu ana haki nayo, na kama mmoja atafanya ujanja na kuibadili, kavunja sheria, na nazidi kusisitiza, kuhariri, kubadilisha kitu kama hiki mlichokubaliana kisheria, bila ya ridhaa ya mwingine ni kosa kubwa, …’akasema mwenyekiti

‘Nimeamua kuacha utaratibu wetu, ili kuliweka hili sawa, ni kutokana na wewe mume wa familia, … kuna kauli kuwa katiba mliyotengeneza awali imegushiwa, imekarabatiwa kiujanja ujanaja…,je wewe kama mume wa familia, unasemaje kuhusu hilo, ?’ akaulizwa.

‘Mimi nalipinga kabisa, hakuna kitu kama hicho, na huyo aliyesema, hivyo hafahamu ukweli wa mambo yetu ndani ya familia, hao ndio wavurugaji wa ndoa za watu, wanastahiki kukemewa…’akasema

‘Una uhakika na hilo..?’ akaulizwa
‘Ndio mwenyekiti...mimi kama mume wa familia, nina majukumu ya kulinda familia yangu, na ni pamoja na kuilinda hii katiba yetu halali, kwani imebeba mambo yetu yote,....sitakubali mtu aibadili, bila kumshirikisha mwenzagu, na haijabadilishwa, ni nani kaongea hilo....’akasema

‘Ndugu mume wa familia, hili ni muhimu sana, uwe na uhakika na majibu yako, usije ukajiweka kwenye hatia,…Ina maana kweli hakuna katiba mbili, hii ya sasa na nyingine ya awali?, je hamjawahi kuikarabati kwa pamoja kutengeneza katiba nyingine mpya..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, hakuna katiba nyingine, kama ipo tofauti na hii ambayo kweli imesajiliwa watuonyeshe hawo watu wanasema hivyo, kwasababu kila kitu kipo kisheria, hata ukienda kwa msajili, utaiona nakala kama hiyo hapo,..’akasema

‘Na je kama itathibitishwa kuwa hii sio katiba halali, na ya kuwa hii imetengezwa kwa kugushiwa kwa malengo maalumu, utasemaje?’ akauliza

‘Nitasema nini,…hahaha ndugu mwenyekiti kauli hiyo inatoka wapi, ..ni kwamba hakuna katiba nyingine, katiba ndio hii, kwanini mwenyekiti huniamini..kwanini
unang’ang’ania kuwa kuna katiba nyingine, mimi ndiye mume wa familia na unatakiwa uniamini mimi, kwani nasema hili kwa masilahi ya familia yangu’akasema kwa kupaza sauti kidogo.

Mwenyekiti akageuka kidogo kuniangalia mimi pale nilipokaa, na kutikisa kichwa akionyesha kusikitika, akasema;

‘Nawaasa sana nyie wanandoa, sawa mume ni mume, ana mamlaka yake makubwa tu, lakini niwaambia jambo moja, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama uaminifu, hakuna kitu muhimu katika ndoa kama kutii yale mliyokubalina nyie wawili kama wanandoa…’akatulia akimuangalia mume wangu.

‘Na zaidi ya hayo,kama wanandoa mtakuwa na ajenda za siri kwa nia ya kuumizana, basi ndoa hiyo haina usalama tena, ndoa hiyo sio ndoa tena bali ni ndoana. Mimi nilishatoa angalizo kuwa kuna mambo yanayosamehewa kama watu watatenda kwa bahati mbaya...’akasema

‘Ni kweli…’akasema mume wangu

‘Lakini kuna mambo ambayo unayaona kuwa kweli ni makusudi, na yana nia mbaya, na ukiyaachia yanaweza kukiharibu kizazi, uwongo, utapeli, kugushi, ni dhambi, unajenga taifa la watu wasio waaminifu..sasa mimi sitaki kuwa mchochezi, nimeletewa mashitaka hayo, kuwa kuna ukiukwaji wa sheria, tena wa hali ya juu, kwani kama mtu anaweza kubadilisha kitu kilichosajiliwa kisheria, akatengeneza kingine, kikiwa na sahihi za wahusika, basi huyo ni mkiukaji wa sheria wa hali ya juu..'akasema mwenyekiti

Mume wangu akawa anaonyesha ishara ya kushangaa, kuwa ni nini mwenyekiti anaongea, ni kama kudharau hivi.

‘Hii hapa ni katiba, ambayo inawahusu watu wawili, na sijui kama ndio yenyewe au la, wanahusika wataithibitisha wao wenyewe.., sasa mume wa familia anasema hii ndio katiba halali, ...maana wewe mwenyewe ndio umelitaka hili, ...kabla sijamuuliza mkeo ,ambaye ni kiungo muhimu, ambaye walikaa pamoja yeye na mume wake, wakaitengeneza,…’akatulia kidogo huku akigeuza kichwa taratibu kuelekea sehemu nyingine,

‘Mimi naona ni bora nimuulize mtengenezaji wa hii katiba kisheria na ambaye alihusika kwenye kuisajili ambaye ni shahidi wa hiki kitu, maana nikikimbilia kumuuliza mke wa familia, nitaionekana nimeweka shinikizo kwa vile ni binti yangu, mnielewe hapo,japokuwa hapa wote ni wajumbe...’akasema mwenyekiti na kutulia kidogo, akamuangalia mume wangu, na mume wangu akawa anatikisa kichwa tu.

‘Mume wa familia, nakuomba wewe mwenyewe, uchukue hii katiba ukamuonyeshe wakili wenu ili athibitishe kwenye kikao hiki kuwa hiyo ndio katiba halali mliyoiandika wewe na mke wako, kwa msaada wa huyo wakili wenu ...'akatulia kidogo

'Sasa yeye akithibitisha kuwa ndio yenyewe, mbona jambo limekwisha, mimi sitakuwa na haja ya kumuuliza binti yangu, nimuulize wa nini tena..eeh ..’akasema akiishika ile katiba kumkabidhi mume wangu.

‘Nitamuuliza tu kwa vile yeye ni kiungo muhimu, na kama yeye atakuwa na pingamizi, kama na yeye hana pingamizi, basi, tufanyeje sasa..

'Au sio wajumbe...?' akauliza wajumbe na wajumbe wakatikia kwa kauli

'Sawa kabisa mwenyekiti..

'Basi, tunataka zoezi hilo lifanyike kwa haraka ili twende na muda,..baada ya hapo, tutaingia kwenye kipengele kingine ama cha kusikiliza malalamiko ya muitisha kikao, au kuzidi kuthibitisha uhalali wa hiyo katiba,...na kama itakuwa tofauti, kukaonekana kuna utata wa hiyo katiba,...mmh, mimi sitasema mengi...'akasema na wajumbe wakacheka

'Msicheke, hili ni tatizo jamani,...kama haya yanatokea ndani ya familia ya mke na mume, watu walio kitu kimoja, mnatarajia wakipewa madaraka nchi itakuwaje,...mimi nipo kwenye siasa, naliangalia hili kwa umbali zaidi,..matatizi mengi huanzia huku kwenye familia, chagueni viongozi kwa kuwachunguza huku wanapotokea...'akasema na mke wake akapiga makofi.

'Kama alivyo dai mume wa familia kuwa tusiingilie mambo yenu , maana katiba yako ndio kila kitu, sasa tuone uhalali wake, na baadae hiyo katiba halali ifanye kazi yake, mkuki kwa nani ni mchungu, sasa mkuki huo utamgeukia, nani..matajaza wenyewe...’akasema mwenyekiti.

'Haya zoezi lianze...'akamalizia hivyo.

‘Sawa kabisa mwenyekiti....’akasema mume wangu, huku akisogea mbele, na kuelekea pale alipokaa mwenyekiti, wakati anapita akapita pale alipokaa mdogo wake, akamnong’oneza kitu, na mdogo wake, akamwangalia kaka yake, kwa macho ya kushangaa, lakini huyo mdogo mtu hakusema neno. Mwenyekiti hakuliona hilo tendo, alikuwa akiteta na mkewe.

Mume wangu akaichukua ile katiba kwa mwenyekiti , akaikagua kwa kiufungua, akatikisa kichwa kama kukubali kuwa ndio yenyewe,huku akiwa anatabasamu akatembea hadi pale alipokaa wakili wa familia yangu na kumuonyesha wakili ile katiba huku akisema;

‘Ndugu muheshimiwa wakili, hii ndio Katiba ambayo tuliitengeneza tukishirikiana na wewe, na kama unavyoona kuna sahihi yako, hii hapa, ...na hii hapa ni sahihi yangu na hii hapa ni ya mke wangu, nataka wewe uthibitishe kwenye kikao hiki kuwa hii ndio katiba halali, ili tuondoe hiki kiwingu cha kutoakuaminiana ...ukumbuke wewe ni wakili wa familia, na mimi ni mume wa familia, mwenye mamlaka yote a familia....’akasema

Kwanza wakili alisita kuipokea ile katiba, akamwangalia mwenyekiti, na mwenyekiti akasema;

‘Labda tufanye hivi, mimi nina wakili wangu, kabla wakili wenu hajathibitisha hilo hebu muonyeshe wakili wangu, ili yeye aione hiyo katiba, ili awe ni mmoja wa mashahidi walioyoiona hiyo katiba, ili baadaye tusije tukarukana, kuwa haikuwa hiyo, pia wajumbe wengine, kuna docta pale, kisheria anatambulikana anaweza naye kuthibitisha hilo, sio mbaya na wajumbe wengine wakaiona maana kwasasa haina siri tena,...’akasema

Mume wangu akatembea hadi pale alipokaa wakili wa wazee wangu akamuonyesha ile katiba, wakili wa mzee, akaichukua na kuifungua, akasoma kidogo, halafu kwa haraka akapitia ukurasa mmoja baada ya mwingine, akachukua simu yake, akawa anaipiga picha sehemu muhimu, halafu akasema

‘Je una nakala nyingine ya hii katiba yenu?’ akauliza wakili huyo

‘Ndio ninayo, nina nakala tatu, unaweza kubakia na nakala hii, kama unahitaji, zipo nyingine, hakuna shida,....’akasema na kwenda kwenye mkoba wake, akatoa nakala nyingine, na kusema;

‘Hiizi hapa nakala nyingine,zote ni sawa sawa,....’akasema

‘Haya kamuonyeshe wakili wenu, ili athibitishe kuwa Katiba hiyo ndio Katiba sahihi ambayo yeye aliitengeneza, na kuipeleka kuisajili kwa msajili wa katiba,...yeye ndiye mtu wenu wa sheria, kwani kwa jinsi ilivyo, hatua itakayofuatia, kama kweli kuna uvunjaji wa sheria kiasi hicho, basi yeye ndiye muwajibikaji mkubwa’akasema mwenyekiti.

Wakili wetu, aliichukua ile katiba, akafungua ukurasa wa kwanza, akawa anangalia kwenye ganda la juu, kwa ndani, akawa kama anashangaa, hakusem neno, akafungua ukurasa wa kwanza na kuangalia kwa ndani, akainua ukurasa wa kwanza ni kufanya kama vile ananinginiza, kama vile mtu anayeangalia pesa kuwa ni halali,.....’akatikisa kichwa na kusema;

‘Hii sio ile katiba halali…’akasema

‘Rudia tena…’akasema mwenyekiti
‘Hii sio ile katiba halali niliyoisajili mimi…’akasema

Watu kimia…sasa wakigeuka kumuangalia mume wa familia, aliyekuwa kashikwa na butwa,

Kwa haraka mume wa familia, akasogea pale alipokaa huyo wakili,akichukua ile katiba kutoka mikononi mwa huyo wakili na kusema;

‘Hii ni katiba halali, unaona sahihi yako hii hapa, na hii hapa ni ya mke wangu, unataka kusema nini, mbona unatupinga sisi wateja wako...wakili gani anayewapinga wateja wake…hapana hufai..’akasema akimuonyesha huyo wakili, lakini huyo wakili hakutaka hata kuiangalia,akasema;

‘Ndugu mwenyekiti, kila fani ina watendaji wake, na wanao jinsi gani ya kulinda mambo yao, sisi, kama mawakili tunafahamu haya yote kuwa yanaweza kutokea, kwa hiyo kila mmoja ana namna yake ya kuweka mambo yake katika usalama, ili mtu mwingine asije akabatilisha kazi yake..hii kazi ni ya hatari na ina dhamana kubwa, ukizingatia kuwa unacheza na maisha ya familia za watu....’akasema.

‘Mimi na wengine tuna mihuri ya siri, ni wachache sana wasio na mihuri hiyo ya siri, inayothibitisha kuwa hii kazi ni ya mtu fulani, hii kazi ni yangu, hasa kwenye kazi kama hizi ambazo zina usiri wa kifamilia. ..’akasema na mume wangu akawa kaduwaa tu.

‘Kiukweli mimi sikutarajia kuwa katiba hii aliyoitoa mume wa familia, ingeliweza kuwa sio yenyewe ambayo niliitengeneza mimi..maana ukiiangalia juu juu, utaona haina tofauti na ile katiba niliotengeneza mimi lakini kuna kitu kinakosekana, hakuna hiyo alama yangu…’akasema na mume wangu akawa anaichunguza ile katiba.

‘Labda nimuulize mteja wangu huyu…je ni kwanini huo muhuri wangu haupo, je ulitoa nakala nyingine, na kama ulitoa nakala nyingine, bado ule muhuri wangu ungelionekana kwa kufifia…, ningelitambua kuwa hiyo ni nakala tu....’akatulia.

‘Kwahiyo huo ndio mtego, hii katiba haina kitambulisho changu, kwa kuiangalia tu bila kusoma kilichopo ndani…’akasema

‘’Huo muhuri, unakaa wapi,lakini mimi ninachojua ni kuwa hii ndio katiba halali, na wewe unachotakiwa ni kusimama kwa ajili yetu, kama unanipinga mimi basi wewe sio wakili wetu...’akasema

‘Mimi ni wakili wenu kisheria… nasimamia taratibu zenu ki- sheria, siwezi kusema uwongo, hii sio katiba niliyoitengeneza mimi, ...na kwa haraka nimeshaipitia ndani, na niliwahi kuipata kabla, kuna mambo mengi yamebadilishwa...’akasema huyo wakili, na mume wangu akabakia kimia.

‘Ndugu mwenyekiti, Wakati mume wa familia anaongea kwa kujiamini, nilijua kabisa huenda huyo aliyewatengeneza atakuwa anafahamu muhuri wangu, kwani kama aliweza kugushi sahihi, zetu, asingelishindwa kugushi muhuri wangu wa kificho, unaowakilisha kazi zangu...ndugu mwenyekiti, kiukweli hii sio katiba halali niliyotengeneza mimi....’akasem wakili.

Mwenyekiti, akakunja uso, akamwangalia mume wangu, na kusema;

‘Mkwe,...nimeamua kukuita hivyo mkwe, ili nikupe heshima, yako, nataka unijibu hayo, ninayokuuliza kama mkwe, mkwe wa kweli hasemi uwongo, useme ukweli wako, kama mkwe, mkwe ana heshima yake, hawezi kumdanganya baba mkwe wake,...eti jamani uliona wapi mkwe anamdanganya baba mkwe wake, ...kwahiyo nakuomba, unjibu haya maswali kwa ukweli wako,, nakuuliza tena;

‘Hiyo katiba ni katiba halali mliyotengeneza wewe na binti yangu?’ akauliza baba.

‘Baba mkwe, mimi ninamshangaa wakili wetu, yeye ndiye anayewakilisha mawazo yetu na kutuwakilisha sisi, nashangaa, leo anapina kazi yake mwenyewe, mimi sijali huo muhuri wake anaosema, ninachojali ni hiyo sahihi, yake, je akiri mbele ya kikao hiki kuwa hiyo sio sahihi yake, je hii sio sahihi ya mke wangu...?’ akauliza

‘Inaweza ikawa ni sahihi yangu,..lakini sahihi hii imechukuliwa kitaalamu na mihuri, kuna mihuri siku hizi, inabandikwa kwenye maandishi, na yale maandishi yanabakia kwenye ule muhuri, na unaweza kwenda kuyabandika sehemu nyingine, kama vile unavyoweza kufanya kwenye komputa kukopi na kupesti, ..’akasema wakili

‘Una ushahidi kuwa ilifanyika hivyo?’ akauliza mwenyekiti

‘Ukiangalia kwa makini, utaona sahihi hizi ni kama zina kivuli, angalia kwa makini, kuna kivuli, na hii kwa wataalamu wa maandishi wanaweza kulithibitisha hili....mimi nilikuwa nashauri kwa vile jambo hilo limefanyika kitaalamu zaidi, ni bora tukawahusisha wataalamu wa maandishi,…’akasema wakili na mume wangu akataka kusema neno lakini akatulia kwanza.

‘Na kwa vile tendo hili limefanyika likisaidiwa na wakili, nina uhakika, kuna wakili yupo nyuma ya hili, kashiriki kulifanya hili, kwani sehemu zilizobadilishwa zimebadilishwa kwa utaalamu wa hali ya juu wa kisheria.....basi hili swala naona liende kisheria, lichunguzwe kisheria, ..’akasema

‘Nikuulize tena kuna kitu gani kingine unachokiona ni tofauti na mkataba halali ulioutengeneza wewe?’ akaulizwa

‘Kuna maandishi yamebananishwa, ukiangalia utaona kama mistari ilikuwa iantaka kupandana, sivyo ilivyokuwa kwenye mkataba halisi,… nahisi ni ili kusije kukaongezeka ukurasa, na kuleta tofauti kati ya mkataba ule halali wa mwanzo na huu wa kugushi...’akasema

‘Inatosha…’akasema mwenyekiti, na hakumuangalia mume wangu ambaye alikuwa bado kaduwaa, akizidi kuikagua ile katiba, kama haamini..

‘Kabla hatujaingia ndani tukaona ni nini kimebadilishwa na kwanini,…maana kama kuna mabadiliko, yatakuwa na maana fulani au sio, narudi kwako mume wa familia, je bado unashikilia msimamo wako huo kuwa hiyo ndio katiba halali ya familia, ambayo uliitengeneza wewe na mke wako?’ akaulizwa.

Mume wangu akabakia kimia kidogo, halafu kwa haraka akasema;

‘Kauli yangu ni ile ile mwenyekiti, mimi nawashangaa, maana mimi ndiye ninayefahamu katiba ipi ni halali, kwanza kwanini niseme katiba ipi, hakuna mbadala wa hii, au sio mke wangu…?’ akasema akiniuliza mimi na mimi nilikaa kimia tu.

‘Ndugu mwenyekiti mimi ndiye ninayewakilisha familia yangu, nashangaa watu wa nje, mnakuja kuipinga katiba yetu, kwani mlikuwepo wakati tunaitengeneza,...hii hapa ndio katiba halali, kama ipo nyingine, nataka niione, ili hii ionekane sio yenyewe...’akasema

Mwenyekiti akatabasamu kidogo, na kutikisa kichwa kama kusikitika, halafu akasema;

‘Kabla hatujathibitisha hilo,kabla hatujafanya unavyotaka wewe, nataka sasa nimgeukie mke wa familia, nataka na yeye, atuthibitishie kuwa hiyo katiba aliyo nayo mume wake, ndio katiba halali mliyokubaliana kati yenu wawili, ..’akasema

Kwa haraka mume wangu akaichukua ile katiba kutoka kwenye mikono ya wakili wetu akaniletea na kunikabidhi mimi, huku akifungua sehemu zile tulizoweka sahihi zetu, ....kiukweli huwezi kuona tofauti kati ya katiba hiyo na ile ya kwetu ya awali, kwani kila kitu kilionekana sawasawa kwa juu-juu, ukiangalia kwa haraka haraka inafanana kabisa na katiba ile ya awali,

Huyo aliyebadilisha alikuwa mtalaamu kweli wa kazi hiyo,..na kwa mtu asiyejua, hutaweza kugundua utofauti wowote mpaka usome ndani,na usome kwa makini kweli, kwani kuna lugha ya kisheria, ukibadili neno moja unaleta maana nyingine na kuna mambo yameongezeka, na mengine kupungua, lakini bila kuongeza ukurasa, au kuhamisha maneno mengine kwenye ukurasa mwingine,

Nilimuangalia mwenyekiti kabla ya kuipokea, na mwenyekiti akasema;

‘Ikague uhakikishe kama kweli ndio yenyewe…’akasema mwenyekiti na mimi ndio nikaichukua na kuanza kuikagua..

Niliingalia kwa makini, na huku mume wangu akinitizama kwa macho yaliyojaa shauku, na aliponiona nasita kutoa majibu, akasema;

‘Mke wangu hii ndio katiba yetu, kila kitu kipo kwa ajili ya masilahi yetu, hakuna kilichobadilika, ukiangalia hapo kuna sahihi zetu, na sahihi ya wakili, mimi sioni kama ni katiba tofauti, ....hii ni kwa ajili yetu na watoto wetu, lifikirie sana hilo akilini mwako, ....’akasema akionyesha sauti ya huzuni, mimi nikamwangalia na kusema;

‘Una uhakika na hayo maneno yako, una uhakika kuwa unalolisema ndio ukweli, mume wangu..?’ nikamuuliza na mume wangu akaniangalia kwa mashaka, na kusema

‘Mke wangu na wewe vipi, unanigeuka tena..’akasema

‘Mume wangu nakuuliza hivi, una uhakika kuwa hii ndio katiba yetu tuliyoitengeneza mimi na wewe siku ile...naomba mume wangu uwe mkweli, na huu ndio mtihani wako, ukweli wako ndio utakaodhirisha kuwa kweli upo na mimi...’nikasema na mume wangu akageuka kumwangalia mwenyekiti.

‘Mwenyekiti unaona hata mke wangu hawezi kulithibitisha hilo maana yeye anafahamu katiba ni moja tu, hio kauli ni yako tu …’akasema mume wangu

‘Nimekuuliza swali mke wa familia, je hiyo katiba ndiyo mliyoitengeneza nyie wawili, ...jibu swali, sitaki umuulize swali mume wako, nataka kauli yako wewe, kwasababu wewe unaifahamu vyema,...?’ akauliza mwenyekiti.

Kiukweli sijui kiliniingia kitu gani,..ule ujasiri wa kujibu kwa haraka ulinitoka, nikamwangalia mume wangu ambaye alikuwa akiniangalia kwa macho ya huruma, na machoni, nikawa nawaona watoto wangu wawili, na sijui kwanini, ilitokea hivyo kuona taswira ya watoto wangu,na mwingine akiwa kwa mbali, na ikaja hisia kama ya watoto wangu wakilia, na kuita baba,baba yupo wapi....,

Nikageuka kumwangalia mwenyekiti, nikasema,;

‘Ndugu mwenyekiti, katiba hii, inafanana sana na katiba ya awali...ni vigumu sana kuitofautisha na katiba..ya....’nikaanza kuongea na mume wangu akatabasamu na kupiga makofi kushangilia, huku akisema;

‘Unaona mwenyekiti, mimi na mke wangu ndio tuliotengeneza hii katiba kwahiyo tunaifahamu sana, namshangaa sana wakili wetu kutegeuka hii leo, sijui ana masilahi gani...’akasema mume wangu, na alipomaliza nikaendelea kuongea

‘Lakini ndugu mwenyekiti, wakati katiba hii inatengenezwa, sijui ni hisia au sijui ni kwanini nilijiwa na kitu kama hicho kuwa huenda ikatokea kubadilishwa badilishwa hii katiba, basi nikajiwa na wazo,..ilinijia tu mungu mwenyewe ndiye anayejua..’nikasema

‘Sawa kabisa waambie..’akasema mume wangu.

‘Kwa vile, shemeji yangu, yaani mdogo wa mume wangu ni mtaalamu wa komputa, na mambo yake, nilimuomba anisaidie kutengeneza maneno ya siri ambayo ninaweza kuyaweka kwenye kumbukumbu zangu, kiasi kwamba mtu mwingine asiweze kugundua hilo....’nikasema

‘Na kiukweli, sikuwahi kumwambia hata wakili wetu kuwa kwenye hiyo katiba kuna maneno nimeyaweka ya siri, kwahiyo hata yeye hajui hilo, niliyaweka wakati wakili wetu aliponiletea katiba hii kwenye mtandao ili mimi niupitie, ndipo hapo nikayaweka hayo maneno, na kila ukitoa nakala,halisi utayaona hayo maneno, yanakuwa huku pembeni, na ukitoa nakala, isiyo halisi maneno hayo hugeuka, yakawa kinyume chake....’nikasema na kumwangalia shemeji yangu ambaye alikuwa kabakia mdomo wazi.

‘Je shemeji hayo ninayozungumza ni kweli ...hukunitengenezea hayo maneno,...’ na akilini nikajiuliza kwanini shemeji yangu hakuweza kuwaambia wenzake kuhusu hayo maneno, wakati wanatengeneza hii katiba mpya, ili wayaweke hayo maneno, huenda hakuwepo, na huenda hakushirikishwa, na huenda hakujua kuwa lengo langu ni kuayaweka kwenye huo mkataba, Mume wangu aliposikia nikimtaja mdogo wangu akasema.

‘Mdogo wangu hahusiki na haya mambo, hii katiba ni kati yangu mimi na wewe, sema ukweli wako kama alivyokuuliza mwenyekiti, mimi ni mume wako,unahitajika kuwa na mimi, na hii katiba ni kwa ajili yangu mimi na wewe, na watoto wetu, wengine hawana masilahi nayo, usikatae ukweli....’akasema kwa huruma, na mdogo wake, akanyosha mkono, akitaka apewe nafasi aongee, mwenyekiti akasema;

‘Unataka kusema nini wewe uliyeingilia vikao vya watu,, ....wewe ni mualikwa tu, ....na muda wako ukifika utaongea,…’akasema na shemeji yangu bado akaendelea knyosha mkono kutaka kuongea

‘Haya hebu niambie wewe unataka kusema nini?’akasema mwenyekiti, na shemeji yangu huyo akasema;

‘Nakubali kuwa kweli nilimtengenezea shemeji hayo maneno, lakini sikujua kuwa alikuwa na nia ya kuyaweka kwenye hiyo katiba,...na pia mimi sijui lolote kuhusu hiyo katiba, kuwa ilibadilishwa, na kama kuna ya zamani na mpya,naomba kwa hilo niliweke bayana kwenu…mnisamehe kwa hilo ndugu zangu...’akasema

‘Nimewaambia mdogo wangu hajui lolote, haya mambo ni kati yangu mimi na mke wangu, hii katiba tuliitengeneza tukiwa wawili, naomba msimuhusishe mdogo wangu kwenye swala la hii katiba, ...’akasema kaka yake.

‘Lakini wewe unafahamu kuwa kuna katiba mbili,au nikuulize hivi je wewe uliwahi kuziona katiba mbili tofauti?’ mimi nikamuuliza shemeji yangu.

‘Siwezi kujibu hilo swali kwasasa, kwa hali niliyo nayo, ila ninachoweza kusema ni kuwa niliwahi kuona katiba sasa sijui utofauti wake maana zote zinafanana, kama zipo mbili tofauti au la...’akasema.

‘Mke wa familia, hujajibu swali langu, naona unaniingilia majukumu yangu ya kuuliza maswali,…, je hiyo katiba ndiyo katiba mliyoitengeneza wewe
na mume wako, jibu swali ili tuendelee,..?’ akauliza mwenyekiti

Hapo wajumbe wote wakawa wananiangalia mimi, na mimi nikamwangalia mume wangu, na nilimuona sasa akionyesha uso wa kukata tamaa, na mimi kawaida yangu sipendi kusema uwongo, hasa mbele ya wazazi wangu, lakini kuna kitu kilikuwa kikiniuma,..ni kwanini mume wangu bado anaendelea kusema hiyo ndio katiba halali.

Akilini nikawaza, huyu ni mume wangu nimezaa naye watoto, na hatima ya hilo, ni kuharibika kwa ndoa, hakuna ujanja hapo, na ikitoka katiba halali, na kwa matendo mengine aliyoyafanya basi, ndio hitimisho maana kila kitu kipo wazi, lakini hata hivyo, mimi nilitaka mume wangu awe mkweli, akiri kosa, na mimi ningelijua jinsi gani ya kufanya,...

Kwa hali ya mume wangu kutokutaka kusema ukweli, ilinipa shida sana, na nikahisi huenda hana ufahamu wa kweli kuhusu kubadilishwa kwa hiyo katiba, huenda maadui zake walihakikisha hilo haligundui, kama sio ujanja wake...,..

Mimi nikasema;

‘Ndugu mwenyekiti, naomba jibu langu lisubiri kidogo kwani kwanza, kwa sababu kuna mambo nahitajia yakamlike, kuhusu uaminifu na ukweli wa mume wangu, unajua yeye ametokea kwenye matatizo ya akili, sasa huenda ni kweli hana ufahamu huo, kuwa katiba hii imebadilishwa, sasa mimi nilitaka mume wangu atoe kauli yake ukweli,kwangu, ....’nikasema.

‘Mwanangu, mimi ndiye mwenyekiti wa hiki kikao, na ukweli, ni kwa wote, na hapa yupo docta, anaweza kuthibitisha kuwa kweli huyu mtu hana akili timamu…’akasema mwenyekiti akimuangalia docta

Docta akashtuka, maana anaona kama ataingizwa kwenye mtihani mnzito.

‘Mimi kama mwenyekiti kwa niaba ya kikao hiki, tunachohitajia ni ukweli wako wewe, usizunguke, ukweli ni ukweli, usije ukaharibu ukweli wako kwa kungalia sura ya mtu, ukigeuza ukweli, ukawa uwongo, kwasababu ya dhamira fulani, hata kama wewe unaiona ni kwa masilahi ya huyo mlengwa, lakini ukasema uwongo, ukweli, ukaugeuza ukawa uwongo, wewe sio mkweli tena, wewe sio mwaminifu tena…’akasema mwenyekiti

‘Oh…na..na..’nikasita kusema na mwenyekiti akasema;

‘Mtu mkweli na mwaminifu husema, ukweli bila kujali huyu ni mume wangu au huyu ni mtoto wangu, au huyu ni mzazi wangu, ukweli utasimama kuwa kweli, kwahiyo ninachotaka hapo ni ukweli wako wewe,...je hiyo katiba, kama ulivyoiona ndio katiba halali mliyoitengeneza wewe na mume wako, usijali kauli ya wakili, au ya mume wako, hapo ni wewe....?’akaniuliza mwenyekiti

Na mimi nikamwangalia wakili wetu, nikaiangalia ile katiba, na sijui kwanini nilikuwa nasita kutoa kauli yangu,kuna hali fulani ilivunja ujasiri niliokuwa nao, kuna hali ya huruma iliniingia, sijui ni kwanini,na hali hiyo ilinijia pale tu nilipomuangalia mume wangu machoni, na kuona zile taswira za watoto wangu .

Pale pale…nikageuka kumwangalia rafiki wa mume wangu, ambaye muda mwingi alikuwa kimiya, alikuwa kakunja uso kama anatafakari jambo, na macho yetu yalipokutana, nilihisi kama ananiambia, 'msaidie mume wako, japo kwa hilo tu, unaweza ukampoteza mume wako ' na alipoona namtizama akatabasamu, na mimi kwa haraka nikageuka kumwangalia mwenyekiti tayari kutoa jibu........

NB: Haya sehemu hii inaishia hapo kwasababu maalumu, tusichoke, nia ni ujumbe ndani ya kisa, kwa wanaofahamu wataona ni kwanini siendi moja kwa moja kwenye kukimaliza kisa, someni na kati kati ya mistari mtanielewa...tukutane sehemu ijayo.



WAZO LA LEO: Ukweli utabakia kuwa ukweli, huwezi ukahalalisha ukweli kwa kusema uwongo , kwa ajili ya kumsaidia mtu, hata kama ni mtu wako wa karibu, ukisema uwongo, ukaukana ukweli, ili kusadidisha jambo, kwa huruma, basi unavunja uaminifu wako, tujifunze kuwa wa kweli popote pale, ili tuwe waaminifu.
 
SEHEMU YA 94


‘Ndugu mwenyekiti, sio kwamba nakataa kusema ukweli, unanifahami fika kuwa mimi sio mtu wa kusema uwongo, hujanialea hivyo, lakini ninachotaka kukifanya hapa ni kumpa mwenzetu muda wa kutafakari…’nikasema nikimuangalia mume wangu

‘Muda gani anahitajia yeye…na hilo sio jukumu lako….’akasema mwenyekiti.

‘Mwenyekiti nazungumza hilo,..kwa nia njema, ikurejea hali halisi aliyokuwa nayo awali,…nap engine kuna kitu anakiogopa, mimi ninamuhakikishia kuwa akisema ukweli, sisi tutamlinda, sisi hapa tupo kama familia, tunachohitajia ni kusawazisha haya mambo ili tuwe na msimamo wa kifamilia, .....’nikasema.

Mungu wangu aliniangalia huku akiwa keshakunja uso wa kukasirika,…hakusema kitu na mwenyekiti akasema;

‘Mimi kama mwenyekiti ndiye ninayefahamu ni kitu gani kinakiwa kifanyike, sioni kwanini uingiwe na kigugumizi kusema ukweli, sisi tumeshampa muda wa kutosha huyo mume wako,na hata ukimpa siku nzima, inavyoonekana, ni kuwa hatageuza kauli yake,…’akasema mwenyekiti na kumuangalia mume wangu ambaye bado alikuwa kimia tu.

‘Kwa jins ninavyomfahamu tutakesha hapa, sasa kama na wewe unaogopa kusema ukweli kwasababu ni mume wako, basi wote labda enu ni moja, lakini sisi kama kikao bado tunahitaji jibu lako, ...umenisikia swali langu au nirudie...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Nimelisikia swali lako mwenyekiti, ukweli upo wazi, hii katiba sio katiba halali, hii katiba imetengezwa upya kwa ku-...’nikaanza kusema na mume wangu akanikatisha, na kusema;

‘Ina maana hata wewe mke wangu unanisaliti, siamini hilo kabisa, huoni kuwa umekiuka katiba….’hapo akasita kidogo.

‘Eti jamani, ni wapi ulisikia mke anakuwa kinyume na mume wake, ....hujui ni kosa kubwa, kumkana mume wako, tena mbele ya watu..na kwanini uukane ukweli,.., hapo umetenda kinyume na maadili ya ndoa,umenikana mimi mume wako…’akasema huku akitikisa kichwa.

‘Yaani mke wangu unataka mimi nionekanae muongo, hebu angalia hii katiba, ina makosa gani, hii katiba ni ile ile, kama kuna makosa yamejitokeza, nilishakuambia tutayaangalia na kuyamaliza kama familia, kwakweli umenivunja nguvu...’akasema

‘Mume wangu, katiba ipi, unayozungumzia wewe, maana hii sio katiba yetu halali, sisi tunaitafuta katiba halali, ambayo mimi na wewe tulikubaliana, na wakili wetu akaipeleka kuisajili,...hadi hapa tulipofikia inaonyesha hii katiba sio halali, na sisi tunajaribu kukupa muda, ili useme ukweli, na wewe hutaki kusema ukweli, unaogopa nini kusema ukweli...’nikasema.

‘Mimi sijaogopa kusema ukweli, ukweli ndio huo niliousema na katiba ninayoitambua mimi ni hii hapa, haya, kama kuna katiba nyingine unayoifahamu wewe nionyeshe, na iwe imetimia, kisheria,iko wapi hebu nionyesheni, mbona tunabishana kitu kidogo tu..’akasema.

‘Hilo tu, usiwe na shaka.....’nikasema huku nikitaka kuichukua kwenye mkoba wangu, ile nakala ya katiba yangu niliyokuwa nayo, lakini kabla sijafanya lolote mwenyekiti akasema;

‘Mim ndiye mwenyekiti wa hiki kikao, heshimuni taratibu za kikao, .., na wewe mke wa familia , huwezi kufanya anavyotaka mume wako, mpaka nikuamuru mimi ufanye hivyo, na ningelipenda kutoa angalizo tena, sitarudia hilo tena, kama mnataka nitaondoka hapa mtafute mwenyekiti wenu mwingine, ...’akasema mwenyekiti.

‘Sitaki tena kurudia, hili, nataka mfuate taratibu, mimi ndiye ninyeongoza hki kikao, na ninasema hivi, hili swala huko linapokwenda ni kubaya, maana kama muhusika mkuu anasema katiba halali ni hiyo ambayo mwanasheria kasema ni batili, na mwenza wake, ambaye ni mke wake waliyeshirikiana naye pia kasema katiba hiyo sio halali...yeye bado anaendelea kusema ndiyo katiba halali, mnataka sisi tufanye nini, nawauliza nyie wajumbe mliopo hapa, ...’akasema mwenyekiti, wajumbe wakakaa kimia

‘Ndugu mume wa familia, unafahamu hatima ya haya yote, kuwa sasa hivi tutashindwa kufanya lolote kwasababu kile tunachokitaka kituongoze, kama ulivyotaka, kinaonekana kina mashaka, eeh, unataka tuongozwe na katiba batili, tuambie sasa…’akasema mwenyekiti

‘Ulituzia kwa mbwembwe kuwa katiba yenu ni kila kitu, katiba yenyewe ndio hiyo, je bado unataka ituongoze, hebu tuambie wewe tufanye nini, tunakuuliza maana muda unakwenda?’ akauliza mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, nikuulize swali tu,..mimi ni nani?’ akauliza swali na watu wakacheka,

'Msicheke jamani, kauliza akiwa na maana yake kubwa,....'akasema mwenyekiti

'Nataka nijibiwe...'akasema, akiwaangalia wajumbe.

‘Wewe ni mmoja wa wajumbe kwenye kikao hiki, au unauliza kuwa wewe ni nani kisifa ya ndoa, kama ni hivyo wewe ni mume, wa mkeo....’akasema mwenyekiti, na wajumbe wakacheka.

‘Au ni mkwe wangu, kwa sifa wanayoitambua hata watu wa magazeti….hasa ya udaku…’akasema

‘Mimi ni mume wa familia tunayoizungumzia hii leo, na wote wamjumuika hapa kwa ajili ya hii familia, na kikao hiki kinagusa mambo makubwa ya familia, sijui kama ndivyo ilivyo maana mke wangu hakuwahi kuniambia…’akasema

‘Sasa mmi kama mume ninaheshima zangu, na moja ya heshima, ni kuwa mimi ni kiongozi wa hii familia, na kama ni kiongozi, mimi ndiye ninayebeba majukumu yote ya familia, na kwahiyo mimi ndiye ninayetakiwa kuaminiwa...na ninachosema ndio msingi, wa familia,....kama hamuniamini mimi, mtamuaminini nani....’akasema.

‘Sikiliza mume wa familia, ...hapa ni kwenye kikao, na mnapoitisha kikao, kuna viongozi wanaokiongoza, wewe kama ni mume wa familia, ni kwako kwenye familia yako, hapa unakuwa mjumbe wa kikao, na unatakiwa kufuata taratibu za kikao,....kikao kinakutaka useme ukweli, ukisema kinyume chake, kikao kitakuhoji, ili kijue ni kwanini, na hicho ndicho tulichokifanya…sasa tuspoteze muda,…, tutahitajai kujua ni kwanini, mkafanya hivyo, ni kwanini kukawa na katiba mbili tofauti, hii na hiyo ambayo ni sahihi…?’ akauliza mwenyekiti.

‘Kwahiyo mnataka nisema mnayotaka nyie, kuwa hii sio katiba halali kuna katiba nyingine halali…maana mimi nimeshausema ukweli wangu, kama mume wa familia kuwa katiba ni hii hapa, kama kuna katiba nyingine, ya kwenu mnayoitambua nyie, basi itoeni,...mbona hiyo katiba nyingine haitolewi,....’akasema.

‘Kabla hatujafanya hivyo, unavyotaka wewe, tunarudia maswali yetu kwako, ili tuwekane sawa, je kama ikitolewa hiyo katiba ambayo ndiyo halali, ikathibitishwa hivyo, kuwa ndio katiba halali, upo tayari kuwajibika nayo…?’ akaulizwa

‘Mwenyekiti ni nini maana ya kuhitajia hiyo katiba, usiniulize maswali ambayo majibu yapo wazi…’akasema

‘Hiki kikao kinataka kauli yako,…maana kwani kwanza utakuwa umesema uwongo, pili umevunja sheria, tatu, umekaidi kikao ,hapo hatujaingia kwenye makosa yaliyosababisha kukiitisha hiki kikao, mke wako ana mashitaka, .....je upo tayari kuwajibika?’akauliza mwenyekiti.

‘Hiyo katiba nyingine ipo wapi, ..hilo ndilo la msingi, kwanini mnapoteza muda, kama ipo,...’akasema

‘Mhh, mimi ndiye nakuuliza swali, upo tayari kuwajibika..?’ akaulizwa

‘Kuwajibika nipo tayari , lakini kwa katiba ninayoitambua mimi, katiba iliyosajiliwa kihalali, sio hiyo ya kwenu, …mimi nitaisimamia hii maana ipo kihalali…’akasema

‘Mhh..jamani huyu mtu tumsaidieje…bodo anadai hii Katiba yake ndio halali…’akasema mwenyekiti

‘Sio swala la kunisaidia mimi, nasema hivi mimi nipo tayari kuwajibika kwa katiba yetu halali, inayotambulikana, hata kwa msajili ipo, hiyo yenu kwanza haipo pili haijasajiliwa, mumeitoa wapi, kama ipo na imesajiliwa mimi naapa nipo tayari kuwajibika nayo, na nyie mfanye hivyo, kama hii ndiyo inayotambulikana kwa msajili..’akasema na mdogo wake aliyekuwa kainama akainua kichwa na kumuangalia kaka yake kwa macho ya mshangao, nahisi kama angelikuwa karibu angemtuliza kaka yake asiendelee kuongea.

‘Unaona eeh, dalili za watu kama hawo zilivyo, wanaweza hata kuapa, inasikitisha sana...mke wa familia, umesikia mwenyewe,..sasa usisite kujibu maswali yetu ukimtegemea mume wako, jibu ukijitegemea wewe mwenyewe, mwenzako yupo kivyake,....’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naona tuendelee, kwani nahisi kuna tatizo, sizani kama mume yupo sawa, huyu sie yule mume niliyemfahamu mimi, mimi naona kuna tatizo....mimi nilitarajia mume wangu ungekiri kosa, ili tuweze kuyaweka haya mambo sawa, lakini naona ana ajenda ya siri, simuelewi tena…’nikasema.

‘Kuna tatizo !!! kwanini mke wangu unasema hivyo… wewe mwenyewe umekimbilia kwa wazazi wako kuitisha hiki kikao, ni mimi mwenye tatizo au ni wewe, na kikao kimefikia kunishutumu mimi, kwa vile nipo peke yangu, wako wapi wazazi wangu, yupo wapi wakili wangu, unahisi ni nani atakuwa upande wangu hapa…’akasema.

‘Swali umeulizwa, upo tayari katiba halali ifanye kazi yake?’ nikamuuliza.

‘Katiba halali ipi, una maana gani ukisema katiba halali, katiba halali ni ile ipo kwa msajili, nendeni mkawaulize,..mimi nipo tayari,...katiba halali ifanye kazi yake...mimi siitambui katiba nyingine na kama ipo nyingine ipo wapi, sasa...’akasema

‘Ndugu mwenyekiti, mume wangu, keshakubali kuwa katiba halali ifanye kazi yake, mimi ninaomba tuendelee, yeye hataki kuwa mkweli, na kutubu makosa yake, basi iliyobakia, kikao ndio kitaamua, na sio kikao, katiba hiyo halali ije ihukumu, basi mimi nimenawa mikono yangu....’nikasema.

‘Namuuliza tena muhusika, kiupendeleo zaidi, je umekiri mwenyewe kuwa katiba halali ikipatikana, ndiyo itakayoongoza yote hayo yatakayofuata,ndivyo hivyo ....?’ akauliza mwenyekiti

‘Msinitege,..ndugu mwenyekiti mimi naona hapo mnanitega, katiba halali ninayoitambua mimi ni hii hapa, kisheria,… sio nyingineyo, kwanza nyie muikubali hii katiba, kwasababu inatambulikana kisheria, halafu hayo mengine yatafuata...’akasema

‘Ni nani ataweza kuikubali katiba iliyogushiwa wewe...’nikasema kwa ukali

‘Ni nani kagushi hii katiba, ina maana serikali wao, hawajui kulinda mali zao, mnawashutumu hata watu wa..aaha, muheshimiwa mwenyekiti wewe na wenzako ndio mnatunga sheria, je sheria halali ni ipi, niambie nyie..ni kile kilichosajiliwa kihalali au ni hicho chenu cha maneno matupu, niambieni jamani....?’ akauliza

‘Kwahiyo wewe unataka kikao hiki kikuthibitishie hilo, kuwa katiba hii imegushiwa, kuwa Katina hiyo haitambulikani kisheria, na walioitengeneza ni wakosaji, na sheria ifuate mkondo wake au sio..maana kama unafikia kunishutumu mimi kuwa kama mtendaji wa serikali sijui wajibu wangu, umefika mbali, sasa wewe unataka tulifanye hilo..?’ akauliza mwenyekiti

‘Mimi nimeongea kwa nia njema tu, …je mlitaka mimi nisemeje, sawa thibitisheni, na mimi ndio nitakuwa nimeamini, maana mpaka sasa mimi naamini hii ndio katiba halali…ikitokea vinginevyo, nipo tayari kuendelea na hiyo Katiba mnayodai nyie kuwa ndiyo halali...sasa thibitisheni, tusipoteze muda…’akasema kwa kujiamini, na mimi nikamwangalia kwa mashaka, na kusema;

‘Sawa mwenyekiti endelea na kikao, nipo tayari kwa lolote lile, nimeamini kuwa mume wangu ana lake jambo, kama hana tatizo kichwani, docta rafiki yake, hebu tusaidie, kweli huyu mtu yupo sawa, ...’nikasema na mweneykiti akasema

‘Mjumbe anataka tuthibitishe kuwa katiba hiyo aliyo nayo sio halali, na kwahiyo tunaingia kwenye kipengele cha kisheria,..hatukutaka tufikie huko, lakini kwa vile mwenzetu kashikilia msimamo wake, basi inabidi tumpe haki yake, kabla hatujaangalia ni jinsi gani swala hili tutakavyolipeleka kwenye nyombo vya sheria ninataka kumuuliza tena mume wa familia...’akasema mwenyekiti.

Mume wangu pale akashtuka na kusema;

‘Kwanini unasema hivyo, ni nani kasema tulipekele hili swala kwenye vyombo vya sheria, ...wakati katiba ipo hapa,...mimi sijasema tushitakiane,mimi nimetaka ushahidi, na kuonyeshwa hiyo katiba nyingine mnayoikubali nyie...hiki ni kikao cha familia, sio kushitakiana hapa..’akasema mume wangu.

‘Umesema kuwa hiyo katiba uliyo nayo ni halali, na hutambui katiba nyingine, mke wako anasema hiyo katiba uliyo nayo sio halali, imetengenezwa, wakili wenu kabainisha wazi kuwa hiyo katiba siyo ile aliyoisajili yeye, ina maana hapo unagusa sheria,, ...hivyo vyote vipo kisheria, na vimesajiliwa, je tutajuaje kipi ni kipi,kama hatutakwenda kwenye vyombo vya sheria, wakathibitisha hilo..’akasema mwenyekiti.

‘Vyombo vipi vya sheria zaidi yangu mimi na mke wangu ambao ndio tulioitengeneza hiyo katiba...hii katiba ipo kwa msajili, ndiyo sheria, mimi na mke wangu, ndio wahusika, tupo hapa, mnachotaka zaidi ni nini, najua lengo lenu ni nini....’akasema

‘Lengo letu ni nini…?’ akauliza mwenyekiti

‘Ni kuvunja ndoa yangu, na mimi sitakubaliana na hilo…katiba halali ni hii nah ii ndio ipo kwa msajili, mpende msipende ndio hivyo…na mimi ni mume wa familia hii, mpende msipende ndio hivyo…’akasema

‘Kwahiyo hiyo katiba unayodai wewe ndiyo iliyopo kwa msajili.si ndio hivyo..?’ akaulizwa

‘Ndio hivyo mwenyekiti, ukitaka kulithibitisha hilo, twendeni huko…’akasema

‘Kumbe tusipoteze muda, ngoja tumuulize huyo mdhamini wa serikali, swali ni kuwa je tukimuuliza akisema kuwa katiba hiyo sio halali, ipo katiba nyingine utasemaje?’ akaulizwa

‘Labda muwe mume-mnunua..maana nitasemaje sasa, maana nina uhakika katiba iliyo huko ni hii…mimi na wakili wangu tulikwenda kulihakikisha hilo, sasa nitaona ajabu ikiwa tofauti,....’akasema

‘Unasema nini, labda tuwe tume-mnunua, una maana gani hapo, hizo kauli zako sio nzuri, lakini sawa, kama umefikia huko, ngoja tuone ubabe wako..upo tayari sio?’ akauliza mwenyekiti kwa hamaki

‘Nasema hivi huko kwa msajili ipo nakala hii, huo ndio ukweli, hakuna katiba nyingine zaidi ya hii, kaulizeni vinginevyo, mnapoteza muda wenu tu, kwanini lakini kwani nyie hamna ndoa zenu..’akasema kwa kujiamini.

‘Jambo gani hebu liweke wazi, maana uunatamka maneno sasa ya zarau, kauli za dharau, mimi mwenyekiti sitaweza kuzivumilia , nataka maelezo kuhusu hiyo kauli uliyoitoa, kumnunua nani… vinginveyo uifute hiyo kauli yako,...’akasema mwenyekiti.

‘Samahani mwenyekiti, kauli hiyo ilinitoka kwa bahati mbaya, sio dhamira yangu, nimeifuta,unafahamu hapa nimechanganyikiwa, najiona kama nipo peke yangu wote mnanisakama mimi...’akasema kwa kusikitika.

‘Hakuna anayekusakama hapa, acha kauli za kienyeji, hapa tupo watu wazima waliosoma, wanaojua sheria, usiseme kauli za kizalili, jitetee kisheria kama mume wa familia, kama unashindwa kujitetea kama mume wa familia, utakuwa hujui majukumu yako kama mume, wewe kila mara unatamba kwa neno hilo, `mimi mume, mimi mume,..’sasa thibitisha uume wako, kwa hoja, zenye mshiko na hapa tupo kwenye sheria..’akasema mwenyekiti.

‘Sijashindwa mwenyekiti , mimi ni mume wa familia,nipo tayari kwa lolote lile, tuendelee na kikao..’akasema

‘Haya tuendeee, mumemsikia mwenyewe akisema, kuwa yupo tayari kuwajibika kama katiba halali,itapatikana, kama katiba aliyo nayo itathibitishwa kuwa ni batili, ...sasa mimi naanza kazi yangu, ya kutaka uthibitisho, kwani katiba zote hizi kama ni halali, zitakuwa zimesajiliwa kwa msajili, na kama wao watakuwa na hii katiba, basi kisheria itabidi tuifuate..au sio...'akasema na wajumbe wakasema

'Ndio, ila mume wa familia akasema 'hapana'

‘Kwanini unasema ‘hapana’ ?’ akaulizwa

‘Lugha za vitisho mwenyekiti,…na pia, hiyo ya kusema kuifuta, huwezi kufuta hii katiba kwa mdomo tu, kwanza muikubali, na mkishaikubali ndipo tukae tuanze kuangalia ni wapi tubadilishe, ..na ndipo, tusajili hiyo ambayo mnaiona ni halali…’akasema

‘Leo wewe unatifundisha sheria…lakini hilo tuliache, sisi kwanza tunataka kukuthibitshia kuwa katiba yako sio halali, ..kama ulivyotaka, kuwa tuhakikishe huko kwa masajili…’akasema mwenyekiti

‘Sawa…’akasema

'Na huko kwa msajili kama wana katiba nyingine, itathibitisha kuwa hio katiba yako ni batili, na kwahiyo kuna udanganyifu umefanyika, kama kuna udanganyifu umefanyika, tunahitaji maelezo ya kina, kabla sheria haijachukua mkondo wake....watuambie na wao huko imekuwaje,...kuna nini, na n nani anahusika na yote hayo...’akasema mwenyekiti na mume wangu akatulia akimwangalai mwenyekiti.

‘Sasa mume wa familia,…subiri, ..’mwenyekiti akageuka kuniangalia mimi,

‘Nikuulize kwanza mke wa familia, je wewe umethibitisha kuwa katiba hiyo aliyoshika mume wako ni batili, sio katiba halali, mliyoitengeneza nyie na kusajiliwa kihalali ?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, nimethibitisha hilo...’nikasema

‘Kwa vigezo gani?’ akauliza mume wangu

‘Kwanza, kuna hizo alama zangu nilizokuwa nimeweka, kwenye hii katiba hazipo, ina maana hii ni katiba iliyotengezwa kivingine, pili kwa kupitia mwanasheria wetu kathibitisha kuwa hii katiba sio ile tuliyompa yeye kwenda kuisajili, na tatu yale yaliyoandikwa ndani yamebadilishwa, hayafanani kabisa na ile katiba halali, yamebadilishwa kiujanja ili kuleta maana nyingine tofauti na ile tuliyokubaliana,...’nikasema

‘Ahsante, sasa naomba mnipe muda kidogo niweke mambo sawa, sio lazima twende kwa msajili, uzuri wenzetu nao wamejipanga, sasa hivi wamerahisisha mambo, wana vyombo vya kisasa…’akasema akifungua laptop yake.

‘Siku hizi kuna vyombo vya kisasa, vitaturahisishia kazi,.. ila ikibidi tufanye hivyo,tutakwenda. Kwanza nataka kumpa nafasi ndugu yetu, kwa ushahidi mwingine, ...kama atazidi kukaidi basi hili tatizo tutalipeleka kwenye vyombo vya sheria ili wathibitishe wao …’akasema mwenyekiti huku akifungua komputa yake aina ya lap top, akafungua sehemu anayoitaka, halafu akachukua simu, na kupiga namba....

‘Siku hizi mambo ya mitandao yapo mbele, dunia sasa imekuwa ni kijiji kimoja, tunaweza kuwashirikisha wajumbe wengine japokuwa hawapo kwenye hiki kikao, ..sasa hivi tunakwenda chumba cha msajili wa katiba, yeye atakuwa nasi, ...’akasema na mara simu yake ikawa hewani.

‘Mimi ni muheshimiwa Malimoto, mkongwe wa siasa…hahaha kumbe namba yangu unayo, sawa sasa nimekupigia kwanza, kama mlivyosema siku hizi mpo ‘online..’ tunaweza kuwapata mbashara, au sio…naombe nikualike kwenye kikao chetu cha familia, kwa kukuweka mbashara, je una nafasi hiyo…?’ akauliza.

‘Sawa muheshimiwa, nipo na nafasi, hamna shida tupo kwa ajili ya wnanchi, nikusaidie nini…’akasema sasa akimuweka huyo muhusika hewani, akawa anaonekana moja kwa moja kwenye laptop ya mwenyekiti.

‘Hapo tupo na wajumbe kwenye kikao cha familia, ni kikao halali cha kifamilia, kikao hiki kinawajumuisha wanafamilia ambao kwa nia moja walikukabidhi mkataba wao, ambao ni katiba yao halali, ya kifamilia katika mambo yao waliyokubaliaan nayo ya kifamilia na makampuni yao,..natambua kuwa hilo ni jambo la siri la familia hiyo ...'akasema

'Ndio muheshimiwa japokuwa hiyo sio njia halali ya kuuliza jambo kama hilo, nafikiria ingelikuwa vyema wahusika wakafika ofisini...'akasema

'Nafahamu hilo , lakini si umenifahamu mimi ni nani..nisingeliweza kulifanya hili kama sio muhimu sana, na wahusika wapo hapa wameridhia hilo lifanyike, na hawa hapa...'akasema mwenyekiti, akielekeza kule kwa mume wa familia na mkewe na wakili wao

'Sawa endelea muheshimiwa...'akasema huyo mtendaji wa masijala ya mikataba.

'Sasa ni hivi kutokana na kutokuelewana kwa wanafamilia hawa waliopo kwenye kikao hiki, nakuonyesha, uwaone tena, na wao wajithibitishe..’akasema mwenyekiti na kuisogeza hiyo laptop, kuelekeza kwetu, halafu akawa anaionyesha kwa mtu mmoja mmoja, mimi na mume wangu na wakili wetu, tukatakiwa kujithibitisha kuwa tumekubali hilo lifanyike

Tukajithibitisha kuwa tupo tayari kwa hilo....na mwenyekiti akaendelea kusema;

‘Kutokana na matatizo hayo wanahitajia kutumia katiba yao halali kuhukumiana, kisheria, na sisi tupo kama wanafamilia kuhakikisha kuwa haki inatendeka, tunahitaji swala hilo limalizwe kifamilia, na kama kutakuwa na kutokuelewana zaidi tutalifikisha hilo swala mahakamani...’akasema mwenyekiti.

‘Lakini, samahani muheshimiwa, kama unasema kuna tatizo la kutokuelewana, hilo sasa ni swala la kisheria, kwa vile mkataba wao umesajiliwa kisheria, ningeliwashauri wakalifikisha mahakamani kwanza, kuliko kulifanya hivyo...’akasema huyo msajili.

‘Hilo litafuata baadaye, kama hatutaelewana, tunachotaka ni kuthibitisha tu jambo moja ambalo limeleta utata, ni kuhusu katiba uliyo nayo kwenye ofisi yako, tunahitajia kuithibitisha hiyo katiba yao kwenye kikao kuwa ipo kwako na imesajiliwa kihalali,...’akasema mwenyekiti

‘Ni kwanini imefikia hapo, tafadhali…?’ akauliza

‘Tatizo lipo kidogo, lakini kama wanafamilia tunaweza kulisahihisha, ni tatizo kuwa kuna kutokuamini kuhusu nakala ya katiba tuliyo nayo sisi, na hiyo iliyopp huko kwa msajili, ,,...’akasema mwenyekiti na huyo msajili akasema

‘Mhh, nimekumbuka, unajua kuwa muda walifika mawakili , tukaongea nao, kukawa na maelekezo kwao, niliwaagiza wafanye hivyo, lakini hakuna aliyefika tena hapa, kwani kuna utata ulijitokeza hapa kwetu....’akasema

'Sasa hayo ni mambo ya ndani ya kiofisi,..lakini kwa vile yapo tayari kisheria, na hukumu imeshapitishwa, na hiyo ni baada ya baadhi ya watu kulalamika, kuwa kuna ubadhirifu wa taarifa huku kwenye ofisi yetu, na sisi tulifanya uchunguzi na kugundulikana kuwa kweli kulikuwa ma mapungufu ya hapa na pale,...na ndio maana kupitia kwa mawakili wote waliowahi kuleta mikataba yao, katiba zao, tuliwaomba waje hapa kuthibitisha mikataba yao tena, kama kuna mashaka...’akasema

‘Ndio kusema kuwa wakili wenu analitambua hilo, ila tulishangaa, siku ambayo tuliwaita mawakili wote wenye mikataba yao hapa,kwa familia hiyo walifika mawakili wawili, kinyume na ilivyokuwa awali..’akasema

‘Na wakili huyo alitumwa na mume wa familia akimwakilisha yeye,kitu ambacho awali hakikuwepo, awali alikuwepo hakikuwepo awali,...huyo wakili,akasema katumwa kuthibitisha, kuwa mkataba uliopo ni huo huo,, cha ajabu zaidi, yeye alikuja na nakala tofauti na tuliyokuwa nayo sisi, ....

‘Nakala aliyokuwa nayo sio ambayo imesajiliwa hapa, nakala zote zikiletwa hapa , tulikuwa kwanza tunaziscan, yaani tunachukua nakala hiyo kwenye mtandao, na kuziweka kwenye huo mitandao, kwahiyo hata kama mtu atafanya mbinu na kuiba nakala, zilizopo hapa masijala, lazima tutakuja kuligundua hilo baadae,...’akasema

‘Sawa wakili aliyetumwa na mume wa familia hiyo, alikuja na nakala, ambayo ilikuwa sawa na nakala iliyokuwa kwenye kabati letu awali, lakini tulikuja kugundua kuwa hiyo nakala sio ile nakala halisi tuliyoiscani, na kuiweka wenye mtandao

‘Yawezekana wawili hao walifanya marekebisho baadae, lakini hilo halikuwahi kuletwa kwetu, ndio maana tukawaambia mawakili hawo kama kuna marekebisho yamefanyika, basi waende wakaelewane, na walete maombi upya, lakini mwenzetu hao hawajarudi tena. Sijui kwanini, na sisi hatuwezi kuondoa ile nakala halisi ya awali kwa nakala nyingine bila utaratibu wa kisheria .....’akasema

‘Sasa niwaambie hivi, kwa ajili ya kuweka mambo sawa, na kwa vile ule mikataba sahihi, umeshatengenezewa nakala yake, wanaweza kuja na barua ya kuwa hiyo nakala iliyopo sasa hawaitaki, wanataka hiyo nyingine mpya,.

‘Samahani kidogo, je kwenye makitaba yenu kulikuwa na nakala gani, kabla ya hilo zoezi la kupitia nakala mlizoziscan…?’ akaulizwa

‘Kama nilivyosema kulikuwa na mazaifu ya utendaji, na muhusika mwenzetu akafikishwa kwenye utawala , baada ya uchunguzi, na akakiri kuhusika kwa namna moja au nyingine, kwa shinikizo la mtu aliyemfanyia mlungula (blackmail),..hilo kwetu halina msingi, kwahiyo sheria imefuata mkondo, kwafukuzwa kazi,..kwahiyo msiwe na wasiwasi kwa hivi sasa kwani kila kitu kimewekwa sawa, na katiba halali nakala yake tunayo hapa, ....’akasema

‘Una maana gani kusema nakala halali?’ akauliza mwenyekiti

‘Kama nilivyosema awali, hilo ni swala la ndani ...kwenye kabati kulionekana nakala ambayo ina marekebisho, kinyume na nakala iliyopo kwenye kwenye mtandao..na sisi tunatambua wazi, hayo yametokana na mapungufu ya kiofisi au labda, ni wenyewe wahusika walitaka kufanya marekebisho, sasa waje wathibitishe hilo, na mawakili wao,...’akasema.
‘Samahani unaweza kutuonyesha nakala hilo hapa, mbashara, ili tuhakikishe kuwa inafanana nah ii tuliyo nayo hapa..’akasema mwenyekit’, na mata muhusika akasimama na kutoweka kidogo baadae akarudi na nakala, akaiweka hewani..halafu akasema

‘Nakala hiyo ipo kwenye mtandao, lakini nyie hamuwezi kuingia huko…’akasema

‘Sawa tufungulie kidogo kidogo…ili tuhakiki…’akasema mwenyekiti

‘Hii hapa ndio nakala halisi,....’akasema huku akiifungua ukurasa mmoja mmoja kwa taratibu...na wakili wa familia hiyo akawa ana hakiki na kupiga picha kwenye simu yake, mpaka ikaisha…na wote waliporizika, mwenyekiti akasema;

‘Je hiyo nakala iliyokuwepo kwenye kabati ambayo haifanani na nakala huyo halisi mnayo hapo..?’ akaulizwa

‘Haipo hapa ipo kwenye vyombo vya sheria kama ushahidi…’akasema

‘Tunashukuru sana, maana sasa tunaweza kuhakiki hili kwenye hiki kikao…’akasema na baadae mwenyekiti akazima laptop, na kumgeukia wakili wa familia, akamuuliza

‘Unasemaje, umehakiki vyema, na kila mmoja kaiona au sio…?’ akulizwa

‘Hiyo ndiyo yenyewe, ...umeona huo muhuri wangu ndio huu hapa…’akasema wakili akionyesha huo muhuri, na huku akifungua ukurusa mmoja baada ya mwingine, sasa kitumia simu yake.

Wakati hayo yakiendelea mume wangu alikuwa anasogea huku akiwa kashikilia ile nakala yake kama vile anataka kumuonyesha huyo msajili, lakini rafiki yake-docta, akamuona na kumsogelea, na kumvuta pembeni na kumnong’oneza , mimi nilikuwa karibu nao, nilimsikia akimwambia rafiki yake;

‘Usionyeshe kabisa hiyo nakala yako, utafungwa, hiyo nakala yako imeonekana ni bandia, kwahiyo kuna ukiuwaji wa sheria, na wote waliohusika, wataweza kushitakiwa, ...achana na hiyo nakala yako, ikibidi uiharibu kabisa, huo ushahidi... kilichobakia sasa ni kukubali kuwa kuna makosa yalifanyika, na ukubali mkataba wenu wa awali ufanye kazi yake, huna jinsi, ...’akambia rafiki yake, na mume wangu akatikisa kichwa kama kuukataa....alionekana hajakubali.

Mimi nikawa bado nipo naangalia yale yanayoendelea kati ya mawakili na wajumbe kuhakikisa uhalali wa mikataba hiyo yote miwili, na baadaye mwenyekiti akasema;

‘Haya zoezi hili limekamilika,na ushahidi alioutaka mwenzetu umekamilika, sasa turejee kwenye viti vyetu, tuingie sehemu inayofuata, na huku tukijiweka sawa, nataka mume wa familia atueleze ukweli, kikao kinahitaji maelezo yake ya ukweli, kwa jinsi ilivyotokea, hadi kupatikana hiyo katiba iliyogushiwa ‘akasema mwenyekiti

Mume wangu akawa kimia sasa

‘Hii sasa ni amri, tunataka ukweli, wenye mshiko, vinginevyo, baba, itabidi swala hili liende mbali zaidi,...’akasema mwenyekiti, akiweka vitu vyake sawa tayari kwa kuendelea na kikao.

Mume wangu alikuwa ameshafika kwenye kiti chake, na kukaa, alitulia akiwa hana raha, na baadaye akageuka kuangalia kulia na kushoto kwake, na sisi tukawa tunamuangalia kwa mashaka, kwa jinsi anavyo angalia huku na kule, halaf akauliza;

‘Mdogo wangu yupo wapi?’ akauliza na sisi ndio tukagundua kuwa kumbe mdogo wake hayupo, haonekani ndani ya chumba cha kikao, na hakuna aliyemuona wakati natoka kwani kila mmoja alikuwa akishangaa katoka muda gani.

‘Huyu mtu wenu kaenda wapi,..au kaenda kujisaidia mara moja, hebu hakikisheni hili maana huyo mtu yupo hapa kwa dhamana yetu…? akauliza mwenyekiti na yeye akiangalia huku na kule

Watu walitafuta huku na kule na baadae ikathibitishwa kuwa mtu huyo hayupo katoweka, katoroka…

'Ngoja niwaite watu wa usalama, ...hili haliwezi kuishia hivi, siwezi kuingia matatani kwa uzembe wa watu wengine...'akasema mwenyekiti, sasa akitaka kupiga simu.

NB: Haya tunaishia hapo kwa leo, sehemu ijayo tutaingia sehemu nyingine ya kikao hicho, cha kifamilia, je ni nini kitafuata.


WAZO LA LEO: Uwongo ni tabia chafu, ukiwa na tabia hiyo utambue kuwa wewe ni mwovu, na hutawahi kuwa na amani maishani mwako…kwani kila muda utakuwa na mashaka, mwenye tabia hiyo ni mtu mchafu , ananuka japokuwa hatoi harufu, ni heri mara mia ya mchafu wa mwili kuliko mchafu wa nafsi mwenye tabia ya urongo, Mtu mwenye tabia hiyo MNAFIKI. Tuepuke tabia hiyo, ili tuwe na maisha ya amani na raha.
 
SEHEMU YA 95

Mwenyekiti, akauliza tena;

‘Huyu mtu ameenda wapi, mnakumbuka nyie ndio mliotaka awepo hapa kwenye hiki kikao mkifahamu kuwa anatafutwa na polisi kwa uhalifu, na mimi nikamthibitishia ofisa wa polisi kuwa, huyo kijana atakuwepo hapa hadi mwisho wa kikao…?’ akauliza mwenyekiti na watu wote wakawa kimia.

‘Hakuna wa kujibu .. mnataka mimi nieleweke vipi kwa hao watu wa usalama, kuwa nilikuwa namuhadaa, au sio,…sasa niambieni huyu mtu kaenda wapi...?’ akauliza mwenyekiti kwa ukali, lakini wote walibakia kimia kuashiria kuwa hakuna aliyemuona akitoka.

‘Mwenyekiti, inawezekana huyu mtu alitoka kipindi tunaangalia hiyo lap-top yako, na kwa kipindi hicho hakuna aliyefikiria kuwa huyu mtu ataondoka…’akasema docta, na wakili naye akasema hivyo hivyo.

‘Haiwezekani mtu atoke humu ndani bila ya mtu yoyote humu, kumuona, docta , wewe na mke wako mlikuwa huku nyuma, karibu na yeye, nakumbuka hata wakati tunaendelea na hilo zoezi, hususani mke wako ambaye kwa muda mwingi alikuwa amekaa huku nyuma, alikuwa wa mwisho kuja kuangalia tunachokifanya, kwahiyo nina uhakika, yeye atakuwa kamuona huyo kijana akitoka, kwanini tusiwe wakweli, ...’akasema mwenyekiti.

‘Hapana mimi sijamuona akitoka, kiukweli mimi muda mwingi nilikuwa nimegubikwa na mawazo yangu, sikuwa nikimtizama mtu, na hata ningelimuona akitoka ningelijuaje kuwa anatoroka, sikumuona kabisa...sikuwa na haja ya kumuangalia yeye, nina mambo yangu mengi kichwani ya kuangalia, kwanini nihangaike kumchunga yeye, ....akili yangu haipo hapa jamani’akasema huyo mke wa rafiki ya mume wangu, na mwenyekiti akamwangalia kwa mashaka, na kumuuliza

‘Unavyozungumza hivyo hueleweki, ina maana haupo pamoja na sisi hapa kwenye kikao, sasa umefuata nini, ni kweli unaonekana kabisa kama vile haupo ndani ya kikao, upo kimwili lakini kiakili unaonekana haupo kabisa, kuna tatizo gani linalokukabili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Haya ni ya kwangu, niachieni mimi mwenyewe, kama ikibidi Itafika muda wake, mtayafahamu, ....mimi naona tuendelee na kikao, huyo muachieni polisi hao ndio kazi yao....’akasema huyo mke, na mimi nikaona niingilie kati nikasema;

‘Baba , hilo la kutoroka kwa shemeji yangu, tuwaachie polisi wakiuliza tutawaambia ukweli, sisi sio walinzi wa huyo mtu na sisi hatutawaficha ukweli,ni kuwa huyu mtu alikuja kwenye hiki kikao na baadaye akatoroka,sisi tungelifanyaje...’nikasema

‘Hilo unalitamka tu kirahisi bila kujali kuwa mimi ndiye niliyemdhamini, hivi kweli kuna mtu atakuamini ukisema hivyo, hivi nyie taifa la leo mna nini akilini mwenu, msipende kuchukulia mambo kirahisi tu, kitendo kama hiki kinatutia dosari, uamanifu wetu unapungua,..'akafoka mzee.

‘Ni kweli baba, lakini imeshatokea swala ni tufanye nini…’nikasema

'Kiukweli mimi sipendi kabisa tabia ya namna hiyo...unapoahidi kitu, unatakiwa ukitimize, ...mimi sio tabia yangu ya kukubali dhamana halafu ninakuja kuihini,mnaniharibia mwenendo na tabia yangu..’akasema mwenyekiti na kuanza kupigia simu, alikuwa akiwapigia watu wa usalama, akaongea na huyo mtu wa usalama, na kumuelezea ilivyokuwa na alipomaliza kuongea naye akasema

‘Sawa tuendelee, wanamfuatilia wao wenyewe kwasasa, ila imewakwaza sana, kwani hatukutimiza wajibu wetu,…sasa wewe kaka mtu, mdogo wako keshaharibu, hata kama tulitaka kumsaidia, sasa haitawezekana tena,.., keshajiharibia yeye mwenyewe kabisa, ...’akasema

*********

‘Kwanini mnamfanyia hivyo mdogo wangu,kwani ungekaa kimiya unafikiri hao polisi wangekuja kukuuliza, nyie mnajipendekeza tu kwa hao watu, lakini hawatawasaidia lolote, siku yako ikifika wanakusweka ndani kama hawakujui…’ akasema mume wangu, na hapo nikakumbuka jinsi alivyomnong'oneza kitu muda uliopita

‘Hiyo ndio tabia ambayo siitaki, na hilo nimekuwa nikiwakanya, ....kama umezoea tabia hiyo ya uwongo, mimi kwangu haipo, na kwanini unasema tumemfanya nini mdogo wako, hakuna aliyemfanya kitu mdogo wako, unajua mimi nilipanga nini akilini mwangu…’akasema mwenyekiti

‘Nilishakuwa na malengo ya kumsaidia, nilitaka tukitoka hapa mimi na yeye mguu kwa mguu hadi kwa hao watu kuona yeye ana hatia gani,....sasa sisi tushatimiza wajibu wetu kama raia wema, ....’akasema mwenyekiti.

‘Mdogo wangu hana hatia yoyote…,yeye sio mhalafu...polisi wanamshuku bure,wameshindwa kazi yao sasa wanapapatika...na huenda kaondoka hapa kutokana na vitisho vyenu, sasa mimi nasema hivi, kama litamkuta baya nyie ndio mtawajibika...’akasema mume wangu.

‘Tuendelee na kikao chetu, atawajibika yeye mwenyewe. Na wewe mkwe…, nakuonya, sasa sitaki utani,tuambie, imekuwaje, ukawa na mkataba tofauti na ule mliokubaliana na mke wako, na ukijua kuwa huo ni ukiukwaji wa sheria,umekiuka kiapo chako ulichokiweka kisheria wewe na mke wako, ndivyo unavyoishi hivyo,...?’ akauliza mwenyekiti.

‘Mimi sijui kama huo mkataba ni tofauti na ule tuliokubalina na mke wangu, kwangu mimi nauona ni ule ule,na kama nilivyowataka, japokuwa msajili kasema hivyo, nahisi na yeye kaongea tu bila ya kuuangalia mkataba huu nilio nao…’akasema akiwa sasa kaushika huko mkataba.

‘Mkataba huo ni ushahidi tosha kuonyesha jinsi ulivyo…’akasema mwenyekiti.

‘Ni ushahid wa nini, mimi sijui kama upo tofauti na huo wanaosema ni halali, kama wlaiona kuna tofauto hiyo kwanini hawakuniita mimi, mimi ndiye mume, niye ninayefahamu ukweli wa huo mkataba, sasa kama kuna tofauti mimi kiukweli sijui...na hiyo tofauti imetoka wapi?’ akauliza mume wangu.

‘Unamuuliza nani hilo swali, hilo swali tunakuuliza wewe, kama sio wewe, na kama hujui wakati wewe umekiri hapa kuwa wewe ni mume na wewe ndiye unayebeba dhamana za familia, haya tuambie ni nani aliyeugushi huo mkataba, kwanini kunapatikana mikataba miwili, huu mkataba ulio nao unatoka wapi, hayo ni maswali yako ya kujibu...’akasema mwenyekiti.

‘Hayo nimeshawajibu, sijui...ninachojua ni kuwa huu mkataba ndio halali.....na kama sio halali mimi sijui, kwangu mimi hadi sasa bado sijaamini kuwa kuna mikataba miwili, mimi sijui..’akasema na watu wakamwangalia kwa mashaka, na alipoona watu wanamwangalia yeye, akasema;

‘Kama ni hivyo, hebu tuuone huo mkataba mnaosema ni halali?’ akauliza

‘Umeshaonyeshwa na msajili wataka upi tena, eeh, usitusumbue .....’akasema mwenyekiti

‘Mke wangu kasema anao mkataba anayo nakala halali ya huo mkataba, kama anavyodai yeye,…nataka anionyeshe tofauti iliyopo kati ya mkataba huo na nakala hii niliyo nayo hapa....’akasema

‘Mimi naona lengo lako ni kutupotezea muda, hebu mke wa familia mtolee huo mkataba, anaoutaka yeye, na kwa amri ya kikao hiki, halali, tunataka ujibue maswali yetu, kwani kila ulichokitaka umekipata, kwahiyo timiza wajibu wako, sisi tumeshatimiza wajibu wetu....’akasema mwenyekiti.

Mume wangu akanigeukia, huku akionyesha kushangaa, pale aliponiona nikitoa mkataba kwenye mkoba wangu, nikauinua juu, na kusema;

‘Mkataba halali ndio huu hapa, mkataba ambao umeuulizia ndio huu hapa, hii ni nakala yangu...’nikasema na yeye akabakia mdomo wazi, akiwa katoa macho ya kutokuamini.

‘U-ulipatia wapi …haiwezekani…’akasema kwa kigugumizi

‘Mpe wakili wenu wa familia authibitishe kuwa ndio wenyewe,..’akasema mwenyekiti, na mimi nikainuka na kwenda kumkabidhi wakili wa familia ambaye aliufunua akaanza kuukagua na kufanya kama alivyofanya kwenye mkataba aliokuwa na mume wangu, halafu akatabasamu na kuuliza;

‘Umeipatia wapi hi nakala, ndio wenyewe kabisa, sasa mambo yamekwisha, tumemaliza kazi...’akasema kwa furaha.

‘Siamini ina maana mke wangu umeamua kunifanyia hivyo, ...ina maana ..haiwezekani, kumbe,..hapana,....umaupata wapi huo mkataba, uli...uli...oh, huyu mdogo wangu yupo wapi’akasema huku akiwa kashika kichwa.

‘Haya mume wa familia, sasa kazi inaanza, natumai sasa upo tayari, kuwajibika kama ulivyoahidi wewe mwenyewe,…hatuna muda wa kupoteza tena..,kama wenzako wamekusaliti, utakwenda kuwauliza baadaye, sasa hivi ni kazi ...jibu swali letu, kama ningelikuwa mimi ndio wewe ningekiri makosa na kukubali yaishe, maana mwisho wa hadaa ni fedheha, kwanini unataka ufedheheke’akasema mwenyekiti.

‘Swali gani,...sikumbuki kama uliniuliza swali...’akasema

‘Nilikuuliza kuwa kwanini huo mkataba uliokuwa nao ni tofauti na mkataba halali, tunahitaji kulitambua hilo, kama wanafamilia, kama wajumbe wa kikao hiki, na ikibidi pia sheria inatakuhitajia uilezee kwani wao bado wanatafuta kiini cha hilo tatizo, ilikuwaje kuwepo na mikataba miwili,..’akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi muda mwingi nilikuwa naumwa, na siwezi kujua jinsi gani huo mkataba ulivyobadilika, mimi hadi sasa sioni tofauti yake, sijaona hayo mabadiliko ni yapi...’akajitetea hivyo.

‘Kwahiyo bado hutaki kukiri kuwa kuna hujuma mlipanga, kuwa mlifanya kosa, kwahiyo kama wanafamilia, kama kikao tukufikirieje, unaonekana unatujaribu, unatuona sisi hatuna akili?’ akauliza mwenyekiti.

‘Sijasema hamna akili, lakini siwezi kusema mimi nimefanya hujuma, nikiri kosa ambalo sijalifanya, hilo halipo,kwani kama ni hujuma iliyofanywa mimi siijui, huenda kuna watu walifanya hivyo, bila ya mimi kufahamu….’akasema

Ni nani zaidi yako wewe ambaaye ni muhusika, na wewe ulianza kutimiza yaliyoandikwa kwenye hiyo katiba tofauti na ile ya kwanza, unafikiri sisi ni watoto wadogo au…’akaambiwa

‘Ninachoongea hapa ndio ukweli, kuwa kipindi hicho nilikuwa mgonjwa, yote haya yamefanyika, nilipopata ajali, ndio maana nimekuwa niking’ang’ania kuwa hiyo katiba ndiyo ile katiba niliyo kuwa awali na ndiyo iliyokuwa sahihi, mimi sikumbuki kuwa na katiba nyingine tofauti..mnakumbuka kuwa ajali hiyo ilinifanya niwe nasahau...’akajitetea.

Kukawa na ukimia kidogo

***********

‘Lakini kama sikosei, katiba hiyo inavyoonyesha ilibalidilishwa kipindi wewe hujapata ajali, ina maana mipango hiyo mliipanga mapema, na mlikuwa mkiifanyia kazi hatua kwa hatua,, na ajali hiyo ilipotokea mkapata sababu nyingine, na hiyo ajali ilitokea mkiwa kwenye michakato yenu ya kukamilisha hiyo hujuma....’akasema mwenyekiti.

‘Ulikuwa unawahi kufanya jambo, bahati mbaya ajali ikakukuta njiani…’akaambiwa

‘Mimi hayo siyajui, nayasikia kutoka kwenu, na kwa jinsi inavyokwenda hapa sasa, mimi naona nimuite wakili wangu, kwasababu mnataka kunitia hatiani, na mimi sitaweza kujitetea kwa hali kama hii, ni lazima mwanasheria wangu awepo...’akasema

‘Hatujafika huko, ikifika huko ikibid tutakupa nafasi hiyo, lakini bado tunakuhitajia wewe uwe mkweli kwetu, unasikia,…’akaambiwa

‘Hata nikisema ukweli ni nani ananiamini kwasasa..hakuna nyote mumeshaniona mimi ni mkosaji..nimekosa nini,…eeh, sasa ili na mimi niwe na amani, nataka hili swala liende kisheria, awepo hakimu wangu hapa…’akasema

‘Kwahiyo wewe, sasa unarudi kule kule, kuwa hili swala kwa vile ni la kisheria zaidi, na linaonekana ni kuvunjwa kwa sheria, kama alivyopendekeza awali wakili, tulipeleke kisheria zaidi, ikibid twende ngazi za juu, tulipeleke hili swala mahakamani, si ndivyo unavyotaka wewe..’akaulizwa

‘Sijasema twende mahakamani, ...sio lazima twende mhakamani, hapa tuna mawakili wenu, lakini hatupo mahakamani, hawa mawakili hawanitetei mimi, wanatetea nafsi zenu , matakwa yenu, mkinisakama mimi wao wataangalia jinsi gani y akunibana mimi kisheria wajuavyo wao,.. basi ngoja ni mimi nimuite wakili wangu ili naye aangalie upande wangu.....’akasema.

‘Hakuna anayekusakama wewe, wewe ndiye uneyeweka kwenye mazingira ya kuonekana hivyo, kama ungelikubali kusema ukweli, haya yote yasingelitokea, kwanini usikubali kuwa kuna shetani aliwapitia, mkaamua kupanga hayo mliyoyafanya, lakini kwa vile dhamira mbaya haijengi, basi imefika kikomo,kubali, tuangalie jinsi gani tutalimaliza hili tatizo...’nikasema.

‘Wewe mke wangu hujui tu, mimi nayafanya haya kwa masilahi ya familia yetu, hapa nafanya kila iwezavyo kuulinda ndoa yangu, wenzako wanataka ivunjike, hili lipo siku nyingi, kama kweli unanipenda, ulitakiwa uwe pamoja na mimi....huoni kuwa wamenitega,...lakini nawaambia hivi hata kama mke wangu haupo na mimi bado wewe ni mke wangu,...’akasema.

‘Sikuelewei ukitaja neno kupenda,....’nikasema.

‘Unaona, nilijua kabisa mnanitega, wewe na familai yenu, mumelipanga hili makusudi,na kwa vile umeshaona mumefanikiwa mipango yako, sasa unatafuta njia za kuniharibu kabisa maisha yangu, mimi sikubali....na kwa hilo la kukubali kuwa nimefanya kosa, mimi hadi hapo sioni kosa langu kabisa, mimi kauli yangu ni hiyo kuwa sijui kama hiyo katiba iligushiwa, na hiyo mipango mnayosema nyie mimi siifahamu, ni nani walifanya hayo nyie ndio mnaofahamu, sio mimi, kwanini mnanilazimisha niseme uwongo.’akasema.

‘Kwahiyo unataka tulitolee ushahidi kama hilo la hiyo katiba kuwa sio katiba halali, ujue kila tutakavyofanya hivyo ndivyo na sisi tunashindwa kukuamini tena, na hapo ina maana kuwa wewe haupo nasi..unajiweka mbali na sisi, unaikimbia ndoa yako kiujanja, huku unajifanya upo nayo’akasema mwenyekiti.

‘Tangu hapo naona mumeshaniweka pembeni, sizani kwenye nafsini mwenu mpo na mimi tena, mumeshaniweka kwenye kundi la wahalaifu, unaona mdogo wangu ambaye hana kosa mumeshamuitia polisi, na nahisi hata mimi mtanifanyia hivyo hivyo,niwaulize kama angelikuwa ndugu yenu wa damu awe anatafutwa na polisi, mngelimfanyia hivyo mnavyomfanyia ndugu yangu,au kwa vile sio ndugu yenu?’ akauliza

‘Huo ni unyonge unaojitakia, nimeshakuambia, wewe kama mume wa familia unatakiwa upambane kiume, lakini katika misingi ya ukweli na haki, hiyo kauli yako uliyoongea sasa hivi kuwa tunakuonea wewe na ndugu yako, ni kauli ya kujizalilisha, kujishusha, ni unyonge wako mwenyewe, ...ongea ukweli, toa hoja zenye mshiko, tuoni ukweli upo wapi,...’akasema mwenyekiti.

‘Ukwelii gani nitakaouongea sasa hivi mniamini, mimi sijajizalilisha, ndio maana ninaendelea kukataa hayo mnayonishinikiza nayo, haya nipeni huo ushahidi kuwa mimi nilikuwepo kwenye huo mpango wa kufanya hayo yaliyotokea...maana ndivyo mnavyotaka nyie, mimi nimeshawambia ukweli wangu, hamunikubalii, sasa kwa vile mnaona nasema uwongo, nikosoeni kwa kulibainisha hilo...’akasema kwa kujiamini.

‘Kwa hali hiyo ni kuwa hutaki kusema ukweli, unataka sisi tuutafute kwa nguvu za ushahidi, ..kama unataka iwe hivyo, sisi tutafanya, lakini kwa mtaji huo ni kuwa wewe hutaki kushirikiana nasi, hutaki kuwa mwenzetu, ukatusaidia tukalimaliza hili tatizo kama wanandugu....na kwa hali hiyo ikibainika na ndivyo ilivyo, tukatoa ushahidi, basi hatuna jinsi nyingine, hukumu itafuatia kitanzi chenu wenyewe kitakuhukumu.’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo nyie mnataka mimi niseme nini?’ akauliza

‘Sema yote yaliyotokea, jinsi gani mlivyoibadili hiyo katiba, na kwanini ,lifanya hivyo. Na mlikuwa na nani na nani, halafu unaomba msamaha yamekwisha,...sisi kama kikao tutakaa na kuangalia jinsi gani ya kulimaliza... huo ndio uadilifu na utawala bora, kwanini mnataka msutane kwanza, mshikane mashati, hata ifikie damu kumwagika, ...hiyo ni tabia ya watu wasio waungwana’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sio mtoto mdogo, wa kudanganywa kihivyo, nawafahamu sana, hapo mnataka kunitega tena, kama mlivyonitega hapo mwanzo, ...ukweli niliouongea ni huo huo, kama kuna ukweli mwingine niambieni nyie, na mnithibitishie na mimi kama nitaona kuna ukwel ambao niliusahau ,au nilikuwa siujui, maana mengi yametokea nikiwa mgonjwa, sikumbuki, nikumbusheni nyie,....’akasema

‘Na ikiwa ni hivyo, tukakuthibitishia kuwa ni mpango ilipangwa na wewe ukiwemo ukiwa na akili zako timamu, ukishirikiana na wenzako, kwa ajili ya masilahi fulani, .. upo tayari kuwajibika?’ akaulizwa

‘Hiyo ni juu yenu...lakini mimi sijui kama kulikuwa na mipango huyo, mimi sikumbuki....’akasema.

‘Unakumbuka sana, unalifahmu sana, ndugu mwenyekiti naona tunapoteza muda, huyo mtu nimeshamuelewa, ...anachotaka ni kuona je tunafaamu hiyo mipango yao, je tunafahamu hayo aliyoyafanya yanajulikana,...hataweza kukubali na kusema ukweli...mimi naona tuendelee na kikao, na hatima ijulikane, mkataba upo utafanya kazi yake...’nikasema.

‘Kutokana na uchungzi uliofanyika, inabainisha wazi kuwa mipango hiyo ilikuwepo kabla ya wewe hujapata ajali, ...watu wanaohifadhi hiyo mikataba, wamelibainisha hilo, na hata huyo mtu mliyeingia naye kwenye hilo kosa, baada ya kubanwa, na baada ya uchunguzi alikuja kusema kila kitu. Hata kama kulikuwa na shinikizo lakini ndani yake kulikuwa na mbinu zenu....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi hayo sijui....sikumbuki, kama nilivyowaambia ninachojua mimi , hii ndio katiba, niliwahi kuwekeana na mke wangu,kama kulitokea kubadilishwa, basi labda kuna mtu alifanya hivyo, akanitumia mimi kama chambo, kwa vile anafahamu kuwa kumbukumbu zangu hazikiwa sawa...’akasema

‘Alikutumia kwa msilahi ya nani, yake au ya kwako, hebu tuangalie hiyo katiba, tutakuja kuiangali vipengele mlivyobadilisha, vilikuwa vinamgusa nani, na kwa masilahi ya nani, na hapo mengi yatagundilikana, kwahiyo ndugu yangu,...usitudanganye hapa, na kama unahisi hivyo kuwa labda kulikuwa na mtu kafanya hivyo kukutumia wewe, basi tuambie ni nani huyo mtu...’nikasema.

‘Ni kwa masilahi ya familia yangu, mimi na wewe na watoto wetu…, ukiangalia hiyo katiba eeh , nilivyoisoma mimi, inatuhusu mimi na wewe mkwe wangu, na ya kwamba hakuna mtu mwingine wa kuingilia masilahi yetu, zaidi ni mimi na wewe, kuilinda ndoa yetu , watoto wetu na familia yetu kwa ujumla....’akasema

‘Ni ile ya mwanzoni ilikuwa haifanyi hivyo?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui hiyo katiba ya mwanzoni ilikuwa inasemaje, sikumbuki, kwani ninachofahamu mimi ni jinsi nilivyosoma kwenye katiba hii, labda nyie mnikumbushe ..’akasema.

Mwenyekiti akamtizama binti yake, na kutikisa kichwa, kama kusikitika, na wajumbe wengine kwenye kikao wakaonekana kuchoka, na hapo mwenyekiti akasema;

‘Naona tupate mapumziko kidogo, tukirudi tunaingia ajenda nyingine, sasa tukitumia katiba halali, mliyojiwekea nyie wenyewe, si ndivyo uliahidi mjumbe, mume wa familia, hakuna kurudi nyuma kwa hilo…’akasema mwenyekiti

Mume wa familia akabakia kimia

‘Tulishajua mbinu zenu, na huu ujanja wenu sijui mlifikiri hamtapatikana, na hapakwenye kikao, limeshafahamika, kuwa baada ya ajali, kuna muendelezo wa mambo mengi, ajali hiyo ilitumiwa kufanikisha mambo mengi, ni kama ilipangwa…’akasema mwenyekiti

‘Ilipangwa…!!’ akasema mume wangu kwa kushangaa.

‘Ni kweli baada ya hiyo ajali, wewe ulipoteza kumbukumbu, na mengi yalifanyika kipindi hicho, ...huenda ilichukuliwa hivyo kama mwanya wa kukamlisha huo mpango, mpango ulikuwa umepangwa kabla ya hiyo ajali, ...’akasema mwenyekiti

‘Kwahiyo unamaanisha kuwa kwenye huo mpango tulipanga mimi nipate ajali, ili baadaye nisingizie kupotewa na fahamu,yafanyike kama yalivyotokea ...hivi kweli kuna mtu mwenye akili zake anaweza kufanya jambo kama hilo la hatari, ina maana hata hawo madakitari walionihudumia wanahusika na huo mnao-uita mpango, maana wao wanajua fika kuwa nilipotewa na fahamu , na kupoteza kumbukumbu kwasababu ya hiyo ajali.....?’akasema mume wangu.

‘Hatukatai kuwa kutokana na hiyo ajali ulipoteza kumbukumbu na hali hiyo akasababisha wewe kutokukumbuka mambo ya nyuma, lakini hiyo kwa mtizamo wenu,na uchunguzi wetu hali hiyo ilikuwa imetokea kwa muda fulani tu, ambao kitalamu inajulikana, ...wewe ukauendeelza ule muda, na kuendelea kujifanya kuwa bado unaumwa, ili kutimiliza malengo yenu....’nikasema.

‘Hivi kweli mke wangu unaweza kusema maneno kama hayo, naona kweli umenichoka, sikujua kama utafiki hatua hiyo, ....kuna nini kibaya nilichokufanyia ambacho kimeweza kukugeuza na kunichukia kiasi hicho…?’ akauliza mume mtu.

‘Hakuna aliyekuchukia ni matendo yako yanatufanye tuwe hivyo, na kwanini hutaki kukiri kosa…’nikasema

‘Nikiri kosa , kosa lipi,..huo ni mtego wenu,..mtego ambao wazazi wako wanausubiria,…kwanini mimi nisingizie ugonjwa, mke wangu, kuwa naumwa na uzidi kuteseka, ili iweje, hapana, siwezi kukufanyia hivyo, hizo ni hisia umepandikiziwa, usiwasikilize watu wasioitakia mema ndoa yetu....’akasema.

‘Mjumbe, usitusingizie sisi wazazi, hilo ni lenu wawili,…mimi huwezi kunidanganya kitu,nakufahamu sana, usijifanye kuwa hayo yaliyotokea huyafahamu, nakufahamu na washirika wako wote nawafahamu…,mimi nilitaka kuona kuwa kweli labda umebadilika kama alivyokuwa akidai mke wako, lakini kwa haya uliyoyaonyesha leo, sioni ajabu ....lakini haya bado tuendelee kukupatia nafasi nyingine ya mwisho..ila kwangu mimi nataka kusikia ulivyofanya hayo, na kwanini…ukiyaeleza kiunaga ubaga, nitajua kweli umekiri kosa na hukumu itabakia kwa wajumbe….’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sielewi hapo…ina maana baba mimi nijifanyize ajali, nijifanyize ugonjwa, hapana , hiyo sio kauli nzuri kutoka kwa wazazi…’akasema

‘Ajali iliyokupata, ilichukuliwa kama nafasi nzuri ya kufanikisha malengo yenu, na huenda kulikuwa na hujuma kwenye gari lako, hicho kitu utakuja kupambana nacho kwenye taarifa ya polisi ambayo haijawekwa wazi,..ajali hiyo...ilipangwa makusudi, ili itokee, ....’akasema mwenyekiti na mume wangu akamuangalia mwenyekiti kwa jicho la kushangaa…

‘Lakini hilo halikuweza kuthibitishwa,…kuna kitu kilitakiwa kifanyike, muulize mke wako aseme ukweli…atakuja kuyaelezea hayo yote kama kweli anataka kuelezea ilivyokuwa, hatujasikia alichopanga kuelezea,..wewe ndio umevuruga utaratibu…’akasema mwenyekiti

‘Unasema nilipanga ajali, baba ni kweli uanongea jambo kama hilo…na mke wangu unabakia kimia, ndivyo mlivyoongea hivyo..’akauliza

‘Inavyoonekana ndivyo..hata polis waliliona hilo, japokuwa halina nguvu, na mimi nikawaoba wasiliongelee maana ni hisia labda ..labda..na vielelezo, inavyoonekana ilitakiwa mimi ndio nije kupata ajali na hiyo gari,… nia ni mimi nife , kwani siku hiyo kama unakumbuka vyema nilikuomba gari lako, nilitumie mimi,....lakini kwa bahati , ukalichukua wewe mwenyewe, sijui ni kwa kusahahu au ilikuwaje, mimi hapo ndio sijui, ndio maana nikawaomba polis waliache hilo kama lilivyo....’nikasema

‘Huo ni uwongo wa hali ya juu, mimi nipange kukua wewe halafu unakubali huo uzushi, kwanini nifanye hivyo...’akasema mume wangu.

‘Hiyo ajali ilipotokea, ikawa imefanikisha baaadhi ya mambo yenu,hata kama utakataa kuwa hiyo ajali ilipangwa, kwa nia ya kumuua binti yangu, na iliposhindikana lengo lake hilo, ikageuzwa, ikachukuliwa kuwezesha mambo mengi,mengi yalifanyofanyika yalifanyika baada ya hiyo ajali, ili usiwepo nyumbani, ili isionekane kuwa wewe unahusika, ...’akasema mwenyekiti na mume wangu akatikisa kichwa kukataa.

‘Kiukweli hii ni kashfa ..mnanikashfu..na sitaweza kuvumilia hili..hiyo kauli yenu inanisikitisha sana…kiukweli siwafichi, imeniuma..na sijui kama nitaweza kuwaamini tena, sawa…ila nitataka hili mlithibitishe,la sivyo..hata sijui..’akasema

‘Kwa vile tumeongea sana na huu ni muda wa kupumzika, ...hiki kikao kinakupa nafasi ya mwisho, ya kufikiria kwa makini..., tukirudi uje na ukweli, kama utaendelea kutuficha huo ukweli ambao sisi tumeshaujua, kikao, kitakuchukulia wewe kama mhalifu ambaye kafanya kosa, lakini hataki kukiri kosa, na hivyo, unatuweka katika nafasi ya kutengeneza kesi, na yote mengine yatabainishwa, na hapo hatutakuwa na kurudi nyuma tena…’akaambiwa

‘Kesi ya nani,..ni nani mhalafu hapa..kuwa nilipanga kumuua mke wangu au…?’ akauliza

‘Ni kesi dhidi yako ndio…kudanganya , kugushi…na mengineo, yatakuja kujitokeza kama hutakubali kusema ukweli tukamaliza na mengine yakamezwa, sisi ni wanadamu, tutaangalia utu,…sasa kaam wewe hutujali, tufanyeje, kama hujijali familia yako, tufanyeje....’akasema mwenyekiti.

‘Hata siwaelezi…mimi nimeshasema yote haya,…ni kwa ajili ya familia, yangu, ndoa yangu, na watoto wangu, hata hiyo katiba imenipa mamlaka hayo,…sasa jaman kichwa kinauma…’akasema mume wangu, akishika mkataba wake mkononi, kama anataka kuondoka.

‘Sasa tukapumzike kidogo, nafahamu bado kuna ajenda nyingi, zenye maswali mengi yanayohitajai majibu mengi, wajumbe hapa wana yao mengi tu…, na yote ni dhidi yako wewe…au nyie wanandoa wawili.., na moja wapo jingine ni kuhusu kifo cha makabrasha,..hili linaanzia ni kwanini ulimuacha wakili wenu wa kawaida ukaamua kumtumia Makabrasha, kifo chake kimeanzia hapo, sasa jipange na hilo…’akaambiwa

‘Hahaha mnataka kusema mimi ndiye nilipanga hili pia, ili auwawe, hapo sasa mumevuka mpaka, hilo, nipo tayari, hata makamani…’akasema

‘Ni katika kuweka haya mambo sawa, kabla hatujaenda kumpumzika, hebu kwanza niambie ulikosa mawakili wa maana, mpaka uamue kumchukua Marehemu, eeh, kila mtu anajiuliza hilo…’akasema mwenyekiti

‘Yeye ni wakili mbona anatambulikana kisheria, mimi sijui kosa lake…’akasema

‘Nasikia , sio nasikia , ndivyo ilivyokuwa, kumbe marehemu ndiye alikuwa kichwa chenu akisemacho ni lazima mkifuate..na uliamua kumchukua kabisa sasa awe wakili wako ili kubadilisha hiyo katiba, lakini baada ya hilo, yeye naye akakugeuka, na ndipo kifo chake kikatengenezwa,…hahaha, mjumbe hili unalo, sisi tutamalizana na wewe lakini una kesi ya kujibu, haya hilo tutakuja kuliongea badae!’ Akasema mwenyekiti na kumfanya mume wangu amuangalie mwenyekiti kwa uso uliokunjamana kwa hasira

‘Sio kweli mwenyekiti, ninapinga hizo shutuma zote…’akasema mume wangu kwa sauti kubwa.

‘Tumeshachunguza na kuligundua hilo, …baada ya kugundua wewe umefanya makosa makubwa ya kukufanya uvunje ndoa ukose kila kitu, maana dhamira yako ni mali, hakuna zaidi…vingine ni visingizio…ukaona njia ya kulikwepa hilo ni katiba…mikakati ikapangwa jinsi gani ya kubadili katiba, marehemu akakuambia hiyo ni kazi rahisi kwake...’akasema mwenyekiti na mume wangu akawa kainama chini.

‘Marehemu anatambulikana kwa uhalifu wake wa milungula, wenzetu huko majuu, wanaita blackmail. Yeye kwasababu alisoma soma huko nje, akaona kwa wabongo, hawana ufahamu sana na mambo hayo, basi anaweza kuutumia njia hiyo kujitajirisha, hapa kwetu...’akasema mwenyekiti

‘Kosa kubwa linalobainsiha mipango yako, ni huko kumtumia Makabrasha, ni kwanini umchukue yeye,… lakini hukujua kuwa unamfuga nyoka, ili akulinde, wakati yeye ana sumu,, sasakwanini usituambie ukweli,ili tuweze kuliweka hili jambo sawa,...tutahitajai majibu yako, ili tukusaidie, kama hutaki, haya tutaona mbio za sakafuni huishia wapi..hilo...tukirudi,...usikimbie kama mdogo wako..’akasema mwenyekiti, na mume wangu akasema;

‘Makabrasha ni rafiki yangu wa siku nyingi, kumtumia yeye, kwangu sio jambo la ajabu sana, hilo naweza kulithibitisha popote pale, waulizeni hata familia yake,.. na mengi anasingiziwa tu, mimi sipendi kumuongelea marehemu, lakini nitajitetea kwa nafasi yangu, na kumtetea yeye ikibidi,lakini mimi sitapenda kumuongelea yeye sana, maana hayupo duniani,…’akasema

‘Sawa tutaliongea hilo baadae…kila kitu kipo tayari, ushahidi wote upo, ukikana huo ushahidi tunauwakilisha polisi, wao watajua jinsi gani ya kukufanya, hapo hatutakuwa na lawama tena ..’akasema mwenyekiti

‘Vyovyote iwavyo, mimi sikubali kuivunja ndoa yangu…’akasema

‘Tutaona hilo tukirudi, kama nikuivunja ndoa yako utakuwa umeivunja ndoa yako wewe mwenyewe,…muda umekwenda jamani…mnasemaje, tukapumzike kidogo halafu tutarejea, au vipi docta… ’akasema mwenyekiti,..na watu wakasimama na kunza kutoka nje

************.

Mume wangu badala ya kutoka nje akanizonga,

‘Wewe mke wangu haya umeyasababisha wewe, sasa nakuambia hivi hata ufanye nini, ndoa haivunjiki…si ndioengo lenu hilo…sasa ndoa itabakia hivyo hivyo, ili tuone mwisho wake…’akasema

‘Kwanini hutaki kusema ukweli tukayamaliza haya mambo..?’ nikamuuliza

‘Tungeyamaliza tukiwa sisi wawili kulikuwa na kosa gani, kulikuwa na haja gani ya kuita watu hapam kuanza kuumbuana na kunitwika makosa ambayo sio ya kweli..?’ akauliza

‘Hilo la kuita watu bado kabisa, sijaliongelea,…huo ni mwanzo tu…maana umesaidia kuweka mambo mengine sawa, kushinikiza kwako kwanza tuongelee mkataba umenisaidia sana, sasa tutaingia kwenye kadhia yenye, ni kwanini nikaitisha hiki kikao, jiandae kwa hilo, mume wangu nimekupa muda wa kutosha umeshindwa kuutumia, nimeshajua lengo lako, sasa kabla hujaniwahi, naona kila mtu alifahamu hilo…’nikasema

‘Hahaha, mke wangu, unafikiri mimi naogopa, utaona..hata kama hilo mumepanga wewe na baba yako, au sio mimi halinitishi kwani wewe unajua mangapi yako ninayafahamu tu,...wewe na rafiki yako mlijadili nini..hilo hutaki lisikiwe na watu, eeh,…na na hapo nakupa angalizo tu,…na jingine nikuambia ukweli, hakuna mwenye uwezo wa kuvunja ndoa yangu, hakuna..…wanasahau kuwa ndona inavunjwa na mume…’akasema.

‘Kwanini unatetea kitu ambacho hakipo, au hulijui hilo..kiimani, kisheria..wewe kwa vitendo vyako ulivyovifanya, ulishaivunja ndoa yako wewe mwenyewe, bado unashikilia kuwa ndoa ipo ndoa ipo, hebu niambie, ina maana gani kung’ang’ania kuwa ndoa ipo na wakati matendo yako yanaikana, una watoto wangapi nje,..eh, kauli zako za kuikana ndoa, umeziongea mara ngapo kwa hao mahawara wako, eeh,....’nikasema

‘Haya ongea tu..utaongea mengi,lakini na mimi utanipa nafasi ya kuongea mengi, nasubiria hio nafasi,…na kuvunja ndoa ni kutoa talaka, ni nani alitoa talaka …wapi nilikutolea tamko kuwa nimekupa talaka,..wapi kwa maandishi gani, acha wewe…huo mkataba uliubuni wewe, haya kama uliubuni wewe ndio mimi nimetoa talaka, humpati mtu hapa…ndoa haivunjiki …hata wafanye nini..’akasema kwa kujiamini kabisa.

‘Ndio ni mkataba…ulishatamka kama ukifanya hili na lile basi ndoa haipo, hukutamka kwenye kile kikao, mbele ya wakili, au hilo umelisahau,…hujazaa nje,…au hilo utalikana, utamkana mtoto wako, huo sio ushahidi yote haya yameandikwa waziwazi, hata ukisema ni mimi nimeubuni huo mkataba, lakini kauli zako je…mume wangu tuliza kichwa, kuwa mkweli, ongea ukweli tuyamalize haya…’nikasema

‘Hahaha..mke wangu, tatizo wewe hujui kuwa mimi nina mambo yako mengi tu, mimi sitaki kusema sana maana wewe ni mkwe wangu nitakulinda wewe na familia yangu…hilo nimeahidi…’akasema

Mara baba akaingia, yeye alishatonga nje akiwa anaongea na simu, na alipotuona tunazozana na mume wangu akasema;

‘Jamani kuna tatizo lolote...?’ akauliza mwenyekiti

‘Hakuna tatizo tunaongea tu na mke wangu...’akasema mume wangu huku akijaribu kukunjua uso wake.

‘Mimi, nimesema huu ni muda wa mapumziko, tutakutana baada ya nusu saa, mimi natoka, nimeitwa na ofisa upelelezi kituoni , nitarudi, kabla ya muda huo wa kikao, nikirudi nataka tuyamalize haya yote leo, nataka haki itendeke, na kashfa iliyotuama kwenye familia yangu isafishike, kwa amani, na vinginevyo, mimi sitakuwa na lawama tena....’akasema mwenyekiti

Na pale muume wangu akamwangalia baba mkwe wake kwa mashaka, na kusema;

‘Unaona, baba yako anakwenda wapi,....ndio zenu hizo, anakwenda kuwaweka sawa hao watu wake, ..kama mlivyowaweka sawa watu wa kusajili mikataba, lakini hayo hayanitishi mimi…’akasema kwa sauti ndoto ili baba asisikie.

‘Eti baba unasema unakwenda kituoni ni kuhusu shemeji, au kuna nini huko kuonana na mtu wa usalama ..?’ nikauliza

‘Ni kuhusu kesi ya mauaji ya Makabrasha kuna mambo wameyagundulikana zaidi na ni muhimu nifike nionane nao mimi mwenyewe kuhusu pia kutoroka kwa huyu mtu, maana mimi ndiye nilimdhamini, ..ni muhimu..’akasema mwenyekiti

‘Ina maana mdogo wa mume wangu wamempata..?’ nikauliza

‘Sijui, nitalifahamu huko mbele, ila walitaka kuja kumkamata na mume wako, wanahisi anahusika na kutoroka kwake..’akasema

‘Kwanini mimi nihusike…?’ akauliza mume wangu.

‘Kuna kitu umemtuma akakifanye, au …?’akasema mwenyekiti na mume wangu akabakia kimia, na mwenyekiti akaondoka zake.

Haya tutaona tukirudi mapumziko kama kikao kitaendelea.


WAZO LA LEO: Kuna matendo tunayotenda kila siku hasa kwa wanandoa, matendo ambayo kiimani, kimila, na kiutaratibu yanakuwa moja kwa moja yameshavunja miiko ya ndoa,…tunavunja mikataba ya yale tuliyokubalina siku ya kufunga harusi,, hata kabla hautajoa kauli zetu.

Kila kitu kina makubaliano na masharti yake, ndoa ina masharti na makubaliano yake, ndio maana ikaitwa ndoa. Je tunafahamu nini maana ya ndoa! Je kama ndoa ni kuhalalisha mahusiano mema kati ya wawili hao, iweje mtu amsaliti mwenzake kwa siri. Mtu anayeisaliti ndoa yake ni sawa na yule mtu anayeacha nyama yake safi nyumbani na kwenda kula nyuma iliyooza maporini, huyo keshavunja ndoa yake kivitendo,...Tuweni makini na ndoa zetu.

 
yan umeanza kuniringia hivi niwekee hata mbili mana imefika kule nataka

Sio kuringa mkuu, kisa ni kirefu nikiweka post nyingi italeta uvivu kusoma.

But kwasababu umeomba sehemu 2 tu, nipe dakika chache, naziweka
 
SEHEMU YA 96


Baada ya mapumziko mwenyekiti alirudi, na kutuambia tuingie ndani, ili yuendelee na kikao chetu, na wakati huo mume wangu alikuwa keshaondoka na haijulikani kama atarudi tena,au ndio keshakimbia kikao, nikataka kwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti, lakini kabla sijainuka kwenye kiti , mara mume wangu akaingia akiongozana, na jamaa mmoja na moja kwa moja wote wawili wakaenda kuonana na mwenyekiti.

‘Mwenyekiti nimeona nimchukue wakili wangu, ili aweze kunijibia maswali, kwani naona nimelemewa, ...’akamwambia mwenyekiti.

‘Kwani tulikubaliana vipi, na kwanini umtafute wakili, kuna kosa gani kubwa umeliona ambalo linahitajia wakili?’ akamuuliza mwenyekiti.

‘Lakini nyie mna mawakili wenu, ..mbona mimi sijalalamika hilo..’akasema

‘Hawa wapo kwasababu ni watendaji wetu wa kila siku wakili wangu ni mtendaji wangu wa kila siku, huyo wakili wenu, ni mtendaji wenu, anahitajika kutoa ushahidi wa huo mkataba,..haya ni mambo yetu hayahitaji mtu mwingine ambaye sie mtendaji wetu wa kila siku, na kama umeamua kuleta wakili, basi tulipeke hilo swala mahakamani...’akasema mwenyekiti.

‘Hapana nia ya kumleta huyu wakili ni kunisaidia tu, kwa saabbu kuna mambo mengine yanahitajia sheria, na natambua kabisa tukimaliza hapa, watakuja maaskari, kama sio mimi ni kwa ajili ya mdogo wangu, ndio maana nimeamua kumleta huyu wakili...’akasema

‘Ili afanye nini....?’ akauliza mwenyekiti.

‘Ili aone kama kweli ninatendewa haki,..’akasema

************

Ni katika kipindi kingine baada ya mapumziko, wajumbe wakaingia ukumbini, na mwenyekiti kama kawaida yake alishafika kwenye kiti chake, na walikuwa wakiteta,na mume wangu, baadae mwenyekiti akasema

'Kuna mjumbe kaongezeka, ...na taarifa hii nimepewa hapa na mjumbe mwenzenu, mume wa mtayarishaji wa hiki kikao;

'Huyo mnayemuona kakaa karibu na mawakili wengine ni wakili wa kujitegemea, yeye ni wakili anayemuwakilisha mume wa binti yangu...siwezi kulipinga hilo, maana huenda mwenzetu ana dhamira yake...' akasema mwenyekiti

'Lakini ndugu zanguni, je kulikuwa na haja gani ya kumleta wakili mwingine,...kulikuwa na haja gani ya kujihami kiasi hicho, sisi kama kikao, ..na ilivyo mujibu wa vikao kama hivi vya kifamilia, ni kutatua matatizo yale yaliyopo ndani ya kifamilia...'akasema mwenyekiti.

'Sasa ikizidi, au tatizo likivuka mpaka, ndio tunaweza kusema sasa tunakwenda mbele ya sheria, lakini kwa historia ya vikao vyetu haijawahi kutokea hivyo, labda hiki ndio kiwe cha kwanza..'akasema mwenyekiti.

'Karibu sana wakili, na huenda umeshaambiwa ni kitu gani kinachoendelea, sisi hatuna pingamizi, nia na lengo letu ni kuweka haya mambo sawa sawa...'akasema mwenyekiti na kunigeukia mimi

'Nikuulize wewe mume mtu, je upo hiari, na ujio wa wakili huyu , maana siwaelezi, kuwa na mawakili wakili, kila mtu na wake kwa jambo hilo hilo,...'akasema mwenyekiti akiniangalia mimi

‘Kama kaamua hivyo, ni vyema tu, ila nilitaka kumwambia huyo wakili atambue kuwepo kwa mkataba huo halali, na ule aliowahi kuonyeshwa awali autambue kuwa ni batili,..sasa kama yeye kaja na ajenda ya kuusimamia mkataba huo, wa awali ajue kuwa atahitajika kuwasiliana na mahakama au na watu wanaodhamini mikataba hiyo,..’nikasema

Wakili huo akanyosha mkono na mwenyekiti akageuka kutuangalia sisi wajumbe na kusema

'Hili jambo litatupotezea muda, lakini sawa, hebu tuambie muheshimiwa wakili,...'

‘Mimi nimeletwa hapa na huyu mteja wangu, alishanisimulai yote siku nyingi, na nilichukua nafasi ya marehemu, wakili wake wa awali,.., kwahiyo yote nayafahamu, sio mtu mgeni kwa hili linaloendelea hapa...’akasema.

‘Kwahiyo wewe unafahamu undani wa kila jambo la kifamilie, ikiwemo mikataba ya kifamilia, na kikazo..ya kuwa wawili hawa waliamua kutengeneza mkataba, ambao umekuwa ukiongoza familia na taratibu zao za kila siku ikiwemo makampuni yake?’ akaulizwa

‘Nafahamu,..’akajibu

‘Kuna uhakika kuwa mkataba huo wa awali uligushiwa, na mteja wako, akishirikiana na marehemu, kwa matilai fulani, je unalifahamu hilo?’ akaulizwa

‘Hilo ndilo limanifanya nifike hapa, kwani mteja wangu anashukiwa kufanya jambo ambalo, halitambui,...'akasema

'Kwa vipi asilifahamu maana yeye ndiye muhusika wa kuandaa mikataba yote miwili, wa awali ambo ndio sahihi, na huo mwingine wa kugushiwa...?' akaulizwa

'Kwa maelezo ya mteja wangu, yeye alikuwa akimtegemea wakili wake, na alifanya hivyo ili kupunguza mambo mengi aliyokuwa nayo, kwahiyo akampa na jukumu hilo la mkataba, kwahiyo likitokea jambo la kisheria kuhusiana na mkataba, yeye alikuwa akimuhusisha wakili wake huyo...'akasema wakili

'Ok...endelea...'akasema mwenyekiti.

'Kwahiyo alipopatwa na ajali, mambo yote ya kisheria yalikuwa mkononi kwa wakili wake huyo,na bahati mabaya akafariki,ikabidi sasa achukue ule mkataba aliomkabidhi wakili wake wa zamani awe anausimamia yeye kwa muda, huku akitafuta wakili mwingine ambaye likuja kunipata mimi.

'Kifupi yeye, hadi leo, ambao mumekuja kugundua kuwa mkataba huo una matatizo, alijua kabisa kwua mkataba ni ule ule, na mkumbuke jamani, kuwa mteja wangu alipatwa na ajali na kipindi kingi alikuwa kwenye matibabu, na huo mkataba, kama ulibadilishwa basi ulibadilishwa kipindi hicho akiwa mgonjwa,...’akasema wakili.

‘Una uhakika na hilo muheshimiwa wakili?’ akauliza mwenyekiti

‘Kwa taaifa za kutoka kwa mteja, wangu ndio nina uhakika..muheshimiwa mwenyekiti.’akasema huyo wakili.

Mwenyekiti akachukua simu na kumpigia msajili wa mikataba,na akaweka sauti a kusikika watu wote, na kumuuliza msajili,

'Samahani muheshimiwa kama nilivyokuomba awali, tutakwua tukikusumbua mara kwa mara, sasa kumetokea tatizo, kidogo, tulitaka kufahamu tu, ni lini tatizo la mapungufu ya kiofisi, lilitokea, nikiwa na maana ni lini iliogundulikana kuwa mkataba wa kifamilia wa hii familia ulibadilishwa

Huyo msajili akataja tarehe , na ikaonekana kuwa tarehe hiyo ni ya kipindi cha nyuma hata kabla mume wangu hajapata ajali,...

‘Umesikia tarehe iliyotajwa hapo, ilikuwa hata kabla mteja wako hajapatwa na hiyo ajali, mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa,je unawezaje kusema hiyo michakato ilifanyika akiwa yeye hajui! Kiukweli yeye alikuwa na ufahamu wake, na alishiriki, na alifahamu ni nini kinechoendelea na ndio maana ugonjwa ukaendelezwa mbele au sio ...’akasema mwenyekiti.

‘Mkataba huo uligundulikana kuwa umebadilishwa, kipindi mteja wangu akiwa hajapata ajali, inawezekana ikawa hivyo, hatukatai, lakini yeye alikuwa hajui kuwa mabadiliko hayo yameshafanyika, hana ufahamu huo kabisa,,...'akasema. na kabla hajatulia akaongezea kusema;

'Na kama waligundua hivyo, hawakumfahamisha mteja wangu, walimfahamisha wakili wake, ambaye na yeye kipindi hicho pengine, nasemea hivyo pengine, alitingwa na shughli nyingi, na alikuwa akisubiri muda muafaka wa kumfahamisha mteja wake,, na wakati anajiandaa kuja kuonana naye ndipo ikatokea hiyo ajali, ni ajali haina kinga, haina taarifa....’akasema wakili huyo

‘Uwongo una mwisho wake, sisi tunataka kuwaonyesha kuwa hayo yalifanyika kipindi ambacho mume wa familia hii akiwa mzima na fahamu zake na alipanga yeye na wezake hiyo katiba ibadilishwe, si ndio mnataka kila kitu kithibistishwe hii leo, hamtaki kusema ukweli, sasa mimi namsimamisha wakili wa familia anayetambulikana kisheria,atuelezee ilivyokuwa;…

Wakili wetu wa familia akasimama na kuanza kuelezea mchakatao mzima wa katiba ulivyoanza, hadi kukamilika, na mangapi yemeshafanyika na kumalizwa kikatiba, na mafanikio yake, na alipofika kwenye changamoto zake, akasema,;

‘Pamoja na nia njema ya katiba hiyo, bado kulikuwa na changamoto zake, lakini zaidi ni hizo zilizofanywa kwa makusudi kwa nia ya kuharibu lile lengo jema la kuanzisha hiyo katiba.

‘Kiukweli katiba au makubaliano kama hayo yangelitumika kwenye ndoa zetu, nahisi ndoa nyingi zingaliimarika zaidi, na hakuna ambaye angelidiriki kuvunja ndoa yake kwa matendo yake. Lakini sasa…’hapo akatulia kidogo akifungua makabrasha yake..

'Ilikuwa tarehe mmh,....’akaangalia kwenye mkabrasha yake na kutaja tarehe,’

'Siku hiyo alinijia mume wa familia ofisini kwangu..’akasema

‘Ina maana huyo hapo au sio..?’ akauliza mwenyekiti

‘Ndio mwenyekiti, ndio huyo hapo, ..alinijia ofisini kwangu, akasema amekuja na ombo la kutaka huo mkataba ubadilishwe baadhi ya vipengele nikamuuliza kwa vipi maana huo mkataba upo kisheria, na ukitaka kubadili chochote kwenye huo mkataba kuna taratibu zake,kwanza inabidi wakae yeye na mke wake wakubaliane, na baada ya hapo, inabidi tuandike barua yenye maelezo ni kwanini tunataka kufanya hivyo.. ...?’nikamwambia hivyo.

'‘Mimi nafahamu jinsi ya kuubadili, hata bila kupitia hiyo milolongo yrnu isiyo na maana, kwani mkataba ni wa nani, ni wa kwangu mimi na mke wangu, kwanini niwahusishe tena watu wengine, kama nataka kubadili sihitaji kumuomba mtu, wewe sema kama hauwezi nimtafute mtu mwingine atakayefanya hiyo kazi...'’akaniambia hivyo mume wa familia..'

‘Sio swala la kuweza, ni swala la utaratibu, yoyote anayefahamu sheria, ni lazima azifuate taratibu hizo,mimi nakushauri kwanza nenda mkaongee wewe na mke wako, muone kama kuna sehemu za kubadili,mkubaliane,ili tukienda kuomba, tufanye kazi ya kujitosheleza, sio leo hiki kesho kile, hatutakubalika kisheria…’nikwambia hivyo

‘Kama huwezi sema..bwana…’akasema
‘Hapana sijasema siwezi..wewe nenda mkaongee na mke wako kwanza, na kama mtanihitajia mimi niwepo kwenye hicho kikao, mimi nitakuja, ili tufuate utaratibu..’'nikamwambia hivyo'

Yeye akasema hivi....

‘Sikiliza wewe nimeshakuona hutufai, nimeshatafuta wakili mwingine ambaye atashughulikia maswala hayo yote, kwani kama jambo dogo kama hili linakushinda huoni utatukwaza, kuna mambo mengi yanahitajika, na hili dogo ni mojawapo, wewe umeshindwa, mimi kuanzia leo nakufuta awakili wa familia, nimeshapata wakili mwingine....’akasema hivyo kuniambia mimi.

‘Mambo hayaendi hivyo bro, kuna taratibu zake bosi, hata kama mimi mnaona sifai, ujue tumeshaandikishana mkataba , na kama mnataka kuukatisha huo mkataba wangu na nyie pia kuna taratibu zake, huwezi kuamua mara moja kuwa wewe sio wakili tena,....ngoja mimi nitongea na mke wako tukutane, tuone jinsi gani ya kulifanya hili jambo kisheria,...’nikamwambia hivyo

Na yeye akasema hivi....

‘Nimekuambia mimi kama mume wa familia, sijakuambia umwambia mke wangu, mke wangu ana shughuli nyingi za kampuni, hili la uwakili kaniachia mimi, kwahiyo haina haja ya kuongea na mke wangu na hata ukiongea naye haitasaidia kitu, maana nimeshapata wakili wetu mwingine..anayejua kazi...’akasema.

Mimi niliwasiliana na mke wa familia naye akaonekana kushangaa na taarifa hiyo, akasema nimpe muda kidogo yeye, ataongea na mume wake, na baada ya siku mbili, nikiwa ofisini kwangu nikafikiwa na ugeni..

'Mgeni huyo alikuwa ni marehemu Makabrasha...akiwa na ajenda ile ile kuwa amekuja kuchukua nafasi yangu, kwahiyo nimkabidhi shughuli zote, ...nikamwambia hilo halipo, na ili ahakikishe nikampigia simu mke wa familia, na mke wa familia akaniambia hakuna kitu kama hicho, na nisitoe chchote kwa huyu mtu, yaani Makabrasha...’

Makabrasha akaniambaia kuwa hilo lipo na litafanyika, kwani hayo ni mambo ya kifamilia, mume anaweza kuamau kubadili chochote kwenye mkataba, kama anaona kuna ulazima, kwa masilahi ya familia, ..akaongeza kusema kuwa mambo mengine yanaweza kusimamiwa na mume wa familia bila mkewe kufahamu,...

‘Na kwa jinsi ilivyo, kwa vile kuna mambo kama hayo ya mke kutingwa na kazi nyingi, na mume anatakiwa kuhakikisha kila jambo linatendeka vyema basi kuna haja, ya kurekebisha baadhi ya vipengele kwenye mkataba huo, umeona eeh, hilo halipo wazi kwenye huo mktaba, ndio maana nataka kufanyiwe marekebisho..’akasema.

'Sikiliza nikuambie jambo, ili wewe undelee kuwepo, fanya kama nitakavyo, ni kitu kidogo tu, hata ukirekebisha mke wangu hatafahamu, au sio…lakini kama hutaki sawa, kazi zote hizo itabidi nizifanye mimi, na wewe utakuwa na kazi,gani, eeh..hebu lifikirie hilo...'akaniamba hivyo.

Mimi nikamwambia;-

‘Wewe ni mwanasheria, unafahamu taratibu zilivyo... haiwezekani hayo mambo kufanyika kwa haraka hivyo, kwasabbu huo mkataba umeshasajiliwa, kuna michakato inatakiwa kupitiwa, kwahiyo ni bora hilo swala tukawauliza wahusika wenyewe kwanza na ni vyema tukalifanya wakiwemo wote wawili, hata hivyo, mke wa familia anasema hakutambui wewe kama wakili wa familia...’nikamwambia.

‘Na mume wa familia hakutambui wewe,a kama wakili wa familia, umenielewa hapo, ni nani mwenye nguvu ya kifamilia, mke au mume....’akaniambia huyo makabrasha.

Sikutaka kubishana na yeye, niliwasiliana na mke wa familia, na mke wa familia akazidi kunisisitiza kuwa huyo mtu hamtambui na kama akizidi kunisumbua,a basi hatua za kisheria zifuatwe,.

Baada ya kikao hicho huyo mtu sikumuona tena kuja kwangu, ila siku moja nilikwenda kwa msajili kwa nia ya kufuatilia mambo aliyonituma mke wa familia, nikiwa pale, nikajiwa na wazo la kupitia mkataba wa familia, nikaenda kuonana na huyo anayesimamia hiyo mikataba,

‘Cha ajabu kabisa huyo jamaa wa masijala ya mikataba akaniambia kwasasa hanitambui mimi,...anamtambua wakili mwingine, aliyeletwa na wahusika, kwahiyo sistahili kuchukua chochote, ikabidi nimpigie simu mke wa familia, na mke wa familia, akaniambia nifuatilie kwa msajili mkuu, na nilipokwenda huko, wenyewe waliona ajabu, wakaniambia niwape muda watalifuatilia hilo swala..

Wakati wao wanalifuatilia huko, mimi nikaona kuwa hilo sasa ni tatizo, hata kama ni ajira,unatafuta kipato, lakini kama kuna sintofahamu ya namna hiyo ni bora uwaachie wenyewe, lakini kwanza nikaona, nionane na wahusika wote wawili.

Nikaongea na mke wa familia dhumuni langu hilo, yeye alinikatali na kuniomba niachane nalo kwa hivi sasa, yeye ataona ni nini cha kufanya, hata hivyo mimi nikamshauri kuwa ni bora tukae kikao yeye na mume wake, na ikibidi tumkaribishe na huyo Makabrasha tuliongee kwa mapana, ili tupate muafaka, lakini mke wa familia alipinga kabisa kumkaribisha huyo Makabrasha akisema anamfahamu sana huyo mtu yeye hawezi kumruhusu mtu kama huyo kuingiza kwenye shughuli zake.

‘Basi tukakubaliana kuwa tukae yeye na mume wake, akakubali na tukakubaliana tufanye hicho kikao mwisho wa wiki hiyo, lakini kabla hicho kikao hakijafanyika ndio hiyo ajali ikatokea...’akasema huyo wakili.

Mwenyekiti akamuangalia wakili wa mume wangu na kumuuliza;

‘Je una swali lolote kwa wakili mwenzako, maana huo ndio ukweli wenyewe,sasa kama ulidanganywa, basi ujue umeingia choo cha kike...’akasema mwenyekiti na watu wakacheka.

‘Mimi hapo sioni tatizo, ..katiba sio msahafu, kuwa hauwezi kubadilishwa, wazo kama hilo la kufanya mrekebisho kumbe lilikuwepo, na alikuwa nalo mteja wangu, kipindi hicho hajapatwa na ajali, na alikuwa katika harakati za kulifuatilia hilo jambo kisheria kwa kupitia kwa huyo marehemu...hilo hatulipingi, ni jambo la kawaida...’akasema huyo wakili na akainama kunong’onezana na mteja wake, halafu akasema;

‘Ni kweli mteja wangu akiwa na nia hiyo alimtumia wakili Makabrasha, ambaye ndiye aliyeanza mchakato wa kufuatilia jinsi gani ya kufanya hayo marekebisho ya hiyo katiba, na wakati anaendelea na mchakato huo, bahati mbaya mteja wangu akapatwa na ajali, ya nyuma yakafutika kwenye ubongo wake, na alipopata nafuu, akaikumbuka katiba yake, na aliyoiona ndio hiyo aliyokuwa akiwaonyesha nyie, hakuwa na kumbkumbu zingine za nyuma, hata mkienda hospitali mtapata taarifa zake...kwahiyo michakato mingine ilifanyika yeye akiwa mgonjwa...’akasema wakili.

‘Nikuulize swali, hayo mabadiliko yaliyofanyika kwenye hiyo katiba mpya ndivyo alivyopendekeza mteja wako kabla hajapatwa na hiyo ajali au kuna mengine yaliongezwa yeye hakuwa hana ufaham nayo?’ akaulizwa

‘Hilo yeye hakumbuki, kwasababu hana kumbukumbu sana za nini kilitakiwa kibadilishwe, na mlipomshinikiza zaidi, ndio kumbukumbu ikaanza kumrejea kuwa hilo jambo lilikuewepo akilini mwake, kipindi cha nyuma, na bahati mbaya akapatwa na hiyo ajali, sasa huenda kweli hayo yaliyopo humo kwenye katiba ndiyo aliyokuwa amependekeza au kuna mengine yaliongezwa kwa ushauri wa wakili wake..yote yawezekana, tatizo lililopo hapa ni Makarasha hayupo, ndiye angeliweza kutupatia majibu ya hayo yote, na mbaya zaidi kazi zake zilikuja kuibiwa zote na watu, sasa sikuweza kujua wapi aliishia...’akasema huyo wakili.

‘Naona tusipoteze muda kwa hio, hapa tumeshaona kuwa kweli, kulikuwa na mbinu za kuibadili hiyo katiba bila ya mke wa familia kuhusishwa, lakini hazikufanikiwa,..vyovyote tutakavyoliweka, litasomeka kuwa kulikuwa na hujuma za hadaa, baada ya kukataliwa na mke wa familia, na wakati mke wa familia anajitahidi waliongee yeye na mume wake, akitafuta ni kwanini mwenzake anataka kuwe na mabadiliko katika hiyo katiba, mwenzake akawa anajaribu kupoteza muda ili wafanikiwe katika mbinu yao hiyo, na kwa haraka wakakimbilia kufanya hicho walichokifanya...’akasema mwenyekiti.

‘Kwahiyo basi katiba hiyo aliyokuwa nayo mteja wako ni batili, haipo, na haitambulikani kisheria, sisi tunaendelea kutumia katiba halali, na hiyo ndiyo tunayotaka ifanye kazi yake hii leo,...sawa muheshimiwa wakili?’ akaulizwa, na kabla huyo muheshimiwa wakili hajajibu, mume wangu akamnong’oneza kitu wakili wake, na wakili wake akawa kama anasita kuongea, na kukawa na kama ubishi , na wakili wake, akasikika akisema;

‘Hayo ni mambo ya kisheria huwezi kuyakwepa, acha iwe kama ilivyo, nitajua jinsi gani ya kupambana nao hawaniwezi hawa...’akasema na mume wangu akaonekana kutokurizika na maamuzi ya huyo wakili, na baadaye kidogo baada ya wao kuongea kidogo huyo wakili akamgeukia mwenyekiti na kusema;

‘Samahani kwa kuwapotezea muda, unafahamu mteja wangu anakuwa na wakati mgumu, kwani hiyo katiba inayotambulikana kisheria, yeye, haikumbuki sana, ...sasa inamuwia vigumu kwake kukubali moja kwa moja...naomba hilo mliweke akilini, ila anahisi hadi kufikia hatua ya yeye kuomba kuwe na mabadiliko, marekebisho, anahisi kulikuwa na vipengele vilivokuwa vikimkandamiza na kutokumpa nafasi ya kutumiza wajibu wake kama mume wa familia...’akasema huyo wakili.

‘Kwahiyo..?’ akawa kama anauliza mwenyekiti.

‘Kwahiyo mteja wangu anasema, tukiendelea kuitumia katiba hiyo ya zamani, yeye anaweza akadhulumia na kutendewa isivyo haki, na ndio maana aliamua hiyo katiba ifanyiwe ukarabati,..anaomba itumike katiba hiyo mpya kwa masilahi ya familia, kwani yeye ameipitia na kuiona ina faa sana kwenye familia yake..’akasema wakili.

‘Wewe kama wakili unaifahamu vyema sheria, hilo kweli ni sahihi, maana ukumbuke huo mkataba, ilishatumika huko nyuma, na hakukuwa na matatizo, matatizo yamejitokeza baada ya mteja wako kufanya mambo kinyume na makubaliano,....’akasema mwenyekiti, na kabla wakili hajasema neno mwenyekiti akaendelea kusema;

‘Hoja kama hiyo alitakiwa mteja wako aisema kabla,hajafanya hayo aliyoyafanya, kama tutakuwa tunabadili mkataba kila tukifanya makosa, au tukitaka kukidhia haja zetu, unafikiri huo mkataba utakuwa na maana kweli, je ni mkataba wa masilah binafsi au ni mkataba wa kukidhi haja za wote, na kwanini alipoona hivyo, hakuongea na mke wake kwanza, ..hizo ni njama za makusudi, hayo yanajulikana , hoja yake kwa sasa haina mshiko, hata wewe wakili unaliona hilo, kama unafahamu vyema kazi yako..mimi ninaona tusipoteze muda tuendelee na kikao chetu au sio muheshimiwa wakili,...?’ akauliza mwenyekiti.

'Mwenyekiti akanigeukia mimi, na kuniuliza

'Au wewe mke wa familia, unasemaje kwa hilo...maana wewe umekuwa mstari wa mbele kumtetea mume wako...haya tukusikilize na wewe...'akasema mwenyekiti.

‘Ndugu mwenyekiti, mimi naomba tuendelee na ajenda nyingine,...katiba yetu ni hiyo hiyo, tumashaona kuwa kulikuwa na njama za kuibadili, kwa vile mume wangu alishaona kuwa kafanya madhambi, tena madhambi makubwa, na akafahamu kuwa kutokana na hiyo katiba, ataingia matatani, akaamua kumshiriksiha makabrasha ,akimfahamu fika kuwa ni mtaalamu wa hadaa, wa kucheza an sheria kibatili, ....’nikasema.

‘Madhambi gani niliyafanya wewe mke, usitie mafuta kwenye moto, ..sisi tunataka kulimaliza hili kwa masilahi a familia, wewe unaleta mambo mengine,mimi ninaangalia mbali kwa ajili ya vizazi vyetu, na sio kwa ajili ya kuwafurahisha watu wengine, wewe hujui kuwa wenzako hapa, nikiwa na maana watu wasioitakia mema ndoa yetu iwepo, wana malengo mengine kabisa, kiuvunja ndoa yetu halali,….akasema mume wangu kwa hasira.

‘Kulimaliza hili kwa vipi ukumbuke hizo ajenda nyingine zinahusiana na huo mkataba, na tumeshindwa kuingia kwenye ajenda hizo kwasababu ya huo mkataba wenu wa bandia..., ‘nikasema na mume wangu akataka kusema kitu na mimi sikumpa nafasi.

‘Ujue fika, …ajenda nyingine, nikuhusu madhambi yako, yale uliyoyafanya ambayo ni kinyume cha katiba hiyo. Tumepoteza muda mwingi kwasababu ya uwongo wako, na sasa uwongo wako umebainika, na madhambi mwenyewe yatakuja kukusuta…’nikasema

‘Madhambi gani wewe…’akasema kwa karaha

‘Ina maana wewe hujafanya madambi, huna makosa…?’ nikauliza

‘Sema ukweli ..kama kwel huna madhambi,...mbona unaogop ahapo kutoa kauli…’nikasema na mume wangu akabakia kimia.

‘Tuendelee na kikao ndugu mwenyekiti…’nikasema, na kabla mwenyekiti hajaanza kuongea mume wangu mara akaanza kuongea kwa kusema;.

‘Sijafanya madhambi yoyote mimi, na wala siogopi, ninachotaka ni kuitetea ndoa yangu ambayo naona wenzako wanataka kuivunja kwa nguvu, kwa kigezo hiki cha kutumia huo mkataba, mkataba ambao uliipendekeza wewe, ukiwa umeshaongea na wazazi wako, mimi hilo nilishalifahamu, lakini kwa muda ule sikuwa na la kufanya...’akasema mume wangu, na mwenyekiti hapo akaingilia kati na kusema;

'Kwahiyo hilo unalikumbuka, kuwa mkataba huo ulipendekezwa na mke wako, wewe hukuhusika, au ...?' akaulizwa

'Sio swala la kukumbuka , ndivyo ilivyo,kila kitu hapa kinajionyesha, mnataka mimi niseme nini zaidi ...'akasema

*************

‘Kwa vile tumeshaona kuwa katiba ya kugushi haina mamlaka tena hapa, sasa tunaingia kwenye sehemu ya nyingine ya ajenda zetu, na ajenda hii, ni kumuacha mke wa familia, aongee ni nini kusudio lake la kuitisha hiki kikao, ...’akasema mwenyekiti. Na pale nikaona mume wangu akiandika kitu kwenye karatasi na kuisogeza hadi kwa wakili …wakili huyo hakuwa amekaa mbali na alipokuwa mume wangu.

Mara wakili wa mume wangu akaonyesha mkono na kusema;

'Mteja wangu anasema hataweza kuingia kwenye ajenda nyingine mpaka swala hili la katiba ya kifamilia litatuliwe, kwani mkataba wao ndio msingi wa mambo mengine yote...'akasema wakili huyo

‘Hatuwezi kupoteza muda zaidi,..tafadhali mkumbuke hapa kuna watu wanataka kusafiri, kuna watu wameacha shughuli zao, kama docta pale, kwa ajili ya hili jambo, kiukweli tutakuwa hatuwatendei haki…’akasema mwenyekiti, na mimi nikaongea hata bila ya kibali.

‘Ndugu muheshimiwa wakili, mteja wako anafahamu fika kuwa kafanya madhambi mengi tu, na aliyafanya hayo akiwa na akili zake timamu, makosa ambayo kikatiba yetu ya kifamilia, ..nikiwa na maana mkataba…madhambi hayo yanatambulikana kama makosa makubwa, ambayo ukiyafanya, kama mkataba unavyojieleza, adhabu yake ni kubwa sana, na haina msamaha..kipengele hicho kwenye katiba ya kugushi kimeondolewa kinamna, ...'nikasema.

'Lakini huwezi kuyaita makosa makubwa , mpaka ibainike wazi kuwa ni makosa au sio na ikiwa na maana ni lazima kuwe na ushahid wenye mshiko, uliothabiti, au sio...'akasema wakili

'Na ndio maana tunahitajia tuendelee na ajenda nyingine ili kuyabainisha hayo makosa,...'nikasema

'Lakini mteja wangu hajakubaliana na hiyo katiba iliyojitokeza kwasasa, huwezi kumshikinikiza kwa kitu ambacho hakitambui unielewe hapo maana baada ya kutaja hayo madhambi ni nini kitafuta, si adhabu au, na je adhabu hizi zitatumia kigezo gani...'akasema wakili

'Ndugu muheshimiwa wakili, ukumbuke hii katiba tumeshaitumia zaidi ya miaka tisa, na haikuwahi kuwa a utata, kwahiyo tuna udhoefu nayo, tatizo ni hivi sasa, utajiuliza ni kwanini, ..jibu ni rahisi hapo,ni kwa vile kumetokea matatizo makubwa, matatizo ambayo mteja wako anafahamu fika kuwa ni madhambi makubwa, na hajataka kuyakiri hayo makosa,anajua ni kwanini...'nikasema.

'Sawa,...tumesikia hayo, lakini huwezi kuyaita madhambi makubwa, kwa mteja wangu, mpaka yathibitishwe, kuwa ni madhambi makubwa, na kwa ushahidi, ..na ushahidi bayana uwepo, hiyo ushahidi bayana ina maana kubwa sana hapo..’akasema wakili

‘Tutaonyesha hilo, halina shaka…’nikasema

‘Hata hivyo, hatuwezi kukimbilia kuhukumu kwenye katiba ambayo imeshatiliwa mashaka, na pande zote mbili, kwanza haikuwepo, imekuja baada ya hiki kikao, pili mteja wangu haiamini, ndio maana mteja wangu anaona kuwa kuna umuhimu kwanza wa kuhakikisha tatizo la mkataba limekwisha, na kila mmoja akawa karizika,…kwanini tukimbilie kwenye makosa kwanza....''akasema wakili.

‘Nimeshakuelezea hilo, kuwa mkataba huu, na matuzimizi yake haukuanza jana au leo, una miaka mingi, kwanini anaogopa hivi sasa, ni kwa vile kafanya madhambi, ndio maana anajihami…’nikasema

‘Mdhambi gani hayo, na kwenye mkataba yana msimamo gani..?’ akauliza wakili na hapo mume wangu akamuangalia wakili huyo kwa hasira, kama kumuonyesha hapo kuwa katoa swali sio mahali pake. Na mimi kwa haraka nikaamua kuitumia nafsi hiyo kuelezea …

‘Kwenye katiba yetu kuna makosa tuliyaanisha kama makosa makubwa, kama zinaa, uzinzi, kuua, kuiba, ushirikina ....hayo ni baadhi ya makosa makubwa, na humu kwenye katiba tulianisha kuwa, mke au mume akigundulikana kutenda hayo makosa,...hukumu yake..’nikatulia nikijaribu kufungua ule mkataba..

‘Haina haja ya kusoma, ile inasema makosa kama hayo, yanaruhusu talaka moja kwa moja, na mwenye makosa, hatapata haki yoyote, tunatambua kuwa mtoaji talaka ni mume, lakini hata mke anaweza kuiomba hiyo talaka, na hilo limebainishwa hapo, kuwa kama ni mume kafanya hivyo, talaka ipo wazi, sio swala kuomba tena, na mume hana haki y akudai chochote….’nikasema

‘Na maelezo hayo hayakubakia kwa mke au mume peke yake, kila mmoja limagusa,..na hata nini haki mtu anazikosa, zote zimeelezewa kwenye kipengele kinachofuata,..sasa ni kwanini kwa hivi sasa aogope mkataba usifanye kazi yake, ...yeye si anadai hana makosa, ..basi tuache ukweli useme...'nikasema na hapo mwenyekiti akaingilia kati, na kusema

‘Mimi sitaki kuingia undani wa huo mkataba kwani wakili wao yupo hapa, yeye ndiye mtaalamu wa huo mkataba ambo kwao waliuita katiba ya familia, kwani yeye ndiye aliyeikamilisha hiyo kazi kisheria, kama ni muhimu atasimama na kubainisha au kufafanua kila kipengele, lakini kwa sasa tunataka kuyafahamu hayo madhambi makubwa aliyoyafanya mume wa familia...au sio wakili..?’ akauliza mwenyekiti

‘Sawa ni vyema tukayaona hayo makosa, ili yabainishwe kama kweli mteja wangu kayafanya,…vinginevyo hatuwezi kuyatambua kama makosa..kwa kipengele gani….na...’akasema wakili na kabla hajamaliza, mume wangu akasema.

‘Hilo haliwezekani, huo ni mtego wakili, nimekuambia kuwa, uhakikishe swala la mkataba linamalizika kwanza, mimi siukubali huo mkataba, kwanini unataka uanze kufanye kazi,…wakili fanya kazi yako,…’akasema mume wangu

‘Ndio naifanya hivyo, usiwe na wasiwasi..bosi…’akasema wakili

‘Lazima niwe na wasiwasi, wewe huwajui hao watu, ni wanjana ndio maana nikakuita upambane nao kisheria,, sio ukubaliane na huo utumbo wao na mbinu zao za ujanja ujanja za kunitega, lengo lao ni ili kunichimbia kaburi, kama huwezi kazi sema, nikatafute mtu mwingine....’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Ina maana huu tunaoongea hivi sasa hapa ni utumbo, wakili mwambie mteja wako achunge kauli zake…hiyo sio kauli ya mtu muungwana, au sio?’ akauliza mwenyekiti aliposikia mume wa familia akilalamika.

‘Samahani ndugu mwenyekiti, hayo yamemtoka mteja wangu, akionyesha wasiwasi tu, ninamuhakikishia mteja wangu kuwa hilo la hiyo katiba lisimtie shaka, cha muhimu ni kuangalia hayo madhambi yanatotajwa, ni madhambi gani, kwani kama yalivyoanza kuelezewa, hayajafafanuliwa na ushahidi ulio dhahiri , kwahiyo hayana msingi, mimi kama wakili nitakutetea kisheria, na haki yako italindwa, una wasiwasi gani, usijali...’akasema huyo wakili kwa kujiamini.

‘Wewe umeharibu kila kitu… huo mkataba ndio msingi wa kila kitu hapa,…haukubaliki, unasikia, haukubaliki…’akasema mume wangu akimtolea macho wakili wake na mwenyekiti akaona asipoteze muda, akaendelea na kikao akisema;

‘Kwanza kabisa kama kawaida ya mambo ya kifamilia huwa tunampa nafasi mtetezi, atoe kauli ya kukiri kosa, kwani jambo hili ni la kifamilia, mtetezi, anaweza akakiri kosa na kuelezea udhaifu wake, na makosa yake, kwanini alifanya hivyo, kwa kupitiwa, au kwa makusudi, na sisi kama familia tutamsikiliza,...mnaonaje jamani tukampa huyu mtu nafasi ya mwisho…'akasema mwenyekiti

'Ujanja huo…swala hapa ni huo mkataba, mimi sina imani nao…'akasema mume wa familia

'Cha muhimu ni kwako ndugu, mtetezi, ni wewe kuongea ukweli, ukweli ni silaha kubwa kwa mtu yoyote, ukikiri kosa ukatubu, watu wanakusikiliza, kwasababu kila mtu ni mkosaji, sasa tunakupa nafasi hiyo mume wa familia, hapo hatuhitaji wakili wako, tunahitaji kauli yako wewe, kauli yako kwetu ni muhimu sana, ....’akasema mwenyekiti.

‘Mimi sijafanya hayo madhambi makubwa mnayonisingizia, yote ni uwongo na ni mbinu za kuniharibia ndoa yangu...’akasema mume wangu kabla hajaruhusiwa.

‘Je uliposema madhambi makubwa, ina maana unayafahamu hayo madhambi makubwa ni yapi, kikatiba?’ akaulizwa na akakaa kimiya na wakili wake akasema;

‘Mteja wangu anasema kuwa hayo madhambi mnayomshutumu nayo hajawahi kuyafanya, kibinadamu kuna kuteleza, yeye kama aliteleza hakupewa muda wa kujitetea, kama kuna jambo lilitokea akalifanya ni yale ya kibinadamu tu, yoyote anaweza kupitiwa, ndio maana alitaka katiba hiyo ifanyiwe marekebisho, maana inahukumu moja kwa moja bila kujali ubinadamu, bila ya kumpa nafasi mkosaji,...’akasema wakili.

‘Sisi tutatoa ushahidi kuwa hayo aliyoyafanya sio kwa bahati mbaya, kama ni kwa bahati mbaya mbona hataki kuyakiri hayo makosa, kukataa kwake, kuwa hajafanya kunaonyesha usugu, na uthubutu wa mteja wako, na tusipoteze muda, .kama hataki kukiri makosa basi sisi kama wanafamilia tunataka kuyaweka makosa yake hadharani, na wanafamilia watayaangalia, kwa mizania, je alifanya hayo madhambi kwa bahati mbaya au alikusudia,...’akasema mwenyekiti.

‘Kwanini anaogoa kama kweli hajayatenda,hajiamini! …muulize mteja wako,kwanini anaogopa hata kuyataja hayo madhambi…’nikasema na hapo mume wangu akaniangali na kusema kwa hasira

‘Ni nani anaogopa…siogopi kabisa, ila nawafahamu nyie, mambo yenu mnayapeleka kimtego, mtego…sasa mimi nawaambia hivi, mimi nitapigania haki yangu mpaka mwisho..ndoa haivunjiki kirahisi hivyo, nimeshalisema hilo, na ndio kauli yangu mpaka mwisho...’akasema na wakili wake, akamwendea na kumnong’oneza jambo, na mume wangu akasema;

‘Sawa fanya unavyoweza wewe, lakini…huo ni mtego, ..kwa hali kama hii, mimi..aah, umeshanikatisha tamaa,...haya endelea, uonavyo wewe...’akasema kwa hasira

Mwenyekiti hakuwasubiria akasema;

‘Mke wa familia uwanja ni wako…na tunataka usiongee maneno mengi, lenga moja kwa moja kwenye makosa, kama ni makosa, na mkataba wenu ndio utakaofanya kazi, kwani tokea mwanzo,mume wako ndiye alisema mkataba wenu ndio kila kitu, basi, sisi hatuna kazi tena, kazi yetu ni kupima uzito wa hayo makosa, kama yapo,..’akasema mwenyekiti, na mimi sasa nikaamua kusimama kabisa, na safari hii, nikiwa sitaki kabisa kumwangalia mume wangu, nikasema;

‘Mume wangu ana makosa makubwa, nikisema makosa makubwa itaeleweka, na hata kwenye mkataba wetu, hayo makosa makubwa yana nafasi yake, na ni mhimu kama tutakubaliana, niweze kuyataja hayo makosa yake kwa kifupi tu, na nitakuja kuyafafanua, au mkataba wenyewe utafafanua…’nikasema

‘Mume wangu kafanya makosa ya uzinzi, na zaidu ya hayo yeye ni mnafiki....’nikasema na mume wangu akasimama na kuniangalia kwa hasira

‘Unaleta matusi hapa..mimi ni mzinzi, una ushahid na hilo…’akasema mume wangu kwa hasira na wakili wake akamkalisha chini na kumnong’oneza kitu, na mimi sikumjali nikaendelea na maelezo yangu.

‘Kwanini nasema kuwa mume wangu ni mzinzi na mnafiki, angalia katika katiba yetu, kosa linalotambulikana kama huyo mtu ni mzinzi na au huyo mtu ni mnafiki..'nikasema

'Maneno haya ni kauli yake yeye mwenyewe siku ya kutunga huo mkataba alitaka hayo maneno yawekwe kama yalivyo, kuonyesha madhambi hayo makubwa, na akataka yawekwe hivyo kama yalivyo,kwahiyo mimi, sijakutukana kama unavyodai wewe, ila umejitukana wewe mwenyewe kwa matendo yako, kauli yangu inashuhudia tu hayo…ila wewwe ulikwisha kuyafanya hayo kwa vitendo vyako mwenyewe, ashakumsi matusi, kuwa wewe ni mzinzi kwa jina jingine wewe ni muhuni na sitasita kukuita malaya....’nikasema na watu wakaniangalia kwa mshangao.

‘Mumesikia wenyewe jamani…’akasema mume wangu akilalamika, lakini wakili wake alikaa kimia.

‘Sitamki haya meneno kwa nia mbaya, hapa wapo wazazi wangu nawaheshimu sana, naomba wakili wetu atusomee kwenye katiba yetu; mzinzi ni mtu gani, au Malaya ni mtu gani:..nikasema na mwenyekiti akatabasamu huku akitikisa kichwa kama kunikubali, na mwenyekiti akanyosha mkono kumruhusu wakili asome maana ya maneno hayo, wakili akasema;

‘Mzinzi ni tabia ya mwandoaa u mtu yoyote ambaye katenda tendo la ndoa kwa asiyekuwa mke wake au mume wake au yoyote akifanya bila kuingia kwenye ndoa..’akasema wakili.

`Na mnafiki ni yule asiyetunza ahadi, mwongo mdanganyifu, mzandiki, aliyeahidi akashindwa kutimiza ahadi yake, aliyeongea uwongo huku akijua anaongea uwongo, aliyeaminiwa akashindwa kutimiza imani yake kwa watu...na ...’akasema wakili. na mwenyekiti akakatisha na kusema

'Endelea na maana ya hilo neno jingine, tusipoteze muda, mtu akitaka kusoma ufafanuzi zaidi mkataba huo sasa upo huru...'akasema mwenyekiti

‘Na Malaya...hebu kidogo hapo..’ akasema mwenyekiti

‘Mwenyekiti mimi naona inatosha....’ nilitaka watu wasikie maana ya hayo maneno mawili ya awali kwanza…’nikasema

‘Mume wangu nimegundua kuwa wewe ni mzinzi, na tabia hiyo ipo kwenye damu,...na wewe ni mnafiki wa hali ya juu, kwa vile umehini ndoa yetu, umezini na wanawake zaidi ya mmoja, ukijua kabisa kuwa hilo ni kosa, na mungu akatoa ushahidi usiokwepeka, ...’nikasema na yeye akajifanya kutabasamu kwa dharau

‘Mume wangu wewe ni mnafiki, kwa vile umeyakana makubaliano yetu, ukadanganya, ukashindwa kutimiza yale uliyoyaahidi, na ukatafuta njia ya kuhadaa, tena kwa kuwaribuni watu waliopewa dhamana hiyo kwa kuwaonga, hilo ni kosa jingine kubwa...’nikasema kwa huzuni.

‘Hayo yote ni makosa makubwa, sio kwa mkataba wetu , lakini kifamilia, umejiabisha,… na uliyafanya hayo ukiwa na akili zako timamu na sio mara moja, ingelikuwa mara moja tungelisema,..ooh, ni bahati mbaya, uliteleza, lakini imekuwa ni tabia yako, hadi ukaumbuliwa ....na mungu hakukufichia madhambi yako, ....’mara mume wangu akasimama na kusema;

‘Sio kweli, wewe umeamua kunitukana tu na kunizalilisha tu, hayo unayoyasema yote ni uwongo, wewe nakuona sasa umeungana na wazazi wako, ili mnisaliti, hayo uliyosema nimeyafanya wapi, ni nani shahidi yako, ..nimeshutikia,lengo lenu, nia yenu ni kunizalilisha tu, wakili wangu yanukuu hayo matusi, kwasababu ninaweza kumchukula hatua huyu mwanamke, hanijui tu mimi..’akasema mume wangu.

‘Hujatukanwa, Katiba yenu inaelezea hivyo, ila wewe ulitakiwa umwambia mke wako athibitishe kauli yake, kama ni ya uwngo basi tutayachukulia kama ni matusi na wewe una hiari ya kumuadhibu mkeo, na hata kumshitaki kikatiba,lakini kama ni kweli, wewe una tabia hiyo, basi usikasirike kuitwa kwa sifa hizo..’akasema mwenyekiti.

‘Sio kweli , mimi sina hiyo tabia, yeye ni mtaalamu wa kuongea tu, anaona sifa sana kumharibia mume wake heshima yake, na hajui hilo kindoa ni makosa, unatakiwa ufiche siri za mwanandoa mwenzako, wewe unazianika hadharani, hiyo ni tabia gani, na wazazi wako wanakuunga mkono, siwaelewi kabisa mimi...’akasema mume wangu kwa hasira.

‘Ndugu mwenyekiti, sio kwamba napenda kutaja siri za mume wangu hadharani, lakini kwa hali kama hii alitegemea mimi nifanye nini, inabidi tufanye hivyo, kwasababu hukutaka kukiri makosa yake, na nilimuomba afanye hivyo, tukiwa sisi wawili, hukutaka kusema ukweli,,ni kweli si kweli...?' nikamuuliza mume wangu akasema

'Si kweli...'akasema kwa sauti kama ya kunishushua..na mimi sikujali, niksema;

'Wewe, uliendelea kufanya jinsi ulivyotaka wewe mwenyewe kwa masilahi yako binafsi, na hawo waliokudanganya, hata kwa kile cha makubaliano ya watu wawili...na mbele ya hiki kikao hukutaka kukiri ukweli, japokuwa kusema tu, kweli nilifanya nisameheni, hutukutaka ataje kila kitu, ...kukiri kosa kashindwa, je mtu kama huyu alitaka mimi nifanye nini, mimi nikae tu kimiya huku ukiendelea kuvunja amri za ndoa, hapana, hilo halipo...’nikasema na kutulia

‘Unanisingizia tu, hayo yote ni uzushi, na wewe nashangaa siku hizi unaukubal uzushi, sijui una malengo gani na mimi, lakini kumbuka mimi ni baba wa watoto, watoto wanajua jinsi gani ninavyowajali…’akasema

‘Mimi hayo yote ninayoyasema hapa sijakusingizia,kama itaonekana ni uwongo, mimi nipo tayari kuwajibika, na kwahiyo, ni bora ukakiri makosa, ili tusipoteze muda hapa,..ongea ukweli, tuone kikao kitasemaje, je upo tayari kukiri kosa,?’ nikamuuliza na yeye akatikisa kichwa kukataa, na baadae akasema.

‘Usinifanye mimi mjinga, nafahamu malengo yenu ni kunitega, nikiri kosa, ili muanze kuhukumu kwa ….mkataba huo…sasa mimi nasema hivi, wewe si unajifanya unayafahamu makosa yangu na una ushidi, utoe huo ushahii, na nasema hivi kama huna ushahidi na lengo lako ni kuniharibia, kibao kitakugeukia wewe, ...nitahakikisha naitumia hiyo hiyo katiba kukufunza adabu...’akasema kwa hasira.

'Subirini kwanza, naona mumekwenda haraka kidogo...'akasema mwenyekiti, huku akimgeukia mume wangu, akamtizama kwa makini halafu akageuka kumtizama wakili wake.

'Ndugu muheshimiwa wakili, mtu unayetaka kubeba dhamana yake ndivyo huyo na ndivyo hivyo alivyo,..pamoja na yote, pamoja na kupewa nafasi ya kukiri kosa, bado kabakia na msimamo wake, je ni wewe ulimshauri hivyo...?' akauliza mwenyekiti

'Mwenyekiti..mimi kama wakili wake, kwanza nilipenda kuyasikia hayo makosa, ili niweze kumtetea mteja wangu, je ndio imanipatia hiyo nafasi, ...?' akauliza wakili huyo.

'Hapana nafasi hiyo utaipata tu,..ila kwa vile uwanja ni wa mwenyeji wa kikao hiki nataka yeye mwenyewe ayathibitishe hayo madai yake, maana kama ni uwongo, basi hata mimi nitachukua jukumu hilo la kumuadhibu, maana hayo ni makosa makubwa, ...je msemaji una ushahid gani wa hayo makosa...?' akauliza mwenyekiti.

‘Ushahidi upo mwingi tu…’nikasema

************

‘Nimeongea kwa kifupi ili kutokupoteza muda, na sasa namuomba shahidi wangu wa kwanza kuthibitisha kauli hizo nilizozitoa, sio matusi, bali ndio ukweli halisi. Wapo wengi wakuthibitisha maneno yangu, ila kwa sasa namuomba....’nikageuka kuwaangalia washiriki,nikamwangalia rafiki yake docta…
Docta akainamisha kichwa, nikajua ni kwanini, nikamwangalia mke wake, mke wake alikuwa kama hayupo, alionekana ana mawazo mengi, na kabla sijatamka neno ...’ mama ambaye muda mwingi alikuwa kimiya akasema;

‘Mimi naomba aje Binti yangu wa kufikia, ..aje yeye kwanza maana anahitajika kwenda kujiandaa kesho anasafiri....’akasema mama na mwenyekiti akauliza

‘Unajuaje kuwa huyo ni shahidi wake, usiharibu utaratibu, au..’akasema mwenyekiti

‘Sawa ila…’nikasema nikiwa sijui lolote kuhusu huyo bint

‘Mimi nina uhakika ni shahidi wake..’akasema mama.

‘Haya, kama muhusika umemkubali kuwa ni mmoja wa shahidi zako, aitwe, au unasemaje mwenyeji wa kikao..?’ mwenyekiti akauliza na mume wangu akawa kabakia kimia, akiwa kashika kichwa.

'Sawa maana shida hapa ni kuthibitisha kauli zangu ambazo mume wangu kasema namkashfu, nimemtukana na sio kweli kuwa ana watoto nje ya ndoa, ...sasa huyo shahidi atathibitisha hayo niliyoyaongea, ili tusipoteze muda..'nikasema.

‘Hahaha…’akacheka mume wangu akionyesha dharau, kuwa labda nahangaika bure

'Na sio huyo tu, hapa ninao, na wengine hawajafika, ...sio kusudio langu kuyaweka haya hadharani, lakini nitafanya nini,..eeh,..basi aitwe huyo binti, akimaliza nitamsimamisha shahidi wangu mwingine,...'nikasema.

‘Sawa…’akasema hivyo mume wangu, lakini sasa akionyesha wasiwasi kidogo.

'Kama nilivyosema awali kikao hiki nimekirejesha kwa mwenyeji wetu, sitapenda mimi kuingilia, haya sasa akaitwe huyo binti,...'akasema mwenyekiti

Na aliposema hivyo, watu wote wakawa na hamu ya kumfahamu huyo binti ni nani, ambaye ataweza kutoa huo ushahidi wa jambo nzito kama hilo, nilimuona hata mume wangu akiwa na hamu ya kumuona huyo binti, hamjui ni bint gani huyo...

Watu wote mle ndani wakakageuza kichwa kuangalia mlangoni, waliposikia mlango ukigongwa, na mara ukafunguliwa, na mwenyekiti akasema;

‘Ingia na njoo huku mbele,...utoe ushahidi wako, tuambie ilikuwaje, na ni nani alikupachika mimba, usiogope, sema kila kitu….’

NB, Ni binti wa kufikia huyo anakuja kutoa ushahidi , je atasema nini



WAZO LA LEO:Kukosa ni kawaida ya binadamu, hakuna anayeweza kujithibitishia kuwa hatendi kosa, yapo ya bahati mbaya na yapo makosa ya kudhamiria, vyovyote iwavyo, unapokosea unastahiki kukiri na kutubu kosa lako, na kumuomba msamaha yule uliyemkosea, unapokosa ukabainika, au hata kama hujabainika, wewe ukalikana lile kosa, unakuwa umetenda kosa jingine. Tujifunze kuwa wa kweli, na tukikosea tujute, tutubu, tuwaombe msamaha tulio wakosea, na tudhamirie moyoni kuwa hatutarudia tena kutenda hayo makosa.
 
Back
Top Bottom