SEHEMU YA 404
Muda kidogo aliingia Sia, ambaye alisogea karibu yao, aliwaangalia kwa muda bila salamu na kusema,
“Bora Oliva umejiongeza kwa kuniletea mwanangu Paul halafu wewe ubaki na mwanao Sarah”
Madam Oliva alimuangalia akimshangaa kwakweli.
Sia akamwambia,
“Mbona unashangaa Oliva? Kwani hujui kama Sarah ni mtoto wako?”
“Sikuelewi”
“Ni hivi, watoto walibadilishwa wakati wadogo kwahiyo wewe ukapewa mtoto wangu, halafu mimi nikapewa mtoto wa Manka, halafu Manka akapewa mtoto wako amlee”
“Haiwezekani”
“Haiwezekani kivipi? Hujazaa na Steve wewe ila mimi ndio nimezaa na Steve, hivi huwa hujishtukii kwa kila mtu kusema kuwa mtoto wako kafanana na Steve? Huyo ni mtoto wangu, ukatae ukubali ila ukweli ndio huo, halafu wewe mtoto wako ni Sarah”
“Una wazimu wewe au? Umeyatoa wapi hayo maneno?”
“Kamuulize dokta Jimmy maana ndio aliyebadilisha hawa watoto”
Madam Oliva akapumua kwanza na kusema,
“Yani dokta Jimmy alishiriki kufanya hiko kwangu? Ananijua vizuri huyu dokta, huwa sipendi ujinga mimi. Haiwezekani”
“Ndio imewezekana sasa, ukweli ndio huo”
Paul hakuweza kuvumilia kwani alitoka nje ikabidi madam Oliva nae amfate mtoto wake Paul maana hata yeye hakuweza kuelewa kabisa yanayosemwa na Sia.
Basi pale, mama Angel alimuuliza Sia,
“Ila Sia una uhakika na hayo maneno yako?”
“Ndio nina uhakika”
Sarah akauliza pia,
“Inamaana mama sio mama yangu?”
“Ndio, sio mama yako. Mama yako mzazi ni yule madam aliyeondoka”
“Jamani!! Haiwezekani”
Sarah alimfata mama Angel na kumkumbatia kisha akamuuliza,
“Kwanini mimi sikulelewa na mama yangu mzazi? Kwanini hivi lakini, hivi inawezekana kweli?”
Mama Angel alimbembeleza kidogo Sarah maana aliona mtoto huyu akiumia sana bila tatizo, basi aliamua kwenda na Sarah chumbani kwake ili kujaribu kuongea nae kabisa, kitendo kile kilimfanya Sia ahisi kudharauliwa kwahiyo akaamua kuondoka zake.
Madam Oliva alifika nyumbani na kijana wake na kuanza kuongea nae, ambapo Paul alimweleza pia mama yake kuhusu alama aliyoambiwa na yule mwanamke, na kumuuliza mama yake,
“Mama, je ni kweli yule ndio mama yangu halisi?”
“Mwanangu, hata mimi sijui ukweli ila nitahakikisha mpaka naupata ukweli halisi, pole mwanangu”
“Ila mama, kwani inakuwaje hadi mtu anabadilisha mtoto? Je ni kweli mimi nimebadilishwa?”
“Mwanangu, sijui kitu”
“Naumia mama”
“Naelewa na mimi ndio ninayeumia zaidi usijali mtoto wangu, ukweli utajulikana tu. Nikipata ukweli sitoona shida kukwambia mtoto wangu. Siku zote nimekulea na kukupenda na bado naendelea kukupenda”
Madam Oliva aliingia chumbani kwake na kumpigia simu baba Angel kwa wakati huu,
“Unajua kipindi kile tulikuwa tukimfatilia dokta Jimmy ila sikujua kama kuna mambo kama haya”
“Mambo gani?”
“Sia kaniambia kuwa dokta Jimmy alinibadilishia mtoto, eti mwanangu ni Sarah halafu mwanae ni Paul. Jamani nasema haiwezekani kabisa”
“Duh!! Pole sana ila tukikutana itakuwa vizuri zaidi”
“Nakuja ofisini kwako muda sio mrefu”
Basi madam Oliva aliondoka muda ule ule na kumuaga tu mtoto wake kisha moja kwa moja alienda ofisini kwa baba Angel.
Alipofika alimkuta baba Angel akiendelea na kazi zake kama kawaida, basi alimsalimia na kuanza kuongea nae kuanzia pale alipokutana na Sia,
“Pole sana madam”
“Asante, ila kilichonifanya nije ni kukuuliza kuhusu dokta Jimmy umeweza kufahamu nyumbani kwake?”
“Ndio napafahamu”
“Nielekeze ili niende”
“Mmmmh peke yako? Yule dokta ni mwehu yule usije pata matatizo bure”
“Sijali kitu chochote, yule dokta ananielewa mimi ni nani katika maisha yake na ataniambia ukweli tu. Tulia, nielekeze halafu nitaenda”
Baba Angel alimuelekeza na kumshauri kuwa kama akitaka kwenda basi aende kesho yake maana muda tayari ulikuwa umeenda halafu anapoishi yule dokta ni mbali.
Baada ya maelekezo, madam Oliva alimuaga baba Angel na kuondoka zake.
Usiku wa leo, madam Oliva aliamua kumsimulia Steve kuhusu kile kilichotokea siku hiyo kwani kilikuwa bado kinamuumiza kichwa,
“Huyo Sia anasema kuwa Paul ni mtoto wake”
“Ooooh ndio maneno niliyotoka kuyapata kwa mama, nasikia Sia alienda tena kwa mama yangu na kusema kuwa Paul ni mtoto wake. Kwani mke wangu ilikuwaje?”
“Mimi sijui ila huyo dokta Jimmy najua atanieleza ukweli”
“Ila unahisi vipi? Hebu jaribu kunisimulia kwa ufupi kuhusu uzazi wako kwa Paul”
“Mimi nilijifungua kabla ya wakati. Kwa maana hiyo nilizaa mtoto njiti kwahiyo alikuwa hospitali kwaajili ya uangalizi maalum, ila sasa kilichotokea kuna kipindi mtoto wangu alipotea na hapo ikawa tatizo, ndipo ugomvi wangu na dokta Jimmy ulipoanza hadi nikamfungulia mashtaka, ndipo alipokuja kuniletea Paul na kusema ndio mtoto wangu kapatikana, eti kuna mama aliondoka na mwanangu ila wamejitahidi na kumrudisha kwangu. Kwahiyo hapo ndio nashindwa kuelewa, sijui ni kweli nilibadilishiwa au la”
“Kwahiyo inawezekana yule Sarah ndio akawa mtoto wako halisi?”
“Hapana, na hilo nakataa pia kwani nakumbuka mtoto wangu alikuwa njiti ila alikuwa ni wa kiume, iweje leo niambiwe wa kike ndio mwanangu? Hilo halipo na hata haiwezekani kabisa, yani labda kama ni kweli basi mtoto wangu yupo sehemu nyingine ila Sarah ni mtoto wa yule yule Manka ingawa haendani nae.”
“Dah!! Haya mambo hayaeleweki kwakweli, na huyo Sia anavyojua kushupalia jambo sipati picha, yani alivyoenda kushupalia kwa mama yangu hatari. Kwahiyo kwa huyo dokta unataka kwenda kesho”
“Ndio, kesho nitaenda”
“Basi tutaenda wote mke wangu”
Madam Oliva alikubali jambo hilo kwani alichokuwa akitaka ni kuongea na dokta Jimmy tu ili aweze kujua ukweli.
Leo mapema kabisa, madam Oliva aliondoka na Steve kuelekea nyumbani kwa dokta Jimmy, na walifika huko na kumkuta dokta Jimmy akimwagilia bustani, ni kitu ambacho dokta Jimmy hakukitarajia kwahiyo alishtuka tu kumuona madam Oliva,
“Kheee Oliva?”
“Ndio ni mimi, sitaki maelezo yoyote yale Jimmy, kwa muda huu nataka ukweli kuhusu mtoto wangu”
“Ukweli upi?”
“Usijifanye hujui dokta, mwanangu mimi yuko wapi? Umenipa mtoto wa mwingine halafu ukanidanganya kuwa ni mwanangu, yuko wapi mtoto wangu?”
“Nimekuelewa Oliva, basi twende tukakae pale ili tuweze kuzungumza hayo”
Dokta Jimmy alikuwa akiongoza sehemu ya kukaa, yani dokta Jimmy alikuwa ni mpole sana kiasi kwamba hata Steve alimshangaa huyu dokta maana huwa anasikia sifa zake kuwa ni mkorofi, ila alishangaa kumuona amekuwa mpole vile kwa madam Oliva.
Walifika kwenye mahali kulikowekwa viti pale nje ya nyumba ya dokta na kukaa kisha dokta alianza kusema,
“Hata salamu oliva?”
“Hivi naanzaje kukusalimia eeeh!! Nakusalimiaje kiumbe mwenye roho mbaya kama wewe”
“Unajua Oliva siwezi kukutendea ubaya!”
“Usingeweza basi usingefanya ubaya juu yangu, ungenipatia mtoto wangu halisi nimlee mwenyewe, sio leo natukanwa na kudhalilishwa, nakuja kuambiwa kuwa mwanangu halisi ni Sarah sijui mtoto wa Manka, kwanini lakini umefanya hivi dokta Jimmy?”
“Nisikilize Oliva, nani kakwambia kuwa mwanao ni Sarah? Unakumbuka kuwa mtoto wako alikuwa ni mtoto wa kiume au umesahau?”
“Nakumbuka ndio, kama mliweza kumpa Manka mtoto wa kike akalea ikiwa alijifungua mtoto wa kiume ndio mnashindwa kufanya na kwangu? Nimekushangaa sana, nasikia unajuana vizuri sana na huyo Manka, laity ungejua Manka yupo vipi kwangu basi usingenifanyia hivi dokta Jimmy”
“Kwanza naomba unisamehe Oliva, ila leo nitakwambia ukweli ingawa sikupanga kuusema leo”
“Ndio niambie, na mwanangu halisi yuko wapi?”
“Mwanao halisi yupo, yupo sehemu nzuri tu hata usijali”
“Niambie bhana, naona kama unanibabaisha tu”
“Sikia nianze kukwambia Oliva kitu kilichokuwepo, naomba unisikilize kwa makini”
“Nakusikiliza, niambie”
“Siku uliyojifungua wewe ni siku ambayo alijifungua mwanamke Fulani hivi ambaye nae alijifungua mtoto njiti kama wewe, ila yeye alikimbia hospitali, watoto wale wawili tulikuwa tukiwalea kwa hali zote ambazo zilikuwepo pale hospitali. Na tuligundua kuwa mmoja kati ya wale watoto ana upeo mpana sana, nilijua ni mwanao nikampenda sana. Ila kuna kitu kilitokea hapo kati mtoto mmoja kati ya wale wawili akaibiwa na hakuwepo kabisa pale hospitali, tukapata mawazo sana, basi nikaamua mwanao kumuweka alama ili asiibiwe. Ila kuna siku ndio mambo yaliharibika kabisa na mwanao pia akaibiwa, ndipo ulipoanza purukushani ya kutaka mtoto wako, hakukuwa na namna zaidi ya kukupa yule mtoto wa yule mwanamke chizi sababu yule mtoto alishamlea na tukaamini kuwa yupo katika mazingira mazuri wakati tunaendelea kumtafuta mtoto wako. Basi ukachukua yule mtoto ila siku zingine sasa ndio tukampata mtoto wako halisi, nami nikaamua kumtunza ila nilijua tunkuwa siku moja utaujua ukweli kuhusu mtoto wako. Hakuna baya ulilowahi kunitendea, kwahiyo hakuna kibaya nilichomtenda mtoto wako, tumemlea kwa upendo wote, na watu wote wanaonizunguka wanajua kuwa ni mtoto wangu mimi.”
“Yuko wapi huyo mtoto?”
“Ngoja nikamuite ila usije kumwambia kuwa wewe ni mama yake kwa gafla hivyo, najua mimi nitakavyomuandaa kisaikolojia na atakukubali tu. Namleta ili akusalimie na umuone, sitaki umtie mawazo kwasasa, najua jinsi ya kumwambia. Nimeamua kukwambia ukweli Oliva maana sina sababu ya kukuficha, sina ugomvi wowote na wewe Oliva”
Kisha dokta Jimmy aliinuka na kwenda kumuita huyo mtoto.
Steve alimuangalia madam Oliva ambaye alikuwa ameonekana kujawa na hasira sana, kisha alimwambia,
“Unajisikiaje kumpokea mtoto wako halisi?”
“Sijui yani, akili yangu hata haipo hapa kabisa, nahisi kama kupagawa vile”
Baada ya muda kidogo, dokta Jimmy alifika na kijana ambapo alimwambia madam Oliva,
“Kijana wangu huyu anaitwa Jimmy”
Madam Oliva alimuangalia sana yule mtoto ambaye alikuwa ni mfanano halisi wa Derrick, yani hakuna ambaye angemuona huyu mtoto halafu angebisha kuwa si mtoto wa Derrick, yani madam Oliva alijisikia uchungu sana katika moyo wake, aliinuka na kumzaba kibao dokta Jimmy kisha akamwambia,
“Mjinga sana wewe, halafu umempa na mjina wako usiokuwa na maana yoyote. Sikupendi wewe dokta”
Pale dokta Jimmy alimwambia kijana wake Jimmy kuwa aondoke na kuwapisha ila madam Oliva alikazana kusema kuwa anataka kuondoka na mwanae,
“Oliva, sikia nikwambia nimesema kuwa kila kitu tutakifanya kwa mpangilio, sio swala jepesi kumueleza kijana mkubwa kama Jimmy kwa haraka haraka hivyo kuwa huyu ndio mama yako. Mimi nitaongea na huyu kijana na nitakuja kukukabidhi kwani tatizo liko wapi?”
“Nipe niondoke nae”
“Nitakuletea Oliva, na pia nakuahidi kuwa kwa hili basi bnipo tayari kumwambia kila niliyemkosea ukweli halisi. Hata mimi roho imeniuma sana kwa hiki nilichokifanya, sijapenda kwakweli, naomba unisamehe sana”
“Mjinga sana wewe, unaomba msamaha wakati umefanya makusudi”
“Sio makusudi Oliva, kumbuka mtoto alipotea halafu wewe ulikuwa ukimuhitaji mtoto wako, sikuwa na la kufanya zaidi ya kukupa mtoto ambaye angekuridhisha wewe na moyo wako. Halafu alipopatikana, sikuweza uja kukwambia maana ningekuchanganya ndiomana niliamua kumlea mwenyewe, nisamehe sana kwa hili Oliva”
Kwakweli madam Oliva alichukia sana na kumuuliza tena dokta Jimmy,
“Kwahiyo lini utakuja kunikabidhi mtoto wangu?”
“Nitakuja kumleta hata mwisho wa mwezi huu lakini nahitaji kwanza kumuandaa kisaikolojia”
Kisha madam Oliva aliinuka na kufatwa nyuma na Steve kisha kuondoka.
Wakiwa kwenye gari wakati wa kurudi, Steve alianza kuongea na madam Oliva,
“Kwa habari nilizowahi kusikia kuhusu huyu dokta ni kuwa ana roho mbaya sana, ila mbona leo amekuwa tofauti? Halafu mbona anaonekana kukuogopa sana wewe?”
“Unajua sijaweza kuamini kama huyu mjinga angeweza kunifanyia mimi kitu cha namna hii jamani, unajua huyu dokta kapata huo udokta wake kwa msaada wa baba yangu”
“Kivipi?”
“Baba yangu alikuwa anatambulika sana serikalini, kwahiyo aliweza kumuombea msaada wa kwenda kusoma nchi za nje, yule dokta Jimmy kwao walikuwa hawana lolote lile, yani baba yangu ndio kamfanya aweze kusoma huo udokta na kumaliza, hata hospitali ile alipata msaada mkubwa kwa baba yangu enzi za uhai wake, halafu leo hii ameenda kunifganyia unyama kama huu kweli? Nahisi baba yangu huko alipo anatokwa na machozi ya damu loh huyu dokta Jimmy kanichefua hatari”
Hadi madam Oliva alifungua kioo na kutema mate, yani alikuwa na hasira kupita maelezo yoyote yale. Kwahiyo waliendelea na safari tu ya kurudi nyumbani kwao kwa muda huo.
Usiku wa leo, baba Angel alikuwa akimuelezea mke wake kuhusu Angel maana yeye ndio anaepata taarifa kuhusu Angel sababu yupo kwa mama yake,
“Yani mama kanipigia simu anasema Angel analala lala hatari, hivi mke wangu kumbe kweli Angel ana mimba eeeh!”
“Sasa ulidhani nakutania au kitu gani baba Angel, mimi nikutanie au nikudanganye ili nifaidike na nini? Siwezi kufanya hivyo mume wangu, Angel nimeenda nae hospitali mwenyewe na tumepima na kumkuta na ujauzito, na kaniambia kwa mdomo wake mwenyewe kuwa ni mimba ya Samir”
“Ila mama Angel, inabidi tujitafakari, hivi tumekosea wapi katika kumlea huyu mtoto? Mbona nahisi malezi yote tumempatia, upendo wote tulimpatia ni kwanini imekuwa hivi?”
“Hata mimi sielewi mume wangu, ila tusilaumiane, kama malezi yote tumempa Angel basi ni akili yake mbovu tu. Sijui karithi kwa baba yake loh!!”
“Yani nimejiuliza mke wangu nilipopigiwa simu na mama balaa, sijui kitu gani kimetokea kwa mtoto wetu Angel, sielewi mpaka muda huu kuwa Angel kapatwa na nini”
Mara simu ya baba Angel ilianza kuita muda huo, basi alipokea na kuisikiliza,
“Dokta Jimmy anaongea hapa”
“Unashida gani wewe mjinga?”
“Nahitaji kuongea na wewe Erick, nahitaji kukwambia ukweli”
“Ukweli upi? Sitaki kuongea na wewe, achana na mimi kabisa”
“Nataka kukwambia kilichowekwa kwa watoto wako na jinsi ya kuwaokoa maana bado kuwaokoa kwasasa, ukumbuke wameanza kwahiyo kitakachoendelea ni kuwa wataendelea na mchezo ule ule waliouona, ukizingatia washapata radha yake”
“Mjinga sana wewe dokta, usiniambie kitu, sikuelewi chochote. Ila jua kuwa dawa yako inachemka, unanifanyia ujinga, halafu bado bila aibu unataka kunitegeshea kesi, hivi bila mwanangu Erick kwasasa si ningekuwa ndani kwa uongo wenu nyie!”
“Eeeeh tena umenikumbusha jambo, nahitaji kuongea nawe kuhusu huyo Erick, kuna sehemu tumpeleke yani huyo mtoto atakuwa hatari hapo badae na ataingiza hela za kutosha”
“Nimekwambia sitaki hata ushauri wako hata kidogo, dokta Jimmy hebu fanya mambo yako”
Baba Angel alikata ile simu, kiukweli hakutaka kuongea na dokta Jimmy kabisa hata kuonana nae hakutaka hilo jambo, kila alipomfikiria aliona kupatwa na hasira zaidi.
Hata aliacha maongezi na mke wake muda huo na kumtaka waweze kulala tu kwani alizidi kupatwa na hasira zaidi katika akili yake .
Siku ya leo, Angel anaambiw ana bibi yake kuwa ajiandae waweze kwenda kutembea nae kidogo kwani bibi anakumbuka jinsi alivyokuwa akiishi na Angel hapo kabla.
Angel anakubali tu na kwenda na bibi yake kutembea, walipofika kule kiliagizwa chakula pale ili waweze kula ila Angel aligoma na kudanganya kwa bibi yake kuwa ameshiba sana,
“Jamani Angel, umekula muda gani nyumbani wakati tumeondoka wote bila ya wewe kula chakula chochote?”
Muda kidogo alifika mr.Peter ambaye ni rafiki wa bibi huyu na kukaa karibu yao, ila bibi alivyoinuka tu kwenda msalani, yule mr.Peter alimwambia Angel,
“Wewe Angel, ni mjamzito wewe!”
“Hapana, mimi sina mimba”
“Unajua mimi ni mtu mzima, halafu niliwahi kusomea udaktari ila niliishia kati. Wewe Angel usinibishie, mimi huwa nikiangalia tu mtu mwenye mimba hata ya mwezi mmoja namtambua, wewe Angel ni mjamzito, haya mtoto mdogo hivyo umeanza kuzini hadi mimba!! Au ni kitu gani hiko?”
“Hapana, sina mimba”
“Ulidanganywa nini na mwanaume? Alikudanganya na hela? Mbona wazazi wako wapo vizuri kwenye swala zima la hela Angel? Alikudanya na simu? Mbona nilikununulia simu ya gharama sana? Alikudanganya na upendo? Mbona wazazi wako wanakupenda sana? Alikudanganya kitu gani huyo mwanaume Angel? Ameahidi kukuoa? Wapi imeandikwa uolewe baada ya kuzaa? Uzao mzuri ni ule wa ndani ya ndo, hata mimi nimeshikwa na uchungu juu yako, yani jinsi bibi yako anavyokupenda na anavyoongea kuhusu maisha unayoyapata wewe, jinsi nilivyoongea na mama yako siku ile, dah Angel imekuwaje umebeba mimba mapema hivi? Hujui mimba inapatikanaje? Ulibakwa au ni kitu gani? Unajua wewe ni binti mzuri sana, ungejituliza ungempata mume bora katika maisha yako”
Bibi Angel alirudi na hapo Angel hakuweza kuendelea kukaa na kudai kuwa anajihisi vibaya, hata kuongea hakuongea chochote hadi wanarudi nyumbani, yani Angel alijifungia chumbani na kujiwa na yale maneno ambayo mama yake aliongea juu yake alijihisi maumivu sana yani aliwaza vitu vingi mno na aliumia sana katika moyo wake na kujiona kuwa alichokifanya hakikuwa sawa kabisa, aliwaza na kujisemea,
“Kwa hakika nimewakosea sana wazazi wangu, ni kweli wamenilea vizuri, mama amejitahidi sana kunilea na kumuondoa Samir mbele yangu, baba nae kafanya jitihada zote hata kunipeleka shule ya mbali, sijui ni kitu gani kimeniingia mimi Angel. Siku zote nimejilinda ila siku moja tu imefanya iondoe thamani yangu nzima, ni aibu kwangu na kwa familia yangu”
Alijikuta akilia kwa muda huku akijutia sana, kitu kingine kilichomuumiza ni vile baba yake ambavyo anampenda sana, basi kwa muda huo aliamua kumuandikia Samir ujumbe wake kuhusu ile mimba,
“Samir, tufanyeje na hii mimba niliyonayo?”
“Sijui Angel yani hata mimi sielewi”
“Je utanioa Samir?”
“Nitakuoa vipi Angel wakati baba kasema wewe ni dada yangu”
“Samir, yamekuwa hayo? Si ulisema hujali chochote wewe jamani, leo unaniambia kitu cha namna hiyo Samir kweli? Kwakweli mimi najiona nimekosa furaha na thamani ya maisha kabisa”
“Usiseme hivyo Angel”
“Unategemea niseme nini ikiwa ninayekupenda unasema huwezi kunioa, na bila kusahau kuwa wewe ndio uliyenishawishi mimi hadi tukafanya na sasa mimi ni mjamzito”
“Angel, vitu vingine huwa nasema tu. Ila kiukweli mimi nahitaji kukuoa kabisa, huwezi amini sikai kwa baba, nipo kwa mjomba ila baba alikuja kunifanyia fujo na sasa nipo kwa mjomba mwingine. Angel nakupenda sana hata sijui kwanini umekuwa ndugu yangu”
“Kwahiyo hitimisho lako kwangu ni nini?”
“Sijui, ila nitakachoamua mimi Angel sijui kama kitakuwa kizuri”
“Kitu gani?”
“Tulia tu”
Hapo Angel alimtumia ujumbe mwingine Samir bila kujibiwa na kumfanya ajihisi vibaya zaidi, alijua tu kinachofuata ni Samir kumuacha yeye moja kwa moja, basi Angel alilia sana na kuamua kumuandikia ujumbe baba yake kwani aliona baba yake ndio atampa faraja kidogo, alilia sana na kuamua kulala.
Baba Angel alipoamka asubuhi kabisa, kitu cha kwanza ilikuwa ni kuchukua simu yake ambapo alikutana na ujumbe wa Angel,
“Baba nisamehe sana, nimekosa mimi, sina raha mimi, sijui nifanyeje, huyo Samir hanitaki tena na sijui cha kufanya. Nisaidie baba yangu, nisamehe sana”
Baba Angel alimsomea mke wake ambaye alisema pia,
“Huyu mtoto mwehu, mbona mimi hajaniandikia huo ujinga wake! Kiukweli huyu Angel katudhalilisha sana, na anapenda kukwambia wewe ujinga wake sababu anajua kuwa wewe unamtetea na ujinga anaoufanya”
“Usiseme hivyo mama Angel”
Basi baba Angel alienda kujiandaa, sababu alitaka kutoka ila alichokuwa akitaka kufanya kwa siku hiyo ni kupita kwa mama yake ili kuongea na Angel sababu alijua kuwa Angel anahitaji kuongea nae kwa kipindi hiko.
Baba Angel wakati anatoka tu nje alikutana na Rahim ambaye alikuwa amefura kwa hasira, kisha Rahim akasema,
“Kwakweli katika siku zote leo nimechukia zaidi na ninaenda kutenda dhambi kwa mtoto wangu mwenyewe”
Kisha Rahim akaondoka, kwakweli baba Angel hakumuelewa kabisa na kuamua kumfata ambapo walienda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Rahim kisha Rahim alimuita Samir ambaye kwa muda huo alikuwa nyumbani kwake, muda kidogo Samir alitoka ndani kwao ila alikuwa akijiamini sana kupita siku zote ambazo alikuwa na uoga, kisha Rahim alimuuliza,
“Jana umenitumia ujumbe gani wewe mjinga?”
“Nimekwambia naenda kumuoa Angel”
“Mjinga wewe”
Rahim alimkaba Samir, kisha alitoa kisu kwenye mkanda wake wa suruali na kutaka kumchoma nacho Samir.