BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Mkulo apasua jipu
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dodoma; Tarehe: 14th June 2009 @ 09:06
Habari Leo
Habari Leo
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, amesema suala la kuondoa misamaha ya kodi kwa vifaa vinavyoagizwa na taasisi za kidini halikufanywa kwa lengo la kuua makanisa yanayojihusisha kwa kiasi kikubwa na utoaji wa huduma za kiafya na elimu, bali kuiokoa serikali kiuchumi.
Waziri huyo pia amekanusha madai kuwa serikali imefanya hivyo kwa kuwa yeye pamoja na Rais wote ni waumini wa dini ya Kiislamu na akafafanua kuwa wanataka kukomesha tabia ya baadhi ya watu kujinufaisha na misamaha hiyo hadi kuwa mamilionea.
Sio mimi wala Rais ambaye ameandaa bajeti hii au kupendekeza kufutwa misamaha hii, kuna jopo la wataalamu na kule naweza kusema kuna Waislamu wawili tu, lakini wengi wao ni Wakristo, hivyo nasema sina nia ya kuua makanisa, alisema Mkulo wakati akizungumza na waandishi wa habari jana, mjini hapa.
Mkulo alisema jopo hilo la wachumi waliobobea waligundua kuwa kuna watu ambao wananufaika na misamaha inayotolewa kwa taasisi hizo za kidini, hali inayoikosesha serikali mapato mengi. Alisema hatua hiyo ya kuondoa msamaha huo wa kodi haikulenga kuzipunguzia taasisi za kidini na zisizo za kidini uwezo wake wa kuendelea kutoa huduma za maendeleo ya kijamii kwenye nyanja za elimu, afya na huduma za maji.
Pia alisema hatua hiyo haikulenga kuwaondolea unafuu wa kodi kwenye bidhaa zinazotumika kwenye majukumu yao ya huduma ya kiroho na ibada, ila alisema hatua hiyo inakusudia kuondoa mianya kwa wafanyabiashara wanaovitumia vyombo vya dini kujitajirisha.
Alifafanua kuwa kuna watu ambao wanaingiza nchini vifaa vya kibiashara bila kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kupitia misamaha inayotolewa kwa vyombo hivyo, hali ambayo imekuwa inaikosesha serikali mabilioni ya fedha. Kuna watu wamekuwa mamilionea kwa kutolipa kodi kupitia mgongo wa dini kwa kweli hawa wanaopata hii misamaha wanaitumia vibaya, kwani wanasingizia dini wakati wanaenda kufanya biashara, alisema Mkulo.
Waziri huyo alitoa mfano wa moja ya madhehebu lililoagiza mabati 4,000 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa likatumia mabati 200 tu na mengine mmoja wa viongozi wa kanisa hilo akaenda kuyauza kwa bei ya soko. Pia alitoa mfano wa madhehebu ya dini ambayo yaliagiza tani 5,000 za sukari kutoka Malawi kwa ajili ya kituo cha watoto yatima, lakini tani tano tu zilienda Singida kwenye kituo hicho na tani zingine zilizobaki zilikwenda Makambako na kufungwa kwenye mifuko na kuwauzia wananchi.
Katika kuelezea namna baadhi ya watu wanavyonufaika na misaada hiyo, alitoa mfano wa kiongozi mmoja wa kidini aliyeagiza magari kwa ajili ya kanisa lakini akayatumia magari hayo kwa kuanzisha kampuni ya kitalii (tour operator) kwa ajili ya kukodisha kibiashara. Alitoa mfano wa taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) kuwa kuna zinazotumiwa na wafanyabiashara kuagiza vifaa mbalimbali sio kwa ajili ya matumizi ya kijamii bali kibiashara.
Hawa wanatumiwa na wafanyabiashara licha ya kuwa zipo chache zinafanya kazi vizuri. Hata hivyo, Mkulo alisema jopo hilo la kitaalamu ambalo limefanya uamuzi huo limeona kuwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani uendelee kutolewa kwa kwa vifaa vya elimu, huduma za afya na vifaa vya hospitali ambavyo vitaagizwa na taasisi za kidini.
Ila alisisitiza kuwa vifaa vitakavyoingizwa na taasisi za kidini kwa lengo la biashara ni lazima zilipewe ushuru na akatoa mfano taasisi ya St Gasper inayoendesha hoteli na zingine zinazofanya biashara hiyo iwapo zitaagiza vifaa vya hoteli ni lazima zilipie kodi. Alisema serikali haiwezi kukubali kuendelea kupoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa kutoa msamaha kwa vifaa ambavyo sio vya kiroho au ibada ila wanataka kuhakikisha vifaa vya biashara vinatozwa kodi vyote.
Waki huo huo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeiomba serikali kuondoa mara moja ushuru wa bidhaa na huduma za mashirika ya dini ili shirika hilo liweze kutimiza wajibu wake kikamilifu kwa jamii. Taarifa ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Issa Shaaban Simba, imesema kuwa kuwepo kwa ushuru huo kutapunguza wachamungu nchini, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi na maendeleo kwa ujumla.
Mashirika ya dini hutegemea misaada na michango ya waumini na wahisani mbalimbali na kamwe hayafanyi biashara au kupata faida yoyote katika shughuli zake, misaada kama hiyo inasaidia masikini, walemavu, wagonjwa na maeneo yenye machafuko na vita, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Amesema kwa kuwa serikali imeshindwa kutekeleza huduma zake katika maeneo mbalimbali, mashirika ya dini yanalenga kutoa huduma kwa wananchi katika mazingira magumu na hasa vijijini na maeneo mengine duni ya mijini. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, athari ya ushuru huu ni pamoja na wahisani kupunguza ama kuondoa misaada, huduma kwa wanyonge, kufifia na mashirika ya dini kushindwa kutoa huduma zake za msingi za ibada kujenga misikiti na kuchapisha vitabu.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Methodius Kilaini amesema serikali ilipaswa kuzungumza na taasisi za dini kabla ya kutangaza katika bajeti kuyafutia msamaha wa kodi mashirika ya dini na asasi za kirai. Akizungumza na HabariLeo Jumapili mapema jana, Kilaini alikiri kuwepo kwa taasisi nyingi za dini na kwamba zipo ambazo zinaweza kutumia msamaha huo vibaya hata hivyo alitahadharisha kuwa ni serikali ndio inayoziandikisha na inayopaswa kuzidhibiti pia.