Huu ni mkutano wa kwanza kati ya China na Afrika tangu mkutano wa FOCAC wa mwaka 2018, na unatarajiwa kuanzisha ngazi mpya katika maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika na kuandika ukurasa mpya katika ujenzi wa jamii ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.
Wataalamu wanasema, lengo la Baraza hili la ushirikiano ni kuendeleza zaidi mikakati ya maendeleo na nchi za Afrika na pia kukabiliana na mahitaji ya pamoja ya zaidi ya nchi 50 za Afrika, na kwamba umuhimu zaidi uko katika kujenga maafikiano kati ya nchi za Dunia ya Kusini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Li Jian ameeleza kuwa, mkutano wa maofisa wa ngazi ya juu wa Baraza hilo utafanyika Septemba 2, huku mkutano wa ngazi ya mawaziri wa Baraza hilo utafanyika Septemba 3 kwa lengo la kuandaa mkutano wa kilele. Kuanzia Septemba 4 hadi 6, mfululizo wa matukio ikiwemo hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, dhifa ya kukaribisha viongozi pamoja na maonyesho, mikutano ya ngazi ya juu pamoja na mkutano wa wajasiriamali wa China na Afrika itafanyika. Msemaji huyo amesema, kuheshimiana, usawa, na majadiliano ya pamoja ni sehemu muhimu ya FOCAC, na kwamba pande hizo mbili za China na Afrika zinadumisha mawasiliano na uratibu wa karibu ili kuandaa shughuli husika za mkutano huo, na hivyo kuendeleza moyo wa ushirikiano na urafiki kati ya China na Afrika.
Mtafiti katika Taasisi ya Elimu ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Kawaida cha Zhejing Shen Shiwei anasema, mkutano huo unafanyika wakati kuna ushindani mkali wa nchi kubwa zenye nguvu, na kwa sababu hiyo, baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, zitaufuatilia mkutano huo kwa makini. Pia anasema, kwa nchi za Afrika, mkutano huo unasubiriwa kwa hamu, kwa maana zinasubiri mambo mapya yatakayozungumzwa kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo na China.
Mwezi Machi mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alisema, kupitia mkutano wa FOCAC, China na Afrika zitaendeleza urafiki wao wa jadi, kuimarisha mshikamano na ushirikiano, na kufungua nafasi mpya kwa ajili ya kuonheza kasi ya maendeleo ya pamoja ya China na Afrika. Wang Yi alisema, wakati nchi za Afrika zinagundua kuwa zinahitaji kutafiti njia za maendeleo ambazo zinaendana na mazingira ya kitaifa na kushikilia hatma zao wenyewe, China itaendelea kusimama kithabiti na Afrika na kuunga mkono Afrika ambayo ni huru kihalisi katika kufikiri na mawazo.
Profesa Song Wei wa Shule ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia katika Chuo Kikuu cha Kigeni cha Beijing anasema, kutokana na changamoto ambazo nchi za Afrika zinakabiliana nazo baada ya janga la COVID-19, huenda ushirikiano kati ya China na Afrika utakuwa wa karibu zaidi, na hii inajumuisha ufadhili wa kifedha. Pia amesema kuna uwezekano wa kuwa na ushirikiano katika mageuzi ya kiviwanda ya barani Afrika na juhudi za kulifanya bara hilo kuwa la kisasa zaidi. Profesa Song anasema, mkutano huo unatarajiwa kutafiti ni kwa njia gani China na Afrika zinaweza kushiriki zaidi katika masuala ya kimataifa, na kuboresha ajenda ya maendeleo ya nchi za Afrika pamoja na Dunia ya Kusini.