12. Jitihada pia zimefanyika na zinaendelea kufanyika za kukabiliana na umasikini wa kipato, yaani kuwafikishia wananchi manufaa ya kukua kwa uchumi kwa wao kufaidika mmoja mmoja. Hili ndilo hasa eneo ambalo sera ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi inahusika nalo. Agenda kuu katika eneo hili ni:-
(a) uwezeshaji
(b) Kupambana na umasikini
(c) Kushiriki katika uchumi wa nchi, na
(d) Ajira.
13. Eneo hili la kuyafikisha kwa wananchi manufaa ya kukua kwa uchumi wa nchi ndilo agenda kuu na changamoto ya msingi ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Na mbinu kuu za kuikabili changamoto hii ni pamoja na zifuatazo ambazo zote ni sehemu ya MKUKUTA:-
(a) Kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi kwa kasi kubwa zaidi (kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2010).
(b) Kuongezeka kunakoendelea, kwa wingi na ubora wa huduma za jamii hasa elimu, afya, maji n.k. na miundombinu hasa barabara, madaraja, mawasiliano, umeme n.k.
(c) Modenaizesheni ya harakati mbalimbali za kiuchumi zinazowapatia ajira za kujiajiri na kipato wananchi, hjasa kilimo, ufugaji, viwanda vidogo, uvuvi, uchimbaji madini, n.k.
(d) Kuzipa uhai rasilimali mfu za wananchi ili ziweze kutumika kama dhamana za kujipatia mikopo, kwa kutumia mkakati wa kurasimisha rasilimali na biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA). Mkakati huu utachangamsha ajira za wananchi za kujiajiri wenyewe.
(e) Kuwawezesha wananchi kutumia fursa mbalimbali za maendeleo zilizopo kujiongezea kipato na kushiriki katika uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kumiliki hisa katika makampuni mbalimbali, kama ilivyokwishaanza kwa mfuko wa umoja.
(f) Mkakati wa uanzishaji wa maeneo maalumu ya uchumi ( Special Economic Zones Strategy) kama unaotumiwa na nchi Asia ambao utazalisha ajira nyingi za kuajiriwa katika sekta rasmi, na za kujiajiri. Kwa jina jingine, mkakati huo unaitwa The Tanzania Mini-Tiger Plan.
(g) Kuimarisha taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi.
14. Kwa vile lengo la juhudi zote hizi zinazobainishwa na ilani ni kuyafanya maisha ya watanzania wawe bora zaidi, CCM imebuni kaulimbiu mbili zifuatazo.:-
(a) "Maisha bora kwa kila Mtanzania",
(b) "Kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya, Tanzania yenye neema tele inawezekana."