CCM imevunja Katiba ya nchi
Bakari M. Mohamed
KATIBA ni mkusanyiko wa kanuni na sera ya serikali juu ya utawala wa nchi (Kamusi ya Maana na Matumizi, 2005 ukurasa wa 144); na vilevile katiba ni jumla ya kanuni ambazo kwazo huwezesha serikali itawale au chama au kampuni iendeshe shughuli zake (Kamusi ya Kiswahili Sanifu, TUKI, toleo la pili, ukurasa wa 149).
Kwa ujumla, katiba ya nchi ni mwongozo wa kuendesha mambo yote ya menejimenti na utawala wa nchi kama ilivyokubaliwa na wananchi.
Ukiachilia mbali ukuukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (JMT) ya 1977 (iliyofanyiwa urekebu mwaka 2005) bado mamlaka ya nchi katika Tanzania inapaswa kuifuata katiba hiyo. Kwa jinsi yoyote iwayo; hakuna mtu, kikundi cha watu na au chama cha siasa kinachopewa dhamana ya kuongoza serikali kwa mujibu wa katiba na kikaamua kufanya kinyume na utashi wa Katiba ya JMT ya 1977 (2005).
Pamoja na ukweli huu, Chama Cha Mapinguzi (CCM) kimekuwa kwa nyakati na mazingira tofauti kikivunja katiba ya nchi ilhali wenye dhamana ya kuilinda katiba hiyo, yaani wananchi, wakizidiwa ujanja na au nguvu na mfumo kwa kutokujua haki za msingi za kikatiba!
Huu ndio mwendo uliyojengwa tangu uhuru hata sasa kwamba sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania hawaijui katiba yao na hawana uelewa wa haki na wajibu wao kama raia.
Inawezekana, hali ya kutowashirikisha wananchi katika kupata uelewa wa wajibu na haki zao za kikatiba, kulifanywa kwa makusudi na au kwa bahati mbaya! Tuchukue dhana ya kwanza kwamba kulifanywa kwa makusudi maalumu. Dhamira ya lengo la kuwafanya wananchi mbumbumbu wa mwongozo (sheria mama) ni matokeo ya kujenga mazingira ya kutumia fursa hiyo katika kutawala fikra nyepesi za raia wasiye na uelewa wa haki, uhuru, usawa na wajibu wao kama wananchi wenye dhamana ya kuendesha serikali yao.
Kwa kulijua hili, CCM ilitumia mwanya huo katika kuficha mambo mengi yaliyotakiwa yawe wazi kwa raia juu ya uhuru wao, haki zao, na wajibu wao katika kuendesha mustakabali wa nchi yao. CCM, kama chama-dola, na kilichotawala satwa zote za uongozi wa nchi kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 10 ya Katiba ya JMT ya 1977 kwa Sheria Namba 15, 1984 Ibara ya 6 iliyofutwa na Sheria Namba 4, 1992. Kwa ujumla, CCM ilishika hatamu (wengine wanauita ukiritimba) kwa muda mrefu na hata baada ya mfumo wa demokrasi ya vyama vingi vya siasa bado wenye dhamana ya chama hicho wamebaki na kasumba ileile.
Munasaba wa kuandika makala hii umekuja baada ya kuichunguza, kuipembua na kuisasambua Katiba ya JMT ya 1977 (2005) juu ya nukta muhimu zihusuzo mamlaka ya nchi na hususan juu ya uendeshaji wa shughuli za serikali inayotokana na chama kinachounda serikali.
Kwa mujibu wa Ibara ya 8(1), Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (JMT) ni nchi inayotakiwa kufuata misingi ya demokrasi na haki ya kijamii ambapo: wananchi ndio msingi wa mamlaka yote; lengo kuu la serikali linatakiwa liwe ustawi wa wananchi; serikali inatakiwa iwajibike kwa wananchi; na kwa jinsi yake wananchi wanatakiwa washiriki kwenye shughuli za serikali yao!
Bila kujali ukweli huu wa kikatiba, CCM kwa nyakati tofauti imekuwa ikipora mamlaka ya wananchi kwa kisingizio kwamba ni chama cha wananchi!
Na kwa jinsi hii makala haya yatajaribu kufanya udondozi wa nukta muhimu na nyeti juu ya malengo mahususi kumi na moja juu ya lengo kuu moja linaloainishwa kwenye Ibara ya 9 ya Katiba ya JMT ya 1977 (2005). Na kwa jinsi hiyo, tuweke mkazo kwenye kila nukta ya lengo mahsusi litakaloainishwa na jinsi CCM inavyofanya na mazingira yalivyo sasa.
Ukiachilia mbali juu ya kuheshimu na kuthamini utu na haki nyinginezo za binadamu, haki ya kufanya kazi halali, haki sawa kwa raia wote bila ubaguzi, na nchi kutawaliwa kwa misingi ya demokrasi na ujamaa kama ilivyo kwenye Ibara 9(a), 9(e), 9(g), na 9(k) bado kuna kusuasua kwa utekelezaji wa ujamaa kwa misingi ya mazingira ya Tanzania.
CCM imeacha siasa ya "Ujamaa na Kujitegemea" na inaendesha siasa za soko huria la siasa. CCM imepoteza maadili ya kiitikadi juu ya "kujenga jamii ya watu waliyo sawa na huru;" sasa inajenga matabaka ya watawala na watawaliwa, walio nacho na wasio nacho.
Sasa tugeukie nukta za muktadha wa makala hii ambazo kwa mtazamo wa jicho la uchunguzi na mantiki (hoja za kisayansi) CCM imezivunja kwa jinsi ya kushindwa kutekeleza haki na wajibu kama chama kinachounda serikali.
Tahadhari juu ya kupupia kusoma nukta hizi inatolewa na kwa jinsi hiyo ni vema msomaji akaweka kielelezo cha Katiba ya JMT ya 1977 (2005) ili kutoa nafasi ya kuziona nukta hizo.
Nukta ya kwanza ni ulinzi na utekelezaji wa sheria za nchi kama ilivyo kwa Ibara 9(b). Hadi sasa serikali ya CCM imeshindwa kulinda na kutekeleza baadhi ya sheria muhimu kwa maslahi ya taifa. Mfano wa karibuni ni kuvunjwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya 2004 na Kanuni zake za 2005; ambapo kuvunjwa kwake ndiko kulikopelekea Tanzania kuingia kwenye zabuni tata ya ufuaji wa umeme wa dharura uliyoipa mkataba ghushi Richmond Development Company LLC uliyohaulishwa kwa Dowans inayoidai TANESCO shilingi bilioni 94 za Tanzania.
Katika mazingira yasiyozoeleka, Waziri Mkuu wa JMT amemzuia Waziri wa Ujenzi, Dakta John Pombe Magufuli kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Barabara ya 2007; na kibaya zaidi, kusimamishwa utekelezaji wa sheria hiyo si kunaweza kujenga kiburi kwa wavunja sheria bali kunaweza kuleta sintofahamu na au vuta-ni-kuvute itakayovuruga utekelezaji wa sheria.
Kama wananchi wataachwa wavunje sheria ilhali kwa jinsi moja na au nyingine serikali inawaacha waendelee na uvunjifu kwa sababu za kisiasa kuna hatari ya sheria nyingi zaidi kuvunjwa.
Ibara ya 9(c) inaitaka serikali kuhakikisha kwamba shughuli zake zinahakikisha kwamba utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine! Cha kusikitisha, CCM imeshindwa kuendeleza sehemu kubwa ya utajiri wa Tanzania na badala yake imewaachia wageni na waporaji wa rasilimali na mali ya asili.
Kwa sehemu kubwa serikali imeshindwa kuhifadhi utajiri wa Tanzania na kuutumia kwa manufaa ya wananchi wengi wa Tanzania; badala yake serikali imeendelea kuwaachia wanyonyaji wachache wanaovuna holela.
Ubinafsishaji umefanywa kuwa unyonyaji kwa jinsi ya aina ya uwekezaji holela. Kama alivyowahi kunukuliwa Mwalimu Nyerere kwamba, "ubinafsishaji ni unyang'anyi;" na ni kweli wananchi wa Tanzania wamenyang'anywa utajiri wao na wanyonyaji wachache wenye choyo, uroho na uchu wa kinyonyaji.
Watanzania wamekuwa wakinyang'anywa ilhali CCM ikitoa usaidizi wa sera na usimamizi wa unyang'anyi huo. Utajiri wa nchi, kama madini, mawe ya thamani na vito unavunwa kwa gharama nafuu na faida kubwa inayopatikana inawatajirisha wanyonyaji wachache wenye kumiliki fursa za uwekezaji kutoka nje.
Maendeleo ya Tanzania yamekuwa yakipangwa kwa mtindo wa zimamoto juu ya menejimenti ya vurugu. Hakuna uwiano wa mizania ya mipango juu ya matumizi endelevu ya rasilimali watu na vitu katika kufikia lengo la ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru katika kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.
Mipango ya Tanzania imekuwa haizingatii uwiano wa upatikanaji wa rasilimali na matokeo halisi ya utumizi wake bila ya kuathiri mazingira ya uchumi, jamii na siasa.
Japokuwa Ibara ya 9(f) inatamka juu ya kuhifadhi na kudumisha heshima ya binadamu kwa mujibu wa Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu bado kuna dalili mbaya ya ukosefu wa heshima juu ya binadamu na haki zake. Kumekuwa na uvunjifu wa moja kwa moja na au kwa taathira yake juu ya heshima ya binadamu.
CCM imeshindwa kutambulisha heshima ya binadamu juu ya haki ya kila mtu kufanya kazi yenye kulinda utu na heshima yake na juu yake kupata malipo yenye kujenga heshima ya kibinadamu.
Wakati huu sehemu fulani ya wananchi wa Tanzania wanajihusisha na kazi haramu na zinazotweza utu na heshima ya binadamu kama vile ukahaba, usafirishaji wa binadamu, uuzaji wa viungo vya binadamu (hususan vya albino), dawa za kulevya na ufuaji wa fedha haramu.
Ibara ya 9(h) imekuwa ikivunjwa kwa nyakati tofauti; hata hivyo kwenye Awamu ya Nne, CCM imebeba mzigo mzito wa lawama juu yake. Serikali ya CCM kwa mujibu wa ibara iliyotajwa inawajibika kuhakikisha kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.
Ushahidi uliopo unaonyesha kwamba CCM imeshindwa kuzuia dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na upendeleo! Kwa ujumla, kumeibuka uharibifu mukubwa wa mfumo na wa ndani ya mfumo (ufisadi) unaohanikizwa na ujambazi wa kiserikali unaotishia mustakabali wa uongozi wa CCM.
Kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 9(c), Ibara ya 9(i) inasisitiza juu ya matumizi ya utajiri wa taifa juu ya mkazo wa maendeleo ya wananchi na hususan kwenye kuondoa umasikini, ujinga na maradhi. Hali ya matumizi ya utajiri wa nchi inakatisha tamaa na maadui hawa watatu wa taifa waliyotangazwa baada ya uhuru bado wanawasumbua wananchi. Serikali ya CCM imekuwa ikitumia nadharia zaidi juu ya utumizi wa utajiri wa taifa katika kuleta maendeleo kinyume chake chama hicho kimekuwa kikiahidi (ahadi za kinafiki zisizotekelezeka) na kuwaacha wananchi kwenye msongo wa kungojea miujiza ilhali utajiri wa taifa unavunwa na wanyonyaji wachache wenye uchu wa kunyonya kwa mtindo wa kunyang'anya!
Hali halisi ambayo CCM imeijenga kwa nyakati hizi ni knyume kabisa na Ibara ya 9(j) inayoelekeza kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi. Ukweli usiyokuwa na shaka ni kwamba CCM baada ya kulitupa Azimio la Arusha na kuruhusu uchumi huria imesababisha njia za uchumi kumilikiwa na wanyonyaji wachache ambao kwa sehemu kubwa wamehodhi mali na utajiri wa Tanzania.
Na hii inaonekana hata ndani ya CCM ambayo imesheheni matajiri wenye satwa hata yakucheza kifisadi juu ya maamuzi nyeti yenye taathira za moja kwa moja kwa uchumi wa Tanzania.
Tazama mfano wa "mgawo wa umeme" na madhara yake kiuchumi! Haya ni matokeo ya mtu mmoja na au kundi la watu wachache wenye nguvu ya kiuchumi (wafanyabiashara) waliyoimeza CCM na kukifanya chama hicho kiwe kama kampuni badala ya kuwa taasisi ya watu (wakulima na wafanyakazi) kama ilivyokuwa wakati kilipoasisiwa tarehe 5 Februari, 1977.
Kwa kuzisanifu nukta zilizoonyeshwa, kujadiliwa na kuwekwa bayana kwa jinsi CCM inavyoshiriki kwa njia moja na au nyingine ni wazi chama hicho kimevunja malengo mahsusi ya Katiba ya JMT ya 1977 (2005) na kwa vyovyote vile hakuna jinsi ya kurekebisha hali hiyo iliyovuruga mwenendo wa uchumi, jamii na siasa.
Wananchi wengi wasiojua nini kinaendelea ndani ya mzingo wa ndani (Kamati Kuu ya CCM) na wapambe wa karibu wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wamebaki vinywa wazi huku wakisubiri hatima ya uongozi wa CCM.
Kama chama kilichopoteza kada ya uongozi wa kisiasa wa kijasiri kama ilivyokuwa enzi za "jeuri ya chama" ambapo wanyonyaji na wahujumu uchumi walikuwa wakiogopa kunyonya au kuhujumu kwa kuwa uongozi wa chama ulikuwa madhubuti (ngangari) na wenye kuzingatia uhuru, haki, usawa na uadilifu kwa minajili ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania; CCM imesheheni "mitandao" ya watu wenye choyo, uchu na uroho wa kutawala kwa utumizi mkubwa ya ujambazi wa kiserikali na utumizi endelevu ya ufisadi wa kimfumo na wa ndani ya mfumo.
CCM imekuwa chama kilichopoteza itikadi ya kuwatetea wanyonge badala yake kimekuwa chama cha kuwalinda wanyonyaji na wanyag'anyi wa utajiri wa taifa.
Mwisho, tumalizie na uvunjaji wa Ibara ya 105(1) juu ya "Muafaka wa CCM na CUF Zanzibar". Kwanza ieleweke hapa kwamba muafaka uliosababisha serikali ya umoja wa kitaifa (SUK) ya Zanzibar ni jambo la kupongezwa na kupigiwa mfano.
Hata hivyo, kufanyika kwa muafaka huo kumesababisha kuvunjwa kwa Ibara ya 105(1) (b) inayotambua kuwapo kwa Waziri Kiongozi wa SMZ.
Utashi wa kisiasa uliosababisha kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ungetumika kufanya mabadiliko ya msingi kwenye Katiba ya JMT ya 1977 (2005) ungekuwa muafaka juu ya kujenga umoja na undugu katika kudumisha muungano.
Kwa jinsi hii, na kwa kuwa CCM imeyaacha malengo mahsusi yaliyoanishwa kwenye Katiba ya JMT ya 1977 (2005) sidhani kama bado CCM ina uhalali wa kuwa chama kinachoweza kuongoza mapambano dhidi ya kuondoa umasikini, maradhi na ujinga. CCM inaonyesha wazi kukosa dhamira ya kuendeleza mapambano ya moja kwa moja katika kuondoa aina zote za ufisadi hususan ufisadi wa kimfumo wa ndani ya mfumo na ujambazi wa kiserikali. Vilevile, hakuna dalili njema na za waziwazi kwamba CCM ina dhamira nzuri juu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hivyo basi, na kwa kuwa CCM ni chama kinachotumia sana mikutano katika kujadili na kutengeneza programu za utekelezaji ni wakati muafaka kwa chama hicho kuanza maandalizi ya kurekebisha makosa makubwa ya kimfumo na ya kiutendaji ili kulinasua taifa kwenye mkwamo wa kiuchumi, kijamii na kisiasa. Au kinyume chake Msajili wa vyama vya siasa Mheshimiwa John Tendwa, kama anaweza, achukue hatua za kisheria dhidi ya chama hicho kilichovunja Katiba ya JMT ya 1977 (2005).
Na kwa wananchi kwa ujumla, ni wajibu wetu wa kikatiba kutumia nafasi yetu katika kuhakikisha kwamba CCM, kwa kuwa ndicho chama kinachoongoza serikali, kinawajibishwa katika yale yanayokwenda kinyume na Katiba ya JMT ya 1977 (2005).
Hatujachelewa, elimu kwa umma ni muhimu. Kwa hiyo, vyama vya siasa vya kidemokrasi huu ni wakati muafaka kutumia fursa iliyopo katika kujenga jukwaa la kuishitaki CCM kwa wananchi.
Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi
Kitivo cha Biashara, Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kwa simu namba 0713593347 au
Barua pepe:
maligwa1968@yahoo.com,
bakari.mohamed@mzumbe.ac.tz
juu