Kikwete kitanzini
• Muswada wa Katiba wapondwa pondwa
na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete anakabiliwa na wakati mgumu wa kuuendeleza mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya, hasa baada ya wadau kuukataa kwa madai una upungufu mkubwa.
Wadau hao wamewaonya wabunge kutoupitisha muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni katika vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza kesho kutwa mjini Dodoma.
Huo utakuwa ni mtihani mwingine mgumu kwa Rais Kikwete ambaye hivi sasa anakabiliwa na jukumu zito la kukisafisha chama chake kinachodaiwa kuwabeba makada waliokifanya kipoteze baadhi ya majimbo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 30, mwaka jana.
Wakizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) lililofanyika jana jijini Dar es Salaam, wadau hao walisema muswada huo hautoi haki kwa wananchi wote kama ilivyotarajiwa.
Wasomi, wanaharakati na viongozi wa vyama vya siasa walisema serikali ichukue maamuzi magumu, hasa kwa kukubali maoni na marekebisho yanayofanywa na wadau badala ya kuendelea kumrundikia madaraka makubwa Rais Jakaya Kikwete.
Akifungua kongamano hilo, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Barnabas Samatta, alisema muswada huo umepotoshwa na umelenga zaidi kutogusa vyombo muhimu katika mabadiliko ya sasa ya Katiba mpya.
Alisema kitendo cha mwandishi wa muswada huo kutaka kutoguswa wala kujadiliwa mamlaka ya Rais na Mahakama ni kwenda kinyume cha mahitaji na matakwa ya Watanzania wa sasa.
Jaji Samatta alisema Katiba mpya inatakiwa kutoa uhuru hata wa kitaaluma na sanaa na kueleza endapo mtu akienda kinyume cha kufafanua haki zake ndani ya Katiba mpya.
"Kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake, neno maoni yake ni muhimu kuzingatiwa, mwandishi wa muswada huu amepotosha, kuna nini hadi hataki watu wajadili mamlaka ya rais katika Katiba mpya, kwa umuhimu huu, je, kama ikitamkwa kuwa kiongozi wa juu hatakiwi kuwa na chama nani atawajibika? Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa muswada huu kuachiwa wananchi kwa maamuzi sahihi.
"Rais kutokuwa sehemu ya Bunge ni muhimu katika mabadiliko ya Katiba mpya, lakini sasa iko haja ya Katiba kutamka Naibu Spika kutoka chama cha upinzani ili kwenda sambamba na ukuaji wa demokrasia nchini," alisema.
Aliongeza kuwa kama mabadiliko yanayozungumzwa kwenye muswada huo hayatazingatia wadau na viongozi wa vyama vya siasa, watu watarajie hukumu nyingi za magereza ya nchini kujaa wafungwa wa kisiasa.
Alibainisha kuwa ili kuepusha hali hiyo serikali ikubali maoni ya wadau na hata kuufanyia mabadiliko muswada wa Katiba kabla ya kupelekwa bungeni.
Alisema ili kwenda sambamba na ujenzi wa Tanzania mpya, mabadiliko hayo ya Katiba ni muhimu kugusa katika kila ibara na haitakiwi rais kuwa sehemu ya Bunge kama ilivyo katika Katiba ya sasa.
Profesa Issa Shivji
Akichangia mjadala huo, Mwenyekiti huyo wa kigoda cha taaluma cha Mwalimu Julius Nyerere, alisema muswada ulioandaliwa kwa ajili ya kupelekwa bungeni umejaa makosa mengi, hasa ya lugha, kimuundo na kikanuni.
Alisema ni lazima serikali ichukue maamuzi magumu, hasa kwa kukubali maoni na marekebisho yanayofanywa na wadau katika mabadiliko hayo ya Katiba mpya ya nchini.
Alisema kwa kutambua hilo, Tanzania inatakiwa kujua haki na wajibu wa mwananchi wa kawaida na si kumfumba mdomo kupitia Katiba mpya.
Dk. Slaa
Akichangia katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema umefika wakati kwa wanasiasa kutoa dira kwa taifa kuhusu mabadiliko ya Katiba mpya.
Alisema kifungu cha 20, kifungu kidogo cha pili katika mabadiliko ya sasa kilikuwepo katika White Paper mwaka 2008, ambapo iliwapa mamlaka watendaji wa vijiji kusimamia maoni hayo na hata kupelekea wananchi wengi kutishwa na hata kukamatwa kutokana na kifungu hicho.
"Kifungu hiki kimewapa mamlaka makubwa watendaji wa vijiji, hali hii tutawashuhudia wananchi wengi wakikamatwa na hata kuogopa kutoa maoni yao katika kuhoji kifungu fulani cha mabadiliko haya ya Katiba mpya.
"Huenda mpaka kufikia mwaka 2020 isipatikane Katiba mpya nchini lakini ni lazima serikali itambue suala la Katiba mpya ni uhai wa Mtanzania na si jambo la kufanyia mzaha kwa kipindi hiki na Tanzania ya leo," alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema ipo haja kwa wabunge kuacha tofauti zao za vyama na kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuukataa muswada huo kwa kauli moja.
Alisema wabunge watakaoupinga muswada huo watapata uungwaji mkono na wananchi ambao ndiyo walengwa wa mabadiliko ya Katiba mpya.
Alisema kama Katiba mpya haitajali maslahi ya makundi ya wananachi wa kawaida ipo siku nchi inaweza kuingia katika hali tete, iwapo mwananchi hatashirikishwa kwa hatua zaidi.
Francis Kiwanga
Mkurugenzi huyo wa Kituo cha Haki za Binadamu nchini alisema mabadiliko ya Katiba ni msingi muhimu nchini.
Kiwanga, alisema kutokana na utungwaji wa muswada ambao unaotarajiwa kuwasilishwa kuwa wa kiwango cha chini, ipo haja ya kufanya makongamano mengi zaidi ili kupata mawazo ya watu wengi.
"Katika hili ni muhimu tupate maoni ya watu wengi na tunasema wote kwa umaskini wetu tutatembea kwa miguu hadi Dodoma ili kwenda kupinga kwa nguvu zetu zote na katu katika hili tunasema wanaharakati kupitia jukwaa la katiba katu hatutarudi nyuma katika madai ya Katiba mpya itakayokuwa na misingi ya haki na demokrasia imara ya nchi," alisema Kiwanga.
Julius Mtatiro
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema kitendo cha serikali kuandaa muswada wa Katiba bila kupata maoni ya wadau hasa vyama vya siasa ni kitendo kinachoashiria kutokuwa tayari kwa mabadiliko ya Katiba mpya.
Alisema upungufu wa makosa hasa katika maandalizi ya muswada huo umefanywa na mtu mmoja akiwa na lengo mahususi la kulinda masilahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na si kuzingatia haki za mwananchi wa kawaida.
Prince Bagenda
Alikuwa akikiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Prince Bagenda, alipata wakati mgumu wa kuendelea kutoa maoni baada ya watu kuzomea na kupiga makofi ili asisikie kile alichokuwa akikisema.
Kabla ya watu kufikia hatua hiyo, Bagenda, alisema hoja ya kujadili Katiba mpya ni ya msingi na serikali inayoongozwa na chama chake imekubali, hivyo ni vema Watanzania waitumie fursa hiyo adhimu.
John Cheyo
Huyu ni Mwenyekiti wa UDP, ambaye alikumbana na zomea zomea kama iliyomkuta mwakilishi wa CCM baada ya kusema kuwa muswada huo si sheria, hivyo ni vema wale wasioridhishwa nao wakapinga kwa amani na utulivu.
Mabere Marando na Sengondo Mvungi
Mshauri wa Sheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi Dk. Sengondo Mvungi na Mabere Marando (CHADEMA) wameupinga muswada huo kwa madai hauna manufaa kwa taifa na badala yake umejaa vitisho.
Walisema muswada huo umeonyesha hauna nia njema kwa Watanzania na una kipengele kinachokataza mtu yoyote au kiongozi wa chama cha siasa kufanya kampeni juu ya Katiba mpya kwa madai suala hilo ni jukumu la tume itakayoundwa.
Katika kongamano hilo wachangiaji wengi walionekana wazi kuupinga muswada huo wa Katiba ulioandaliwa na serikali.
Kutoka Zanzibar, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa baadhi ya wanasheria na wanaharakati wamelalamikia kuwepo serikali kubwa ya Zanzibar ambayo ni matokeo ya madaraka makubwa aliyopewa rais na katiba iliyopo ya 1984.
Walisema tangu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, kutangaza baraza lake lenye mawaziri 19, wakiwemo watatu wasiokuwa na wizara maalumu, kumekuwa na malalamiko mengi ya ukubwa wa serikali, wakati Zanzibar ikikabiliwa na uchumi duni.
Akiwasilisha mada katika mjadala uliofanyika jana na kuandaliwa na taasisi tatu zisizokuwa za kiserikali, mwanaharakati, Salma Maulid, alisema Katiba ya Zanzibar imempa mamlaka makubwa rais na ndiyo maana kunaweza kuwepo mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu."Rais amepewa madaraka makubwa kikatiba, kuna haja gani Zanzibar kuwepo mawaziri wasiokuwa na wizara maalumu?" alihoji.
Aidha, alisema kwamba wananchi wanahitaji kuiangalia kwa umakini Katiba ya Zanzibar kwa vile kuna vifungu vinampa mamlaka makubwa rais, ikiwemo uwezo wa kulivunja Baraza la Wawakilishi, uwezo wa kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu na uwezo wa kusamehe mtu yeyote aliyehukumiwa kufungwa.
Salma alisema sura ya nne hadi 38 kuhusu mamlaka ya rais imetoa uwezo mkubwa kwa rais na kutoa mfano wa Baraza la Wawakilishi, limepewa uwezo kumjadili rais, lakini kutokana na uwezo aliopewa anaweza kulivunja Baraza hilo hata kabla halijamjadili.
Naye, mwanasheria Ali Ali Hassan alisema rais amepewa uwezo wa kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu kama kutatokea hali ya vita, lakini katiba hiyo haijaeleza ni vita ya aina gani.
Alisema kwamba, rais amepewa uwezo wa kuteua nafasi mbalimbali nyeti kwa mtu yoyote atakayeona anafaa na katiba hiyo hiyo imempa uwezo wa kumfukuza mtu aliyemteua; awe waziri, katibu mkuu au naibu.
Mwanasheria huyo alisema mjadala huo wa katiba una umuhimu mkubwa kwa wananchi kuifahamu katiba na kuainisha vifungu vyenye kasoro na hivyo kutumia fursa hiyo kupata katiba yenye masilahi.
Aliongeza kuwa suala la uteuzi wa nafasi za uongozi Zanzibar bado lina kasoro, kwa vile baadhi ya watu huteuliwa bila ya kuangaliwa sifa kwa aliyeomba na wakati mwingine hukosekana uwazi na usaili kutofanyika, kama ulivyopangwa.
Taarifa hii imeandaliwa na Bakari Kimwanga (Dar) na Hassan Shaaban (Z'bar).