Ombi la mawakili katika kesi dhidi ya Ditopile:
Viongozi wazuiwe kuwafariji wafiwa
Wadai kuhani msiba ni kama kutoa hukumu
Na Ester Bulaya
JOPO la mawakili wanaomtetea mkuu wa zamani wa mkoa, Ditopile Mzuzuri (58), katika kesi ya mauaji, limeiomba mahakama kutoa amri ya kuwakataza viongozi kwenda kuifariji familia ya Hassan Mbonde, kwa sababu kitendo hicho kinaweza kuingilia uhuru wa mahakama na kufanya haki isitendeke.
Ditopile, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, anashitakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mauaji ya Mbonde, aliyekuwa dereva wa daladala. Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika Novemba 4, mwaka huu kwenye makutano ya barabara za Kawe na Bagamoyo.
Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Michael Lugulu, anayesikiliza shauri hilo, Wakili Nimrod Mkono, ambaye ameongezeka katika jopo la mawakili na kuifanya idadi yao kuwa watano, alidai kitendo cha viongozi kutembelea familia hiyo na kutoa fedha za rambirambi kinaleta hisia mbaya katika jamii dhidi ya mteja wao, wakati kesi bado haijaanza kusikilizwa wala kutolewa uamuzi.
Akiwawakilisha mawakili wenzake, Dk. Ringo Tenga na Cuthbert Tenga waliokuwapo mahakamani, Mkono alidai wanapata wasiwasi juu ya maamuzi yatakayotolewa dhidi ya kesi hiyo.
Mkono alidai jamii tayari inakuwa imeshatoa hukumu kutokana na viongozi wazito kwenda kuhani msiba huo kwa niaba ya Serikali, hivyo kuonyesha mshitakiwa ametenda kosa hilo moja kwa moja, kabla ya hukumu kutolewa.
Tunaweza kusema vitendo vinavyofanywa na viongozi wetu vinakwenda kinyume cha Katiba ya nchi na misingi ya sheria
inatupa hofu kuona viongozi wazito wamekwenda kutembelea familia ya marehemu.
Alikwenda Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, akasema amekwenda kwa niaba ya Rais kutoa pole, amekwenda Makamu wa Rais
hii inaleta picha gani katika jamii si ina maana wao wanaamini kuwa huyu mtu amefanya kosa? Sisi tunaomba upige marufuku, mteja wetu hatendewi haki, alisema Mkono.
Mkono aliongeza: Wakienda kutoa pole bila magari ya vingora na mapikipiki hatutakuwa na tatizo, lakini kama wanaenda kiserikali basi waende na gerezani kumtembelea mteja wetu, isiwe ubaguzi wa upande mmoja.
Hii kesi hata upelelezi bado, mimi sitaona ajabu nikisikia Jaji Mkuu naye amekwenda sijui na Spika naye atakwenda au hata wewe mheshimiwa unaweza kwenda, kwa kweli inatupa hofu, hii kesi ipo mahakamani tunaomba waiachie mahakama.
Kama wanataka basi waende kwa siri kuliko hali ilivyo sasa, yaani kila anayejisikia na msaada wake anataka kwenda kutoa rambirambi, mbona kuna watu wengi wanapigwa risasi hatuoni wakipewa pole na kutembelewa kama ilivyo kwa kesi hii? Waende basi na hizo zawadi gerezani kumpa mteja wetu, alisema Mkono.
Akijibu hoja hizo Mwendesha Mashitaka Charles Kenyela, alidai mahakama imepewa mamlaka na serikali pamoja na uhuru wa kufanya kazi na kutoa maamuzi bila ya kuingiliwa na viongozi au mtu yeyote.
Mahakama haifanyi kazi ama kutoa maamuzi kwa ajili ya maneno ya mtaani au kwa ajili ya shinikizo, hivyo kwa mawazo yangu sidhani kama matukio hayo yataingilia utoaji maamuzi ya kesi hii, alidai Kenyela.
Akijibu maombi ya mawakili wa Ditopile, Hakimu Lugulu alisema mahakama hiyo, haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji, hivyo hata maamuzi mengine yoyote yanayohusu kesi hiyo yataamuriwa na Mahakama Kuu. Hata hivyo, alisema malalamiko hayo yatabaki katika kumbukumbu za mahakama .
Kama nilivyosema awali, kesi hii inasikilizwa Mahakama Kuu, hivyo hamna namna ya kuagiza hilo litendeke, lakini ninaimani viongozi wa Serikali watakuwa wamesikia na waandishi wa habari watakuwa wamesikia, lakini pia malalamiko haya yote nimeyanoti kwenye kumbukumbu ya mahakama, alisema Hakimu Lugulu.
Ditopile aliyepandishwa kizimbani mara ya kwanza Novemba 6, mwaka huu na kusomewa shitaka la mauaji ya Mbonde (33), jana akiwa kizimbani alionekana mwenye simanzi muda wote, akiwa amejishika tama na kuinamisha kichwa chini.
Kesi hiyo tofauti na zingine za mauaji, imevuta hisia za watu wengi ambao jana walijaa mahakamani. Itatajwa tena Desemba 4, mwaka huu.
Chanzo: Gazeti la Uhuru, Jumanne 21, Novemba 2006