Wizara ya Ardhi
Govt Institution
- May 14, 2024
- 306
- 165
★ Asema maeneo yanapoachwa kama mapori hujenga dhana kuwa hayana mwenyewe
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya, amewataka wawekezaji nchini kuhakikisha wanaendeleza maeneo waliyopewa kwa mujibu wa madhumuni yaliyokusudiwa, akisema kuyaacha bila shughuli na kugeuka kuwa mapori kunaweza kuwafanya wananchi kuyavamia wakiamini hayana mwenyewe.
Mhe. Mmuya ameyasema hayo Oktoba 4, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mkoani Ruvuma, alipofanya ziara katika Shamba Na. 274, Mhukulu Lilahi, lenye ukubwa wa hekta 4,679.72 na linalomilikiwa na Kampuni ya Soagro Co. Ltd kwa ajili ya ufugaji
Amesema umiliki wa eneo unaambatana na wajibu wa kulilinda na kuliendeleza kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa, hivyo wawekezaji wanapaswa kuhakikisha maeneo yao yanaonekana kuwa na matumizi na uendelezaji unaoendelea.
Mhe. Mmuya amesema maeneo makubwa yanapoachwa bila shughuli kwa muda mrefu na kuonekana kama mapori, yanaweza kuwapa wananchi hisia kuwa maeneo hayo hayana matumizi wala mwenyewe, hali inayoweza kuchochea uvamizi na migogoro ya ardhi.
Ametaka wawekezaji kuchukua hatua za kuyaendeleza maeneo yao na kutimiza wajibu unaoambatana na umiliki huo, ili kulinda uwekezaji wao na kusaidia kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza kutokana na uvamizi wa maeneo.