Taasisi ya Mifupa-MOI
Senior Member
- Apr 15, 2025
- 118
- 214
Ziara hiyo, imefanyika leo Septemba 2, 2026, ikihusisha timu ya MOI ikiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, Dkt. Lemeri Mchome, ambapo pamoja na mambo mengine, pande hizo zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika mifumo ya utoaji huduma, matumizi ya miundombinu na kubadilishana utaalamu wa kitabibu.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mchome amesema ushirikiano huo utasaidia taasisi hizo kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuboresha mifumo ya utendaji kazi, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi katika maeneo ya moyo, mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.
Amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, yaliyolenga taasisi za afya kutembeleana, kujifunza na kubadilishana uzoefu ili kubaini fursa za ushirikiano na hatimaye kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Tumeona hali ya utoaji huduma hapa JKCI ni ya kuridhisha sana. Taasisi imewekeza katika miundombinu na huduma mbalimbali, ikiwemo maabara ya kisasa, huduma kwa wagonjwa maalum pamoja na wagonjwa wa kimataifa na kuboresha maslahi ya watumishi. Kuimarika kwa ushirikiano wetu kutasaidia kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za kibingwa nchini,” amesema Dkt. Lemeri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter *******, amesema ziara hiyo imefungua fursa mpya za ushirikiano baina ya taasisi hizo, hususani katika kuboresha miundombinu, mifumo ya utoaji huduma na kubadilishana utaalamu kwa manufaa ya wagonjwa.
“Kuna maeneo mengi ya kushirikiana ili kuboresha miundombinu ya taasisi zetu na hali ya utoaji huduma, ili wagonjwa wetu wapate huduma bora zaidi. Tunapendekeza kuundwe kamati ndogo itakayopitia maeneo ya ushirikiano na kuweka namna bora ya kutekeleza ushirikiano huo. Hatuwezi kufika mbali kwa kufanya kazi kwa kujitenga,” amesema Dkt. *******.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza ushirikishwaji wa wataalamu, kubadilishana uzoefu na teknolojia, kujenga uwezo wa watumishi, pamoja na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kibingwa ndani ya nchi.