WAHESHIMIWA WANA JAMBO EBU NAOMBA MUDA WENU KAMA DAKIKA 10-15 HIVI ILI MUWEZE KUSOMA HII ARTICLE KIDOGO.. NAAMINI HAKUNA ANAYEONEWA !!
HAKUNA anayeweza kukana ukweli kuwa Waziri John Magufuli ni mchapa kazi. Hii inatokana na rekodi aliyojiwekea kwa takribani miaka 12 tangu alipokuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kati ya mwaka 1995-2000, Waziri wa Ujenzi 2000 hadi 2005 na sasa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Katika kipindi hicho chote alichofanya kazi, Magufuli ameweza kuonyesha kwamba anaweza kuwajibika. Tunakumbuka jinsi alivyosimamia usajili wa magari na mitambo ya serikali iliyokuwa inatumiwa kwa maslahi binafsi.
Tunamkumbuka Magufuli alivyopambana pengine hata na wakubwa wenzake ndani ya serikali, akionyesha ni jinsi gani anataka kusimamia haki, sheria na taratibu. Ni Magufuli huyu huyu alitangaza kufutwa kwa makandarasi zaidi ya 3,000, ambao alisema walikuwa wameshindwa kukidhi sheria inayowatambua.
Magufuli ni miongoni mwa mawaziri wachache wa nchi hii wanaoweza kukumbukwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukumbuka takwimu muhimu za barabara alizokuwa akisimamia, wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi. Magufuli hata kama ungemwamsha usingizini, angeweza kutaja urefu wa kila barabara iliyokuwa ikijengwa, inajengwa na kampuni gani, nani ni mshauri (consultant), itagharimu kiasi gani cha fedha na hata itakamilika lini. Magufuli alikuwa na uwezo wa kukumbuka vitu vyote hivyo kwa kichwa.
Huu ni ushahidi kwamba kiongozi huyu alikuwa anafanya kazi yake vizuri, hivyo halikuwa jambo la ajabu mchambuzi wa mambo ya kijamii na kisiasa, marehemu Bugingo kumpachika jina la Mtakwimu.
Alimpachika jina hilo baada ya kumsoma katika makala moja ndefu aliyofanya mahojiano na Salva Rweyemamu wa gazeti la Rai. Katika makala hiyo, mwandishi alisema kwamba Magufuli aliweza kutoa takwimu za barabara zote kuu nchini zilizokuwa zikisimamiwa na wizara yake bila kusoma mahali.
Hata hivyo, ni katika makala hiyo, kasoro moja muhimu ya Magufuli ilijionyesha, jinsi alivyoshughulikia suala zima la uuzaji wa nyumba za serikali. Ingawa hakuweza kujenga hoja ya msingi sana katika makala hiyo kuhusu uuzwaji wa nyumba hizo, mfumo wa uuzaji uliotumika, na hasa swali la kwanini nyumba hizo ziuzwe? Hapa ukawa mwanzo wa kudadisi utendaji wake na uadilifu sawia!
Hivi karibuni gazeti hilo hilo (Rai), lilikuja kubainisha mambo fulani kuhusu nyumba ambayo Magufuli alihusika nayo na kwa hakika hadi leo hajaweza kusema lolote kuhusu ukweli wa nyumba hizo ambazo anadaiwa kujipendelea mwenyewe akiwa kiongozi wa serikali. Kwamba kumbe naye ana kile Wazungu wanachosema dark side.
Lakini lililofurahisha hapa, kama ambavyo amekuwa akilalamika wakati wote kwamba kuna watu wanamwonea wivu; ni maadui wake; hawamtaki, wanataka kumuua hali ambayo iliilazimu serikali ya awamu ya tatu kumwekea ulinzi wa ziada hadi ulipokuja kuondolewa na awamu ya nne, hata sasa bado ana visingizo vya namna hiyo, kuwa anaonewa kwa sababu ya utendaji wake hata kama atakuwa anahojiwa kuhusu kukosea kwake. Ndiyo, anaweza kukosea kwani yeye ni binadamu wa kawaida tu licha ya uwezo wake wa kukariri.
Safari hii suala la nyumba likafunuliwa na Rai, Baada ya Rai kumgusa tu kidogo kuhusu nyumba hizo, Magufuli alikimbilia polisi kuwashitaki wahariri wawili wa Habari Corporation, John Bwire na Muhingo Rweyemamu.
Kwamba wahariri hao wakitumia tu kalamu zao kujua kilichomsibu hata akajipendelea katika ununuzi wa nyumba za serikali, yeye akasema waandishi hao wasiomiliki silaha ya aina yoyote mbali ya kalamu zao tu, eti wanataka kumuua kwa sababu wamehoji kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali ambazo amehusika kama kiongozi wa umma. Kesi hii hadi sasa haijulikani majaliwa yake, isipokuwa wahariri hao walihojiwa na polisi kuhusu kutaka kumuua Magufuli!
Hili likiwa halijafutika vichwani mwa watu, karibuni hapa imeibuka hoja ya baa ya Rose Garden, iliyoko Barabara ya Garden eneo la Mikocheni.
Sakata hili limemuweka Magufuli kwenye mgongano mkubwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Mgogoro huo unaodaiwa kuwa ulianza mwaka 2004, wakati huo Magufuli akiwa Ujenzi, umeingia sura mpya kwa sababu moja tu, kwamba juhudi zote za Manispaa ya Kinondoni ya kutaka sheria na taratibu za mipango miji ifuatwe, zimetupiliwa mbali na Magufuli, na baada ya kufanya hivyo analia kwamba kuna watu wanamwandama kisiasa.
Suala lenyewe kama lilivyoandikwa na gazeti la Tanzania Daima Jumapili Februari 25, 2007, ni mgogoro wa baa ya Rose Garden, ambayo inaelezwa kumilikishwa kiwanja juu ya eneo la hifadhi ya barabara, Waziri Magufuli anaelezwa kuhalalisha kiwanja hicho licha ya kwamba kwa muda wote tangu mwaka 2004 Manispaa ya Kinondoni ilikwisha kusema wazi kwamba ni eneo la hifadhi ya barabara.
Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni lilitoa tamko kwamba baa ya Rose Garden ipo kwenye eneo la hifadhi ya barabara na hivyo itabomolewa, lakini Waziri Magufuli anasema mwenye baa hiyo amemilikishwa kihalali eneo hilo na hivyo yeyote atakayembughudhi atawajibika kumlipa fidia.
Sakata hili hasa linaanzia wapi? Mwaka 1995 mwenye baa ya Rose Garden aliomba kibali kwa Kampuni ya Simu ili aendeshe biashara ya maua mbele ya eneo lao, ambalo ni kiwanda cha kuchapa (Printing Unit) cha TTCL. Aliruhusiwa na kuendesha biashara hiyo ya maua na miche ya miti.
Baadaye alijenga kibanda na kuanza kuendesha baa, kisha baadaye viwanja vikapimwa eneo hilo, ambalo kimsingi ni hifadhi ya barabara, lakini pia ni eneo la mbele la viwanja namba 171/5, 717/3 na 717/4, ambavyo ni sehemu ya kilipokuwa Kiwanda cha Printing Unit.
Baada ya kupimwa viwanja sehemu hiyo kijanja, vyombo vya serikali vilishtuka, na kushauri vifutwe na asimilikishwe mtu. Miongoni mwa vyombo vya serikali vilivyopendekeza kufutwa kwa viwanja hivyo, ambavyo vilipimwa bila kufuata taratibu na sheria za upimaji, ni pamoja na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Manispaa ya Kinondoni; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; lakini juu ya yote ni ukweli uliothibitika baadaye kwamba, eneo hilo lililobuniwa viwanja 948, 949, 950 na 951, kimsingi vililazimishwa hapo na maofisa wa ardhi wa Kinondoni ambao hawakufuata taratibu za upimaji.
Mawasiliano ya kiofisi kati ya Manispaa ya Kinondoni na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, yapo kuthibitisha ukweli huu hata kabla ya Magufuli kuteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo Januari 4, mwaka jana.
Ninaamini Waziri Magufuli alijua kwamba kiwanja hicho cha Rose Garden kilikuwa na mgogoro, na alijua wazi kabisa kwamba kulikuwa na kesi mahakamani kuhusu kiwanja hicho, na kwa hakika kabisa alijua watangulizi wake katika wizara hiyo walikwisha kutambua matatizo ya kiwanja hicho, ndiyo maana michoro yake (plan) ilipendekezwa kufutwa sambamba na hivyo vingine, yaani viwanja namba 948, 949, 950 na 951.
Haya Magufuli aliyajua, lakini mwaka jana akiwa amekaa wizarani hapo kwa takribani miwezi sita tu, aliamua kuruhusu umilikishwaji wa kiwanja chenye mgogoro bila hata kutaka kupata taarifa za suala hilo kutoka Manispaa ya Kinondoni. Uamuzi huo umezua mgogoro wa kiutendaji baina yake mwenyewe na mamlaka nyingine za serikali kama manispaa na hata watu wengine wenye maslahi na eneo hilo, kwa sababu wapo hapo kisheria.
Baada ya kuibuka yote haya, Magufuli, ambaye kama ilivyoelezwa hapo juu kwamba ni mchapakazi, amerejea moja kwa moja kwenye ile ngome yake ya kulia kila anapoelezwa awajibike kwa maamuzi yake mengine ambayo si mazuri.
Safari hii hoja inayojengwa hapa, eti ni ya kummaliza kisiasa! Yaani kisiasa maana yake nini? Yaani anamalizwa na Manispaa ya Kinondoni ili wapate kiti chake? Kwani nani katika madiwani wa Kinondoni anatoka Biharamulo ili ielezwe kwamba wanataka jimbo lake la uchaguzi?
Kwani Magufuli si alipita bila kupingwa, hata kama kuna mtu alikataliwa kupokewa kwa fomu zake ndani ya CCM? Mizengwe ya ajabu jimboni kwa Waziri Magufuli!
Katika mgogoro wa kiwanja cha Rose Garden, ni lazima Waziri Magufuli atambue kwamba amevurunda kama ifuatavyo:
Moja, amepuuza mamlaka nyingine za serikali ambazo zilifanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Pili, ni lazima ajue kwamba pamoja na kujua kwamba suala la kiwanja hicho lilikuwa mahakamani, alishindwa kuheshimu uhuru wa mahakama na hivyo kuchukua hatua ambazo zilifanya shauri lililokuwa mahakamani kupoteza maana.
Tatu, kwa maamuzi hayo ya kutambua kiwanja hicho na kukipa hati, sasa amefanya kiwanja namba 717/4 kiwe kisiwa ambacho hakiwezi kufikika kabisa.
Nne, muhimu zaidi sasa waziri anafungua ukurasa mpya kwamba watu waliovamia maeneo ya hifadhi ya barabara nchini kote, watakuwa na haki ya kumilikishwa viwanja hivyo - amejenga precedent.
Pamoja na haya yote, sasa Magufuli inabidi akiri kwamba wale wakazi wa Ubungo, tena masikini wa kutupwa, aliosimamia wakabomolewa nyumba zao ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo hadi Mbezi Luis, aliwaonea na sasa anawajibika kuwaomba radhi kwa sababu eneo la hifadhi ya barabara linaweza kumilikishwa mtu, kwani hata pale Ubungo Kibo walikuwako watu waliokuwa na hati za kumilikishwa viwanja vyao.
Kama Magufuli hawezi kuomba radhi, anachofanya sasa kwamba eti anafanyiwa vita ya kisiasa, ni sawa na machozi ya mamba, tunamwomba aendelee kusimamia haki na sheria za matumizi ya ardhi kama alivyofanya akiwa Ujenzi, sheria ya ardhi ni moja tu, tunamshauri afikiri upya.
Maamuzi kama haya hayasaidii kujenga nchi wala kutanda kwa utawala bora na matumzi mazuri ya ardhi kwa maendeleo ya taifa hili.
HAKUNA ANAYEONEWA !! SASA BASI, MZEE MWANAKIJIJI KAMA UNGEKUWA DAR NA UNGECHAPISHA MADA YAKO ILE YA UUZAJI NYUMBA ULIOFANYWA NA MAGUFULI, NADHANI KICHWA CHA HABARI KILIKUWA "JE MAGUFULI NI MCHAPAKAZI AU NA YEYE NI MJANJA MWINGINE" SOMETHING LIKE THAT, NADHANI UNAJUWA NINI KINGEKUTOKEA...............