Monitoring thread: John Pombe Magufuli katika Awamu ya Nne

Monitoring thread: John Pombe Magufuli katika Awamu ya Nne

KadaMpinzani

Maneno ya Waziri Magufuli ni hayo hapo juu, sasa nini unaongea? Issue ninayokupinga ni ya wewe kuandika uongo wa maneno yako tofauti na yale aliyosema, ndio kwamba huna credibility ya yale unayoandika. Sina sababu ya kubishana na wewe tena, ulitakiwa ukubali tangu ukurasa wa 9 lakini ukatoa visingizio lukuki. Asiyekubali kushindwa sio mshindani na hapa hatushindani bali tunaanika ukweli na wewe unataka kupindisha ukweli huo.
 
Magufuli aandaa risasi kujibu mashambulizi Sakata la Rose Garden
Charles Mullinda na Agnes Yamo

MGOGORO wa kiwanja namba 951, ilipojengwa Baa ya Rose Garden jijini Dar es Salaam, umechukua sura mpya baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, mmoja wa viongozi walio katikati ya sakata hilo kuandaa hoja za kujisafisha dhidi ya tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Aidha, mgogoro huo ambao taarifa za karibuni zinaonyesha unatafutiwa njia ya kufikishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, umeshafikishwa au kuwagusa kwa namna tofauti, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba.

Habari kutoka vyanzo kadhaa vya kuaminika zinaeleza kwamba, tayari maofisa wa wizara hiyo wameshaanza kukusanya taarifa mbalimbali ili kujua sababu hasa ya suala hilo linalohusu baa, ifikie hatua ya kugusa hisia za viongozi wa juu kama Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa CCM na Baraza la Madiwani wa Kinondoni.

Kikubwa kinachoanza kutia shaka sasa ni namna Makamba ambaye kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuingia kwake moja kwa moja katika suala hilo kwa kiwango cha kutaka mmiliki wa Rose Garden apokonywe kiwanja hicho.

Aidha, kumbukumbu za kimaandishi zinaonyesha kuwa, Makamba alianza kujihusisha na suala hilo kwa karibu kabisa, akisema anafanya hivyo akipata taarifa kutoka kwa watu anaowataja kuwa wasamaria wema (wasiotajwa kwa majina).

Kwa mara ya kwanza Makamba alianza kujihusisha moja kwa moja na suala hilo Juni mwaka 2004 kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni na baadaye mwaka huo huo akaandika barua kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo.

Baada ya suala hilo kugonga mwamba na kukosa kumalizwa, Januari mwaka jana tena, siku 12 baada ya Kikwete kuunda Baraza la Mawaziri, aliandika barua ndefu yenye kurasa nne kwenda kwa Magufuli akihoji kuhusu uhalali wa mmiliki wa Rose Garden kuendelea kuwapo hapo kinyume cha sheria.

Katika hali inayoweza ikazusha maswali mengi baadaye, Makamba alituma nakala za barua hiyo kwa Rais, Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Waziri wa Miundombinu, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

Katika hali ambayo bado haijawa wazi hadi hivi sasa, Makamba huyo huyo tena, katika tarehe na siku isiyojulikana wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, aliamua kuandika barua kwa Waziri Mkuu akimlalamikia mmiliki huyo wa Rose Garden.

Hatua hiyo ya Makamba kwa nyakati tofauti ilikwenda sambamba na msimamo wa Manispaa ya Kinondoni, moja ya eneo linaloongoza kwa migogoro ya viwanja hapa nchini, wa kutaka kuivunja baa hiyo kwa madai kwamba imejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara.

Hata hivyo jitihada hizo za Makamba na za Manispaa ya Kinondoni kwa nyakati tofauti zilionekana kugonga mwamba baada ya Magufuli kuchukua njia tofauti na wao ya kuamua kutumia sheria kumhalalisha Assey kumiliki kiwanja ilipo baa yake, ambacho kabla ya kukitumia kwa shughuli hizo, ilikuwa ni sehemu ya kuuzia maua.

Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kwamba, kikubwa kilichosababisha suala hilo linaloonekana dogo libadilike sura na kuchukua taswira kubwa hata kuwagonganisha viongozi wa kiserikali, si Rose Garden, bali suala jingine tofauti kabisa.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kiini cha mgogoro huo ni malalamiko ya ama moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja ya mmiliki wa kiwanja kilicho nyuma ya Rose Garden (jina tunalo).

Vyanzo vya habari vya kuaminika vinaeleza kuwa, mmiliki huyo ambaye alinunua kiwanja hicho kwa mamilioni ya fedha, anakusudia kuwekeza kwa kujenga kituo maalumu cha biashara kinachojulikana kwa jina la ‘Dar es Salaam Village Centre’.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mradi huo mkubwa wa mamilioni, umekwama kuanza kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni kuwapo kwa Rose Garden mbele yake, jambo ambalo linaweza kukamisha uwekezaji mzima wa kituo hicho cha kibiashara kinachokusudiwa kujengwa.

Kwa sababu hiyo basi, malalamiko ya mmiliki wa kiwanja hicho kilicho nyuma ya Rose Garden ndiyo hasa yaliyoamsha hoja za kuhoji uhalali wa baa hiyo kujengwa hapo, hali inayozuia wamiliki wengine na hatimaye kuzaa mgogoro wa sasa.

Mgogoro huo, ambao umevuta hisia za Watanzania wengi na kuwahusisha baadhi ya viongozi wa juu serikalini, huku ukiibua mvutano baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni inayoongozwa na Meya Salum Londa kwa upande mmoja na Waziri Magufuli kwa upande mwingine, sasa unaonekana dhahiri unaweza ukapanda ngazi za juu kuchukua sura nyingine.

Habari zaidi ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka vyanzo vya kuaminika katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaeleza kwamba, Magufuli amelazimika kuandaa vielelezo vya maandishi na vya kauli kuhalalisha kuridhia kwa uamuzi wa Kamishna wa Ardhi wa kumpa mmiliki wa Rose Garden hati halali ya kumiliki kiwanja namba 951, ilipojengwa baa hiyo maarufu.

Inaelezwa kuwa moja ya vielelezo hivyo ni majibu ambayo Magufuli alimwandikia Waziri Mkuu, Edward Lowassa, akielezea sababu hasa za kummilikisha, Damas Assey, kiwanja hicho.

Ofisa mmoja wa juu wa wizara hiyo aliyezungumza na gazeti hili alisema, Magufuli katika majibu yake hayo, amebainisha kiini cha mgogoro huo kuwa ni mmiliki mwingine wa kiwanja kilicho karibu kabisa na kiwanja ilipojengwa Rose Garden.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, uamuzi wa Magufuli kuridhia kupewa hati kwa mmiliki huyo kulichangiwa kwa kiwango kikubwa na ripoti aliyopewa na wataalamu wa wizara hiyo waliokwenda kuchunguza kiini cha malalamiko ya kuonewa yaliyofikishwa hapo na Assey dhidi ya Manispaa ya Kinondoni.

Aidha, majibu ya maelezo hayo yaliyoandaliwa na Magufuli yanaweza kuibua kashfa nyingine ya rushwa ndani ya Wizara ya Ardhi, Manispaa ya Kinondoni na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa hapa jijini wanaotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mgogoro huo.

Katika maelezo yake, Magufuli anabainisha jinsi mmiliki wa kiwanja hicho, Damas Assey alivyoomba na kumilikishwa eneo hilo na Kamishina wa Ardhi, Albert Msangi na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni kupewa taarifa ya maandishi kuhusiana na suala hilo.

Anaeleza kuwa eneo la Rose Garden liko kwenye safu ya viwanja namba 948, 949, 950 na 951 ilipojengwa baa hiyo, katika eneo la Mikocheni, kandokando ya barabara ya Garden na Mikocheni.

Magufuli anaeleza katika maandishi yake kuwa, viwanja hivyo vilibuniwa katika mchoro wa mipango miji TP.NO 1/518/369 ‘B’ na upimaji kukamilishwa kwa ramani ya upimaji namba ‘E’ 320/224 ya Aprili 16, 2004.

Sehemu ya maelezo hayo ya maandishi ambayo gazeti hili limepata nakala yake, inasomeka kuwa: ‘Aidha ubunifu na upimaji wa viwanja hivi ulikuwa ni muendelezo wa upimaji wa eneo lenye viwanja kati ya 383 hadi 385 kwa ramani namba E 320/74.

“Baada ya upimaji huo kukamilika, mmiliki wa Rose Garden, Damas Assey aliwasilisha maombi ya kumilikishwa kiwanja hiki kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

“Taratibu za umilikishaji zilifuatia kwa kuandaliwa nyaraka stahili lakini hazikuweza kukamilishwa kutokana na kuwasilishwa kwa hoja ya kupinga umilikishaji huo kupitia viongozi ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, na jirani/mmiliki wa kiwanja namba 717/5 kilichopo nyumba ya kiwanja namba 951 baada ya kiwanja hicho kununuliwa na Kampuni ya ZEK GROUP LTD.

“Tarehe 7, Machi 2006, Damas Assey ambaye ndiye mmiliki wa Rose Garden, alileta malalamiko yake kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akilalamikia kutotendewa haki.

“Waziri aliagiza ufanyike uchunguzi juu ya ukweli wa suala hili na yalibainishwa mambo yafuatayo; ramani ‘E’ 320/224 bado ni hai na haijafutwa,” yanasema maandishi hayo ya utetezi wa Magufuli.

Maandishi hayo ya Magufuli yanavitaja viwanja vingine vilivyobuniwa na ramani hiyo hapo juu kuwa ni, 948, 949 na 950 na vilipimwa kwa ramani namba ‘E’ 320/74 ambavyo ni 383 -385 havilalamikiwi japo vyote vipo kwenye safu moja kando kando ya barabara ya Garden.

‘Wenye viwanja namba 948 na 950 hawabughudhiwi na wanatambulika na mamlaka husika isipokuwa mwenye kiwanja namba 951(Rose Garden).

‘Waziri aliagiza haki itendeke kwa kummilikisha Damas Assey ambaye ni mmiliki wa Rose Garden’.

Aidha, katika maelezo yake, Waziri Magufuli anabainisha kuwa, ubunifu na upimaji wa kiwanja namba 951, ilipo Baa ya Rose Garden, umezingatia sheria, kanuni na sheria za mipango miji na kwamba, eneo hilo halipo kwenye hifadhi ya barabara.

Maelezo haya ya Magufuli yanaondoa shaka iliyopo kuhusu uhalali wa kujengwa kwa Baa ya Rose Garden katika kiwanja hicho na yanaondoa nguvu za msimamo wa madiwani wa Kinondoni wa kutaka baa hiyo ivunjwe kwa sababu yanadhihirisha wazi kuwa, halmashauri hiyo iliridhia kuwepo kwa kwa kiwanja hicho.

Vielelezo vingine vilivyoandaliwa na Magufuli ni pamoja na barua ya Kamishna wa Ardhi ya Juni 21 mwaka jana, yenye kumbukumbu namba LD/247419/9/LMK, inayoridhia kumilikishwa kwa viwanja hivyo na kumtaka mmiliki wa Rose Garden kulipa sh mil. 6,121,200 ndani ya siku 30 ili hatua za kumilikishwa eneo hilo ziweze kukamilishwa.

Katika kuhakikisha maamuzi yake hayaingiliwi wala kutenguliwa na viongozi wakuu ambao wamekwisha kuhoji kuhusu ukweli wa jambo hilo, Magufuli ameshamwandikia Waziri Mkuu Lowassa kumtaarifu kuwa kwa mujibu wa sheria namba 167 ya mwaka 1967 inayohusu hifadhi ya barabara, eneo ilipojengwa Baa ya Rose Garden halipo katika hifadhi ya malipo.


Maelezo hayo ya Magufuli yanajibu barua ya Lowassa ya Agosti 4, 2006, yenye kumbukumbu namba PM/P/1/567/38 iliyotumwa kwa Magufuli ikimtaka kueleza ukweli wa jambo hilo.

Magufuli alipewa siku tano na Lowassa kutoa maelezo kuhusu kuwapo kwa baa hiyo katika eneo hilo baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, ambaye amekuwa akimwandikia barua (Lowassa), kuhusu utata wa kujengwa kwa baa hiyo katika eneo hilo.

Alipoulizwa kuhusu mgogoro huo na hatua zinazochukuliwa na Magufuli dhidi ya halmashauri yake juzi, Meya wa Manispaa wa Kinondoni, Salum Londa, alikataa kuzungumza lolote kwa maelezo kuwa suala hilo, sasa linashughulikiwa na viongozi wa juu serikali.

“Siwezi kuzungumza lolote, kama kuna makombora yanaandaliwa dhidi yetu sawa tu, mimi niko kimya, ….andika unavyoona,” alisema.

Londa amefikia hatua hiyo, siku chache tu baada ya yeye na madiwani wenzake wa Kinondoni kutoa msimamo mkali dhidi ya maamuzi ya Magufuli ambaye hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari alisema bayana kuwa mmiliki wa Rose Garden alikuwa na hati halali za umiliki.


Habari hii inapatikana: Magufuli aandaa risasi kujibu mashambulizi
 
Sakata la Rose Garden linafichua mambo mengi kwenye Manispaa ya Kinondoni hususani ktk ugawaji, upimaji na umilikishwaji wa viwanja!

Ni dhahiri hapa kuna harufu ya rushwa, rushwa ambayo kuna watu ndani ya idara husika kwenye Manispaa Kinondoni hawakuipata. Utafiti wa gazeti hapo juu umeweka mengi hadharani kwamba kuna urasimu, rushwa na kazi ambayo ingefanywa na mtu mmoja wanaifanya watu zaidi ya mmoja bila hata kuwa na coordination! Matokeo yake huyu anapima hivi na mwingine anapima vile nakadhalika.

Huyo aliye nyuma ya Rose Garden (huyu ni Zadock, mmiliki wa Advert International - kampuni ya matangazo ya mabango, huwa anapewa tenda na CCM mara kwa mara) watu wanatilia mashaka jinsi alivyomilikishwa kiwanja / viwanja katika eneo lililokuwa linamilikiwa na Tanzania Post and Teleommunications Corporations baadaye TTCL. Hapa kuna double allocation ya hako kakipande ka Rose Garden - Zadock hatajwi tajwi kama Assey. Na Zadock pale ametengeneza apartments!

Kama kawaida ya serikali yetu naona itaundwa tume kufanya uchunguzi - uchunguzi utakaogharimu mapesa mengi ya walipa kodi, na itapofika mwisho wa siku Assey na wenzie wataondoka ili kumpa njia ya kujenga Dar es Salaam Village Center bwana Zadock kwani ni mtu wa karibu mno na First Lady aliyepita!
 
kuna jambo sielewi hapa. Makamba kama katibu wa CCM anamamlaka gani au anahusika vipi kisheria na kesi hiyo ya Rose garden hadi amwandikie barua Lowassa?
 
kuna jambo sielewi hapa. Makamba kama katibu wa CCM anamamlaka gani au anahusika vipi kisheria na kesi hiyo ya Rose garden hadi amwandikie barua Lowassa?

Hizo barua ziliandikwa wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar na sasa anafanya some clarifications on certain issues, that is my belief.
 
kuna jambo sielewi hapa. Makamba kama katibu wa CCM anamamlaka gani au anahusika vipi kisheria na kesi hiyo ya Rose garden hadi amwandikie barua Lowassa?

Alishapewa mgao wake Tangu akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-salaam na aliahidi kwamba atahakikisha kwamba Assey anaondolewa kwa kuvunjiwa na kutoa mwanya wa upanuzi wa ujenzi wake.swala si kwamba kiwanja kipo kwenye hifadhi ya barabara bali swala ni kwamba aondoke RG apishe nafasi ya utanunuzi wa muwekezaji ZADOK!

Baada ya kusoma maelezo ya Mh.Magufuli hapo juu na yale ya mwanzo kwenye Press Conference MAGUFULI HAPA AMAEINGIA KWENYE HUU MGOGORO Kwa nafasi yake kuhakikisha na RG aliyepeleka malalamiko yake kwake ya uonevu anapatiwa haki yake kutokana na maamuzi ambayo wenyewe madiwani waliyahalalishwa kwa kupima hiyo sehemu kuwa si sehemu ya eneo la barabara na kuwa ni la makazi walifanya hivyo wakitumaini wangempa mtu wao, lakini baada ya kuhalalishwa hiyo sehemu kuwa sehemu ya makazi aliyekuwepo hapo ambaye ndie RG naye aliomba na akapewa pamoja na Halmashauri kumwekea ngumu.

Sasa tunachokiona hapa ni wale wote waliokwisha kula cha ZADOK na kumuahidi ndiyo wanafuatilia na kwabahati mbaya wamekuja wakati mbaya kwani Kuna mtu anaitwa Magufuli kwenye hiyo wizara.
 
Magufuli alipewa siku tano na Lowassa kutoa maelezo kuhusu kuwapo kwa baa hiyo katika eneo hilo baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, ambaye amekuwa akimwandikia barua (Lowassa), kuhusu utata wa kujengwa kwa baa hiyo katika eneo hilo.

ole kwa jinsi nilivyosoma habari inaonyesha makamba amemwandikia barua lowasa akiwa tayari ni katibu wa ccm. Na hata kama aliandika wakati ni mkuu wa mkoa angemwandikiaje lowasa wakati lowasa alikuwa ni waziri wa maji?
habari hii ina utata mwingi inaelekea kuna watu wengi wenye interest na hii kesi
 
Msimamo wa Magufuli ungekuwa kwa wachimba madini nafikiri tungekuwa na viongozi Tanzania lakini ndio hivyo. Hii issue ya kiwanja kimoja tena cha mtu binafsi kakivalia njuga wakati nchi inafilisiwa!..

Kwa vyovyote vile kwani sheria inayotumika kuwaondoa watu wenye vibanda vyao (wakiwa na hati za kumiliki za muda) ni ipi tofauti na sheria ambayo inatumika hapa?.
 
Mkandara!

Fikra zako za msimamo kuhusu madini ni sawa LAKINI Kumbuka kwamba tumeamua kuliona hilo la madini kwamba linahitaji msimamo kama huu kwasababu ya msimamo wa huko nyuma akiwa miundombinu na bado msimamo wake kwa hili.

Facts za Magufuli zinakubalika zaidi Yao hao ambao hawatoi facts bali wanamtishia mara kumsemea kwa makamba,mara kwa Waziri Mkuu Lakini jamaa pamoja na yote hayo amesimamia msimamo wake na kwa mtizamo wangu kama kweli viwanja katika ramani moja iliyoombewa kibali ili viruhusiwe na vikaruhusiwa kwanini IWE RG?

Kama alivyouliza magufuli na si na hivyo vingine vilivyotolewa sambasamba na hicho cha RG wakati wa kuhalalisha hilo eneo lisiwe la barabara na liwe la makazi au whatever?Swala hawa hawatetei barabara bali wanamtetea ZADOK Kama mwekezaji Chini ya kivuli cha sehemu ya barabara wakati wanasahau hata huyo ZADOK Na viwanja vingine vilivyotolewa chini ya RAMANI E ya mipango miji vilikuwa ni sehemu ya barabara vikafutwa na kuruhusiwa watu kumiliki wakiwemo hao wote.sasa hapa wasiyemtaka ni RG. Kwanini?

Sababu ZADOK ANATAKA KUPANUA ENEO LAKE,Sasa kauli ya magufuli ndiyo inasema kama wanalitaka sio wampokonye kwa kumuonea wapatane.

Na Tanzania watu ni wajeuri anaweza asipatane na Mhusika lakini atembeze Rushwa ili tu Amdhulumu mhusika na kuonyesha jeuri na hapa ndivyo anavyofanya muwekezaji ZADOK!.Huyu RG Amewashika pabaya hao wakubwa kwa turufu ya msimamo wa MAGUFULI.

Magufuli akilegalega tu na RG amekwenda na maji.Halafu huo upandemwengine kama wanaona wameonewa yaani et al si waende Mahakamani kama alivyowahi sema Magufuli na akabainisha yeye na kamishina watakuwa shahidi wa RG kwani ndiye mwenye haki kwa mtazamo wao na sheria ya umilikishwaji wa ardhi.
 
KNKU,

Mimi mshikaji naamini kabisa usawa ktk sehemu zote. nachojaribu kusema hapa ni kwamba Magufuli kesha fanya mengi kama hawa jamaa yote inategemea ni nani mhusika. Ukienda sehemu kibao watu wamevunjiwa nyumba zao na baadhi zimeachwa ama kupindisha ramani. Sheria ipo mikononi mwa viongozi zaidi ni personal interest inatangulia zaidi. Kujuana ni part ya mila yetu ktk utendaji kazi na nina hakika kiwanja hicho kingekuwa cha Mzee Juma pasingekuwepo na uvutano kama huu.

Nakumbuka wakati wa Kujengwa kwa Sheraton kulitokea hoja kubwa sana ya kiwanja hicho na viongozi walishinda kwa sababu zao binafsi.
Hao madiwani wanatafuta kula la huyo Magufuli pia hana tofauti zaidi ya kutazama nani muathirika....Period!
 
Mkandara!
unajua kwanini mimi hapa ninaona maelezo ya magufuli ni logic kuliko ya upande mwengine katika hatua zote za awali za maamuzi ya utoaji wa hivyo viwanja vyote Magufuli hakuhusika toka kutoka hilo eneo kuligeuza kutoka eneo la barabara na kumilikishwa watu hao wanne tofauti.Sasa Tu -assume magufuli kavuta Lakini je aliyoyasema kweli si haki hususani kwa issue hii?
 
KNKU,

Nashindwa kuamini hata haya kwa sababu ile report ya kwanza inasema RG alipoletewa barua ya kuondoa kibanda chake alimwandikia barua Magufuli na barua ikatajwa nambari zake baada ya mahakama ilipitisha kuvunjwa kwa kibanda hicho. Nao sielewi ni wakati ulipita kati ya barua hiyo na RG kupewa kibali pamoja na wahusika wengine.

KNKU, Bongo mshikaji huna haja ya kuwa waziri wa Ardhi, mtu kama Magufuli anaweza kukuweka ndani ama kukutoa kwa simu tu. Anaweza kutoa mzigo wako bandarini kwa simu tu. Nitarudia kusema viongozi wetu wako above the law kwa hiyo mara nyingi hupenda kuchukua maelezo ya wanyonge dhidi yao.

Tazama Mtikila anavyohangaika kwa kesio ambazo zina kila ushahidi? tazama mauaji ya Pemba, Mwembechai na sasa nimesikia ati Ditto kapewa kesi ya - Kuua bila kukusudia ikishinikizwa na upande wa Defence, hiyo uliona wapi?..Upande wa mashtaka hawana sauti wakati wao ndio wanaotakiwa kuweka madai.

Tutafika lakini!
 
KNKU,

Nashindwa kuamini hata haya kwa sababu ile report ya kwanza inasema RG alipoletewa barua ya kuondoa kibanda chake alimwandikia barua Magufuli na barua ikatajwa nambari zake baada ya mahakama ilipitisha kuvunjwa kwa kibanda hicho. Nao sielewi ni wakati ulipita kati ya barua hiyo na RG kupewa kibali pamoja na wahusika wengine.

Mkandara!
Nilivyoelewa mimi kwa mujibu wa maelezo yaliyoandikwa ndani ya TD ni hivi hayo yote yalifanyika na hiyo sehemu ilikubaliwa kuwa kumilikishwa watu.Initiator wa process nzima ni jiji, lakini baada ya watu kupeleka maombi hao wenye viwanja vingine vitatu walikubaliwa na halmashauri ndiyo ikawa inamzungusha RG,Sasa RG baada ya kuzungushwa muda mrefu toka enzi ya Makamba alipokuja Magufuli kwenye hiyo wizara baada ya ombi lake halmashauri kutokushughulikiwa na kutaka kumpa jirani ndiyo akaomba msaada wa magufuli..................................Na hapo ndiyo maamuzi ya magufuli ya sasa baada ya kuita vielelezo husika akayatoa!
 
Mwanasiasa,
Hapo sasa!... lakini tutafika na ndipo Wadanganyika watakuja fumbua macho na kujikuta porini!...Na ajabu unaweza kuwasikia Wadanganyia wakisema sisi watalii bwana pori ndiko tunalotaka!
Anyway, kila barabara ina mwisho wake hii ndio slogan ya Kibongo.
 
Kitu cha kushangaza wakati wa vunjavunja ya Magufuli Watanzania wengi tulikuwa tukifurahia ubabe ule.

Katika nchi kama Japan waziri akishindwa kesi, na kuitia serikali hasara, huwa anajiua kwa kunywa sumu. Hapa Tanzania Magufuli ataendelea kungangania madaraka.

Tusubiri tuone kama serikali itakata rufaa, na kushinda.

Vilevile angalieni fidia aliyopata huyo Mfanyabiashara halafu mjiulize Wakili wake anapata kiasi gani? Ndiyo maana mkimlaumu Nimrod Mkono au Maira huwa nacheka tu.

Mahakama yaamru serikali kumlipa mfanyabiashara Sh 15 bilioni

Na Frederick Katulanda, Mwanza

MAHAKAMA imeiamuru Serikali kuilipa kampuni ya Mansoor Oil Industries Ltd (MOIL) ya jijini Mwanza jumla ya Sh14.7bilioni

kutokana na uamuzi uliotolewa na Waziri wa Ujenzi wakati huo John Pombe Magufuli wa kuvunja kituo cha mafuta cha kampuni hiyo.

Uamuzi huo umetolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza katika kesi ya madai namba 2 ya mwaka 2002 ambapo

kampuni hiyo ilikuwa ikiwashitaki Waziri Magufuli, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (wakati huo) Brigedia Hassani Ngwilizi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Andrew Chenge pamoja na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Katika kesi hiyo madai ya kampuni hiyo ya MOIL kwa serikali yalikuwa jumla ya Sh.18bilioni kutokana na kuvunjiwa kituo hicho cha mafuta kilichokuwa kimejengwa katika kiwanja namba 178 Kitalu ‘A’ eneo la Kirumba kando ya barabara ya Makongoro.

Katika madai hayo, kampuni hiyo iliomba kulipwa kiasi cha Sh 593milioni kama thamani ya jengo ambalo lilibomolewa kwa amri ya Waziri Magufuli, Sh13.4 bilioni ikiwa ni kiasi cha faida ambacho ingekipata katika kipindi cha miaka 33 ambacho ilitarajiwa kufanya biashara na Sh 4 bilioni kama hasara ya jumla ya mradi huo.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 30, mwaka huu na Hakimu Mfawidhi H. Mushi kwa niaba ya Jaji Lawrence Mchome, mahakama ilisema baada ya kusikiliza pande zote ikiwa ni pamoja na kupitia vielelezo na ushahidi mbalimbali iliridhika na hivyo kutoa uamuzi kuwa mlalamikaji anapaswa kulipwa fidia katika madai yake.

Katika hukumu hiyo, Mahakama imesema kwamba mdai alikuwa na vibali halali vinavyoruhusu kuendesha shughuli zake katika eneo hilo, na kwa mujibu wa sheria, Rais ndiye alikuwa na uwezo wa kubatilisha vibali hivyo na si waziri.

“Mahakama iliamuru Serikali Kuu kwa niaba ya washitakiwa watatu ambao ni Waziri Magufuli, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (wakati huo) Brigedia Hassani Ngwilizi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Andrew Chenge kulipa fidia kama ifuatavyo.

Kuilipa kampuni hiyo kiasi cha fidia ya Sh 490 milioni badala ya Sh 593 milioni alizoomba, kumlipa Sh13.4 bilioni kama fidia ya faida ambayo angepata katika kipindi cha miaka 33 na kumlipa kiasi cha Sh 730 milioni ambacho ni sehemu ya Sh 4 bilioni, aliyoomba kama hasara ya jumla katika mradi huo wa kituo cha mafuta.

Katika hukumu hiyo, mahakama imemwondoa mlalamikiwa mmoja ambaye ni Halamshauri ya Jiji la Mwanza kwa kuwa hakuhusika na uvunjaji wa kituo hicho.

Pia mahakama imeamuru serikali kumlipa mdai huyo kiasi cha asiliamia 17 ya madai yake ya hasara ya jumla ya Sh730 milioni kwa mwaka tangu siku jengo hilo lilipobomolewa Juni 21, 2001 hadi siku ya hukumu ilipotolewa.

Makahama imeamuru kulipwa kwa mdai huyo tena kiasi cha asiliamia hizo 17 ya Sh13.4 bilioni kwa mwaka ambayo ni madai yake ya hasara kutoka siku jengo lilipobomolewa hadi siku ya hukumu.

Kituo hicho kilibomolewa wakati tayari kikiwa kimekaguliwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kutoa hati ya umiliki wa kiwanja hicho Na. 033005/167 ya muda wa miaka 33 pamoja na hati ya kuruhusu ujenzi wa kituo hicho na Na. 00785.

Katika kesi hiyo MOIL ilikuwa ikitetewa na mawakili Salum Magongo na Paulin Rugaimukamu wote wa jijini Mwanza wakati serikali ilikuwa ikitetewa na mawakili Michael Kamba na Edwin Kakolaki.
 
Jokakuu,
kuhusu hayo malipo ya uwakili usichanganye madawa hapo,serikali inataratibu zake na watu binafsi wanamakubaliano yao.ni sawa kununua kiwanja cha serikali moja kwa moja bei ni tofauti na kununua kiwanja hicho hicho kwa mtu binafsi.

Hapa tuanalie hasara ambayo waziri na watendaji wake wametupa ikiwa na yeye kujiuzuru wadhifawake pamoja na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kulitia hasara taifa.
 
Naona hizi habari ziko mbili. Hii kesi ni ya kutoka 2002 inawezekana kabisa kuna uzembe mahali fulani. Tunaomba mwenye dossier ya hii story atuwekee hapa.
 
Serikali kukata rufaa faini ya mabilioni Mwanza

Frederick Katulanda, Mwanza

SERIKALI imesema kuwa itakata rufani kupinga uamuzi wa mahakama kumlipa fidia mmiliki wa kampuni ya Mansoor Oil Industries Ltd (MOIL) ya jijini Mwanza.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwanasheria wa Serikali Edwin Kakolaki alisema tayari walikwishapeleka ombi la kukusudia kukata rufani tangu Septemba 10 mwaka huu.

Kakolaki alisema uamuzi huo wa kukata rufani umefikiwa kutokana na wao wakiwa watetezi upande wa serikali kutoridhika na uamuzi huo wa mahakama hivyo kutumia haki ya msingi ya kukata rufani.

"Tayari tumeshapeleka ombi hilo la kukusudia kukata rufani, tunachongoja ni kupata nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi ili tuweze kupitia na kubainisha sababu za msingi," alieleza.

Alisema katika sababu yao ya kwanza na ya msingi katika uamuzi wao wa kuamua kukata rufani, wanapinga pia mlalamikaji kulipwa fidia ya Sh 730 milioni kama fidia ya hasara ya jumla.

Katika hatua nyingine mwanasheria huyo alisema kuwa kiasi cha fidia kilichoamuliwa kulipwa ni jumala ya Sh 1.2 bilioni na kusema mahakama ilitupilia mbali fidia ya Sh13.4 bilioni ikiwa ni faida ambayo angekipata katika kipindi cha miaka 33, lakini ilikataliwa na mahakama.

Kutokana na ufafanuzi huo Kakolaki alisema kiasi ambacho serikali inapaswa kuilipa kampuni hiyo kama watashindwa pia katika rufani yao waliokata ni Sh 1.3 bilioni na si Sh15 bilioni kama ilivyokuwa imeripotiwa na gazeti hili jana.

Alisema katika uamuzi huo wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza dhidi ya kesi ya madai namba 2 ya mwaka 2002, kampuni hiyo itapaswa kulipwa fidia ya Sh 490 milioni badala ya Sh 593 milioni alizoomba pamoja na Sh730 milioni ambazo ni sehemu ya 1/5.5 ya Sh4 bilioni aliyoomba kama hasara ya jumla katika mradi huo wa kituo cha mafuta hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa ni Sh1.2 bilioni.

Alisema katika uamuzi wa mahakama fidia ya kesi haikujumuisha na wala haipaswi kujumuishwa kwa vile suala la fidia ya gharama za kesi litasimama kama dai jipya ambalo litapaswa kuthibitishwa na mwombaji mahakamani.

Katika kesi hiyo, kampuni hiyo ilikuwa ikiwashitaki aliyekuwa Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Brigedia Hasani Ngwilizi, Mwanasheria Mkuu wa serikali, Andrew Chenge na Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Katika kesi hiyo kampuni hiyo ilikuwa inadai jumla ya Sh18 milioni kutokana na kuvunjiwa kituo hicho cha mafuta kilichokuwa kimejengwa katika kiwanja namba 178 Kitalu A eneo la Kirumba kando ya barabara ya Makongoro.


Source: Mwananchi
 
Back
Top Bottom