Mhariri
HabariLeo; Tuesday,February 20, 2007 @00:01
STAILI ya utendaji ya John Pombe Magufuli, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, ina mwelekeo wa kuifanya serikali ya awamu ya nne isieleweke kwa wananchi. Baadhi ya maamuzi ya mheshimiwa huyo yanakwenda kinyume na utaratibu wa kuheshimu sheria na wakati mwingine yanakejeli mfumo mzima wa utawala bora.
Katika hali isiyoeleweka, Magufuli inasemekana ameidhinisha utoaji wa hati ya kumiliki ardhi katika eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya akiba ya barabara huko Mikocheni Dar Es Salaam.
Wale wanaolifahamu eneo hilo watakubali kwamba kilichojengwa pale hakikustahili kuwapo.
Kwanza, kuna jengo la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kulikofungwa vifaa vya kudhibiti na kufuatilia mwenendo wa masafa yote ya mawasiliano, kuanzia redio, televisheni na simu za mkononi na upepo ili kusiwe na muingiliano.
Eneo hilo lingehitajika kuwa na ulinzi wa hali ya juu na kutokuruhusiwa kwa aina yoyote ile shughuli za biashara, hasa biashara ambazo zinaendeshwa hadi usiku wa manane. Isitoshe, katika hali ya kejeli na dharau, wamiliki wa eneo ambalo Magufuli amelitolea hati wamediriki kujenga choo ambacho kimeegemea ukuta wa eneo la mitambo hiyo nyeti ya Taifa.Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni wameshalalamikia kuwapo kwa jengo kwenye eneo la barabara.
Manispaa imehoji uhalali wa hatua ya Waziri Magufuli kutoa hati ya kumiliki ardhi kwenye eneo la hifadhi ya barabara. Hivi ni nani anaielewa zaidi wilaya ya Kinondoni kama sio madiwani wake? Nini maana ya serikali za mitaa kama zinaingiliwa na mawaziri ambao hata hawahusiki na sekta hiyo?
Tunajiuliza: hivi si Magufuli huyu huyu aliyeongoza ubomoaji wa kituo cha mafuta kilichojengwa kwenye kile alichokiona kuwa ni hifadhi ya barabara kule Mwanza? Hivi si Magufuli huyu huyu, aliyesimama Bungeni na kumkosoa hadharani Naibu wake, ambaye kwa wadhifa wake wa ubunge ni diwani Kinondoni akimshutumu kuwa emehodhi viwanja? Madiwani wa Kinondoni na Watanzania kwa ujumla wana uhalali wa kutaka umiliki wa eneo hilo la Mikocheni ubatilishwe mara moja ili kulinda hadhi ya serika