MOSSAD: "A" "BE" na "CHE" ya mashetani wenye ithibati ya mauaji

MOSSAD: "A" "BE" na "CHE" ya mashetani wenye ithibati ya mauaji

Kudos mzee unachambua bila bias endelea kutushushia mavitu aisee
Ahsante sana mkuu. Tutaendeleza hiki kitu pasi na shaka. Natumia simu hivyo nitakuwa taratibu kidogo. Ningependa tuwe pamoja.
 
Mkuu uwe unanitag sana. Napenda sana vitu hivi vya Intelijensia.

Sawa Lepalai?
 
the bold kula tano mkuuuu nashukuru unavyokubali machapisho ya wengine hyo ndo njia rahisi ya kujifunza vitu vingine vipya hongereni kwa watu mliochukua muda wenu kutujuza mambo tusioyajua pamoja sana mungu awabariki wote kwenye jukwaa hili
Shukrani zirejee kwako tena mkuu
 
Kumekuwa na haja na kiu kubwa ya baadhi ya watu humu kutaka kuifahamu MOSSAD na kazi zake. Kwa msukumo wa hilo, nimeona si mbaya tukajuzana angalau machache juu ya hawa watu na baadhi ya mifano hai ya kazi zao.


Jiandae kwenye karatasi zijazo kujifunza namna gani tumishi za Israel, zikiongozwa na Mossad, zinavyopambana, usiku na mchana, kulinda nchi yao, na pia kwa ziada nchi za magharibi vilevile.



Kwa muono wa Israel, hawana la kupoteza kwenye vita yoyote ile. Hawana chaguzi nyingi zaidi ya kushinda kila muda. Lolote litafanyika kuhakikisha hilo. Na nadhani mimi na wewe twaweza kuwa mashahidi kwenye hili. (Rejelea vita kubwa ya mataifa kadhaa ilivyomalizwa na taifa la Israel ndani ya siku sita tu, watu wakaomba poh!)



Siku za migogoro zaja. Iran anaweza jaribu kufanya kitu fulani kwa mujibu wa nguvu yake kinyuklia; magaidi pia waweza jaribu kufanya jambo hatarishi, au vyote kwa pamoja vikatukia. Raisi wa Marekani, kwa uhakika kabisa, atauliza;
"Kipi Israeli wanasema juu ya hili? Kipi wanajua? Ni nini wanachodhamiria kufanya ambacho sisi hatukifahamu?"
Na mwishowe;
"Nini Mossad watafanya? (Kupanga, kutekeleza, ama vyote)."
Marekani ni taifa kubwa, sina haja ya kuelezea kwenye hili. Kijografia huwezi ukailinganisha na Israeli hata kidogo, nchi ambayo itakulazimu uwe na microscope ili upate kuiona kwenye ramani ya dunia.



Kitendo cha nchi kubwa kama Marekani, kijografia na kiuchumi, kuiulizia Israeli, ni jambo la kufikirisha kichwa. Lakini pia la kutufumbua macho kwamba kuna kitu ndani ya Israel; Kuna kitu cha kurejelea Israel; Kuna kitu cha kukitazama ndani ya Israel; kuna kitu cha kuhofia ndani ya Israel.
Na si kingine, hata kama kuna kingine basi kinazungukia hapa, kwenye taasisi nyeti ya kijasusi ya Mossad. Taasisi ambayo kwa mujibu wangu naweza sema ndiyo taasisi bora zaidi ya kijasusi kuwahi tokea duniani, hapa hatuhitaji kubishana.



Kama vile sanamu la uhuru (statue of liberty) pale Marekani ama McDonald zilivyokuwa majina ya uwakilishi wa nchi hiyo kubwa, basi Mossad imekuwa ikitambuliwa kama "brand name" ya taifa la Israel. Hakuna Israel bila Mossad.
Shirika hili la kijasusi limekuwa kiungo kikubwa sana, japo kwa maficho, kwenye mambo mengi yanayotukia kwenye muda wetu, haswa mashariki ya kati.



Lakini tusisite kujiuliza, Hivi Mossad ni wazuri kiasi hiki, cha kusemwa, kuogopwa, na kuongelewa?
Ndani ya zaidi ya miaka sitini, shirika hili la kijasusi la Israel limefanya pia makosa. Kufanikiwa ama kushindwa kwake kulitokana na ubora na ufanisi wa watu wake kazini. Wanapewa motisha. Lakini haibadilishi dhana kwamba na wao ni binadamu, hivyo hukosea ama kushindwa.



Jina kamili la shirika hili la kijasusi ni HaMossad l’Modi’in u’l’Tafkidim Meyuchadim, kiebrania kinachomaanisha shirika la ujasusi na kazi maalum. Shirika hili lina wafanyakazi elfu ndogo, na katika muda mfupi hapo nyuma lilijipambanua kiasi kidogo kwa hadhira kwa kutumia tovuti ya Mossad.gov.il likienenda na motto rasmi usemao;
"Pale ambapo hamna shauri (counsel), watu huanguka; lakini penye wingi wa washauri (counselors) pana usalama."
Motto huu ulitoholewa toka kwenye biblia, Methali 11:14. Mstari huo ukisema;
"Pasipo na ulinzi (guidance), taifa huanguka; ila penye washauri wengi pana usalama."



Lakini basi, je pana shaka lolote kuhusu motto huo? Aidha twaweza sema kwamba kwakuwa umetoholewa kwenye Biblia, basi dhamira yaweza kuwa njema, safi na yenye utukufu. Ila Mossad je, walidhamiria vivyo?
Neno "counsel" kwa lugha ya kiebrania hutafsiriwa kwa neno "takhbulot." Neno hili halina maana moja (ambigious word). Humaanisha maana kadhaa kama zifuatazo; ulaghai (deception), ujanja ujanja (trickery), mbinu (stratagem), au mwelekeo wenye hekima (wise direction). Hivyo basi kutokana na maana hizi tunashindwa haswa kujua dhamira halisi ya Mossad ndani ya motto huo. Kwani yaweza pia maanisha:


"Bila ya ujanja ujanja, Israel itaanguka ..."


Ama,


"Bila ya mbinu, Israel itaanguka ... "


Au,


"Bila ya ulaghai, Israel itaanguka ... "


Nani anajua?


Aliyewahi kuwa kiongozi (director) wa Mossad, bwana Efraim Halevy aliwahi kusema kwamba motto mwingine wa Mossad ungeweza kuwa;


"Kila kitu kinawezekana (kufanyika)." "Everything is do-able." Msukumo huu ndio ambao umekuwa ukiwasukuma Mossad, wakiamini kila kitu kinawezekana. Udogo wa nchi yao hauwazuii kwa njia yoyote ile wala kuwafanya wadhaifu.
Mbele ya macho yao (Mossad) kila kitu chao kina faida; kuanzia udogo wa nchi yao, upungufu wa wafanyakazi wao n.k



Heshima ya shirika hili la kijasusi kwenye kufanya maamuzi ya tija, na kufanya shughuli zilizozidi hata ufanisi, imepelekea mambo makubwa kujiri; wana nguvu, wanajua karibia kila mambo, katili na wanaweza kupenya kona yoyote ya ulimwengu.
Israel wanaweza wakawa wamelitengeneza hili pasipo kujua, ila mpaka sasa wananufaika nalo. Pale ambapo jambo kubwa limetokea. Vyombo vya habari vikiwa vinabweka huku na huko wakitaja jina la Mossad, wakilituhumu ama kulipongeza. Hawa majasusi (Mossad) hawatii hata haladari ya neno. Hali hii ikajenga hofu ndani ya mioyo ya maadui zao, kwani hata pale Mossad wanapokuwa hawajahusika, bado hawabakizwi kutotajwa.



Lakini wahenga na washenga walishawahi sema; "avumaye baharini papa lakini si kwamba wengine hawamo."



Unapoongelea ujasusi wa dunia nzima, au haswa wa Israel, jina la kwanza kuja ni Mossad. Ila hawa hawafanyi kazi peke yao, na hata kwenye mafanikio hayo kuna mchango pia wa shirika lingine pacha "Domestic Shin Bet" ama kwa jina lingine hujulikana kama Shabak. Shirika hili uhusika sana na ulinzi wa ndani (internal/domestic affairs) ya taifa la Israel. Lakini pia juu ya hizi shirika, kuna 'mama' aendaye kwa jina la "Military - Aman", ama kwa kifupi; Aman.
Miongoni mwa hizi ogani tatu, zenye kuhusiana, Military Aman ndiyo yenye rasilimali kubwa kifedha na hata kinguvu kazi na ndiyo ambayo imechangia usalama wa Israel kwa kiasi kikubwa sana.



Lakini pia mbali na hapo, katika mwendelezo wetu huuhuu tutapata nafasi ya kufunua vijisehemu vidogovidogo vya ulinzi wa siri (clandestine defense) wa nchi ya Israel, mbali na Mossad. Aidha utakuwa hauvifahamu vijishirika hivi, au basi kama wavifahamu basi si kiundani. Moja; ni ile inayoitwa ujasusi wa kiyahudi "Jewish Intelligence", ambayo hii husaidia wayahudi kuendesha ama kusimamia haki ya kisheria ya Israel kurejea kwenye ardhi wanayoamini wao kuwa ni ya mababu zao (ancients), ambapo huko hupewa uraia - lakini pia huendelea kuwalinda dhidi ya matamko, miongozo na nguvu za mataifa ama oganaizesheni kubwa za kimataifa kuligusa ama kutishia uwepo wa taifa hilo.



Kijishirika kingine kidogo kilikuwapo kwa minajili rasmi ya ushirikiano wa karibu sana wa kisayansi "science liaison", ambacho husemekana kilifutwa baada ya jasusi; Jonathan Pollard kukamatwa akiwa anaipeleleza Marekani mwaka 1985. Kijishirika hiki kilifanikiwa sana kitunza siri za nguvu ya kisayansi ya Israel ikiwamo nyuklia, na taarifa zingine za kisayansi ambazo mpaka sasa hatuzijui, na ambazo mpaka sasa hazijathibitishwa na serikali ya Israel.




MEZA MATE ... HAYA, TUANZE TARATIBU...




Taifa la Israel limekuwa vitani tokea kipindi David Ben-Gurion alipotangaza utaifa wa jamii hiyo mnamo mwaka 1948. Na viongozi wa Israeli bado wanajichukulia wapo vitani kila siku. Lakini 'vita' hii siyo ile ya utaifa (1948), wala ile ya siku sita za mapambano (1967). La hasha! Jumuia zao za kijasusi zinataka kuhakikisha kwamba haitokuja kujirudia yale ya vita ya Yom Kippur, ama vita ya Ramadan (1973), ambapo shambulizi la ghafla la waarabu (Egypt na Syria), kama lipizo la vita ya siku sita (six days war), lililoigharimu nchi ya Israel, lingeweza kuzuiwa endapo kama majasusi waliopandikizwa nchini Misri wangepata kutiliwa maanani.
Kama ilivyo kazi ya taasisi ama shirika lolote la kiusalama, kazi yao ya kwanza si kupambana vita, bali ni kuzuia vita ama basi kuimaliza vita kabla ya 'kupambana vita'.


Kumuacha adui aanze kurusha kombora ni hatari sana kwani huwezi jua hilo kombora lina uwezo gani, laweza kukusambaratisha ama kukupoteza kabisa kwenye uso wa dunia. Na hapa Mossad ndio wanahangaika usiku na mchana kuhakikisha adui haanzi, bali anaanzwa na kumalizwa ikilazimika. Lengo ni ushindi tu, kuharibu ama kuchelewesha mipango ya adui bila ya kuhatarisha usalama wa wanajeshi lukuki na rasilimali ama wananchi wa Israel.



HARAKATI KAZI ZA MOSSAD; MISHENI YA KWANZA. MPELELEZI NYUMA YA KINYAGO CHA CHUMA.



Makazi ya watu wenye uwezo nje ya kitongoji cha Afeka kaskazini mwa Tel Aviv, yalikuwa yanatumika kumtazamia mwanaume ajulikanaye kwa jina la Rafael “Rafi” Eitan. Mwanaume mzee, mwenye uono hafifu na pia kiziwi wa sikio lake moja la kulia tangu apambane katika vita ya uhuru wa Israel.
Muonekano wake wa kimavazi ambao haupendezi machoni, huwafanya majirani zake kuamini kwamba ni mojawapo ya njia ya mwanaume huyo kuyakwepa, kiakili, yale mambo ya kikatili aliyowahi kuyafanya. Majirani hawa wanajua wazi bwana Rafi aliua watu kadhaa kwa ajili ya nchi yake (Israel), lakini si kwenye uwanja wa wazi wa vita (open battle) bali kwenye uwanja wa siri (secret battle) ambao ndio uwanja pendwa kwa Israel, uwanja wenye vita isiyokoma dhidi ya maadui zake.
Hakuna jirani anayejua haswa idadi ya watu waliouawa na Rafi, aidha kwa silaha ama kwa mkono wake wenye nguvu. Yale yote aliyokuwa anasema bwana huyo (Rafi) kwa majirani zake ni kwamba;
"Punde nilipotaka kuua, nilitaka kuyaona macho yao, uweupe wa macho yao. Basi nilikuwa mtulivu sana na mwenye mwongozo, nikifikiria kile tu ninachotakiwa kufanya. Alafu nikafanya. Hivyo ndivyo ilivyokuwa."



Maneno hayo alikuwa akiyaambatanisha na tabasamu, tabasamu ambalo unaweza ukalifananisha na la mtu mwenye nguvu aliyedhamiria kumtisha mdhaifu.



Kwa karibu robo karne, Rafi amekuwa naibu kiongozi wa harakati za Mossad. Sio kwa kukaa nyuma ya meza akisoma ripoti na kutuma wemgine kufanya kazi. Kwa kila fursa iliyotokea, alienda kwenye uwanja wa mapambano, alikuwa mbele akiwa anaongozwa na falsafa aliyofanikiwa kuifupisha ndani ya sentensi moja isemayo; "Kama wewe si sehemu ya jibu, basi ni sehemu ya tatizo."
“If you are not part of the answer, then you are part of the problem.”




Hakukuwahi kuwapo kama yeye (Rafi) kwa ukatili usio na huruma hata punje (cold-blooded ruthlessness), mipango ya ulaghai na ushawishi, na uwezo wa haraka mno wa kuandaa jambo ghafla. Ujuzi wa kupanga, na kutochoka kwenye ufwatiliaji wa mlengwa wake. Sifa zote hizo zilikuja kwake kwenye oparasheni moja tu iliyompa umaarufu mkubwa usiokoma kwenye nyanja ya ujasusi. Oparasheni hiyo si nyingine bali ni ile ya kumteka kiongozi mkubwa wa utawala wa ki- Nazi, Adolf Eichmann, ambaye ni mojawapo wa wahusika wa maamuzi ya mwisho yaliyotolewa na Adolf Hitler ya kuwaua Jews (6 million).



Kwa majirani zake (Rafi) kwenye mtaa wa Shay, Rafi ni mfano mtakatifu, mwanaume aliyelipiza kisasi cha ndugu zao waliokufa, mwanaume mpiganaji aliyepewa fursa ya kuukumbusha ulimwengu kwamba hakuna kiongozi yeyote wa Nazi aliye salama baada ya kuwaangamiza watu milioni sita.
Hawachoki (majirani) kutembelea nyumba ya Rafi na kumsikiliza tena na tena akielezea oparasheni ambayo bado inatikisa kwa uthubutu wake.



Akiwa amezungukwa na vitu vya thamani, Rafi angefungua mikono yake yenye misuli na kukaa kimya kwa muda, akiwaruhusu wasikilizaji wake wazame fikirani kipindi kile taifa la Israel linazaliwa. Alafu kwa sauti yenye nguvu, pasipo kuacha kitu, alianza kuwaambia majirani zake hao namna gani alipanga kumkamata Adolf Eichmann.
Kwanza, alitengeneza mazingira mazuri mno ya kuelezea simulizi yoyote ya utekaji nyara kwa muda wowote.



Baada ya vita vya pili vya dunia, zoezi la kuwafuatilia wahusika wa mauaji ya Jews lilianza kufanywa na wale walionusurika na mauaji hayo. Walijiita "Nokmin" wakimaanisha walipiza kisasi. Hawakujisumbua kufuata mfumo wowote wa kisheria, wao walikuwa wanamnyonga mhusika yeyote wa Nazi waliyemtia mikononi.



Rafi Eitan hajui wala hakumbuki kama kuna mahali popote walipowahi kumuua mtu asiyestahili kufa.
Lakini liwekwe rasmi kwamba, ndani ya Israel kulikuwa kuna haja hafifu sana ya kuwatafuta wahusika wa mauaji ya watu wao. Lilikuwa ni jambo la kipaumbele. Kama taifa, Israel walikuwa bado wachanga, tena wakizungukwa na mataifa adui ya kiarabu. Walikuwa na mambo mengi kwanza ya kuyazingatia kabla ya hilo, ila si kwamba walikuwa wamelipuuza. La hasha! Taifa la Israel lilikuwa mlemavu, lisilo na nguvu, na kama vile linapotea baada ya siku moja mbele.



Ndani ya mwaka 1957, Mossad walipokea taarifa za kusisimua kwamba Adolf Eichmann, ameonekana nchini Argentina. Rafi, ambaye alikuwa ni nyota inayong'aa kutokana na ufanisi wa kazi zake dhidi ya waarabu, aliteuliwa kwenda kumkamata Eichmann na kumleta Israel kwa ajili ya kupewa anachostahili.



Rafi aliambiwa oparasheni hiyo itakuwa na faida lukuki endapo ikitimia. Itakuwa ni hatua moja takatifu kwa watu wake kueleka kutendewa haki dhidi ya kile walichofanyiwa na wa -Nazi. Itaikumbusha ulimwengu wa kambi za vifo (death camps) na uhitaji wa kuhakikisha jambo kama lile haliji kutokea tena duniani. Lakini mwisho ni kwamba itaifanya Mossad kuwa mbele ya shirika zote za kijasusi ulimwenguni.



Hakuna tumishi yoyote ya kijasusi ambayo ingethubutu kufanya oparasheni kama hiyo. Hatari yake ilikuwa ni kubwa mno. Rafi atafanya kazi maelfu ya maili toka nyumbani, atatumia dokumenti za kufoji, na kutegemea kwa kiasi kikubwa rasilimali zake mwenyewe kwenye mazingira adui. Argentina ilikuwa ni mahala salama kabisa kwa wa - Nazi, hivyo wana - Mossad wangeweza kukamatwa, kufungwa na mwishowe hata kuuawa punde tu wakigundulikana.



Kwa miaka mirefu miwili, Rafi Eitani kwa uvumilivu alingojea wakati kuonekana kwa mara ya kwanza kwa Adolf Eichmann kunathibitishwa kwamba mwanaume huyo alikuwa yupo katikati ya kitongoji cha watu wa daraja la kati Buenos Aires akitumia jina la Ricardo Klement.
Pale amri ya mwisho ya kufanya tukio ilipotoka (go order), Rafi alikuwa 'barafu.' Alishafanya mafikirio yake yote juu ya nini kinaweza kikaenda kombo. Kisiasa, kidiplomasia, na kwake pia bila kusahau madhara yatakayofuata baadae.



Alijiuliza nini kitatukia akimkamata Eichmann na polisi wa Argentina wakaingilia ama kumzuia?
"Niliamua nitamnyonga kwa mikono yangu mpaka afe. Kama nikikamatwa, nitasema mahakamani kwamba nimefuata maneno ya biblia; jino kwa jino." Alisema Rafi.



El Al, shirika la ndege la taifa, ambalo ndege yake (hii iliyotumika) ilitoka kwenye shirika la kutengenezea ndege la Uingereza huku pesa ikitoka mfukoni mwa Mossad, ndilo lilimsafirisha Rafi kwenda Argentina. Rafi alisema;
"Tulimtuma mtu Uingereza akanunue moja. Alitoa pesa tukapewa ndege."
Lakini rasmi ndege hiyo iliyoelekea Argentina ilikuwa ni kwa ajili ya kubebelea maafisa wa ki Israel waliolenga kuwasili kwenye sherehe ya maadhimisho ya uhuru wa Argentina (115th). Hakuna afisa hata mmoja aliyekuwa anajua kwanini walikuwa wanaongoza na wao (Rafi na wenzake), na wala hawakuwa wanajua kama ndani ya ndege hiyo kulikuwa kuna chumba mahususi cha kumuhifadhia Adolf Eichmann.



Rafi na timu yake walifika Buenos Aires May mosi, 1960. Walichukua nyumba moja iliyokodiwa na mkubwa wao, ambaye alipewa kificho (code) cha kiebrania "Maoz". Na mahali hapo ndipo palikuwa mahususi kama eneo la kuendeshea oparesheni yao. Walitengeneza pia mahali pengine maalum kwa ajili ya kumtunzia Adolf Eichmann baada ya kumkamata. Nyumba zingine pia zilikuwepo lakini mahususi kwa ajili ya kukabiliana na presha ya msako inayoweza kutokea toka kwa polisi wa ki Argentina. Pia magari kadhaa yakaandaliwa kwa ajili ya kazi.




Kila kitu kikiwa sawa, Rafi alitulia na kuzingatia. Shaka lolote lingeweza kupelekea wao kushindwa, lilikuwa limekabiliwa na sasa msukumo mkubwa ukawa kwenye kungojea.
Kwa siku tatu, Rafi na timu yake walifanya upelelezi kumfatilia Adolf Eichmann, ambaye awali alikuwa akiendeshwa ndani ya gari refu Mercedes limousine. Sasa siku hiyo Adolf Eichmann alikuwa anasafiri kwa basi na alishuka kwenye kona ya mtaa wa Garibaldi.



Usiku wa siku hiyo, May 10, 1960. Rafi alikuwa ndani ya gari akiwa na dereva mwenye mafunzo ya kutosha, pamoja pia na mmojawapo wa wanaume wenye uwezo wa kumtageti mtu wanayemtaka mtaani. Yeye (Rafi) alikuwa pembeni ya dereva tayari kusaidia lolote litakalotokea. Walipopata walichokuwa wanakihitaji waliondoka wakilenga kufanya oparesheni jioni ya kesho yake.
Kwenye majira ya saa mbili usiku May 11, gari lililobebelea timu ya Rafi liliwasili kwenye mtaa wa Garibaldi. Hakuna yeyote aliyekuwa na presha. Hakuna yeyote aliyeongea. Hakukuwa na kitu cha kuongea bali kutenda. Rafi alitazama saa yake ya mkononi, saa mbili na dakika tatu. Walisogeza gari mpaka eneo fulani pweke.



Mabasi kadhaa yalikuja na kuondoka. Kwenye majira ya saa mbili na dakika tano, basi lingine likaja. Wakamuona Eichmann akishuka.
"Mtaa bado ulikuwa mtupu. Nyuma yangu nilimsikia mtaalamu wetu wa ukamataji (snatchman) akifungua mlango wa gari. Tuliendesha gari taratibu kumfuata Adolf Eichmann. Alikuwa anatembea haraka kama mtu anayewahi chakula cha usiku nyumbani. Nilimsikia mkamataji mtaalamu wetu akihema taratibu, namna alivyofundishwa mafunzoni." Alisema Rafi.



"Alikuwa ana sekunde kumi na mbili tu za kufanya tukio. Kutoka ndani ya gari, kukamata shingo ya Eichmann na kumvutia ndani ya gari kisha tuondoke upesi!"



Gari lilisonga karibu na Eichmann, aligeuka nusu kumtazama mtaalamu wetu aliyekuwa anashuka toka kwenye gari, ambaye hakufika mbali kabla ya kudakwa na kamba ya kiatu iliyokuwa haijafungwa vizuri. Nusura imwangushe.



Kwa huo muda Rafi alitamani ashuke akamalize kazi. Alitoka karibia nusu ya dunia mpaka kufika pale kwa ajili ya kumkamata mtu anayehusika na kifo cha watu milioni sita wa nchi yake, na sasa walikuwa wanaelekea kumpoteza kwa sababu ya kamba za viatu! Eichmann aliongeza mwendo, ni kama alishajua yupo kwenye mazingira hatarishi. Akianza kutupa miguu yake, Rafi aliruka toka kwenye gari.



"Nilimdaka shingo kwa nguvu ambayo kama ningeiongeza kidogo tu basi ningemuua. Macho yake yalitoka nje. Mtaalamu wetu alifungua mlango upesi, nikamrushia Eichmann viti vya nyuma, haraka mtaalamu naye akajitupia humo ndani na kuketi juu ya nusu ya mwili wa Eichmann. Tukio hilo lilidumu kwa sekunde tano tu!"
Toka kwenye siti ya mbele, Rafi alikuwa anasikia Eichmann akihangaika kuhema. Mtaalamu wao alikuwa amemdhibiti mwanaume huyo vema kiasi kwamba kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele, alizidi kuwa mpole zaidi. Ilifikia mahali akauliza nini ilikuwa maana ya kile anachofanyiwa.



Hakuna aliyemjibu. Kwa ukimya walifika kwenye nyumba salama iliyoko umbali wa maili tatu toka eneo la tukio. Rafi alimtaka Eichmann avue nguo kisha akamkagua akitazama vipimo vya kifizikia vya mwanaume huyo kama kweli ndiye. Rafi hakushangazwa na hali ya kutokuta tattoo ya SS (Schutzstaffel) mwilini mwa mwanaume huyo kama ilivyokuwa kwa wa - Nazi wengine, ilikuwa imeondolewa. Lakini vipimo vingine vyote vilikuwa sawa kabisa. Walimfungia Eichmann kitandani kwa pingu. Kwa masaa kumi wakamwamcha mwanaume huyo gizani pasipo na sauti yoyote.



"Lengo lilikuwa ni kuchochea hisia za kukosa matumaini ndaniye. Mpaka asubuhi tayari Eichmann alikuwa yu mnyong'ofu kiakili. Nilimuuliza jina lake akanitajia la kihispania ... Nilisema hapana, hapana, hapana, jina lako la kijerumani, akataja jina alilotumia kukimbilia nalo huko Ujerumani, nikasema tena hapana! Nataka jina lako la ukweli, jina lako la SS. Alijinyoosha kitandani kisha akasema kwa nguvu akisikika 'Adolf Eichmann'. Sikumuuliza tena, sikuwa na hitaji hilo."



Kwa siku saba zilizofuata, Eichmann alikuwa bado gizani. Alikula na kulala gizani. Hakuna yeyote aliyemuongelesha.



"Kumuweka kimya na gizani kilikuwa ni zaidi ya matakwa ya oparesheni. Hatukutaka kumwonyesha Eichmann namna tulivyokuwa na hofu kwani hilo lingempa matumaini. Na matumaini humfanya asiye na matumaini kuwa hatari. Nilihitaji ajisikie hana msaada wowote kama vile watu wangu walivyokuwa kabla ya kupelekwa kuteketezwa kwenye kempu za vifo." Anaeleza Rafi.




**Siku ya kumsafirisha Adolf Eichmann.**



Kwanza Eichmann alivalishwa nguo za wafanyakazi wa ndege ya El Al, ambazo nguo hizo zililetwa na Rafi toka Israel. Alafu alinyeshwa chupa nzima ya Whiskey na kumwacha katika hali ya kulewa chakari.
Rafi na timu yake walivalia suti zao na kidogo wakanywa Whiskey. Walimvalisha Eichmann kofia ya shirika la ndege na kumweka kwenye viti vya nyuma.



Rafi aliendesha gari mpaka kwenye kambi ya jeshi huko ambapo ndege ilikuwa inawangojea, injini tayari zikichemka. Katika geti la kambi hiyo ya jeshi, gari likasimamishwa na wanajeshi wa Argentina. Kwenye viti vya nyuma Eichmann alikuwa anakoroma.


"Gari lilikuwa linanuka kama kiwanda cha pombe. Tulijifanya kama Jews walioparamia na kushindwa kuendana na vinywaji vikali vya ki-Argentina. Wanajeshi wale walifurahishwa na hilo jambo, hawakumtazama Eichmann mara mbili." Anaeleza Rafi.



Ikiwa ni saa sita kasoro tano siku ya tarehe 21, May 1960, ndege iliacha ardhi ya Argentina huku Adolf Eichmann akiendelea kukoroma, sasa akiwa katika chumba chake mahususi ndani ya ndege.



Baada ya kusikikizwa kwa urefu kwa kesi yake (Adolf Eichmann), alikutwa ana makosa dhidi ya ubinadamu. Kwenye siku yake ya kunyongwa, May 31, 1962, Rafi alikuwa kwenye chumba cha unyongaji.



"Eichmann alinitazama na kusema 'muda wako unakuja, myahudi', nikamjibu, 'lakini sio leo, Adolf, sio leo.



Shingo yake ilimezwa na kitanzi, Eichmann akatoa sauti ndogo sana ya kukabwa. Kisha kukawa kunasikika sauti ya mwili wake tu ukibembea. Sauti ya kuridhisha sana." Anasema Rafi.



Jiko maalum liliandaliwa kwa ajili ya kuuchoma mwili wa Adolf Eichmann. Ndani ya masaa majivu yake yalimwagiwa baharini ndani ya eneo kubwa. Hakikutakiwa kibakie kiashiria chochote cha Adolf Eichmann juu ya uso wa dunia.
Baada ya hapo, jiko lililomchoma liliharibiwa na kutotumika tena. Jioni hiyo Rafi alisimama ufukweni na kutazama bahari, akijisikia amani kabisa.



"Kumaliza kazi yangu, hilo siku zote ni hisia nzuri."




Tutaendelea na visa vya MOSSAD moja baada ya moja ... karibu..
Tunaitaji mossad yetu kuwamaliza mafisadi
 
Nazipenda hizi simulizi mkuu ukileta nyingine unishitue zinapendeza sana kuwaona Israel wakiwa ktk kiwango cha juu kabisa ktk uwezo wao

Ila naona kwa sasa Irani ni kitisho chao kikuu.
 
Leo kwenye bbc news. Hamass wanaituhumu MOSSAD kwa kumuua engineer wao wa kutengeneza mabomu, huko tunisia. Siku ya alhamis na wamepanga ku-revenge.
 
Back
Top Bottom