KATIBA ni msingi mkuu wa uendeshaji wa nchi na hii ni sheria mama katika nchi au jumuiya yoyote, kwa kawaida sheria nyingi za nchi zinatungwa kwa mujibu wa katiba. Wapo wanaoitafsiri sheria kama mkataba kati ya watawala na watawaliwa, kwa hiyo katiba ni nyaraka muhimu inayotoa dira ya nchi kwa kuamsha mamlaka ya nchi na vyombo vingine vya kuendesha nchi.
Katiba za nchi nyingi zinazoendelea zinahusiana na nchi za kikoloni kwa karibu sana, vivyo hivyo Katiba ya Tanzania. Baada ya Ujerumani kushindwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika kama ilivyojulikana wakati huo, iliwekwa chini ya usimamizi wa ushirika wa mataifa na baadaye kama mdhamini chini ya Umoja wa Mataifa.
Historia ya Katiba ya Tanzania
Katiba ya kwanza ya Tanzania ilijulikana kama Katiba ya Uhuru ya mwaka 1961 (Independence Constitution).
Hii ni Katiba iliyodumu kwa mwaka mmoja tu, yaani kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 1962, ambapo Tanzania ilipata katiba mpya, iliyojulikana kama Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1962.
Hii ndiyo Katiba iliyotambua Tanganyika kama Jamhuri, vilevile ilipunguza kwa kiasi kikubwa madaraka ya Bunge kama yalivyotolewa na katiba ya uhuru. Mnamo mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 1965, nchi ilipata katiba mpya iliyotambulika kama katiba ya muda ya mwaka 1965 (Interim Constitution 1965). Lengo na dhumuni ya katiba hii ilikuwa ni kuongoza kwa muda tu na kuipisha katiba ya kudumu.
Hata hivyo, kinyume na madhumuni hayo, katiba hii ilidumu kwa muda mrefu zaidi, yaani miaka kumi na mbili, mpaka mwaka 1977.
Mwaka huo wa 1977 ndipo Tanzania ilipopata katiba ya kudumu. Hii ndiyo inayoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, iliyotungwa na Bunge maalumu la kutunga katiba.
Katiba hiyo ilitungwa na kamati ileile iliyotumika kuunda katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama ilivyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Machi 16 mwaka 1977, iliyooongozwa na hayati Thabit Kombo.
Tarehe hiyo hiyo ndiyo rais aliteua Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa hakika, zoezi zima la kuijadili na kuipitisha katiba hii halikuhusisha wala hakukuwa na majadiliano na wananchi.
Haki za binadamu katika katiba hii
Haki za binadamu ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi na ustawi wao na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa wananchi walio wengi wa nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, suala la haki za binadamu kuwapo katika katiba si suala la msingi na halipewi uzito unaostahili.
Hivyo basi, ni muhimu sana kwa suala hili kujadiliwa kwa sababu ni vigumu kwa wananchi kudai haki zao endapo hazikuanishwa katika katiba na sheria za nchi.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilipitia mabadiliko mbalimbali, miongoni mwa mabadiliko hayo ni yale yaliyofanywa na sheria namba 8 ya mwaka 1975, ambayo yalikigawia chama tawala madaraka makubwa sana juu ya serikali.
Hakukuwa na mfumo wa kudhibitiana kwa dhati kati ya vyombo vikuu vya dola na hii ilileta mkanganyiko mkubwa sana, kwani watu walewale waliofanya maamuzi katika chama ndio haohao waliokuja kuhakikisha maamuzi hayo yanatekelezwa upande wa serikali.
Mkanganyiko huu na mengineyo ulisababisha mahitaji makubwa ya tamko la haki za binadamu katika katiba yetu.
Hivyo ni sahihi kusema kwamba katiba na sheria za nchi hazitoi haki hizi bali inazitambua tu.
Wakati huo, katiba wala sheria za Tanzania hazikuzitambua haki hizi, bali kilichofanyika ilikuwa ni kuziweka haki hizo katika utangulizi/ dibaji (preamble) ya katiba hiyo.
Kisheria, jambo hili lilikuwa na athari hasi, kwani kisheria sehemu hiyo si sehemu ya katiba au sheria yoyote ile.
Kwa maana hiyo, mwananchi yeyote ambaye haki yake ingekiukwa na chombo chochote cha dola, au mtu yeyote asingeweza kudai haki yake hiyo/hizo katika chombo cha kudai haki kama mahakama.
Kwa takriban miaka mingi tangu Tanganyika (Tanzania Bara) ipate uhuru mwaka 1961 sehemu inayotambua haki hizo haikuwepo.
Kupitia mabadiliko ya katiba ya mwaka 1984 yaliyofanyika chini ya sheria namba 15 ya mwaka 1985, kwa mara ya kwanza Haki za Binadamu ziliingizwa rasmi katika katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Haya yalikuwa ni matunda ya wadau wa sekta mbalimbali kama wahisani, mashirika yasiyo ya kiserikali na jumuiya ya kimataifa.
Haki hizi hata hivyo zilianza kutumika mwaka 1988 na katika katiba hii haki na wajibu wa wananchi uko katika sehemu ya tatu ya katiba.
Sehemu hii inaanzia ibara ya 12 hadi ibara ya 29. Miongoni mwa haki hizi ni pamoja na haki ya kuwa hai, haki ya uhuru wa mawazo, haki ya kufanya kazi, haki ya uhuru wa mtu kwenda atakapo na haki ya usawa.
Vilevile wajibu kwa wananchi upande mwingine umewekwa ili mwananchi aweze kupata haki yake, kwa maana hiyo ni kwamba Hakuna haki pasipo na wajibu.
Kwa mfano, katika ibara ya 25 ya katiba hii kila mwananchi amepewa wajibu wa kushiriki kwa kujituma kwa uaminifu na katika kazi halali na ya uzalishaji mali. Hata hivyo, kwa mujibu wa ibara ya 30 ya katiba hii, kuna mipaka kwa haki na uhuru ambazo katiba imezitambua, miongoni mwa mipaka hiyo ni pale haki hizi katika utekelezaji wake zitakapoingilia uhuru na haki ya mtu mwingine au kama itaingilia masilahi ya umma.
Hata hivyo, neno: Masilahi ya umma halijatafsiriwa na mara kadhaa linaweza kutumiwa kwa maana pana, ikiwa pamoja na kuhalalisha matendo ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
News Archives - The Free Media of 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀