Katiba nyingi nilizowahi kusoma huwa hazitoi definition ye terminologies kama inavyofanyika kwenye sheria na mikataba; katiba ya Tanzania pia haina definition yoyote.
Ibara ya 151 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 ina tafsiri (definitions) mbalimbali kama ifuatavyo:
151. Ufafanuzi Sheria Na. 14 ya 1979 ib. 13; 1 ya 1980 ib. 17; 15 ya 1984 ib. 52 na 53; 4 ya 1992 ib. 38; 3 ya 2000 ib. 19; T.S. Na. 133 la 2001
(1) Katika Katiba hii, ila iwapo maelezo yahitaji vinginevyo–
"amri ya jeshi" maana yake ni sheria au amri iliyotolewa kwa mujibu wa sheria, ya kusimamia nidhamu katika jeshi;
"askari" likitumika kuhusiana na jeshi lolote maana yake ni pamoja na askari yeyote ambaye kwa mujibu wa amri ya jeshi hilo ni mtu anayewajibika kinidhamu;
"Baraza la Wawakilishi" maana yake ni Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lililotajwa katika ibara ya 106 ya Katiba hii na linalotekeleza madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii na Katiba ya Zanzibar, 1984;
"Bunge" maana yake ni Bunge la Jamhuri ya Muungano lililotajwa katika ibara ya 62 ya Katiba hii;
"Chama cha Siasa" maana yake ni chama cha siasa kilichoandikishwa kikamilifu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992; *
"Idara ya Mahakama" maana yake ni kama ilivyofafanuliwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 116 ya Katiba hii;
"Idara ya Mahakama ya Zanzibar" maana yake ni Idara ya Mahakama inayojumlisha mahakama zote ambazo ziko katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
"Jaji Mkuu" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani aliyetajwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara ya 118 ya Katiba hii ambaye ameteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (2) ya ibara hiyo ya 118 au iwapo Jaji Mkuu hayupo au anashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, Kaimu Jaji Mkuu aliyeteuliwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (4) ya ibara hiyo ya 118 ya Katiba hii, na kama Kaimu Jaji Mkuu naye hayupo au anashindwa kutekeleza kazi za Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyepo kazini kwa wakati huo na ambaye yuko kwenye daraja la juu zaidi la madaraka kupita Majaji wote wa Rufani waliopo;
"Jaji Mkuu wa Zanzibar" maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar ambaye, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar 1984, ndiye Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Zanzibar;
"Jeshi" maana yake ni jeshi lolote kati ya majeshi ya ulinzi na ni pamoja na jeshi lolote jingine lilioundwa na Katiba hii au kwa mujibu wa sheria na linalotawaliwa kwa amri ya jeshi;
"Jumuiya ya Madola" maana yake ni jumuiya ambayo wanachama wake ni Jamhuri ya Muungano, Uingereza na kila nchi ambayo iliwahi kutawaliwa na Uingereza;
"kiapo" maana yake itabidi ifahamike kwa maana ya kawaida ya neno hilo na ni pamoja na tamko rasmi la namna yoyote linaloruhusiwa kisheria kutumiwa badala ya kiapo;
"kiapo cha uaminifu" maana yake ni kiapo cha kuwa mwaminifu kwa Nchi na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
"Maadili ya Kazi ya Jaji" maana yake ni masharti ya kimaadili yanayoongoza mwenendo wa watu wafanyao kazi ya Jaji au ya Hakimu;
"madaraka ya kazi katika utumishi wa Umma Jamhuri ya Muungano" maana yake itabidi ifahamike kwa mujibu wa maana ya kawaida na maneno hayo na ni pamoja na utumishi katika Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Muungano na katika Jeshi la Polisi au jeshi linginelo lilioundwa kwa mujibu wa Sheria;
"mahakama" maana yake ni mahakama yoyote yenye mamlaka katika Jamhuri ya Muungano isipokuwa mahakama iliyoundwa kwa amri ya jeshi; lakini kwa ajili ya ibara ya 13, ya 14 na ya 15 za Katiba hii, itakuwa ni pamoja na mahakama iliyoundwa kwa amri ya jeshi;
"Mahakama Kuu" maana yake ni Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Mahakama Kuu ya Zanzibar;
"Mambo ya Muungano" maana yake ni mambo yote ya umma ambayo yametajwa na ibara ya 4 ya Katiba hii kuwa ni Mambo ya Muungano;
"Mamlaka ya Nchi" ni pamoja na Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano, pamoja na Serikali na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
"Mwanasheria Mkuu" maana yake ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano aliyetajwa katika ibara ya 59;
"Serikali" maana yake ni pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au Halmashauri ya Wilaya au ya Mji, na pia mtu yeyote anayetekeleza madaraka au mamlaka yoyote kwa niaba ya Serikali au Halmashauri;
"Serikali za Mitaa" maana yake ni vyombo vya kiserikali vilivyoundwa kwa mujibu wa ibara ya 145 ya Katiba hii kwa madhumuni ya kutekeleza madaraka ya umma;
"Tanzania Bara" maana yake ni eneo lote la Jamhuri ya Muungnao ambalo zamani lilikuwa eneo la Jamhuri ya Tanganyika;
"Tanzania Zanzibar" maana yake ni eneo lote la Jamhuri ya Muungano ambalo zamani lilikuwa eneo la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na ambalo kabla ya Sheria hii kutungwa liliitwa Tanzania Visiwani;
"Uchaguzi Mkuu" au "uchaguzi unaofanywa na wananchi" maana yake ni uchaguzi wa Rais na uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha wilaya za uchaguzi unaofanywa baada ya Bunge kuvunjwa;
"Ujamaa" au "Ujamaa na Kujitegemea" maana yake ni misingi ya maisha ya jamii ya kujenga Taifa linalozingatia demokrasia, kujitegemea, uhuru, haki, usawa, udugu na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano;
"Waziri" maana yake ni Mbunge aliyekabidhiwa madaraka ya kazi ya Waziri, isipokuwa Naibu Waziri, na maana hiyo itatumika pia kwa Makamu wote wa Rais;
"Zanzibar" maana yake ni sawa na maana ya Tanzania Zanzibar.
Sijui mwenzetu ulitaka kuwe na definition zipi!