Z`bar wagawanyika
2008-07-27 14:25:40
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
Suala la Zanzibar kuwa nchi au si nchi limewagawa wananchi wa visiwani hapa wengine wakiunga mkono kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wengine wakipinga.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Zanzibar walisema umefika wakati wa kuanzishwa Mahakama ya kikatiba ili iweze kutoa tafsiri sahihi juu ya suala hilo.
Mkazi wa Chukwani, Bw. Shabani Salum, alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 126 imesema kutakuwepo na mahakama ya kikatiba ambayo haijaundwa tangu kuungana kwa nchi za Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964.
``Kwa mtazamo wangu hakuna mtu anayeweza kutoa tafsiri sahihi zaidi ya mahakama ya Katiba�suala hili si la kisiasa bali linahusu mambo ya kisheria,`` alisema Bw. Shabani.
Alisema kwamba mvutano uliojitokeza hivi sasa umesababishwa na waasisi wa muungano kutowashirikisha kwa karibu wanasheria wakati walipokuwa wakikubaliana mambo 11 ya Muungano.
Naye Bw. Said Millo (53), mkazi wa Kikwajuni, alisema ufumbuzi wa kutatua kero za muungano ni kuwepo kwa serikali tatu.
Alisema kwa maoni yake Zanzibar sio nchi kwa vile utaifa wa Zanzibar ulikufa kama wa Tanganyika ulivyokufa mara baada ya kusainiwa kwa Muungano wa nchi hizo.
``Suala hili Waziri Mkuu Pinda hakuhitaji kuulizwa, liko wazi kabisa katika Katiba yetu�wakulaumiwa hapa ni Wazanzibari wenyewe,`` alisema Millo.
Alisema kabla ya marekebisho ya 11 ya Katiba, Rais wa Zanzibar alikuwa Makamu wa pili wa Rais wa Muungano, lakini Wazanzibari kupitia vikao vya Bunge na CCM walipitisha marekebisho hayo.
``Mamlaka ya Zanzibar ilianza kupotea kuanzia hapa, sasa nani wa kulaumiwa wakati haya yalifanyika katika vikao halali,`` alisema Millo.
Naye mkazi wa Michenzani, Bw. Othman Magomba (56), alisema jambo la msingi hivi sasa ni pande mbili za Muungano kukaa na kujadili kero zinazojitokeza za kisiasa na kiuchumi.
``Zanzibar ilikuwa nchi kamili lakini sisi wenyewe Aprili 26, tukaamua kuinganisha na Tanganyika, sasa SMZ wasitutafutie mchawi ambaye anajulikana kuwa ni wao wenyewe,`` alisema Bw. Othman.
Alisema malalamiko yanayotolewa na wanasiasa hivi sasa hayana tofauti na msemo wa Kiswahili `maziwa yakimwagika hayazoleki`.
Mkazi huyo alisema ni jambo la kushangaza tangu kufikiwa Muungano huo asilimia 80 ya Wazanzibari hawaitambui Katiba ya Muungano na hivyo kushindwa kufahamu mambo ya msingi ya muungano na yasiyokuwa ya muungano.
Naye mkazi wa Mbweni, Mwajuma Shalah, alisema anaunga mkono kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bw. Iddi Pandu Hassan, kuwa Zanzibar ni nchi kwa vile baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Serikali ya Tanganyika iliingizwa katika Serikali ya Muungano wakati Serikali ya Zanzibar iliendelea kubakia hadi hivi sasa.
``Kwa kweli Waziri Mkuu atuombe radhi Wazanzibari sisi tunachagua Rais, na huwezi kuwa na Rais bila ya kuwa na nchi�sasa Rais wetu ni wanchi gani?
Alihoji Mwanajuma.
Naye Mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Bw. Mohamed Raza, alisema hakuna wa kutengua kitendawili hiki zaidi ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Amani Karume kutoa tamko la pamoja ili kuuzima mjadala huo.
Alisema CCM Zanzibar itakuwa katika wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 endapo viongozi wa CCM Bara wataendelea kusisitiza kuwa Zanzibar si nchi.
``CCM Zanzibar itakuwa katika wakati mgumu kushinda uchaguzi wa mwaka 2010 iwapo itasisitiza kuwa Zanzibar si nchi, Wazanzibari watashindwa kujua wanampigia kura Rais wa mkoa wa wilaya`` alisema Raza.
Naye Makamu Mwenyekti wa NCCR-Mageuzi, Bw. Khamis Hambar, alisema mtego huo unaweza kunasuliwa na mahakama ya katiba pekee.
Alisema kimsingi, Zanzibar ni nchi lakini haina mabawa kwa vile mamlaka yake yanaishia ndani ya Tanzania huku ikiwa haina uwezo katika nyanja za kimataifa hasa utiaji wa saini wa mikataba ya kimataifa.
Alisema pande mbili za Muungano zianzishe haraka mahakama ya katiba badala ya suala hilo kujadiliwa na CCM kwa vile linahusu wananchi na si vyama vya siasa.
Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Zanzibar si Nchi kwa vile Tanzania ni nchi moja yenye serikali mbili ya Zanzibar na ya muungano na eneo lote la ardhi Bara na Zanzibar pamoja na eneo la usawa wa bahari ni sehemu ya Jamhuri ya muungano.
Hata hivyo, kauli ya Waziri Mkuu ilipingwa na Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Bw. Iddi Pandu Hassan, ambaye alisema baada ya Muungano Serikali ya Tanganyika, iliingizwa ndani ya muungano na SMZ ilibakia na kusisitiza kuwa haiwezekani kuwa na Serikali bila ya kuwa na nchi .