Kwanza, bila kujali vitisho vya Jakaya Kikwete, Baraza la Wawakilishi katika kikao cha mwezi wa kumi walijadili kwa kina suala la Muungano. Spika, Mhe. Pandu Ameir Kificho, aliahidi Oktoba watalijadili. Muungwana hutimiza ahadi.Pili, huu Mkataba wa Muungano, Articles of Union,umegubikwa na mambo mengine sana ambayo hayaeleweki. Sasa tunataka Articles of Union, Mkataba wa Muungano, uwekwe bayana ujadiliwe upya. Na tunataka ujadiliwe vipi? Kwamba sisi Wazanzibari kwa umoja wetu tujadili Mkataba, tukubaliane mambo yapi tunataka yawe kwenye Muungano, tukubaliane Muungano wenyewe uwe na sura gani, tukubaliane Muungano wenyewe uwe na mamlaka gani. Na Watanganyika nao wafanye hivyo hivyo, kama Watanganyika, kwa upande wao.
Hotuba ya kihistoria ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kwa Wazanzibari katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa maalum na wazee wa jimbo la Chaani, Jumamosi 30 Agosti, 2008, Kaskazini Unguja, kutoa msimamo wa hatima ya Zanzibar kwenye Muungano
Maamkizi na Shukrani
Waheshimiwa Wazanzibari wenzangu, nianze kwa kuungana na wenzangu kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Chaani wakiongozwa na wazee ambao wametualika kuja kufanya mkutano huu hapa Chaani. Nasema ahsanteni sana.
Pili, niwashukuru viongozi wa chama chetu cha CUF wa ngazi mbali mbali: wilaya, wodi, jimbo, na matawi, kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu. Nasema ahsanteni sana.
Lakini bila ya kuhudhuriwa na nyiyi tungekuwa hatuna mkutano huu. Pamoja na maandalizi mazuri, kilichofanikisha mkutano huu ni nyinyi muliohudhuria. Kwa hivyo, hakuna budi shukrani nyingi zije kwenu.
Salamu za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
Baada ya hilo, kama alivyosema Mhe. Salim Bimani (Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma), baada ya siku mbili tunatazamia tutampokea mgeni Ramadhani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aijaalie iwe Ramadhani ya kheri kwetu sote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu, kwa barka za mwezi mtukufu wa Ramadhani, matatizo waliyonayo Wazanzibari ayaondoe. Yeye ni Muweza wa yote, yeye ni kusema jambo kuwa linakuwa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu, kwa baraka za mwezi Mtukufu wa ramadhani, aulinde umoja wa Wazanzibari ili atupe nguvu kuweza kutetea nchi yetu ya Zanzibar. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azitakabalie funga zetu na atusamehe makosa yetu kwa fadhila za mwezi wa Ramadhani.
Waheshimiwa, hali ya maisha ni ngumu na Ramadhani mara nyingi hali huwa ngumu zaidi, kwa hivyo tupeane pole. Inshallah, Mwenyezi Mungu, atatusahilishia. Inshallah. Lakini niiombe Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ioneshe mfano. Ipunguze mzigo wa gharama za maisha kwa Wazanzibari angalau kwa mwezi huu wa Ramadhani. Na kubwa, wakiweza kutupunguzia kodi katika mafuta ya petroli na dizeli na katika baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje katika mwezi huu, hali itakuwa nafuu kidogo. Waekeze na wao kwa Mwenyezi Mungu wakalipwe kesho, Akhera. Lakini pia niwaombe Wazanzibari, sisi kwa sisi, tusaidiane. Tunahimizwa kusaidiana, kupeana sadaka, na hasa katika mwezi huu wa Ramadhani.
Kwa hivyo, kila yule aliyenacho, amsaidie yule asiyenacho. Na hususan wafanyabiashara wasiutumie mwezi wa Ramadhani kuzidi kuwakamua watu ambao hawana kitu. Tunawaomba san asana, waache kuwakamua, na wao vile vile waekeze kwenye akhera zao, wasiangalie kwenye faida za duniani. Tukifanya hivyo, inshallah, ule ukali utaweza kupungua.
Udhaifu wa Hoja za Rais Kikwete na Mjadala wa Hadhi ya Zanzibar
Baada ya salamu hizo za kuikaribisha Ramadhani, sasa naomba muniruhusu kuzungumzia yale ambayo wazee wa Chaani wametualika kuja kuyazungumza hapa.
Waheshimiwa, kama munavyojuwa kwamba katika kipindi cha siku za hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkali katika nchi yetu. Mjadala ambao chanzo chake ulianzia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, kule ambako Kiongozi wa Upinzani katika Bunge, Mhe. Hamad Rashid Mohamed, alipomuuliza Waziri Mkuu Mizengo Pinda: Je Zanzibar ni nchi? Mhe. Pinda akajikaza, akajitutumua, akasema: Zanzibar si nchi! Mjadala ukaanza hapo. Na ulikuwa mjadala mkali.
Hatimaye Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akatinga Bungeni kwenda kuzungumza na Watanzania kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano. Mimi sikuwepo, lakini waliokuwepo wananiambia kwamba katika hotuba yake alianza na suala hili, kwamba je Zanzibar ni nchi ama si nchi. Na naambiwa: Wewe unamjuwa rafiki yako (Kikwete) anapenda kuchekacheka, lakini alipokuwa kazungumza suala hili hakucheka. Alikuwa kidogo kakasirika hivi!
Ningeelewa pengine ni kwa uzito wa suala lenyewe, akaona haifai kuchekewa. Kwa hivyo, Watanzania, na hususani Wazanzibari wakatazamia watapata majibu ya kuwaridhisha. Basi Mhe. Kikwete akalizungumzia suala hili na mambo mengine mengi, lakini leo ajenda yetu ni hili alilozungumza Kikwete juu ya kwamba Zanzibar ni nchi ama si nchi. Sawa sawa waheshimiwa!?
Udhaifu wa Hoja ya Kwanza: Mshangao wa Kikwete kwa Wanaohoji Muungano
Mheshimiwa Kikwete alisema mengi katika suala hili, lakini mambo matatu ndiyo ya kushika: la kwanza alisema anashangaa kwamba leo ni miaka 44 tangu Muungano huu kuasisiwa na bado kuna watu hawauelewi. Bado watu hawaelewi dhamira za waasisi kuunganisha nchi hizi. Anashangaa.
Mimi namwambia rafiki yangu, kwa heshima zote with due respect hapo Mhe. Kikwete hakutwambia jipya. Nataka nimkumbushe Mhe. Kikwete kwamba mwaka 1967, muasisi mmoja wa Muungano huu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anasema kwamba yeye hashangazwi na wageni ambao hawauelewi Muungano wa Tanzania, lakini anashangazwa kwamba Wazanzibari na Watanganyika, Watanzania wenyewe, kwamba hawauelewi Muungano huu. Kwa hivyo alilosema Kikwete tarehe 21 Agosti, 2008, kule Bungeni tayari lilishasemwa miaka 41 iliyopita na Mwalimu Julius Kambrage Nyerere.
Mwalimu (Nyerere) alipozungumza ulikuwa Muungano una umri wa miaka mitatu tu, leo Kikwete anazungumza Muungano una miaka 44, na bado Watanzania hawauelewi. Sasa nani wa kulaumiwa? Nani wa kulaumiwa, kwamba miaka 41 imepita, bado wananchi hawaulewi Muungano wao? Huwezi kuwalaumu wananchi. Kama kuna wa kulaumiwa, ni wao watawala.
Nami nasema, ni kweli Muungano huu haueleweki. Utaeleweka vipi, na bado wananchi hawajaelezwa Muungano huu ni vipi? Bado wananchi hawajaelezwa dhamira za Mzee Karume na Mwalimu Nyerere kuunganisha nchi. Kwa kipindi chote cha utawala wa Nyerere ilikuwa wewe unaambiwa ni haini ukizungumzia masuala ya Muungano. Kwa hivyo, Muungano utaeleweka vipi na nyinyi wenye madaraka hamtaki, kwa makusudi kabisa, kuwaeleza wananchi ni nini Muungano huu? Hamtaki. Vipi wataelewa wananchi?
Mambo yenyewe yamefanywa siri siri, yamegubikwagubikwa katika guo jeusi, hujui ndani muna nini mule. Ndio ukweli wenyewe ulivyo hivyo. Lakini tulianza kuanzia mwanzo, Muungano unafanywa kwa siri kubwa.
Mwaka 1964, baada ya Mapinduzi, miezi mitatu tu baada ya hapo, tunaambiwa Mwalimu Nyerere na Mzee Karume wakazungumza, watu wawili. Watu wawili! Waheshimiwa, hata Baraza la Mapinduzi, wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, ambalo wakati huo pia lilikuwa Baraza la Mawaziri la Zanzibar, walikuwa hawajui kitu. Wao tarehe 25/26 Aprili 1964, wanasikia kama sisi wanyonge wengine kwamba nchi mbili zimeungana. Basi hata viongozi wa serikali hawaaminiki? Hata viongozi wa serikali nao hawaaminiki?
Mwanasheria mkuu wa wakati huo, Bwana (Wolfgang) Dourado, kasema wazi wazi, yeye kama ndiye mshauri mkuu wa mambo ya sheria kwa serikali ya Zanzibar, hakuambiwa, hakushirikishwa chochote katika suala hilo. Mwalimu wangu, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, anasema waziwazi kwamba pamoja na kuwa alikuwa karibu na Mzee Karume, hakujua lolote juu ya Muungano huu. Hii ndiyo hali halisi. Tumezungwazugwa na watu wawili tu, basi!
Na yule Nyerere, yeye alikuwa na wanasheria wa Kiingereza wakimshauri, lakini alimkataza Mzee Karume asimtumie mwanasheria wake. Ndiyo suala lenyewe hilo. Mpaka leo unafichwafichwa, hatujui nini Muungano huu! Sawa sawa wananchi!?
Tunaambiwa katika Mkataba wa Muungano, ambao ulitarajiwa ndio uongoze Muungano huu, ilikubaliwa baada ya maraisi wawili kuweka saini zao basi vyombo vya kutunga sheria katika nchi mbili wakati huo Tanganyika walikuwa na Bunge, Zanzibar tulikuwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri kwa pamoja vyombo hivi, kila kimoja kwa upande wake, kiidhinishe Muungano. Lugha ya Kiingereza wanasema to ratify kuidhinisha sawa sawa!?
Mpaka hivi leo, 2008 miaka 44, Mhe. Kikwete kama hujuwi tunakwambia, mpaka leo Baraza la Mapinduzi la Zanzibar halijauidhinisha Muungano huu. Mpaka leo hii. Mpaka leo. Walilofanya wale wa Bara, chini ya Nyerere, kumtaka mwanasheria wa Tanganyika, mzungu mmoja shonga mmoja anaitwa Feefurt, huyu ndiye akaandika sheria yeye ya kuthibitisha Muungano, halafu akaifanya ni sheria iliyotungwa na Baraza la Mapinduzi. Lakini la ajabu, sheria ile haikutangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali ya Zanzibar, ilitangazwa katika Gazeti Rasmi la Tanganyika. Tazama watu walivyo wabaya hawa!
Halafu ukisema, anakwambia sakubimbi, sakubimbi wewe! Tunadai tujuwe mambo, unatwambia sakubimbi. Kama tafsiri yako ya sakubimbi ni watu wasidai haki zao, umechelewa. Yaguju! Tutadai haki yetu. Tutadai haki yetu.
Kwa hivyo, ninalosema kwa ufupi, Zanzibar mpaka leo haujathibitishwa Muungano huu. Mpaka tarehe ya leo, bado.
Makubaliano hayo hayo, au Mkataba wa Muungano, yalitaka katika kipindi cha mwaka mmoja wa kutiwa saini kuweko na Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano. Na katiba hiyo ingelipatikana vipi? Makubaliano hayo yanasema, Rais wa Muungano kwa kushirikiana na Makamo wake kutoka Zanzibar, yaani kiongozi wa Zanzibar, Mzee Karume, wangeunda tume ya kutayarisha rasimu ya katiba hiyo, halafu baada ya hapo, ukaitishwa Mkutano Maalum wa Katiba, Constituent Assembly, (ambao) ni mkutano maalum wa kuipitisha. Hapo tungekuwa na katiba ya kudumu. Mpaka hapo jua lilipofika, hilo halijafanyika wananchi. Miaka 44, hilo halijafanyika.
Walilolifanya ni nini? Ni ule ule usungurasungura tu, basi! Ule usungurasungura aloufanya Nyerere mwaka 1977. Wakati Afro-Shirazi Party na TANU zinaungana, aliteua tume ya kuunganisha vyama hivi na kutayarisha katiba ya chama kipya kitakachokuja. Kamati ile ikiongozwa na mzee wetu, Marehemu Sheikh Thabit Kombo, na upande wa pili, Katibu wa ule, alikuwa ni bwana mmoja ni mwalimu wangu vile vile wa Chuo Kikuu anaiwa Pius Msekwa. Wakakutana, wakatayarisha katiba ya CCM.
Hatuna ugomvi na hapo. (Lakini) walipomaliza, Nyerere akasema kamati hii hii, ndiyo ifanye mapendekezo ya katiba mpya. Halafu akasema Bunge hili hili la Jamhuri ya Muungano ligeuzwe tu, liitwe Bunge la Katiba, lipitishe katiba hiyo. Na mimi nasema, nasimama juu ya hoja kwamba katika hilo Serikali ya Zanzibar haikushirikishwa kabisa. Serikali ya Zanzibar haikushirikishwa. Ulaghai tu, basi! Halafu ati tusiseme. Tutasema. Tutasema.
Lakini kubwa zaidi, waheshimiwa, ni kwamba katika Mambo ya Muungano, Mkataba wa Muungano unasema ni mambo 11 tu, basi. Na mpaka leo, Mkataba ule haujarekebishwa, na ili urekebishe ni lazima upate Zanzibar kwa upande mmoja na Tanganyika kwa upande wa pili wakubaliane kurekebisha. Mpaka leo haujarekebishwa, lakini Mambo ya Muungano yametoka 11 mpaka sasa hivi tunaambiwa ni 23, lakini ukiyachambua moja moja yanafika 32.
Na sasa hivi wana mpango mpya wa kuchukua tu, hupitisha Sheria ya Bunge, kisha wakasema sheria hii itatumika Zanzibar. Kwa hivyo, hata jambo ambalo si la Muungano, sasa wao kwa utaratibu huo wanalifanya la Muungano, (maana) kwa watu wa Tanganyika kuimarisha Muungano maana yake ni kuongeza mambo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano kuinyima Zanzibar, kuichukulia madaraka yake, na kuyapeleka katika Serikali ya Muungano. Ni ule ule utaratibu wa kijanjajanja kuhakikisha pole pole wanaimungunya Zanzibar mpaka wanaimaliza. Lakini, inshallah, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hawatofanikiwa.
Waheshimiwa, katika njama zao hizo hizo, katika Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, wakamuondolea Rais wa Zanzibar nafasi yake ya kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kama Mkataba wa Muungano ulivyosema. Tena wakayafanya (mabadiliko haya) kwa njia ambazo ni kinyume na taratibu walizoziweka wenyewe za kubadilisha mambo kama hayo.
Kwa hivyo, musishangae waheshimiwa wananchi, kwamba hata hii kauli ya Mhe. Pinda kwamba Zanzibar si nchi ni katika mtiririko ule ule wa kuhakikisha kuwa wanaimaliza Zanzibar. Kiasi Wazanzibari waje juu.
Kwa hivyo tunalomwambia, kwa hoja ya mwanzo ya Rais Kikwete hajasema jipya. Na pengine hajuwi dhulma iliyofanywa, hajui khiyana iliyoafanywa dhidi ya Zanzibar. bahati njema kuna profesa mmoja anaitwa Issa Shivji. Huyu si Mzanzibari, lakini kafanya utafiti wa kina na kaonesha wazi wazi dhulma ambayo Zanzibar imefanyiwa na katoa kitabu (Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika Zanzibar Union, Mkuki na Nyota Publishers - 2008). Hiki kitabu cha Shivji hiki, kaeleza mambo hayajapata kuelezwa hata siku moja. Profesa mmoja wa Bara alipokisoma kitabu hichi, tena mtu wa Bara huyo, alisema Mzanzibari yeyote akisoma kitabu hiki lazima kwanza akasirike tu kwa vile dhuluma ilivyoelezwa walivyofanyiwa Wazanzibari.
Kwa hivyo tunakwambia Mhe. Kikwete hujatupa jibu. Hilo la kwanza alilolisema.
Udhaifu wa Hoja ya Pili: Kusitisha Mjadala Mara Moja
La pili alilolisema Mhe. Kikwete tarehe 21 Agosti mwaka huu ni kuwa hapakuwa na sababu ya mjadala huu kufikia ulipofikia. Na yeye anashangaa tena yeye kazi yake ni kushangaa tu kwamba viongozi ambao wamo katika kamati zilizoundwa kuzipatia ufumbuzi kero za Muungano ndio wao kwa wao wanalumbana. Kwa hivyo, akataka hilo lisite mara moja.
Mimi nasema, namwambia rafiki yangu, ndugu yangu Kikwete, kwamba nyinyi mnasema huu ni Muungano wa wananchi, au sio? Munasema si Muungano wa viongozi, ni Muungano wa wananchi. Sasa, kwa nini mukasirike wananchi wakiujadili Muungano wao? Kwa nini mukasirike? Jambo gani linakufanya Mhe. Kikwete na wenzako mukasirike kwa wananchi kuujadili Muungano wao
Mimi nasema wananchi hatuna budi tuujadili Muungano. Miaka mingi walituziba midomo, waliishona midomo: Huna ruhusa kuzungumzia mambo ya Muungano!Sasa mazingira yamebadilika. Na kwa sababu ulikuwa hauzungumzwi, matatizo yamejikusanya, sasa yanahatarisha uhai wa Muungano wenyewe. Watu wanazungumza, mnataka kuwapiga full stop. Hilo haliwezekani, No, kabisa kabisa!
Mimi nasema kuna kila sababu ya kuuzungumza, kuujadili Muungano huu. Tuuelewe, tuufahamu. Kwa kweli, mimi ni mtu ambaye nimefurahi sana, kwamba kwa mara ya mwanzo katika historia tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi (mwaka 1992), wawakilishi na wabunge kutoka Zanzibar, bila ya kujali itikadi zao, wamekuwa na msimamo mmoja juu ya suala la Muungano. Nimefurahi sana, nimefurahi sana, na napaswa kuwa hivyo.
Na hawa, Mhe. Kikwete, ni wawakilishi wa Wazanzibari waliopelekwa katika Baraza la Wawakilishi na Bunge la Jamhuri ya Muungano la Wazanzibari. Wao, kwanza kabisa, wanawajibika kwa Wazanzibari wenyewe, ndio tena wawajibike kwa vyama vyao. Na Wazanzibari wanasema hawaridhiki na Muungano huu. Sasa kwa nini wawakilishi wetu, tuliowapa madaraka watusemee, wakisema muwaone wabaya?
Mimi nawapongeza sana. Nawapa hongera. Hata mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi, nao vile vile wamekuja wazi wazi kuwatetea Wazanzibari. Mfano mzuri ni Mhe. Ali Juma Shamhuna. Ali Juma Shamhuna hajapatapo hata siku moja kuipenda CUF, lakini nasema mtu mpe haki yake. Myonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Kwa hili, Ali Juma Shamhuna, Hamza Hassan Juma, Mansour Yussuf Himidi, na wenzao wote, wamesimama upande wa Wazanzibari.
Na mimi, hasa, Mansour kanifurahisha kwa msimamo wake wa kutetea haki ya Zanzibar katika suala zima la mafuta. Sasa wawakilishi hao, na wale wa CUF wakiongozwa na Mhe. Aboubakar Khamis Bakari, akina Said Ali Mbarouk, Bi Zakia na wengine wote. Kwenye Bunge, tuna watu wa CCM, akina Hafidh Ali, wote wameutetea vizuri Muungano wetu. Akina Hamad Rashid, Ali Taarab, wote wameutetea vizuri Muungano wetu. Hatuna budi tuwashukuru, tuwapongeze waendelee na msimamo huo. Msishtushwe, msitishwe na kauli ya Kikwete. Kama nilivyosema, nyinyi mnawajibika kwa Wazanzibari wenyewe sio kwa Kikwete.
Lakini hata lile alilosema Kikwete, kwamba suala hili linajadiliwa katika vikao na watu wanaoshiriki katika vikao hawawajibiki kulizungumza, mimi nasema Kikwete kakosea. Yako mambo yanaweza yakazungumzwa katika vikao hivyo, lakini kuna mambo hayawezi kuzungumzwa katika vikao hivyo.
Vikao vile ni kuondoa tafauti masuala ya utawala juu ya mambo ya Muungano. Lakini mjadala mzima ulivyokwenda, umeonesha kuna mawazo tafauti baina ya Bara na Zanzibar, kwa hivyo hapo kunaashiria kuna mgogoro wa kikatiba. Anayeweza kuutatua mgogoro wa kikatiba si vikao hivi, bali ni Mahkama ya Katiba. Na yeye Kikwete anaogopa kuinda Mahkama ya Katiba. Kwa hivyo undeni Mahkama ya Katiba muzungumzie masuala haya. Kwa hivyo na hili, Mhe. Kikwete hakutupa jibu. Bado hajatupa jibu dhaifu wa Hoja ya Tatu: Zanzibar ni Nchi Ndani ya Jamhuri ya Muungano, lakini si Nchi nje ya Mipaka ya Muungano.
Jambo la tatu alilozungumza Mhe. Kikwete, na naomba hapa mumsikilize vizuri, kwamba anasema dunia nzima inajua kwamba mwaka 1964 Tangayika na Zanzibar ziliungana kufanya jamhuri moja ya Muungano. Akaendelea kusema Kikwete kwamba ukiwa nje ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano, kuna nchi moja tu ya Tanzania. Kwa maana nyengine, anavyosema Kikwete, ukiwa nje ya Tanzania, Zanzibar si nchi. Unchi wa Zanzibar unaishia Chumbe. Ndivyo anavyosema Kikwete. Na akaendelea kusema, ukiwemo ndani ya nchi, kuna nchi ya Zanzibar na kuna nchi ya Tanganyika, ambazo zote ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano. Kizungumkuti! Ukiwa Uingereza ni Tanzania tu, ukiwa Matemwe, Zanzibar ni nchi. Ukiwa Bukoba, Zanzibar ni nchi na Tanganyika ni nchi. Nasema kizungumkuti.
Mimi nasema kuna moja tu hapa: sikubaliani na uchambuzi wa Kikwete juu ya hilo. Sikubaliani. Suala ninalomuuliza ndugu yangu Kikwete ni kwamba, sisi nchi yetu ya Zanzibar, kwa hivyo unavyotaka weye, tuna serikali yetu, serikali ya nchi yako ya Tanganyika iko wapi?
Waheshimiwa, pale mwanzo Nyerere aliposema wao hawataki serikali, hoja aliyoitumia kutetea kwa nini Tanganyika isiwe na serikali, ni kwamba Zanzibar ni ndogo kieneo na ina wananchi kidogo, kwa hivyo kama hawana serikali yao watakuwa na khofu kwamba wanamezwa. Kwa hivyo, kumbe madhumuni ya kufanya serikali mbili ni kuwafanya Wazanzibari waondoe khofu kwamba watamezwa, lakini Nyerere hajapata kusema kwamba madhumuni ya (Muungano wa) serikali mbili na Zanzibar kuwa serikali yake ni kwamba haki za Zanzibar zilindwe. Hajapata kusema hilo. Kiini macho tu, muoneshwe kuwa nyinyi muna serikali yenu, lakini kumbe ni ganda tupu, hamuna kitu.
Wao waliikataa serikali kwa sababu moja kuu: kuifanya serikali ya Tanganyika iwe ndiyo serikali ya Muungano, kuifanya Tanganyika iwe ndiyo Muungano wenyewe, Jamhuri ya Muungano. Sisi Zanzibar tukae huko, lakini washayachukua madaraka yetu washayachukuwa wao chini ya mwevuli wa Serikali ya Muungano. Hawakupoteza kitu wao. Hakuna walichopoteza. Tuliopoteza ni sisi. Mambo ambayo yalikuwa chini ya mamlaka yetu yamekwenda huko. Kwa maneno mengine, kwa kifichoficho hivi, chini ya pazia ni Muungano, lakini kwa kweli ni Tanganyika.
Kwa hivyo, nasema waheshimiwa, Rais Kikwete anaposema kwamba Tanganyika ni nchi, serikali yake iko wapi? Waruke watoje ni lazima paje kuwa na serikali tatu, msimamo wa CUF.
Sasa tuangalie huu uchambuzi wa Kikwete kwamba ukiwa ndani ya nchi, Zanzibar ni nchi, ukiwa nje Zanzibar si nchi. Nasema hiyo ni kauli ya kisanii. Na nasema hilo kwa sababu Mkataba wa Muungano haujapatapo kuifuta nchi ya Zanzibar wala haukuifuta nchi ya Tanganyika. In fact, Mkataba wa Muungano unaashiria kutaka nchi hizi ziendelee kwa kusema kuwa shughuli za Muungano kwa upande wa Bara zitaongozwa na katiba ya Tanganyika, na shughuli za Muungano kwa Zanzibar zitaongozwa na sheria ya Katiba zilizotungwa na Baraza la Mapinduzi. Sasa unapokuwa na katiba, ambayo sheria ile ndiyo hatimaye ilizaa Katiba ya Zanzibar, katiba ya nini? Ya Yanga? Katiba ya Miembeni? Ile ni katiba ya nchi ya Zanzibar.
Wao katika janja janja zao, siku ya pili baada ya Muungano wakatuga sheria katika Bunge la Tanganyika kuifuta Tanganyika.
Na wameifuta kama nilivyosema ili wao wawe ni Tanzania. Sasa kama wameifuta ni shauri yao. Sisi Zanzibar haikufutwa, na kwa hivyo Zanzibar ipo.
Waheshimiwa, Mkataba wa Muungano umesema kuna mambo yatakayoshughulikiwa chini ya mamlaka chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na katika hayo, hakuna chombo chengine chochote duniani kinachoweza kuingilia Serikali ya Zanzibar. maana yake nini? Katika mambo hayo, kwa lugha ya Kiingereza Zanzibar is sovereign, ina mamlaka ya mwisho hakuna wa kuwaingilia. Mambo ya elimu, mambo ya kilimo, mambo ya afya, mambo ya mawasiliano na uchukuzi, ambayo ndiyo hasa yanayogusa maisha ya mwananchi wa Zanzibar, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, yako chini ya Serikali ya Zanzibar; na katika hilo hakuna mtu mwengine anayeweza kuwaingilia. Katika mambo hayo, Zanzibar wana haki ya kuzungumza na nchi yoyote nyengine kutaka maendeleo ya Zanzibar.
Hii ni haki yetu, lakini wameibinyabinya. Kukiwa na mkutano wa Shirika la Afya Duniani wanakwenda wao. Haya jamani matatizo ya Zanzibar ya afya kule yatazungumzwa na nani? Kuna Shirika la Kilimo na Chakula duniani, wanakwenda wao. Sasa matatizo ya Zanzibar ya kilimo kule atayazungumza nani kule?
Kwa hivyo nasema we are a sovereign, sisi ni nchi. Mhe. Kikwete with due respectuchambuzi wako hatuukubali.
Hapa nakumbuka mimi nilipokuwemo kwenye serikali, tukizungumza na nchi mbali mbali kuhusu mambo yasiyokuwa ya Muungano na wakitusikiliza. Tulikuwa na mahusiano bila ya kupitia Dar es salaam. Wamefanyafanya mpaka sasa wamewaambia (nchi na jumuiya za kigeni): Hao jamaa (Zanzibar), mpaka mushirikiane na sisi (serikali ya Muungano). No, hiyo ni dhulma munatufanyia wenzetu. Ni dhulma.
Lakini zuri zaidi ni kuwa katika Makubaliano ya Muungano, jambo lililowekwa kama jambo la Muungano ni Mambo ya Nje (foreign affairs) mahusiano ya nchi na nchi nyengine ya kisiasa, ya kiserikali lakini suala la mashirikiano ya kimataifa (international cooperation) halijapata kuwa la Muungano hata siku moja. Wao katika ujanja wao, wamefanya na kuuita Wizara Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa ili kuinyima Zanzibar haki ya kushirikiana na mashirika mbali mbali kwa maendeleo ya Zanzibar.
Kwa hivyo, mimi nasema, kwa sababu tuna haki ya mashirikiano ya kimataifa chini ya serikali ya Zanzibar, Zanzibar ilikuwa na haki na Zanzibar itaendelea kuwa na haki ya kuwa mwanachama wa OIC. Ile kulazimishwa kujitoa ni kwa sababu ya choyo chao tu, lakini haki ile tunayo. Na mashirika mengine kama hayo, Zanzibar inayo haki hiyo.
Nani Mwenye Ajenda ya Siri?
Sasa, nimwambie Mhe. Kikwete kwamba sisi hatuna ajenda ya siri, kama kuna mtu ana ajenda ya siri ni wao, sio sisi. Nimeonesha usiri wa Muungano huu ulivyokuwa, nimeonesha hata ule Mkataba wa Muungano ulivyokiukwa kabisa. Sasa yote hayo yanaashiria kuwa wenzetu wana ajenda ya siri. Lakini sisi hatuna ajenda ya siri.
Na kuthibitisha kuwa wenzetu wana ajenda ya siri, mutakumbuka wananchi, baada ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislam Duniani (OIC), Bara kulizuka kundi linaloitwa G55, yaani kundi la watu 55, wabunge wa Bara, wakadai serikali yao ya Tanganyika. Wakaenda kwenye Bunge na Bunge likapitisha azimio kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Agosti 1993, serikali ya Tanganyika iwe tayari imeanzishwa. Nyerere hakufurahishwa na azimio hilo halali la Bunge. Akaweka shinikizo kubwa, ikambidi Mzee Ali Hassan Mwinyi aitishe kikao cha wabunge wote wa CCM wa wakati huo kuingalia tena hoja hii. Mwisho wakaambiwa kuwa serkali tatu si sera ya CCM, wakatakiwa warudi Bungeni wakalifute azimio la 1993, wapitishe azimio jipya.
Hiyo ilikuwa ni Agosti 1994, ambapo tunangojea serikali ya Tanganyika. Haikuundwa. Kilichofanyika ni wabunge, ambao wakati huo wote walikuwa wa CCM, walikwenda kwenye Bunge wakalifuta Azimio la Kuanzishwa Serikali ya Tanganyika na badala yake wakasema katika Azimio jipya la Bunge kwamba: Lengo letu ni kuwa serikali mbili kuelekea serikali moja. Sasa ukishakuwa na serikali moja, kuna Zanzibar hapo. Kwa hivyo, nia ya kuifuta Zanzibar ipo. Wao, wenzetu, ndio wenye nia hiyo.
Na kama mmefuatilia mjadala katika Bunge, hasa walipokuwa wanajadili Wizara ya Muungano, bila ya shaka mumeona, kila mbunge wa Bara aliyekuwa akisimama anasema serikali moja. Kila mbunge wa Bara aliyekuwa akisimama, anasema serikali ya Zanzibar lazima ifutwe. Hata watu kufika pahala wakasema kwamba Waziri Mkuu yuko juu wa mawaziri wote wa Zanzibar akiwemo hata Waziri Kiongozi. Matusi ya hali ya juu!
Kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano, serikali hizi mbili ziko sawa sawa. Hakuna serikali moja iliyo juu ya nyengine. Kwa hivyo Waziri Mkuu Pinda hawezi kuwa juu ya Waziri Kiongozi Shamsi Nahodha. Isipokuwa ikiwa mwenyewe Nahodha kakubali akaliwe, shauri yake! Akikubali mwenyewe, shauri yake, lakini tunavyojuwa sisi Pindaet paar na Nahodha. Waziri wa Kilimo wa Bara ni sawa sawa na Burhani Saadat wa Zanzibar. Mwenyewe Mzee Burhani akikubali: Haya bwana, inshallah bwana! hiari yake mwenyewe, lakini constitutional arrangement iko hivyo.
Wala si kweli kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano iko juu ya Katiba ya Zanzibar. No, no, no, ni sawa sawa kabisa. Mwakyembe anafika hadi leo kusema kwamba mawaziri wa Zanzibar hawana nidhamu wanapingana na Waziri Mkuu Pinda! Ebo! Kwani ni Mungu yule hata asipingwe? Hata kama ni serikali moja, wanayo haki, sikwambii kama ni serikali tafauti.
Msimamo wa CUF: Hakuna Usakubimbi, Hakuna Vitisho, Wazanzibari Mkataba wa Muungano Ujadiliwe Upya
Sasa, tunasema waheshimiwa, Zanzibar ni nchi ndani ya mipaka ya Zanzibar, Zanzibar ni nchi nje ya mipaka ya Zanzibar.
Nimwambie rafiki yangu Kikwete, katika hotuba yake kanivunja moyo aliposema wanaozungumza suala hili na masakubimbi. Sikumtazamia hata kidogo. (Lakini) sasa tunasema Wazanzibari tunalotaka ni mambo yafuatayo:
Kwanza, bila kujali vitisho vya Jakaya Kikwete, Baraza la Wawakilishi katika kikao cha mwezi wa kumi walijadili kwa kina suala la Muungano. Spika, Mhe. Pandu Ameir Kificho, aliahidi Oktoba watalijadili. Muungwana hutimiza ahadi. Kwa hivyo, Mhe. Kificho tunakuomba waruhusu wawakilishi walijadili hili. Isijekuwa hotuba ya Kikwete, ukasema lakini Rais kasema. Rais kasema sawa, si ndio tushamsikia? Kwa hivyo, lijadiliwe.
Na kama Kificho hataki, kiongozi mkuu wa kisiasa katika CCM Zanzibar ni Mhe. Amani Karume. Mhe. Karume amdhibiti Kificho, amuamuru Kificho, suala hili lizungumzwe katika Baraza la Wawakilishi.
Wajumbe wetu wakizungumza wazungumze nini? Kwanza wadai kwamba Mkataba wa Muungano uheshimiwe kama ulivyosainiwa na Mwalimu Nyerere na Mzee Karume. Kwa maana hiyo, Mambo ya Muungano 11 tu, yale mengine yote yaliyoongezwa juu mpaka kufika 40 yatolewe yarudishwe kwenye Mamlaka ya Zanzibar.
Na hata hayo mambo 11 yanajadilika. Mimi nakumbuka, katika Kamati Kuu moja, Mwalimu Nyerere, akiwa mwenyekiti wa kikao, alisema wazi wazi mambo kama ya polisi si lazima yawe ya Muungano. Nchi mbali mbali zilizo kwenye Muungano, kila state inakuwa na polisi yake. Kwa hivyo, mambo hayo yaangaliwe na yajadiliwe.
Pili, huu Mkataba wa Muungano, Articles of Union, umegubikwa na mambo mengine sana ambayo hayaeleweki. Sasa tunataka Articles of Union, Mkataba wa Muungano, uwekwe bayana ujadiliwe upya. Na tunataka ujadiliwe vipi? Kwamba sisi Wazanzibari kwa umoja wetu tujadili Mkataba, tukubaliane mambo yapi tunataka yawe kwenye Muungano, tukubaliane Muungano wenyewe uwe na sura gani, tukubaliane Muungano wenyewe uwe na mamlaka gani. Na Watanganyika nao wafanye hivyo hivyo, kama Watanganyika, kwa upande wao.
Tukishakubaliana Wazanzibari, tutakuwa na Waraka wetu wa tunayoyataka. Na Watanganyika watakuwa na Waraka wao. Sasa Wazanzibari na Watanganyik wanateua Tume ya kwenda kukaa juu ya meza kujadiliana mpaka waafikiane. Sio waseme kwamba vikao hivi vya mawaziri ndio vijadili. No, no, no.
Tunajadili nini? Katika hali ya sasa, fikra na mawazo ya watu wa Bara kwamba Serikali ya Zanzibar iko chini yao, Waziri Kiongozi yuko chini yao, sasa unapokwenda kumpeleka Waziri Kiongozi ambaye unaamini huyu yuko chini yangu, unampeleka na Waziri Mkuu aliye juu ya Waziri Kiongozi, pana mazungumzo hapo? Si Hewallah Bwana!?
Tunataka tupate watu competent, wenye uwezo, kwa sehemu zote mbili. Wakishajadili na kukubaliana, sasa iundwe tume yenye wajumbe sawa sawa kutoka Tangayika na kutoka Zanzibar kuandika rasimu ya Katiba mpya ya Muungano.
Mwisho unaitishwa Mkutano Maalum wa Katiba, sio Bunge liliopo ulibadilishe kuwa Bunge la Katiba, hapana. Unaitisha wajumbe hasa waliochaguliwa na Wazanzibari na Watanganyika kwa madhumuni hayo ili wakatunge Katiba.
Hayo ndiyo matakwa ya Wazanzibari, na mimi nayazungumza kwa niaba yenu Wazanzibari.
Hayo ndiyo matakwa yetu, Mhe. Kikwete. Nyinyi mna tabia ya kutupuuza, Wazanzibari. Tangu wakati wa Maalim Aboud Jumbe, serikali iliandika mapendekezo kadhaa wa kadha kupeleka juu ya kuboresha Muungano, yakatiwa chini ya carpet. Wakati wa Dk. Salmin Amour, waliandika mapendekezo mbalimbali yakatiwa kwenyedustbin. Nina hakika chini ya Karume, nao wameandika hivyo hivyo. Lakini wenzetu wa Bara, mapendekezo kutoka Zanzibar hawayataki.
Na sisi wakati umefika kushikilia. Na kwa sababu sasa tumeungana, tumeshikamana, tudai. Nimwambie Kikwete aache tabia yake ya kutisha. Wakati wa kutisha umekwisha. Wakati wa kuburuzana umekwisha, hakuna anayeogopa tena. Tunalotaka ni haki itendeke.
Sasa kwa ufupi, naomba waandishi wa habari wanisikilize vizuri nitakayoyasema sasa hivi. Wanisikilize vizuri na waripoti kama nitakavyosema, na mimi nasema hivi: Muungano kama ulivyo sasa, narudia, Muungano kama ulivyo sasa, Wazanzibari hatuutaki. Haina maana kwamba hatutaki Muungano, lakini hatutaki Muungano kama ulivyo sasa. Mzee Karume alisema kwamba Muungano ni koti, likikubana unalivua. Na sisi Muungano huu wa sasa koti linatubana sana, kiasi ya kwamba ni sawa kuchukua koti la Mhe. Jussa umvishe Hamad Masoud. Litamtosha?
Tunataka sasa tushone koti jipya kwa mazingira ya karne ya 21.
Hakii.