Mheshimiwa IGP,
Watanzania wengi wanaupongeza uongozi wa jeshi la polisi kwa hatua ya kuwafikisha mahakamani baadhi ya vijana waliofanya shambulio la kiubakaji katika matundu matatu makubwa yaliyo katika mwili wa mwanamke, katika sehemu za mdomoni, ukeni na matakoni.
Lakini kuna dosari mbili ambazo zinaonekana kujitokeza na zinaweza kulifanya Jeshi la polisi kutiliwa mashaka katika namna yake ya kushughulikia suala hili.
Kwanza, tayari uchunguzi wa kipolisi umethibitisha katika upeo usio na shaka juu ya wasifu wa mtu aliyewatuma vijana hawa kufanya uhalifu huu.
Ushahidi usiokanushika uko hivi:
- Namba ya simu iliyokuwa inatumiwa na binti aliyebakwa imepokelewa na jeshi la pilisi;
- Binti aliyebakwa kataja namba ya simu ya mwanaume aliyekuwa anatongozana naye tangu mwanzo;
- Kitengo cha makosa ya mtandao kinao weledi mkubwa wa kukusanya ushahidi wa kielektroniki kwa kutimia namba hizi za simu;
- Mwanaume aliyekuwa anamtongoza huyu binti amemtaja mke wake kwa jina; na
- Vijana waliofanya ubakaji wamemtaja bosi wao kwa jina, yaani mtu aliyewatuma.
- Lakini bado "afande" huyo hajaunganishwa kwenye kesi.
Na pili, kuna watuhumiwa wawili hawakufikishwa mahakamanui kwa sababu hawajakamatwa hadi leo. Katika taifa hili ambako kila ekari moja ya mraba kuna "government security officer" (GSO) haiyumukiniki kwamba Jeshi la Polisi limeshindwa kazi yake ya “kusaka na kukamata” watuhumiwa hawa.
Badala yake imejengeka hisia kama ile iliyoanzia kwenye kesi ya Jamhuri dhidi ya Zombe na Wenzake 12, yaani, Kesi Na. No. 26 of 2006.
Katika kesi hii Zombe alichomoka kwa sababu mhusika mkuu aliyepokea na kutekeleza maagizo ya mauaji kutoka kwa Zombe, yaani CPL Saad, alilazimishwa kuwa “mgeni wa Mungu” kabla ya kufika mahakamani kutoa Ushahidi.
Hofu ya umma ni kwamba hawa vijana ambao hawajaunganishwa kwenye kesi hii ya binti wa Yombo wanaweza kufanyiwa “kitu mbaya” kama ilivyokuwa kwa yule CPL Saad.
Ukiweza kurekebisha dosari hizi mbili, itakuwa ni hatua kubwa katika kujenga Imani ya jamii kuhusu umakini na weledi wa Jeshi la Polisi.
Nimalizie kwa kufupisha maudhui ya kifungu cha 22 cha Sheria ya “Mkusanyiko wa Kanuni za Adhabu,”hapa chini, ili wasomaji wasio na muda wa kupekua aya zote za “Kanuni ya Adhabu” wasikwame. Kifungu hiki kinasema mambo manne:
- Mosi, mashtaka dhidi ya mtu aliyeshawishi wenzake kutenda kosa yanaweza kuendelea bila mtenda kosa halisi kushtakiwa kwanza;
- Pili, mashtaka dhidi ya mtenda kosa halisi yanaweza kuendelea bila mtu aliyeshawishi wenzake kutenda kosa hilo kushtakiwa kwanza;
- Tatu, mashtaka dhidi ya mtenda kosa halisi na dhidi ya mtu aliyeshawishi wenzake kutenda kosa yanaweza kuendelea kwa wakati mmoja kupitia kesi moja.
- Na nne, ushahidi wa kesi unanoga pale mtenda kosa na mtu aliyeshawishi kosa litendeke wanapounganishwa kwenye kesi moja kwa wakati mmoja.
Ni kwa sababu hii, Watanzania wanaomba sana mtu aliyeshawishi wale vijana kufanya ubakaji wa mdomoni, ukeni na matakoni dhidi ya yule binti wa Yombo, Dar, kuunganishwa kwenye kesi hii.
Picha za baadhi ya watuhumiwa katika sakata hili ni hizi hapa:
Watuhumiwa wanne wa ulawiti wakiwa mahakamani:
Assistant Superintendent of Police (ASP), Fatuma Kigondo, Afande anayetuhumiwa kuwatuma walawiti
Nakutakia utendaji kazi mwema,
Dr. Mama Amon,
Sumbawanga Town,
P.O.Box P/Bag,
Sumbawanga,
Tanzania.