Baada ya kuomba ushauri hapa jukwaani, watu walichangia kwa hekima, kuna waliosisitiza nikatoe mahala ninapoabudu pia kuna walionishauri nikatoe kwa watu wenye uhitaji.
Pia kunawaliosema nikatoe ninapoabudu halafu pia nikatoe kwa wahitaji.
WOTE MLIOCHANGIA, NAWASHUKURU SANA.
Mm na mke wangu tulionelea tukatoe kwenye kituo cha yatima.
Si kwamba hatuheshimu madhabahu, Ni kwamba uwezo wetu kwa sasa ni duni hatuwezi kumudu kutoa sehemu zote mbili.
Hata huko kwa yatima tulikoenda tulienda kwa aibu, maana tulichonacho nikidogo mno.
Ila mkipata nafasi nendeni mkawaone hao watoto, maana kwa mujibu wa alietupokea ni kwamba several times wanalia uji.
Ni hayo tu.
ITOSHE KUSEMA AHSANTE KWA USHIRIKIANO
Nilijizuia kusema cho chote kwenye uzi wa swali, lakini kwa kuwa umeshatekeleza, acha na mimi niseme kidogo kwa njia ya ushuhuda binafsi.
Kwa mtazamo wangu, fungu la kumi ni la Mungu. Na kama ndivyo, anaweza kuamua itakavyotumika.
Nilianza kujifunza masuala ya fungu la kumi kwenye miaka ya elfu mbili hivi, mmoja wa walimu wangu wa mwanzoni kabisa akiwa ni dada yangu katika ukoo ambaye tulikuwa tukisali madhehebu tofauti.
Alinifundisha kwa msisitizo mkubwa sana umuhimu wa kutoa fungu la kumi. Na aliniambia, mahali pekee pa kulitoa fungu la kumi ni Kanisani ninakoabudu (Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni, amebadilisha mtazamo).
Na mimi nilijitajidi kufanya hivyo tokea kipindi hicho.
Lakini miaka kadhaa baadaye, nikamsikia mtumishi mmoja akifundisha kuwa kwa kuwa fungu la kumi ni la Mungu, hupaswi kutoa tu mahali po pote, bali umwulize kwanza ndipo upeleke atakakokuelekeza. Kupitia mafundisho hayo, nilifahamu kuwa Mungu anaweza akakuelekeza ulipeleke hilo fungu la kumi Kanisani, kwa Mchungaji, kwa mtumishi, kwa yatima, kwa mjane, kwa mhitaji, n.k.
Siku zilienda, na hatimaye mwishoni mwa mwaka 2006, nikapata nafasi ya kulifanyisha hilo kazi. Baada ya kupata kimuujiza "kibarua" mahali fulani, nililitenga fungu la kumi, na kuiahidi nafasi yangu kuwa safari hiyo, sitapeleka tu Kanisani kama kama kawaida, bali atakakonielekeza Mungu. Japo sikujua angenijibuje, lakini nilidhamiria kuitii sauti Yake.
Niliichukua hiyo sadaka nikaiweka kwenye bahasha na kuanza kuiombea kila siku Mungu anielekeze anakotaka niipeleke. Niliomba kwa siku kadhaa lakini sikusikia chochote, wala kupata ishara yo yote ile kuhusiana na hilo.
Niliamua kubadilisha namna ya uombaji. Nilianza kuomba kwa kumweleza Mungu anijulishe anakotaka hiyo sadaka iende kati ya maeneo matatu: mahali nilikokuwa nikiabudi, kwenye huduma ya mtumishi fulani niliyekuwa nikibarikiwa sana na huduma yake, au kwa watoto yatima.
Kituo chenyewe cha watoto hakikuwa kikubwa. Ilikuwa ni huduma iliyoanzishwa na dada yangu katika ukoo (aliyenifundisha kutoa fungu la kumi) akishirikiana na rafiki yake. Kwa kuwa rafiki yake alikuwa na nyumba kubwa, na dada yangu alikuwa anapenda sana kuwasaidia watoto wahitaji, alimshwawishi rafiki yake
mpaka akakubali waitumie nyumba yake kuanzisha huduma ya watoto. Hawakuwa na maandalizi yo yote, waliamua kuanza na kidogo walichokuwa nacho.
Sasa, nilipokuwa nimeanza kuomba kwa kuyataja hayo maeneo matatu, kulitokea hali fulani ambayo niliichukulia kuwa ni ishara ya maombi kujibiwa. Siku moja niliamka, na nilipotaka kuendelea kuomba kumwuliza Mungu, sikujisikia kuomba. Na nilipofikiria kuipeleka hiyo sadaka Kanisani ninakoabudu au kwenye huduma ya mtumishi binafsi, moyo wangu ulikataa kabisa. Nilikuwa nikikosa amani kabisa kila nilipofikiria kuipeleka Kanisani au kwenye huduma ya mhubiri binafsi. Ilikuwa nikiwazia tu mojawapo ya hayo maeneo mawili, nilikuwa nahisi hali ya mshtuko wa kupgofya sana. Ni kama vile ningeenda kufa kama ningepeleka maeneo hayo.
Lakini nilipofikiria kuipeleka kwenye kituo cha watoto kilichokuwa kinasimamiwa na hao wadada, nilikuwa nikipata amani ya hali ya juu mno. Niliamua kusubiri hadi kesho yake kuona kama hiyo hali itabdilika.
Lakini hata kesho yake, hali ilikuwa vile vile. Kwa siku hiyo, niliamua kuwa siku hiyo, nitakapoenda kula chakula cha Mchana, nitaipeleka hiyo sadaka.
Mchana, baada ya kumaliza kula, kwenye saa tisa Alasiri, niliamua kuahirisha tena hadi Jioni nitakaporidi kutoka kazini. Kwa sababu nilikuwa nikifundisha tuisheni mahali fulani, nililichukua daftari lenye notisi nikaanza safari ya kwenda kwenye kipindi, akilini nikiwa na wazo kuwa nirudipo tu, naipeleka hiyo sadaka kwa hao wadada wanaowalea watoto wahitaji.
Lakini nilipokuwa njiani kuelekea kwenye kipindi, tena nikiwa nimefika katikakati ya safari, kulitokea kiti cha ajabu kilichoniogofya mno. Nilijishtukizia kama vile nimekamatwa bega la kulia na kushoto na kugeuzwa ghafala kwa nguvu nikajikuta nimetazama nilikotokea. Sikumwona mtu yeyote aliyenishika na kunigeuza, lakini nilielewa maana yake.
Kwa haraka sana , nilienda hadi nyumbani nikaitupa mezani daftari na kuichukua hiyo sadaka ambayo tayari nilikuwa nimeshaiweka kwenye bahasha, na moja kwa moja hadi nyumbani wanakolelewa hao watoto wahitaji.
Nilimkuta mmoja wa hao wasimamizi wa hicho kituo. Dada "yangu" yeye hakuwepo muda huo.
Nilipofika, nilimkabidhi hiyo bahasha huyo niliyemkuta na kumwambia huo ni i ujumbe niliopata kibali kuupeleka hapo. Nilikwepa kumwambia kuwa ni fungu la kumi kwa sababu nilihofia huenda wasingepokea. Baada tu ya kukabidhi na kumwambia hayo, alitamka hivi"Mungu wa Israeli", na kubaki akiwa ameduwaa. Ili asije akapata nafasi ya kunihoji, niliamua kuaga na kuondoka huku yeye akiwa angali ameduwaa. Wakati naondoka, na mimi nilikuwa namshangaa kilichomduwaza wakati hajui kilichomo humo kwenye bahasha niliyomkabidhi.
Siku chache baadaye, nilionana na mwenzake ambaye hakusita kunisimulia ushuhuda waliotendewa na Mungu kwenye huduma yao ya kuhudumia watoto.
Alinisimulia kuwa siku niliyopeleka hiyo sadaka, walikuwa wameishiwa na mahitaji muhimu ukiwemo unga. Na Jana yake Usiku, baada ya kushauriana cha kufanya, waligundua kuwa hawakuwa na ujanja zaidi ya kuomba. Walikubaliana kumwomba Mungu kwa kuisimamia Ahadi ya Neno Lake kuwa Yeye ni Baba wa yatima. Walimweleza kuwa watoto Wake hawakuwa na chakula kwa hiyo awapelekee hela ya chakula.
Aliendelea kunisimulia kuwa Usiku, Mungu "aliwaonesha" kuwa kesho yake hela itapelekwa. Kwa hiyo kilipokucha, walimshikuru Mungu na kuendelea kusubiria pesa kwa shauku kubwa mno.
Asubuhi ilipita bila ya hela kupelekwa. Mchana nao ukapita vivyo hivyo. Kumbuka watoto walikuwa hawana hata unga wa uji, na walishakubaliana kuwa hawataenda kukopa popote, watasubiria mpaka Mungu awapelekee. Ingelikuwa ni wewe ungefanyeje? Unafikiri wao walifanyeje zaidi ya kumwuliza Mungu pesa aliyowaahidi?
Mpaka hapo, kama unaamini kuwa ni kweli Mungu aliwaonesha hela ikipelekwa hapo kituoni kwao, utanilewa ni nini kilichonigeuza ghafla kinyume na ratiba yangu na hatimaye nikaenda kuipeleka hiyo hela.
Kwa hiyo ungeniuliza mimi suala la fungu la kumi, ningekujibu kuwa ni sahihi kupeleka Kanisani, ni sahihi kuwapa watumishi wa Mungu, ni sahihi kuwapa yatima, wajane, wahitaji mbali mbali, n.k. lakini muhimu, msikilize Mungu kwanza.
Mungu akisema nawe, na ukawa na uhakika kuwa ni Mungu, fanya akuambiavyo hata kama ni kinyume na dini yenu.