Chama cha demokrasia na maendeleo
CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu 2025 kimekuwa kikiendesha ajenda inayojulikana kama 'No reforms, No election' yenye lengo la kuhamasisha na kuchochea kufanyika kwa
mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili kuwezesha uchaguzi huru na wenye haki ili kuepusha malalamiko yaliyotokana na mapungufu yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita. Kupitia ajenda hiyo mara kwa mara, chama hicho kimekuwa kikisisitiza kuwa bila mabadiliko hakutakuwa na uchaguzi.
Mara kadhaa kumekuwapo na taarifa potoshi zinazosambazwa mtandaoni kuhusu ushiriki wa CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu 2025. Rejea taarifa zilizohakikiwa na kuhifadhiwa
hapa,
hapa na
hapa.
Madai
Ipo taarifa inayosambazwa mtandaoni kuwa msajili wa vyama vya siasa amekiri kupokea barua ya CHADEMA kushiriki uchaguzi mkuu 2025, huku ikitumia utambulisho wa grafiki za ITV.
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu umejiridhisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli, kwani haijatolewa na msajili wa vyama vya siasa nchini.
Vilevile grafiki iliyotumika kusambaza taarifa hiyo ni ya kughushi kwani haijachapishwa na ITV. Hata hivyo yamebainika mapungufu kadhaa ambayo yanadhihirisha kuwa taarifa hiyo ni ya kutengenezwa na wapotoshaji. Mathalani picha inayomuonesha Msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis S. Mutungi imehaririwa ili kuonesha ameshikilia barua ambayo ni ya kughushi. Rejea picha halisi
hapa.
Pia muundo wa barua inayoonekana haufanani na muundo rasmi ambao hutumiwa na CHADEMA, mfano sehemu ya nembo ya chama, kasoro za kiuandishi mathalani kutokufuata mpangilio sahihi wa sentensi.