Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 23,526
- 34,057
Weka ushahidi Mkuu
Mystery,
Nakuwekea hapa ushahidi wa matatizo yaliyotokea mara baada ya uhuru kama
nilivyoandika katika kitabu changu, ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes...'':
Uthibitisho wa Njama Dhidi ya Uislam
Hivi sasa kuna vitabu viwili vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe vinavyothibitisha kuwa Wakristo wametumia nyadhifa zao katika serikali kuuhujumu Uislam na Waislam. Jan P van Bergen katika kitabu chake, ''Development and Religion in Tanzania,(1981),'' ametoboa siri kuhusu uadui aliokuwa nao Rais Mstaafu, Nyerere dhidi ya Uislam na Waislam. Kitabu kinaeleza kwa ufasaha jinsi Nyerere wakati alipokuwa madarakani alivyokuwa akifanya mikutano ya siri na viongozi wa Kanisa kuweka mikakati ya kuupa nguvu Ukristo. Katika mikutano hiyo Nyerere aliwahakikishia viongozi wa Kanisa kuwa anaaunga mkono Ukristo. Kitabu hicho kinaeleza jinsi Nyerere alivyotimiza ahadi yake hiyo kwa Kanisa kwa kuhakikisha kuwa anawapa Wakristo nafasi za juu katika serikali na chama. Kitabu hiki kilikuwa kinauzwa Catholic Bookshop, Dar es Salaam. Lakini ilipokuja kudhihirikia Kanisa kuwa kitabu hiki kilikuwa kinatoa habari nyeti na siri za Kanisa kuhusu njama dhidi ya Waislam, kwa haraka sana kikaacha kuuzwa. Hadi hivi sasa kitabu hicho ni marufuku kuletwa tena Tanzania.
Kitabu cha pili ni cha Dr John C. Sivalon, ''Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985 (1992).'' Kitabu hiki kinaeleza njama ndani ya serikali kuuhujumu Uislam. Sivalon anafichua kuwa kuanzia mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru, Kanisa lilikuwa na hofu mbili. Hofu ya kwanza ilikuwa umoja wa madhehebu za Kiislam kati ya Sunni, Bohora, Ismailia na Ithnasheri. Hofu ya pili ilikuwa kuhamishwa kwa makao makuu ya EAMWS kutoka Mombasa kuja Dar es Salaam. Kanisa lilikuwa linahofu kuwa mali walizokuwanazo Waasia Waislam zikitiwa katika harakati za Waislam ambao walikuwa na nguvu kubwa katika uwanja wa siasa zitaathiri maslahi ya Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Kwa ajili hii Kanisa likatanganza kuwa Uislam ni adui wake na ikaanza mikakati ya hujma dhidi ya Uislam ili kuudhoofisha.
Kuna kazi mbili zilizoandikwa na Waislam kuhusu uhusiano baina ya serikali na Waislam. Kazi ya kwanza ni tasnifu ya Kiwanuka, ‘’The Politics of Islam in Bukoba Districtí (1973);’’ kazi ya pili ni makala ya utafiti ‘’Islam and Politics in Tanzaniaí (1989)’’ iliyoandikwana mwandishi wa kitabu hiki. Ilikuwa baada ya kusoma tasnifu ya Kiwanuka na kuona jinsi ukweli wa kuvunjwa kwa EAMWS kulivyopoteshwa ndipo kama Muislam na kama ada ya Uislam inavyodai kuwa pande mbili za mgogoro zote lazima zisikilizwe, ndipo nilipoamua kufanya utafiti na kuandika tatizo lile kwa mtazamo wa Waislam. Ukweli ambao kwa miongo miwili ulizuiwa usifahamike kwa Waislam. Kiwanuka anadai na kuafiki kuwa Nyerere alikuwa na haki ya kutumia vyombo vya dola dhidi ya Waislam kwa kuwa kama asingefanya hivyo nchi ingekuwa na mamlaka mbili, yaani ya Waislam na ya serikali. Kwa ajili hii aliamua kuivunja EAMWS ili ‘’kulinda umoja wa kitaifa.’’
Halikadhalika ipo ‘’Kwikima Report (1968),’’ ambayo imeeleza kwa ufasaha tatizo la EAMWS, chanzo chake na mchango wa serikali katika kuhujumu umoja wa Waislam. Taarifa hii inafaa kutumika leo kama dira ya kuelewa tatizo la Waislam wa Tanzania kama ilivyokuwa wakati ule ilipotolewa kwa mara ya kwanza. Taarifa ya Kwikima inaeleza jinsi TANU, serikali na Waislam wachache katika TANU walivyodanganyika kudhani kuwa katika kuisaidia serikali kuivunja nguvu EAMWS walikuwa wanatimiza uzalendo na maslahi ya taifa. Rejea hizi tano ni muhimu kwa wanafunzi wa historia ya siasa Tanzania; na kwa mtafiti yeyote anaetaka kujua chanzo cha chuki baina ya Waislam na serikali na chanzo cha hisia kali za kidini zinazoikumba nchi yetu kuanzia miaka ya 1980. Rejea zote hizo za vitabu, makala za utafiti na taarifa mbalimbali, ingawa zimeandikwa na waandishi tofauti na kwa muelekeo tofauti zote hizi zinadhihirisha kitu kimoja, kuwepo kwa njama zinazoendelea kwa zaidi ya karne moja dhidi ya Uislam na Waislam, kwanza zilikuwa zikifanywa na wakoloni walioitawala Tanganyika na sasa zinafanywa na Wakristo wananchi kuhakikisha kuwa Uislam haupati nguvu.