Jidu La Mabambasi
JF-Expert Member
- Oct 20, 2014
- 18,653
- 31,010
PROFESA ASHANGAA SERIKALI YA TANZANIA KUWAKAMATA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU!
Baada ya serikali ya Tanzania kuwakamata kwa tuhuma za kuchochea maandamano wahadhiri watatu na kuwanyima dhamana, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam enzi za utawala wa Julius Nyerere, Prof. Joseph Mbele amedai kuwa vichwa vya watu wanaoitawala Tanzania vimepwaya.
Prof. Mbele ametoa maoni hayo katika ukurasa wa Askofu Mwamakula wakati akichangia hoja katika andiko lake juu ya mhadhiri wa Chuo cha Dodoma, Melkisedeki Kaijage aliyekatamatwa na Jeshi la Polisi na kisha kunyimwa dhamana.
Wahadhiri wengine wawili wa Chuo Kikuu, St. John's University of Tanzania kule Dodoma ambao ni Johaiven Revelian Bikongolo na Titus Kituli nao wanaelezwa kukamatwa 3 Julai 2026 kwa tuhuma za kuchochea maandamano nao wamenyimwa dhamana. Soma kwa kina andiko la profesa hapa chini
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Itunge, Dar es Salaam; 20 Julai 2026; Saa 5:10 asubuhi
WATAWALA WAMEPWAYA VICHWANI MWAO
Duniani, vyuo vikuu vinafahamika kuwa taasisi zenye uhuru wa pekee, maarufu kama "academic freedom." Vyuo vikuu vinahesabika kama mahali ambapo watu wanatafiti na kutafuta ukweli bila kipingamizi, wanahoji na kuchambua mambo, wanalumbana, na wanachochea fikra.
Kuhusu hili suala la uhuru wa chuo kikuu, Mwalimu Nyerere alishaliweka wazi kwa mateńdo yake na kauli zake. Mfano hai ni hotuba yake "Relevance and Dar es Salaam University" ya 28 Agosti, 1971, ambayo ilichapishwa katika kitabu chake "Freedom and Development/Uhuru na Maendeleo" (Oxford University Press, 1973), kurasa 192-203.
Ninaposema matendo, ninakumbushia kwa mfano alivyokuwa anakuja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupambana na wanachuo kwa hoja. Nilishuhudia mimi mwenyewe tangu nilipoanza kusoma pale mwaka 1973 na nilipohitimu mwaka 1976 nikachaguliwa kubaki pale kama mhadhiri. Nilishuhudia jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa anashambuliwa kwa hoja na yeye anajibu mapigo na kushambulia. Aliheshimu sana "academic freedom."
Wanachuo kwa ujumla tulipinga nadharia yake ya "Ujamaa wa ki-Afrika" kwa msingi kwamba haikuzingatia suala la matabaka na ukinzani wa matabaka ("classes and class struggles"). Sisi tulipigania kile tulichoita kuwa "scientific socialism" na hapo ndipo mtifuano kazi yetu na Mwalimu Nyerere ulipojikita. Lakini aliheshimu uhuru wa malumbano, wala hakuleta vyombo vya dola kutukamata au kutupiga mabomu.
Katika maandishi yake, si hilo nililotaja hapa juu pekee, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba Chuo Kikuu kina wajibu wa kutafiti mambo ya nchini, kama vile siasa, uchumi, na matatizo mbali mbali, sambamba na kutafiti mambo ya ulimwengu. Mwalimu Nyerere aliwaasa sana waTanzania kutoingilia uhuru wa Chuo Kikuu hata pale wanachuo wanapoibua hoja na fikra zilizo kinyume na ilivyozoeleka katika jamii.
Mwalimu Nyerere alikuwa anahimiza uthubutu wa namna hiyo. Alikuwa ni msomi, ambaye alitambua wajibu wa wasomi. Leo ni wazi kuwa nchi imo mikononi mwa watu ambao hata maandishi ya Mwalimu Nyerere hawayasomi. Yaani wapo wapo tu, vichwani kumepwaya, ila kwa mbwembwe na vitisho dhidi ya wananchi hawajambo.
Prof. Joseph Mbele,
Chuo Kikuu, Olaf College, USA; 20 Julai 2026
Toka mitandaoni, kuna kitu cha kujifunza hapa.