Mswada wa sheria ya kuunda Baraza la Usalama wa Taifa wakataliwa!

Mswada wa sheria ya kuunda Baraza la Usalama wa Taifa wakataliwa!

Wabunge waikaanga serikali

• Waziri Simba agaragazwa, apewa pole

na Rahel Chizoza na Hellen Ngoromera, Dodoma

KATIKA kile kinachoonekana kugoma kuburuzwa na serikali wabunge kwa mara ya pili jana wamegoma kuupitisha muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa wa mwaka 2009.

Muswada huo uliowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, umeibua mjadala mkubwa kwa wabunge ambao wameweka bayana serikali isipokuwa makini kuna kila dalili ikashindwa kuendelea.

Kukwama kwa muswada huo hiyo jana ilikuwa ni mara ya pili baada ya mwaka jana kupelekwa bungeni na wabunge kuukataa kwa madai kuwa una upungufu mkubwa lakini haukuweza kufanyiwa marekebisho kama walivyopendekeza wabunge.

Muswada huo ambao ulikuwa ukitarajia kupitishwa pasi na upinzani ulijikuta unakwama baada ya wabunge kubaini kuwa serikali ilikaidi mapendekezo yao ya kuuboresha na kuamua kuupeleka bungeni kama ulivyokuwa awali.

Wabunge wote waliochangia kuhusu muswada huo walionyesha kutoridhika nao huku wengine wakitamka wazi kutouunga mkono isipokuwa Mbunge wa Nkasi, Ponsiano Nyami (CCM), ambaye alitamka kuuunga mkono mara tatu wakati akichangia.

Wabunge hao wamebainisha kuwa muswada huo unakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuingilia madaraka ya Rais kwa kumuundia chombo ambacho kitafanya kazi zake za ulinzi na usalama wa nchi.

Aliyefungua pazia katika kuupinga muswada huo ni mwanasiasa mkongwe na mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM), ambaye alisema hakubaliani nao hasa katika suala zima la wajumbe wa Baraza la Ulinzi na Usalama wa Taifa.

Ngwilizi alisema baraza hilo lina mlolongo wa watu wengi ambao ni kama vile kuunda baraza jingine jipya la mawaziri na kuwa litakuwa si baraza la usalama tena bali ni suala la kisiasa.

“Mimi naona hili ni baraza la pili la mawaziri, maana katika hali ya kawaida haiwezekani chombo muhimu kama hiki kikawa na mlolongo mkubwa wa watu kiasi hiki, kuna siri gani tena hapa. Mimi sikubaliani na hili!” alisema Ngwilizi.

Alibainisha kuwa kutokana na wingi wa wajumbe ambao kwa mujibu wa muswada watakuwa si chini ya wajumbe 15, haitakuwepo tena maana ya siri kwani hata masuala ya Usalama wa Taifa yatakayojadiliwa si ajabu kesho yake yakawa kwenye magazeti.

“Tunataka kuwa na baraza la mawaziri jingine au baraza la usalama? Mambo ya Usalama wa Taifa ni siri kwa nini tuwe na watu wengi kiasi hiki? Kikatiba chombo cha kumshauri rais kipo; siona haja ya baraza hili!” alisisitiza Ngwilizi.

Naye mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM), alisema chombo hicho ni hatari kwa usalama wa nchi kutokana na wingi wa wajumbe wake ambao si rahisi kwa kila mmoja wao kutunza siri nzito zihusuzo nchi.

Dialo alisema kuundwa kwa baraza hilo kutaongeza matumizi ya serikali bila sababu na tayari kuna vyombo vinavyotekeleza majukumu yanayotaka kutolewa kwa baraza hilo.

“Inaonekana Bunge halina kazi ya kufanya ndiyo maana hata tunaletewa hii miswada mingine, ni vizuri kuangalia kitu kinachopelekwa bungeni kabla ya kuwasilishwa,” alisema Dialo.

Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, ndiye alikuwa wa kwanza kuja na mtazamo tofauti wa kutaka muswada huo urejeshwe serikalini kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho; hoja ambayo iliungwa mkono na Mbunge wa Mtera na Waziri Mkuu wa Zamani, John Samwel Malecela.

Dk. Slaa alisema muswada huo unalenga kunyang’anya madaraka ya rais na kuwa iwapo utapitishwa utaiweka nchi pabaya.

Alihoji sababu za kuletwa bungeni kwa muswada huo ukiwa bado haujafanyiwa marekebisho.

“Ninachojua mwanzoni muswada huu uliletwa, ukarudi ili ufanyiwe marekebisho lakini sioni kilichorekebishwa maana umekuja kama ulivyokuwa na kama umerekebishwa basi wamedonoa donoa tu kwani hoja tulizozikataa ziko palepale,” alisema Dk. Slaa.

Alibainisha kuwa Bunge ni chombo makini na muhimu hivyo hakiwezi kutoa maamuzi ambayo kinajua kwamba yataleta athari kwa taifa na kutoa hoja ya kutaka muswada huo upangiwe muda mwingine wa kuwasilishwa utakapoiva.

Naye Mbunge wa Mtera, John Malecela, aliunga mkono hoja ya Dk. Slaa kwa kulitaka Bunge liahirishe muswada huo na kuuwasilisha siku nyingine jambo ambalo lilisababisha Naibu Spika Anna Makinda kusitisha mijadala na kumuita mtoa hoja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, alitumia kanuni ya namba 87(1) na kukubali hoja iliyotolewa na Dk. Slaa na Dk. Malecela ya kuurudisha muswada huo katika Kamati ya Sheria na Katiba kwa lengo la kupitiwa upya na kufanyiwa marekebisho.

Waziri huyo aliomba kupangiwa siku nyingine ya kuwasilishwa kwa muswada huo bungeni kabla ya kumalizika kwa mkutano wa kumi na nane wa Bunge.

Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Tanzania Daima Jumapili, lilimshuhudia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko, Dk. Mary Nagu , Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia na Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Margaret Sitta, wakimpa mkono wa pole Waziri Simba.

Wakizungumza nje ya ukumbi wa Bunge kwa nyakati tofauti baadhi ya wabunge waliunga mkono hoja ya kuahirishwa kwa muswada huo ambao wakati unawasilishwa kwa mara ya kwanza pia ulipingwa ukitakiwa kujadiliwa upya katika Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ili kurekebisha mapungufu yaliyopo.

Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema utaratibu wa kuleta miswada isiyokidhi masilahi ya taifa ni mbovu kwani unaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa.

Alisema kitendo cha kumwekea rais watu wapige kura katika maamuzi ya usalama ni cha hatari. Rashid aliunga mkono hoja ya kutokuwepo kwa msululu wa wajumbe wa Baraza la Usalama wa Taifa.

Naye Mbunge wa Kahama, James Lembeli(CCM), alisema maamuzi yaliyotolewa bungeni ni mazuri na kwamba anayaunga mkono na kwamba kitendo cha muswada huo kurudishwa kwa mara ya pili bungeni na kukataliwa tena ni tatizo kwa serikali.
 
teh teh mambo haya bwana...kazi kweli kweli
 
Kila apandacho mtu ndicho atakachovuna! Ukipanda maharage kamwe usitegemee kuvuna mahindi!
 
Mods please unganisha naile makala ya usalama wa taifa ya happy
 
kama watu wa usalama wa taifa wameshindwa kupitia mswada wao wenyewe je wataweza kuilinda nchi zidi ya mikataba mibovu,ufisadi, na utawala mbaya, yani mswada wao hadi unawashangaza wabunge kwani kuna kasoro nyingi mno,

je usalama wa taifa utaweza kuokoa jahazi wakati wao wamejishindwa kujiokoa ?
 
kama watu wa usalama wa taifa wameshindwa kupitia mswada wao wenyewe je wataweza kuilinda nchi zidi ya mikataba mibovu,ufisadi, na utawala mbaya, yani mswada wao hadi unawashangaza wabunge kwani kuna kasoro nyingi mno,

je usalama wa taifa utaweza kuokoa jahazi wakati wao wamejishindwa kujiokoa ?

Sasa hii ni news kweli, tena Breaking news??? Mod saidia kurekebisha heading ya hii kitu!!!
 
Back
Top Bottom