Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
SHEIKH YUSUF BADI WA LINDI
Inaaminika kuwa hakuna picha ya Sheikh Yusuf Badi popote kwani alikuwa hapendi kupigwa picha.
Juhudi zangu za kupata picha yake hazijafanikiwa hadi hivi sasa.
Rafiki yangu ameweka kibao cha mtaa wenye jina ‘’Sheikh Badi.’’
Mtaa huu uko Lindi.
Nimelisikia jina la Sheikh Yusuf Badi Lindi mjini miaka mingi iliyopita wakati nafanya utafiti wa kitabu cha historia ya TANU kupitia maisha ya Abdulwahid Sykes.
Siku ya kwanza nilianza mahojiano yangu na Salum Mpunga tukiwa tumekaa kwenye kibaraza za msikiti mkubwa wa Lindi mjini ulioko karibu na kituo cha mabasi.
Baada ya mazungumzo yangu na Salum Mpunga siku ya pili asubuhi nikawa na mazungumzo na Yusuf Chembera nyumbani kwake kwenye varanda yake ndogo lakini nadhifu.
Hawa watu wawili Salum Mpunga na Yusuf Chembera ndiyo waasisi wa TANU Southern Province mwaka wa 1955.
Kisa cha wazalendo hawa na jinsi walivyoweza kumleta Mwalimu Nyerere Southern Province ni kisa cha kusisimua sana.
Sasa niko na Yusuf Chembera nyumbani kwake mwezi wa Ramadhani.
Yusuf Chembera anasema Kiswahili kizuri na alikuwa mtu fasaha sana akijua kupanga maneno yake.
Alianza kunieleza historia ya TANU kwa kunitajia maisha yake ya udogoni na hapo ndipo kwa mara ya kwanza nikalisikia jina la Sheikh Yusuf Badi.
‘’Nilipofika umri wa kusoma baba yangu akanipeleka chuoni kwa Sheikh Yusuf Badi kusoma.
Chuo cha Sheikh Badi ndicho kilikuwa chuo kikubwa na yeye mwenyewe alikuwa sheikh akiheshimika kusini nzima.’’
Yusuf Chembera akanieleza yote waliyokutananayo katika kuasisi TANU wakisaidiana na mzee wao Suleiman Masudi Mnonji ambae nyumba yake ndiyo ilikuwa ofisi ya TANU ya kwanza Lindi.
Southern Province kulikuwa na vitisho vingi dhidi ya TANU watu wakitishwa kwa kuambiwa kuwa TANU ni chama cha Waislam ambao wanataka kuleta vita vingine vya Maji Maji.
Uongozi wa TANU Lindi ukaamua kumtuma Salum Mpunga na Ali Ibrahim Mnjale Dar es Salaam kumwalika Nyerere aje Lindi ili asafishe hii propaganda na wananchi waiunge mkono TANU kupigania uhuru wa Tanganyika.
Nyerere akiongozana na Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifika Lindi, Mikindani, Masasi na Nachingwea na baada ya ziara hii TANU haikuwa tena na kizuizi ila watu walijiunga na chama kwa wingi.
Hii ilikuwa mwaka wa 1955 na Nyerere alikuwa amekwenda na kurudi UNO safari ya kwanza.
Mwaka wa 1956 Nyerere alirejea tena Lindi na safari hii mapokezi yake yalikuwa makubwa na ya kupendeza.
Katika ile safari ya kwanza serikali ilikataza maandamano ya kumpokea Nyerere mjini.
Ilibidi Nyerere na ujumbe wake upokelewe kijiji cha Mbanji nje ya mji na wanachama wa TANU waingie mjini kimya kimya na wageni wao kama vile wanasindikiza msiba.
Mara baada ya safari ya kwanza ya Nyerere Lindi ili kukipa chama nguvu mwanafunzi wa Sheikh Yusuf Badi, Yusuf Chembera alimfuata mwalimu na sheikh wake Sheikh Badi kumuomba ajiunge na TANU ili chama kipate nguvu.
Sheikh Yusuf Badi alipojiunga na TANU alikuja na jeshi kubwa la na murid wake wa Tariqa Qadiriyya.
Sheikh Yusuf Badi aliipa TANU mjini Lindi na pembezoni heshima kubwa.
Mwaka wa 1956 Nyerere alipokuja Lindi hali ya TANU ilikuwa imebadilika chama kikiwa na nguvu kubwa isiyo na kifani.
Katika mapokezi ya Nyerere Sheikh Yusuf Badi alitoka na chuo chake na wanafunzi wake kwa maandamano wanafunzi wakipiga dufu huku wakisoma kasida sauti za matari zikisikika kote.
Hii ilikuwa siku ya shamrashamra kubwa mjini Lindi.
Usiku wake Mtaa wa Makonde nyumbani kwa Suleiman Masudi Mnonji Sheikh Yusuf Badi alifanya dua kubwa iliyohudhuria na Waislam aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo.
Dua hii ilihudhuriwa pia na masheikh wengine maarufu pale Lindi na kutoka vijiji jirani.
Katika dua hii alikuwapo Bi. Sharifa bint Mzee mmoja wa akina mama waliofanya kazi kubwa kuwavuta wanawake kujiunga na TANU.
Mussa Athumani Lukundu, kiongozi wa Dockworkers Union Lindi aliandaa karamu kubwa kwa heshima ya Nyerere.
Siku ya ukumbusho mkubwa sana mjini Lindi ilikuwa siku ya uhuru, tarehe 9 Desemba, 1961.
Sheikh Badi, ambae alikuwa bingwa wa kutunga mashairi, aliombwa na TANU kuandika hotuba ya uhuru.
Hotuba hii ilisomwa na mwanafunzi wake Yusuf Chembera mbele ya DC akiwa kama mwakilishi wa utawala wa Kiiereza uliokuwa uking’oka.
Hotuba hiyo ya Sheikh Badi iliandikwa kwa Kiarabu na Chembera alinionyesha nikaishika kwa mikono yangu.
Sheikh Badi hakuona kama ipo hotuba yoyote iliyoandikwa na mwanadamu iliyostahiki hafla kama ile ya siku ya kujikomboa kutoka minyororo ya ukoloni.
Sheikh Badi alimsomea mwanafunzi wake Chembera, dua ya kunut ambayo husomwa na Waislam katika kila sala ya alfajir.
Usiku wa manane wa tarehe 9 Desemba, 1961 ulikuwa usiku adhim sana kwa wote wawili, mwalimu na mwanafunzi wake, pale watu walipokusanyika katika Uwanja wa Gofu kumsikiliza Chembera akisoma kunut kupokea uhuru wa Tanganyika.
Maspika yalisikika yakitoa sauti ya Yusuf Chembera akisoma Dua ya Kunut na wananchi wakiitika Amin, Amin, Amin.
Hakuna popote jambo kama hili lilitokea katika kupokea uhuru wa Tanganyika.
Hakika kwa watu wa Lindi hawakukosea kumpa mtaa Sheikh Yusuf Badi.
Sheikh Badi anastahili kukumbukwa na anastahili heshima hii.
Picha ya kwanza Mtaa wa Sheikh Badi, Bi. Sharifa bint Mzee katika utu uzima na wajukuu zake, Yusuf Chembera na Salum Mpunga.