Mtambo Wa Mauti

Mtambo Wa Mauti

19.
Muda mfupi baadaye.

“Ni kweli hujui… Hujui kama unabaka. Na unambaka afisa

wa ngazi ya juu wa Jeshi la Polisi…” Kicheko.

“Sikujua… nilidhani mimi pia nimebakwa.” Kicheko.

“Ni wazi kuwa hujaipitia vizuri sheria ya ubakaji. Mwanaume habakwi, anabaka. Unaijua adhabu yake?”

“Sijui.”

“Miaka ishirini na minane jela. Lakini kwako wewe adhabu hiyo haitoshi. Utafungwa kifungo cha maisha, pingu mkononi.”

Kicheko.

“Naanza lini kuitumikia adhabu hiyo?”

“Toka sasa uko chini ya ulinzi. Huruhusiwi kukutana na mwanamke mwingine. Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…”

Kicheko. Usingizi…

Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyomjia Joram hayo yalikuwa maongezi yake ya mwisho na Mona Lisa kabla hajaamka na kujikuta akiwa amekumbatia maiti yake, tundu kubwa la risasi kifuani pake likiendelea kuvuja damu.

Huo ulikuwa usiku wa Jumamosi au alfajiri ya Jumapili. Kilichomshangaza ni hii hadithi mpya ya kuwa leo ni Jumatatu. Ukweli ni upi, Jumapili au Jumatatu?

Joram hakuona kama alikuwa na haja ya kuupoteza muda wake kufikiria kama leo ilikuwa Jumapili au Jumatatu. Kama daktari ameandika tarehe ya Jumatatu na kama hata gazeti lilikuwa la Jumatatu, kwa vyovyote siku ya leo ni Jumatatu. Alichohitaji kufanya ilikuwa ni kukusanya akili yake ili imwambie kitu gani kilimtokea hata akalala kwa saa ishirini na nne bila kujua kinachoendelea.

Ilikuwaje? Alijiuliza.





Taratibu, ule utandu uliokuwa ukiudumaza ubongo wake ukaanza kumtoka na picha mpya kuingia akilini. Ilikuwa kama mkanda wa video ambao unarudishwa nyuma na kuchezeshwa upya.

Sasa alikumbuka vizuri kabisa kuwa mara baada ya Mona kumwambia, “Huruhusiwi kuoa wala kuolewa…” na usingizi kuwachukua, Mona Lisa alitoweka.

Joram alibaini kutoweka huko pale alipoamka na kushituka mida fulani baina ya saa tatu au nne na kujikuta peke yake. Ubavuni mwake, pale alipolala Mona Lisa, sasa palikuwa na mto ambao yeye, Joram, aliukumbatia. Hakujali, akijua kuwa msichana huyo alikuwa ameondoka kimyakimya kwa kuchelea kumsumbua. Akaurudia usingizi wake ambao aliuchapa hadi saa saba za mchana huo. Baada ya kuoga, kunywa supu na chupa mbili za club soda alirejea chumbani kwake ambako alijilaza chali na kuendelea na mswada wa Mona, UBONGO WA MWALIMU NYERERE.

Ilikuwa riwaya tamu. Ilimvutia na kumsisimua kiasi kwamba alijikuta amezama moja kwa moja katika msitu huo wa maneno yaliyopangiliwa kisanii. Ilimwia vigumu zaidi kuamini kuwa mbunifu mwenyewe alikuwa msichana mpole na mrembo kama yule. Ufundi wa matumizi ya lugha, hila katika mpangilio wa matukio na zaidi ya yote uhalisia wa matukio ya mambo katika hadithi hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram amezwe moja kwa moja, bila kujua kuwa muda umekwenda, hadi aliposikia mlango wake ukigongwa.
 
20.
Kabla ya kuinuka kuufungua aliitazama saa yake ya mkononi. Tatu kasoro! Hakuamini. Alipoufungua mlango umbile zuri la Mona Lisa lilikuwa limesimama pale, tabasamu lenye hayahaya na kutojiamini likiwa limechanua usoni pake. “Darling! Karibu sana,” Joram alisema akimshika mkono na kumvuta ndani ambako alimkaribisha tena kwa busu jingine. Kiasi fulani Mona Lisa alionyesha kushangazwa na mapokezi hayo. Alimtazama Joram kwa muda, kisha akayakwepa macho yake na kujiinamia. Joram pia alishangazwa na hali hiyo. Muda mfupi tu uliopita ulikuwa mchangamfu kuliko mie, mara hii umebadilika tena! Achana na tabia hizo za kinyonga!





Alitamani kumweleza. Lakini hakufanya hivyo. Badala yake alimwambia taratibu, “Chumba hiki chako, chagua kukaa ama kitandani, ama kwenye kochi.”

Mona aliliendea kochi na kuketi.

“Kitabu chako kimenishika kwelikweli,” Joram alimwambia. “Sikujua kama muda umeisha kiasi hiki. Nikuagizie chakula na kinywaji gani?”

Mona alitabasamu, “Kizuri?” “Kitu gani?”

“Kitabu. Ni kizuri kweli?”

Joram akatabasamu. “Kizuri kama alivyo mtu aliyekiandika. Kikitoka utapata washabiki kila pembe ya dunia. Utakula nini?”

“Unaamini kitakubaliwa?” Mona alihoji tena kwa shahuku. “Ni mchapishaji kipofu wa taaluma peke yake anayeweza kukataa kitabu kama hiki. Ingawa kuna mambo mawili matatu atakayoyatoa na kuyaongeza. Hata hivyo, sijafika mwisho,”

Joram akasita, “Hujaniambia utakula nini na utakunywa nini.”

Ilikuwa dhahiri kuwa akili za Mona hazikuwa kwenye chakula wala kinywaji, bali kwenye maandishi yake, hali ambayo ilimshangaza Joram. Jana hakukitaja kabisa kitabu hicho, leo hataki kusikia jambo lolote zaidi ya kitabu.

Kinyonga!

“Siwezi kukaa hapa na msichana mrembo kama wewe, bila kumkirimu walao maji ya uhai. Nawapigia jikoni watuletee kuku mzima, chupa mbili za wiski na tonic. Sawa?”

Joram alisubiri jibu la Mona Lisa.

“Samahani sijisikii kula wala kunywa chochote.” “Kwa nini? Za jana bado zipo kichwani?”

“Jana!” ilikuwa zamu ya Mona Lisa kushangaa. “Jana nimekunywa wapi! Sijawahi kunywa pombe toka nizaliwe.”

Joram hakuyaamini masikio yake.

“Wacha mzaha Mona,” akamwambia akicheka. “Jana umerudi hapa ukanipa company ya nguvu, ukanywa kiasi cha kunifariji hapo kitandani hadi ulipotoweka bila kuniaga!”

Kilichofuata baada ya hapo Joram hakukitegemea. Joram alimwona Mona Lisa akisimama na kumtumbulia macho





ya mshangao, akiwa ameusahau mdomo wake wazi, huku akitetemeka mwili mzima. Taratibu mshangao ulianza kutoweka katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na hasira, hasira za mwanamke, hasira ambazo Joram, pamoja na ujabali wake wote hakupata kuziona kwa mwanamke yeyote yule. Lakini hali hiyo pia ilitoweka taratibu katika macho yake na nafasi yake kuchukuliwa na kitu kama msiba au maombolezo, jambo lililofuatiwa na kilio cha kwikwi, kwa sauti ndogo, huku machozi mengi yakimtoka.
 
21.
Kwa Joram Kiango ile picha ya kusisimua ilikuwa imerudi, picha ya msichana mpole, mrembo, mwenye maumivu fulani rohoni mwake, picha ya malaika anayeteseka! Ambayo mwanaume yeyote asingeivumilia. Hivyo, bila ya kujipa wasaa wa kutafakari zaidi alimwendea na kumkumbatia. Akamvuta taratibu hadi kitandani ambako alimketisha na baadaye kumlaza huku akiwa amemkumbatia, mkono wake wa pili ukijipa kazi ya kumfuta machozi.

Mona alinyamaza kidogo na kumuuliza Joram kwa sauti ya mnong’ono, “Unaniambia kweli, Joram?”

“Kwamba?”

“Kwamba jana nimerudi hapa na kuwa nawe hadi asubuhi ya leo?”

“Kwa nini nikudanganye?” Joram alimjibu kwa swali vilevile. “Kwani kulikoni, Mona, mbona sikuelewi!”

Mona akaanza kulia tena. Baadaye alinong’ona tena kama anayezungumza peke yake. “Hata wewe! Hata Joram Kiango! Nifanye nini jamani?”

“Kuna nini?” Joram alihoji tena. “Kuna jambo gani la muujiza wewe kurudi hapa na kuwa nami?”

“Hujui Joram, hujui; huelewi. Na uwezi kuelewa,” Mona alisema na kuongeza, “Hujui kuwa tayari nimeyaweka maisha yako hatarini. Sijui kitu gani kinachonitokea. Lakini naamini nimekuweka katika hatari kubwa sana katika maisha yako.”

“Hatari gani?” “Ya kifo.”

Joram akaangua kicheko. “Yaani kufurahi na wewe usiku mmoja kwangu ni hukumu ya kifo! Acha mzaha Mona. Mie sio mshirikina kiasi hicho!”





“Joram, hufahamu,” Mona aliongeza. “Kwanza, hukulala na mimi. Halafu, suala la ushirikina halipo.”

Joram akacheka tena. Akasema, “Kwa hiyo tuachane na ushirikina. Twende kwenye elimu ya akhera. Ni kwamba nimelala na jini linalotumia sura yako, jini ambalo baadaye litaniua, sio? Usinichekeshe Mona”

“Huwezi kuelewa,” Mona alinong’ona tena. Ingawa sasa kile kilio cha kwikwi kilikoma, machozi yaliendelea kutiririka juu ya mashavu yake laini, Joram akiendelea na kazi ya kuyafuta na kumfariji.

Kuna ugonjwa fulani. Ugonjwa adimu, ambao ni madaktari wachache hadi sasa wanaoufahamu. Ni aina fulani ya matatizo ya akili ambapo mhusika hujikuta amesahau yeye ni nani na kujihisi kama mtu mwingine kabisa mwenye jina na tabia tofauti. Akiwa katika hali hiyo anaweza kufanya chochote, hata kuua bila kujua analolifanya.
 
22.

Maradhi hayo yanaweza kumfanya mtu kuwa na nafsi mbili au tatu zenye majina na tabia tofauti. Anaweza kuwa Amina, Asha au Aisha kivitendo na kitabia kwa nyakati tofauti. Wakati mwingine Amina au Asha huyo anaweza kuchukiana au hata kuoneana wivu na Aisha, kwa kutegemea wakati huo mgonjwa yuko katika taswira ipi.

Zipo kesi kadhaa za aina hiyo, baadhi zikihusisha hata mauaji, lakini watuhumiwa wakaachiwa huru na mahakama baada ya kuthibitisha kuwa wanaugua ugonjwa huo.

Joram aliamini kuwa Mona Lisa alikuwa na tatizo hilo. Aliamini kuwa alipomfuata jana na kunywa, ambako anaapa kuwa hajawahi kunywa maishani, alikuwa katika taswira yake mpya ambayo yeye binafsi haifahamu, taswira ya msichana wa kileo, sister doo, asiye na haya na mwingi wa mbwembwe. Ni hilo lililomfanya aamue kumfariji na hata pale Mona Lisa alipoomba kuondoka Joram alikataa katakata kwa maelezo

kuwa asingemruhusu kuondoka katika hali hiyo.

“Joram, mara hii naona unafanya jambo ambalo hujui hatma yake. Laiti ungenisikiliza…” Mona alimtahadharisha.

“Najua… Usijali…”

Wakiwa katika hali hiyohiyo ndipo usingizi ulipowapitia. Na ndipo Joram Kiango alipozinduka alfajiri na kujikuta akiwa





amekumbatia maiti ya aliyekuwa Mona Lisa huku tundu la risasi katika kifua chake likiendelea kuvuja damu.

Ndivyo ilivyokuwa.
 
23.
W 4 X

ATIKA nchi hii iliyokumbwa ghafla na ubepari wa kutisha, kwa kisingizio cha ‘utandawazi’; katika nchi ambayo rushwa imekuwa maarufu kama dini, kiasi

cha kuwafanya wachache mamia yao waendelee kuneemeka huku wengi kwa mamilioni yao wazidi kudidimia katika lindi la ufukara, njaa na kukata tamaa; katika nchi ambayo serikali yenyewe haioni soo kumpa mtumishi wake mshahara wa shilingi 40,000 kwa mwezi huku ikijua fika kuwa maafisa wake wa ngazi za kati peke yake fedha hizo haziwatoshi hata kwa kutwa moja; vifo vya hapa na pale vimeondokea kuwa jambo la kawaida kabisa.

Redio, televisheni na magazeti siku zote yamekuwa yakitoa habari ambazo zamani kidogo zingeonekana kuwa za ajabu machoni mwa watu: Ajinyonga kwa deni la shilingi elfu tano; Mama amuua mwanae kwa kumuibia shilingi mia mbili; Mpiga debe amuua mwenzake kwa kugombea senti hamsini; Kibaka achomwa moto hadi kufa kwa kukwapua simu ya mkononi; na kadhalika na kadhalika.

Kama Mtanzania mwingine yeyote, Inspekta Haroub Kambambaya, alikuwa akizisikia, au kuzisoma habari hizo siku zote na kuishia kujiuliza maswali yaleyale ambayo kila mmoja alijiuliza, “Tunaelekea wapi?” au “Hatma ya nchi hii ni ipi kwa kasi hii ya maisha?”





Lakini Haroub Kambambaya hakuwa Mtanzania wa kawaida. Alikuwa afisa mzito, katika kitengo kizito, chenye dhamana maalumu katika masuala ya Usalama wa Taifa. Awali, kitengo hicho kiliongozwa na Inspekta Kombora ambaye sasa amestaafu na kuanzisha shughuli za kilimo katika wilaya moja ya mkoa wa Tanga. Huu ulikuwa mwaka wa pili toka Kambambaya alipoteuliwa kukikalia kiti hicho, ambacho awali hakujua kuwa kilikuwa ‘kiti cha moto’ kiasi hicho, kiti ambacho kilihusiana na kudokezwa juu ya kila tukio nyeti linalotokea nchini, ambalo kwa namna moja au nyingine linahusiana na Usalama wa Taifa. Macho yake yalitakiwa kuuona kila mkataba nyeti wa kibiashara baina ya mtu na mtu, mtu na asasi au serikali kwa serikali. Dawati lake lilitakiwa kupokea taarifa zote za nani anatoka na nani anaingia nchini kulingana na uzito wa majina au nafasi zao. Kuingia na kutoka kwa idadi kubwa ya pesa katika mabenki nchini, pia ni miongoni mwa mambo ambayo yalitakiwa kuifikia meza yake kwa ajili ya tathmini. Si hayo tu, hata mambo ambayo yalionekana ya kawaida, kama masuala ya kujiua, kuua, kutoweka au hata kutishia kujiua yalipitishwa mbele ya macho yake; mengi yakiwa yale ambayo hayakupata kuyafikia masikio ya wanahabari.

Ni mengi yaliyomfikia, mengi kati ya mengi hayo yalikuwa ya kusisimua. Lakini ni machache sana yaliyohitaji kufanyiwa kazi. Aidha, kati ya machache hayo, mengi yalirejeshwa mikononi mwa asasi za kawaida, ama polisi, au Usalama wa Taifa.

Ni katika mlolongo huo, Kambambaya alipolipokea jalada jipya lenye tuhuma dhidi ya Joram Kiango ‘kuua’ mtu na kisha kutoweka.

Kambambaya hakuwa mgeni wa jina la Joram Kiango. Alilisikia mara nyingi likitajwa katika mifereji na vichochoro vya ugaidi, ujambazi au uhaini. Hali kadhalika, alikuwa amesoma majarida na vitabu vingi vilivyochapishwa juu ya harakati za mtu huyo anayeitwa au kujiita Joram Kiango.
 
24.


Alipitia jalada hilo harakaharaka kabla ya kuinua uso wake kumtazama msaidizi wake aliyeketi mbele yake akimsubiri.

“Kwa nini limeletwa hapa?” alimuuliza baadaye.





“Linaonekana kama tukio la kawaida kabisa la mauaji. Polisi yeyote aliyehitimu hatashindwa kujua aanzie wapi, aishie wapi katika kesi kama hii.”

“Ni kweli kabisa afande,” kijana huyo mkakamavu, mtanashati, anayeitwa Chaku Chikaya, alimjibu akitabasamu kidogo. “Lakini,” aliongeza. “Nadhani wameleta jalada hili hapa harakaharaka kwa kuwa wanafahamu jinsi ambavyo ofisi hii imekuwa ikishirikiana na Joram Kiango kwa njia moja au nyingine katika pilikapilika zake.

“Kushirikiana!” Kambambaya alimuuliza. “Kushirikiana, Sajenti!” alihoji tena. “Hapa tuna msichana asiye na hatia aliyeuawa kinyama. Hapahapa tunaye mtuhumiwa ambaye kutoweka kwake ni ushahidi wa kwanza wa kuwa kwake na hatia. Alama za vidole kwenye mwili wa marehemu na sehemu mbalimbali chumbani humo ni zake. Isitoshe ni yeye aliyekodi chumba hicho kwa jina lake na amekiacha bila kutoa taarifa yoyote mapokezi. Wewe, afisa hali kama hiyo unaichukulia kuwa ni ushirikiano?”

Sajini Chikaya alitamani kutabasamu. Alisita kwa jinsi alivyoyaona macho ya bosi wake yalivyokuwa hayana mzaha, jambo ambalo lilimfanya ashangae badala ya kucheka. Chikaya amekuwa na kikosi hiki kwa zaidi ya miaka kumi. Katika kipindi chote hicho amekuwa akishuhudia au kuhusika kwa namna moja au nyingine na harakati za Joram Kiango, harakati ambazo huanza kwa kumfanya Joram aonekane kama mhalifu na kuishia katika hali ya kumfanya aonekane shujaa wa Taifa. Kwa ufupi, Chikaya alikuwa mshabiki wa Joram Kiango.

Kitu ambacho hakufahamu ni kuwa bosi wake hakuwa mshabiki wa Joram Kiango. Kinyume na Mkuu wa Idara hii zamani, mzee Kombora, Kambambaya alimchukia Joram Kiango. Ni kweli, alihusudu mtindo wake wa kupambana na majanga mazito, ambayo yangeweza kuhatarisha usalama wa nchi na bara zima kwa namna anazojua mwenyewe. Hata hivyo, namna zake hizo, ambazo siku zote ziliishia kuvifanya vyombo vyote vya usalama vilivyofundishwa na kuhitimu, vionekane mbumbumbu visivyojua kazi zao, ndilo lililomfanya Kambambaya ajikute akijenga chuki dhidi ya Joram Kiango.





Siku zote alikuwa akiomba itokee siku, Joram ateleze na aangukie mikononi mwake ili amfunze adabu na baadaye kumpeleka chuoni. Aliiona siku hiyo kama inayokaribia.
 
25.


“Sikiliza Sajini. Ushirikiano au ushoga katika suala hili ni ndoto. Hapa tunazungumzia kifo cha mtu. Tunazungumzia mtuhumiwa ambaye anafahamika, ambaye anaweza kuua tena. Ni wajibu wetu kushirikiana na polisi, kwa hali na mali ili tumpate. Mengine yatafuata baadaye.” Alisita kidogo kuitazama saa yake. Kisha, akauinua tena uso wake kumkazia macho Chikaya kabla ya kumuuliza, “Unadhani anaweza kuwa amejichimbia wapi?”



***

Supa D na maiti alikuwa kama bata na maji. Maiti zilikuwa sehemu ya maisha yake. Hakuna siku iendayo kwa Mungu ambayo hakupata kuhusika na maiti, kwa njia moja au nyingine. Mwaka wa kumi na sita sasa toka alipoingia katika kazi hii ambayo si kwamba ilimlazimisha tu bali pia ilimfanya aichukulie miili ya binadamu wenzake, ambao tayari uhai ulikuwa umewatoka, kwao awe kama fundi mwashi anayelichukulia tofali.

Supa D alikuwa mtendaji mkubwa wa chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, ajira ambayo awali aliichukulia kama kupelekwa jehanamu, lakini sasa aliiona kama pepo.

Kama ilivyo kwa maelfu ya watu wengine, Supa D alizaliwa kijiji fulani huko wilaya ya Mpwapwa. Aliona milango ya neema isingemfungukia bila kuja Dar es Salaam, kwani wote waliomtangulia toka kijijini hapo na kupotelea Dar es Saam walirudi miaka kadhaa wakiwa wamebadilika kiuchumi. Wanawake walinona na kupendeza, wanaume walinawiri na kuvutia. Ni hawa waliovaa vizuri, kula vizuri na kuwajengea wazazi wao nyumba nzuri. Ni wao waliowachukua wadogo zao na kuwapeleka mjini ambako walipata elimu nzuri.

Supa D alikuwa mtoto mkubwa katika familia yenye watoto tisa, akiwa mwanaume pekee. Akiwa amemaliza darasa la nne, ambalo wakati huo lilikuwa la juu zaidi katika elimu ya msingi, alijichukulia kama msomi aliyekosa kazi. Hivyo,





alifanya kila jitihada hadi alipopata nauli ambayo ilimfikisha

Dar es Salaam.

Kama kawaida, jiji la Dar es Salaam lilimpokea kwa kila aina ya dhiki na dhihaka. Hakuwa na ndugu, hakuwa na mahala pa kulala. Kwa zaidi ya wiki mbili alilala katika vituo vya mabasi, katika magofu na mara nyingine shimoni Kariakoo. Kutokana na idadi kubwa ya watu jijini Supa D hakupata kuulizwa na mtu yeyote ‘Wewe ni nani’, ‘Unafanya nini hapa’ au ‘Kwenu wapi.’ Hata kufungwa yeye alisikia juujuu tu.
 
26.


Nyota yake ya jaa ilianza kufunguka asubuhi ile alipokutana na kijana mmoja wa kijijini kwao ambaye alikuwa ametoroka nyumbani kwao miezi kadhaa kabla yake.

“Uko huku?” “Wewe pia?” “Ulikuja lini?” “Wewe ulikuja lini?” “Unakaa wapi?”

Baada ya kipindi cha maswali na majibu mwenyeji alijitolea kumpeleka Supa D kwa mwajiri wake kwa ahadi ya kumpatia ajira na mahala pa kulala.

Mwajiri wake aliondokea kuwa mama mmoja mnene, wa Kimanyema, aliyekuwa na nyumba katika mtaa mmoja Mchikichini, Kariakoo. Alikuwa mwajiri wa vijana wengine wasiopungua kumi. Kazi yao ilikuwa kumuuzia kahawa, toka asubuhi hadi usiku wa manane, katika mitaa yote ya Kariakoo, ujira ukiwa chakula, mahala pa kulala na senti chache zilizotokana na faida iliyopatikana. Malazi yenyewe hayakuwa na gharama yoyote kwa mama huyo. Wote walilala uwani, ambako kila mmoja alitandika ama gunia au kirago sakafuni na kuubembeleza usingizi. Kunguni, mbu na viroboto pia walikuwa wapangaji wa nyumba hiyo na kwa ajili ya ugeni wake, walimlaki Supa D juujuu.

Kwa Supa D, ambaye wakati huo bado alikuwa akiitwa Charles Matonya, hiyo ilikuwa hatua kubwa katika maisha yake. Alifanya kazi ya mama huyo kwa moyo wake wote na juhudi zake zote, hali iliyofanya aondokee kuwa kipenzi cha mama. Lakini alikuwa pia kipenzi cha takribani wateja wake wote. Kila aliyeionja kahawa yake aliondokea kuwa mteja





wake wa kudumu. Uchamgamfu wake na ari yake ya kujifunza zaidi na zaidi kwa wateja hao vikamfanya awe zaidi ya ‘kijana muuza kahawa.’

Ni katika mlolongo huo mzee mmoja aliyekuwa akifanya kazi ya uhasibu hapo Muhimbili alimdokeza kuwa zilikuwepo nafasi nzuri za utunzaji wa usafi katika wodi ya wagonjwa. Matonya hakusita kuandika barua ya maombi. Na aliposhauriwa ‘kuongeza’ uzito wa barua yake kwa kutoa ‘kitu kidogo,’ hakushindwa kutokana na akiba ndogo aliyokuwa amejiwekea.

Wiki chache baadaye akawa mtumishi wa wakati huo lililokuwa likiitwa Shirika la Afya Muhimbili.

Kama ilivyo ada, enzi hizo kupata kazi Dar es Salaam ilikuwa rahisi kuliko kupata chumba cha kuishi. Supa D alihangaika kwa takribani mwaka mmoja, akichangia chumba na marafiki hadi alipobahatika kupata chumba huko Magomeni Mikumi, mitaa ya bondeni.

Aliendelea kuwa mchapakazi mzuri. Hata yule bosi mkorofi

kiasi gani hakuwahi kupata kigezo cha kumshutumu Supa

D. Aliwahi kuliko mtunza ufunguo, alichelewa kutoka hadi mtunza ufunguo alipomfukuza. Mara mbili aliwahi kufungiwa stoo akifanya usafi, kumbe muda wa kazi umekwisha! Hali kadhalika, alikuwa akijisomea, pamoja na kuzingatia mafunzo ya kazini na, hivyo, kujikuta akipanda ngazi kidogokidogo.

Ikaja siku ambayo alipokea barua ya uhamisho wa kuwa msaidizi wa mtunzaji chumba cha maiti, kazi ngumu iliyoambatana na nyongeza kwenye mshahara wake.
 
27.


Kati ya yote aliyotarajia maishani, Supa D, au Matonya, hakupata kufikiria kuwa angeweza kufanya kazi katika chumba cha maiti. Alisoma barua ile mara mbilimbili huku akitafakari la kufanya. Kwa mara ya kwanza alifikiria kuacha kazi. Lakini kwa kuwa hakujua angeweza kupata wapi kazi nyingine, aidha kwa jinsi hisia zake zilivyomtuma kuwa kuacha kazi itakuwa sawa na kushindwa kazi akaamua kufanya; kwani si inafanywa miaka yote na wanaume kama yeye? Alijifariji.

Lakini pamoja na kujifariji huko bado alichokutana nacho chumbani humo hakukitegemea. Siku ya kwanza tu ya ajira





yake alilazimika kupokea maiti tatu za watu waliokufa kwa ajali. Walikuwa wanatisha kwa jinsi walivyoharibika na kutapakaa damu. Mmoja alikuwa amepasuka kichwa na, hivyo, kuufanya ubongo wake ambao ulichanganyika na damu kuzagaa mwilini mwake kama uji. Mmoja alikatika kabisa miguu yote miwili na kuwa kipande tu cha mtu. Mwingine hakuwa na jeraha lolote mwilini lakini kwa jinsi alivyotoa macho na kuacha kinywa wazi kama anayezomea, alitisha kuliko wenzake.

Ilikuwa ni wajibu wa Matonya kuwaosha, kuwarekebisha kwa kurudishia kichwa cha yule aliyepasuka, kumfumba mdomo na macho yule aliyeuacha wazi na kumtengeneza yule aliyekatika miguu, tayari kwa kuhifadhiwa katika majokofu ili ndugu zao watakapokuja wawakute katika hali inayotazamika. Pamoja na ujabali wake wote Matonya alishindwa kuifanya kazi hiyo. Alitetemeka mwili mzima, alitapika zaidi ya mara tatu na kujikuta akiweweseka ovyo. Wenzake waliokwishaizowea hali hiyo walicheka sana na kuendelea na kazi yao. Mmoja hata alikuwa akinywa chai huku kikombe kakiweka juu ya

maiti mmojawapo.

Jioni hiyo Matonya aliporudi nyumbani alishindwa kabisa kula. Usiku pia alishindwa kulala. Kila alipotaka kulala alimwona yule maiti aliyetoa macho akimkodolea huku wale wengine wakiwa kando. Hadi saa sita za usiku alikuwa hajapata hata lepe la usingizi. Ndipo lilipomjia wazo. Akakurupuka toka kitandani, akavaa na kuiendea baa moja ya jirani ambayo ilikuwa haijafungwa. Kwa mara ya kwanza maishani mwake akatoa hela yake na kununua bia. Kwa mara ya kwanza akanywa pombe. Akalewa. Alipokwenda kulala alipata usingizi.

Kwa mbali, moyoni mwake, ile hofu juu ya maiti ilikuwa palepale. Hata hivyo aliifukuza hofu iyo kwa kujizamisha katika mitungi ya pombe kali na kuogelea katika mabwawa ya bia. Kila alipokuja kazini alikuwa tayari amelewa na alipotoka kituo chake cha kwanza kilikuwa baa. Ulevi ambao uliambatana na ukarimu na hivyo kumfanya azidi kuwa maarufu mtaani.

Taratibu, hatimaye Supa D alijikuta amekizowea chumba cha maiti hadi nazo zikamzowea. Kupitia mapenzi yake kwa kazi yake alijikuta amezipenda maiti. Alizishika, hata baadhi
 
28.



alizikumbatia. Si hilo tu, alianza hata kuzungumza na baadhi ya marehemu. Wako ambao alicheka nao na hata kuna wale ambao aliteta nao.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa jina lake la Charles Matonya kutoweka na lile la Supa D kuchukua nafasi yake. Ni watu wachache sana waliokijua kirefu cha jina la Supa D kuwa lilimaanisha Super Drunker, kwa maana ya ‘Mlevi’ mashuhuri. Kiuchumi haikuwa ajira mbaya hata kidogo. Kwa jinsi binadamu wengi wanavyowaogopa wenzao mara uhai unapowatoka, kila mara alikuwa na fedha za ziada toka kwa ndugu, jamaa na marafiki waliohitaji msaada wa ziada wa kuandaliwa maiti wao. Wale bahili aliwatia hofu kwa kuwaonyesha maiti mbalimbali za kutisha kwa kisingizio cha

kumtafuta mtu wao hadi walipotokwa na ‘kitu kidogo.’

Siku hizi ambazo binadamu walikuwa wakiteketea kama nzige kutokana na maradhi mbalimbali, yakiongozwa na UKIMWI, wateja walikuwa wengi sana kwa Supa D. walitoka na kuingia, kila mmoja akitaka huduma ya haraka. Hivyo, senti za matumizi hazikuwahi kumpiga chenga.

Si hivyo tu, senti nyingine zilimjia kwa njia ambazo hakutegemea. Wako wateja waliomfuata kwa minajili ya kununua viungo mbalimbali vya maiti. Wako waliotaka sehemu za siri, wako waliotaka ubongo, wako waliotaka hata maiti nzima ya mtoto mchanga. Yote haya Supa D aliyatekeleza kwa hila sana, hasa kwa kutumia miili ya marehemu wa ajali na wale ambao hawakuwa na wenyewe.

Fedha ziliendelea kumiminika. Kinywaji kikaendelea kutiririka katika koo lake.

Lakini kila siku si Jumapili. Ziko siku ambazo wateja waliadimika bila sababu za msingi. Siku hizo Supa D alitumia mbinu za ziada kuhakikisha mfuko wake unajaa. Kwa mfano, iko siku… Supa D aliwahi kuwachekesha watu baa, wakati akimwaga ofa za bia. Baada ya muda aliuliza ghafla, “Mnadhani fedha hii ninayoinywa nimeipata wapi?” hakuna aliyejibu. “Hii ya leo nimeitolea jasho,” aliongeza. Kwamba jioni hiyo alikuwa hana pesa za kunywea. Na ‘wateja’ walikuwa adimu. Zilipofika dakika za majeruhi ndipo alitokea Mpemba mmoja bahili aliyetaka kumshughulikia marehemu ndugu yake ili





amsafirishe. “Nilijitahidi kumshawishi anipe angalao shilingi elfu thelathini ili aniachie kazi ya kumwandaa marehemu, alikataa katakata na kushikilia kuifanya mwenyewe. Nikamwachia na kukaa pembeni nikichora mbinu. Ikatokea wakati fulani nilimwona kageuka upande. Kwa hila, bila yeye kujua niliinua mkono wa marehemu na kuutumia kumpiga kofi la kisogo ambalo lilimshtua sana. Alipogeuka aliuona mkono wa marehemu ukianguka kurudia sehemu yake ya kawaida, huku mimi nikijifanya sikuuona. Pamoja na ubahili wake mpemba huyo alinipa zile elfu thelathini harakaharaka na kuniomba kuifanya kazi ile aliyoikatalia awali. Moyoni mwake aliamini kabisa kuwa amepigwa na marehemu kwa ajili ya ubahili.”

Huyo ndiye Supa D, Supa D ambaye jioni ya leo alikuwa akiushughulikia mwili wa msichana ambaye katika uhai wake alijulikana kama Mona Lisa.

Toka awali kabisa Supa D alibaini kuwa ama marehemu hakuwa mtu wa kawaida ama kifo chake hakikuwa cha kawaida. Maiti ilikuwa imeletwa hapo hospitalini toka saa tano na robo asubuhi hiyo, ikiwa imepakiwa katika gari la wagonjwa lililosheheni pia takribani polisi wanane, watatu kati yao wakiwa na mavazi ya kiraia. Mwili wa marehemu ulipelekwa chumba maalumu cha uchunguzi ambako daktari wa zamu alikaa nao zaidi ya saa nne. Alipomaliza kuufanyia uchunguzi na kuandika taarifa ya uchunguzi wake ambao aliwapa polisi nakala ndipo alipokabidhiwa Supa D kwa matayarisho zaidi na hifadhi.

Mara tu alipomfunua marehemu na kukutana na sura yake Supa D alipata hisia kuwa marehemu hakuwa mtu wa kawaida. Pamoja na kupokea maiti wa aina mbalimbali, wakiwemo wabaya na wazuri wa sura, Supa D hakupata kukutana na maiti ya mrembo kama huyu. Huyu alikuwa mzuri kuliko wazuri wote waliowahi kupita chumbani humo. Tazama sura yake inavyovutia! Tazama anavyotabasamu, hata baada ya roho yake kutoweka!
 
29.
Kwa mara ya kwanza Supa D alijikuta amesahau lipi la kufanya kwa maiti huyo. Badala yake, kwa takribani dakika tano nzima, alikuwa bado kamkodolea macho; bado haamini





kama anatazama maiti au binadamu hai, kama anamtazama binadamu au malaika.

Baadaye aliukumbuka wajibu wake. Akauinua mwili huo na kuulaza juu ya meza maalumu. Akauvua nguo na kuuacha kama ulivyozaliwa. Pigo lingine likakipasua kichwa cha Supa

D. Haukuwa mwili wa kawaida! Kilikuwa kipande cha sanaa, iliyochorwa, ikachongwa na kisha kupuliziwa uhai! Uhai ambao sasa ulitoweka kutokana na jeraha kubwa la risasi ambayo ilikitoboa kifua hicho kizuri!

Zaidi ya pombe na pesa Supa D hakupata kupenda kitu chochote kingine, wanawake ikiwa sehemu ya vitu hivyo. Ndiyo, alipata kutamani, walio hai na maiti. Lakini ilikuwa kutamani tu. Huyu alimpenda! Alitamani afufuke, amwambie jinsi alivyompenda.

“Mpenzi, yeyote aliyekuua ni mnyama, mnyama aliyelaaniwa,” alijikuta akizungumza naye. “Ni mtu ambaye hafai kuishi. Wewe sio mtu wa kufa hata kidogo.” Alitulia kidogo akimwangalia. “Lakini mpenzi,” aliendelea. “Ilikuwaje hadi Mungu akakupendelea kimaumbile kiasi hiki? Unajua kuwa ni binadamu wachache sana wanaoukaribia uzuri wako?” Halafu akatulia tena kabla ya kuongeza, “Halafu mpenzi, nimeshakwambia kuwa nakupenda? Naomba ufahamu hivyo, tafadhali.”

Wakati Supa D akizungumza hayo alikuwa akiendelea na kazi yake. Mikono yake ilikuwa ikitambaa na kuteleza juu ya mwili huo mzuri kuusafisha, huku akifarijika vilivyo na mguso huo. Alifanya kazi kwa uangalifu mkubwa na mapenzi makubwa huku akiendelea kumnong’oneza marehemu hili na lile. Aliosha masikio, macho, pua na shingo. Alisafisha damu ambayo ilianza kuganda kwenye kifua chake na kuliosha vizuri tundu la risasi, ambalo baadaye aliliziba kwa pamba. Aliuacha mkono wake uteleze juu ya tumbo hilo laini na kuishia katikati ya miguu yake. Hapo mkono wake ulitulia kwa muda na kuviachia kazi vidole vyake. “Samahani,” alimnong’oneza. “Si unajua kuwa nakupenda?” Kisha alitabasamu ghafla. “Wewe ni bikira!” alisema. “Nilijua wewe ni bikira. Nilijua kuwa usingemruhusu mwanaume yeyote mwingine zaidi yangu. Nilijua…”





Ghafla, Supa D alipata hisia kuwa alikuwa anatazamwa. Akageuka. Watu wawili walikuwa wamesimama nyuma yake, kimya kama vivuli, wakimtazama. Walikuwa wanaume warefu, waliovaa suti nyeusi na miwani ya jua. Kwa kiasi fulani walimtisha Supa D, hasa kwa kutojua waliingia chumbani humo muda upi na waliingia vipi. Kama anakumbuka vizuri alikuwa amejifungia kwa ndani kabla hajaanza kazi ya kumwandaa marehemu.

Supa D akasimama na kuwakodolea macho ya hofu na aibu yanayouliza bila kutoa sauti “Sijui niwasaidie nini?”

“Endelea na kazi yako,” Mmojawao alijibu baada ya kusoma maswali katika macho ya Supa D. “Huyo mrembo si mtu wa kukaa chumba cha maiti. Wala si mtu wa kukaa kaburini. Muda mfupi baadaye atafufuka na kupaa angani. Endelea kumwandaa.”

Supa D aliduwaa. “Nyie ni nani na mmeingiaje humu?”
 
30.
W 5 X

WA Insepkta Haroub Kambambaya alfajiri hiyo ilikuwa mbaya, ya kutisha na inayosikitisha kuliko alfajiri nyingine zote alizowahi kuishi katika uhai wake. Labda angeweza kuifananisha alfajiri hii na ile ya miaka kumi na sita iliyopita, wakati huo akiwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Mzumbe, mkoani Dodoma. Alikuwa katika likizo fupi, akijiandaa kwa mtihani wake wa mwisho, likizo ambayo aliitumia kukaa na mama yake mzee katika kimojawapo cha vijiji vya Shinyanga. Akiwa mtoto wa mwisho, asiye na ndugu, baada ya dada zake wawili na kaka zake wanne kufa kwa maradhi mbalimbali utotoni, baba yake pia akiwa marehemu tangu yeye anatambaa; mama yake, binti Kaundime, alikuwa kila kitu kwake. Alikuwa bibi, babu, mama, kaka, dada na zaidi ya yote rafiki. Waliishi kwa mapenzi makubwa na kuridhika kwa chochote walichokipata kutokana na jasho la

mama huyu katika kijishamba chake cha mahindi.

Binti Kaundime alijinyima kila kitu na kujidhiki kwa kila hali ili kumpatia mwanae huyo wa pekee elimu. Kwa upande wake, Haroub hakuwa kipofu wa hali hiyo. Alifanya kila jitihada katika masomo yake ili apate elimu ya kutosha, ambayo ingempelekea kupata mshahara wa kutosha, ili aweze kuchukua jukumu la kumlea mama huyu.

Hivyo, alfajiri ile, wakati akiwa na hakika kuwa safari





ya kutafuta uhakika wa maisha ilikuwa inafikia ukingoni, aligutushwa toka usingizini na kelele za watu walioizingira nyumba yao. Baadhi walikuwa wakiimba nyimbo za kuwalaani wanga, baadhi wakitukana kwa sauti huku wengine wakipiga milango na madirisha yao kwa miguu, mawe na magongo. “Toka nje mchawi wewe. Toka upesi, zako zimefika leo,” mtu mmoja alisikika akisema.

Kwanza Haroub hakuelewa kinachoendelea. Alipotoka chumbani kwake na kumfuata mama yake kwake alimkuta amejiinamia akilia kwa kwikwi.

“Kuna nini mama?” aliuliza.
 
31.


Mama yake alipomtazama alizidi kulia. Akainuka na kumkumbatia mwanae huku akisema kwa sauti ya dhiki, “kwa heri mwanangu. Nimekulea, nilitegemea unilee. Shetani ametushinda nguvu. Kwa heri ya kuonana.”

“Kwani kuna nini mama?” Haroub aliuliza.

Mama yake alimtazama kwa mshangao. “Kwani hujaelewa tu?” alimuuliza. “Hao watu wanakuja kuniua.”

Haroub hakuyaamini masikio yake. “Unasemaje?... Kwa nini?” alihoji.

“Siku zote wamekuwa wakidai kuwa mimi ni mchawi. Wanadai kuwa mimi ndiye niliyemuua baba yako na wanangu wote waliotangulia. Majuzi amefariki mtoto wa jirani yetu yetu mmoja ambaye tuliwahi kugombea mpaka wa shamba. Naamini ni yeye aliyewatuma kwa kudhani kuwa nimehisika na kifo cha mtoto wake. Haroub baba, ningekuwa mchawi kweli ningeshindwa kukuarifu wewe mwanangu?”

Kabla Haroub hajaua afanye nini, ajibu nini mlango wa mbele ulipigwa jiwe kubwa lililofanya ufunguke. Ulifuatiwa na moshi mkubwa ulioashiriwa kuwa nyumba yao tayari ilikuwa imechomwa moto. Wakati huohuo kundi kubwa la watu waliofunika nyuso zao kwa matambara liliingia ndani na kuwatenganisha yeye na mama yake. Alijaribu kupigania roho ya mama yake kwa nguvu zake zote, lakini mikono yake ilikuwa dhaifu sana mbele ya umati huo wenye mikono iliyokakamaa kwa uhalifu. Aliburuzwa nje na kutupwa chini, ambako alishuhudia mama yake kipenzi akipigwa kwa michi, mawe na magogo hata akakata roho. Alishuhudia pia mama





yake akimwagiwa mafuta ya taa na kuchomwa moto kabla ya watoa hukumu hao kuondoka zao huku wakiimba nyimbo za kujisifia.

Baada ya watu hao kuondoka ndipo majirani walipofungua milango yao na kumzoa Haroub ambaye alikuwa ameteguka mkono na kuumia mbavu kwa purukushani. Baadhi ya majirani walikimbilia polisi kutoa taarifa, taarifa ambayo haikuzaa matunda yoyote zaidi ya kuruhusu mwili wa marehemu uzikwe na ahadi ya “Upelelezi unaendelea.”

Ni tukio hilo lililomfanya Haroub Kambambaya afikie uamuzi wa; Nitakuwa polisi. Daima nitapambana na wahalifu wa aina zote na kuwatokomeza.

Alirejea shule na kufaulu vizuri masomo yake. Alijiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya sheria. Alipohitimu alikuwa miongoni mwa wasomi wachache wa awali walioona umuhimu wa kujiunga na jeshi la polisi.

Akiwa askari shupavu, mkakamavu na mwadilifu alijikuta akipanda cheo baada ya cheo hadi majuzi alipoteuliwa kukalia kiti hiki, ambacho uteuzi wake ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, cheo ambacho madaraka yake yanawiana na yale ya Kamishna Mwandamizi wa Polisi au Mkuu wa Majeshi, ingawa kinafichwa kwa pazia la uinspekta. Naam, cheo ambacho kilimfanya akalie kiti hiki “Cha moto,” ambacho alfajiri hii alianza kuuonja.

Kufuatilia kwake nyendo za Joram Kiango ili aweze kuelewa kilichotokea pale hoteli ya Comfort na kusababisha kifo cha yule msichana mrembo, Mona Lisa, Kambambaya alichukua hatua kadhaa madhubuti kwa lengo la kumtia mikononi Joram Kiango.
 
32.


Akiwa kingunge wa kitengo, Kambambaya alikuwa na siri nyingi ambazo wasaidizi wake wa karibu hawakuzifahamu. Moja ya siri hizo ni ile ya kujua namba ya simu na jina la bandia ambalo Joram Kiango alikuwa akitumia katika simu zake za mkononi. Akiwa na namba mbalimbali katika makampuni AIRTEL, TIGO na VODACOM, huku akizungumza au kuandika ujumbe wa maandishi kwa namna ya mafumbo, haikuwa kazi rahisi kuzinasa simu zao. Hata hivyo, wataalamu wa sauti waliwahi kushirikishwa kuthibitisha kuwa huyo hakuwa





mwingine zaidi ya Joram Kiango.

Hivyo, lilipotokea hili, na Joram kutoweka Kambambaya aliitega mitego yake yote. Mmoja wa mitego hiyo ilifyatuka na kuinasa sauti yake pale alipotuma ujumbe wa maandishi kwenye namba fulani ambayo bila shaka iliorodheshwa kwa jina jingine la bandia. Kambambaya isingemchukua muda mrefu kumjua mtu huyo, lakini maadamu kwa sasa alichohitaji ni kumpata Joram Kiango mwenyewe, alichofanya ni kuwasiliana na kampuni ya simu iliyotumiwa ili kujua eneo ambalo ujumbe huo ulitokea.

Lilikuwa eneo la Manzese, lenye maelfu ya watu, maelfu ya majumba na maelfu ya vichochoro visivyo na mpangilio, eneo ambalo halina jina la mtaa wala namba za nyumba. Lakini hayo hayakumkatisha tamaa Kambambaya. Alitumia timu ya vijana wake sita, kuungana na polisi wa kawaida sitini, kulizingira eneo hilo usiku kucha na kumhoji kila atakayetiliwa mashaka hadi Joram Kiango atakapopatikana, operesheni ambayo aliichukulia kuwa ndogo sana na ya kawaida kabisa, hadi pale alipoamshwa usingizini na kupewa taarifa ya kuuawa kwa polisi wanne waliokuwa katika jukumu hilo.

Hakuyaamini masikio yake. “Wameuawa!” alinguruma katika simu yake ya mkononi, “Wameuawa vipi?... Nani kauawa?”

“Haijafahamika, afande. Ndio kwanza nafika katika eneo la tukio. Tuko katika vichochoro fulani, hatua kama mia moja hivi toka darajani. Inaonyesha…”

“Nakuja!” Kambambaya alisema akichupa toka kitandani. Alivaa shati na suruali ya karibu juu ya mavazi yake ya ndani, akaichukua bastola yake na kuitupia mfukoni. Dakika mbili baadaye gari lake lilikuwa likitafuna lami, toka Masaki kuelekea Manzese.

Alimkuta msaidizi wake, Chaku Chikaya, akimsubiri chini ya daraja, akiwa miongoni mwa askari wa kawaida wanne, wenye silaha. Chikaya akiwa mtu aliyekabidhiwa operesheni hii alimweleza Inspekta kwa tuo tukio zima lilivyokuwa.

“Marehemu hawa walikuwa na jukumu la kulinda vichochoro vyote vilivyotokea katika barabara kuu. Walikuwa wakitembea wawiliwawili. Inaonekana kama walioingia kwa





bahati mbaya katika mtego wa adui. Askari waliokuwa mbali kidogo ya eneo hili walisikia milio ya risasi ikilipuka ghafla tu. Walipokuja eneo la tukio walikuta miili ya wenzao ikiwa imedondoka chini. Hawakumwona mtu wala kusikia mtu akikimbia.
 
33.


“Ni wazi kuwa yeyote aliyefanya mauaji haya bado yuko katika eneo hilihili. Kwa ajili hiyo nimeongeza ulinzi na kupanua wigo.” Chaku alisema.

Kambambaya alitikisa kichwa na kuunga mkono hatua hiyo, “Walisikia mlio wa bunduki aina gani?” alihoji.

“AK-47, mzee.”

AK! Kambambaya alishangaa. Ile bunduki hatari iliyogunduliwa na Mrusi, Kalashnikov, kwenye vita kuu ya pili ya dunia! Basi hii ni vita! Aliwaza.

Chikaya alimwongoza hadi mahala ilipokuwepo miili ya marehemu. Walilaliana wawiliwawili, baadhi wakiwa wameziangukia silaha zao, mmoja silaha yake ikiwa mkononi kama anayejiandaa kufyatua. Haikuhitaji utaalamu wowote kubaini kuwa kifo kiliwakuta marehemu hawa bila ya wao kutegemea. Ama walivamiwa ghafla, au waliingia katika mtego wa mauti.

Kuiona miili ya vijana hao wasio na hatia, wakiwa hawapo tena duniani, kuliamsha hasira katika nafsi ya Kambambaya. Nani aliyewaua? Kwa nini amewaua? Afanye nini kuwapata haraka wahalifu hawa ili wafikishwe mikononi mwa sheria? Alijiuliza harakaharaka, swali baada ya swali, maswali ambayo yeye binafsi hakutegemea majibu yake yawe karibu kiasi hicho, jambo lililozidi kumpandisha hasira.

Kiasi fulani hasira hizo ziliambatana na hofu, si hofu ya kujua kuwa mahala fulani, katika mtaa fulani, kuna mtu au watu hatari, wenye silaha hatari, ambao wanaweza kuwaua polisi wanne bila ya kigugumizi chochote. Ndiyo, hilo lilimtisha, lakini hofu nyingine ilikuwa juu yake binafsi. Hatua yake ya kuamua kumwinda Joram Kiango kwa nguvu nyingi kiasi hiki ilionyesha kuwashangaza na kutoungwa mkono na wasaidizi wake. Wanavyomjua Joram hawakuona kama ni mtu wa hatari kiasi hicho, wengine hawakuona umuhimu. Lakini maadamu yeye alikuwa na madaraka, alilotaka liwe, likawa.





Hivyo, sasa ilimtisha kwa kutojua atauambia nini umma wa Watanzania umwelewe; kwamba Joram Kiango alishukiwa kuua msichana hotelini! Kwamba kwa ajili hiyo alituma kikosi kikubwa cha askari kumtafuta! Kwamba katika purukushani hizo askari wanne wameuawa kinyama! Nani atamwelewa? Nani atamsikiliza?

Wakati akiwaza hayo Kambambaya alikuwa akiendelea na uchunguzi wa eneo hilo. Akiongozana na Chikaya, na askari wengine wawili, walipita uchochoro hadi uchochoro, wakiikagua nyumba baada ya nyumba. Ikiwa alfajiri ya siku ya kazi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walianza kuamka. Walishangazwa kuona mitaa yao ikiwa ‘imevamiwa’ na polisi wenye dalili za madaraka makubwa. Kambambaya hakutaka kuwabugudhi raia kwa wakati huo. Aliwahoji wawili watatu, maswali mawili matatu, lakini wote walionekana kama wanaoulizwa, “Wewe ni mwanamume?” wakati anajiona ni mwanamume au “Wewe ni mwanamke?” wakati kila mtu anaona kuwa ni mwanamke. Kambambaya aliachana nao na kuendelea na uchunguzi wake.

Uchochoro mmoja uliwafanya watokee kwenye hospitali ya Daktari Omari. Alishangazwa na umati wa watu walioukuta umezingira hospitali hiyo, kila mmoja akiwa anatokwa na machozi ya hofu.

“Kuna nini hapa?” alihoji.

“Daktari ameuawa,” mmoja wa majirani alimjibu. “Daktari yupi?”

“Dokta Omari, mwenye hospitali hii. Wagonjwa waliokuja kupata sindano za masaa wamemkuta akiwa amelala kifudifudi, tundu kubwa likivuja damu toka kisogoni mwake.” Kambambaya hakusikiliza zaidi. Alipenya umati huo wa watu hadi ndani. Mwili wa Daktari Omari ulikuwa bado umelala sakafuni, katikati ya mlango wa kutokea ofisini kwake kuelekea wodini. Risasi iliyomuua ilikuwa imemfumua kisogo na kupotelea katika ubongo wake ilikuwa tayari imeganda na

kufanya kichwa chake kiungane na sakafu.

Kambambaya alitupia macho mezani. Majalada, vitabu, magazeti na vikorokoro vingine vya kiganga vilikuwa katika hali ya mpangilio mzuri. Viti na meza pia vilikuwa katika





utaratibu wake maalumu, hali ambayo ilimfanya apate hisia kuwa kifo kilimkuta marehemu bila purukushani yoyote.

“Mzee unaona pale?” msaidizi wake mmoja alimzindua.
 
34.


Kambambaya akamtazama. Kisha akayafuata macho ya askari huyo yalikoelekea. Yalikuwa yakitazama ukuta mmoja uliokuwa na tundu dogo ambalo lisingekuwa limesababishwa na kitu kingine zaidi ya risasi. Kambambaya alitoa kisu chake na kukipenyeza ndani ya tundu hilo. Baada ya kuchokonoa kwa muda risasi kubwa ilidondoka. Akaiokota na kuitazama. Kama alivyotegemea, ilikuwa ya bastola aina ya AK.45, ambayo mara nyingi hutumiwa na maafisa wa polisi na jeshi pekee.

Risasi ukutani! Kambambaya aliwaza. Ilikuwa ya onyo au mpigaji alikosa shabaha? Kwa jinsi mwili wa marehemu ulivyokuwa, Kambambaya hakuona kama muuaji alihitaji kumtisha au kukosea shabaha!

Aliirudia meza na kuanza kupekua majalada hadi alipopata lile ambalo alikuwa akilitafuta, jalada lenye kumbukumbu ya wagonjwa wote walioingia na kutoka siku hiyo. Alilipitia jina kwa jina, akitazama aina ya maradhi yaliyowaleta, umri na taarifa nyinginezo. Wengi hawakuwa watu wa kutilia shaka. Majina yalikuwa ya kawaida, magonjwa ya kawaida. Lakini alipochukua jalada la wagonjwa waliolezwa na kukutana na mgonjwa mmoja tu mwenye jina la ajabuajabu mara moja alijikuta akisisimkwa na mwili wake:

Sheriff Mkono wa Birika! Miaka sitini na mitano! Maradhi yasiyoeleweka! Vipimo baadaye!

Kambambaya alipiga hatua za harakaharaka kukiendea chumba cha wagonjwa waliolazwa. Kama alivyotegemea alikuta chumba hicho kikiwa kitupu.

“Joram alikuwa hapa,” alinong’ona akimwelekea Chaku Chikaya. “Amelala katika chumba hiki. Tumechelewa sana. Tayari ametoweka tena.”

Chikaya hakumwelewa bosi wake. “Umesema Joram, afande? Una hakika?” alimuuliza.

“Bila shaka!” Kambambaya alimjibu. “Na kwa namna moja au nyingine anahusika na mauaji haya. Sasa umuhimu





wa kumpata ni mkubwa zaidi na wa haraka zaidi. Lazima apatikane katika saa ishirini na nne zijazo,” aliamrisha.

Wakati huo ikikaribia saa kumi na mbili za asubuhi, uwanja wa hospitali hiyo ulikwishafurika watu. Minong’ono ya hapa na pale iliendelea na, hivyo, kuzidi kuvuta watu wengine. Kambambaya alitoa maelekezo kwa wasaidizi wake, “Eneo hilo lifungwe; taratibu za kawaida, ikiwa pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na ripoti ya daktari zifuatwe.”

Kisha alilirudia gari lake ambalo lilimpeleka nyumbani kwake ambako alioga, akavaa mavazi yake rasmi, akanywa kikombe chake cha kahawa chungu, kisha akarejea ofisini kwake.

Kwa muda fulani Kambambaya aliduwaa ofisini, akiwa ameiinamia meza yake. Hakujua aanzie wapi, aishie wapi katika kulitafakari suala hili lililojaa utata, suala ambalo lilianza na kifo cha msichana mmoja tu hotelini, likafuatiwa na kutoweka kwa mtuhumiwa nambari moja na sasa tayari askari wanne na daktari mmoja ni marehemu.

Msaidizi wa ofisi yake alimletea kahawa nyingine ambayo aliinywa. Alipoingia tena alimletea jalada lililokuwa na taarifa ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu aliyeuawa hoteli ya Comfort.

Kambambaya alikuwa na mzigo mzito kichwani mwake zaidi ya jalada hili. Alikuwa na jukumu zito la ‘kuhalalisha’ vifo vya askari wale wanne na daktari wa Manzese. Ulikuwa wajibu wake, tena wa haraka, kupata ufumbuzi au kiini cha mauaji hayo. Aidha, jukumu la kumnasa au kuwanasa wahalifu kwa kiasi kikubwa lilikuwa mabegani mwake. Kila dakika iliyopotea, kabla ya kupiga hatua yoyote katika hayo, ilimtisha zaidi. Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa msichana yule, ambaye hata jina lake lilikuwa halijafahamika, alikuwa wa kwanza katika mlolongo huo wa vifo, Kambambaya alijikuta hana jinsi, isipokuwa kulisoma jalada hilo kwa tuo.

Taarifa ya daktari ilikuwa na kurasa tatu zilizoandikwa kwa mtindo wa kitabibu. Juu ya ripoti hizo ziliambatanishwa picha kadhaa za marehemu zilizopigwa na polisi. Mojawapo ya picha ilimvutia Kambambaya kiasi cha kufanya aamue kuiweka chini taarifa ya maandishi na kuzikodolea macho.
 
35.
Alikuwa amewasikia wasaidizi wake wakizungumza uzuri wa msichana huyo aliyeuawa. Hakuwa amefikiria kuwa alikuwa mzuri kiasi hiki! Picha hii ikiwa imeandaliwa katika hali ya kumfanya msichana huyo asionekane kuwa amekufa, marehemu alikuwa amevalishwa nguo na kuketishwa kwenye kochi, macho yakiwa yamefumbuka. Alionekana msichana mzuri sana, ambaye hakustahili kufa kifo cha kinyama kiasi kile. Picha nyingine zilipigwa kabla hajaguswa, zikionyesha alivyolala chali kitandani, tundu la risasi kifuani, kitu kama tabasamu mdomoni. Nyingine, bila shaka ilipigwa Muhimbili, ilimwonyesha akiwa mtupu kama alivyozaliwa. Isipokuwa kwa tundu la risasi lililoutia dosari mwili huo ulikuwa mwili pekee, ambao Kambambaya hakupata kufikiria kama binadamu wa kawaida angeweza kuwa nao.

Baada ya kuzitazama kwa makini picha hizo Kambambaya aliirudia taarifa ya daktari. Kwanza aliisoma harakaharaka. Baadaye aliirudia taratibu, akiitafakari kipengele baada ya kipengele.

JINA: Halijafahamika

UMRI: kati ya miaka ishirini hadi ishirini na mitatu.

JINSIA: Mwanamke.

MUDA WA KIFO: kati ya saa saba hadi saa tisa usiku.

SABABU YA KIFO: kutokwa na damu nyingi katika tundu lililotoboa moyo.

MAELEZO MENGINE: Marehemu alikuwa mtu mwenye afya nzuri kabla ya kifo chake. Isipokuwa kwa harufu ya lotion na pafyumu mwilini mwake, marehemu alikuwa msafi. Hakuwa amefanya mapenzi na mtu yeyote. Kwa ujumla, alikuwa bado bikira.

Taarifa hiyo ya mwisho ilimchanganya Kambambaya. Marehemu alikuwa bikira! Marehemu, ambaye taarifa alizonazo zinaonyesha kuwa alikuwa na mpenzi wake, Joram Kiango, wakinywa, kula na kulala zaidi ya mara moja! Haikumwingia akilini. Kama wanamtafuta Joram Kiango, kwa tuhuma za kumuua mpenzi au hawara yake, vipi hawara huyu awe safi kiasi hicho!

Kambambaya akaichukua tena picha ile ya marehemu aliyeketishwa kwenye kiti. Akaitazama kwa makini kana





kwamba alitarajia imwambie chochote. Haikumwambia. Alirejea katika jalada na kuendelea kufikiri. Mara akashikwa na hamu ya kumwona marehemu kwa macho yake mwenyewe. Akainuka na kutoka nje ya ofisi.

“Muhimbili,” alimwelekeza dereva wake wakati akiingia kwenye gari.

Dakika chachee baadaye alikuwa katika ofisi ya daktari wa uchunguzi wa maiti. “Naomba kumwona marehemu,” alisema baada ya kujitambulisha. Kambambaya alimwona daktari akibabaika kidogo kwa rai hiyo. “Vipi docta, mbona unawaza sana. Au kuna taratibu ambazo sijazifuata?”

“Hapana,” daktari alijibu.

Hakuona kama alihitaji kumwambia askari huyo tatizo lake. Ukweli ni kwamba pamoja na udaktari wake bado hakuwa mzoefu sana wa chumba cha maiti. Mara nyingi aliwategemea wahudumu wa chumba hicho, hasa Supa D ambaye alitekeleza majukumu yake kwa uhakika zaidi. Tatizo ni kwamba toka jioni jana Supa D alikuwa hajaonekana, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake.

“Twende,” alijikongoja daktari huyo baada ya kusitasita. Chumba cha maiti kiliwalaki kwa ile harufu isiyoelezeka,

harufu ambayo siku zote Kambambaya alishindwa kufahamu iwapo ilitokana na kuharibika kwa maiti, mchanganyiko wa madawa au yote kwa pamoja, harufu ambayo haizoeleki.

Alistahimili harufu hiyo kwa kusimama nyuma ya daktari alipovuta jokofu lililokuwa na taarifa za marehemu huyo. Mara Kambambaya alimsikia daktari huyo akitoa sauti ya mshangao, iliyofuatiwa na kutokwa na macho ya mshangao kama mtu aliyegusa waya wa umeme. Kambambaya akayafuata macho ya daktari huyo humo ndani ya jokofu. Yeye pia alipigwa na butwaa.

Badala ya msichana mrembo jokofu hilo lilikuwa na maiti ya mzee wa kiume, yenye ndevu nyingi zilizoachwa ovyoovyo. Ulimi wa marehemu huyo ulikuwa nje, shingo upande kama iliyovunjika huku damu ikiwa imeganda mdomoni, puani na masikioni.

Hatimaye, daktari alitokwa na sauti, “Supa D!” alisema kwa mshangao. “Jesus, kitu gani kimetokea hapa?”
 
Kiongozi ubarikiwe sana. Kwa kweli una stahili nafasi ya mbele kabisa peponi. Hapa nimekaa na kikombe cha tangawizi na karanga, hebu tupia episode kadhaa jioni iwe njema hii.
 
Back
Top Bottom