Bob Marley alikufa na miaka 36, akiwa bado kijana mbichi kabisa.
Malcom X alikufa na miaka 39 akiwa na mipango mingi tu ya kuleta mabadiliko ya kisiasa kwa wamarekani weusi.
Martin Luther King alikufa na miaka 39 akiamini kwamba yupo tayari kuelekea mbinguni.
John Lennon alikufa na miaka 40, mmoja wa mashabiki wake alimpiga risasi.
Mwanamuziki Gerard Levert mzee wa Cassanova alikufa na miaka 40 baada ya kunywa dawa aina mbili tofauti zilizotengeneza sumu mwilini mwake.
Rajiv Gandhi alikufa na miaka 46, akiwa bado kijana mng'avu na mwenye matumaini mengi tu.
John F Kennedy alikufa na miaka 46, akiamini kuwa uchaguzi wa mwaka 1964 angeweza kushinda na kuiongoza Marekani kwa mihula miwili.
Edward Moringe Sokoine alikufa na miaka 46, akiwa katikati ya vita dhidi ya wahujumu uchumi.
Mjasiriamali Ruge Mutahaba kaondoka duniani na miaka 48 akiwa na mipango mingi mikubwa.
Nahisi Marehemu Ephraim Kibonde ni wa umri huo huo wa Ruge, nae kaondoka na uchangamfu wake maskini!.
Maishani unaweza usifikishe hata miaka 50 kwa mipango ya Mungu, unaweza ukawa na miaka 45 au chini ya hapo lakini kumbe wewe ni "mzee" tayari.
Ujumbe wa hao wote niliowataja na ambao waliaga dunia wakiwa hata hawajaishi nusu karne ni kwamba muda wetu ni mfupi.
Uhairishaji wa mambo (procrastination) wakati hujui kama wewe tayari ni "mzee" kwa mipango ya muumba wetu sio jambo jema.
Kesho hatuijui, kwanini tunapoteza muda kwenye kuendekeza siasa za makundi na upambe na uhasama wakati muda wetu hatujui utaisha lini?.
Vipaji vyetu na tuvitumie kwa ajili ya kuinua maisha yetu binafsi na kuuinua mustakabali mwema wa Tanzania.
Tunajua tumekuja lini duniani lakini hatujui hii sinema yenye mengi iitwayo maisha, itamalizika lini na sehemu gani.
RIP Kaka Kibonde, RIP Kaka Ruge. Siku zetu chini ya jua sio nyingi kama tunavyozipanga katika mipango yetu, dakika ya kufanya masuala ya muhimu ndio hii ya sasa.