Mtanzania Upendo Lyimo ashinda tuzo ya AI ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2026

Mtanzania Upendo Lyimo ashinda tuzo ya AI ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 2026

Waufukweni

JF-Expert Member
Joined
May 16, 2024
Posts
5,383
Reaction score
18,776
Mtanzania Upendo Ernest Lyimo ametangazwa mshindi wa tuzo ya AI for Climate Action Award 2026 kupitia jukwaa lake la CLIMAID, linalotumia teknolojia ya akili unde (AI), taarifa za satelaiti na takwimu za mazingira na jamii kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

🇹🇿🏆 TANZANIAN INNOVATOR WINS UN CLIMATE AI AWARD 2026Tanzanias Upendo Ernest Lyimo has won t.jpg

Upendo alitangazwa katika Jukwaa la AI for Climate Action Forum 2026 lililofanyika Oktoba 13 na 14, 2026, jijini Phnom Penh, Cambodia, likiwakutanisha watunga sera, wataalamu wa teknolojia, wabunifu na wadau wa maendeleo kujadili namna akili unde inavyoweza kuharakisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea.

Akizungumzia ushindi huo, Upendo amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa na utambuzi wa uwezo wa ubunifu katika kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani. Ameongeza kuwa ushindi huo utaipa CLIMAID mwonekano mpana zaidi na fursa ya kujenga ushirikiano na serikali, taasisi za utafiti na wadau wa teknolojia na ufadhili wa masuala ya tabianchi.

Amesema Tanzania ndiyo mwanzo wa safari yake, lakini si mwisho wa malengo yake, akieleza azma yake ya kuipanua CLIMAID ili iwe suluhisho linaloaminika katika kusaidia maamuzi na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika na maeneo mengine duniani.

CLIMAID ni jukwaa huria linalotumia akili unde kusaidia nchi na jamii kutambua mapema, kuelewa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Jukwaa hilo linaunganisha taarifa za tabianchi na satelaiti, taarifa za kijiografia na tathmini ya mazingira magumu ya kaya ili kusaidia kutambua maeneo yaliyo katika hatari ya ukame na majanga mengine yanayohusiana na tabianchi.

Aidha, teknolojia hiyo inasaidia kutoa tahadhari za mapema, kupanga hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutathmini hasara na uharibifu unaotokana na athari zake. Taarifa hizo zinaweza kuwasaidia viongozi na watunga sera kutambua kaya zilizo katika mazingira hatarishi, kupanga vipaumbele vya fedha za kukabiliana na tabianchi na kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa.

Upendo amesema wazo la kuanzisha CLIMAID lilitokana na uzoefu wake wa kukua nchini Tanzania na kufanya utafiti katika jamii zilizo katika hatari ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ambako alishuhudia namna ukame, mafuriko na mabadiliko ya mazingira yanavyoathiri maisha, kipato, utamaduni na maarifa ya jadi.

Ameeleza kuwa taarifa zinazohitajika kukabiliana na changamoto hizo mara nyingi huwa zimetawanyika na kutounganishwa ipasavyo na mifumo ya kufanya maamuzi, hali iliyomchochea kutengeneza jukwaa linalobadilisha taarifa za tabianchi kuwa maarifa yanayoweza kutumika kupanga na kutekeleza hatua za kukabiliana na athari hizo.

Tuzo hiyo imeandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Teknolojia ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), kwa ushirikiano na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) na Serikali ya Cambodia, kupitia mpango wa kuendeleza matumizi ya akili unde katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika tuzo hizo za mwaka 2026, timu tano zilichaguliwa kuingia fainali, huku CLIMAID ikiibuka mshindi na miradi mingine minne ikitambuliwa kuwa miongoni mwa wabunifu waliofanya vizuri. Miradi hiyo ni Ai-Moris kutoka Indonesia, FirePredict kutoka Tanzania, ClimateVoice AI kutoka Mali na Climate Action Copilot kutoka Bangladesh.

Kupitia tuzo hiyo, waandaaji wanalenga kutambua na kukuza matumizi bunifu ya akili unde katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuunganisha wabunifu na wataalamu pamoja na washirika wa maendeleo na kuhamasisha matumizi mapana ya teknolojia zinazosaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za tabianchi.
 
Back
Top Bottom