Barua kwa Lowassa yamletea matatizo Mtikila
na Ratifa Baranyikwa
BARUA yenye maneno makali ambayo Mchungaji Christopher Mtikila alimwandikia Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ndiyo chanzo cha mwanasiasa huyo kutiwa mbaroni na kuhojiwa na Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Tangu Ijumaa iliyopita, Mtikila amekamatwa na kuhojiwa mara mbili, na hivi sasa anasubiri kufikishwa mahakamani wakati wowote, habari za uhakika zinaeleza.
Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema kuwa wanaangalia kwa undani maelezo yaliyotolewa na Mtikila, pamoja na maneno yaliyomo kwenye barua yake, na iwapo itathibitika kuwa ni vya uchochezi, mwanasiasa huyo, ambaye pia ni kiongozi wa kidini, atafikishwa mahakamani mara moja.
Kwa mujibu wa Polisi, kuna uwezekano mkubwa Mtikila akafikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi ya uchochezi.
Moja kati ya kauli ambazo zinamtia matatani Mtikila zilizomo katika barua hiyo (Tanzania Daima ina nakala yake), inamshutumu Lowassa kwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete kuisilimisha Tanzania kwa mbinu na mipango ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana, alisema kuwa Mtikila bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi na kwamba iwapo upelelezi unaoendelea utabaini kuwa ana kosa, atafikishwa mahakamani mara moja.
"Amekamatwa kwa tuhuma za uchochezi kupitia barua hiyo aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita… atawekwa chini ya ulinzi mpaka uchunguzi utakapokamilika na ikibainika ana kosa atafikishwa mahakamani," alisema Tibaigana.
Barua hiyo, ambayo Mchungaji Mtikila ameisaini kama mwangalizi wa kanisa, mbali na kusambazwa kwenye vyombo vya habari, pia inaonyesha kuwa nakala nyingine zimesambazwa kwa viongozi wa makanisa yote nchini na mitandao ya Kikristo.
Katika barua hiyo ya Novemba 1 mwaka huu, Mtikila anamshutumu vikali Lowassa kwa usaliti wake wa kumsaidia Rais Kikwete kuileta Mahakama ya Kadhi, ilhali (Lowassa) akijua kwamba kikatiba ni mwiko kwa kiongozi yeyote wa taifa hili kujihusisha na masuala ya kidini.
"Kikatiba ni mwiko kabisa uongozi wa taifa hili ambalo ni secular kujihusisha na dini fulani, ambapo dini inabaki kuwa ni uhusiano wa mtu binafsi na Mungu wake, hivyo kwamba jukumu la Serikali ni kulinda tu haki ya msingi ya uhuru wa kuabudu (ibara ya 19 na 20(1) ya Katiba ya Jamhuri.
"(Ulifanya hivyo) huku ukijua kwamba katiba inakupiga marufuku wewe na mamlaka yoyote ya nchi hii kutunga sheria au kuweka taratibu na kanuni yoyote yenye ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote ile kwa dhahiri au kwa taathira yake," inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Mtikila, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Full Salvation, pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP).
Kupitia barua hiyo, Mchungaji Mtikila anamshutumu Waziri Mkuu kuwa wakati akiwa kwenye ziara mkoani Mbeya Oktoba 20 mwaka huu, alitumia madaraka yake mwenyewe kuelezea suala hilo aliposema kuwa wameipa mamlaka tume ya kurekebisha sheria chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, kuandaa utaratibu wa kubadili katiba ili kuanzisha Mahakama ya Kadhi kwa kutumia Bunge la Jamhuri ya Muungano, wakati akifahamu kuwa kuna kesi mahakamani kuhusiana na suala hilo.
"Na wewe ndiye uliyewezesha kuzungumzwa bungeni suala hili la kigaidi, na kuridhia azima hii ya hatari ifanyiwe kazi na Wizara ya Sheria," inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Mtikila pia amesisitiza katika barua hiyo kuwa lengo la Mahakama ya Kadhi ni kuuangamiza Ukristo nchini, na kuwaua watu wasiokubali Uislamu na pia kuwaua Waislamu watakaoiacha dini hiyo na kujiunga na imani nyingine.
Oktoba 18 mwaka huu, Mchungaji Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu, iliyopewa namba 80 ya mwaka 2007, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga mchakato wa urejeshwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara, akidai kuwa kufanya hivyo ni kuvunja katiba ya nchi kwa sababu Mahakama ya Kadhi ni chombo cha Jihad na ugaidi.
Akirejea katika kesi yake hiyo, Mtikila alimwambia Lowassa: "Umeusaliti Ukristo kiasi kwamba ulipojua kwamba kesi ipo mahakamani wewe ulitangaza kule Mbeya kuendelea na Jihad kwa kutumia Tume ya Kurekebisha Sheria ili hatimaye mtumie Bunge la nchi kuupa ugaidi nguvu ya sheria nchini, umefanya kosa hili wakati ukijua kuwa ni mwiko kabisa kwa serikali au Bunge kushughulikia jambo lolote ambalo liko katika Mahakama Kuu."
Source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/11/5/habari4.php
Du kumbe isu ni na EL?