Mithali 11:24 NENO
[24] Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi, mwingine huzuia, lakini huwa maskini.
Tukizungumza kuhusu utoaji, kila mtu ana picha yake kuhusu utoaji, wapo hufikiri wakitoa watapungukiwa, wapo hufikiri kutoa sio jambo la lazima, wapo wanajua wakitoa watabarikiwa zaidi.
Utoaji ni utoaji, tunaweza kuuweka katika maeneo tofauti tofauti, ila ujue utarudi kwenye eneo lile lile la utoaji.
Tunaweza kutoa sehemu sahihi, na tunaweza kutoa sehemu isiyo sahihi, ila kwa pamoja unaitwa utoaji.
Utoaji wetu unaweza kusababisha baraka, na utoaji wetu unaweza usisababishe chochote katika maisha yetu.
Lakini utoaji ninaouzungumzia hapa, ni ule utoaji wa kibiblia, utoaji unaompa mtu matokeo mazuri ya utoaji wake, na kutokutoa kunavyoweza kusababisha ukavu wa maisha ya mtu.
Mtu anayetoa kwa ukarimu, kwa unyenyekevu, kwa moyo wa kupenda, anayetoa mali zake, muda wake, moyo wake, kwa ajili ya kazi ya Mungu au kanisa, au mambo ya kijamii, mtu huyo hupewa zaidi na Mungu.
Yule mtu mwenye ubinafsi, mtu asiyependa kutoa pesa zake, au mali zake, mtu huyo anakosa baraka za muhimu, na anakaribisha ukavu kwenye maisha yake.
Kanuni hii ipo kiroho na kimwili, mtu anayetoa kwa kanisa au jamii, uwe utoaji wa mali, msaada, au kutoa upendo kwa wengine, vitendo hivi au tendo hili la utoaji huleta baraka na ustawi katika maisha yake.
Mtu anayetoa kwa moyo safi, awe na uhakika atakutana na baraka za Mungu za kutosha, atazidishwa mara dufu katika maisha yake, hasa yale maeneo anayowajibika.
Mtoaji haishii hapo, anaimarisha mahusiano yake na jamii, mtoaji anavuta upendo kwa jamii, na mahusiano yake yanakuwa imara zaidi na wale wanaopokea vitu kutoka kwake.
Hatutoi ili kuwahonga watu watupende, tunatoa kwa sababu ni kanuni ya Mungu kuwabariki wale wanaotoa, wapokeaji wanaweza wasipate hii baraka, ila watoaji hupata baraka nyingi za ki-Mungu.
Tunaweza kuweka eneo la utoaji katika eneo la fedha au mali tu, ila tunaweza kutoa upendo wetu kwa jamii, na muda wetu, tukajenga mahusiano mazuri.
Mtu mwenye upendo wa kweli, kutoa kwake ni jambo la maana sana katika maisha yake, upendo wa Mungu unatusukuma kutoa mali zetu, muda wetu, fedha zetu, na mambo mengine mengi.
Elewa kwa usahihi kuhusu utoaji wa kibiblia uweze kuneemeka na baraka za Mungu katika maisha yako.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma Biblia na kutafakari
Mungu akubariki sana
Samson Ernest