Mtu mzima anatakiwa kutembea hatua 10,000 kila siku

Mtu mzima anatakiwa kutembea hatua 10,000 kila siku

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janab ametoa angalizo kuwa licha ya kuharibu bajeti ya afya kila mwaka, maradhi hayo yataathiri uchumi wa familia na nguvukazi ya Taifa.

Profesa Janab ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita wiki chache tangu wataalamu wa afya wakadirie kuwa ifikapo mwaka 2027, asilimia 54 ya vifo vyote vitakuwa vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza kutoka asilimia 33 ya mwaka 2018.

Katika mahojiano maalum na Mwananchi, mbobezi huyo tiba ya magonjwa ya moyo alisema saratani, kisukari, shinikizo la damu, moyo na figo yaliyokuwa yakiwaathiri wazee sasa yanaonekana hata kwa watoto.

Kutokana na hali hiyo, alisema Taifa linapaswa kuchukua tahadhari kwa sababu baadhi matibabu yake yanadumu kwa muda mrefu hivyo mgonjwa kuendelea kuwa tegemezi kwa maisha yake yaliyobaki na gharama ni kubwa.

“Magonjwa ya kuambukiza yamekutana na yasiyoambukiza, hivi ni vitu viwili vikubwa ambavyo vyote vinahitaji fedha nyingi kushughulikiwa. Yasiyoambukiza gharama zake ni kubwa ukilinganisha na malaria ambayo ukiwa na Sh500,000 unaweza kuyatibu kwa wilaya nzima lakini kusafishwa figo mara moja ni karibu Sh300,000 na kwa wiki ni Sh900,000 kwa mwezi inakwenda mpaka Sh16 milioni ukijumlisha vitu vyote,” alikumbusha.

Alitolea mfano mwaka wa fedha 2021/22 kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulitumia Sh99 bilioni kutibu magonjwa yasiyoambukiza pekee.

Alisema ni kitu ambacho Taifa linatakiwa kukichukua kwa tahadhari kubwa kwani, licha ya kuharibu bajeti ya afya itaathiri nguvu kazi ya Taifa kwa sababu ukiwa nayo haya magonjwa ambayo baadhi yake kama siyo yote matibabu yake ni ya maisha.

“Nilipokuwa nasoma, mkipita wodini tulikuwa tunaonyeshwa wagonjwa wa utapiamlo au kwashakoo lakini sasa hivi wanafunzi tunawaonyesha kwenye ‘power point’ kwa kuwa wagonjwa hao hawapo tena ila wapo watoto waliozaliwa na tatizo la moyo, figo hazifanyi kazi au amepata kisukari katika umri,” alisema Profesa Janabi.

Daktari huyo bingwa alishauri nguvu iongezwe katika kinga kwasababu ni nafuu kufanya hivyo kwa watu kufuata masharti, kuongeza elimu kwenye vyakula vyenye lishe bora kwani wengi wanadhani vya mafuta pekee ndiyo hatari kumbe kula wanga nao ni hatari zaidi.

Alisema kuna haja kwa akina mama kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote zinazohitajika kuwakinga na maradhi ya moyo, polio na mengine.

Hatua 10,000 kwa siku

Ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, Profesa Janabi alisema ni muhimu kutembea walau hatua 10,000 ndani ya saa 24.

“Kufanya mazoezi ni muhimu kwa sababu mtu mzima anatakiwa atembee hatua 10,000 kwa siku ambazo ni kati ya kilomita sita mpaka saba hivi kutegemea ukubwa wa hatua unazopiga,” alisema.

Pamoja na kutembea, alisema ni muhimu kujenga tabia ya kupima afya kila mwaka sababu magonjwa yasiyoambukiza yakigundulika mapema yanatibika. Alisema ni muhimu kupunguza uzito, unywaji pombe kitu ambacho baadhi hawapendi kukisikia bila kujua kuwa unywaji uliopitiliza una athiri moyo, figo, ubongo na viungo vingine vya mwili .

“Niwakumbushe tu, kinga ni bora kuliko tiba na inapotokea magonjwa ya mlipuko kama Uviko-19 wananchi waende kupata chanjo,” alisema Profesa Janabi.

Si ya watu wazima pekee

Profesa Janabi alisema kumekuwa na dhana potofu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kwa vijana wengi kuyachukulia kama ni ya wazee tu.

“Magonjwa ya saratani au moyo hauyapati Jumatatu kisha Jumamosi ukaanza kuugua. Yanaenda miaka 10 mpaka 15, sasa kama una miaka 30 utaugua ukifika miaka 50 ambapo utakuwa mzee tayari kama hukujikinga. Yanakusubiri tu. Kwa hiyo jitihada zote ulizozifanya ukiwa kijana ukipokea pensheni yote inaishia kulipa ada ya kumwona daktari na kutafuta muuguzi wa kuja kukupiga sindano nyumbani. Katika umri huo ndio unaambiwa chakula hiki usile lakini kama ungekuwa unakula kwa wastani ukiwa kijana ungeendelea kula hata ukiwa na miaka 80,” alisisitiza.

Jinsi ya kuepuka

Kuhusu namna ya kuyaepuka magonjwa yasiyoambukiza, Profesa Janabi alisema umakini unatakiwa kuelekezwa kwenye vitu viwili muhimu ambavyo ni chumvi na sukari. Alisema si vibaya kula vyakula vyenye sukari lakini usile mpaka ukakinai.

“Iwe asali au sukari ukianza kuisikia kwenye ulimi ni kwamba imezidi. Vinywaji kama juisi mimi mara ya mwisho nimekunywa mwaka 2000. Kupata glasi moja ya juisi unahitaji machungwa manne mpaka matano, ina maana ukinywa glasi tano kwa siku ni saw ana kula machungwa 20 kwa siku 10 machungwa 200, mwezi 600 sasa nani anakula machungwa 600? Tunashauri kula matunda zaidi kuliko juisi,” alisema.

Alisema wagonjwa wa kisukari hawawashauri kula matunda mchanganyiko kwa sababu unapoyachanganya sukari inapanda juu.

“Umri unapokuwa mdogo chakula kinasagwa haraka kwa sababu metabolism ipo juu sana lakini kadri unavyokua spidi inapungua ndiyo maana inabidi kuwa mwaangalifu na unachokula, kuzingatia muda wa kupumzika na kufanya sana mazoezi,” alisema.

Wagonjwa wengi wa magonjwa ya moyo na figo, alisema hawafurahii maisha kwenye makazi yao kutokana na matatizo yanayowakabili. Hata wanaishi Mbezi Beach, Masaki au majumb amazuri ya Oysterbay yanayotizamana na bahari lakini hawawezi kupanda ngazi kwenda juu kwa sababu pumzi zinakata. Wengine wanatakiwa kunywa maji nusu lita tu kwa siku kwa sababu figo zimekufa,” alisema na kuongeza:

“Sasa hawa ni watu ambao wamehangaika kwa maisha yao yote kujenga uchumi na wakafanikiwa kifedha, kielimu na kadhalika sasa umefika wakati ambao sasa inabidi wafurahie jitihada zao zote walizozifanya huko nyuma lakini wanapambana na ugonjwa yanayowalaza kitandani muda mrefu.”

MWANANCHI
 
Hatua 10k sio mchezo.

Huo ni umbali mrefu sana, kwa hapo dar ni kama kutoka mwenge mpaka kimara mwisho.
 
Back
Top Bottom