Tuhuma dhidi yake zinadaiwa kuanza muda mrefu ambapo Machi 31, mwaka huu, majira ya saa nane usiku, Kadashi akiwa na watu wengine, alionekana katika kata za Nansimo, Kitengule na Kibara, akiendelea “kukusanya kodi za serikali, kutoka kwa wavuvi eneo hilo la ufukwe wa Ziwa Victoria.
Pambazuko limeelezwa kwamba mtumishi huyo wa serikali, katika kukusanya kinachoelezwa kuwa ni kodi, amekuwa akitumia askari wa Jeshi la Polisi “kumsaidia kukusanya fedha kutoka kwa wavuvi.”
Katika mazingira ya kuchoka malalamiko ya wavuvi hao, Diwani wa Kata ya Nansimo, Andrea Namwata (maarufu kwa jina la Mniga), Machi 31, mwaka huu, nusura apigane na Kadashi alipokuwa akikusanya fedha katika Kijiji cha Namibu, Kata ya Kibara.
“Siku hiyo Kadashi alikuwa na boti mbili za uvuvi na watu kama 15 hivi na askari polisi wanane wakiwamo waliokuwa na bunduki…” “Hiyo oparesheni yao ya kukamata nyavu ilianza saa nane usiku katika Kijiji cha Genge, Kata ya Nansimo, kisha ikaelekea Kijiji cha Nansimo na Nambaza na baadaye wakaelekea katika Kata za Kitengule na Kibara.
“Walipofika katika Kijiji cha Namibu, Kata ya Kibara, majira ya asubuhi, Mniga aliibuka hapo, akawauliza kwanini walikwenda katika kata yake usiku bila taarifa na hapo ndipo ukaibuka mzozo na kidogo Kadashi na wenzake wachapane makonde na Diwani Mniga,” alisema mtoa taarifa wetu.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani Mniga ambaye alithibitisha kutaka kupigana na baadhi ya watu waliokuwa katika msafara wa Kadashi baada ya kukerwa na tabia ya ofisa uvuvi huyo. “Ni kweli, siku hiyo Kadashi na watu wake walivamia katani kwangu saa nane usiku na kukamata wavuvi pamoja na nyavu.
“Wakati wanafika, sikuwepo, kwa hiyo, nilipopigiwa simu majira ya asubuhi, nilikwenda ziwani kuwaona, lakini sikuwakuta,” alisema Mniga. Diwani huyo alisema kwamba, aliwafuatilia watu hao na kufanikiwa kuwakuta katika Kijiji cha Namibu, Kata ya Kibara, wakiwa na mali mbalimbali za wavuvi tofauti tofauti.
“Niliwauliza kwanini walikuja saa nane usiku kukamata watu ziwani, lakini hawakuwa na majibu mazuri, nikawauliza kwanini walikuja katani kwangu bila viongozi nikiwamo mimi kupewa taarifa, hawakuwa na majibu sahihi...”
“Kwa hiyo, nikawaambia kama ningewakuta huko katani kwangu usiku huo, lazima idadi yao ingepungua tu maana walikuja kama majambazi na dawa ya majambazi inajulikana,” alisema Mniga.
Katika maelezo yake, Diwani Mniga alimshutumu Kadashi kwa kushirikiana na watu wasiokuwa watumishi wa serikali katika oparesheni zake nyingi za kukamata nyavu na wavuvi
“Kama anafanya patrol (ukaguzi) ya kiserikali, kwanini hatumii boti ya serikali ambayo ipo kwa ajili hiyo, kama anafanya kazi hiyo kwa nia njema, kwanini anawatumia raia wasiokuwa watumishi wa serikali na kama ana nia njema na zoezi lake, kwanini amekuwa akiwatumia askari polisi kutoka Bunda mjini badala ya polisi walioko katika Kituo cha Polisi Kibara?” alihoji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Lenatus Mujungu, aliliambia Pambazuko kwamba Kadashi huenda alifanikiwa kupata mabilioni ya fedha kwa kuwa alikuwa akikusanya fedha na kuzipeleka anakojua yeye badala ya kuziwasilisha kwenye mifumo ya serikali inayotambulika.
“Huyo mwenzetu alikuwa na utaratibu wa kupewa kiasi kinachofika shilingi milioni nane kila mwezi kutoka kila mwalo ulioko katika Jimbo la Mwibara, hapahapa Wilaya ya Bunda…”
“Katika utaratibu wake huo, alikuwa na mialo ipatayo 40 ambayo kila mwezi ilikuwa ikimkusanyia shilingi milioni nane kila mwalo, fedha hizi tunaamini hazikuwa zikingia katika mfumo wa halmashauri wala katika mfuko wowote wa serikali,” alisema Mujungu.
Kwa mujibu wa madai hayo, endapo Kadashi alikuwa akichukua kiasi hichohicho kila mwezi, alifanikisha kupata shilingi milioni 320. Kiasi hicho kinakaribia shilingi bilioni nne kwa mwaka. Fedha hizi zinaweza kujenga kilomita nne za barabara kiwango cha lami. Inadaiwa kuwa Kadashi alikaa eneo hilo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Baada ya tuhuma hizo kuzidi, Mujungu alisema Februari, 2026, yeye na Kamati ya Kudumu ya Halmashauri ya Huduma za Uchumi inayoongozwa na Diwani wa Kata ya Kibara, Lenatus Kaloli, walitembelea mialo ya Kisorya na Kibara ambako walipokea malalamiko mengi juu ya utendaji kazi wa Kadashi. Katika malalamiko hayo, alisema wavuvi walidai kumchangia fedha Kadashi kila mwezi na kwamba fedha hizo hukusanywa na kundi la watu wakiwamo askari.
Ikadaiwa kuwa mara nyingi kiasi hicho hutolewa na wavuvi ikiwa ni njia ya kurahisha Maisha ya kazi zao, kwani bila kufanya hivyo hupokea vitisho na kunyang’anywa nyavu zao.
“Wavuvi walitueleza kila kitu, walituambia fedha wanazomchangia wanaziita kifurushi, walituambia jinsi kwenye msafara wake wa kusaka fedha anavyoongozana na askari polisi wenye silaha na wakasema yeyote anayekataa kuchanga fedha, jina lake linapelekwa kwa Kadashi na hapo anaanza kushugulikiwa kwa kukamatiwa nyavu zake.
“Kwa kuwa hizo zilikuwa ni tuhuma, tulimuita kwenye kikao cha kamati yetu ili aje atueleze ukweli wa malalamiko hayo, lakini hakufika na badala yake aliwatuma watu wawili, maofisa katika ofisi yake,” alifafanua Mujungu. Pamoja na hayo, alisema mwanzoni mwa mwaka huu, ofisa uvuvi huyo alihojiwa kuhusu tuhuma hizo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Bunda, ingawa hadi sasa hajui suala hilo lilimalizikaje.
Wakati huohuo, alisema Aprili 2, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Enock Kaminyoge, aliitisha kikao cha dharura kujadili masuala ya uvuvi wilayani Bunda.
“Aprili 2, mwaka huu katika ukumbi wa halmashauri uliopo Kibara, mkuu wa wilaya aliitisha kikao cha dharura ambacho nilishiriki, walikuwapo pia madiwani ambao kata zao ziko kandokando mwa ziwa, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya pamoja na viongozi wanaosimamia rasilimali za ziwani tunaowaita BMU …”
“Baadhi ya wajumbe walimgusia Kadashi, lakini ukitaka kujua mambo mengine, unaweza kuzungumza na mkuu wa wilaya atakueleza,” alisema mwenyekiti huyo wa halmashauri. Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, aliiambia Pambazuko kwamba, alipata taarifa za wavuvi kukamatwa saa nane usiku, baada ya kupigiwa simu na wananchi wa Kata ya Nansimo na kwamba anafuatilia jambo hilo kwa ukaribu.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Enock Kaminyoge, akizungumza na Pambazuko alisema serikali imeshachukua hatua dhidi ya Kadashi kwa kumhamisha kituo chake cha kazi.
“Malalamiko dhidi ya Kadashi ni ya kweli na jana (Alhamisi, Aprili 2), niliitisha kikao cha watu wa BMU, madiwani wote ambao kata zao ziko kandokando ya Ziwa Victoria na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
“Kikao chetu kilikuwa ni kwa ajili ya kujadili suala la uvuvi haramu na katika majadiliano, wajumbe waligusia suala la Kadashi ambaye ninakiri kwamba hakuwa na mahusiano mazuri na wananchi…” “Kwa hiyo, uongozi wa mkoa umeamua kurudisha ajira yake Wizara ya Mifugo na Uvuvi maana mwajiri wake ni katibu mkuu wa wizara hiyo.
“Kwa maana hiyo, hawezi tena kufanya kazi katika eneo lolote la Mkoa wa Mara maana hatakiwi tena huku,” alisema Kaminyoge.
Kadashi alipopozungumza na Pambazuko kwa njia ya simu Aprili 29, mwaka huu, saa 9:44 mchana, alisema tuhuma za rushwa zinazoelekezwa kwake ni za kisiasa na kumtaka mwandishi wetu aachane nazo.
“Hizo tuhuma zingekuwa kweli ningekuwa nimeshachukuliwa hatua za kisheria. Sijawahi kuhojiwa popote wala kutuhumiwa kula rushwa kutoka kwa wavuvi.
“Hayo ni maneno ya wanasiasa, waache waendelee nayo wewe achana nayo. Kuhusu suala la kuhama ni kweli Bunda nimehama ila sikuhama kwa ubaya, ukitaka kujua nimehamia wapi, muulize mwajiri wangu ndiye anayejua,” alisema Kadashi kwa kujiamini.
Mkurugenzi Mtendaji (DED), Halmashauri ya Bunda, George Mbilinyi, alipozungumza na Pambazuko hivi karibuni, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na kumtaka mwandishi wetu awasiliane na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda (DAS), Salum Mtelela.
“Huyo jamaa hakuwa mtumishi wa halmashauri na alikuwa haripoti ofisini kwangu kwa sababu alikuwa anatokea Serikali Kuu. Kwa hiyo, siwezi kumzungumzia, mpigie DAS ndiye analijua vizuri jambo hilo,” alisema Mbilinyi.
Mtelela alipopigiwa simu na Pambazuko juzi, alikata simu na kumtaka mwandishi wetu amtumie ujumbe wa maneno na alipotumiwa ujumbe huo akiulizwa kuhusu tuhuma dhidi ya Kadashi, hakujibu.
Mkurugenzi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Baraka Sekadende alipozungumza na Pambazuko wiki iliyopita akiwa jijini Dodoma, alimtaka mwandishi wetu awasiliane na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Dkt. Charles Mhina, kwa kile alichosema kuwa huyo ndiye mwenye uwezo wa kujua mwenendo wa suala hilo.
“Hilo suala la huyo mtumishi wetu wa Bunda silijui kwa sababu sikuwa ofisini kwa kama wiki mbili hivi, nilikuwa Dar es Salaam kwenye shughuli za uzinduzi wa meli yetu ya uvuvi. “
“Kwa sasa katibu mkuu wa wizara hayupo, nakuomba umuone Dkt. Mhina atakueleza kwa kina kwa sababu hata hivi tunavyozungumza najiandaa kurudi Dar es Salaam kuna kikao na mheshimiwa waziri,”alisema Sekadende.
Dkt. Mhina alipozungumza na Pambazuko ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, alithibitisha Kadashi kuhamishwa kituo cha kazi baada ya kupata ripoti ya utendaji kazi wake kutoka mkoani Mara alikokuwa anafanyia kazi.
“Huyo Masanja na staff wenzake kama watatu au wanne hivi waliokuwa katika kituo cha Bunda, tumewahamisha hivi karibuni na kupeleka staff (watendaji) wengine hapo Bunda na hata ukipiga simu huko Bunda watakwambia hivi sasa kituo kina watumishi wapya wote.
“Sikumbuki Masanja amehamishiwa wapi ila nadhani ni Nyumba ya Mungu. Lakini, uelewe kwamba, suala la uhamisho kwa wafanyakazi ni la kawaida hasa unapopata ripoti ya mwenendo wa utendaji kazi wa mtumishi.
“Hayo mambo mengine ya kusema alikuwa anakula rushwa, hatukuelezwa ila kama yapo na viongozi wa wilaya wana ushahidi nayo, atawajibishwa tu licha ya kuhamishwa kituo,” alisema Dkt. Mhina.