Wakuu naomba mnisikilize:
Siungi mkono muungano wa serikali mbili kwa sababu hata tukisema tutatue kero za muungano wa haina hiyo leo; kesho zitakuja nyingine na nyingine. Kwa kifupi kero zake ni endelevu!
Mimi nadhani kilichotufanya tuungane kwanza ni kutaka kuonesha njia kwa mataifa mengine ya Afrika. Kuonesha njia ambayo baadaye ingetufikisha pale ambapo Afrika nzima ingekuwa moja. Nyerere alikuwa na haki na wajibu wa kuipoteza Tanganyika ili kuidhihirishia Afrika na dunia imani yake kwenye Muungano wa Afrika! Kipindi kile ilikuwa ni sifa kubwa sana kupigania Umoja wa Afrika.
Sababu ya pili ilikuwa ni ya kuhimarisha ulinzi na usalama kwa wakati ule!
Sababu zote hizo hapo juu hazina mashiko tena kwenye zama hizi za ubepari! Sasa kwa nini tuendelee kuishi imani zisizokuwepo!
Ikumbukwe kuwa zile juhudi za kuliunganisha bara la Afrika zilikufa hata kabla hazijafika mbali kwa sababu wengi wa waliokuwa wanaamini kwenye umoja wa Afrika walitoweka na mawazo yao!
Hata zile juhudi za kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki hazina uhai tena. Sisi ni mashuhuda wa kifo chake kitakatifu; tunasubiria tu kitangazwe rasmi siku za usoni!
Nauliza maswali hapa: Ni kwa nini kuwepo na muungano ambao mshirika mmoja anakubali kupoteza ili kumwokoa mwingine? Hata kwenye ndoa haiwezekani ndugu ni lazima walete chokochoko mwenzi mmoja akitoweka!
Eti serikali tatu haiwezekani kwa sababu Zanzibar haina uwezo! Ni kwanini nchi ijione haina uwezo wakati ilitafuta uhuru wake ili ijiendeshe?
Kama kujiendesha kwake ni kwa kutegemea taifa lingine haioni kuwa ina uhuru wa bendera tu?
Kama Zanzibar wa hofu wakiungana rasilimali zake kama mafuta n.k zitapotea; je, Tanganyika yenye gesi, mafuta, wanyamapori, makaa ya mawe, madini ndiyo iendelee kujitoa sadaka???! Basi Tanganyika itakuwa ni nchi nzuri sana ya kuishi kwa sababu haina hofu ya kuishiwa rasilimali!
Endapo atajitokeza mtu wa kuainisha pasipo shaka mipaka ya mapato na matumizi baina ya Tanzania Bara, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nitafarijika sana! Nasema hivi kwa sababu ninachokiona mimi ni kuwa chochote kipatikanacho Tanzania Bara ni faida ya wote na cha Zanzibar ni kwa faida ya Zanzibar tu pekee.
Je, hii inaonesha kuwa Tanzania Bara inajiamini kuwa yenyewe ndiyo yenye uwezo wa gharamia serikali ya muungano na inaona fahari kufanya hivyo?! Au labda kuna masuala mengine Tanzania Bara inanufaika nayo ambayo sisi wananchi hatujui!
Je, Zanzibar nayo inaona fahari tu kuhudumiwa kila kitu kwenye muungano na wala haioni kuwa Tanzania Bara imebeba jukumu zito? Na je Zanzibar isipotimiziwa mambo kadhaa watakuwa radhi kulalamika ilhali wamebebwa katika mambo mengi?
Nionavyo mimi kama tatizo ni gharama za kuendesha serikali tatu ambazo ndo halali ni sharti tutafute mfumo wa kudumu kutatua tofauti zetu! Tukumbuke kuwa upande mmoja wa muungano umeingia gharama kubwa kuhudumia serikali ya muungano kwa zaidi ya miaka 49 sasa! Au iaonekana Tanganyika hajichoka kulea muungano na Zanzibar nayo haijachokaa kubebewa!
Tusijidanganye; Tanzania ni jina! Nchi ni sisi wananchi! Na wananchi wa pande zote za Muungano wamechoka kulazimishiwa muungano wa serikali mbili! Tunaowaona wanatetea ni baadhi ya watawala ambao muungano uliopo sasa unawanufaisha kwa namna fulani.
Kama wananchi wengi wanadai muungano hauwatendei sasa inabidi tuseme imetosha tutafute kitakachotupa haki na usawa. Na hiki si kingine zaidi ya nchi zote kuungana na kuwa chini ya serikali moja itakayohakikisha kila raia anakuwa na haki sawa na mwenzake bila kujali atokako!
Ingependeza tuwe na serikali tatu kila nchi ijihudumie kwani kila nchi ilidai uhuru ili iwe huru! Lakini watu wanaeneza mawazo hasi ya ukubwa wa gharama!Umaskini na uvivu wa fikra! Ikumbukwe chochote kizuri ni sharti kiwe na gharama yake; tena gharama kubwa!
Kama tunakimbilia unafuu wa serikali mbili tufahamu wazi kuwa nafuu mara zote ni ghali zaidi na mara zote hazidumu!
Muungano wa serikali mbili vilio vya unyonyaji! Muungano wa serikali tatu tunaogopa gharama! Basi muungano unaotufaa ni wa serikali moja. Kama hatuwezi muungano wa serikali moja, muungano wowote ule utakaokuwepo aidha wa serikali mbili, tatu au zaidi hautatuliza kiu ya wananchi! Narudia tena: Tanzania ni jina; nchi ni wananchi!
Nashangaa nchi zenye watu zinaogopa kujiwekea mifumo ambayo itawastawisha na kumaliza chokochoko kwa visingizio visivyoisha! Ina maana pamoja na rasili mali tulizonazo viongozi wetu wanataka kututhibitishia kuwa hawawezi kuweka mifumo ya kuliendesha taifa kwa ustawi!
Hoja ya kuwa kuna udugu wa damu kati ya Tanganyika na Zanzibar ni hoja ya kibaguzi kwani uhusiano wa damu upo pia baina ya Tanganyika na nchi nyingine. Swali hapa: Ni kwa nini tusiungane na Kenya, Uganda, Msumbiji, Burundi, Malawi, Zambia, n.k kwa sababu hata huko wapo watanganyika wana ndugu zao?
Kama hoja ni udugu ni kwanini Zanzibar wanapochagua wabunge wa kuja kwenye bunge la Jamhuri wa Muungano, upande wa Tanzania Bara nao wasichague wawakilishi wachache kwenye Baraza la Wawakilishi ili kuukuza zaidi huo unaoitwa udugu???
Udugu unaonufaisha upande mmoja zaidi ya mwingine si mzuri jamani! Tuache propaganda. Kama tunaamini umoja ni nguvu utengano ni udhaifu basi tuungane tuwe nchi moja, serikali moja, rais mmoja na Tanzania moja ili tuwe ndugu kweli!
Watasema ni chuki lakini kama hatuwezi kumaliza tofauti zetu kwa kuunda serikali tatu au moja basi ni bora kila nchi ijendee kivyake! Hata Kenya na Uganda ni ndugu zetu lakini hatujaugana nao kutengeneza taifa la kusadikika!
Litakuwa ni kosa sana kuendelea kuwa na muungano ambao upande wa Tanganyika tu ndiyo unaendelea kupoteza historia yake wakati mshirika wake Zanzibar akibakiwa na ziada hata kama ni sawa na wilaya moja ya Tanganyika!
Wakuu; naombeni kuwasilisha hoja!
Hoja imefika lakini mbona ndugu yangu hoja yako umeijenga katika mambo mengine yasiyokuwa ya kweli?
zanzibar ikiwa na serikali kamili ndiyo ya kuonewa huruma kwani inajukumu la kuwaendeleza na kuwahudumia watu wake kwa yale yanayoambiwa si ya muungano na baadae kuja kuchangia katika jungu kubwa ambalo sehemu kubwa inaliwa na walio wengi na ambao matumizi yao hayatenganishi baina ya walichozalisha wao au wenzao.
Hili la kutotafautisha baina ya kipato na matumizi ya pamoja na yale ya Tanganyika pekee ndio hufanya wazanzibari wawepo bungeni ambako hayo matumizi hufanywa. Kule zanzibar matumizi yanayopangwa na wawakilishi ni ya zanzibar peke yake sasa hiyo haja ya kuwaleta watu wasiohusika ya nini?
Hata hivyo nakubaliana nawe kuwa hakuna uwazi na hili lazima lilete manunguniko, na dawa yake ni rahisi tu, tuchukue mfano wa zanzibar wa kuwa na serikali yake na hivyo Watanganyika watajuwa nini wanachuma na nini wanatumia kwa serikali yao na kama tunahitaji tuwe na mambo fulani ya pamoja basi tufanye donation kwa mujibu wa tumbo la mtu na anavyokula!