Muunganiko wa maendeleo ya miji na vijiji nchini China yahimiza ukuaji wa miji

Muunganiko wa maendeleo ya miji na vijiji nchini China yahimiza ukuaji wa miji

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,310
Reaction score
1,265
VCG211328616680.jpg


Mwanzoni wakati China inaanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, serikali ilichagua maeneo ya mashariki kuwa ya mwanzo kujipatia maendeleo. Baada ya maeneo hayo kupiga hatua yakaanza kutumia uwezo wake kiuchumi kuhimiza maendeleo ya maeneo ya magharibi yaliyokuwa nyuma kiuchumi.

Kwenye mchakato wa maendeleo ya eneo la Mashariki mwa China yalitokea maeneo yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi, kijamii na hata miundo mbinu. Hapo awali kulikuwa na pengo kubwa kati ya watu ndani ya miji, baadaye kukawa na pengo kati ya miji na miji, na baadaye kukawa na pengo kati ya eneo la mashariki na eneo la magharibi. Lakini kutokana na utekelezaji endelevu wa sera, hatua kwa hatua pengo la maendeleo kati ya makundi yote linazidi kupungua.

Moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya China katika kupunguza pengo la maendeleo ya vijiji, ni mpango unaoitwa Mkakati wa Kuendeleza Vijiji. Hatua za msingi katika mkakati huu ni kufikisha miundombinu ya usafiri katika maeneo ya vijijini, na kuimarisha nafasi ya teknolojia katika sekta ya kilimo ili kuongeza mavuno ya kilimo na kuchangia uhakika wa chakula.

Kwa sasa maeneo mengi ya China yanafikika kama sio kwa ndege basi kwa treni, na kama sio kwa treni kwa barabara ya lami, na kama sio kwa barabara ya lami, basi inaweza kuwa kwa barabara iliyojengwa kwa saruji. Sekta ya kilimo ambayo ndio nguzo ya uchumi katika maeneo mengi ya vijijini pia imekuwa na maendeleo. Mwaka 2022 Kamati ya maendeleo na mageuzi ya China ilitangaza kuwa, kwa sasa zaidi ya asilimia 72 ya kazi za kulima ardhi, kupanda na kuvuna zinafanywa kwa mashine, kiwango kilichoongezeka kwa asilimia 6 ikilinganishwa na mwaka 2017. Hali hii imeongeza uzalishaji na kufanya watu wa vijijini wawe na mapato zaidi.

Matumizi ya teknolojia pia yamesaidia kuchochea maendeleo ya biashara ya mazao ya kilimo kutoka vijijini. Kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya usafirishaji na matumizi ya Internet, kwa sasa watu wa vijijini wanaweza kuuza bidhaa zao za kilimo moja kwa moja kwa wateja wa mijini, na hata kuweza kuagiza vitu kutoka mijini bila kulazimika wao wenyewe kwenda mjini kufuata bidhaa hizo.

Pengine eneo la huduma za jamii katika maeneo ya vijijini, hasa elimu na afya, ni eneo lililopata maendeleo ya haraka kutokana na matumizi ya teknolojia. Katika baadhi ya vijiji ambavyo ni vigumu kufikika, wanakijiji wanaweza kwenda kwenye zahanati ndogo zilizopo vijijini, lakini wanaweza kuchukuliwa vipimo vinavyokaguliwa na madaktari bingwa na wabobevu walio umbali wa maelfu ya maili kwenye miji mikubwa, na manesi au madaktari wapya wanaweza kusaidia kuwatibu wagonjwa hao kwa kufuata maelekezo. Baadhi ya shule katika maeneo hayo pia zinaweza kuunganishwa na kwa satellite au hata njia ya simu na wanafunzi kushiriki kwenye madarasa yanayofundishwa moja kwa moja na walimu walioko mijini.

Maeneo ya vijijini yaliyo karibu na miji yanaendelea kupata maendeleo ya haraka kutokana na ukaribu wake na miji. Vijiji vinaweza kutumia mazingira yake ya “kijijini” yasiyokuwa na pilika na misongamano, kuvutia watu kutoka mijini wanaotaka kupumzika katika maeneo hayo. Kwa sasa vijiji vingi vimeanzisha hoteli na migahawa inayovutia watu kutoka mijini, wengine wanapenda tu kuhisi hali ya kuwa katika mazingira ya kijiji na kula chakula kinachotoka shambani moja kwa moja, na wengine hata wanapenda kujaribu shughuli za kilimo kama vile kuchuma mboga au matunda wao wenyewe.
 
Back
Top Bottom