Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya National Super Alliance NASA, umemteua aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu
Bw. Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia Chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili
Makamu wa Rais wa zamani Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubali kumuunga mkono mgombea huyo mmoja
"Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa", alisema
Amesema mpango wao ni kuwa wadhifa wa kinara wa mawaziri na msaidizi wake
Mgombea mwenza wa Bw. Odinga atakuwa Makamu wa Rais wa zamani Bw. Kalonzo Musyoka, kiongozi wa chama cha Wiper.
Waziri mkuu mratibu wa shughuli za Serikali atakuwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi
Naibu Waziri mkuu mratibu wa uchumi atakuwa kiongozi wa Ford Kenya Moses Watengula
Kiongozi wa chama mashinani CCM Isaac Ruto atakuwa Naibu Waziri mkuu atakayesimamia utawala wa huduma za jamii
Bw. Odinga ni Mwanasiasa aliyesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika mstari wa mbele kuunda vyama vya muungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.
Chanzo: BBC/Swahili